Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. Christopher Kajoro Chizza (18 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri na watendaji wote kwa kuleta hotuba hii. Napenda kuchangia maeneo mawili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzishwa kwa Mfuko wa Kinga ya Bei za Mazao (Price Stabilization Fund). Eneo hili limechangiwa pia na Mheshimiwa Bashe. Nilitamani kumpa taarifa lakini nikaamua kuleta mchango kwa maandishi. Kati ya miaka ya 2012 – 2014, Wizara ya Kilimo ilianzisha mchakato wa kuanzisha Price Stabilization Fund kwa mazao ya korosho, kahawa, pamba na tumbaku kwa lengo la kukabiliana na madhara yanayotokea pindi bei ya mazao zinapoanguka hasa katika masoko ya dunia. Sijapata habari kwa nini mchakato huo haukuendelezwa au kama uliendelezwa ulifikia hatua gani. Nashauri Mheshimiwa Waziri alipeleleze suala hili, inawezekana bado lina umuhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maafa yako ya aina mbalimbali kama vile njaa, ukame, moto, matetemeko, mafuriko na kadhalika. Leo napenda kuchangia suala la maafa yanayotokana na mafuriko. Mafuriko yanapotokea yanaathiri mazao, miundombinu kama ya biashara, reli, nyumba na kadhalika. Yako maeneo yenye mito ambayo mara kwa mara inaleta mafuriko yanayoharibu madaraja, barabara, reli, simu na kadhalika kama kule Kilosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ijipange kujenga mabwawa makubwa ambayo yatakuwa na manufaa makubwa mawili. Kwanza kuepusha uharibifu wa miundombinu na pili yatumike kwa kilimo cha umwagiliaji wakati wa kiangazi. Suala hili linahitaji utayari wa kukabiliana na majanga, je, Serikali inao mkakati wa disaster preparedness? Hasara ambayo Serikali inapata kutokana na gharama za kurudishia miundombinu inayohabiriwa na mafuriko ni kubwa lakini pia uharibifu unapotokea unasababisha fedha na rasilimali nyingine kuelekezwa katika ukarabati wa miundombinu badala ya kuelekezwa kenye maeneo (miradi) mipya ya maendeleo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE.DKT. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wake wote kwa hotuba nzuri. Nimesikiliza hotuba kwa makini sana, imenikumbusha mambo kadhaa yanayohusu mawasiliano Serikalini Standing Orders na hata Financial Orders (Stores Regulations) nakadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC.Katika kupitia hoja za ukaguzi za CAG zinazohusu Serikali za Mitaa na baada ya ziara ya kukagua miradi katika Halmashauri 12, nimejiridhisha kwamba Serikali inaweza kupunguza hoja za ukaguzi kama watumishi wanaopewa dhamana kuwa Maafisa Masuuli (DEDs) wangepata uelewa wa shughuli za Serikali.Watendaji wengi wakiwemo Wakuu wa Idara wapo wasiojua kanuni na taratibu za uendeshaji shughuli za Serikali. Baadhi yao hata hawajajua nini maana ya uwajibikaji na utunzaji wa siri za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kamani gharama kuwapeleka viongozi wa Serikali kufundishwa katika Chuo cha Utumishi Serikalini, nashauri Chuo na Maafisa Waandamizi wa Serikali wafanye semina hizo katika maeneo ya kazi. Athari ya kuwa nawatumishi wasiojua Miiko ya Utumishi (The DOS and DONTS) inaweza kuigharibu Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria na watendaji wote kwa kuleta hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika eneo la urejeshwaji wa wahalifu wa kimataifa katika makosa ya jinai (P.36). Tanzania inapakanana nchi za jirani za Maziwa Makuu. Kwa mfano,Mkoa wa Kigoma umepakana na nchi jirani za Congo DRC, Rwanda na Burundi. Kuna matukio mengi ya kihalifu yanayohusishwa na raia wanchi jirani kuvuka mipaka kuingia Tanzania na kufanya uhalifu kwa kupora mali za wananchi, kuteka, kubaka na wakati mwingine kufanya mauaji. Matukio kama haya yanatokea Kakonko, Kobondo na Kasulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine nashawishika kuamini kwamba wahalifu hao wa kigeni wanao wenyeji wanaowawezesha kuingia na kutoka nchini bila kutiwa nguvuni. Je, Wizara inazo taarifa za wahalifu wa kigeni (wakiwemo wakimbizi) katika Mkoa wa Kigoma ambao wamerejeshwa nchini ili wajibu mashtaka? Katika eneo hili, naishauri Wizara kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani hususan Polisi na Uhamiaji ili kudhibiti wimbi la uhalifu unaoaminika kutekelezwa na wenyeji kwa kushirikiana na wageni ambao inasemekana wakishavuka mipaka kwenda kwao hawapatikani kwa urahisi kuja kujibu mashataka yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru na nafasi hii naomba kwanza na mimi niwapongeze mawaziri hawa mahiri kabisa ndugu yangu Mpango na dada yangu Kijaji, kwa kweli ninyi ni mahiri kwa sababu hata mnavyojenga hoja zenu na mnavyojibu maswali yetu hapa inaonesha kabisa kwamba ninyi ni mahiri na kwa maana hiyo ndio maana mmetuletea bajeti proposal ambayo pia ni mahiri inatekelezeka, kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)

Pia naomba kabla sijaingia kuchangia niwashukuru kwa sababu Serikali inapotenga bajeti hata kama mambo mengine yanajitokeza hata kama hatuwezi tukatekeleza bajeti yote kila mwaka, kwa kweli sidhani kama kuna bajeti ambayo inatekelezwa 100% lakini ukiweza kuitekeleza kiwango percentage fulani hilo ndilo tunalolitaka. Kwa maana hiyo nataka niwashukuru leo hii nikiwa hapa hapa nataka niwashukuru Serikali yangu sikivu dada yangu Ndalichako amepeleka fedha shilingi milioni 66 kule Kigoma kwenye shule ambayo aliahidi alipotembelea kule shilingi milioni 66; nakushukuru sana Mheshimiwa Ndalichako nashukuru sana Serikali kwa sababu ndio maana ya kutenga bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikiwa hapa hapa nimepata taarifa kwamba Profesa Mbarawa ametuma ma- engeneer kule kwangu baada ya kukagua miradi ya maji ambayo imejengwa wakati ule wa vijiji kumi tukapoteza shilingi bilioni 1.8, miradi haikujengwa vizuri lakini akaja akaahidi kwamba sasa nitatuma wataalam na wataikarabati ili iweze kufanya kazi iliyokusudiwa na hapa nikiwa hapa hapa nimepata taarifa kwamba ametuma kwa kweli nakushukuru sana, naishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na mwenzake na Wizara nzima kwa kuleta pendekezo la kuondoa tozo hizi mbalimbali 54 na nitajikita kwa chache kama muda utatosha nitakwenda kwa mambo mengine. Naomba nizungumzie pendekezo la marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, nadhani iko kwenye ukurasa wa
57. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi nadhani alikuwa Mheshimiwa Shabiby alizungumzia masuala ya mashine za EFD, na hapa nimeona Serikali inapendekeza kuondoa ushuru au kupunguza ushuru wa mashine za EFD kutoka 10% mpaka 0%. Kwa kweli ni jambo jema kwa sababu mashine hizi zinatusaidia kukusanya mapato. Nataka nikwambie Mheshimiwa Waziri, mimi niliwahi kuhudhuria mkutano wa TCCIA na alikuja mtu wa TRA akatufundisha jinsi mashine zile zinavyoagizwa. Akatuonesha pia kwamba mashine zile kama zilivyo gadgets nyingine hizi za simu, hata zile nazo watu wanaweza ku-temper nazo na kwa maana hiyo mashine zile wakati mwingine zinaweza zikawa hazitoi taarifa sahihi, zikawa ama zinaiumiza Serikali au zinamuumiza mlaji. Kwa hiyo, mimi ushauri wangu hapa ni kwamba mashine hizi zikaguliwe mara kwa mara, kwa sababu mtu huyu aliyetuambia alikuwa mtu wa TRA mwenyewe. Naamini watu wa TRA ndiyo wanaozisimamia mashine hizi, bila shaka alikuwa anasema kitu anachokijua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la pili kwa Mheshimiwa Waziri, kwa mfanyabiashara anayetaka kutunza taarifa zake ili baadaye aweze kujikagua au akaguliwe anahitaji kutunza kumbukumbu. Mashine nyingi za EFD hasa hizi za kwenye mashine za petrol ukiweka nyumbani baada ya miezi mitatu, minne haisomeki tena yamefutika yote, kama hujaweza kuzipiga photocopy basi hizi taarifa na kumbukumbu utakuwa hunazo tena.

Kwa hiyo, naomba kwa kweli hizi ziangaliwe upya, kama ikiwezekana zikaguliwe, kama ni mashine ziwe improved kwa sababu tunapopata zile risiti tunazihitaji kuzitunza ili mwisho wa mwaka tuweze kufanya tathmini kwamba na sisi katika biashara zetu tumefanya nini, lakini unapokwenda kukagua tena risiti zako unakuta haisomeki huna tena mahali pa kufanyia reference. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kidogo sasa nizungumzie habari ya sukari; umependekeza kupunguza ushuru wa sukari hasa ile ya matumizi ya kawaida (brown sugar) kutoka asilimia 100 kwenda asilimia 35. Hili ni jambo ambalo nadhani mara nyingi karibu kila mwaka tunapopata upungufu wa sukari linajitokeza na kwa kushirikiana na wenzetu Afrika Mashariki linatekelezwa. Jambo ambalo sikuona Mheshimiwa Waziri labda sikusoma vizuri, lakini sikuona ukizungumzia habari ya sukari ya viwandani (industrial sugar).

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaja hapa nimeongea na Bodi ya Sukari, wakaniambia mahitaji ya sukari yote yaani ile ya mezani na ya viwandani tani 670,000. Mahitaji ya viwandani kwa maana ya sukari ile ya kutengeneza bia, pipi, biscuit na vitu vingine peremende ambavyo ni viwanda hivyo ni tani 155,000. Sukari yote hii tani 155,000 hakuna inayozalishwa ndani, hakuna labda kama wameanza sasa, lakini mimi ninavyojua viwanda vyetu vyote TPC, Kagera, Mtibwa, Kilombero sidhani kama kuna kiwanda kinachozalisha industrial sugar, yote hii inatoka nje. Kama inatoka nje kwa uzoefu najua na yenyewe huwa inasamehewa kodi na ikisamehewa kodi sukari hii ikiingia basi inabidi kwa kweli iangaliwe vizuri maana uzoefu umetuonesha wakati ule wa sakata la sukari kwamba sukari hii hii ambayo inaingizwa ikiwa imesamehewa ushuru mara nyingine tena unaikuta kwenye supermarkets ikitumika kama sukari ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili siyo jambo zuri, kwa kweli hata kwa wafanyabiashara siyo jambo zuri lakini hata kwa walaji maana yake ile sukari sidhani kama inatakiwa itumike kwa ajili ya chai au kwa ajili ya uji. Ile ni purely kwa ajili ya viwandani, I stand to be corrected, lakini mimi ndivyo ninavyoelewa, sasa sikuiona ikizungumziwa katika hotuba yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya kawaida ni tani 515,000 na uzalishaji wa ndani mwaka huu kwa brown sugar nimeambiwa ni tani 359,219 angalau kwa mwaka huu. Ukitazama hesabu zote hizi ukijumlisha ile sukari ya viwandani na sukari ya mezani ambayo ni upungufu wa tani 155,781 unakuta bado tuna upungufu wa zaidi ya tani laki tatu na kitu. Maana yake ni kwamba lazima tutaendelea kuagiza sukari na hii ya industrial sugar hii ndiyo hasa nataka niizungumzie.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri, mimi ushauri wangu ni kwamba tuongeze uwekezaji katika mashamba ya miwa, lakini mashamba ya miwa hayawezi kuendelezwa bila umwagiliaji. Mashamba ya miwa lazima yaende sambamba na umwagiliaji, yako mazao karibu matatu ambayo sasa kitaalamu huwezi uka- break even bila kumwagilia. Moja ni miwa, lingine ni mpunga na lingine ni mazao ya bustani (hot cultural crops). Mazao haya sitaingia kwa undani kwa nini, lakini huwezi uka-break even bila kumwagilia, mengine utakuta kwamba hata circle yake uzalishaji yanakwenda zaidi ya miezi sita hakuna mvua inayokwenda zaidi ya miezi sita katika nchi hii lazima ufanye supplementary irrigation.

Kwa hiyo, katika kuwekeza katika uzalishaji wa miwa ni lazima tuongeze uzalishaji, tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji vinginevyo hatutaweza ku-break even. Kwa maana hiyo ni kwamba wale wanaolima miwa wakiwa ni wazalishaji wakubwa wao wanaweza kuweka miundombinu yao, lakini wale wana-nuclears farms, outgrowers lazima wasaidiwe. Ukienda Kilombero kuna outgrowers, wale hawawezi kujiwekea miundombinu wenyewe ya umwagiliaji ili wazalishe miwa mingi ya kukiuzia kiwanda kwa hiyo hapa ni lazima Serikali itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu namba mbili, naomba sasa kwa kuwa viwanda vyetu vya ndani havizalishi sukari ya viwandani na ninajua sababu kubwa, sababu kubwa ni kwamba wanaogopa kuweka mitambo ile ya kusafisha sukari maana ile industrial sugar ile siyo sukari nyingine ni kwamba ni hiyo hiyo inakuwa refined vizuri, sasa hawaiweki hii mitambo hii. Kwa hiyo, ninaomba wakati tunawahamasisha wawekezaji hawa tuwawekee na component hii kwamba jamani eeh mnapotuzalishia sukari mjitahidi kuweka na mitambo ya kusafisha sukari hii tuzalishe sukari ya viwandani. Maana sukari ya viwandani hii ni malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu, viwanda hivi vya pipi vinginevyo viwanda hivi tutaendelea kuagiza malighafi kutoka nje kwa ajili ya kulisha viwanda hivi. Ushauri wangu namba tatu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba nimeshausema lakini nataka nirudie, industrial sugar isiuzwe kama sukari ya kula mezani, isikutwe katika supermarkets. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nirudi tena kwenye kilimo, wengi wamezungumzia kilimo, wamezungumzia umwagiliaji na kwamba ili tutoke kwenye agrarian reforms sasa tuingie kwenye mambo ya viwanda, kilimo bado ndicho kitaendelea kuwa mhimili wa kutoa malighafi. Ninachotaka kuzungumza…. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. DKT. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ENG.CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri na wasaidizi wenu wote kwa kazi nzuri katika masuala ya Muungano na Mazingira. Kipekee, naipongeza Serikali kwa hatua yake ya kuondoa mifuko ya plastiki sokoni ifikapo tarehe 31 Mei, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika maeneo matatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania siyo kisiwa. Kwa kuwa nchi nyingi zilizoendelea zinaratibu matumizi mazuri ya mbegu za GMO, nashauri wataalam waendelee kufanya utafiti wa kitaalam hususan kwenye mbegu za mazao zinazotumia teknolojia ya GMO ili kujua faida na madhara yanayotokana na teknolojia hiyo badala ya kuchukua uamuzi wa jumla wa kuikataa teknolojia ya GMO. Kwa mfano, utafiti umeonesha kuwa uzalishaji wa pamba kwa kutumia teknolojia ya GMO umeongezeka maradufu katika nchi zinazozalisha pamba kwa GMO (Wizara ya Kilimo wanazo takwimu).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiongeza uzalishaji wa pamba tutawezesha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vya nguo tunavyoanzisha sasa. Hata hivyo, kutakuwa na haja ya kufanya utafiti wa kina kuhusu matumizi ya mafuta ya kula yanayotokana na pamba itakayozalishwa kwa teknolojia ya GMO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi makubwa ya maji ni yale ya kilimo cha umwagiliaji kwa sababu consumptive use ya mimea inayomwagiliwa ni kubwa kuliko matumizi ya nyumbani (domestic use), viwandani na yale ya miradi ya kuzalisha umeme ambayo consumptive use ni sawa na hakuna kwa sababu karibu maji yote yanayotumika kuendesha mitambo yanarudishwa kwenye mto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kushirikiana kwa karibu na Wizara inayohusika na kilimo cha umwagiliaji na Wizara ya Maji, makampuni makubwa ya miwa (sukari) na mashamba makubwa ili wazingatie mambo muhimu yafuatayo:-

(a) Matumizi sahihi ya maji kwa mazao husika (crop water requirements) na water rights ili kuepuka matumizi makubwa yanayosababisha vyanzo vya mito kukauka.

(b) Kulinda uharibifu wa ardhi kwa chumvi na kuwa na kilimo endelevu. Kila mradi wa umwagiliaji, hasa ile ya flooding iwe na miundombinu ya kutoa maji ya ziada shambani (drainage systems) kwa sababu ukosefu wa miundombinu hiyo husababisha chumvi kuongezeka (salinity) na ardhi inaharibika. Gharama za kurejesha ardhi inayoharibika kwa salinity ni kubwa sana.

(c) Usimamizi wa sheria nyingine zinazoshabihiana na Sheria ya Mazingira, mfano Sheria ya Rasilimali za Maji ya 2009. Wenye viwanda vinavyotumia maji ni lazima waheshimu sheria hii pamoja na sheria nyingine. Katika miaka ya 1990, kulikuwa na mgogoro mkubwa kwenye Kiwanda cha Karatasi Mjini Moshi (Kibo Pulp and Paper Board). Tatizo lilianza pale ambapo kiwanda kilipewa water right kwa ajili ya kutumia kiwandani kuzalisha karatasi. Katika kiwanda hicho, matumizi mengine yalikuwa ya kemikali ya aluminium sulphate ambayo ina sumu (toxic).

Sheria ya Rasilimali Maji iliwataka wenye kiwanda kujenga mtambo wa kusafisha maji (treatment plant) kabla ya kuyarudisha maji katika Mto Karanga baada ya kuyatumia kiwandani. Kiwanda hakikufanya hivyo badala yake kilichepusha maji katika mfereji na kuwapelekea wakulima wa mpunga. Matokeo yake yalikuwa mawili; moja, wakulima waliwashwa na sumu ya Al (SO ) ; pili, mazao ya mpunga yalipungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana suala hili lilisharekebishwa kwa sababu wanamazingira waliingilia. Ushauri wangu ni kwamba sheria zote ambazo zinashabihiana na utunzaji wa mazingira, zisimamiwe vizuri na zieleweke kwa ngazi zote katika Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kuleta hotuba nzuri Bungeni.

Mheshimiwa Spika, Kampeni ya Uzalendo yenye kaulimbiu “Kiswahili Utashi Wetu, Uhai Wetu” imenigusa sana. Umuhimju wa lugha unaonekana siku zote katika kufikisha taarifa sahihi kwa walengwa. Lugha isipoeleweka, hata ujumbe unaotumwa haufiki vizuri na wakati mwingine inawezekana kusababisha madhara.

Mheshimiwa Spika, watoto wadogo ni wepesi kujifunza lugha, wakifundishwa lugha vizuri wanadaka mafundisho haraka na kutumia mafundisho hayo katika maisha yao ya kawaida. Ili kuwajengea uwezo watoto wetu ni lazima lugha fasaha ya Kiswahili itumike katika mafundisho, mihadhara, makongamano na kadhalika. Kuna neno kama “NANILII” ambapo vijana wengi hata wa shule za sekondari na vyuo vikuu wanalitumia sana, mimi silipendi. Katika kuhamasisha uzalendo wetu, ni muhimu sana kutumia lugha fasaha ya Kiswahili kutoa mafunzo kwa vijana wetu katika shule, vyuo na wahariri wa magazeti na kadhalika ili kupeleka ujumbe sahihi kwa umma.

Mheshimiwa Spika, Muungano wetu. Bunge hili kupita mjadala wake katika bajeti ya Makamu wa Rais limedhihirisha kwamba kuna haja ya kutoa elimu ya Muungano kwa watu wote (elimu kwa wanafunzi wadogo na watu wazima) ili dhana ya Muungano ieleweke vizuri kwa watu wote. Nashauri Wizara hii ishirikiane na Wizara inayoshughulikia Muungano ili kuratibu mafunzo ya uzalendo, ukiwemo Muungano wetu kwa watu wote. Katika hili, lugha fasaha ya Kiswahili ni lazima itumike vizuri, vyombo vyote vya habari vitakavyoshiriki vielekezwe kutumia Kiswahili fasaha katika kufikisha ujumbe kwa walengwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. DKT. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa kuandaa Hotuba na Hoja iliyowekwa mezani.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia eneo moja tu la hali ya usalama wa wananchi katika Mikoa inayopakana na nchi jirani hususan katika Mkoa wa Kigoma. Katika Mkoa wa Kigoma kuna mwingiliano wa wahamiaji/wageni haramu ambao mara kwa mara wanavuka mpaka wa nchi na kuingia nchini wakati mwingine wakiwa na silaha, tena za kivita. Wakati mwingine wahalifu hawa wanaingia nchini kwa kisingizio cha kufanya vibarua mashambani na baadaye wanafanya uhalifu. Uhalifu wa mara kwa mara ni pamoj na kuteka magari, kuua na kuwaibia mali abiria, kuvamia nyumba, kuiba na kubaka wanawake na wasichana na kufanya uhalifu mwingine.

Mheshimiwa Spika, binafsi nimekuwa nafanya mawasiliano ya mara kwa mara na Mheshimiwa Waziri ili kuonesha uzito wa tatizo. Kwa kuwa wahalifu wanavuka mpaka tena wakiwa na silaha, nashauri Wizara yake ishirikiane na Wizara ya Ulinzi na JKT kudhibiti wahalifu kuvuka mpaka wa nchi wakiwa na silaha. Aidha, pale ambapo wahalifu wanafanikiwa kuvuka na kuingia nchini, Wizara yako iangalie uwezekano wa kuanzisha Kanda Maalum ya Kipolisi itakayodhibiti maeneo korofi hususan katika Wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu na Ngara, katika Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyomweleza Mheshimiwa Waziri tulipokutana katika kikao chake na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka Mkoa wa Kigoma, kuna kila dalili kwamba wageni na wahamiaji haramu wanaofanya uhalifu wana ushirikiano mkubwa na wananchi wenyeji wa maeneo husika. Naishauri Wizara itumie ujuzi na pengine kuwaruhusu wananchi kufanya/kupiga kura za siri ili kuwabaini wananchi wanaoshirikiana na wahalifu kutoka nje. Naamini Wizara ina wataalam wa kuendesha zoezi hilo kwa ufanisi bila kuathiri wananchi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nitaongelea mambo mawili tu. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na viongozi wote wa Wizara hiyo kwa kuleta hotuba nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, nataka niongelee mambo mawili tu; moja ni Mfuko wa Barabara; la pili ni kasi ya ujenzi wa barabara za lami hususan katika Mkoa wa Kigoma.

Mheshimiwa Spika, kabla hatujaingia kwenye uchumi wa kati na uchumi wa viwanda bado Watanzania tunategemea kilimo na tutaendelea kutegemea kilimo kama ndiyo mhimili wa uchumi wetu. Wataalam wanasema asilimia 60 ya upotevu wa mazao hutokea katika level ile ya postharvest, yaani miundombinu hafifu ya kuhifadhi mazao, lakini pia miundombinu hafifu ya kusafirisha mazao kutoka shambani kwenda sokoni (farm to market roads). Hapa ndipo ninapotaka kusisitiza umuhimu wa Mfuko huu wa Barabara. Nikitazama kwa mfano mkoa wangu wa Kigoma wote kwa pamoja tumetengewa shlingi milioni 694 ndizo ninazoziona kwenye kitabu hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hizi ambazo ndizo zinatarajiwa zinategemewa na wakulima watoe mazao yao wasafirishe sasa waje kwenye truck road tunazojinga, kupeleka sokoni, bado bado sana. Kwa kweli tunahitaji mfuko huu upate pesa, TARURA wapate pesa tuwajengee wakulima miundombinu ya barabara waweze kutoa mazao yao kwenda shambani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niunganishe hapa hapa kwamba katika Jimbo langu kule tumejenga soko la kisasa, la Kimataifa katika Kijiji cha Muhange, soko ambalo litatufanya sisi tuunganishe tufanye biashara na wenzetu wa Burundi. Soko hili ili liweze kufanya kazi vizuri sasa, ni muhimu barabara ile inayojengwa kutoka Nyakanazi kwenda mpaka Kigoma ipate barabara ya kiungo kutoka Kakonko kupita Kinonko, kwenda Gwarama, kwenda mpaka Muhange sokoni ili sasa wananchi wetu waweze kufanya biashara na ndugu zao wa Burundi kwa kutumia barabara nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakwenda haraka kidogo. Miundombinu hii tunayoijenga sisi watu tunaotoka Kigoma; kuufungua Mkoa wa Kigoma tunahitaji sasa miundombinu hii ijengwe kwa kasi kubwa ili mkoa huu uweze kuwa hub ya biashara hususan katika baadhi ya nchi za maziwa makuu. Tatizo tulilonalo kama nilivyosema awali ni usimamizi au ucheleweshaji wa ujenzi wa barabara hizi.

Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Nyakanazi, mpaka Kabingo pale kijijini kwangu mpaka hivi tunavyozungumza tangu mwaka 2014 ni asilimia 60 tu ambazo zimetekelezwa tangu 2014. Tumeikagua tukiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu tukakuta hata Mkandarasi mwenyewe yuko nje ya mkataba (out of contract) kwa siku 986. Naiomba Wizara isimamie kwa karibu Mkandarasi anayejenga barabara hii Nyakanazi mpaka pale Kabingo ili aweze kuongeza kasi ya utekelezaji. 2014 - 2019 asilimia 60, kwa kweli tunaendelea kuchelewa sana.

Mheshimiwa Spika, naomba tu nimalizie kwa kuishukuru Serikali. Nimeona katika kitabu sasa, mmesema kutoka Kabingo kwenda Kasulu kwenda Kibondo Kasulu hadi Manyovu, Benki ya Maendeleo ya Afrika imetutengea shilingi bilioni 15 ili tuweze kujenga kilomita hizi 260 za barabara hii. Huu ndiyo mwendo ambao kwa kweli kama tutatekeleza, hii itapelekea kufungua…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika hoja hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wa Wizara hii ambayo nami niliwahi kuitumikia kwa kuleta hotuba nzuri ambayo inatuelekeza tuchukue mwelekeo gani ili kuweza kuwafikishia wananchi wetu maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua bado ziko changamoto nyingi, najua yako malengo mengi ambayo hatujayafikia, lakini hatuwezi kuyafikia bila kuwa na utaratibu ambao tumejiwekea. Kwa sababu hii, naanza moja kwa moja kuunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hata kama sijaunga mkono, haitatusaidia sisi kueleza ule upungufu ili akaufanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono kabisa kwa asilimia mia moja ili niweze kusema mambo yangu sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa na Mheshimiwa Waziri mwenyewe kwa sababu kwa nyakati tofauti Waheshimiwa hawa wamefika katika Wilaya yangu ya Kakonko, wakakagua miradi ya maji ambayo ni kero kubwa, miradi ambayo haijakamilika tangu miaka karibu kumi iliyopita na kwa nyakati tofauti wakatoa maelekezo ni hatua gani zifanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua nimepitia kwenye kitabu hiki, nimekuja leo tu, sikuwepo kwa muda mrefu kwa sababu zisizozuilika, baadhi ya mambo nimeona yametekelezwa, lakini yako mengine ambayo hayakutekelezwa; na hayo ndiyo nataka angalau nizungumze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri mara kadhaa anapojibu maswali anasema vizuri sana kwamba maji ni uhai, maji hayana mbadala na huo ni ukweli. Mahali ambako hakuna maji hakuna uhai, hata watu wanaokwenda mwezini huko au katika sayari zingine wanaridhika kabisa kwamba kule hawajaona maji na kwa kuwa hakuna maji hata viumbe hai havionekani. Kwa hiyo Mheshimiwa Aweso anachosema ni kweli kabisa kwamba maji hayana mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sera yetu ya Maji, nakumbuka vizuri nadhani ilikuwa mwaka 2002 na mimi nilishiriki, tulikwenda mpaka Zimbabwe mpaka South Afrika tukajiwekea malengo kwamba ifikapo Mei, 2010 upatikanaji wa maji mijini miaka ile ungekuwa asilimia 90, upatikanaji wa maji vijijini mwaka ule ungekuwa asilimia 65. Najua bado ziko changamoto nyingi, kila unapokwenda sasa hivi kilio ni maji, maji, maji. Upatikanaji wa maji Wabunge wengi wamezungumza, mimi sikuwepo lakini nilikuwa nafuatilia angalau kwa vyombo vya habari, upatikanji wa maji bado hatujafikia malengo, bado hali ni tete. Kwa mfano katika Halmashauri ya Kakonko, idadi ya vituo vya maji ni 576, vituo visivyofanya kazi 283, ukokotoaji wa upatikanaji wa maji inasemekana ni asilimia 52 au 53 kulingana na taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nafuatilia wakati mwingine huu ukokotoaji wa upatikanji wa maji na naomba Mheshimiwa Waziri nimefuatilia nikagundua wakati mwingine ukokotoaji hauendani na hali halisi, kwa sababu kwa mfano nilimuuliza Mhandisi mmoja unakokotoaje upatikanaji wa maji ukapata percentage? Akaniambia naangalia visima vilivyopo huenda vinafanya kazi au havifanyi kazi yeye anahesabu visima vilivyopo. Anaangalia kisima kimoja kinatoa maji kiasi gani, per capita onsumption ya maji vijijini na mijini ni kiasi gani? Sasa yeye anajumlisha anasema upatikanaji wa maji kulingana na visima vya maji vilivyopo kulingana na vyanzo vya maji ni huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili naomba lisahihishwe kwa sababu huo si ukokotoaji halisi, huo ni ukokotyoaji ambao unajumuisha vyanzo vinavyotoa maji, vyanzo vya maji ambavyo miradi bado haijaanza kufanya kazi au imekamilishwa lakini haitoi maji, lakini akikokotoa anasema tumepata asilimia kadhaa. Haitusaidii sana kwenda namna hii, ni bora kabisa kwenda na hali halisi ili tunapokuja sasa kuiomba Serikali twende tukiwa na takwimu halisi, ni afadhali tuwe na miradi michache inayotekelezwa mara moja na kutoa maji, halafu tukimaliza tunahamia kwenye miradi mingine kidogo kidogo hivyo kuliko kujiwekea malengo au takwimu ambazo hazitoi hali halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri upatikanaji wa maji katika Wilaya yangu ya Kakonko bado sidhani kama ni asilimia hii. Mheshimiwa Waziri alipokuja mwenyewe nilimpeleka akaona alitembelea baadhi ya miradi akaona mahali ambako miradi mingine walimwambia imetekelezwa kumbe iko asilimia tano, pale Kakonko Mjini aliona mwenyewe, tulikwenda katika miradi mingine Gwijima, tukaenda Kiduduye, Miradi ya Muhange, Katonga, Kiga, Gwalungu, Nyeguye, yote hiyo ama haifanyi kazi au imetekelezwa kwa kiwango ambacho hakistahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ziko wazi kwa nini baadhi ya miradi haitekelezwi vizuri. Naomba ku-declare interest mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC, nimepata nafasi kupitia miradi mingi hasa ya ujenzi, barabara, shule, maji, changamoto kubwa ambazo niliziona na hizi ndizo nataka nizisemee halafu niketi, lakini Mheshimiwa Waziri azifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo nimeiona katika miradi yetu ya maji, Mheshimiwa Waziri amesema tuna uwezo wa kitaasisi katika mikoa, katika mabonde ya maji na katika halmashauri na nimesoma katika kitabu chake ukurasa nadhani wa 12, lakini hali halisi kwa kweli bado bado hasa katika halmashauri, bado uwezo wa kitaasisi ni mdogo na uwezo huu naupima. Mimi nimekuwa katika Kamati ya LAAC tunachokifanya, tunatazama kwanza taarifa za CAG, halafu tuna- single out miradi fulani Fulani, unaikagua. Tulichokibaini na wenzangu akina Mheshimiwa Mwalongo na Waheshimiwa wengine bila shaka watakubaliana na mimi, tulichokibaini ni uwezo mdogo kwanza katika mchakato mzima wa kutoa zabuni hizi, zabuni hizi zinatolewa kwa wakandarasi, baadhi ya wakandarasi wasio na sifa hawana…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara kwa kuleta bajeti yenye vipaumbele vya miundombinu inayochochea ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, kwenye utekelezaji, kipande cha barabara ya Kidahwe – Kibondo - Nyakanazi kinachotekelezwa kutoka Nyakanazi ni Nyakanazi - Kabingo kilometa 50, siyo Nyakanazi - Kibondo. Nashauri Wizara isahihishe kwa sababu kati ya Kabingo na Kibondo kuna kilometa 50 ambazo hazina Mkandarasi, ndiyo maana kwenye mradi utakaofadhiliwa na AFDB zinaonekana kilometa 260 za Kabingo – Kibondo – Kasulu – Manyovu. (I stand to be corrected)

Mheshimiwa Spika, wakazi wa Mkoa wa Kigoma katika wilaya zote za Kigoma, Uvinza, Kasulu, Buhigwe, Kibondo na Kakonko wanafanyia biashara zao nyingi katika Kanda ya Ziwa, hususan Mwanza na Shinyanga. Naishukuru Wizara kwa kuliona hili na kutenga fedha za kujenga barabara yote ya Nyakanazi – Kabingo – Kibondo – Kasulu - Manyovu ili kuunganisha Mkoa wa Kigoma na mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kama ufuatao:-

(i) Mkandarasi wa Nyakanazi - Kabingo asimamiwe kwa ukaribu, he is very slow. Tulipokagua utekelezaji na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mkandarasi alikuwa ametekeleza asilimia 60 tu na tayari alikuwa na siku 986 nje ya mkataba.

Mheshimiwa Spika, nashauri kwa kipande cha Kabingo - Manyovu AFDB utaratibu wa fidia uanze mapema.

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara itekeleze ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ya 2015 ya kujenga kilometa tatu za barabara za lami Mjini Kakonko. Kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri, RC wa Kigoma, kupitia TANROADS ameshatuma Wizara ya Ujenzi makisio ya gharama ya kujenga kilometa tatu za Mjini Kakonko. Chonde chonde, hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kuleta hotuba nzuri. Nampongeza pia Mwenyekiti mpya wa Bodi ya TANTRADE aliyechukua nafasi niliyoiacha wazi baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu. Kipekee nampongeza Director General wa TANTRADE, Ndugu Edwin Rutagezuka kwa utendaji wake mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo nipende kuchangia na kushauri katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya vitambulisho vya Taifa katika kurasimisha biashara; kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, hadi sasa, vitambulisho vya NIDA vilivyopatikana ni takribani milioni 16 tu katika nchi nzima. Sharti la kutumia vitambulisho hivyo katika kurasimisha biashara lililowekwa na BRELA limezuia malalamiko kutoka wajasiriamali wengi ambao wanashindwa kusajiri na kurasimisha biashara zao kwa kutokuwa na vitambulisho hivyo. Ushauri wangu ni kwamba, BRELA iendelee kutumia vitambulisho mbadala hadi hapo Serikali itakapokuwa imewapa Watanzania wote vitambulisho vya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, utafutaji wa masoko ya mazao ya kilimo; masoko ya mazao ya kilimobado ni changaoto kubwa ukizingatia kwamba bei za mazao zinatawaliwa na uzalishaji katika nchi zinazotuzunguka na mahitaji yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri TANTRADE ijikite katika kufuatilia ubora wa mazao ya kilimo kwa matumizi ya chakula na viwanda kutafuta masoko ya mazao ya chakula, ni vema TANTRADE ishirikiane na Mashirika ya Kilimo na Chakula ya Kimataifa kama FAO na WFP ili kuwa na takwimu halisi za mahitaji ya mazao na kuwaelekeza wafanyabiashara kutafuta masoko hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ni muhimu TANTRADE ishirikiane na Wizara nyingine kama vile Wizara za Mambo ya Nje na Kilimo ili kubaini vikwazo vya usafirishaji wa bidhaa (mazao) kutoka Tanzania kwenda katika nchi nyingine ili kuviondoa. Mifano iliyopo ni pamoja na vikwazo vya kusafirisha mazao ya chakula kwenda katika nchi za Sudan Kusini kupita Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na Congo DRC. Kipekee napenda kujua status ya soko la muhogo la China.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha vituo vya kuunganisha zana za kilimo. Inakadiriwa kuwa Tanzania ina eneo la hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo ambapo eneo linalolimwa hadi sasa ni kama hekta milioni 10.1 tu (I stand to be corrected). Hata hivyo, eneo linalolimwa kwa kutumia zana (very roughly) ni kama ifuatavyo:-

Eneo linalolimwa kwa jembe la mkono 70%, eneo linalolimwa na wanyamakazi 20% na eneo linalolimwa kwa matrekta 10%, jumla 100%

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri, kwa kuwa ni vigumu kwa kila mkulima kumiliki trekta, ni vema Serikali ianzishe vituo vya kuunganisha, kukodisha na kuhudumia (serving) vituo vya zana za kilimo, yaani Tractor Assembling, Hiring and Service Centers) ambavyo vinatoa huduma kwa wakulima wetu ili walime maeneo makubwa zaidi. Vituo hivyo vitasaidia pia kutoa ajira za mafundi mbalimbali watakaoandaliwa na vyuo vya ufundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa Saturday Bonanza; wakati nikiwa Mwenyekiti wa TANTRADE, tulikuwa na mawazo ya kuanzisha magulio wa ajili ya kuwaelimisha wafanyabiashara wasio rasmi (Almaarufu-Machinga) ili waweze kutumia viwanja vya maonesho (SABASABA- Mwalimu Nyerere) Dar es Salaam. Je, mchakato huo umefikia wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwa kutumia mfumo huo, tungeweza kuwasaidia Wamachinga na kujua wenye bidhaa wanazoziuza na kuiwezesha Serikali kupata ushuru unaostahili kuliko hali ilivyo sasa mitaani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia naomba niungane na wenzangu niipongeze Serikali nzima kwa maana ya Rais na Serikali yote ambayo imetuletea Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ambayo nataka niishauri Serikali kwa sababu tunapojadili Mpango maana yake ni kuboresha rasimu hii, ndiyo process ya budgeting inaanza hivyo. Nianze na suala zima la disaster preparedness. Nimeona katika Mpango ambao Waziri ametuletea, nadhani ukurasa wa 85, sikumbuki vizuri lakini napenda nijikite hapo kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajenga miundombinu, tena ya gharama kubwa; viwanja hivi vya ndege, barabara, madaraja, miundombinu ya umeme, mabwawa makubwa kama haya ya Stiegler’s Gorge; miundombinu yote hii inataka pesa nyingi. Nachotaka kusema kwa kuwa tunajenga miundombinu hii lazima pia tuwe na utamaduni wa kuilinda miundombinu yetu tunayoijenga kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama siku za nyuma Serikali ilikuwa na lugha ya maintenance sasa hivi ni kama lugha hiyo inaanza kupotea. Kwa mfano zamani tulikuwa na Public Works Department inajenga barabara lakini kila mwaka kulikuwa na periodic maintenance na wanapita wanatengeneza; ile yote ilikuwa ni kuhakikisha kwamba miundombinu hii inayojengwa kwa gharama kubwa inatunzwa na inalindwa ili baadaye tusije tena kutumia pesa nyingi za bajeti ambazo tumepanga kwa ajili ya maendeleo kutengeneza miundombinu ambayo imeharibika. Kwa kufanya hivi tutaokoa gharama kubwa au kuepusha ile pesa ambayo imepangwa kwa bajeti ya mwaka huu tunaanza kuitumia kwenye kurekebisha miundombinu ambayo imeharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna majanga mengi, yako mafuriko ambayo kama tumekuwa tunafuatilia yamegharimu Serikali pesa nyingi, watu wamekufa, hata Kenya mambo haya yamewapata; yapo majanga yanayotokana na moto, yapo matetemeko, zipo radi, lakini vyote hivi vinapotokea lazima viigharimu Serikali, lazima Serikali irudi tena kwa sababu huwezi kuacha kitu kimekwishatokea ukasema tukiache kwa sababu hakimo katika mpango wa maendeleo. Kwa hiyo, nachotaka kuishauri Serikali yangu ni kwamba lazima tujenge utamaduni wa kuwa na utayari wa kupambana na majanga yanapojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano huu mradi mkubwa ambao tunaujenga wa Stiegler’s Gorge, mradi huu kwa kweli ni mfano mzuri. Ukitazama mradi kama huu tungekuwa na approach kama hii katika miradi mingi maana yake katika kuwa prepared kwa kujenga miradi hii siyo lazima kuweka bajeti tu kwa ajili ya kusubiri janga litokee maana majanga ni matukio, matukio ndiyo hayo majanga. Hata hivyo, katika utamaduni ule wa wa kusanifu miradi,kwa mfano, unajenga mradi wa bwawa, unatengeneza mradi ambao ni multipurpose, mradi kama wa Bwawa la Rufiji, utafua umeme, utatoa maji ya kunywa, maji ya kumwagilia; mradi huo unaweza kutengeneza flood control kwa maana ya kwamba hata haya mafuriko mengine ambayo yanajitokeza utakuwa umeyapunguza kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, approach hii ya kutengeneza miradi ambayo ni jumuishi inaweza kutufanya tukawa tayari kupambana na majanga kila yanapotokea. Kwa hiyo, natamani kuona kwamba katika miradi tunayoijenga tunajiwekea utaratibu wa kujikinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-declare interest; niko katika Kamati ya LAAC, nimetembelea miundombinu mingi midogomidogo; ujenzi wa madarasa, ujenzi wa health centers, public buildings nyingi, lakini sehemu zote ambazo nimepita kama nimeona nyingi labda ni moja au mbili, hata kukumbuka tu kuweka kitu kidogo kama mtego wa radi, hatukumbuki. Kila wakati unasikia radi imepiga darasani watoto wamekufa, walimu wameumia lakini unakuta hata kitu kidogo kama hicho tu; kuweka mtego wa radi kwenye jengo ambalo ni la public, kwenye makanisa yetu, hatukumbuki kuweka vitu kama hivyo. Kwa hiyo, nataka nijikite hapo, kwenye suala la disaster preparedness Serikali kwa kweli hata kama sio lazima kuweka kitengo na kukigharamia sana lakini kila sekta basi angalau ijikite katika kujiandaa na kupambana na majanga yanapotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni suala la kugharamia kilimo. Kilimo ndiyo kila kitu lakini Wabunge wengi wamelalamika, fedha tunazotenga kwa ajili ya kilimo bado hazikidhi mahitaji. Fedha tunazotenga kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji, tuna
23.4 million hectors, tumefanya hekta laki sita tu lakini fedha tunazotenga kwa ajili ya shughuli ni ndogo na bado tunataka twende katika uchumi wa viwanda, ili tujenge uchumi wa viwanda lazima kilimo nacho tukipe msisitizo. Tutenge fedha za utafiti kwa ajili ya pembejeo, tutenge fedha za kilimo kwa ajili ya maghala, kujenga silos ili kilimo hiki kikue kiweze kutusaidia kutoa inputs kwa ajili ya viwanda hivi tunavyotaka kuvijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni wanachama wa SADC. Nakumbuka mwaka 2003 kulikuwa na mkutano Maputo, pale Maputo nchi zote wanachama walitoka na Azimio la Maputo 2003 (Maputo Declaration). Maputo Declaration iliazimia na sisi tulisaini kwamba kila nchi mwanachama itenge asilimia 10 ya bajeti yake kwa ajili ya kugharamia kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio lazima kwa mwaka mara moja utenge asilimia 10 lakini kuanzia mwaka 2003 mpaka leo natamani kuona on an incremental basis towards ten percent, kwamba kila mwaka tumeongeza kiasi gani ili angalau tufikie asilimia 10 ya bajeti zetu kwenda kwenye kilimo. Hilo namuomba Mheshimiwa Waziri na Waziri wa Kilimo waliangalie kwa sababu ni sisi wenyewe tulikubali kwamba tutatenga asilimia 10 kupeleka kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa bado niko kwenye kugharamia kilimo, naomba nizungumzie suala la Mfuko wa Kuhimili Bei za Mazao. Asubuhi nimemsikia Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe, alisema vizuri tu kwamba intervention ya Serikali kwenye masuala haya ya masoko ya mazao haitakuwa tena kama ilivyokuwa. Nami nakubaliana naye kwa sababu lazima turuhusu soko liji- regulate lakini masoko ya mazao ni very fragile. Matatizo yanapotokea lazima tuwe na utaratibu wa kuhimili mtikisiko wa bei hizi, hasahasa bei zinapoanguka katika masoko ya dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka fulani tulikubaliana kwamba tuanzishe Mfuko wa Kuhimili Bei za Mazao. Tukasema tuanze na mazao mkakati manne ya kahawa, korosho, tumbaku na pamba. Nakumbuka Wabunge wengi walikubaliana na jambo hili lakini tangu tumelizungumza na nafikiri mpaka leo sijapata mrejesho kwamba hivi uanzishaji wa utaratibu huu wa Mfuko wa Kuhimili Bei za Mazao angalau kusaidia wakulima ku-absorb shocks umefikia wapi?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Engineer.

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa jambo moja tu, nalo ni suala la usimamizi wa miradi (contract management). Hii culture ya usimamizi wa miradi (contract management) bado inatugharimu. Narudia tena kusema niko katika Kamati ya LAAC lakini mambo nayoyaona huko hasa kwa miradi midogomidogo Serikali inaingia hasara kubwa sana kutokana na poor contract management. Miradi mingi inaingia kwenye gharama ambazo sio za lazima, inaingia kwenye variation orders ambazo siyo za lazima. Yote hii inatokana na miradi ambayo haiwi managed vizuri. Kwa hiyo, ipo haja kabisa kusimamia suala hili la kusimamia miradi kwa ajili ya kuokoa fedha na gharama za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa haya machache, sisi tunasema kusema mengi sio kuyamaliza, mengine tutaendelea kuchangia, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya pamoja ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu Uwajibikaji Kisheria na Fidia kwa Madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa katika Kutekeleza Itifaki ya Cartagena (Nagoya – Kuala Lumpur Supplementary Protocol on Liability and Redress on Cartagena Protocol on Biosafety) pamoja na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Haki Miliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea. (Protocal for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeder’s Rights) in The Southern African Development Community – SADC) pamoja na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Marrakesh wa mwaka 2013 unaowezesha upatikanaji wa kazi zilizochapishwa kwa watu wasioona, wenye uoni hafifu au ulemavu unaomfanya mtu kushindwa kusoma (The Marrakesh Treaty to Facilitate Access to Published Work For Persons Who Are Blind, Visually Impaired or Otherwise Print Disabled)
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami naomba niipongeze Serikali kwa kuleta maazimio haya. Kwanza hata mimi naona tumechelewa, tungeanza jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba moja kwa moja niipongeze Serikali kwa kufanya mabadiliko katika kanuni zile za matumizi salama ya bioteknolojia. Kwa wale ambao walikuwa wanafuatilia kwa jambo hili, jambo hili la Strict liability, hiki kipengele kwa muda mrefu kimekuwa kikwazo kikubwa sana kwa watafiti wetu katika nchi hii. Maana mtatiti anapoona kwamba yeye akifanya utafiti halafu yeye mwenyewe tena anakamatwa, anashikiliwa, anaadhibiwa kwa utatiti ambao ameufanya, basi amekuwa anakosa nguvu ya kuendelea na utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Ibara hii ya 12 ambayo Mheshimiwa Waziri wa Mazingira ameileta, kwa kweli naona imeleta ahueni na motisha kwa watafiti wetu kuendelea sasa kujikita kwenye utafiti. (Makofi)

Mwenyekiti Mwenyekiti, mbegu bora, mbegu zenye ukinzani na magonjwa, mbegu ambazo zinazalisha, zinaleta tija katika uzalishaji ndizo tunazozitaka. Tukijifanya sisi hatutaki kufanya utafiti, tutaendelea kutumia tafiti ambazo wenzetu wamefanya uko nje ambazo haziendani na ekolojia ya nchi yetu. Kwa hiyo, tusiogope kufanya utafiti katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo, nashauri tuache kabisa tabia ya kutotenga fedha za utafiti. Nakumbuka kabisa mwaka 2003 nchi yetu tulikubaliana, tuliridhia pamoja na ile nchi za SADC katika Azimio la Maputo, pamoja na nchi za AU kwamba nchi zetu zitenge kila moja asilimia kumi ya bajeti zake kwenda kwenye kilimo. Nasi tukajiongeza kwamba katika hiyo, asilimia moja iende kwenye utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina uhakika jambo hili tumelifanya kwa wakati gani, lakini kama tumechelewa, basi huu ndiyo wakati sasa tuanze kutenga fedha hizi, watafiti wetu wafanye kazi vizuri kwa uhuru, wapate motisha ili angalau waweze kutupeleka mbele sasa katika kutafiti mbegu za mimea ili tuweze kuongeza tija katika uzalishaji hasa wakati huu ambao tutahitaji zaidi kuzalisha malighafi za kilimo kwa ajili ya viwanda vyetu vya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri, tunapokwenda kwenye utafiti huu, tunazungumza pia hakimiliki za kulinda wagunduzi. Amesema vizuri Mheshimiwa Dkt. Ishengoma, watafiti hawa hawafanyi kazi peke yao, wanafanya kazi na wakulima. Baadhi ya watu watakaoathirika na matokeo ya utafiti yakiwa ni hasi au chanya, ni wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza tuweke utaratibu, tukitenga fedha za utafiti, tutenge fedha za kutosha za kutoa elimu kwa wagunduzi, wafanyabiashara wa mbegu pamoja na wakulima wetu ikiwa ni pamoja na kuwafundisha wakulima wetu wajue haki zao ni zipi nao wanalindwaje wakati wanapopata matatizo yanayotokana na matokeo hasi yanayotokana na utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono maazimio haya kwa asilimia mia kwa mia. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. ENG. CHRISTOPHER CHIZA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara kwa kuleta hotuba nzuri na kuibua changamoto.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, atakapohitimisha hoja yake naomba atoe maelezo kuhusu maeneo matatu yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ilileta muswada wa Sheria (mwaka 2013) ulioweka muundo wa Kitaasisi (Tume ya Umwagiliji) uliolenga kugatua madaraka na huduma za umwagiliaji kutoka ofisi ya kanda na kuanzisha ofisi za mikoa na kwenye halmashauri za wilaya.

Mheshimiwa Spika, hoja ya kuomba wataalam/ wahandisi wa umwagiliaji hawatoshi kusambazwa wilayani haina nguvu. Wataalamu wanaendelea kuzalishwa na wengine wanastaafu kila mwaka. Hata extension officers hadi leo hawatoshi lakini huduma za ugani zipo wilayani. Nashauri utekeleze yaliyomo katika Sheria ya Umwagiliaji kwa sababu Wabunge waliipitisha Sheria ya Umwagiliaji na Muundo wa Tume.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali; na Wizara ilianzisha mchakato wa Price Stabilization Fund kwa kuanzia na mazao ya tumbaku, kahawa, korosho na pamba. Mchakato huu umekwamia wapi? Je, bado kuna nia ya kuanzisha Commodity Exchange Market kwa ajili ya mazao ya kilimo?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara kwa kuleta hotuba nzuri. Napenda kuchangia maeneo mawili ya migogoro baina ya wafugaji na makundi mengine hususan wakulima na soko la samaki.

Mheshimiwa Spika, migogoro kati ya wakulima na wafugaji (pastoralists) imegharimu maisha ya watu, mifugo na uharibifu wa mazao. Wafugaji wanaohamahama kwa sehemu kubwa wanatafuta malisho na maji. Haya ndiyo maeneo yanayosababisha wafugaji kuchunga katika mashamba ya wakulima na wakati mwingine wanaingia katika maeneo yasiyoruhusiwa kama Hifadhi za Taifa. Hata mifugo wanaposafirishwa wakati mwingine wanaswagwa kupitia barabara kuu, wanaharibu barabara na kadhalika. Kwa nini usafirishaji wa mifugo usiwe na vyombo rasmi na inapobidi watumie National Stock Routes? Kama zimefifia, kwa nini zisifufuliwe?

Mheshimiwa Spika, suluhu ya migogoro ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja ni maandalizi ya matumizi bora ya ardhi, lakini kwa upande mwingine ni usimamizi wa sheria, sheria ndogo na kanuni zinazotawala matumizi ya ardhi. Aidha, ni muhimu Serikali ikajenga mabwawa maalum kwa ajili ya kunywesha mifugo na inapowezekana mifugo ijengewe mabirika ya kunywea maji (cattle troughs). Zamani Wizara ya Mifugo ilikuwa na kitengo cha kujenga mabwawa ya mifugo, kwa sasa ni vema watumie DDCA.

Mheshimiwa Spika, Soko la samaki (tuner fish); mwaka 2017 nilifanya ziara nchini Spain kutafuta soko la samaki aina ya tuner. Nilichokikuta huko ni kwamba, viwanda vya kusindika samaki hao vilikuwa vinaagiza samaki kutoka China. Sina uhakika kama samaki wote wanaotoka China kweli wanatoka huko. Hata hivyo, nilipofika Spain, walinipa ripoti iliyoandaliwa na wataalam kutoka Denmark inayoonesha kwamba tuner fish wanapatikana kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu kwa mwaka hapa Tanzania. Naleta swali hili Wizara ilifanyie kazi; je, ni kweli upatikanaji wa tuner fish hapa Tanzania ni mdogo na seasonal kiasi kwamba wawekezaji hawavutiwi kuanzisha kiwanda? (Mheshimiwa Waziri apeleleze).

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watndaji kwa kuleta mapendekezo ya mapato na matumizi mazuri. Baada ya kuchangia kwa mazungumzo sasa napenda kuchangia maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Haja ya Kuweka Mkakati Maalum wa Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji. Bado nchi yetu ni ya wakulima, kilimo kitaendelea kuwa muhimili wa kuimarisha utoshelevu na usalama wa chakula, kuchangia Pato la Taifa na pia kilimo kitaendelea kuwa chanzo cha malighafi ya viwanda ambavyo tunavijenga sasa. Ili tufikie malengo hayo, ni lazima tukubali kufanya uamuzi wa maksudi wa kuwekeza katika kilimo. Tanzania ilikubaliana na nchi wanachama wa SADC kupitia Azimio la Maputo kwamba kila nchi mwanachama itenge asilimia 10 ya bajeti yake kwenye sekta ya kilimo ili kuharakisha ukuaji wa sekta hiyo. Je, utekelezaji umefikia wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zifuatazo zinaonesha haja ya kuwekeza katika kilimo.

(1) Eneo linalofaa kwa kilimo ni 44,000,000 Ha

(2) Eneo linalolimwa ni 14,000,000 Ha

(3) Eneo linalofaa kwa umwagiliaji 29,400,000 Ha

3.1. High Irrigation Dev. Potential 2, 300,000 Ha

3.2. Medium Irrig. Dev. Potential 4,800,000 Ha

3.3. Low Irrig. Dev. Potential 22,300,000 Ha

3.4. Eneo linalomwagiliwa (2019) 47,052 Ha. Only

(4) Zana za kilimo

4.1. Wakulima wanaotumia zana (matrekta)-10%

4.2. Wakulima waotumia (zana) wanyamakazi 20%

4.3. Wakulima wanaotumia jembe la mkono 70%

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu hizo hapo juu zinadhihirisha maomba yafuatayo:-

(1) Ni lazima tuwekeze kwenye ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji (irrigation and drainage) ili tulitumie eneo linalofaa kwa umwagiliaji ambalo kwa sasa tumeliendeleza kwa takribani 0.1%.

(2) Tunahitaji kutumia zana za kilimo ili tuweze kulima eneo lote linalofaa kwa kilimo ambalo hivi sasa tumeliendeleza kwa takribani 33% tu (angalia pia taarifa ya CAG ya March 2019 Chapter 2, p.5 sec.2.1). Hatuwezi kuendekeza hekta milioni 44 kwa jembe la mkono. Nashauri Serikali ianzishe tractor hire and service centers ambazo zitatoa huduma kwa wakulima wadogo kwa sababu haitawezekana kila mkulima kujinunulia zana za kilimo.

(3) Cropping intensity and productivity, kwa kuwekeza katika kiundombinu na mashamba ya umwagiliaji tutaweza kuongeza uzalishaji kwa kulima eneo moja zaidi ya mara moja kwa mwaka (increased cropping intensity) kwa kuwa maji yatakuwepo kwa kuwa maji yatakuwepo. Aidha ni rahisi kuongeza uzalishaji wa mazao katika eneo moja kwa kuwezesha upatikanaji wa maji na pembejeo na huduma za ugani (increased productivity/ production per unit area).

Mheshimiwa Naibu Spika, Masoko ya Mazao.

(1) Tunapokuwa na ziada ya mazao, hususan nafaka, nashauri Serikali iweke utaratibu (kama inavyofanya kwenye sukari) wa kuwasimamia wafanyabiashara ili wauze ziada nje ya nchi.

(2) Serikali ianzishe mfuko wa kuhimili bei za mazao (Price Stabilization Fund) pindi bei za mazao zinapoanguka hasa katika soko la dunia. Mwaka 2013, Serikali, kupitia Wizara ya Kilimo ilianzisha mchakato wa price stabilization fund kwa mazao manne ya Korosho, Kahawa, Pamba na Tumbaku. Kwanini mchakato huo haukuendelea? Mimi nashauri wazo hilo lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi, Makatibu Wakuu na watendaji wote katika Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri iliyosheheni mafanikio katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, mimi niko katika Kamati ya LAAC, katika ziara nyingi tulizofanya kukagua utekelezaji wa miradi mikoani, nilijikita sana kuchunguza miradi ya ujenzi wa madarasa, zahanati, vituo vya afya, stendi za mabasi, masoko, miradi ya maji na umwagiliaji na kadhalika. Ninapongeza juhudi kubwa inayofanywa na Serikali kutekeleza miradi hiyo kwa gharama nafuu na mahali pengine kwa kutumia mtindo wa force account na ushirikishaji wa wananchi.

Napenda kushauri mambo yafuatayo; kwanza mara kadhaa tumeshuhudia radi zikiharibu majengo, yakiwemo madarasa na hata kujeruhi na kuua walimu na wanafunzi. Nashauri suala la kuweka mitego ya radi katika public buildings zote zikiwemo nyumba za ibada hasa katika maeneo yenye radi liwe la lazima ili kuokoa maisha ya watu na fedha za umma.

Pili, baadhi ya majengo yanalalamikiwa kwa kujengwa chini ya kiwango. Naishauri Serikali iajiri wahandisi wachache na mafundi sanifu wengi katika Halmashauri zetu ili wazisaidie Kamati za Ujenzi kudhibiti ubora wa kazi katika majengo ya umma. Hali ilivyo sasa ni uchache mkubwa wa wataalamu hasa katika Halmashauri na TARURA. Bado kuna udhaifu mkubwa katika kusimamia ubora wa kazi na usimamizi wa mikataba ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, tatu, mafuriko yanayoendelea sasa kuharibu miundombinu yetu tuyatumie kama changamoto. Trend and periodicity ya miaka mingi ya ukame na mafuriko inaonesha kwamba kila baada ya miaka takribani minne huwa nchi yetu inapata ukame na upungufu wa chakula. Tutumie fursa hii sasa kuyavuna maji yanayopotea na kuyahifadhi katika mabwawa ili baadaye tuyatumie kwa kilimo cha umwagiliaji na matumizi mengine.

Mheshimiwa Spika, hali ilivyo sasa ni kwamba tunatumia fedha nyingi sana kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko huku tukiyaachia maji hayo hayo kutiririka hadi baharini bila kutunufaisha.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi tunakumbuka jambo hili tunapopata ukame, njaa na upungufu wa chakula. Mifano hai ni mafuriko ya El-nino yaliyotokea katika miaka ya 1990 na njaa ya mwaka1974. Rejea pia Azimio la Moshi la Kilimo cha Umwagiliaji, Kilimo cha Kufa na Kupona na maazimio mengine yaliyohusu kupambana na ukame.Naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2019
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nianze kwa kumpongeza Mwanasheria Mkuu kwa kutuletea mabadiliko haya ya sheria mbalimbali. Kwanza naomba niseme kwamba mabadiliko haya ya mara kwa mara tumekuwa Bungeni humu muda mrefu wala sio mabaya, ni jambo la kawaida tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikiliza Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani akiwa na wasiwasi kwa nini kila mara tunafanya mabadiliko katika sheria hizi. Katiba zinabadilika, sheria zinabadilika kulingana na wakati, kwa hiyo haya mabadiliko yanapokuja wala hayalengi mtu fulani kwa sababu yanakwenda na wakati ule na mabadiliko yaliyoko kwa wakati huo. Sheria sio msahafu, kwa hiyo kwa kweli haya mabadiliko ambayo Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu ametuletea, nayaunga mkono na nina sababu za kusema hivyo. Nina maeneo machache ambayo ningependa niyazungumzie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nizungumzie Sheria ya Makampuni. Nimepitia Sheria ya Makampuni na mimi kama Mbunge kule kwangu wako watu ambao wangependa sana kurasimisha biashara zao, lakini unakuta wakati mwingine wakitaka kurasimisha biashara zao kutokana na mabadiliko ya kila mara kwa mfano sasa hivi ukitaka kurasimisha biashara yako, sharti ambalo BRELA wametuwekea ni lazima uwe na kitambulisho cha Utaifa. Hata hivyo, vitambulisho hivi ni wangapi wanavyo?

Mimi mwenyewe nimeuliza swali hili hapa Bungeni kama mara mbili hivi, hatujaweza kuwafikia Watanzania wengi kuwapa vitambulisho hivi. Sasa unapoweka kipengele kama hiki kwamba usipokuwa na kitambulisho cha Taifa, huwezi kurasimisha biashara yako na mtu yuko vijijini, yuko Kakonko au Nachingwea huko anataka kurasimisha biashara yake na hajapata kitambulisho, mtu huyu hawezi kurasimisha biashara yake hata kama alikuwa na lengo zuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, na sasa hivi tunataka kuingia katika uchumi wa kati, ambao ni pamoja na kuanzisha makampuni na viwanda. Sasa nilazima tuangalie, sheria hizi tunapoziweka, tuwe na flexibility. Baadhi ya mambo ambayo yanaweza kukwamisha tuyarekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la BRELA, nadhani, tunahiaji BRELA nayo kidogo i-extendtentacleszake. Nilikuwa naongea naMheshimiwa WaziriMstaafu kwamba, hivi BRELA sasa hivi, area yake ya operations, mahali pake, ofisi ziko wapi mpaka sasa! Hadi sasa kama niko sawasawa, sijakosea, BRELA haija-extend mpaka huko mikoani, yenyewe iko kwenye kanda tu. Sasa unawata watu walioko kwenye wilaya huko, watoke huko wote wakarundikane au wakasafiri kwenda kumfuata BRELA, ama kwenye kanda au Dar es Salaam. Urasimishaji unakuwa mgumu, hata kutengeneza returns wakati mwingine inakuwa ni vigumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu, katika sheria hii, tuliangalie jambo hili tunapotaka watu waweze kutekeleza, wafanye shughuli zao za biashara, wapeleke returns kwa wakati tuwape flexibility wasipate matatizo katika kutekeleza matakwa ya sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nije kwenye suala la Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Mimi nafikiri, kama alivyosema Mwanasheria Mkuu, kwa kweli hizi NGO’s lazima ziwe regulated. Hatuwezi kuwa na utitiri wa NGO’s nyingi, zinazo-operate katika nchi hii yetu ambazo hazina regulation, tutashindwakuzidhibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama wananchi wa kawaida tu wanakuwa regulated, sasa itakuwaje NGO’s zisiwe regulated? Kwa hiyo, mimi nafikiri, kwa kweli tunahitaji kuwa na utaratibu, na ninakubaliana na Mwanasheria Mkuu, lazima tuzi regulate na nina sababu kama tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ziko NGO’s ambazo, sitaki kuzitaja, utaiona NGO imekuja, inaingia mpaka hata vijijini, inajinasibu kwamba inapeleka misaada inakwenda kuwanufaisha jamii inayohusika, lakini unapofika kule mwisho wa siku unakuta fedha zile zilizoletwa, labda waliozichukua ni walewale waliovaa t-shirt za NGO, waliozichukua ni wale wale waliozileta na wengine kama ni international NGO’s hizi, fedha zile kwa wingi zinarudi huko zilikotoka. Sasa ukija kutazama, zimenufaishaje ile jamiihuoni. Kwa hiyo, mimi nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu kwamba lazima tuzi-regulate.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini liko suala lingine ambalo mimi nimelishuhudia mwenyewe, nalo ni kwenye fedha zinazokwenda moja kwa moja kwenye halmashauri zetu. Sijui kama kiutalam mnaziita defunds au nini. Nimeshuhudia mahala pengine, miradi ambayo tumeipanga kuitekeleza kupitia kwenye halamshauri zetu miradi hiyo hiyo inapata fedha kupitia kwenye NGO.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakinikwa sababu NGO’s hizi nyingine zinakwenda moja kwa moja mpaka kwenye halmashauri, zinapeleka fedha zao wakati mwingine ukija Wizarani hata hawana habari hiyo, kwamba NGO fulani imepeleka fedha kiasi gani na inatekeleza mradi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa athari yake ni nini; mimi sina tatizo kwamba NGO’s zisipeleke fedha, lakini kuna mahali pengine; mimi niko katika Kamati ya LAAC; unakuta mradi huo huo umekasimiwa fedha za Serikali, lakini mradi huo huo kuna fedha za NGO zilizokwenda kwa utaratibu mwingine; sasa wengine wanaweza hata waka-take advantage, maana fedha zimekuja mara mbili, zinatumika kwa mradi huo huo, inakuwa double accounting, kumbe zingeweza zikatumika mahali pengine. Sasa kamaNGO imepeleka fedha ingekuwa inajulikana basi Serikali ingeelekeza fedha zake mahala pengine.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho linalofanana na hilo ni katika mambo ya regulation. Mimi nakumbuka nilipokuwa mkurugenzi ndani ya Serikali niliwahi kukutana na miradi kama miwili inayotekelezwa na NGO’s; imetekelezwa na imekamilika lakini katika viwango visivyokubalika. Unajua hata katika kutekeleza miradi lazima kuna viwango; katika designs kuna engineering standards.Sasa unakuta NGO imekwenda, wamefika wameongea na wananchi, wameanza kutekeleza mradi, unapokuja sasa kufanya auditing ya mradi, mradi ule hauna viwango, haukidhi viwango vinavyotakiwa kwa maana ya viwango vya kiserikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hapa ndipo ninaposema, kwa kweli, mimi nakubaliana kabisa kwamba NGO’s hizi, kwa nia njema kabisa lazima ziwe regulated na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)