Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa (8 total)

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja na ombi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo mazuri ya Serikali, naomba kupata commitment ya Serikali, lini mradi huu utaanza kufanya kazi kwa sababu vijana wengi waliopo katika Kijiji cha Ikweha wanategemea sana kupata ajira katika eneo hili ukichukulia kwamba muda wa matarajio ya kukamilika kwa mradi huu uliishia mwezi Agosti, 2016 na sasa hivi Serikali imesema wataanza rasmi Aprili 17. Sasa ni lini mradi
huu utakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ulikuwa
unashughulikiwa kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi pamoja na wafadhili, Serikali Kuu ilikuwa bado haijajiingiza. Naomba nichukue fursa hii kumuomba Mheshimiwa Waziri, wakati wa Bunge lako hili tukufu tuambatane nae aende akaone hali halisi na umuhimu wa mradi huu kwa ajili ya wananchi wa Kijiji cha Ikweha.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mgimwa kwa kufuatilia miradi hii ya umwagiliaji. Pili, lini anasema utakamilika. Kama tulivyoeleza kwenye jibu la msingi, kwa sababu fedha hizi zilikuwa zimetolewa na wafadhili na ndio maana kulichelewesha kukamilisha marekebisho yanayotakiwa. Na kwa sababu wamekubaliana na Halmashauri waanze mwezi wa nne kwa hiyo, tunafikiria kulingana na kazi zenyewe ni ngapi
zinazotakiwa kurekebishwa, siwezi kusema muda hasa, lakini natarajia kwamba, katika miezi 12 iliyokuwa imepangwa mwanzo ndio hiyo ina-carry forward kwamba tutaanza mwezi wa nne kurekebisha marekebisho ambayo yamefanyika ili
kusudi mradi ule uweze kufanya kazi. Lakini pia mwaliko wa kutembelea mradi huo naupokea na tutakwenda kuutembelea na kuona hali halisi jinsi ilivyo.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimwa Naibu Spika, pamoja na maelezo ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, nataka tupate tamko la Serikali lini wataanza kulipa malimbikizo hayo ya likizo za wafanyakazi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri haki zao hizo za msingi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni mwaka wa
pili sasa hakuna increment yoyote kwa walimu wala kupandishwa madaraja. Nataka kauli ya Serikali ni lini wataanza kupandisha madaraja na kuongeza increment hasa za walimu ambao morali zao zimeanza kushuka katika maeneo yao ya kazi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende tu kusema kwamba Serikali imekuwa ikijitahidi kulipa malimbikizo mbalimbali ya mishahara pamoja na madai mengine yasiyokuwa na mishahara kwa watumishi wa umma na itaendelea kufanya hivyo kila mara. Nipende tu kusema kwamba katika mwaka huu wa fedha kupitia bajeti za OC mbalimbali za waajiri wetu wametenga ulipaji wa madeni, lakini vilevile kupitia Serikali kwa ujumla wake tumetenga fedha zaidi ya shilingi trilioni moja kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi pamoja na madeni ya wazabuni wengine mbal imbali waliotoa huduma katika Serikali. Kwa hiyo, wakati wowote tu kuanzia sasa pindi tu madeni hayo yatakapokuwa yameshahakikiwa basi watumishi wataweza kuona madeni hayo yakilipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na increment na kupanda madaraja, nilipokuwa nikijibu swali hapa Jumatatu au Jumanne nilieleza kuhusiana na suala hili. Tayari taratibu zimeanza na hivi sasa tunakamilisha tu taratibu za mwisho ili kuweza kuanza kulipa nyongeza hiyo ya mwaka ya mishahara kwa watumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa upandishwaji wa madaraja, nilishasema fedha zimeshatengwa na niwahahakishie tu watumishi wote wa umma wenye stahili za kupanda madaraja hakuna ambaye ataachwa. Niendelee tu kuomba waajiri wahakikishe kila ambaye anastahili kupanda daraja basi ameingizwa katika orodha, lakini bila kuacha kuzingatia seniority list ili watumishi wenye stahili waweze kupatiwa madaraja hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kurudia kusema tena tumeshatenga fedha kwa ajili ya watumishi 193,166 ambao watapanda madaraja mwaka huu. Niendelee kuwatoa hofu watumishi wa umma hakuna ambaye atakakosa daraja lake analostahili katika mwaka huu.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo ya Serikali, nina swali moja na ombi moja.
Ombi, namuomba Mheshimiwa Naibu Waziri mara baada ya Bunge hili aje pale kwenye Kijiji cha Nundwe atembelee mradi huu aweze kujionea hali halisi na mahitaji ya mradi huu ambao unatarajia kuajiri vijana wasiopungua takribani 5,000.
Mheshimiwa Spika, swali langu, mradi huu ni miongoni mwa miradi ya FP I ambao ulikuwa na thamani ya milioni 660. Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu alipokuja kufungua mradi huu, tayari shilingi milioni 101 zilikuwa zimeshatumika lakini ilionekana kulikuwa kuna mahitaji ya shilingi milioni 295 ili mradi uweze ku-take off.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi kwamba baada ya miezi mitatu shilingi milioni 295 zingekuwa zimefika, maana zingekuwa zimefika Juni, 2015, lakini mpaka leo hizi hela hazijafika. Sasa nataka Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie, lini watatuletea hizi hela, shilingi milioni 295, ili vijana waweze kupata ajira?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, moja, kuhusu ombi la mimi kwenda katika Kijiji cha Nundwe, nataka nimhakikishie, kwa kuwa anayelala na mgonjwa ndio anayejua mihemo ya mgonjwa, nipo tayari kwenda kuukagua mradi ule ili usikwame, ili uweze kuleta uwezeshaji wa kiuchumi na chakula cha kutosha kwa kijiji kile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu swali la pili; lengo la Serikali ni kukamilisha miradi yote ili iwe endelevu katika suala zima la utekelezaji. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutatafuta fedha katika vyombo mbalimbali ili kuhakikisha fedha zile zinapatikana ili mradi usikwame uende kutekelezwa mara moja. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa majibu mazuri lakini nina swali la nyongeza.
Pesa hizi zilizokuwa zinakusanywa na Halmashauri zilikuwa zinasaidia kazi ndogo ndogo kwenye zile Halmashauri. Namuomba Mheshimiwa Naibu Waziri atuambie Serikali imepanga vipi kuhakikisha inaziba hilo gap?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Halmashauri mwanzo zilikuwa zinajielekeza kwa kukusanya tozo hizi ambazo zilikuwa zinasaidia katika kuendesha Halmashauri. Nadhani hiki kilikuwa ni kilio cha Watanzania wote, ambao Watanzania wadogo wadogo kule chini ilikuwa inapigwa kelele sana ndio maana Serikali sasa imeomua kulichukua hili na Wizara ya Fedha hapo alipoweka hotuba yake hapa nilizungumza hili wazi. Kwa hiyo, naomba tukifika katika Finance Bill mtaona jinsi gani Serikali imejipanga na ku-address jambo hilo vizuri kwa mustakabali wa Halmashauri zetu unavyoenda.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Mtikila kilijenga zahanati ambayo ilikamilika mwaka 2015, lakini mpaka leo haijafunguliwa kwa sababu ya tatizo la vifaa na wataalam. Namuomba Naibu Waziri aniambie, ni lini watafungua zahanati hii ili kutokudhoofisha nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tulipokea katika michango ya Mheshimiwa Bobali na nikayarudia katika moja ya maswali ambayo nilikuwa najibu hapa, kwamba ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba zahanati ambazo zimekamilika huduma itatolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimetangulia kusema muda siyo mrefu kwamba ni siku ya leo ambapo Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Utawala atakuja kuhitimisha na atasema neno kuhusiana na suala zima la kupatikana wahudumu wa afya na waganga, maana na sisi tunategemea kupata kibali cha ajira kutoka kwake.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu mstaafu alipotembelea kwenye kijiji hiki alikuta tayari Serikali imeshaanza kutekeleza, lakini yalijitokeza mapungufu ambayo yalikuwa yanagharimu milioni 295,000,000 kwa ajili ya kujenga mifereji (main canal), kwa ajili ya kujenga vivuko vya watu na wanyama na kwa ajili ya kujenga vigawa maji kuelekea mashambani. Pia kumalizia na kuongeza eneo la mfereji lifike kilometa 2.2 na ndiyo maana Mheshimiwa Waziri Mkuu baada ya kuona hilo akaahidi kwa wale wananchi wa Nundwe kwamba niko tayari kutoa shilingi 295,000,000 mradi huu uweze kukamilika. Mradi huu ukikamilika utaajiri vijana…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakwenda kwenye swali, utaajiri vijana walio wengi. Sasa swali langu hapa linasema lini hiyo shilingi 295,000,000 itatoka kusudi haya mambo ambayo tunayazungumza yaweze kutekelezwa Mheshimiwa Waziri? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nilikuwa namuomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri au Waziri aje kwenye site aone hili jambo ambalo tunalizungumzia.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge mzee wangu Mgimwa, lakini pia nitumie nafasi hii kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji. Kwa hiyo kama Mwenyekiti wangu ahadi ni deni na sisi kama viongozi wa Wizara hii hatutokuwa kikwazo katika kuhakikisha tunakamilisha ahadi ile ambayo imetolewa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mizengo Pinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu ahadi ya mimi kwenda kule katika jimbo lake, nipo tayari Mheshimiwa Mbunge na Mwenyekiti wangu kuongozana pamoja katika kuangalia hali halisi ya utekelezaji wa mradi ule ili hatimaye tuongeze jitihada kwa haraka. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, alipokuwa kwenye ziara yake Wilaya ya Mufindi alisema ahadi ni deni na hii barabara ni ya muda mrefu. Akaahidi kwamba hii barabara itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya ya Mufindi na Rujewa na ni short-cut kwa wasafiri wanaotoka Mbeya. Nini commitment ya Serikali, lini wataanza kujenga barabara hii hata kwa kilometa mbili-mbili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri uko tayari kuja Wilaya ya Mufindi kukutana na wananchi wote waliopo kandokando ya barabara hii kusudi uweze kuwaambia hatma ya tathmini na malipo yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mgimwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mgimwa kwa sababu anafuatilia kweli siyo barabara hii tu peke yake lakini pia barabara inayoenda kumuunga kule Kihansi na kila wakati yuko Wizarani kufuatilia barabara hii. Kwa hiyo, nampongeza sana naamini kwamba wananchi wa Mafinga hawakukosea kumpa nafasi ya Ubunge.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba ahadi ni deni ni kweli na ndiyo maana tumeendelea kuiwekea kipaumbele barabara hii ili tuweze kujenga kwa lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mgimwa nakubaliana na wewe lakini tatizo ni fedha, tukipata fedha tutaendelea kupunguza kwa maana ya kujenga kwa awamu kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba kadiri tunavyopata fedha tutaendelea kujenga barabara hii muhimu kwa sababu inapita maeneo ya uzalishaji mkubwa wa mpunga kule Mbarali.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kutembelea eneo hili, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili nitatembelea eneo hili ili kuweza pia kuwahakikishia wananchi wa Tarafa hii ya Sadani na maeneo mengine kwamba tumejipanga kuwaletea barabara ya lami lakini pia kuwalipa fidia ili kupisha mradi huu muhimu. Ahsante.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Mindombinu ya Bunge ilitoa maelekezo kwa Serikali kwamba iangalie sasa barabara zinazounganisha Wilaya na Wilaya, Mkoa na Mkoa zipewe kipaumbele za kupandishwa hadhi kuwa barabara za TANROADS. Barabara hii mchakato wa kupandishwa hadhi ulianza mwaka 2013, lakini mpaka leo hii kumekuwa kuna maneno haya kwamba tumesimamisha. Nataka nipate tu kauli ya Serikali, sababu zipi zilizopelekea kusimamisha barabara ambayo tayari mchakato wake ulishaanza mwaka 2013?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mpaka sasa hivi barabara haipitiki kabisa na nimeuliza katika swali langu la msingi, ni hatua gani za dhararu Serikali inaweza kuzichukua ili kuhakikisha barabara hii inapitika.

Sasa maelezo yaliyozungumzwa na Mheshimiwa Naibu Waziri ni mipango ya muda mrefu. Sasa hivi watu hawapati nafasi ya kupita, watu wanakufa katika maeneo yao, mazao yanaharibika, ni hatua zipi za dharura zitakazosaidia barabara ipitike?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Mgimwa kwa sababu barabara hii ameizungumza sana hata wakati akichangia kwenye bajeti ya Wizara, ameizungumza barabara hii. Pia niseme tu kwamba tumekuwa na chombo hiki cha TARURA na niseme kwamba TARURA imeanza vizuri kwa sababu imefanya kazi kubwa sana kwa muda mfupi. Hivi ninavyozungumza TARURA wamemaliza zoezi la kuzitambua barabara zetu ili sasa kuona urefu wa barabara zote kwenye Halmashauri za Wilaya zetu, kuangalia hali za barabara na idadi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi linafanyika kuangalia idadi ya magari yanayopita katika maeneo, lengo kubwa ni kuweza kufanya uchambuzi na hivi ninavyozungumza iko kamati maalum ambayo inakaa kule Morogoro itamaliza kazi yake mwezi huu wa Juni, ikiwa na wajumbe kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara, Wizara ya Ujenzi, TAMISEMI, Maliasili na Utalii, TANROADS, TARURA wenyewe, Wizara ya Ardhi na Ofisi ya AG ili sasa kuweza kuzipanga upya barabara zetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mgimwa naomba uvute subira tu kwamba pamoja na status ya barabara pia itatazamwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza juu ya maboresho ya haraka kwenye maeneo haya kama hapapitiki. Nafahamu kwamba kipindi kilichopita tumekuwa na mvua nyingi sana na maeneo mengi yamekuwa hayapitiki kwa sababu pia kumekuwa na changamoto hii ya wakati wa mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuelekeze tu Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Iringa ashirikiane na wenzetu upande wa TARURA tuone maeneo ambayo wananchi hawapiti tuweze kukwamua waweze kupita.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi hili nitalifutilia ili wananchi wapite wakati hizi hatua nzuri ambazo nimezitaja za kuiboresha hii barabara ili kuiunganisha kutoka eneo hili la Mufindi kwenda Morogoro kupitia Mlimba liweze kwenda vizuri.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mgimwa naomba uvute subira, natambua pamoja na Kamati kutoa maelekezo lakini hatua za haraka tumezichukua, tutazipanga barabara zetu na hii barabara yako Mheshimiwa Mgimwa tutaitendea haki.