Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Gibson Blasius Meiseyeki (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimefurahi jinsi ulivyolipatia jina langu, limekuwa likiwapa shida sana watu hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza pia kuzungumza katika Bunge lako, nichukue fursa hii kuwashukuru sana wananchi wangu wa Arumeru Magharibi kwa kura nyingi za kishindo ambazo wamenipatia. Labda tu ili uweze kuweka rekodi zako, mimi ndiyo niliyeshinda kwa tofauti ya kura nyingi kuliko Mbunge mwingine yeyote, takribani kura 62,000; siyo kidogo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti nakwenda moja kwa moja kwenye mchango. Nimefurahia, hotuba ya Waziri ilikuwa nzuri kama ambavyo zimekuwa zikitolewa hotuba nyingi nzuri humu ndani, lakini kwa kweli nina mashaka sana na utekelezaji wake. Takribani miaka kumi iliyopita, Wizara yake ya Kilimo ilikuwa ndiyo wimbo wa Serikali iliyopita, Kilimo Kwanza, lakini mpaka sasa hivi tumeshindwa kujua kilimo hicho kimetufikisha wapi na sasa kwa Serikali hii ambayo hatuoni namna gani ina-incorporate Kilimo Kwanza na Serikali hii ya viwanda ambayo mnakwenda kuifanya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi pia katika hotuba ya Waziri unanijia ni jinsi gani, sijapata kuona ni kwa namna gani anakwenda kumaliza matatizo ya migogoro ya wakulima na wafugaji; na wafugaji kwa wafugaji wenyewe? Ni matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wilaya yangu kuna triangle moja ambayo sisi Monduli na Longido, wafugaji ambao wote ni Wamasai wanajeruhiana kila kukicha, wanagombania mpaka, kwamba ng‟ombe akitoka Arumeru Magharibi akaenda upande wa Monduli ni tatizo; akitoka Monduli akaja Arumeru Magharibi ni tatizo; akitoka Longido akaingia kwenye mashamba, sasa tunashindwa kuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii migogoro ya namna hii ni kweli kwamba Serikali imeshindwa namna ya kumaliza matatizo haya ya wafugaji? Inakuwa vipi ng‟ombe wanaweza kutoka Arusha kwenda mpaka Morogoro, wakazunguka mpaka Mkoa wa Pwani; ukiondoa ile migogoro yao na wakulima; wafugaji kwa wafugaji hawagombani kwenye maeneo hayo, lakini wale ambao wanakaa, wako settled wanagombania mipaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Serikali ingekuja na kauli kama ambavyo tulivyo sisi Watanzania ambao tunaweza kuingia kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kama ni maeneo ya wafugaji kwa wafugaji, hakuna sababu ya kupigana kugombania nyasi, nchi hii ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ambayo ina ukubwa kuzidi nchi karibu nne za Afrika Mashariki; Kenya, Uganda na Rwanda ukiziweka pamoja bado Tanzania ni kubwa kuliko hizo nchi. Hizo nchi zina watu karibu milioni 100, sisi tuna milioni 50 tu. Nchi hii ni kubwa, ni nzuri ina karibia kila kitu kinachotakiwa. Hii ndiyo nchi ile ambayo ni ya asali na maziwa, lakini Serikali imeshindwa kuwatenga wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kutenga maeneo ya wanyamapori, tumeweza kutenga maeneo ya misitu, lakini tumeshindwa kuwatengea wakulima maeneo yao, wafugaji maeneo yao. Ni masuala ya kutoa kauli tu, tutengeneze corridor. Tutengeneze corridor ambayo wafugaji watakuwa wanaitumia bila kujali ni wa asili gani; awe Mmasai, Msukuma, Mnyamwezi, nani, kama kuna malisho na hayo maeneo yawe kama ni ya Serikali vile. Maana ni vigumu sana kwa wafugaji kupata hatimiliki kwa ajili ya kulisha mifugo mingi ambayo wanaifuga. Kwanza mifugo yenyewe inakwenda kulingana na malisho yanavyopatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungetengeza corridor, kama ambavyo tumetengeneza Game Reserves kama ilivyozungumzwa hapo awali, tutengeneze corridor ambayo itakua ni ya wafugaji. Kama alivyosema Mbunge mwenzangu ambaye alitangulia awali, maeneo hayo yawe ni maeneo ambayo kuna maji, watawekewa miundombinu ya majosho na pia kuwa na maeneo ya masoko pia ili wafanyabiashara waweze kupata access ya kununua mifugo hiyo. Hii nchi ni kubwa na ina kila kitu. Kwa hiyo, tunaomba mtusaidie kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kiukweli hotuba hii ya Waziri kama hataidadavua vizuri namna gani anakwenda kukabiliana na tatizo la migogoro kwa kushirikiana na mwenzake Waziri wa Ardhi na pengine na Waziri wa Maliasili, ili tuweze kupata maeneo sasa na kuhitimisha suala hili la migogoro ya ardhi ambayo inalitia Taifa letu aibu, Taifa hili ni kubwa lina kila kitu tunashindwa kuvigawa. Kwa hiyo, Mawaziri hawa wakae pamoja na watuletee mpango ambao utatuonyesha ni kwa namna gani wakulima wetu wanakuwa safe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna tatizo kubwa sana la upatikanaji wa hatimiliki za ardhi kwa ajili hata ya hawa wakulima. Mimi kama nilivyosema, wakati mwingine ni mkulima lakini pia mfugaji. Ni mkulima wa ukweli, nalima kweli kweli, lakini tumekuwa tukipata shida sana ya kupata hatimiliki ya maeneo ambayo tumeomba na pengine hata Serikali ilitoa kabisa kwa ajili ya kulima lakini kuipata hatimiliki inakuwa ni shida sana. Kwa hiyo, Mawaziri wahusika wakae na wakubaliane kwa sababu bila hati pia unashindwa kupata misaada kwenye mabenki.
Kwa hiyo, Mawaziri wahusika wakubaliane namna gani wanaweza kuharakisha wakulima waweze kumilikishwa ardhi ili waweze kupata pia access ya mikopo ambayo inatolewa na mabenki na taasisi nyingine za kifedha. Kwa hiyo, tungependa tupate hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye suala la mbegu bora kwa ajili ya mazao ambayo wenzangu wamezungumza sana. Labda niseme tu Mheshimiwa Waziri, hii picha uliyoipiga hapa kwenye cover yako; hii picha ya dume inanipandisha mori kidogo. Hii ndiyo mbegu ambayo nilikuwa nasema tunataka tuzipate; mbegu bora ya ng‟ombe wa nyama, ndiyo kama hii. Mbegu hizi kwa kweli kwenye taasisi zako zinazozalisha mbegu bora, wanaziuza ghali sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dume kama huyu akiwa mdogo tu na mwaka mmoja, anauzwa shilingi 800,000 au shilingi milioni moja na kuendelea. Hii ndiyo bei halisi iliyopo. Kwa dume kama hili lililopo kwenye picha yako Mheshimiwa Waziri, mimi nimetoka mnadani juzi tu, shilingi milioni moja, shilingi milioni moja na nusu unapata hili dume, lakini ninyi mbegu mnauza shilingi 800,000, shilingi milioni moja. Hii mbegu ni kubwa na haionyeshi ile commitment ya Serikali kuwasaidia wakulima kuweza kubadilisha mbegu zao ambazo ni zile tunaita katumani. Kama ni mahindi tuite katumani; unalisha miaka mingi sana haifikishi kilo 100.
Kwa hiyo tusaidie tena, ulinijibu juzi kwenye swali lakini nisisitize tu kwamba bei mnayouza bado ni ya juu sana, mtusaidie ili tupate ng‟ombe wa namna hii ikiwezekana nchi nzima. Kwa hiyo, hilo naliomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alizungumzia ushuru wa mazao kutozwa sokoni. Naomba kabisa kwamba ikiwezekana ushuru huu utozwe shambani inapotoka. Kwa sababu haiwezekani Maafisa wa Halmashauri zetu wawasaidie wakulima lakini wakati wa kuvuna tozo inakwenda kuchajiwa Kariakoo; itakuwa mmetupunja. Kwa hiyo, naomba ushuru uchajiwe mara moja tu; kama ni mashambani au kwenye road block zilizopo kwenye Halmashauri na sokoni wasitozwe tena; kwenda kuitoza sokoni utakuwa umewadhulumu Halmashauri ambayo imekuwa ikiwasaidia wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chakula cha njaa; enzi za Mwalimu kulikuwa na ile programu ya kwamba kila mkulima ni lazima awe na akiba ya chakula anapokuwa amevuna. Hiyo imekwisha, siku hizi hakuna na Serikali inahangaika na vigaloni au vidumu, chakula kiasi kidogo ambacho inakwenda kuwadanganyia wananchi na tunaona kama hii ni siasa ya kura. Serikali ije na mpango kama ule wa Mwalimu, kwamba kila mtu anapovuna awe na kichanja cha kuhifadhi chakula ili wakati wa njaa aweze kukabiliana na njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wanavuna halafu wanauza yote, halafu kesho Serikali inaanza kuhangaika kuwagawia kilo mbili mbili au tatu tatu za mahindi, kitu ambacho hakiwasaidii. Kwa hiyo, tuwe na mpango wa kisera kwamba wakulima waweze kushawishiwa kuhifadhi chakula baada ya kulima na tuepukane na hii kusambaza chakula ambacho hakiwatoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyeikiti, kwa hiyo ningependa pia kuishauri Wizara, nilipata fursa, nilikuwa Diwani hapo awali, nikatembelea nchi moja ya jirani hapo, sitaitaja. Kwa kweli tuliona wana mpango mzuri sana wa kuwasaidia wakulima. Wakulima wanapovuna kwa fujo, wamebahatika kupata mazao, wanakwenda kuyahifadhi vizuri kwenye maghala ya Serikali; na yale maghala yanakuwa yanathaminisha kile chakula au yale mazao ambao mkulima ameyazalisha na anapewa hati. Nafikiri nilishasikia hapa, sijui mnasema sijui ghala sijui nini, kitu kama hicho. Ile hati inamwezesha mkulima kwenda kukopa benki wakati anasubiria bei ya mazao yake yaweze kupanda value. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inamsaidia yeye kuweza kusomesha watoto wake au kujiandaa kwa msimu mwingine wa kilimo na kwa maana hiyo halazimiki kuyauza kwa bei ya haraka haraka. Tena anakuwa ameweka sehemu ambayo ni salama kimatunzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alisema hapa kwamba kuna dawa ambazo unawanyunyizia wadudu lakini wanaogelea tu na kutokea upande wa pili. Sasa kwenye maghala ya Serikali watapata fursa ya kuweza kuyatunza vizuri na kwa maana hiyo anakuwa na uhakika wa uhifadhi wa chakula kile na wakati huo Serikali ikimtafutia bei nzuri ya mazao hayo. (Makofi)
Naishauri pia Serikali, kama ambavyo ina kitengo kinachoshughulikia kutafuta ajira ndani na nje ya nchi, kuwe na chombo, kuwe na bodi kama ilivyo Bodi ya Utalii ambayo itakwenda nje ya mipaka yetu kutafuta masoko ya bidhaa ambazo tunazizalisha hapa nchini ili tuweze ku-entertain wananchi wengi kuingia kwenye kilimo kwa maana ya kwamba masoko yatakuwa yanapatikana. MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwa bahati mbaya siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja ya Wizara ya Ardhi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Waziri Mheshimiwa William Lukuvi kwa kuchaguliwa tena kuongoza Wizara hii, hakika anaweza. Nampongeza pia na kumshukuru kwa ziara aliyoifanya Jimboni kwetu kwani ilitupa mwanga wa utatuzi wa migogoro mingi ya ardhi iliyotuzunguka. Bado tunamhitaji Mheshimiwa Waziri Arumeru ili tuweze kumaliza kabisa changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya sababu ambazo zinasababisha migogoro ni Serikali kuwapa wawekezaji maeneo makubwa mno kuliko uwezo wao na kuyaendeleza. Hii hupelekea wawekezaji kufanya biashara kukodisha ama kugawia wananchi mashamba hayo ambayo baadaye hushindwa kuwaondoa pindi wanavyotaka kufanya shughuli nyingine katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo kama haya hasa katika shamba ya Fill Estate na Tanzania Plantation yote katika Jimbo la Arumeru Magharibi, Kata ya Bwawani. Wananchi wameumizana sana na vyombo vya dola na zaidi ya watu 11 wapo rumande kwa miezi miwili sasa kwa kubambikiziwa kesi ya wizi wa kutumia silaha eti kwa sababu tu wanagombania shamba na askari polisi ambao wawekezaji wakawakodisha katika shamba ambalo wananchi tayari walikuwepo kwa lengo la kuwatoa kwa nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Arumeru karibu sasa yote inakuwa mji, hivyo mashamba mengi ya wawekezaji yamemezwa na idadi kubwa ya wananchi wanaoongezeka kila kukicha na hivyo mashamba haya yanalimwa mjini na bado hayajaendelezwa vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali huchukua muda mrefu sana kubatilisha haki za umiliki za wawekezaji zilizopita muda wake na kupelekea wananchi kuvamia mashamba hayo na kuanza kujigawia. Serikali sasa ichukue hatua madhubuti kutengua hati za ardhi ambazo muda wake umeisha. Hii ni pamoja na kuwatafutia maeneo mengine wawekezaji ambao mashamba yao yameingia ndani ya miji kuepusha migongano zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu linaelekea pabaya hasa jinsi suala la migogoro ya ardhi inavyoshughulikiwa, Taifa linaelekea Zimbabwe. Kwa Mkoa wetu wa Arumeru hali siyo shwari kwa wawekezaji na hivyo wapo kwenye hofu kubwa sasa, wananchi kila wanapoona shamba kubwa basi hulazimisha wanasiasa kufanya liwezekanalo ili wanyang‟anywe na wapewe wao, jambo ambalo siyo zuri kwa ustawi wa Taifa letu ambalo bado linahitaji wawekezaji kwa ustawi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kwa Serikali, hasa kwa Mkoa wa Arusha kuboreshewa miundombinu inayounganisha mikoa mingine hasa Manyara, Wilaya ya Simanjiro ili kuwaunganisha wananchi hawa na maeneo hayo ambayo bado ardhi ni virgin. Mashamba yaliyo mjini na muda wake umekaribia kwisha, Serikali iyatwae na kufanya mipango mipya ya ardhi/mashamba hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wanasiasa siyo rahisi kutoa elimu ambazo siyo rafiki kwa wananchi kuhusu umiliki wa mipango ardhi, Serikali kwa kutumia vyombo vyake, elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi kuhusu sera za ardhi na umiliki mashamba ili wananchi waache tabia ya kuvamia mashamba ambayo nyaraka zake ziko thabiti/genuine ili kuhakikisha kwamba wawekezaji ambao Serikali inahangaika kuwaalika wanakuwa salama na wanafanya kazi zao kwa amani na utulivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninamwalika tena Mheshimiwa Waziri Jimboni Arumeru Magharibi ili tumalizie migogoro iliyopo once and for all. Ahsante sana, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kabla sijachangia nikiri kwamba mimi ni mfanyabiashara wa utalii kwa takribani miaka 12 sasa kwa hiyo ni field yangu ya experience.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachangia kwa masikitiko kwa kiasi fulani, wengi wamezungumza hapa kila mmoja anafahamu ni kwa kiasi gani nchi yetu ni nzuri, iko kwenye at least top ten za dunia, lakini tumekaa hapa tunashangilia, wakati fulani Wabunge huku walipiga makofi kwamba tumefikia watalii milioni moja. Watalii milioni moja ni wachache mno, sana kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama South Africa ambayo tuko equally beautiful I would say. Wanakwenda sasa hivi watalii milioni 12 kwa mwaka, Misri wako milioni 15, wakati ule kabla hawajagombana sijui sasa hivi iko ngapi. Nchi kama Thailand nazungumzia nchi ambazo hazina uchumi mkubwa kama sisi, wana watalii milioni 25 kwa mwaka, Indonesia, Singapore milioni 15; Tanzania watalii milioni moja tunashangilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa umefika tufanye jitihada za maksudi kuhakikisha kwamba tunanyanyua kiwango hiki cha watalii wanaokuja Tanzania, kiukweli kama sasa hivi wanakuja milioni moja tu wanachangia asilimia 17 ya GDP yetu wangefika milioni tano ingekuwaje, kwa mfano? Ingekuwa ni zaidi ya nusu ya GDP; kwa maana hiyo ingeweza ku-observe shock zote hizi za matatizo ya ajira kwenye Taifa letu, ningekuwa nina mamlaka ningeweza kusema kwamba Serikali yenu hii ya sasa angalau ingechukua vitu vitatu comprehensively. Ingechukua viwanda vya Mheshimiwa Mwijage kama anavyokuja navyo vizuri; amejipambanua vizuri Mheshimiwa Mwijage kwenye viwanda, mchukue Mheshimwia Mwigulu kwenye kilimo, mifugo na uvuvi, ukaweka na utalii hapo tunaweza kuchukua watu wengi ambao hawana ajira katika Taifa letu tukawa-absorb kwenye maeneo haya. Hivyo, ningeshauri tu kwamba tuangalie ni sababu zipi zinapelekea Taifa letu kukosa watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uzoefu nilionao mimi, nimekwenda kwenye trade fair za kutosha na watu wa Mheshimiwa Maghembe wa TTB nimekwenda nao na nina masikitiko makubwa sana kusema kwamba watu wetu wa TTB wanakwenda kwenye trade fair kupumzika, hawaendi kufanya kazi ukilinganisha na mataifa mengine ambayo tunayakuta kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata nilivyosikia mmewanyang‟anya sijui fungu mmelipeleka wapi niliona ni sawa tu, kwa sababu wenzetu wale wanakwenda kupumzika hawaendi kutafuta biashara, mara nyingi nimekwenda nao kwenye masoko mbalimbali nje ya nchi. Kwa hiyo, niseme kwamba tuangalie tena ni maeneo gani ambayo mojawapo ni kwamba Tanzania ni destination ambayo ni very expensive, ni ghali mno kuja Tanzania ukilinganisha na kwenda maeneo mengine ambayo naona watu wanaweza wakawa wanavutika kwenda kutalii maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tu-review tena hizi sababu ambazo zinasababisha tuwe ghali. Kwa mfano, airport zetu wanasema handling fees ni mojawapo inayosababisha tiketi ziwe ghali kwa watalii wanapotaka kuja Tanzania. If that is the case na kwamba kweli tunataka ku-promote utalii Tanzania tufike hiyo namba ya watalii ambayo mmeiweka target kwa sasa hivi ambayo ni milioni tatu ambayo naiona ni wachache, tuangalie hivi sababu vidogo vidogo, handling fees, airport departure taxes zile mnazi-regulate vipi ili kupunguza gharama ya mtu kuja Tanzania, maana yake mtalii anapokuja tusizungumzie ile package tu ambayo anailipa kuja kufanya utalii, lakini zungumzia pia na fedha anazokuja nazo mfukoni nyingi ambazo Watanzania wengi huko mitaani wanazisubiri kuuza bidhaa zao, vitu mbalimbali ambavyo wazungu wanavinunua. Tena wanavinunua kwa kusema mzungu price, tourist price, siyo kama wengine. Sisi tunakunywa soda shilingi 600, shilingi 700; mzungu anakunywa kwa shilingi 2000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakifika milioni tano ina maana kutakuwa na dola nyingi ambazo tutazi-retain hapa, ambazo zimekuja indirect. Kwa hiyo, tuangalie mapato ambayo ni indirect, mtalii anaweza kutuletea. Kwa hiyo, tujaribu kuwa-entertain waje kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine vitu vingine vinavyosababisha tukose watalii wa kutosha, kuna hizi issue za viza, tusishindane na Uingereza, Ufaransa sijui na ninyi mnapokwenda kutembea nje mnalipa viza kubwa. Muingereza aki-charge laki mbili kwenda Uingereza, tusishindane nao kwa sababu wale wanapokea watalii karibu milioni 50 kwa mwaka, sisi watalii 1000! Kwa hiyo, tuangalie namna gani tunawa-entertain kupunguza mzigo ili hawa watu waje wakishafika hapa ndiyo tutajua jinsi ya ku-deal nao, mnafahamu pia kwamba mtalii anapofika hapa anachukua precautions nyingi sana.
Mheshimiwa Waziri, nisikitike kwamba figures ambazo umetupa hapa za watalii waliokuja mwaka jana siyo sahihi. Utalii mwaka 2014/2015, ume-drop kwa zaidi ya asilimia 50 mzee. Ugonjwa wa Ebola ilitu-affect sana na tumepunguza wafanyakazi sana kwenye makampuni yetu huko Arusha. Niseme tu kwamba ukitaka kufanya uhakiki vizuri wa hili jambo kesho kutwa week end inayokuja kuna Karibu Fair, nenda pale utawakuta wadau wa utalii, wahoji, waulize biashara ilikuwa vipi bila kujali ninyi mmekusanya kiasi gani, kwa sababu kuna mbinu nyingi za ninyi kukusanya mapato, kwa hiyo, utalii uli-drop sana, toka Ebola ilivyozuka, tulipoingia kwenye uchaguzi pia watalii wanatabia ya kutotembelea nchi, lakini ninyi rekodi zenu zinasema ni 80 percent, siamini kama hiyo ni sahihi na tukafanye utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazungu wanapokuja, sorry kule Arusha tumezoea kusema wazungu, badala ya kusema watalii. Watalii wanapokuja wanameza dawa za malaria, lakini pia kwa baadhi ya nchi wanapofika airport wengine kama hawajadungwa sindano, wanandungwa sindano ya yellow fever, pale panatokea kizungumkuti kikubwa sana unajua siyo kila mmoja anapenda kudungwa sindano, wakija pale maafisa walioko pale wengine hata kwa yale mataifa ambayo hayatakiwi kudunga hizo sindano wanakamatwa wanakuwa harassed, wakati mwingine hongo zinatembea wanaingia bila kudungwa hizo sindano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme kwamba tufanye overhaul ya marketing strategies zetu tukafanye kazi. Ningeshauri kwamba yale mataifa ambayo ni makubwa yanaleta utalii kama Ujerumani, Uingereza, Canada, USA nimesema, Japan tuseme na China; kwanini tusifungue ofisi kule na tukawapa watu kazi na wapewe target ya kuhakikisha kwamba wanaleta wageni Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachina ni watu ambao wana uchumi mzuri sana sasa hivi lakini kiukweli tumeshindwa kuwa-reach kwenye soko lile. Pamoja na kwamba kweli tunataka kujilinda wenyewe hapa ndani kwenye suala la utalii wawekezaji kutoka nje ni muhimu sana. Kuna matatizo ya lugha na connection, tukisema kwamba sisi wamatumbi hapa ndiyo tuifanye tu peke yetu hatutafikia hiyo target.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo Immigration waangalie namna gani tuna collaborate na hawa watu wanaotoka nje, maana hawa ndiyo wana access na masoko ya kule kwao. Tuwarahisishie utaratibu wa kuingia hapa na wao watakapoleta wageni wakifika hapa kwetu na sisi tutapona hapo. Lakini tukisema tufanye wawekezaji wa ndani na nini? Kumchukua mzungu kutoka ya kuwekeza kwetu, tuwawekee mazingira mazuri, na yawekwe rahisi kama Rwanda wanavyo fanya, Tanzania tumekuwa na bureaucracy kubwa sana, ningeshauri kwamba tuangalie hivyo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Airlines, pamoja na kwamba mnakwenda kununua ndege zenu ambazo ni chache kwa kweli na ningeshauri pia kwamba tununue na zile ndege ndogo kama hizi za Precision Air - HR kwa ajili ya kuweza kuhudumia viwanja vyetu vidogo vidogo hapa ndani, kulikoni kuwaachia private sectors ambao flight charges zao ni ghali sana. Kutoka tu Arusha kwenda na kurudi Serengeti shilingi 800,000. Kwa hiyo, tuwe na ndege za Serikali au ambazo tunaweza tukawa na ubia ili tuweze ku-regulate price za fares. Tuweze kutoa wageni Arusha kuwapeleka Ruaha, Katavi na maeneo mengine kama Mikumi, kufanya hivyo sasa hivi ni tatizo, mgeni akileta enquiring kwenye makampuni yetu anataka kwenda Kusini na sisi tuko Kaskazini huwa hatufanyi hiyo biashara, kwa sababu ya jinsi ya kufika kule gharama ni kubwa sana na pengine kwa sababu ya uchache wao tunakuwa hatuna contacts. Kwa hiyo, tuboreshe maeneo hayo ili tuweze kutanua huu uwigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini airlines za kimataifa…
MWENYEKITI: Ahsante sana.