Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Nuru Awadh Bafadhili (13 total)

MHE. NURU AWADH BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kuna baadhi ya kaya ambazo ni maskini sana lakini hazikuorodheshwa katika zoezi hili la kuwezeshwa katika mradi huu wa TASAF na kuna wengine wana uwezo lakini vile vile wanapokea pesa hizi za TASAF; je, Serikali inatuambia nini kuhusu hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA
BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nipende kusema kwamba ni kweli ziko kaya ambazo zilikuwa ni kaya maskini sana lakini unakuta haijaorodheshwa katika mpango na kinyume chake kaya ambazo si maskini au angalau zina ahueni ziliorodheshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika mchakato huu mzima wa uandikishwaji wa walengwa, ni mikutano yetu mikuu katika kata, kijiji na shehia ambayo inashirikishwa. Kwa kiasi kikubwa baadhi yao katika mikutano mingine mikuu unakuta itikadi za kisiasa zimetumika lakini pia unakuta kuna wengine wameorodheshwa wanaogopa kusema kuwabaini kwamba huyu ameingizwa lakini hastahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kutoa rai kwa wananchi wetu pamoja na mikutano mikuu, watakapoona kuna kaya zimeorodheshwa hazistahili basi waweze kutoa ushirikiano na waweze kuziondoa na tunaamini wataweza kufanya hivyo kwa sababu mpaka sasa tumeshaondoa zaidi ya kaya 73,851 na tutaendelea kufanya hivyo. Tunaomba wananchi waweze kutoa ushirikiano ili wawe ni wale tu ambao kweli wanazo sifa ndio waweze kunufaika na mpango huu. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, miundombinu ya vyoo hususan katika Kambi ya Polisi wanaoishi katika eneo la Msambweni Madina ni mibaya sana kiasi ambacho wenyewe wanaita ni SACCOS.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatengenezea vyoo vyao wakati wanasubiri utaratibu wa kujengewa hizo nyumba?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa askari wale wanatumia maji ambayo Serikali ndio inawalipia, lakini maji hayo hayo utakuta wenyewe hawayatunzi vizuri, utakuta maji yanamwagika na wanayaachia.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawekea mita kama walivyoweza kuwawekea LUKU?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mawili madogo ya nyongeza. Nikianza na lile la uchakavu, la vyoo, niseme tu kwamba naelekeza wafanye tathmini na nitawaambia watu wangu Wizarani ili tuweze kuangalia namna ambavyo tunaweza kusaidia kwa sababu hilo ni jambo ambalo linahitaji uharaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili la kuhusu maji kumwagika ni suala la miundombinu na ni suala la umakini katika utumiaji wa maji. Tutayaangalia yote pamoja, lakini la msingi sana ambalo linafaa kwa askari wetu ni upatikanaji wa maji wa kila wakati. Tumejaribu kwenye LUKU, maeneo mengi sana tumepata shida sana kwa sababu ya wakati fulani fedha ambazo zinatakiwa zilipie kuchelewa na hivyo kuwafanya askari walipe kwa fedha zao na baadae kuanza kuhangaika kupata fedha za kufidia. Kwa hiyo, tutayaangalia yote kwa pamoja, ili tuweze kuhakikisha kwamba, tunatunza maji ili askari wapate maji kwa kila wakati. (Makofi)
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vijana wengi wanaopelekwa katika sober houses wanalipishwa kiasi fulani cha fedha ili waweze kujikimu kwa vyakula. Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka kuwasaidia kwa sababu kuna baadhi ya jamii hazina uwezo wa kuwasaidia watoto wale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sober houses nyingi zinamilikiwa na watu binafsi na waathirika hawa wa dawa za kulevya wamekuwa wakilipishwa. Mpango wa Serikali ni kuandaa utaratibu sasa ambapo na sisi tutatengeneza sober houses za kwetu ili kufanya huduma hii ipatikanike kwa urahisi na kila mmoja ambaye hana uwezo wa kumpeleka katika sober house za private aweze kupata tiba hii na imsaidie kurudi katika hali ya kawaida.

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imetenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya kuendeleza jengo la OPD; na kwa kuwa pesa hizo huenda zisikidhi kukamilisha jengo hili, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha inawaongezea fedha Wilaya ya Tabora ili waweze kupata Hospitali ya Rufaa ili kuepuka wagonjwa kupelekwa Hospital ya Bugando au Muhimbili? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bafadhili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Tabora tayari tunayo Hospitali ya Rufaa. Katika swali la msingi ambacho kinaulizwa ni Hospitali ya Wilaya. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha Wilaya zote ambazo hatuna Hospital za Wilaya zinajengwa. Ndiyo maana tumeanza na hospitali 67. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba fedha ambayo inapelekwa inaenda kutumika vile ilivyokusudiwa. Naomba nimkikishie, kama hicho kiasi cha fedha kilichotengwa shilingi milioni 70 hazitakidhi, Serikali itakuwa tayari kuhakikisha kwamba inaongeza fedha ili Hospitali ya Wilaya iweze kukamilika.
MHE. NURU AWADHI BAFADHIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa wananchi wengi wamehamasika katika kujiunga na bima ya afya, wananchi hawa wanapofika hospitalini daktari anaweza akamuandikia dawa moja paracetamol nyingine anaambiwa akanunue. Je, Serikali inatwambiaje kuhusu hawa Wananchi wanaoambiwa wakanunue wakati wao wamejiunga na Bima ya Afya, ili waepuke makali ya maisha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano imeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 30 hadi shilingi bilioni 270 katika bajeti ambayo tumeipitisha mwezi Julai mwaka huu; hali ya upatikanaji wa dawa nchini sasa hivi ni zaidi ya 90%; lakini sambamba na hilo mwezi Februari tulitoa mwongozo wa utoaji huduma za afya na aina za dawa ambazo zitatumika katika kila ngazi kwa aina ya ugonjwa na orodha hii tumejaribu kuihuisha pamoja na wenzetu wa Bima ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo tumeanzisha utaratibu wa maduka ya dawa muhimu ambazo haziko katika orodha yetu ya dawa zile muhimu ambazo ni 167 ili yale maduka yaweze kutoa dawa zile ambazo ziko nje ya utaratibu wetu wa hizi standard treatment guideline lakini zinahitajika katika utaratibu wa bima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe na nimhakikishie Mbunge kuwa tunaendelea kuboresha mfumo huu kuhakikisha kwamba dawa zote ikiwa na zile ambazo zilikuwa zinahitajika kwa wagonjwa wa bima zinapatikana katika hospitali zetu za umma.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Katika Kata za Jiji la Tanga miaka ya 1990, kata zilihamasishwa kujenga vituo mbalimbali vya Polisi ambavyo vilisaidia kupunguza uhalifu, matokeo yake sasa hivi vituo vile vimetelekezwa, vimekuwa ni nyumba za vibaka.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuvifufua vituo hivyo ili kuweza kuweza kuzuia uhalifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, mara zote tumekuwa tukihamaisha Waheshimiwa Wabunge na wananchi kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na upungufu wa Vituo vya Polisi nchini. Kwa hiyo, ni jambo la ajabu sana kama Serikali tutakubali kuona kwamba jitihada hizi za wananchi wanavunjwa moyo.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo dhamira ya Serikali kuvitelekeza vituo hivyo ambavyo vina umuhimu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge hakutaja kituo gani ambacho kimetelekezwa, kwa hiyo, ni vigumu kumpa sababu ya kituo hicho ambacho amekusudia kwamba hakitumiki mpaka sasa hivi kwa sababu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, baada ya Bunge hili nitakuwa tayari kukutana naye ili aweze kunipa taarifa za kina tufuatilie na kuchukua hatua za haraka. (Makofi)
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika Kata ya Mabanda, Diwani wa Kata hiyo alijitolea kukarabati bwawa kwa fedha zake mwenyewe milioni tano; lakini Bwawa hilo linatumiwa na wananchi hao pamoja na wanyama. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwachimbia haraka visima ili kunusuru afya zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Kata ya Madanga Wilaya ya Pangani katika Vitongoji vya Jaira, Nunda, Barabarani, Zimbiri, Kidutani wananchi wanatumia maji kutoka katika taasisi za dini. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwachimbia visima ili waepukane na adha ya kusumbuliwasumbuliwa wakati wanapokwenda kuchota maji kwenye hizo taasisi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza huyo Mheshimiwa Diwani ambaye alikarabati bwawa kwa ajili ya matumizi ya wananchi wake, lakini pamoja na matumizi ya wanyama. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradina fedha hizo tulizielekeza katika Halmashauri husika. Hata hivyo baada ya kuona pengine mambo hayo yalikuwa hayatekelezwi vizuri, ndiyo maana Mheshimiwa Rais sasa ameelekeza kwamba utekelezaji wa miradi yote itafanywa moja kwa moja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyomjibu Mheshimiwa Mwamoto kwamba mchana leo saa sita tunatoa tamko la Serikali ni jinsi gani sasa miradi kwa sasa hivi itatekelezwa. Kwa hiyo, tutahakikisha kwamba wananchi katika hilo eneo pamoja na Mheshimiwa Diwani kukarabati bwawa, lakini na visima vitachimbwa ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; maeneo ya Nunda na maeneo mengine ambayo amesema taasisi za dini zinasaidia, huwezi kutenganisha Serikali na taasisi za dini. Tunazishukuru sana taasisi za dini, zimetusaidia sana katika kuhudumia wananchi. Hata hivyo, nimeshaelekeza katika Halmashauri ya Handeni tutachimba visima zaidi ya 20 na huo ni uchaguzi wa Mheshimiwa Mbunge Mboni pamoja na Mbunge mwenzake kuhakikisha ni maeneo gani ya vijiji ambayo tutachimba visima.
Mheshimiwa Naibu Spika, jioloji ya Handeni ina tatizo la maeneo mengi maji yana chumvi, kwa hiyo katika kuchagua miradi hiyo itabidi tuwe waangalifu na pia nimeshaelekeza Mradi unaotekelezwa wa Wami, ule Mradi wa Wami bomba litachukuliwa kutoka Tenki la Manga ili maji yaweze kupelekwa mpaka Mkata. Kwa hiyo suala la maji Handeni baada ya muda mfupi litakuwa ni historia. (Makofi)
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Serikali imebaini kuwa kuna bandari bubu na haziepukiki bandari bubu hizo. Je Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha hizi bandari bubu, wenye vyombo katika bandari bubu wanasajiliwa ili kuepusha ajali za mara kwa mara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna changamoto ya bandari bubu na kama Serikali tumekuwa tukiendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuzirasimisha bandari hizo kwa msaada mkubwa sana wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuwasiliana na wadau ambao wanaendesha bandari bubu. Kwa sababu nyingine huwa zinakuwa zinachangamka kabisa na zinatakiwa zipewe miundombinu mbalimbali ya Kiserikali ili ziwe salama kwa ajili ya Watanzania. Nimhakikishie tu kwamba tutaendelea kuzitembelea na kuwapa elimu na inapotakiwa tutaendelea kuzirasimisha ili kuokoa maisha ya Watanzania waweze kusafiri salama. (Makofi)
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Takwimu ya ufaulu zinaonesha kuwa wanafunzi wa Serikali wanapata idadi ndogo ya ufaulu kuliko private. Hiyo inasababisha kupata nafasi ndogo ya udahili katika vyuo na inasababisha kupata watalaam wachache kutokana na uchache wa nafasi zao ya udahili.
Je, Serikali haioni kwamba inaweza ikapoteza watalaam kutokana na uchache wa wanaodahiliwa kwa kuwa wanafunzi wengi wa private wanaachwa kwa dhana kwamba wana uwezo wa kulipia ada za vyuo kutokana na uwezo wao uliokithiri wa kusoma katika shule hizo za private? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, miaka ya nyuma shule zilikuwa za sekondari na msingi zikifundisha masomo ya ufundi mbalimbali; uhonaji, useremala na kadhalika, je, Serikali ina mpango gani ya kuhakikisha inarudisha tena masomo haya ya ushonaji, ufundi mbalimbali kwa vitendo ili kuweza kuwawezesha wanafunzi wanapomaliza masomo yao wajiajiri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nuru swali lake la kwanza amezungumzia habari ya takwimu ya wanafunzi wanaomaliza kwenye private school na wale wanaomaliza kwenye shule za Serikali. Naomba nimhakikishie kwamba hili suala ni la kitakwimu na anachokisema sidhani kama ana uhakika kwamba wa private ni wengi kuliko wale wa shule za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni swali la kitakwimu, basi tutalichukua ili tuweze kuleta takwimu sahihi kulingana na alichokizungumza. Kwa imani natambua ya kwamba hakuna ambapo shule za Serikali zimekuwa nyuma sana ukilinganisha na za private kitakwimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili linazungumzia habari ya wanaomaliza ni namna gani wataweza kuendelezwa akirejea kwamba zamani mitaala ilikuwepo ya kufundisha useremala na mambo mengine. Naomba nimhakikishie kwamba Shule zetu au vyuo vyetu vya VETA zinafanya kazi hiyo ya kuweza kufundisha wanafunzi wanaoishia form four au darasa la saba mambo ya ufundi, lakini vile vile tuna vyuo 55 ambavyo vilikuwa ni Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na sasa hivi kati yake karibu vyuo 20 vinakarabatiwa ili kuweza kufundisha ufundi stadi kwa wanafunzi wale ambao wanakuwa wameshindwa kuendelea na masomo ya sekondari aidha kwa A’ level au kwa form one.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Hospitali ya Bombo katika Jiji la Tanga ndiyo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa; na kwa kuwa hospitali hiyo haina lift kiasi kwamba wanawake wazazi wanatengenezewa theater kule kule kwa ajili ya kuwasaidia wasipate taabu ya kubebwa na mabaunsa: Je, ni lini Hospitali ya Bombo itapatiwa lift?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nuru kuhusiana na suala la Hospitali ya Bombo. Nikiri ni kweli Hospitali ya Bombo, jengo la akina mama na watoto halina lift. Nami bahati nzuri nilipata fursa ya kwenda kulitembelea, nimeiona hiyo adha, nasi kama Serikali tumeingiza katika mipango yetu ya bajeti ili tuweze kukarabati hiyo lift.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mbali na hayo masomo yaliyokwishafundishwa kuna somo la TEHAMA ambalo sasa hivi linafundishwa katika shule mbalimbali lakini kuna baadhi ya walimu katika shule za msingi hawana ujuzi wa kutumia kompyuta. Je, Serikali ina mpango gani ya kuwapa mafunzo walimu hao ili tuendane na wakati huu wa utandawazi na digitali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa walimu wanafanya kazi zao vizuri na tunastahili kuwapa motisha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa ile Teaching Allowance kama walivyowapa Wakuu wa Shule pamoja na Waratibu ili nao waweze kuipenda kazi yao na kupata morali ya kufundisha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nuru Awadh, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kuwajengea walimu uwezo katika masuala ya TEHAMA, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa TEHAMA ni kati ya maeneo mapya ambayo lazima walimu wote wajengewe uwezo kwa sababu katika enzi tulizopo sasa TEHAMA ni moja ya vitu muhimu katika elimu. Kwa hiyo, katika mipango ya Serikali TEHAMA ni moja kati ya maeneo muhimu ambayo walimu watajengewa uwezo na hili litafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la motisha, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya walimu kadiri ya uwezo utakavyoruhusu. Siku za mbele hata masuala ya motisha ni moja kati ya masuala ambayo yanaweza yakaangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mimi ni Naibu Waziri wa Elimu, naomba nitumie fursa hii vilevile kuwatakia kila la kheri vijana wetu 91,440 wa Kidato cha Sita na wale 12,540 wa Vyuo vya Ualimu ambao leo wanafanya mitihani yao ya mwisho. Hata hivyo, nitoe rai kwao kwamba wafuate sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza mitihani na kamwe wasije wakajihusisha na vitendo vya wizi na udanganyifu katika mitihani.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika Mtaa wa Kalimaji, Kata ya Moshono, katika Jiji la Arusha kuna tatizo la mawasiliano ya tigo, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha mawasiliano hayo yanapatikana kwa vile wananchi wanayakosa hayo mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nuru Bafadhili, Mbunge wa Viti Maalum na Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri tumekwishaongea sana na Mheshimiwa Nuru Bafadhili kuhusu suala hilo na bahati nzuri nimekwishamuonesha kwenye vitabu jinsi ambavyo maeneo aliyoyataja tulivyoyaweka na nimpongeze sana kwa jinsi alivyofuatilia maeneo yale mpaka tumeyaingiza kwenye tenda ya awamu ya tano. Nimhakikishie tu kwamba kuanzia mwezi wa Tatu tutatangaza tenda ili makampuni ya simu yaweze kuchukua kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi hiyo na wananchi wa maeneo yale waweze kupata mawasiliano. (Makofi)
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika eneo la Ilazo, Extension C katika Jiji hili la Dodoma, wananchi wanajenga nyumba zao kwa bidii sana lakini tatizo linakuja kwenye umeme. Wananchi wamefika TANESCO wameambiwa nguzo hakuna na anayetaka nguzo kuanzia nguzo mbili ni Sh.600,000 na kuanzia nguzo tatu na kuendelea inakuwa ni Sh.2,000,000. Hili suala linakuwaje kwa sababu kazi ya Serikali ni kusambaza miundombinu kama walivyofanya Idara ya Maji wamepeleka maji, barabara zimechongwa lakini hili la umeme linakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kujibu swali la nyongeza la mama yangu, Mheshimiwa Nuru. Ameulizia suala la maeneo ya Ilazo hususani swali lake limelenga kwamba wananchi wanakwenda TANESCO wanaambiwa walipie gharama ya nguzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili ni zuri, nataka pia nirejee maelekezo na maagizo ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani kwamba nguzo zote ni bure na kwa nini tumetoa agizo hilo? Gharama ya kupeleka umeme ina vitu vingi; kuna masuala ya transfoma, waya na kadhalika, lakini imekuwa tu ni mazoea kwa Shirika letu la TANESCO kutanguliza kipaumbele cha nguzo wakati ni sehemu tu ya gharama ya kuwaunganishia umeme Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niendelee kusisitiza agizo la Waziri wa Nishati lipo palepale, wananchi waendelee kuhudumiwa kwa TANESCO yenyewe kujiandaa na mpango wa manunuzi wa nguzo kwa sababu zile nguzo zinakuwa mali ya TANESCO. Kwa hiyo, nataka nilichukue suala hili la kulisimamia baada ya kutoka hapa. Kweli nimepokea salamu nyingi sana za wananchi kuhusu kuendelea kwa lugha ya Mameneja kusema nguzo hakuna, kuwachaji wananchi gharama za nguzo na kuwarudisha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tuendelee kusisitiza, tumesema Meneja ambaye hayupo tayari kupanga mipango ya kuwaunganishia wananchi kwa kutumia ubunifu wake kwa gharama za nguzo za Serikali, Meneja huyo atupishe ili tuwape Mameneja wengine mamlaka ili waendelee kuwaunganishia umeme wananchi. Kwa sababu yapo maeneo wanaweza kuunganisha kama kuna maeneo wanaona wanashindwa kutekeleza agizo hili la Serikali yetu ambayo imeamua kuwapunguzia gharama wananchi atupishe tu ili wengine waendelee kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kusisitiza hili agizo lipo na yeyote anayeona hawezi basi atupishe ili tumteue mtu mwingine aweze kupanga mipango ya kuwaunganisha wananchi umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.