Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Adelardus Lubango Kilangi (2 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea lakini kwa sababu ndiyo nafungua mdomo wangu kwa mara ya kwanza katika Bunge hili Tukufu, basi nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai. Nimshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Spika, Naibu Spika Mwenyekiti na Wenyeviti wote. Naomba kuwashukuru na kuwapongeza Wabunge wote na hata Watanzania wote ambao wako nyuma yetu (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kuchangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii yalizuka masuala kama mawili hivi matatu ya kisheria yaliyohitaji ufafanuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Swali la kwanza lilitoka kwa Mheshimiwa Abdallah Mtolea aliyependa kufahamu uhalali wa Mheshimiwa Rais kumpatia msamaha Nguza Viking maarufu kama Babu Seya pamoja na Johnson Nguza maarufu kama Papii Kocha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa msamaha kwa wafungwa upo kwa namna mbili kisheria; namna ya kwanza ni msamaha wa Rais ambao unatolewa chini ya Ibara ya 45 ya Katiba. Hata hivyo, nieleze hii inaitwa prerogative of mercy ni kama Kiswahili chake nimeshindwa kukipata kwa haraka, lakini ni kama mamlaka ya kutoa msamaha au huruma. Sasa mamlaka haya yanaongozwa na sheria itwayo Presidential Affairs Act na kifungu husika ni kifungu cha tatu (3) (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna ya pili ya utoaji wa msamaha ni kupitia Bodi ya Parole huu unaitwa msamaha wa Parole. Aina hii inaongozwa na sheria itwayo The Parole Boards Act na kifungu husika ni kifungu cha nne (4) cha sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msamaha uliotolewa na Mheshimiwa Rais kwa Nguza Viking pamoja na Jonson ni ule wa aina ya kwanza na ambao unaongozwa na hiyo sheria niliyoitaja ya Presidential Affairs Act.

Mheshimiwa Mwenyekiti, palikuwa pia na maswali kutoka kwa Mheshimiwa Suzan Lyimo ni maswali mawili. La kwanza, aliuliza kama ni halali na inakubaliwa kisheria kwa Serikali kukata rufaa dhidi ya uamuzi kuhusiana na Sheria ya Ndoa baada ya miaka miwili kupita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kwamba kwa Serikali kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya kesi hiyo je, inakubaliana na ndoa za utotoni. Kesi aliyokuwa anaizungumzia ni miscellaneous civil cause No. 5 ya 2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza kama ni halali kukata rufaa baada ya miaka miwili kupita ni suala la procedure na kwa vyovyote vile swali hili linaweza likajitokeza rufaa itakapokuwa inasikilizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ndiyo hilo kwamba kwa Serikali kukata rufaa dhidi ya kesi hiyo inakubaliana na ndoa za utotoni. Ni wazi Serikali ilivyokata rufaa imetoa sababu na sababu hizi zitakuwa ni sehemu ya vitu vinavyobishaniwa ile rufaa itakapoanza kusikilizwa. Kanuni ya 64(1)(c) ya Kanuni za Kudumu za Bunge inakataza kuzungumzia jambo lolote linalosubiri uamuzi wa Mahakama na kwa hiyo hatuwezi kulizungumzia hapa. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja iliyoko mezani. Nitaanza kwa kuchangia kwa maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ambayo ilizungumza mambo mawili yanayohusu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Kamati imeshauri na kupendekeza kwamba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inahitaji kuimarisha Mfumo wa Uandishi wa Sheria pamoja na usimamizi wa mikataba kwa namna ambayo itaweza kusaidia kulinda maliasili zetu za Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba ushauri huo wa Kamati umepokelewa na kwamba hatua tayari zimeanza kuchukuliwa. Katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali sasa tunaanza kujenga uwezo mahsusi kuiwezesha ofisi hiyo iweze kushughulika na hii mikataba, kwa sababu hii mikataba ina mambo ambayo yako a bit complex, yanahitaji utaalam wa juu. Kuna sheria za mikataba huko ndani, kuna sheria za uwekezaji, kuna sheria za Kimataifa, kuna sheria za aina mbalimbali ambazo zinahusika humo. Tumeligundua hilo na tunalifanyia kazi tuweze kuwa na wanasheria waliobobea katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu, hata Mheshimiwa Rais amechukua hatua kadhaa za kuweza kuiboresha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kiasi kwamba sasa inaweza ikakabiliana na changamoto na technicalities zote zilizomo katika masuala ya mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imetoa ushauri kwamba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iongezewe rasilimali ili iweze kufanya kazi zake vizuri. Naomba tu nikuhakikishie kwamba ombi hili limeshapokelewa tayari na Serikali, kwa maana ya kwamba bajeti ya mwaka huu nafikiri kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaongezeka kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna michango kadhaa ya Waheshimiwa Wabunge na baadhi imeelekezwa kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, labda nitaomba niizungumzie kidogo. Mheshimiwa Zuberi - Mbunge wa Liwale ambaye mchango wake pia umeongezewa nguvu na Mheshimiwa Richard Ndassa ambaye amezungumzia uwezo wa Wanasheria katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa kuingia mikataba kwamba pengine imeonekana mikataba hiyo haikuwa na tija na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, hatua zinachukuliwa. Mheshimiwa Rais ameanza kutusaidia kwa kuchukua hatua kuirekebisha na kuibadilisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sisi huko ndani tumejipangia mikakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ndassa alisema ni vyema sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikawa na specializations kule ndani. Tunakubaliana naye kwa asilimia mia moja. Yanapokuja masuala ya ujenzi, ni vema ukawa na mtaalam wa sheria za ujenzi; yakija mambo ya kodi, uwe na mtaalam wa sheria za kodi; yakija mambo ya mipaka, migogoro ya mipaka na kadhalika uwe na mtaalam wa sheria hizo na ndiyo ofisi nyingine za Wanasheria Wakuu duniani zinavyofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Ndassa kwamba tumeona hatuhitaji tu kuwa na wanasheria ambao wako specialized, lakini kuna baadhi ya maeneo tunahitaji tulete ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hata wataalam wasio wanasheria. Kwa mfano, una mambo ya construction ya ujenzi wa barabara, kwa kweli inafaa sana mkawa na engineer wa mambo ya barabara. Kuna mambo labda ya afya, ni vema mkawa na mtaalam wa mambo ya afya ambaye sio mwanasheria, atatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia na michango mingine nitapenda nijielekeze kwa mchango wa Mheshimiwa Lema, amezungumza kwa kweli kwa hisia juu ya mwenendo wa kesi mbalimbali na ametaja kesi ya Mwale, Ringo Tenga, Kitillya na Sioi; ninafikiri kwa ujumla sekta ya sheria ina lengo moja la kuboresha utoaji wa haki. Hilo ndiyo lengo la sekta ya sheria. Nikisema sekta ya sheria ninachukua kwa ujumla wake Mahakama, Wizara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ni vema nikalisema hili kwa sababu mchango huo unazungumzia kwa kweli kusimamia utawala wa sheria na alikuwa akipata mashaka kidogo tunapozungumza kwamba kama kesi iko Mahakamani tusizungumzie hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukitaka kuweka msisitizo katika kusimamia utawala wa sheria, ukitoa hoja ambayo inapingana na essence ya utawala wa sheria, inaleta matatizo kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana nyingine ni kwamba Mheshimiwa Mbunge nadhani alipenda kusema kwamba tusifungwe sana na taratibu zetu zinazosema tusilizungumzie suala linapokuwa liko Mahakamani. Hili liko katika Kanuni zetu za Kudumu za Bunge, kanuni ambazo Bunge lenyewe limetunga, Kanuni ya 64(1)(c) ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016 inasema kwamba tusijadili jambo ambalo Mahakama haijalitolea uamuzi; ni kanuni zetu. Hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi wazi kwamba Mahakama itafanya kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa wala kutiwa shinikizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatari ya kujadili mambo ambayo yako Mahakamani ni namna moja ya kuipa Mahakama shinikizo. Kwa hiyo, labda niseme tu kwamba wale wote tulioko katika sekta ya sheria, tunafanya kazi ya kuhakikisha kwamba mfumo wa sheria unakuwa bora zaidi. Mifumo yote duniani, hata ukienda Marekani, utakuta kuna matatizo yake. Watasema mfumo huu una shida na mfumo huu una shida. Siku zote kinachofanyika, ni kufanya juhudi ya kuuboresha. Basi tusipendekeze kuboresha mfumo wetu wa sheria kwa kuvunja sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo, huo ndio mchango wangu na ninaunga mkono hoja. Ahsante.