Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Wilfred Muganyizi Lwakatare (12 total)

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kuniruhusu kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Mkoa wa Kagera enzi hizo ukiitwa Ziwa Magharibi baada ya kupata uhuru ilikuwa ni miongoni mwa mikoa minne ambayo ilikuwa na utajiri na pato kubwa ikiwa ni Kilimanjaro, Dar es Salaam pamoja na Mbeya, na wakati huo ikiwa na Chama cha Ushirika (BCU) ambacho kilikuwa na nguvu kubwa kiasi cha kuikopesha hata Serikali, sasa maswali yangu.
La kwanza, je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba miongoni mwa mambo ambayo yamesababisha umaskini kwanza ni vita ya Kagera ambayo hata baada ya kualizika na Serikali ya Uganda kulipa fidia, wananchi hawakupewa fidia yoyote?
Pili, ugonjwa wa UKIMWI, lakini tatu Chama cha Ushirika cha KCU ambacho kimesambaratika na hususan kutokana na mambo mengi ya kisiasa badala ya kutetea zao la kahawa. Lakini pia Reli ya Kati ambayo kimsingi imesambaratika na haifiki Kemondo na hivyo wananchi wa Mkoa wa Kagera kupokea bidhaa kwa njia ya barabara ambayo inawagharimu vibaya sana.
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja pamoja na mambo aliyozungumza ambayo kimsingi bado yanaeleaelea na hayana mashiko, kuweka mkakati mahsusi wa kuyaweka katika utekelezaji na hata kuyaweka katika mpango wa BRN (Matokeo Makubwa Sasa), lakini sambamba na hilo kwa kupitia Mpango wa TASAF, kama Serikali imetathmini kwamba mkoa ni maskini na kaya ni maskini kwamba bajeti ya TASAF iongezeke ili kaya ziweze kupokea pato zaidi na kaya ziweze kuongezeka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kufuatana na sababu zilizotolewa na takwimu zilizotolewa, je, hizi takwimu zinatoa takwimu sahihi ambayo inaashiria ni kwa Wilaya zote au ni kwa baadhi ya wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Kagera ndiyo zenye umaskini wa namna hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nakubaliana na sababu alizozisema na ndiyo maana Serikali iko kwenye mpango mkakati wa utekelezaji wa mpango wetu ambao tumeuwasilisha humu Bungeni kama alivyosema tuje na mpango mahsusi wa utekelezaji kupeleka kwenye BRN, Serikali iko kwenye mchakato wa kuja na utekelezaji wa maazimio yote na malengo yote yaliyopo ndani ya BRN.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo utakumbuka ni kwamba tayari sasa hivi mchakato wa kutengeneza Reli ya Kati kwa standard gauge unaanza mwezi Disemba tunaanza utekelezaji na ambayo inaelekea upande huohuo wa Mikoa ya Magharibi na Kagera ikiwepo ili tuweze kufungua uchumi wa Mkoa wa Kagera na uchumi wa mikoa mingine ya upande wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu takwimu hizi, naomba niliambie Bunge lako Tukufu, takwimu hizi ni sahihi na zinaashiria Mkoa mzima wa Kagera kwamba upo katika kiwango cha umaskini wa asilimia 39 kama nilivyosema.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana. Swali langu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyozungumza hivi sasa wananchi wa Bukoba Town ambao walipata matatizo ya tetemeko, wako katika shida. Mbaya zaidi ni kwamba pamoja na miongozo, kamati hizo, mikakati tunayoizungumza, imepelekea kuona hiyo miongozo haiwasaidii, kwa sababu, hadi hivi sasa pamoja na miongozo na Kamati zenu ni kwamba hata misaada ambayo wamepewa au kuelekezewa na mashirika na taasisi mbalimbali ikiwemo Bunge hili, bado hawajapata misaada hiyo. Hebu uhakikishe hiyo miongozo inawaondolea uhalali wa kupata michango inayochangwa na taasisi mbalimbali, likiwemo hata Bunge hili lililowachangia, lakini misaada hawakuipata.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, miongozo tuliyoitoa ilikuwa ni miongozo ambayo inasaidia katika masuala yote ya maafa na zile Kamati zipo kwa ajili ya jambo hilo. Sasa kwa kesi ya Bukoba, michango iliyotolewa na taasisi mbalimbali likiwemo Bunge hili; na ukisoma hata katika Hansard ya tarehe 13 Septemba, 2016 wakati hoja ya Mheshimiwa Shangazi imesemwa hapa ya kuchangia, maelezo ya mwisho hayakusema michango ile inakwenda kufanya shughuli gani, lakini ilisema michango ile ni kwa ajili ya waathirika, kwa maana ya wahanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa twendeni pole pole.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa siku, maelekezo yalikuwa ni fedha hizi ziende zikawaguse wale ambao wameathirika (wahanga). Wakati huo huo, katika Kiti cha Waziri Mkuu hapa, alikuwepo Mheshimiwa Lukuvi kama Kaimu na alitoa tamko la Serikali kwamba fedha hizi zitawafikia wahanga, kwa maana ya wale ambao wameathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa turudi katika hoja ya msingi. Serikali ikijenga hospitali, Serikali ikiboresha shule ambazo zimebomoka, mwisho wa siku anayekwenda kuhudumiwa ni yule muhanga ambaye ni mwathirika. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba fedha hizi hazijawafikia walengwa. Zimewafikia walengwa kupitia katika huduma za hospitali na katika mashule.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali la kwanza, kufuatia majibu ambayo yametolewa na Serikali na kukubaliana na ukweli kwamba kweli kingo za Ziwa Victoria zinalika na maji kusogea. Kutokana na majibu ya Serikali itakubaliana nami kwamba mita 60 za mwaka juzi siyo mita 60 za mwaka jana na mita 60 za mwaka jana siyo mita 60 za mwaka huu kiasi kwamba inaondoa hata usahihi wa majibu au ushauri uliotolewa wa kuwazuia wananchi wasifanye maendeleo ndani ya mita 60 kufuatana na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004. Kutokana na ukweli huo, Serikali inatoa maelekezo gani kwa experience hii ya Ziwa Victoria ambalo linaendelea kusogea na kuondoa usahihi wa application ya sheria hiyo ya mita 60 kama ambavyo Serikali imeshauri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 57(1) na kufuatia ukweli wa kijiografia wa Bukoba town na Mkoa wa Kagera kwa ujumla ambao kimsingi una milima, mabonde na mtiririko wa mito mingi na kwamba wananchi hawawezi kuwa na mahali pa kuweka makazi yao, Serikali inatoa maelekezo gani kwa experience hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza anazungumzia usahihi wa ziwa kusogelea wananchi na kwamba inaleta shida katika kutambua zile mita 60. Nilisema katika jibu langu la msingi kwamba tutaenda kufanya utafiti ili tuweze kuona hali halisi yenyewe ikoje. Kama maji haya yamesogea, yamesogeaje kwenda kwenye makazi ya watu ili tuweze kujua. Tutakapofanya hiyo tathmini ndiyo itakayotupa majibu kwamba ni ziwa lenyewe limewasogelea wananchi au wananchi wenyewe wamejenga ndani ya mita 60 au wamejenga ndani ya mwambao wa ziwa ambao hauruhusiwi. Kwa hiyo, tathmini ndiyo ambayo itatupa majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopata majibu haya ya tathmini huwa kuna njia nne za kufanya:-
(a) Unaweza usichukue hatua yaani not doing anything katika ulichokiona.
(b) Unaweza ku-accommodate tatizo kwamba wananchi waishi kulingana na hali ya mazingira ilivyo kwa maana ya kwamba sasa wao wenyewe wazuie uharibifu wa mazingira, wakubali hali ya mazingira ilivyo, wajenge nyumba na miundombinu ambayo inaendana na hali halisi.
(c) Unaweza kupeleka njia za kuwazuia (protection) kama ambazo alipendekeza mwenyewe Mheshimiwa Lwakatare kwamba unaweza ukajenga ukuta, unaweza ukapanda miti, unaweza ukafanya mbinu nyingine za kuzuia maji yale yasiendelee kuwasogelea wananchi.
(d)Unaweza uka-retreat ambapo sasa unawataka wananchi wao wenyewe wahame na wasipotaka kuhama unawahamisha kwa lazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapofanya tathmini tutakuja na jibu la usahihi wa ziwa hilo na hali ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mahali pa kuweka makazi na lenyewe vilevile linategemea tathmini tutakayoifanya ndipo hapo tutakapopata mwanya mzuri wa kuwashauri wananchi wa Bukoba nini cha kufanya. Ahsante.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri, takwimu zinaonesha ukweli kwamba changamoto alizozizungumza zinasababisha kupeleka vijana wachache ukilinganisha na idadi ya vijana wanaomaliza kidato cha sita. Nataka kujua, kutokana na ufinyu huo, ni vigezo gani hivi sasa wanavyovitumia katika kuteua vijana wa kwenda kwenye mafunzo haya na wale wasiokwenda watawafanyaje sasa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hakuna vigezo maalum vinavyotumika isipokuwa tunachofanya ni random selection. Kwa maana hiyo katika kila shule wanachaguliwa vijana wachache kwa utaratibu wa random. Kwa hiyo, wale wote ambao wanachaguliwa ni wale waliopatikana kwa utaratibu huo; hakuna vigezo maalum kwa sababu wote wanastahili kuchukuliwa, lakini ni kwa sababu ya muda na rasilimali fedha ambazo nimezizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba kwa wale ambao hawajapata fursa ya kwenda huko, kwa sasa hivi hakuna utaratibu wowote uliopangwa, ni matumaini yetu kwamba uwezo ukiongezeka wa kuweza kuwachukua hata wale ambao wamemaliza vyuo vikuu, basi tutafanya hivyo wakati ukifika.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba mojawapo ya faida zilizomo katika mradi wa REA ambayo kawaida inaleta mvuto kwenye mradi huu ni pamoja na complementary au unafuu wa bei ambao wanapewa watu wanaosambaziwa umeme huo. Kwa mazoea ambayo yamezoeleka kwa umeme ambao unasambazwa na TANESCO ni kwamba bei za TANESCO zinakuwa kubwa kuliko zile bei au gharama za REA.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba Mheshimiwa Waziri anihakikishie kwamba hizi fedha zilizotengwa kwa ajili ya TANESCO na kwa maeneo ambayo ameyazungumza, ikiwemo na vijiji vya Ijuganyundo B ambavyo havina umeme kabisa, maeneo ya Makongo kule Kahororo na maeneo ya Chaya kule Busimbe, hizi gharama pia za TANESCO zitakuwa complimented au itakuwa ni gharama zilezile za TANESCO ambazo zimekuwa kubwa na watu wa maeneo haya ambao hawana uwezo wasiweze kupata umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili,...
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba tu atajibu mojawapo atakaloliona linafaa kwenye…
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba baadhi ya vijiji ambavyo vinaonekana viko ndani ya mji vinapelekewa umeme kupitia Shirika la Umeme TANESCO na ni kweli kabisa bei ni tofuati, bei za TANESCO kwa wateja wa awali kabisa ni shilingi 177,000 na kwa upande wa REA ni shilingi 27,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Lwakatare kwa jinsi anavyofuatilia maslahi ya wananchi wa Bukoba Mjini, ni mdau mzuri, lakini tunamhakikishia kwamba tutafanya upembuzi kwa ukina kabisa tuangalie kama vijiji vina sifa ya kupelekewa umeme kwa mradi wa REA tutafanya hivyo, tutakaa naye pamoja ili ikibainika basi wapelekewe kwa utaratibu wa REA.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie pia Mheshimiwa Muganyizi Lwakatare kwamba vijiji vyote ambavyo amevitaja vikiwemo vya Kashai, Mafumbo Tweyambe, Turabirere, Kahororo pamoja na visiwa vyake vya Nyabisaka pamoja na Msira vitapata umeme kupitia Mradi wa REA. (Makofi)
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pia niishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi yake ya kuwalipa wananchi hawa pale niliposhika Shilingi hapa ndani na wananchi wangu wakawa wamelipwa fedha hizi, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.Kwanza; ningependa kujua kutoka kwa Serikali hususan Waziri; ni lini wananchi hawa watalipwa riba ya fedha walizolipwa za fidia zaidi ya milioni 200 ambazo wanadai hadi sasa na hawajalipwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa bahati nzuri wananchi wa Bukoba Town wana Mbunge mahiri ambaye anaweza akasimamia na wakalipwa madai yao. Serikali inasemaje kwa watu wa maeneo mengine katika maeneo mbalimbali ya nchi hii ambao hawajalipwa fidia zao?Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme fidia inalipwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2001 kupitia Tangazo la Serikali namba 79. Si suala la umahiri wa Mbunge, ni Sheria imewekwa katika utaratibu wa kulipa fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijibu swali lake la kwanza la juu riba. Mheshimiwa Mbunge tarehe 10 Februari, 2017, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Salama BUWASA alileta barua ya kuomba fedha Sh.202, 164,107.75 kwa ajili ya malipo ya nyongeza baada ya malipo ya fidia kuchelewa zaidi ya miezi sita. Malipo hayo yalichelewa kwa muda wa miezi kumi na sita na sasa hivi Serikali tayari inafanya utaratibu wa kupeleka fedha hiyo ili wananchi waweze kulipwa haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maeneo mengine; utekelezaji wa miradi; na nizungumze kwamba Waheshimiwa Wabunge fidia siyo ajenda yetu, ajenda yetu ni miradi ya maji safi na salama; suala la fidia linaingia katika utaratibu wa kawaida wa kisheria, kwamba unapotekeleza mradi ukikutana na mali ya mwananchi Serikali imeweka Sheria kwamba lazima umlipe fidia kabla utatekeleza huo mradi. Kwa hiyo, Sheria hii inatekeleza kwa nchi mzima na tutaendelea kufanya hivyo.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri na kwa niaba ya Serikali, kwamba matukio ya moto ambayo yanatokea katika shule, yamekuwa pia yakitokea katika maeneo mbalimbali yakisababisha maafa makubwa. Lakini tatizo kubwa ambalo limeonekana kuchangia maafa kuwa makubwa ni pale ambapo vikosi vyetu vya Zimamoto vinapofika kwenye eneo la tukio na vikishafika pale magari yanaonekana yanakuja tu, labda kuja kutembea yanakuwa hayana maji na wala hawana vifaa, matokeo yake wakati mwingine wamekuwa wakiambulia kipigo au matusi kutoka kwa wananchi wenye hasira kali.
Je, Serikali inasemaje juu ya hili na wamejipangaje kuliondoa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kunachangamoto nyingi ambazo panatokea maendeleo na zenyewe zinajitokeza. Kwa mfano, miji inapokua majengo yanapojengwa, kuna maeneo mengine yanakuwa hayajatoa provision za magari ya kisasa kuweza kufanya kazi ile ya zimamoto.
Kwa hiyo, sasa hivi tunashirikiana na Wizara zingine zinazohusika ili tuweke provison hizo ambazo zitawezesha wenzetu wa zimamoto waweze kufanya hivyo. Lakini pia hilo jambo alilolisema lilishajitokeza maeneo mengi tumechukua hatua kuweza kuhakikisha kwamba, magari yanakuwa yako standby na vitendea kazi vyote vinavyotakiwa kwa ajili ya kwenda kuzima moto ili wasije wakafika kwanza halafu wakajikuta kwamba walikuwa na upungufu wa vitendeakazi vinavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumelizingatia na hata tulivyopitisha kwenye bajeti tulilielezea jinsi ambavyo tunakiunda upya kikosi kile kiweze kuwa na vitendeakazi vinavyostahili kwa ajili ya kukabiliana na matukio ya aina hiyo aliyoyasema. (Makofi)
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Spika, yako makabila ambayo kwa jadi yamekuwa yanatumia bangi kama mboga na wakati mwingine kuvuta, je, Serikali inatambua hilo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili Mbunge Musukuma wa Geita aliwahi kutamka hadharani hapa Bungeni kwamba kule Geita vijana wanatumia bangi, wakivuta bangi wanalima kuliko trekta, sasa majibu ya Serikali ambayo yanasema kwamba vijana waweze kusaidiwa kuacha matumizi ya bangi, je, Serikali haioni kwamba tunakwenda kudumiza kilimo na uchumi wao wa vijana wa Geita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba atambue bangi ni dawa za kulevya, ni katika dawa za kulevya na adhabu zake zote kwa mujibu wa sheria tulizotunga hapa nchini, inaunganishwa kwa pamoja na koka, heroin inaunganishwa pamoja na dawa nyingine zote za jamii ya opium na kwa msingi huo sisi kama nchi ambao tumesaini mkataba wa dawa za kulevya wa mwaka 1961, tumetunga sheria ambazo zinakataza matumizi ya bangi katika nchi yetu. Na kwa msingi huo sasa, hii anayoisema kwamba kuna makabila yanatumia bangi kwa asili kama chakula, kama mboga ni jambo ambalo sisi kama Serikali hatulitambui na ni jambo ambalo sisi kama Serikali tunasema ni kitendo cha uhalifu na watu hawa wakibainika kutumia majani ya bangi, ama maua ya bangi, ama magome ya bangi watachukuliwa hatua za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba bangi inaongeza nguvu, pamoja na Mheshimiwa Musukuma kumkana lakini naomba nilijibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwamba bangi haiongezi nguvu kwa sababu bangi katika mwili wa binadamu inapoingia na kuwa metabolized, inavunjwa vunjwa kwenda kwenye kemikali zaidi ya 500 na katika hizo kemikali 500, kemikali 113 ni sumu kwa mwili wa binadamu zilizo kali zaidi na kwa wingi zaidi kwenye bangi ni pamoja na hiyo niliyoitaja wakati wa jibu langu la msingi inayoitwa THC au tetrahydrocannabinol lakini zipo CBD na zipo CBG na zipo CBE zote hizi kemikali ni hatari sana kwa afya ya akili na mtu akivuta hivi kemikali nilizozitaja 113 kwanza anadhoofu mwili wake, anakuwa na uchovu, kwa maana ya kupata refuge, lakini pili anachanganyikiwa kwa muda mfupi na kama hujawahi kuona mtu ambaye amepata kichaa cha ghafla, basi baada ya kujibu swali hili njoo uniulize nitakupa historia ya kijana mmoja ambaye tulisoma naye Kigoma secondary school, ambaye alijaribu kuonja bangi akiwa kidato cha tatu na alianza kuona barabara ikinyenyuka hivi, na kwa hiyo alikuwa akitembea kwa kunyanyua miguu kama mtu anayepanda ngazi. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kusema kwamba bangi ambayo inadhoofisha mwili, inaongeza nguvu hilo nalikubali kisayansi.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali iliyoyatoa hapa, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na takwimu kubwa alizozitoa ambazo zinaonyesha kupanda kwa mapato ni ukweli usiopingika kwamba yapo maeneo mengi kwelikweli ambayo hayajafikiwa na TRA kwa sababu ya mtandao wake mdogo, kiasi kwamba TRA hata kufanikisha hiki kilichofanikisha imelazimika kuwatumia Maafisa Watendaji wa Kata ambao ni waajiriwa wa Halmashauri hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Serikali isichukue wazo langu la kujaribu kuweka category mbili kwamba baadhi ya tozo hii ya property tax na hasa za majumba makubwa zitozwe na TRA lakini kwa majengo ya chini yatozwe na Halmashauri zetu na hiyo itaongeza ufanisi badala ya kuzi-tight kwenye Majiji 30? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; suala la mapato na makusanyo kupanda limekuwa ni wimbo wa kila siku, kutoka kwenye taarifa za Serikali pamoja na TRA, lakini Bunge kupitia Kamati zake na kupitia kwenye Halmashauri zetu…
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini taarifa zinaonesha Taasisi nyingi za Serikali na Serikali yenyewe na Mashirika pamoja na Halmashauri zetu hata Bunge lenyewe limeshindwa kwenda sambamba na bajeti kiasi kwamba maeneo mengine ina-read zero, zero wakati wanasema wanakusanya sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpomngeze kwa kukiri kwamba anaelewa sasa mapato ya Serikali yamepanda katika nyanja zote kwa kodi zote zinazokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania ikiwemo kodi ya majengo, nakupongeza sana shemeji yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hili alilolisema sasa tugawanye kwamba majengo makubwa yakusanywe na Mamlaka ya Mapato na madogo yakusanywe na Serikali za Mitaa, tutajikuta tunatumia nguvu za aina mbili katika eneo moja bila sababu yoyote ya msingi. Serikali yetu na Bunge lako Tukufu tulipitisha Sheria ya Fedha, kwamba kodi ya majengo ikusanywe na Mamlaka ya Mapato kwa lengo la kuimarisha ufanisi wake katika ukusanyaji na ufanisi wake katika matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali tutaendelea kusimamia sheria hii kuhakikisha kwamba lengo la kuchukua kodi hii linafikiwa na wananchi wetu wanapata huduma stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kwamba sasa bajeti hai-reflect mapato. Ni siku mbili zilizopita Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI amesema tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani kwa mwaka huu wa fedha kwa robo tu ya kwanza Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepata zaidi ya shilingi trilioni moja katika bajeti zao. Serikali inafanya vizuri kwenye ukusanyaji lakini pia tunafanya vizuri kupeleka fedha hizi katika kila taasisi ya Serikali yetu. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Ningeomba niulize maswali mawili ya nyongeza mafupi. Kwa kuwa, Serikali inatambua kuwa eneo hilo ambalo limetajwa kama vyanzo vya maji kwamba halipashwi kupewa huduma zozote na inawataka wananchi kuhama. Serikali inasemaje kuhusu huduma nyingine ikiwamo ya kuwepo viongozi ambao wamechanguliwa kwa kura na kura zinaendelea kufanyika pale eneo hilo na viongozi waliochaguliwa wengine ni wa CCM ambao wanaongoza eneo hili, Serikali inasemaje hiyo huduma ya kiuongozi nayo hawaitambui. Kwa hiyo, waondokeje wakati kuna uongozi uliochaguliwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Sheria namna ilivyo kwa hali halisi inajichanganya sana kutokana na tafsiri ya chanzo cha maji cha mita 60, lakini Serikali imewahi kujibu hapa kutokana na hali halisi kwamba kuna maeneo ambayo kijiografia leo hii ukiwaondoa watu kwa mita hizo 60 wakiwemo wananchi wa maeneo mbalimbali ya Bukoba Town ni kwamba Mji wa Bukoba Town hautakuwepo kwa sababu kila mita 60 kuna mto kuna chanzo cha maji. Serikali inasemaje katika kuleta kanuni ambazo ilisema itazileta ambazo zinaweka tafsiri pana na inayofafanua hizi mita 60 zina maana gani? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, huduma za kiuongozi katika eneo tengefu, niseme watoke. Watoke na wala huduma ya kiuongozi huko haitakuwepo, wala huduma ya aina yoyote watoke, wakisubiri wataondolewa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu mita 60, namshukuru sana Mheshimiwa Lwakatare, definition ya mita 60 inalenga maeneo fulani fulani. Sasa hivi tumeanza kuzungumzia suala hili ukiangalia katika mito kuna mito kuna vijito na kuna vi-stream vingine ni vidogo sana ambavyo pengine mvua ikinyesha kinaweza kikatiririsha maji kwa wiki moja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, inabidi tuwe na definition pana, mita 60 inalenga wapi, ni kwa kila kamto hata mto kama Rufiji kwenye mito ambayo ni mikubwa ina mabonde makubwa definition ya mita 60 haipo na ndiyo maana kwenye bwawa la Nyihongo mipaka yake imekuwa ni mikubwa zaidi kuliko hiyo mita 60. Tunalenga pia lile eneo ambalo ni oevu ambalo ndiyo linafanya sasa lile bwawa liweze kuishi. Kwa hiyo, hii tutaiweka vizuri ili kuondoa mkanganyiko kama uliotaka kujitokeza hapa wa vinyungu.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza.La kwanza, kwa wananchi wa Bukoba Town na Kagera kwa ujumla usafiri wa meli ni ajira, usafiri wa meli ni usafiri wenye nafuu na wenye kuaminika na usafiri wa meli unatoa unafuu wa bidhaa mbalimbali zinazokwenda Mkoa wa Kagera kuliko ilivyo sasa. Sasa miaka 22 tangu MV Bukoba izame na ahadi za kupata meli mpya zianze kutolewa tangu awamu ya Mheshimiwa Mkapa ni miaka mingi; je, wananchi wa Bukoba na Kagera kwa ujumla wakijenga hisia kuwa wanatengwa watakuwa wanakosea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nini kimekuwa chanzo cha mazungumzo baina ya Serikali na makampuni kutofikia makubaliano ili meli mpya ijengwe na wananchi wa Kagera ambao wanaadhimisha mwezi Mei huu kukumbuka waliotwaliwa ili waweze kuwa na matumaini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. Eng.ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi wananchi watakuwa wanafanya kosa kubwa sana kuona kwamba wanatengwa kwa sababu hatua mbalimbali za Serikali zimekwishaanza kuchukuliwa na nimeeleza wazi kwamba tayari kuna Mkandarasi ambaye amekuja kwa ajili ya kuingia mkataba wa kujenga meli hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi hasa tumeshindwa kuingia nao mkataba kwa sababu hatupendi tuwadanganye wananchi na vilevile hatupendi Serikali yetu iingie kwenye gharama zisizokuwa na sababu kutokana na kuingia mikataba ambayo siyo ya uhakika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili tumeshindwa kuingia mkataba nao kwa sababu kuna vigezo mbalimbali vya kiufundi na kiutaalam ambavyo walitakiwa waviingize katika mkataba wao, wao walivisahau. Sasa hivi nimhakikishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wameviingiza na wao tena wameomba tender katika kuhakikisha kwamba wanatengeza hiyo meli mpya, tunahakikisha kwamba tukishapatana nao vizuri meli itajenga na inawezekana wakapata wao au wakapata watu wengine. (Makofi)
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kuanzisha Makambi ya vijana ni jambo linaloonekana linaweza kuwa na tija. Lakini je, kutokana na experience ya makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa kwamba wako vijana ambao wanamaliza Jeshi la Kujenga Taifa lakini wanaachwa idle. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja kwanza kuimarisha mafunzo yanayotolewa JKT na kuwa-accommodate vijana wanaomaliza JKT ili tujifunze kutokana na JKT kabla hatujaingia kwenye mpango huo wa makambi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa zimekuwepo programu mbalimbali za mafunzo ya ujasiriamali pamoja na kilimo na kupitia mafunzo hayo vijana wengi wameanza kuhamasika kufanya shughuli za kilimo na sisi Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, tumeanza majadiliano na mpango kati ya kwetu sisi na JKT ili vijana hawa wote ambao wanapata mafunzo baadaye tuwasaidie katika uwezeshaji ili wafanye shughuli za kilimo. Kwa hiyo, mpango huo upon a tunaendelea kufanya mazungumzo na JKT.