Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Venance Methusalah Mwamoto (5 total)

MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. KHATIB SAID HAJI) aliuliza:-
Kumekuwa na mfululizo wa migomo, misuguano na migongano ya mara kwa mara kwa wafanyakazi wa viwandani na Kampuni binafsi zinazotokana na malalamiko ya mishahara na maslahi ya wafanyakazi:-
Je, ni mfumo upi na viwango gani vilivyowekwa kisheria wanavyotakiwa kulipwa wafanyakazi wa viwanda na Kampuni binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatibu Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo unaotumika katika kupanga viwango vya chini vya mshahara unasimamiwa na taratibu zilizoainishwa katika Sheria Na. 7 ya Taasisi za Kazi ya mwaka 2004 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine, sheria imetoa madaraka kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi, kuunda Bodi ya kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi. Bodi hii inaundwa na Wajumbe 17 ikiwa na Wawakilishi wa Wafanyakazi, Waajiri na Serikali. Majukumu ya Bodi hii ni kupanga kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwango cha chini cha mshahara kilichopangwa na kinachoendelea kutumika hadi sasa katika Sekta ya Viwanda ni shilingi 100,000/= kwa mwezi na viwango vingine vya mshahara katika sekta 12 vimetajwa kwa GN.196 ya mwaka 2013.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza:-
Kwa nini Serikali isifute michezo Tanzania?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Methuselah Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimtambue Mheshimiwa Venance Mwamoto kama mwanamichezo ambaye amewahi kucheza mpira wa miguu katika timu ya ligi daraja la kwanza wakati huo, sawa na ligi kuu Tanzania kwa sasa, yaani timu ya Majimaji ya Songea na RTC ya Kagera lakini pia timu ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, hapa Bungeni Mheshimiwa Venance Mwamoto ndiye Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kufuatia sifa hizo za Mheshimiwa Venance Methuselah Mwamoto, binafsi naamini kuwa swali lake limelenga kupata maelezo ya kwa nini michezo haiendelei kwa kasi wanayotamani wapenda michezo wengi hapa Tanzania na wala siamini kuwa anayo nia ya kutaka Serikali ifute michezo kwa kuwa anafahamu fika umuhimu wa michezo kwa Taifa paoja na wananchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania haiwezi na wala haina nia ya kufuta michezo nchini kwa sababu yoyote ile, badala yake nia ya Serikali ni kuiendeleza sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa hili kwa kuwekeza katika miundombinu ya michezo, elimu ya michezo ya kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa sekta ya michezo inaendelezwa ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge lako Tukufu kushirikiana na Serikali kuhimiza maendeleo ya michezo katika majimbo yetu. Aidha, tunashauri na kuhimiza wadau wote wa michezo ikiwemo Serikali za Mitaa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Waheshimiwa Wabunge, sekta binafsi na wadau wengine kuibua vipaji vya michezo kwa watoto kuanzia umri mdogo na kuviendeleza.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara na Taasisi zake itaendelea kutenga fedha kupitia bajeti yake na vyanzo vingine kadri inavyowezekana kila wakati ili kuendeleza michezo katika ngazi mbalimbali.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza:- Mkoa wa Iringa ulitenga eneo la EPZ katika Wilaya ya Kilolo. Je, ni lini eneo hilo litaanza kuendelezwa na ni nini faida ya EPZ?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Venance Methusalah Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni maagizo ya Serikali kwa mikoa yote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji kwa mfumo wa EPZ na SEZ. Baada ya Serikali katika ngazi ya Mikoa na Wilaya kutenga maeneo hayo inatoa taarifa kwa Mamlaka ya EPZ, ili maeneo hayo yaweze kutangazwa kama maeneo huru ya uwekezaji nchini chini ya Mamlaka ya EPZ. Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Mamlaka ya EPZ haijakabidhiwa eneo lililotengwa kwa ajili ya uzalishaji katika Wilaya ya Kilolo kama ilivyobainishwa. Hii inazingatia kuwa tangu kufutwa kwa umiliki wa kwanza wa shamba hilo, kupitia Tangazo la Serikali Namba 130 la tarehe 17 Februari, 2012 taratibu za kulitangaza kama EPZ zilikuwa hazijakamilika. Hata hivyo, Halmashauri imeanza hatua ya awali ili iweze kukamilisha taratibu za kukabidhi eneo la Ruhundamatwe lililotengwa kwa ajili ya uendelezaji wa viwanda. Michoro (master plan) ya eneo husika imekamilika na kazi inayoendelea sasa ni kupima eneo husika. Kazi hiyo ikikamilika Halmashauri hiyo itakabidhi rasmi eneo husika kwa Mamlaka ya EPZ kwa ajili ya uwekezaji. Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji chini ya Mamlaka ya EPZ una faida zifuatazo:- Mheshimiwa Spika, kwanza, kukuza mauzo nje ya nchi hivyo, kuongeza mapato ya fedha za kigeni; pili, kukuza sekta ya viwanda; tatu, kuongeza ajira na kufundisha stadi za uzalishaji viwandani; nne, kuendeleza uhawilishaji wa teknolojia ya viwanda; tano, kuhamasisha isindikaji wa mazao yetu na uchakataji wa malighafi ili kuongeza thamani; na ksita, uchangia katika kuongeza kipato kwa wananchi, hivyo kupunguza umaskini.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza:-
Vyanzo vingi vya maji vinavyojaza Bwawa la Kihansi vinatoka Wilaya ya Kilolo.
Je, Wilaya hii inanufaika vipi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Methusalah Mwamoto, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli vyanzo vingi vya maji vinavyojaza Bwawa la Kihansi vinatoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa Bwawa la Kihansi unategemea sana vyanzo hivyo muhimu ambapo Taifa linanufaika kutokana na shughuli kubwa inayofanyika katika bwawa hilo ya kufua umeme. Uhifadhi wa Bwawa la Kihansi unatokana na vijiji 22; kutoka Wilaya za Mufindi vijiji nane, Wilaya ya Kilolo vijiji nane na Kilombero vijiji nane ambapo kwa sasa kuna mradi maalum unaosimamiwa na Baraza la Mazingira la Taifa kwa ajili ya uhifadhi mzima wa Bonde la Mto Kihansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo inanufaika na bwawa hilo kwa kupata umeme ambao umesambazwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika maeneo mengi ya vijijini ambapo katika Wilaya ya Kilolo vijiji vilivyonufaika ni pamoja na Masisiwe, Boma la Ng’ombe, Mwatasi, Ng’ingula na Wangama. Pia uwepo wa Bwawa la Kihansi umesababisha mashirika mbalimbali kuanzishwa kwa lengo la kusaidia jamii katika mambo mbalimbali kama vile upandaji wa miti kwa lengo la kuhifadhi mazingira, ufugaji wa nguruwe, mbuzi pamoja na ufugaji wa samaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wananchi wa Halmashauri ya Kilolo wameendelea kupata huduma ya maji kupitia miradi mbalimbali iliyotekelezwa chini ya mpango wa miradi ya vijiji kumi, ambapo jumla ya miradi saba ya Irindi, Ihimbo, Mwatasi, Kipaduka, Vitono, Ikuka na Ilamba imekamilika na miradi mingine ipo katika hatua mbalimabli za utekelezaji.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza:-
Timu yetu ya Taifa imeendelea kufanya vibaya katika michezo ya kimataifa. Je, Serikali imeliona hilo na imechukua hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Methusalah Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya juhudi katika kuendeleza michezo ili kuwa na timu bora za michezo katika ngazi mbalimbali hasa ngazo za timu za Taifa na baadhi ya juhudi hizo ni pamoja na:-
(i) Kuboresha mazingira ili wadau wa michezo wawekeze kisayansi katika michezo kuanzia umri mdogo kwa lengo la kugundua na kukuza vipaji na hatimaye kupata wachezaji mahiri wa timu za Taifa.
(ii) Kuendesha mafunzo mbalimbali ya michezo kwa wataalam wa michezo nchini katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
(iii) Kutoa mafunzo ya michezo mbalimbali ya muda mfupi kwa Wilaya na Mikoa kupitia Baraza la Michezo la Taifa.
(iv) Kutoa ushauri elekezi kwa vyama vya michezo wakati wa maandalizi ya timu za Taifa zinazoshiriki kwenye michezo ya Kimataifa mfano Olympiki, Michezo ya Afrika (All African Games) na michezo ya Jumuiya ya Madola.
(v) Serikali imetenga shule mbili kila Mkoa kama shule maalum za michezo na pia inaendelea kuhamasisha wadau kuanzisha shue za aina hiyo (sports academy).
(vi) Kuelekeza vilabu na vyama vya michezo kuwa na timu za umri wa chini na kuanzisha ligi zao kwa michezo hiyo.
(vii) Kushirikiana na Wizara nyingine kuendesha na kuratibu mashindano ya michezo kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi (UMITASHUMTA) na ile ya shule za sekondari (UMISETA).
Mheshimiwa Spika, ili tufanikiwe katika hilo, Wizara inatoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya michezo katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na zile za uibuaji wa vipaji na ujenzi wa miundombinu kwa kuhamasisha wadau mbalimbali. Aidha, Wizara inatoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuendelea kuyalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za michezo na burudani pamoja na kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo yao inazingatia utengwaji wa maeneo ya michezo na burudani.