Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mendard Lutengano Kigola (6 total)

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini pamoja na majibu yake Naibu Waziri kwamba hili gari kwenye bajeti ya mwaka 2013/2014 na swali la msingi niliuliza mwezi wa Tisa na kwenye bajeti walisema kwamba wametenga milioni 150 kwa ajili ya ununuzi wa hili gari la wagonjwa wa kule Mgololo, mpaka leo hili gari halijapelekwa. Niliwahi kumuuliza Waziri wa Afya akaniambia kwamba kuna magari matano yamenunuliwa mojawapo litapelekwa kule, lakini mpaka leo halijakwenda. Je, bajeti ya mwaka uliopita ambayo ilitengwa kwa ajili ya hilo gari, hiyo fedha ya shilingi milioni 150 ilikwenda wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hii gari ni ya msingi sana, kwa sababu itahudumia Kata tatu, kuna ya Kiyowela, Kata ya Idete na Kata ya Makungu. Kule kuna watu wanakaribia karibu 120,000 hivi, akinamama wanapata taabu sana kuna milima, jiografia ya kule ni ngumu sana. Sasa naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anithibitishie kwa sababu hii pesa ya Halmashauri haina uhakika, ni lini hii gari hili la wagonjwa litapelekwa Mufindi?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri wazi kwamba nilifika Mufindi katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge mpaka Mgogolo. Hili ni miongoni mwa Jimbo ambalo lina changamoto kubwa kutokana na jiografia yake ilivyo. Hata hivyo, nipende kumshukuru pia kwa juhudi kubwa anayofanya katika kuhakikisha mambo yanakwenda katika Jimbo lake kwa sababu katika miaka mitano iliyopita alikuwa akipigania mambo mbalimbali katika maeneo yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la msingi la kwanza aliposema bajeti ya mwaka ilitengwa lakini haikupatikana ni kweli, na nyinyi mnafahamu sio bajeti ya ambulance peke yake, isipokuwa miradi mingi sana ya maendeleo katika kipindi kilichopita, imekumbwa na changamoto kubwa sana hasa ya upelekaji wa fedha. Maombi haya yalikuwa ni katika maombi maalum, hivyo ni imani yangu kwamba katika bajeti ya mwaka huu sasa kwa vile jiografia yake inajulikana, Ofisi ya Rais - TAMISEMI tutaweka kipaumbele kuhakikisha gari hilo linapatikana. Kikubwa zaidi katika hayo yote maana yake maombi maalum wakati mwingine yana changamoto kubwa sana na sana sana zinalenga katika collection ya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote tushikamane kwa pamoja kuisaidia nchi yetu ili tupate mapato ya kutosha, yale maombi maalum yote tuliyoyapeleka, Serikali iweze kuona ni jinsi gani yatayafanyiwa kazi.
Sehemu ya pili, ni kwamba ni lini gari litapatikana, nimesema kwamba, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sababu tunaguswa na hili, katika uongozi wetu wa sasa tutapambana kwa kadri iwezekanavyo. Ndugu yangu wa Mufindi tujitahidi kwa pamoja Mungu akijalia tutapata gari, naomba amini Ofisi yako.
kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Katika Mpango wa REA kwamba itapeleka umeme vijijini, kuna vijiji vya Jimbo la Mufindi Kusini vyapata karibu 30 havijapata umeme, kuna nguzo zilipelekwa kule na baadaye zile nguzo zikaenda kuhamishwa na wananchi wana wasiwasi. Mheshimiwa Waziri naomba uwathibitishie wananchi kwamba kwenye mpango huu wa tatu wanaweza kupata huo umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika maeneo ya Mufindi kuna nguzo zilipelekwa na mashimo yakachimbwa, lakini kutokana na scope ya kazi ile ilionekana kwamba mashimo yalikuwa yamechimbwa maeneo ambayo siyo yenyewe. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu, tumeshakaa na Mheshimiwa Mbunge, tumetathmini vijiji vyake vyote vya Mufindi Kusini na vyote alivyoviorodhesha vitaingia kwenye REA III na vitapatiwa umeme kwenye REA III inayoanza mwezi Julai mwaka huu.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, hii barabara ni ya muhimu sana na ni ya miaka mingi sana na bahati nzuri sana hata Naibu Waziri wa Ujenzi mwaka 2015 alifika kule Mufindi na alifanya mikutano miwili na aliwaambia wananchi kwamba, baada ya kumaliza uchaguzi hii barabara itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kufuatana na umuhimu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea viwanda, viwanda kule tayari viko, kuna kiwanda cha Kibwele pale, kuna kiwanda cha Kilima Factory, kuna kiwanda cha Lugoda factory, hivi ni Viwanda vya Chai na vinategemea hii barabara. Mheshimiwa Waziri aniambie kwa sababu upembuzi yakinifu walishamaliza na Serikali iliahidi na Chama cha Mapinduzi kimeahidi kwamba kitaweka kiwango cha lami. Ni lini hizi fedha zitapatikana na wataanza kujenga kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi walishaambiwa tayari kuna nyumba zao zilishawekewa alama ya X na wanatarajia kuhama! Je, Serikali ni lini itaenda kutoa fidia kwa wale ambao walijenga nyumba jirani na barabara na Serikali ilisema itawalipa fidia kwa mfano, wananchi wa Kijiji cha Nzivi, Igowole, Kibao, Mtwango na pale Lufuna, kuna nyumba ziliwekewa X, Serikali itaenda kuwalipa lini ili waanze kuhama?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii. Tunapoongelea ujenzi ni pamoja na fedha za fidia pamoja na fedha za ujenzi wenyewe. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama ambavyo barabara hii ipo katika ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020, namhakikishia ahadi hiyo itatekelezwa, asiwe na wasiwasi!
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri, lakini tunajua kabisa kwamba kuna tatizo kubwa sana la walimu wa sayansi katika Wilaya zote. Sasa je, Serikali ina mkakati gani wa kuchagua chuo kimoja kuweza kusomesha walimu wa sayansi tu? Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Mkwawa pale, tungeamua kitoe masomo ya sayansi ili tuweze kupata walimu wengi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa nini Serikali sasa isitoe mkopo kwa asilimia mia moja kwa wale wanafunzi ambao wanasomea masomo ya sayansi ili kuwavutia wanafunzi waweze kujiunga na ualimu wa sayansi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la mkakati wa kuwapata walimu wa sayansi, kama unavyofahamu kwamba tayari Serikali ilishachukua hatua na kama mnavyokumbuka kwamba tulikuwa na wanafunzi zaidi ya 7,800 ambao walikuwa katika Chuo cha UDOM ambao kwa sasa tumewatawanya katika vyuo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale ambao wana vigezo sasa hivi kwa kufundisha shule za sekondari ni zaidi ya walimu 6,305 wakishamaliza masomo yao wataweza kwenda kwenye hizo shule. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kufundisha walimu wa sayansi na wakati huo huo kuhakikisha kwamba maabara kwa ajili ya shule za sekondari ili kupata wanafunzi wengi zaidi katika maeneo ya sayansi yaweze pia kukamilika na kupewa vifaa vinavyostahili.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Suala la umeme vijijini pamoja na ahadi nzuri za Serikali na kwenye bajeti hii ya 2016/2017, Serikali imeahidi vizuri sana na tunasema vijiji vyote vitapewa umeme. Kwenye shule za sekondari, shule za misingi, zahanati na sehemu nyingine za hospitali. Tunaomba Serikali itoe commitment kwamba katika mwaka huu wa fedha tuta-specialize hasa kwenye vituo vya afya na zahanati ili tusi-generalise kwamba tutapeleka kila sehemu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumekuwa tukieleza, labda niwaombe Waheshimiwa Wabunge watupe ushirikiano kuhusu jambo hili. Wananchi na Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wakiomba sana kupelekewa umeme kwenye vijiji vyao badala ya huduma za afya na taasisi nyingine. Namshukuru sana Mheshimiwa Kigola lakini niseme tu mpango wa Serikali wa awamu ya tatu ya REA, unazingatia sana vipaumbele vya kuwapelekea umeme taasisi za jamii pamoja na kwamba tunawapelekea pia kwenye matumizi ya nyumbani. Kwa hiyo, mpango wetu unatekelezwa hivyo. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge ikibidi anilitee taasisi zake za umma kabla hatujatoka kwenye Bunge hili ili nimhakikishie kwamba tutaanza na hizo kabla ya kuwapelekea umeme kwenye nyumba zao.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini nina maswali mawili tu ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; katika upelekaji wa umeme vijijini, REA wanapeleka kwa kufuata barabara na kwenye centres, lakini unaweza ukaona kwamba kwenye shule za msingi, sekondari, vituo vya afya na zahanati kule umeme haupelekwi. Sasa Naibu Waziri naomba anihakikishie wananchi wa Jimbo la Mufindi Kusini kwenye maeneo haya niliyotaja kama watapewa umeme?
Mheshimiwa Mwenyekiti la pili, namuomba Naibu Waziri, kwa majibu haya aliyoeleza vizuri, kwa programu ya awamu ya tatu ambayo inaanza, je, utakuja lini Mufindi ukafanya mkutano angalau hata mmoja kuongea na wale wananchi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu utapeleka umeme katika maeneo yote ya taasisi ikiwemo shule za msingi, sekondari, hospitali na katika taasisi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Kigola, jimbo lako la Mufindi Kusini, maeneo yote niliyoyataja ikiwemo pia katika vijiji vyako vya Mbaramaziwa, Tambarang‟ombe kwenda mpaka Tengereo mpaka kule Kilowelo vitapelekewa umeme kwenye taasisi nilizozitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu suala lake la pili, kwamba ni lini sasa tutatembelea katika maeneo yale? Nimhakikishie Mheshimiwa Kigola; kwanza kabisa nikupongeze umeshaanza kuchimba visima kwa ajili ya kuhitaji umeme. Napongeza sana kwenye Kitongoji chako cha Msumbiji umeshaanza kujenga, lakini pale Idambaravumo pia umeshaanza kujenga na pia unatarajia kupeleka umeme pale Kilowelo centre, na pia kwenye vijiji vyako vingi sana ikiwemo kama nilivyosema pale Kisaula tutakupelekea mashine ya umeme, lakini pia kwenye vijiji vyako vingine mbali na vijiji na Kitongoji cha Msumbiji na pale Changarawe kwa Mheshimiwa Kigola kwa vijiji vyako 47 vilivyobaki vyote vitapata umeme wa uhakika.