Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mendard Lutengano Kigola (8 total)

MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Serikali iliahidi kupeleka gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Mgololo lakini hadi sasa gari hilo halijapelekwa:-
Je, ni lini gari hilo litapelekwa ili liweze kusaidia Vijiji vya Idete, Itika, Holo, Isaula, Rugema, Makungu, Rugolofu na Kitasengwa?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ina gari moja linalotumika kuhudumia wagonjwa. Hata hivyo, gari hilo ni chakavu kiasi cha kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila Halmashauri inapaswa kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kubebea wagonjwa kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Halmashauri imeomba shilingi milioni 543.0 kwa ajili ya kununua magari matatu (ambulance) ambapo kati ya hayo gari moja litapelekwa katika Kituo cha Afya Mgololo na mengine katika Vituo vya Afya vya Sadani na Kasanga ili yasaidie kuwafikisha wagonjwa wenye dharura kwenye vituo vya kutolea huduma kwa haraka.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Jimbo la Mufindi Kusini linazungukwa na msitu wa Serikali na vijana wanaishi humo hawana ajira.
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa vibali vya kupasua mbao ili kwa kazi hiyo wajiajiri?
(b) Je, Serikali haioni haja ya kuwapa vijana hao mtaji ili waanzishe viwanda vidogo vya mbao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mufindi Kusini linapakana na msitu wa shamba la miti la Sao Hill ambalo ni miongoni mwa mashamba ya misitu ya kupandwa 18 nchini. Upasuaji wa mbao ni sehemu moja tu ya mchakato mzima wa uvunaji wa mazao ya misitu unaotekelezwa na Wizara yangu kwa mujibu wa mwongozo wa uvunaji endelevu na biashara ya mazao ya misitu yanayovunwa katika mashamba ya miti na misitu ya mikoko kwa mwaka 2014, chini ya Sheria ya Misitu namba 14 ya mwaka 2002 na Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998. Mwongozo huo umeweka vipaumbele mbali mbali katika uvunaji wa mazao ya misitu ikiwemo vikundi vya vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua changamoto za kiuchumi na kijamii kwa vijana katika maeneo husika Serikali imekuwa ikishirikiana na umoja wa vikundi vya kijamii Wilayani Mufindi kwa kuwapatia vibali kwa ajili ya kuwezesha kupata mitaji ili kuwekeza katika miradi mingine ya kiuchumi. Kwa miaka mitatu mfululizo 2013/2014 hadi 2015/2016 vijana kupitia umoja huo wamekuwa wakigawiwa mita za ujazo 200 kila mwaka. Fedha inayotokana na vibali hivi huratibiwa na umoja wao, na imewawezesha kuanzisha shughuli mbalimbali ikiwemo kununua mizinga ya ufugaji nyuki, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ufugaji wa kukuna hata mitaji kwa ajili ya biashara ndogo ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha uwezeshaji wa vijana wanaoishi jirani na msitu kwa namna endelevu, shamba la miti Sao Hill hutoa miche ya miti kwa ajili ya kupanda kwenye mashamba wanayomiliki wenyewe ili waweze kuvuna na kuuza mbao na kujipatia mfanikio ya kiuchumi na kijamii ikiwemo upatikanaji wa ajira. Kwa mfano katika mwaka 2015/2016 shamba lilitoa bure miche 600,000 yenye thamani isiyopungua shilingi 120,000,000 kwa ajili ya kuwawezeshavijana hao.
Aidha, ili kuhakikisha kuwa jamii inanufaika na uwepo wa shamba hilo na kuwapunguzia adha ya michango kwa shughuli za maendeleo vijiji vinavyozunguka shamba hilo vinapatiwa vibali vya kuvuna miti kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo ikiwemo kutengeneza madawati, kazi ambayo pia hupewa mafundi ambao ni vijana wanaishi katika vijiji vinayozunguka shamba hilo. Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 2011/2012 hadi 2014/2015 jumla ya meta za ujazo 40,000 zilitolewa kwa vijiji vya jirani na kwa mwaka 2013/2014 pekee baadhi ya vijiji vilitumia mgao huo kutengeneza jumla ya madawati 2,469.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inatoa ushauri kwa vijana kuungana pamoja na kuunda ushirika ambao utawezesha kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha na hatimaye kujenga uwezo wa kuendesha shughuli zao za kila siku ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika viwanda vya mbao yaani saw mills ili waweze kuomba vibali vya uvunaji kajadiliwa kama wateja wengine wenye viwanda.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Upembuzi yakinifu wa barabara ya kutoka Nyololo hadi Mtwango yenye urefu wa kilomita 40 umefanyika mwaka 2013/2014:-
Je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa barabara ya Nyololo - Igowole hadi Kibao ilikamilika mwaka 2014 yakiwa ni maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara TANROADS, itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii kwa kiwango cha changarawe ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka wakati taratibu za kutafuta fedha za kuijenga kwa kiwango cha lami zinaendelea na ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo imeelekeza hii barabara katika ukurasa wake wa 61.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y. MHE. MENDRAD L. KIGOLA) aliuliza:-
Mradi wa maji katika Kata ya Mtwango umechukua muda mrefu bila kukamilika na wananchi wanaendelea kupata shida ya maji:-
Je, ni lini mradi huo utakamilika na kukabidhiwa kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi wa maji katika Kata ya Mtwango ulianza rasmi mwezi Juni, 2015. Mradi huo katika bajeti ya mwaka 2015/2016 ulitengewa shilingi milioni 488.8 ambapo utekelezaji wa mradi huo umefikia 60%.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukamilisha mradi huo katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imetengewa shilingi milioni 643.5 kwa ajili ya kazi zilizobaki, ili mradi huo uanze kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kata za Mtambula, Idunda, Maduma, Kiyowela na Idete ili wananchi waweze kufaidika na huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa ya kiti chako, niombe dakika moja niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kabla sijajielekeza kwenye kujibu maswali yaliyoulizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge jinsi ambavyo walijitoa kwenye msiba mzito wa mama yangu uliotokea wiki tatu zilizopita, nawashukuru sana na ningependa kwa ruhusa yako kwa uwakilishi wa Waheshimiwa Wabunge niwatambue wachache walioweza kufanikiwa kufika Chato kwa ajili ya msiba, lakini nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa ridhaa hiyo. Baada ya kusema hayo Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na madini, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kufikisha umeme nchi nzima ikiwa ni pamoja na maeneo ya vijiji vya Mufindi Kusini. Vijiji vya Kata ya Idete, Idunda, Kiyowela, Maduma pamoja na Mtambula vitapatiwa umeme kupitia mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu unaoanza Disemba mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji hivyo nilivyovitaja vya Wilaya ya Mufindi itahusisha itahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovolt 33 yenye urefu wa kilometa 242, ujenzi wa njia ya msongo wa kilovolt 0.4 yanye urefu wa kilometa 81, ufungaji wa transfomer 24 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 3,533. Kazi inatarajiwa kuanza mwezi huu wa Disemba, 2016 na kukamilika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 11.92.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza kujenga mradi wa maji wa Sawala, Mtwango, Rufuna na Kibao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa Sawala - Kibao ambao utahudumia vijiji vya Sawala, Mtwango, Rufuna na Kibao vilivyopo katika Kata ya Mtwango ulianza kutekelezwa tarehe 01/06/2015 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 01/06/2016 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.55.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi huo ulipangwa kufanyika kwa awamu tatu ambazo ni kujenga intake na kupeleka maji kijiji cha Sawala, kujenga mfumo wa bomba kuu kutoka kijiji cha Sawala hadi Kibao na kujenga mtandao wa kusambaza maji katika vijiji vya Mtwango, Rufuna na Kibao. Awamu ya kwanza utekelezaji umefanyika katika kijiji cha Sawala kwa mkataba wa gharama ya shilingi milioni 644.21.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa, jumla ya shilingi milioni 261.64 zimetumika kwenye mradi. Kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa intake, sump well, pump house, ulazaji wa bomba kuu, ujenzi wa tenki la mita za ujazo 200, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 16 na sehemu ya mabomba ya usambazaji kilometa 3.4; kwa wastani kazi iliyofanyika imefikia asilimia 50 kwa kijiji cha Sawala tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo haukuweza kukamilika kwa wakati kutokana na mkandarasi kushindwa kukamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba. Mwezi Novemba, 2016 Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ilivunja mkataba na mkandarasi huyo, na kuamua kuutangaza upya tarehe 07/02/2017 ili kuweza kupata mkandarasii mwingine wa kumalizia kazi zilizobaki. Mkandarasi anatarajiwa kupatikana mwezi Juni, 2017 na kazi itakamilika katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara ya kilometa 40 ya kutoka Nyololo - Igowole - Mtwango kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nyololo- Igowole hadi Mtwango au hadi Kibao yenye urefu wa kilometa 40.4 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami yanaendelea ambapo upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii yamekamilika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika katika majira yote ya mwaka wakati ikiendelea kutafuta fedha kwa ajilii ya ujenzi wa kiwango cha lami. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 450.077 na katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 160.511 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza kujenga Mradi wa Maji kwa Kata ya Mtwango katika Vijiji vya Sawala, Mtwango, Rufuna na Kibao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Sawala, Mtwango, Rufana na Kibao katika Kata ya Mtwango ni miongoni mwa vijiji 12 vilivyopendekezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kupatiwa huduma ya maji kupitia Programu Ndogo ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini. Utelekezaji wa mradi ulipangwa kufanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Ujenzi wa mradi huo ulianza tarehe 01 Juni, 2015 na ulitakiwa kukamilika tarehe 01 Juni, 2016 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.36. Awamu ya kwanza ilikuwa ni ujenzi wa miundombinu ya maji katika Kijii cha Sawala pekee ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mwezi Novemba 2016 mkandarasi alikuwa hajakamilisha kazi na hivyo Halmashauri kuamua kuvunja mkataba. Halmashauri ilitangaza upya zabuni kwa ajili ya ukamilishaji wa kazi zilizobaki. Mkandarasi mwingine amepatikana na utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Desemba, 2017 kwa muda wa miezi 12 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.81. Serikali katika mwaka wa 2017/2018 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.56 kwa ajili ya Halmashauri ya Mufindi ili kukamilisha mradi huo katika Vijiji vyote vya Sawala, Mtwango, Rufuna na Kibao na kuendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya vijijini.