Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Amb Dr. Diodorus Buberwa Kamala (21 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa hii fursa ya kutoa mchango wangu. Nianze kwa kuwashukuru wapiga kura wa Nkenge kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kunirejesha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii pia, kupongeza hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Rais alipozindua Bunge hili. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa taarifa aliyowasilisha leo hii hapa Bungeni ambayo imezingatia pia maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Rais katika ukurasa wa 16, alibainisha kwamba matarajio yake ifikapo mwaka 2020 angalau viwanda viweze kutoa ajira 40% ya ajira zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa sasa na taarifa za Mheshimiwa Waziri alizowasilisha, inaonesha kwamba kwa mwaka 2014 viwanda vimetoa ajira kwa asilimia 3.1. Sasa lengo letu ni kuhakikisha sasa viwanda vitoe ajira ifikapo mwaka 2020 kwa 40%. Sasa kutoka asilimia 3.1 kwenda 40% kuna kazi kubwa ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu wa leo, nitabainisha masuala muhimu ambayo yakizingatiwa tutaweza kufikia 40% ya ajira kutolewa na viwanda. Jambo la kwanza, ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amebainisha kwamba, kwa vyovyote vile itakavyowezekana lazima tutekeleze utekelezaji wa miradi mikubwa ya kielelezo au wanasema flat projects.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimepitia ile orodha ya ile miradi, nikagundua kuna mradi mkubwa umesahaulika kwa bahati mbaya na mradi wenyewe ni ujenzi wa Kajunguti International Airport. Mheshimiwa Rais alipokuwa kwenye kampeni, jambo mojawapo aliloahidi wana Misenyi, alisema akiingia Ikulu, fedha zote atakazozikuta atazileta Misenyi kulipa fidia kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa Kajunguti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwakumbusha wasaidizi wake, wahakikishe katika Mipango ijayo, wahakikishe wanazingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, lakini pia Kajunguti International Airport ni muhimu siyo tu kwa Misenyi, lakini pia kwa Taifa. Tunazungumza kuanzisha masoko ya kimkakati kwa sababu uwanja huo wa Kajunguti, siyo tu tutajenga uwanja wa Kimataifa lakini utaendana na ujenzi wa viwanda, utaendana na kuendeleza maeneo maalum (Special Economic Zones), utaendana na kuweza kuzalisha bidhaa mbalimbali zilizo karibu na Soko la Afrika Mashariki ukizingatia ukweli kwamba tunapakana na Rwanda, Burundi na Uganda, lakini pia tunaweza kuuza maeneo mengine. Kwa hiyo, naomba hilo lizingatiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kuchangia, tunaposema kwamba tunahitaji kuwa na uchumi wa viwanda, hatuwezi kusahau kilimo. Nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri aliyowasilisha leo hii hapa, nimesoma yote, lakini sioni maneno ya kilimo kwanza yakijitokeza, nikafikiri labda tumeanza kusahau sahau kilimo kwanza. Nitoe ushauri, kilimo kwanza ni jambo la muhimu, hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda bila kuwa na kilimo kinachozalisha kwa ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimesoma hotuba hii, mara tatu, mara nne, sikuona maneno Big Results Now yakijitokeza. Nikaanza kufikiri kwamba labda sasa Big Results Now siyo msisitizo tena, lakini nikumbushe kwamba Big Results Now ni muhimu, zile sekta sita ni muhimu, zisipozingatiwa kwenye mipango yetu tutafika sehemu tuisahau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni kwamba unapozungumza kwamba unataka uwe na uchumi wa viwanda lakini unapenda vilevile kuhakikisha una kilimo kinachozalisha kwa ziada, lazima tuhakikishe migogoro ya wafugaji na wakulima inakoma. Jimboni kwangu kuna mgogoro mkubwa wa Kakunyu. Mgogoro huu umechukua zaidi ya miaka 15. Sasa kuwa na mgogoro ambao haumaliziki. Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alishatoa maelekezo mgogoro huu uishe na Mheshimiwa Magufuli ametoa maelekezo mgogoro huu uishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Lukuvi, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi pia washirikiane kuhakikisha wanamaliza mgogoro huu kabla sijaanza kuchukua hatua nyingine ambazo nitaona zinafaa kama mwakilishi wa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda niseme naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hotuba muhimu iliyowasilishwa leo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla kwa kutekeleza kwa ufundi na ustadi mkubwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi, yako mambo mengi ya kuthibitisha hilo, mambo mawili yanathibitisha jinsi Ilani inavyotekelezwa vizuri, Serikali imeweza kuongeza mapato kutoka bilioni 870 Novemba, 2015 hadi trilioni 1.3 kwa mwezi ilipofika Machi, 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali imeweza kuanza kutekeleza mkakati wa elimu bure hata kabla ya bajeti mpya ya 2016/17 haijawekwa, hiyo imewezekana tu kwa kubana matumizi, kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima, yakaelekezwa kwenye utekelezaji wa elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa tunalojifunza baada ya kuanza kutekeleza elimu bure ni kwamba ukiangalia shule ya awali pamoja na darasa la kwanza uandikishaji wa wanafunzi wameongezeka zaidi ya asilimia 100. Kwa maneno mengine, wako Watanzania wengi walioshindwa kuanza shule ya awali, walioshindwa kuanza darasa la kwanza, kwa sababu ya gharama zisizokuwa na tija ambazo wazazi walikuwa wanalazimishwa kwamba lazima zilipwe hivyo kuna watoto walioshindwa kuendelea na shule, sasa baada ya kuanza kutekeleza elimu bure tunaona vijana wakiongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba wako wengi tuliowapoteza. Ni matarajio yangu katika Wizara inayohusika itakuja na mpango wa kuonesha ni jinsi gani wale tuliowapoteza Watanzania wengi tu ni kwa jinsi gani tutaweza kuwapa elimu ya msingi kwa sababu wao tayari wameshaikosa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa ziara aliyoifanya katika Jimbo langu la Nkenge, na pia kuweza kutembelea Wilaya ya Misenyi, kwa kweli niseme amekuwa Waziri Mkuu wa kwanza kutembelea kata ya Kakunyu katika Wilaya ya Misenyi, nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika ziara ile alitoa maelekeza mbalimbali ambayo yatasaidia kumaliza mgogoro kati ya wakulima, wafugaji wazawa, na wawekezaji mbalimbali waliopewa blocks katika Ranchi ya Misenyi. Matarajio yangu ni kwamba maelekezo hayo yataweza kutusaidia kuondoa mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 na ningependa kuchukua nafasi hii kushauri baadhi ya mambo yakizingatiwa yatatusaidia kumaliza mgogoro huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo lazima lizingatiwe ni dhana na maneno ya watu ambao wamekuwa wakisema vijiji vilivyo ndani ya Kata Kakunyu, Kilimilile, Nsunga na Mtukula viliingilia maeneo ya Ranchi za Mabale pamoja na Misenyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivi vilikuwepo kabla ya Ranchi mbili za Mabale na Misenyi hazijaanzishwa. Kwa hiyo, wale wanaosema vijiji viliingilia maeneo ya ranchi kuanzia leo naomba waseme kwamba ni Ranchi za Mabale na Misenyi zilizoingilia maeneo ya vijiji kwa sababu vijiji vilikuwepo na vilishasajiliwa na vinatambulika Kiserikali na vina hati. Kwa kuwa vijiji ndivyo vilitangulia kuwepo kabla ya ranchi ni makosa na dharau kwa wananchi wa Misenyi kusema wameingilia ranchi wakati wao walikuwepo hata kabla ya ranchi haijakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nashauri lizingatiwe Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea kule na kutoa maelekezo, tunatarajia kwamba Mawaziri watayafanyia kazi na bado wanaendelea kuyafanyia kazi. Kabla hawajamaliza kuyafanyia kazi, wananchi wameshaanza kubugudhiwa, tarehe 17 mwezi uliopita na tarehe 18 mwezi huu, baadhi ya wananchi wamenyang’anywa majembe ili wasiendelee na kilimo. Kufanya hivyo ni kuchelewesha kutekeleza sera ya Hapa Kazi tu! pia ni kutoheshimu maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lazima lizingatiwe ili tupate ufumbuzi wa kudumu ni lazima Waziri wa Mifugo ashirikiane na Waziri wa Ardhi, ashirikiane na Waziri wa Ulinzi na Waziri wa TAMISEMI; nina uhakika hawa wote wakishirikiana kwa pamoja na siyo kila mmoja anakwenda kwa wakati wake na kufanya yanayomhusu eneo lake, tutaweza kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme na nisisitize kwamba kuna umuhimu ukiangalia mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano ambao tunalenga kuutekeleza unabainisha kwamba tunahitaji trilioni 107 kuweza kuutekeleza, na kati ya hizo Serikali itatoa trilioni 59 na zilizobaki zitatolewa na private sector, hivyo, ukiangalia Mpango wa Pili tunaopanga kuutekeleza, sehemu kubwa ya fedha zitatokana na private sector. Sasa ili private sector waweze kufanya kazi lazima tuongeze nguvu za kujenga mazingira wezeshi kama ambavyo imebainishwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira wezeshi ni muhimu kwa sababu ndiyo yatawezesha private sector kuweza kuchangia vizuri katika utekelezaji wa Mpango wetu. Nitaeleza mambo matatu muhimu kama mfano wa mambo muhimu ambayo yakifanywa na ambayo hayahitaji fedha za kigeni kuyafanya, lakini ukiyafanya unaweza kusaidia kuharakisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa mfano, hivi sasa hapa Tanzania viwanda vinavyozalisha simenti vikitaka kuuza simenti yake ndani ya Afrika Mashariki vinalazimika kutafuta kibali kutoka kwa Mkemia Mkuu kabla hawajauza, lazima watoe asilimia 2.5 ya thamani ya simenti wanayouza. Ukifanya hivyo unakwamisha viwanda bila sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera wanapotumia sukari na wengine wa Kanda ya Ziwa na Watanzania wengine kila kilo ya sukari inakatwa kodi ya reli. Sasa mtu unajiuliza, kuna uhusiano gani kati ya sukari na kodi ya reli? Utaratibu huu unaongeza gharama ambazo hazina tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunaambiwa waliopo kwenye kilimo cha alizeti kama wataanzishiwa utaratibu wa kupata mbegu mpya wataweza kuongeza ajira kutoka milioni moja ya Watanzania wanaopata ajira hivi sasa hadi Watanzania milioni kumi, lakini ili kupata mbegu mpya waliopo kwenye sekta ya alizeti kwa Tanzania unahitaji miaka saba ili kuweza kupata kibali cha kupata hiyo mbegu mpya, wakati Uganda wanahitaji miezi sita tu ya kuweza kupata hiyo mbegu mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba naunga mkono hoja na naomba nimalizie kwa kusisitiza kwamba ili tuweze kujenga Tanzania yenye viwanda, lazima tuhakikishe tunaunga mkono zoezi la Export Processing Zones na tutafanya hivyo kwa kutenga maeneo na kuhakikisha maeneo ya wawekezaji yanapatikana siyo ya kutafutwa. Vilevile kule Nkenge kuna mpango mkubwa wa kujenga uwanja wa Kimataifa wa Mkajunguti natarajia kwenye bajeti hii zitatengwa fedha za kulipa fidia kama tulivyoahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kupitia Wizara ya Viwanda tunataka kuanzisha Export Processing Zone ya Kimataifa ili uwanja wa kimataifa wa Mkajunguti usiwe uwanja tu usiyokuwa na cha kusafirisha, vilevile tuwe na Export Processing Zone. Tukifanya hayo tunaweza kupiga hatua na kwenda kwa kasi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho tuondoe utitiri wa ukiritimba katika kuratibu masuala mbalimbali. Kwa mfano, mwekezaji yeyote akitaka kuwekeza Tanzania lazima kabla hajaanza kufanya hivyo aende TBS kutafuta kibali, lazima aende TFDA kutafuta kibali cha kitu kile kile, akitoka huko lazima aende kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Sasa ukiangalia yote haya yanaongeza ukiritimba usio kuwa wa lazima na kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyosema Tanzania ni ya 139 sasa ili tuweze kuboresha mazingira ya wawekezaji, lazima hatua za makusudi zichukuliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono haja. Katika ukurasa wa 63 hadi 64 wa hotuba ya Waziri imeandikwa ifuatavyo:-
“Katika mwaka 2015/2016 Wizara imesambaza na kutoa elimu kwa wadau kuhusu Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 na Mkakati wa Taifa wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo wa mwaka 2011. Jumla ya nakala 300 za Sera ya Taifa ya Mifugo na nakala 200 za Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo zimesambazwa”.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakala hizi ni kidogo ukizingatia umuhimu wa sekta ya mifugo. Nashauri nakala nyingi zaidi zichapwe na kusambazwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri Mkuu akifuatana na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi alitembelea Kata ya Kakunyu-Missenyi na kutoa maelekezo ya jinsi ya kumaliza mgogoro wa wafugaji wa Kakunyu na wawekezaji waliopewa blocks za kufuga katika Ranchi ya Missenyi. Nitashukuru Mheshimiwa Waziri akibainisha alivyotekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mgogoro wa Kakunyu umedumu muda mrefu. Wakati umefika tupate ufumbuzi wa kudumu. Katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu itakuwa vyema kuzingatia yafuatayo:-
(i) Vijiji vyote vilivyo ndani Kata ya Kakunyu, Nsunga, Mutukula, Kilimilile na Mabale vilishasajiliwa, vina hati na vinatambulika kisheria;
(ii) Vijiji husika vilikuwepo hata kabla ya Ranchi ya Missenyi na Mabale kuanzishwa;
(iii) Mipaka ya asili kati ya Ranchi ya Missenyi na vijiji inatambulika ni vizuri izingatiwe; na
(iv) Mahitaji ya ardhi ya sasa na vizazi vijavyo lazima yazingatiwe kama alivyoelekeza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri achukue hatua kwa haraka ili tuweze kupata ufumbuzi wa kudumu. Nashauri pia Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ashirikiane kwa karibu na wa TAMISEMI, Ulinzi na Ardhi ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nafasi ya Makamu Mkuu wa Chuo ni muhimu sana katika maendeleo ya Chuo Kikuu chochote. Kwa muda mrefu Chuo Kikuu Mzumbe kinaendeshwa na kusimamiwa na Kaimu Makamu Mkuu (Acting Vice Chancellor), ninaomba Wizara iharakishe na ikamilishe taratibu za kupata Vice Chancellor wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uhaba wa walimu wa awali kwa walimu wa awali ambao wamehitimu katika vyuo mbalimbali na wamekuwa wakijitolea kufundisha kwa muda mrefu ingekuwa vizuri waajiriwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya China ilibainishwa nia yake ya kushirikiana na Serikali yetu kujenga chuo cha Veta Mkoa wa Kagera. Naomba Wizara iongeze msukumo ili chuo cha VETA – Kagera kianze kujengwa. Eneo la kujega chuo hicho lipo na Balozi wa China Tanzania alishatembelea eneo hilo. Ninaomba pia Mheshimiwa Waziri akipata nafasi atembelee eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna walimu wengi ambao wanapandishwa madaraja lakini mishahara yao haibadilishwi, naomba Wizara ijitahidi kuhakikisha walimu wote wanalipwa stahili zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utaratibu wa kufundisha unaitwa Montessori utaratibu huu ni mzuri na una manufaa mengi ukilinganisha na utaratibu wa kawaida tunaotumia. Aidha, hapa Tanzania kuna vyuo vinavyofundisha kwa kutumia mfumo huu. Ninaomba walimu waliofundishwa kutumia mfumo wa Montessori waajiriwe na Seikali. Aidha, kwa kuanzia, madarasa ya awali yanaanza kutumia mfumo wa Montessori kufundisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti nilikuwa nimejipanga kwa ajili ya dakika kumi lakini nitajitahidi nitumie muda mfupi kadri itakavyowezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti tarehe 22 Februari, 2016 wananchi wa maeneo ya Omukajunguti ambao walielekezwa wasiendelee na shughuli za maendeleo katika eneo hilo na tathmini ikafanyika kwa ajili ya kulipwa fidia kwa ajili ya uwanja wa Kimataifa wa Omukajunguti; na tarehe 22 Februari, 2016 wakapokea barua kutoka Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano iliyowekwa sahihi na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Ndugu G. Migire kwamba fedha hizo zitatengwa katika bajeti hii. Sasa wananchi wakaniomba wakisema ukienda huko unga mkono bajeti ya Wizara ili tuweze kupata fedha yetu ya fidia. Lakini nimepitia kitabu hiki na vitabu vingine, sioni fedha hizo za kulipa fidia. Kwa hiyo nachelea kuunga mkono bajeti hewa inapokuja kwenye suala la kulipa fidia watu wa Omukajunguti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo nataomba Mheshimiwa Waziri anisaidie kunipa maelezo nielewe vizuri ili nitakapokuwa naunga mkono bajeti yake nikikutana na mpiga kura wangu akaniuliza niwe na majibu sahihi ya kumueleza kwanini niliunga mkono bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ningependa kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, tunayo ahadi thabiti ya Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye kampeni alituahidi akiingia Ikulu fedha zote atakazozikuta atazichukua azilete Omukajunguti kwa ajili ya kulipa fidia. Mheshimiwa Rais akishazungumza, Mheshimiwa Waziri natarajia asaidie katika kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais. Vigezo vingine vyote vinathibitisha ule uwanja ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wa Kagera, kwa ajili ya Kanda ya Ziwa na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jambo la pili kwa harakaharaka tunayo ahadi ya kilometa tatu za lami kwa ajili ya Mji wa Bunazi, nimeangalia kwenye kitabu hiki sizioni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kilometa 40 za barabara kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia Katoma hadi Kashenye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ukiangalia hesabu kwa haraka haraka, barabara hii imekuwa ikijengwa kwa kiwango cha lami kwa mita 500 kila mwaka. Kwa mwendo huu itachukua miaka 80 ya kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo. Sasa miaka 80 kujenga kilometa 40, huo sio mwendo wa hapa kazi tu, ni mwendo wa konokono ambao nakuomba Mheshimiwa Waziri unisaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa sababu dakika zenyewe ni chache tuna ahadi inayotoka kwa Makamu wa Rais juu ya barabara ya lami kutoka Kaja hadi Mugana, Hospitali Teule ya Wilaya. Naomba Mheshimiwa Waziri akiwa anjibu atusaidie kufafanua hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningependa kulizungumza kwa sababu ya muda, naona figisufigisu katika ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria. Ahadi ilikuwa kujenga meli nne, mbili Ziwa Tanganyika, moja Ziwa Victoria na nyingine kule Ziwa Nyasa. Lakini ukisoma kitabu hiki, ahadi hiyo sasa taratibu inabadilika sasa tunaona fedha zilizotengwa ni shilingi bilioni 20 za kuanza kujenga meli katika Ziwa Victoria, sioni lini tutaanza kujenga kule Ziwa Tanganyika wala Ziwa Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ukisoma kitabu hiki kwa haraka haraka kama una akili ya kufikiria kidogo unapata mashaka, kwa sababu inaonekana zimetengwa shilingi bilioni 20 za kujenga meli mpya katika Ziwa Victoria, lakini hatuelezwi, meli hiyo mpya itagharimu Shilingi ngapi. Lakini katika kitabu hiki hiki tunaambiwa itakarabatiwa MV Victoria kwa shilingi bilioni 20. Sasa kama shilingi bilioni 20 zinatumika tu kukarabati inakuwaje tena unatenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kujenga meli mpya? Mimi nadhani kama ni kweli shilingi bilioni 20 ndizo zinazotakiwa kwa ajili ya ukarabati basi zingetengwa fedha nyingi zaidi kwa ajili ya kujenga meli mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri anafahamu Serikali ilitoa shilingi bilioni 600 kwa ajili ya ukarabati MV Victoria lakini fedha hizo hazikufanya kazi iliyokusudiwa. Namshukuru Mheshimiwa Waziri alichukua hatua. Lakini napenda niseme kama siku chache zilizopita, shilingi bilioni 1.3 zilikuwa zinatosheleza kukarabatia MV Victoria, imekuwaje leo sasa inabadilika si shilingi bilioni 1.3 tena ni shilingi bilioni 20 zinazohitaji kufanya ukarabati. Ndiyo maana nakuwa na wasiwasi, ningependa Mheshimiwa Waziri, anieleze kwamba katika maamuzi haya hakuna figisufigisu bali kweli tunataka kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na kuji-adress kwa yale tunayokusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiit, kwa sababu ya muda naomba niishie hapo. Nachelea kuunga mkono hoja mpaka hapo nitakapokuwa nimepewa maelezo yatakayoniwezesha mimi kurudi kwa wananchi na kuwaeleza kwa nini nimeunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendeleza Sekta ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jumuiya ya Ulaya inatekeleza sera ya malighafi (mkakati wa malighafi) kwa lengo la kukabiliana na upungufu wa madini muhimu kwa maendeleo ya nchi za Ulaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkakati huo wa malighafi wa jumuiya kuna madini zaidi ya 26 ambayo Jumuiya ya Ulaya imeyawekea mkakati wa kuyatafuta na kuyapata kwa gharama yoyote, mahali popote yalipo. Nashauri Wizara itambue uwepo wa mkakati huo na ijipange vizuri kuwezesha Tanzania kunufaika na madini yaliyo katika kundi hilo la madini muhimu kwa kuzingatia mtazamo wa Nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkakati huo wa Jumuiya ya Ulaya wa malighafi raw material strategy. Jumuiya ya Ulaya inaelekeza nia yake kusaidia Mataifa mbalimbali katika jitihada zake za kutafiti upatikanaji na madini mbalimbali na kuweka kumbukumbu za uwepo madini hayo hasa madini muhimu. Nashauri Serikali ijipange vizuri kunufaika na mpango huo wa Jumuiya ya Ulaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tunajipanga kuwa nchi ya viwanda pamoja na jitihada nzuri zinazofanyika kusambaza umeme vijijini kuna changamoto ya umeme unaosambazwa maeneno mbalimbali kuwa wa low voltage. Nashauri jitihada ziongezwe za kuwekeza miundombinu ya kuongeza nguvu za umeme na hivyo kuondokana na tatizo la umeme wa low voltage. Kwa kufanya hivyo, itasaidia sana kupatikana umeme wa uhakika utakaosaidia mapinduzi ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kielelezo namba nne katika ukurasa wa 83, kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa nchini hadi Aprili, 2016 ni asilimia 1.9 iliyoendelezwa. Iinaonekana kama nchi tuna kazi kubwa ya kufanya hasa kuendeleza kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji na kuwahimiza kuendeleza visima vya gesi ambayo imeshagundulika. Kama nchi lazima tujiulize kwa nini inachukua muda mrefu kuendeleza visima vya gesi asilia na tunatakiwa kufanya nini kuendeleza kwa haraka visima vya gesi asilia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwa hoja muhimu iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kwa kazi nzuri wanayoifanya kuisimamia sekta hii muhimu na kwa maana hiyo, sitamung’unya maneno, ninaunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 84 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kuna jedwali linaloonesha marejesho ya asilimia 30 kwa Halmashauri. Nimefuatilia pale nikagundua katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Misenyi hatujarejeshewa fedha. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri na wataalam wake watusaidie kwa sababu tulishawasilisha maombi yetu ya kurejeshewa asilimia 30 kama tunavyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kusema kwamba katika kitabu cha utekelezaji wa miradi ya Wizara ya Ardhi pamoja na Shirika la Nyumba katika ukurasa wa 25 wamebainisha pale kwamba Mutukula Commercial Complex Center ule mradi umeshakamilika kama walivyoonyesha kwenye kitabu, lakini mimi kwa macho yangu hivi karibuni nilitembelea lile jengo, kwa kweli halijakamilka. Niliwauliza wenzangu baada ya kuona hapa leo hii kwamba imekamilika, lakini Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misenyi amenihakikishia akasema bado. Kwa hiyo, nadhani limekamilika tu kwenye vitabu, lakini kwa hali halisi, bado. Nawaomba wahusika walifanyie kazi ili jengo hilo likamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia kupongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kazi nzuri wanayoifanya. Pale Mutukula wamenunua eneo na wamepima viwanja 22. Ni jambo jema kwamba sasa Mutukula itapendeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakaribishe waungane nami na waungane na Wanamisenyi katika jitihada za kujenga mji wa kisasa wa Bunazi unaofanana na miji ya Ulaya. Mji huu tumejipanga kuujenga na niwakaribishe Shirika la Nyumba washirikiane na sisi. Mpango wetu tulionao, tutaanzia Mutukula, tutajenga Bunazi, tutaenda Kyaka na kwa kweli utaratibu tunaotaka kutumia, siyo kutoa ramani za kujenga nyumba tu, tutakupa kiwanja lakini pia tutakupa na ramani ya nyumba ya namna gani uijenge sehemu ipi. Tunataka tujenge mji wa kisasa unaofanana fanana na miji ya Ulaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawakaribisha Shirika la Nyumba waungane nami katika kutekeleza lengo hilo na kwa kweli Mheshimiwa Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini, naomba nimwahidi kwamba ndani ya miaka mitano ijayo Mji wa Bunazi utafunika Mji wa Bukoba, siyo kwa nia mbaya ni kwa sababu ya masuala ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto ya upungufu wa wataalam wa ardhi, namwomba Mheshimiwa Waziri na wataalam wake, watusaidie kutupa wataalam wa ardhi pale Halmashauri ya Misenyi ili tunapopanga mipango yetu, iweze kutekelezwa kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa tisa wa kitabu cha orodha ya migogoro alichotoa Mheshimiwa Waziri, naomba tu niongeze katika vijiji vilivyotajwa mle ni vijiji vya Kakunyu na Bugango pamoja na Byeju, lakini kijiji cha Nkerenge sijakiona pale, naomba kiongezwe. Pia katika Kata ya Mabale, hii ni Kata mpya, kuna mgogoro pia kati ya ranchi ya Mabale na vijiji vya Kenyana na Kibeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jitihada ambazo amezifanya kumaliza mgogoro wa Kakunyu. Namuomba pia Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na yeye afuatilie kwa karibu mgogoro huu umalizike; na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Lukuvi utendaji wako mzuri unaouonyesha umechangiwa na kupata bahati ya kuwa DC wa Bukoba wakati fulani. Sasa Wanamisenyi tunatambua unaifahamu vizuri Misenyi, utusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mgogoro huu uweze kumalizika, jambo muhimu ni kuwa watu wote wanaohusika wafanye kazi kwa uadilifu kwa sababu bila kutanguliza uadilifu mbele, hakuna kitakachopatikana. Ipo migogoro mingine kwa mfano Hifadhi ya Msitu wa Miziro kuna mgogoro kati ya hifadhi na vijiji; vile vile katika Kata ya Buyango, Kijiji cha Kikono kuna mgogoro kati ya kijiji pamoja na Msitu wa Miziro na Kata ya Bugandika kuna mgogoro katika Kitongoji cha Ishozi na hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nianze kwa kukupongeza kwa kazi nzuri unayofanya. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi walivyowasilisha vema bajeti ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu cha Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/2017 ukurasa wa tisa mpaka wa kumi inabainisha kwamba kuna mikoa mitano ambayo inaongoza kwa umaskini. Nimesikia wenzangu walivyosema, sina sababu ya kukataa jinsi hiyo mikoa ilivyobainishwa kwa sababu nitaingia kwenye ubishi wa kiuchumi na wachumi siku zote huwa hawana jibu moja, kwa hiyo kwa sasa hilo naliacha. Nakubaliana na jinsi Mheshimiwa Waziri alivyowasilisha mikoa mitano lakini hoja yangu ni kwamba baada ya kuwa nimeiona hiyo mikoa mitano nikisoma kitabu cha bajeti sioni sasa kwa nini Mheshimiwa Waziri aliwasilisha hiyo mikoa mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifikiri baada ya kuibainisha basi bajeti hii ingekuja na mikakati maalum ya kusaidia hiyo mikoa mitano. Kwa kuwa sijaona, nitajaribu kubainisha baadhi ya maeneo ambayo tukitumia hoja hiyo hiyo kwamba tunayo mikoa mitano maskini sana, mambo yapi tusifanye ili kuendelea kuifanya hiyo mikoa kuwa maskini zaidi. Najua yapo mambo mengine ambayo yanaweza yakafanywa lakini nijikite kwenye bajeti yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, katika ahadi tulizotoa kwa wananchi, maana ukiangalia mikoa hii baadhi yake inalima kahawa na wengine wanalima pamba, lakini kahawa kwa mfano tuna aina ya kodi 26 ambazo tulibainisha kwamba kodi hizi zitapunguzwa au kufutwa kabisa. Bajeti hii mapendekezo pekee ya kodi inayopendekezwa kufutwa ni ada ya kukaanga kahawa kwa ajili ya kuuza soko la nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, ile ada inayofutwa ni moja kati ya 26 zilizopendekezwa kupunguzwa au kufutwa. Kwa hesabu ya haraka haraka maana yake ni kwamba, hapo Mheshimiwa Waziri atakuwa ametekeleza asilimia tatu ya kile tulichoahidi. Kwa hiyo, mapendekezo yangu ni kwamba zile kodi 25 zilizobaki ingekuwa vizuri na zenyewe zikafutwa na zifutwe sasa katika bajeti hii kwa sababu hivyo ndivyo tulivyoahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia haraka haraka, je, wenzetu waliotuzunguka ndani ya Afrika Mashariki wanafanya nini? Uganda wao wana kodi ya asilimia moja tu katika zao la kahawa na ndiyo maana utakuta Watanzania wengi wanapenda kahawa yao wauze kupitia Uganda kwa sababu kule kuna unafuu wa kodi lakini sisi tuna kodi 26. Ukiangalia kwa nini tusifute kodi hizo hupati sababu. Vietnam kwa mfano wao wana asilimia moja tu kwenye zao la kahawa ambayo inakuwa charged kwenye point of exit, Uganda wana asilimia moja, sasa sioni sababu kwa nini na sisi tusifanye hivyo na tufanye hivyo katika bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, wataalam wa uchumi wanatuambia mkulima wa Tanzania hasa wa kahawa yeye anatozwa wastani wa asilimia 70 ya fedha yote inakwenda kwenye kodi, lakini kwa Tanzania corporate tax ni asilimia 30 na akiwa amepata hasara halipi kodi hiyo, lakini kwetu sisi mkulima asilimia 70. Huyu mkulima apate faida, apate hasara, asilimia 70 ipo palepale. Kwa hiyo, nadhani hilo eneo tunaweza kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukiangalia hii ada ya kukaanga kahawa inayopendekezwa kufutwa inamnufaisha nani? Ada hiyo inayanufaisha makampuni makubwa yanayofanya biashara ya kuuza kahawa nje na siyo wakulima wadogo wadogo. Kwa hiyo, nadhani kuna haja ya kulitazama hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tulipopitisha sheria hapa ya kuruhusu haya makampuni makubwa kuingia kwenye ushindani wa kununua kahawa, tulitoa angalizo na sheria iko wazi kwamba hawa tuliowaruhusu kununua kahawa kushindana na Vyama vya Ushirika, wasishindane na Vyama vya Ushirika kwenye grass roots. Tuliwaambia wakitaka kununua kwenye grass root, basi kule Moshi wasiende kushindana, wasifanye mambo mawili. Huwezi ukawa unanunua kwa mkulima, halafu unakwenda Moshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichotokea hadi sasa ninavyozungumza, wanunuaji hawa wakubwa, kina OLAM na wengine wananunua kwenye grass roots, wakienda mnadani wanakwenda kununua kahawa yao tu waliyonunua, kwa hiyo unaua ushindani na inaleta tatizo kubwa kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo napenda kuizungumza haraka haraka, maana tuna mikoa mitano ambayo tunaambiwa ni maskini sana na sina ubishi lakini tufanye nini sasa. Kuna ugonjwa wa mnyauko fizari. Huu ugonjwa wa mnyauko fizari umeleta janga la kitaifa kwa sababu kwa muda mrefu Mikoa ya Kigoma, Kagera na mingineyo tumekuwa tukijitosheleza kwa chakula lakini baada ya huu mnyauko fizari kuanza hatuwezi kujitosheleza kwa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nafikiri kutaja tu mikoa hii inaongoza kwa umaskini haitoshi, ningefurahia kama Mheshimiwa Waziri angetangaza kwamba kuna janga la kitaifa la kupoteza migomba, kwa hiyo tunakuja na mkakati maalum. Tunajua wataalam wetu wa kilimo wamejitahidi kutafuta ufumbuzi, ufumbuzi peke yake waliopata ni kufyeka, kwamba migomba ikipatwa na ugonjwa wa mnyauko fizari dawa ni kufyeka tu, kwa hiyo wanatembea na mapanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani dawa si kufyeka tu, hata kama ni kufyeka Mheshimiwa Waziri anaweza akaja na physical, bajeti inaweza ikasema tutakuja na panga la kufyeka lakini wakati huo huo tuna milioni moja, tunasema tukifyeka hapa kwa sababu umekumbwa na ugonjwa wa mnyauko fizari tunakupa fedha ya kukuwezesha kuishi kwa miezi sita, miezi saba, mwaka mmoja mpaka hapo utakapoanza kuvuna. Watakuita wenyewe wakulima kwamba njoo ufyeke hapa, lakini kama unatembea na panga tu na kama akili yetu inaishia kwenye kutembea na panga tu na kufyeka, basi tujue tutazidi kuongeza umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la msingi kuna Benki ya Maendeleo ya Wakulima. Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo yenyewe inasema kahawa si zao la food security. Napenda nitoe hoja hapa kwamba kahawa ni zao la food security kwa sababu mkulima akiweza kuvuna vizuri atauza atapata chakula. Kwa hiyo, ni uwezo mdogo wa kufikiri kusema kwamba zao la kahawa halihusiani na food security, si kweli. Kwa sababu ukishasema hivyo maana yake Vyama vya Ushirika vinalazimika kuendelea kukopa kutoka CRDB asilimia 18 ili viende kununua kahawa na vinakwenda kushindana na wanunuzi wengine wanaokopa nje kwa asilimia tatu na kuendelea, huwezi kushindana namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa harakaraka naomba nimtahadharishe Mheshimiwa Waziri, anafahamu kwamba alipokutana na wenzake katika Afrika Mashariki wamekubaliana kwa Kenya, vile viwanda vinavyozalisha ngozi na mambo mengine, wanapozalisha wa-offload kwenye soko la Kenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, unapo-offload bila kulipa italeta madhara makubwa kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, natarajia Mheshimiwa Waziri atanipa ufafanuzi akiwa anajibu hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami ningeungana na wenzangu kuzungumza kama walivyozungumza. Hata hivyo, kwa kuwa tetemeko lililoanzia jimboni kwangu bado linatetemesha na bado linamtetemesha na Mbunge mwenyewe kwa hiyo naomba nijikite kwenye tetemeko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu tarehe 10/9/2016 saa tisa na dakika 27 mchana katika eneo lililo kilometa 27 Kaskazini Mashariki mwa Nsunga kulitokea tetemeko kubwa la ardhi. Eneo hilo si pengine bali ni Wilaya ya Misenyi katika Kata ya Minziro, Kitongoji cha Murungu B. Tetemeko hilo lilileta madhara makubwa na madhara hayo yameelezwa na Waheshimiwa mbalimbali waliochangia katika Bunge hili na viongozi mbalimbali walitembelea eneo hilo na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda niseme machache kwamba katika Mpango wa maendeleo tunaoupanga niungane na wale ambao wameshauri ingekuwa vizuri basi katika mpango huo tujipange pia jinsi ya kukabiliana na madhara hayo. Kwa mfano, katika Kitongoji cha Murungu pale tetemeko la ardhi lilipoanzia karibu nyumba zote zilienda chini. Kwa hiyo, matarajio ya wananchi makubwa waliyonayo ni kwamba, Serikali itaweka utaratibu mzuri na kuchukua hatua za kibajeti za kuwawezesha kuweza kujenga nyumba zao upya. Sasa linaweza kufanyika vipi, Waziri wa Fedha anafahamu Serikali inaweza ikatumia mbinu mbalimbali lakini hayo ndiyo matarajio ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya tetemeko la ardhi kutokea lazima tujifunze. Jambo la kwanza ambalo ni muhimu tujifunze, tujipange kwa changamoto kama hizo zitakazotokea baadaye. Kwa sababu kubwa lililojitokeza ni kwamba tulikuwa hatujajipanga vizuri kwa sababu hakuna aliyejua kwamba tunaweza kupata tetemeko la ardhi, sasa limejitokea ni vizuri tujipange kwa siku zijazo likitokea tuwe tumejipanga vizuri. Inapochukua zaidi ya wiki tatu kufanya tathmini ya tetemeko la ardhi inakuwa ni majanga ndani ya majanga. Kwa sababu hata yule ambaye angependa kukusaidia haji kukusaidia kwa sababu wewe mwenyewe hujui tatizo lililokukuta ni lipi na hujui unatakiwa kufanya nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tetemeko la ardhi kutokea ilitolewa taarifa kwamba utaratibu wa kukusanya michango utaratibiwa, ni jambo jema. Pia utaratibu wa kutoa matamko baada ya kutokea tetemeko la ardhi na wenyewe unahitaji kuratibiwa kwa sababu kila mtu anapokuwa anasema analofikiri linaenda kwa wananchi walewale, tunapeleka taarifa za kuchanganya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiongozi mmoja mzito baada ya tetemeko kutokea alisema kwamba wananchi wasiwe na wasiwasi watawezeshwa kupata vifaa kama cement pamoja na mabati ili waweze kujenga, wakafurahia. Baadaye likatoka tamko lingine zito kwamba hakuna atakayetoa
vifaa vya ujenzi bali wenye uwezo waanze kujenga na wananchi wakaanza kutuuliza Mheshimiwa Mbunge mnasema wenye uwezo tuanze na je, wasiokuwa na uwezo mnawafanyaje, sikuwa na majibu kwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini na mtaalam mmoja kiongozi akatoa kauli akasema tetemeko hili ni kubwa, tunafanya uchunguzi wa miamba, kwa hiyo msianze kujenga msubiri mpaka tukishajua miamba imekaaje huko chini ya ardhi. Mpaka leo nazungumza taarifa ya miamba ikoje chini ya ardhi haijatoka. Nayasema mambo haya kwa sababu tusipojipanga vizuri mbele ya safari yatatuletea matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia hata jinsi tulivyokuwa tukijitahidi kusaidia wananchi, nilienda kwa mfano upande wa Minziro kule nikakuta wananchi wengi walikuwa wanasaidiwa na wataalam wetu wa maafa kwa kupewa kitu kinaitwa sheeting. Wanasema nimefika pale nimekuta watu hawana nyumba, wataalam wanaeleza, tumetoa sheeting, sheeting ni turubai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwenye kutembeatembea nikakuta maeneo mengine wana tents zimetengenezwa vizuri, nikawauliza nyie hizi mmetoa wapi? Wakasema jirani zetu hapa ambao ni ndugu zetu wametutolea hapa wanatusaidia kujenga na kila tent linajengwa kwa Sh. 70,000 na linakuwa limejengwa vizuri. Nikagundua kwamba wataalam wa maafa wa Tanzania wao wanachojua inapotokea maafa ni kugawa sheeting tu lakini hawachukui hatua kuangalia kidogo kwa wenzao wanafanya nini inapotokea matatizo kama yale. Si lengo langu kumlaumu mtu yeyote, lakini ni vizuri kujifunza ili siku zijazo tusirudie katika matatizo yale yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia humu kwenye kitabu cha mapendekezo ya Mipango tunafikiri kwamba hali ya hewa itakuwa nzuri Afrika Mashariki lakini ukweli hali ya hewa si nzuri hata huko Kagera kwenyewe ninakozungumzia, kila mahali unapopita agenda kubwa ni ukame, kule Karagwe ni ukame, Misenye ni ukame na kila sehemu ni ukame. Kwa hiyo, matarajio yetu katika Mpango huu basi changamoto hizi za ukame zizingatiwe ili tuone tunaweza kufanya nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango yote mingi tuliyonayo katika kitabu hiki yako mambo mengi, wengi wetu huwa tunazungumzia fedha lakini tunalo tatizo lingine. Miradi mingi haitelezeki si kwa sababu ya fedha kutokuwepo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha alielewe hili, wakati mwingine fedha za kutosha zinakuwepo, lakini uwezo mdogo wa wale wataalam wetu tuliowapa majukumu kushindwa kusimamia hii miradi ni tatizo kubwa kuliko hata tatizo la ukosefu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili nitatumia mifano miwili, kwa mfano tunao mpango wa SEDP unaeleweka Wizara husika ilitoa zaidi ya shilingi milioni 790 za kuweza kujenga nyumba za Walimu katika shule za Sekondari za Kashenye, Bwanja, Nsunga na Kakunyu. Wakandarasi wamefanya kazi yao vizuri, shilingi milioni 709 zilishatolewa, lakini juzijuzi nilikuwa kwenye ziara nimefuatilia kwenye Halmashauri yangu wakandarasi waliojenga nyumba katika sekondari nilizotaja wamelipwa tu shilingi milioni 600 zaidi ya shilingi milioni 200 hazijulikani ziko wapi, viongozi wote hawajui lakini kazi imefanyika, sasa hilo ni tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna tatizo la mradi wa maji katika Wilaya yangu. Kwa mfano, tuna miradi ya maji mikubwa, kule Ruzinga tuna mradi mmoja wa maji wa shilingi milioni 567, Rukurungo, Igurugati shilingi milioni 400, Bugango, Kenyana, Kakunyu ni mabilioni ya fedha lakini miradi yote hii ukiitembelea unachokiona ni mabomba ambayo yanatoa hewa badala ya kutoa maji. Mabilioni ya fedha yametumika lakini hakuna maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkutano mmoja wa hadhara mtaalam mmoja akaniambia Mheshimiwa tumepata maji mpaka mabomba yamepasuka. Nikamwambia hongera nitakuja unioneshe mabomba yalivyopasuka. Nikamuuliza mabomba mliyotumia yakapasuka yako wapi? Akasema Mheshimiwa ni haya hapa. Nikamwambia bomba hili haliwezi kupasuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mkutano tukachimba pale nikakuta bomba lililo ndani ya ardhi siyo kama lile alilonionyesha kwamba walitumia. Nikamwambia mbona bomba ni tofauti, akasema Mheshimiwa unajua sikuelewa swali ulilouliza. Kwa hiyo, umefanyaje? Akasema tumetumia mabomba yaleyale ya zamani yaliyokuwepo. Kwa maneno mengine wale wana Ruzinga hadi leo hawajapata maji na zaidi ya shilingi bilioni 2.7 zimetumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Waziri wa Fedha na kwa Serikali ni kwamba, tatizo siyo fedha tu, tatizo pia ni kuwa na wataalam ambao uwezo wao ni mdogo. Lazima jambo hili tuliangalie, Serikali itupe wataalam wenye uwezo, kama hawajaenda shule sawasawa wapelekwe shuleni, hata kama ni kuazima popote pale tuazime tunachotaka ni utekelezaji wa yale mambo tuliyoahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nilijibiwa hapa kwamba siku za karibuni kule Kajunguti International Airport wananchi wataanza kulipwa fidia na niliambiwa hapa kwamba kabla ya mwezi Oktoba watakuwa wamelipwa. Naomba nieleze masikitiko yangu kwamba hadi leo hii hakuna aliyelipwa hata shilingi moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuzingatia kuwa ninazo dakika tano tu nitaongelea hoja mbili. Naomba nibainishe kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati, sote kwa pamoja tuna nia ya kujenga Tanzania ya viwanda; lakini kwa masikitiko makubwa baadhi ya wawekezaji tunaowakabidhi viwanda hivi ili watusaidie kuviboresha kwa kuleta teknolojia za kisasa, wao badala ya kufikiria kujenga Tanzania ya viwanda wanafikiria kujenga Tanzania ya ma-godown. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni kiwanda chetu cha nguo cha Urafiki. Tulipotemebelea sehemu ile tulishangazwa na tulishtuka kuona Mkurugenzi Mkuu hajui mission kwa nini wapo pale na hajui vision kwa nini wapo pale, jambo hili lilitusikitisha sana. Lakini baadaye tukabaini kwamba wakati fulani zilitolewa fedha kwa ajili ya kununua mitambo, fedha zilitumia lakini hakuna mtambo hata mmoja ulioletwa, kwa hiyo ulinunuliwa mtambo hewa. Wakati Serikali inahangaika na watumishi hewa wakati umefika pia kubaini mitambo hewa inayonunuliwa, badala ya kuendesha kiwanda, inanunuliwa mitambo hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tulibaini kuna mpango wa makusudi wa kuhakikisha spare ambazo zinatakiwa kutumika kwenye kile kiwanda hazinunuliwi na wala haziagizwi, mashine inapoharibika inabidi sasa ing‟olewe kwa sababu hakuna spare, huo ni mkakati wa kubadilisha kile kiwanda kuwa godown. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukabaini kwamba pamoja na kung‟oa ile mitambo pale kuna menejimenti mbili; kuna menejimenti inayoongozwa na wazawa na kuna menejimenti inayoongozwa na wawekezaji. Wawekezaji wanajua ya kwao na wazawa wenzetu wanajua ya kwao. Kwa hiyo, ni menejimenti mbili katika kiwanda kimoja, matokeo yake hakuna kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili ambayo ningependa niimalizie na nyingine niziache, tumeona tatizo la kutotenga fedha za kulipa fidia, kaka yangu Mheshimiwa Mwijage anajitahidi kuhangaika lakini kwa mfano pale Omkajunguti tunataka kuweka Export Processing Zone, zinatakiwa fedha za kulipa fidia, lakini hadi sasa tumeendelea kuzungumza tu hakuna fedha iliyotolewa. Labda tu nimshauri waziri muhusika kwa kuwa alishaniaidi kulipa fidia hizo, alisema ifikapo mwezi wa kumi atakuwa amelipa na sasa hajalipa, ikifika wakati wa bajeti tusigombane, nitafuata taratibu za Kibunge zinazotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia hii fursa ya kuwa mchangiaji katika hoja muhimu iliyo mbele yetu. Naomba niseme awali kabisa kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia ukurasa wa 26 kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu; huduma za kiuchumi; amebainisha kwamba Serikali iko kwenye mchakato wa kuanzisha mfumo unganishi; mfumo wa kuweka kumbukumbu za ardhi, mfumo funganishi wa kuhifadhi
kumbukumbu za ardhi na tayari wameshaanza kujenga.
Mheshimiwa Spika, jambo hili ni zuri na nitaomba liharakishwe na liweze kukamilika kwa wakati kwa sababu litatusaidia sana katika kuondoa migogoro ya mara kwa mara ya ardhi ambayo kwa kiasi kikubwa ukiangalia inachangiwa na kutokuwa na utaratibu mzuri wa kuweka kumbukumbu za ardhi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nyote mnafahamu kuna mgogoro mkubwa kule Misenye uliochukua muda mrefu, lakini ukiuangalia ule mgogoro kwa nini umechukua muda mrefu, sababu kubwa ni kutokuwepo kwa mfumo wa kuweka kumbukumbu za ardhi; na hasa kutokuwa na kumbukumbu
za kielektroniki. Nitaeleza hoja tano kwa nini nasema kutokuwa na mfumo huu kumechangia sana kuleta migogoro ambayo ingeweza kuepukika?
Mheshimiwa Spika, la kwanza, ramani inayotumiwa na NARCO kwa mfano, ramani inayotumiwa na NARCO na iliyotumika katika kugawa blocks kule Misenyi. Ramani hiyo kwanza inatumika kwa siri kubwa, lakini ramani yenyewe ukiwauliza NARCO wenyewe kwamba iko wapi hawawezi kukupa ramani ambayo inatumika; kila mtu anatumia ramani yake kulingana na anavyoona inafaa.
Mheshimiwa Spika, siku moja nilisikitika sana nilipoelezwa na mtaalam mmoja kwamba ramani waliyonayo iliyoanzisha Misenyi Ranch, mpaka ukishavuka Mto Kagera kwenda mpaka Uganda yote ni Misenyi Ranch. Sasa maana yake, mwenye ramani ile na anayetumia ramani
ile anakuwa hatambui na anapuuza ukweli kwamba katika eneo hilo kuna Vijiji, Kata na watu wanaishi. Pia ukiangalia hata blocks zenyewe zilizotengwa katika Misenye Ranch, migogoro iliyopo kati ya blocks na vijiji inasahau ukweli kwamba vijiji vilikuwepo kabla Ranch haijaanzishwa. Kwa hiyo, hii imekuwa ikileta mgogoro.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nasema tukiwa na kumbukumbu za vijiji, maana vijiji vinapimwa, vinakuwa na hati, ziwe kwenye mfumo mmoja ili mtu asitoe hati juu ya hati. Maana kwa kufanya hivyo, matokeo yake inakuwa ni kuleta vurugu.
Mheshimiwa Spika, pia ukiangalia ni kwamba mipaka ya blocks zile zilizotengwa inabadilishwa kila kukicha na tuliowapa hizi blocks wana mamlaka siku hizi wanabadilisha blocks kadiri wanavyoona inafaa. Akiamka asubuhi anaanza kutembea anaweka mipaka na leo kwa mfano nimeletewa taarifa zaidi ya kaya 3,000, sasa ni displaced persons ni watu ambao wapo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
lakini hawana sehemu ya kuishi, wameondolewa katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, sababu nyingine ambayo inatokana na kutokuwepo na mfumo wa kuweka kumbukumbu, sote tunafahamu kwamba vijiji katika Misenye Ranch vilikuwepo kabla ya ranch na mipaka inajulikana kwamba ni Mto Kyaka, Kuru na Kigoroga lakini historia hii imepotoshwa, hakuna anayejua historia hii na kumbukumbu hazipo.
Mheshimiwa Spika, tuna tatizo lingine kubwa ambalo sote tunalijua ni kati ya misitu. Kwa mfano kule Minziro ukiangalia migogoro inayojitokeza kule Kata ya Minziro ni mipaka kati ya Minziro kama Kata na Vijiji vilivyo ndani ya Kata ile na Msitu wa Minziro.
Mheshimiwa Spika, sasa nasema ndiyo maana nimefurahia sana huu utaratibu wa kuanzisha mfumo unganishi wa kuweka kumbukumbu za kieletroniki ukianzishwa na taarifa zinaonesha unaanza itatusaidia sana. Hilo ni jambo la kwanza, ndiyo maana nimesema naunga mkono hoja hii kwa sababu inakuja na utaratibu ambao unaweza kutusaidia.
Mheshimiwa Spika, pia migogoro mingi ya ardhi tuliyonayo; iliundwa tume hapa ya kusaidia kutafuta ufumbuzi hadidu za rejea na akasema jambo moja kubwa kwamba tuwe na subira. Akatuomba viongozi tuwe na subira, tusubiri hiyo tume imalize kazi yake.
Mheshimiwa Spika, matarajio yangu tume hiyo ikimaliza kazi yake Wabunge watapewa fursa ya kupokea ripoti hiyo na kushirikishwa kama tulivyoahidiwa; lakini subira hii naona Mheshimiwa Waziri Mkuu iko kwa wanasiasa tu, lakini kwa viongozi wengine kule Kagera, wao hawana
subira yoyote. Hawasubiri cha tume, wala nini, wanaendelea kila mtu anafanya anavyoona anataka.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa ninapozungumza imetolewa ultimatum ya miezi minne watu wote kuondoka na kwenda kule watakapoona inafaa; jambo ambalo mimi kama mwakilishi wao silikubali, kwa sababu limetolewa kabla hata Tume yenyewe iliyoundwa kufuatilia suala hili
haijatoa taarifa yake.
Mheshimiwa Spika, ni vizuri wakati wanasiasa tunaombwa kuwa na subira, basi hawa Waheshimiwa wengine nao niombe pia na wao wawe na subira. Subira ikiombwa kwa upande mmoja tu, hiyo siyo subira; sote ni viongozi lengo letu ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi waliniomba kule wakasema Mheshimiwa inaonekana sasa ng’ombe wanapendwa kuliko watu, nikawaambia hapana watu kwanza, ng’ombe baadaye. Wakaniomba wakasema Mheshimiwa sasa uturuhusu tushike fimbo tuweze kupambana; nikasema hapana, siwezi kuwaruhusu kwa sasa kwa sababu tuliombwa tuwe na subira. Kama ukifika wakati huo, basi mimi nitakuwa wa kwanza kuongoza mapambano hayo lakini kwa sasa tuwe na subira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwa kazi nzuri sana wanayoifanya ya kuongoza Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunatambua kama alivyoeleza kaka yangu Mheshimiwa Lwakatare, tetemeko lililotukumba Mkoa wa Kagera, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri alipofika pale Jimboni kwangu Misenyi kuna eneo moja linaitwa Kabyaile akakuta zahanati imeenda chini yote kwa sababu ya tetemeko, akanipigia simu akaniuliza Mheshimiwa Kamala hapa zahanati yako imekwenda bado unahitaji zahanati au unahitaji kituo cha afya. Nikamwambia Mheshimiwa mimi ni nani kuombwa na Waziri nipewe kituo cha afya nikaendelea kung’ang’ania jambo dogo! Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu kituo cha afya hicho kimejengwa na kinafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua ziko changamoto zinaendelea, lakini nichukue nafasi hii kumshukuru Waziri wa Nishati na Madini kwa kuhakikisha umeme unafika pale kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais, umeme umefika pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais alituahidi kutupa access road ya lami ya kwenda pale Kabyaire na lami hiyo sasa itajengwa kwenda pale Kabyaire ili wagonjwa waweze kufika pale bila matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa kuwa tunayo na ahadi ya Makamu wa Rais ya kuhakikisha tunapata barabara nzuri ya kwenda Mgana basi tuunganishe hii access road ya Kabyaire na access road ya kwenda Hospitali Teule ya Mgana ili mambo yaweze kwenda vizuri.

Pia nichukue nafasi hii kushukuru kwa kweli kwa mambo yote hayo ambayo yamefanyika ndani ya kipindi kifupi na wenzetu wa Bukoba Vijijini walipoona Kabyaire sasa inapata kituo cha afya na wao wakatuomba wakasema tunaomba nasi tupate huduma kutoka kwenye kituo hicho na hatuna sababu ya kuwabagua wenzetu, niombe basi Serikali ifanye utaratibu iunganishe barabaa ya Kabyaire pamoja na ile inayokwenda Bukoba Vijijini kwa kaka yangu Mheshimiwa Rweikiza ili wananchi wote waweze kupata huduma safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa siyo mkweli kama nitamaliza kuzungumza hapa bila kueleza ukweli kwamba Hospitali Teule ya Mgana (DDH) pamoja na taarifa nzuri zilizopo ya fedha tunazooneshwa kwamba tumepokea kwa ajili ya kutoa huduma, lakini ukweli pale huduma ya mama na mtoto hakuna, hakuna huduma ya bure kama inavyotarajiwa itolewe, hili limekuwa tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Baraza la Madiwani walikuwa na kikao na wakazungumza, Mwenyekiti wa Halmashauri akaniambia wanakaa na mimi nikamwambia nilishamueleza Mwenyekiti wangu wa Halmashauri wakiona jambo lolote wakae na wakiona hawaoni siendi wajue bado naamini wanafanya kazi.

Kwa hiyo, wamekaa na wamezungumza walipomaliza akanipigia akasema Mheshimiwa mambo hayaendi, nikasema sasa kama mambo hayaendi, basi kabla mimi mwenyewe sijaja nitamuomba kwanza Mheshimiwa Waziri wa Afya kwa sababu leo atawasilisha hoja yake basi nitamuomba atusaidie na yeye kuja hapo Mgana aweze kuangalia na kujifunza nini kimetokea, Hospitali ya Mgana ambayo ilikuwa inatoa huduma nzuri kwa watoto sasa haitoi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumuomba Mheshimiwa Waziri aungane nami tuende tutembelee hiyo hospitali ya Mgana tuweze kuondoa hii pandora’s box inayojitokeza ya maajabu ambayo yameanza kujitokeza ya hospitali kushindwa kutoa huduma….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. BALOZI. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja muhimu iliyo mbele yetu. Hoja ya kwanza niliyonayo leo ni kuhusu Wakala wa Huduma za Misitu. Wakala huyu anajitahidi kufanya kazi yake na kwa kweli tatizo kubwa linalojitokeza ni kwamba kwa muda mrefu alikuwa likizo lakini baada ya kuhimizwa na baada ya Wakala huyu kwenye mipango yake kuona kwamba ni muhimu sasa waanze kuweka mipaka ya kuonyesha eneo lao lakini kubwa linalojitokeza hapa ni mabadiliko ya tabianchi, lazima sote tukubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilayani Misenyi kwa muda mrefu sana hali ya hewa ilikuwa nzuri. Hakuna mtu aliyefikiria kuna sababu ya kwenda kulima kwenye maeneo ya matingatinga, hata hawa wenzetu wa huduma za misitu hawakuona umuhimu wa kubainisha mipaka kwa sababu kila mtu alikuwa na eneo la kutosha, kwa hiyo kulikuwa hakuna tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na mahitaji ya maeneo kuongezeka, sasa kila mmoja anajitahidi kuweka mipaka yake. Watu wa hifadhi wanajitahidi kubainisha mipaka ya maeneo yao kuonesha wanaanzia wapi na wanaishia wapi lakini na wananchi pia wangependa wawe na maeneo ya kutosha ya kuchungia mifugo yao. Wananchi wanafuata maelekezo ya viongozi ambapo tumezoea inapokuja wakati wa ukame wanawahimiza waende kulima kwenye maeneo ya matingatinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia pale Wilayani Misenyi, kuna hifadhi inaitwa Lusina; hii inagusa Kata za Bugandika na Bugorora; kuna hifadhi inaitwa Kikuru; hii inagusa Kata za Buyango na Ruzinga, lakini pia kuna hifadhi nyingine kubwa tu inaitwa Minziro. Hifadhi zote hizi zina changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi na changamoto ya hawa wenzetu wa hifadhi kuanza kubainisha maeneo ya hifadhi zao na kwa kufanya hivyo unakuta wananchi wanaona wameingiliwa maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa ya Mheshimiwa Waziri utagundua kuna kipengele kinasema kuna vijiji 228, hii ni kwa nchi nzima na maeneo mengine, vipo ndani ya hifadhi na vijiji 157 vimeshasajiliwa. Sasa kama kwenye kitabu chake cha hotuba Mheshimiwa Waziri anatambua vipo vijiji 228 ndani ya hifadhi katika maeneo mbalimbali Tanzania na anabainisha kwamba vijiji 157 vimeshasajiliwa maana yake alichokuwa anajaribu kutueleza Mheshimiwa Waziri ni kwamba kuna migogoro hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ikishatokea kinachotakiwa ni kuitafutia ufumbuzi. Hatuwezi kuacha migogoro hii ikaendelea kwa sababu ukiacha na wewe unakuwa sehemu ya mgogoro. Kwa hiyo, nimwombe Profesa najua amebobea katika masuala haya, najua ana nia nzuri, najua wataalam wake kupitia hizi hifadhi za misitu wana nia nzuri pia basi tushirikiane kuhakikisha kwamba migogoro hii tunaipatia ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii nishukuru wenzetu wa TANAPA kwa sababu nilipoteuliwa mara ya kwanza kuwa Balozi, maana kazi nyingine hizi hujasomea, nakumbuka baada ya kuteuliwa Mheshimiwa Rais akatuambia Ubalozi husomei nenda tu mtafanya kazi. Nikauliza wenzangu pale tunaanzia wapi? Tutakubaliana kwamba hebu tuwaombe TANAPA ambao wanasimamia hizi hifadhi watupe angalau mafunzo kidogo, tukienda nje huko basi tuweze kuitangaza Tanzania kwa sababu huwezi ukatangaza kitu usichokijua. TANAPA wakatupangia safari nzuri, tukaenda Northern circuit lakini pia wakatupeleka Southern circuit, tukatembelea Ruaha ni nzuri kweli kweli, tukaenda Katavi kule tukajifunza mambo mengi. Nakumbuka tulikuwa na Mabalozi mbalimbali, Mheshimiwa Balozi Batilda, Mheshimiwa Balozi Marmo, Balozi aliyeenda Msumbiji, Misri na Mabalozi wengine, kwa kweli tulijifunza vitu vingi kutokana na ziara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipoenda kwenye vituo vya kazi tukajikuta kumbe kazi yetu kubwa ni kuitangaza Tanzania lakini huwezi kuitangaza Tanzania usiyoijua, ziara ile kwa kweli ilitusaidia sana. Nachukua nafasi hii kuwashukuru TANAPA na kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Kijazi kwa sababu nilikuwa sijapata nafasi ya kurudi katika Bunge hili kushukuru. Kwa hiyo, nilienda, nilifanya kazi, nilijifunza na nimerudi na nawashukuru sana kwa kutupeleka maeneo hayo ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jedwali Na.3 la kitabu cha Mheshimiwa Waziri linaonyesha estimates za maduhuli kwa mwaka 2015/2016 ni shilingi bilioni 25 lakini ukiangalia estimates za mwaka uliofuata ni sifuri. Sasa sijui ni makosa ya uchapaji, huwezi ukawa na makisio sifuri sijui nini kilitokea. Pia ukiangalia hata maduhuli upande wa wanyamapori ni shilingi bilioni 13 kwa 2015/2016, lakini ukiangalia mwaka unaofuata estimate ni sifuri. Nimwombe Mheshimiwa Waziri na watalam wapitie ili waweke rekodi vizuri ili vitabu viweze kueleweka isije ikaonekana kwamba mwaka huu unapata shilingi bilioni 25 mwaka unaofuata unapata sifuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa kazi ambayo wanaifanya najua kutangaza utalii ni kazi ngumu. Niseme jambo moja, nimesikiliza kwa makini hotuba ya wenzetu wa upinzani, hili suala la Loliondo limechukua muda mrefu na naomba niseme tusipoangalia, hatutapata ufumbuzi kwa sababu kuna wadau wengi wanaoshiriki kwenye changamoto ile lakini nzuri na mbaya zaidi kuna na hela nyingi pia. Sehemu yoyote ikishakuwa na hela nyingi zinazunguka, usipokuwa makini huwezi kupata ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia OBC inaongelewa sana lakini nyuma ya OBC kuna wadau wengine pia ambao na wao wanachochea mgogoro huu. Ukitumia nguvu nyingi kuzungumzia OBC ukasahau wengine kama Wamarekani na watu wengine, ndugu zangu ule mgogoro wa Loliondo utaendelea miaka mingi kwa sababu kuna hela zinazunguka na watu hela wanazihitaji na hakuna anayependa kusema kwamba kuna hela. Kwa hiyo, ule mgogoro tusipokuwa makini utaendelea miaka nenda miaka rudi, watakuja Mawaziri hapa, tutawawajibisha, tutasema Waziri hapa umechukua mlungura ondoka, tutafanya kile na kile lakini Loliondo itaendelea kuwa Loliondo miaka nenda, miaka rudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa pale Brussels, ndani ya Bunge la Jumuiya ya Ulaya ilitolewa hoja nzito na Tanzania wakatuazimia pia, hoja ile ilikuwa inahusu land grabbing. Land grabbing ni hoja mpya na ya kisasa ambayo wanasema unamnyang’anya mtu ardhi unaenda kutumia kwa maslahi yako au kwa vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ile ya land grabbing ilipokuja, Bunge la Jumuiya ya Ulaya likaiazimia, likaleta hoja, likasema Mheshimiwa Balozi jibu. Balozi kazi yako ya kwanza lazima utetee nchi yako, kwa hiyo, unapoambiwa jibu, majibu unayotakiwa kutoa ni yale ya kutetea nchi yako siyo jibu lingine. Nilipopitia zile hoja zilizotolewa ambazo ni nyingi sana kuzipitia kwa sababu hapa Tanzania tuna zaidi ya mashirika 70 yote yako Loliondo na kila shirika lina taarifa na kila shirika linaongelea kivyake kuhusu masuala ya land grabbing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiacha tatizo tunaloliona Loliondo ndiyo wanasema kuna Loliondo nyingine kubwa inatengenezwa na Bunge la Ulaya limeshapitisha azimio. Tusipojipanga sasa, siku azimio likirindima ndani ya Bunge hili, ndugu zangu hatutaweza kupata majibu, tutaanza kutafutana mchawi ni nani, ndiyo maana nasema mapema ili tujipange. Yale majibu niliyotoa nikiwa Balozi, ukiwa Balozi unazungumza kama Balozi, nikija humu siwezi kuzungumza kama Balozi, nitazungumza kama Mbunge na hiyo itakuwa lugha tofauti kabisa, ndiyo maana nawaombeni ndugu zangu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. BALOZI. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jambo la kwanza, mpaka wa Tanzania na Uganda uko Mtukula, Minziro, Kakunyu na hauko Bunazi. Kwa hiyo, wale wote wenye mawazo ya kufikiri kwamba ukifika Bunazi umemaliza Tanzania na hivyo wanazuia mchele, mahindi na sukari kufika Mtukula. Naomba kuanzia leo ninapozungumza hapa wakome mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inaeleza na kubainisha kwamba kuna nia ya dhati ya kuanzisha masoko ya mpakani, masoko ya kimkakati. Huwezi ukaanzisha masoko haya na huwezi ukatekeleza mkakati huu kama una watu ambao wanafikiria mpaka wa Tanzania ni Bunazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kuondoa tozo kama tulivyoziondoa ni jambo jema, lakini itakuwa na maana tu kama faida itamfikia mkulima moja kwa moja. Lengo pia liwe kuhakikisha sasa tunaongeza fedha anazozipata mwananchi kutoka asilimia 88 ya sasa walau tupandishe hadi asilimia 90 ya bei ya soko la dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, makato ya 0.75% yaliyopunguzwa mpaka 0.375% ni jambo jema. Hata hivyo, lengo na best practice ni kufuta kabisa mwisho wa siku.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, kinachoitwa mifuko ya mazao ambapo kuna fedha zinakatwa na kupelekwa kusaidia mifuko hiyo ni makosa kwa sababu tulipoamua kuondoa gharama za kuendesha bodi mbalimbali hatukumaanisha kuleta makato mengine tukayaita makato ya mifuko ya mazao. Jambo hilo likome mara moja kwa sababu ni kumbebesha mkulima gharama ambazo tulishaziondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, cess 5% ambayo tunamtoza mkulima wa kahawa kupitia kwenye vyama vya msingi si jambo jema. Nchi zilizoendelea duniani kama vile Vietnam, Mexico na India, hivi sasa hutoza 1% tu kwenye border na si vinginevyo. Huu utaratibu tunaweza kuufuata na ukatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, kumkata mkulima wa kahawa kilo mbili kila gunia kwamba hiyo ndiyo gharama ya gunia si jambo jema na ni wizi wa mchana. Ukienda maeneo mengi vijijini unakuta mizani haikaguliwi na matokeo yake unaweza ukapeleka kilo 50 ukaambiwa hizo ni kilo 45, huo ni wizi wa mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kule Kigarama, kuna mtawala mmoja anaitwa Pastory Kabeba, mtawala huyu amekuwa akisababisha hasara kubwa kwa kupima mwenyewe kwa kufikiria anachoona kinafaa na kumbebesha hasara mkulima. Jambo hilo likome. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nane, soko la kahawa katika Afrika Mashariki tulikuwa tukifikiria sehemu tatu, tunazungumzia Jumuiya ya Ulaya, Sudan na Honduras lakini sasa South Sudan imeshajiunga na Afrika Mashariki. Kwa hiyo, badala ya kuzungumzia soko la Ulaya ambalo kwa maamuzi yetu tumeanza kujiondoa na kwa kuwa hatuwezi kuzungumzia Honduras, basi Mheshimiwa Tizeba peleka tume ya wataalam hapo South Sudan na tujiunge na Sudan tukauze kahawa yetu kwa sababu kuna soko kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Kyakakera Wizara ilitumia shilingi milioni 497 kwa ajili ya maji ya umwagiliaji, maji hayo hata ukitaka kikombe kimoja hauwezi kukipata. Naomba hilo jambo ahangaike nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Sehemu kubwa ya mpaka kati ya Tanzania na Uganda iko Wilaya ya Misenyi – Kagera. Kama unavyofahamu kuna mambo mengi yanayoendelea katika mpaka huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iwe karibu zaidi na ifuatilie kila siku yanayoendelea kwenye mpaka huo kwa nia ya kuimarisha ulinzi, ujirani mwema na kuimarisha utangamano. Aidha, suala la ng’ombe wanaoletwa kutoka nchi jirani (Uganda) na kuja kula majani Tanzania inabidi liangaliwe kwa umakini na lidhibitiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo uwe kwamba ardhi ya Tanzania itumiwe na Watanzania tu na kwamba wanaoleta mifugo kutoka nchi jirani wadhibitiwe na watumie ardhi ya nchi zao. Jambo hili la kudhibiti mifugo kutoka nchi jirani litawezekana tu kama wale tunaowapa majukumu ya kulinda mipaka wakizingatia miongozo wanayopewa na kuzingatia maadili ya Tanzania. Aidha, usalama wa Watanzania wanaoishi maeneo ya mipakani na mali zao upewe kipaumbele pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate orodha ya wawekezaji wenye vitalu vya kufuga ng’ombe katika ranchi ya Misenyi. Nitashukuru sana nikipata orodha yao ikibainisha na uraia wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko taarifa kwamba wafugaji wengi wanaofuga ng’ombe Misenyi ranchi haijulikani wanakouza ng’ombe wao. Je, Serikali inazo taarifa kuhusiana na jambo hili? Kwa mwaka ng’ombe wangapi wanauzwa Misenyi ranchi na nani ni wanunuzi wakuu? Pia je, Serikali inatumia shilingi ngapi kupambana na magonjwa yanayosumbua ng’ombe katika ranchi ya Misenyi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufugaji wa samaki Ziwa Victoria unazinufaisha sana nchi jirani isipokuwa Tanzania. Kwa upande wa Tanzania mfugaji wa samaki akitaka kufuga samaki Ziwa Victoria anatakiwa kufanya nini? Hapa Tanzania kwa hivi sasa tunao wafugaji wangapi wa samaki katika Ziwa Victoria? Je, kuna samaki ambao hivi sasa wamepotea au kutoendelea kupatikana katika Ziwa Victoria? Samaki hao kama wapo ni aina gani? Tanzania tuna mpango gani wa kuhakikisha chakula cha samaki cha viwandani kinapatikana kwa gharama nafuu na je Tanzania tuna viwanda vingapi vinavyozalisha chakula cha samaki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. BALOZI. DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nibainishe kwamba naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Nkenge kuna miradi ya maji ambayo tayari imepokea fedha zote za miradi husika ya maji lakini maji hayajapatikana. Miradi hiyo ni Mradi wa Maji wa Ruzinga, zimetumika zaidi ya shilingi milioni 400 na mradi wa maji wa Igurugati ambao umetumia zaidi ya shilingi milioni 300. Aidha, kuna miradi mingine ambayo nayo haitoi maji kama ilivyotarajiwa. Miradi hiyo ni miradi ya maji Kilimililite, Kakunyu, Kenyana na Kibeho.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ifuatilie kwa karibu miradi tajwa na hasa mradi wa Maji wa Ruzinga na Mradi wa Maji wa Igurugati ulio katika Kata ya Bugandika. Pia mradi wa Maji wa Kakunyu nao umeshindwa kutoa maji. Miradi yote tayari ilipokea fedha ya Benki ya Dunia lakini maji hayajapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitashukuru nikipata maelezo ya kina kuhusiana na miradi niliyobainisha.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Ahsante Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, chimbuko la hoja mbalimbali za kwamba fedha za Serikali zinatumika nyingi pasipokuwa na sababu, mara nyingi tumekuwa tukisikia viongozi mbalimbali wakisema huu ni mfano tu, kwamba pen ingweza kununuliwa shilingi 100 au 200, lakini kwa sababu ya Sheria ya Procurement tunalazimika kununua pen hiyo kwa shilingi 1000, 2000, 3000 au hata 10,000. Sasa chimbuko la tatizo hilo ni kifungu namba 50 na 56 kilichoanzisha Mamlaka ya GPSA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko yote haya tunayoyafanya kwa lengo la kuhakikisha tunaokoa fedha ya Serikali isitumike pasipokuwa ya lazima, bila kufanya marekebisho ya makusudi kuhusu utaratibu unaotumiwa na GPSA tutakuwa hatujafanya lolote.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana wale wachache wanaofanikiwa kuingia kwenye GPSA; Taasisi mbalimbali na hasa kwa hizi items ambazo zinatumika kununua kwa utaratibu wa GPSA ni zile items zinazotumika kila siku, computer, masuala ya pen, uchapishaji na mambo mengine madogo madogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kuwa GPSA inakuwa imeshaweka orodha kwamba hawa ndio wanahusika nchi nzima, na Taasisi kama iko Kagera ikijikuta kwamba kati ya wote waliobanishwa ndani ya orodha ya GPSA hakuna anayetoka eneo hilo, maana lazima watalazimika kufuata ile bei ambayo imewekwa na GPSA. Hili ni tatizo kubwa ambalo kama hatutaligusia katika mabadiliko haya huenda tukaendelea na matatizo kama tuliyokuwa tukiyazungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia katika kifungu cha 4A(1) ambapo inasema; all public procurement and disposal by tender shall be, lakini neno by tender nashauri liondolewe kwa sababu njia ya manunuzi by tender ni njia mojawapo, zipo njia nyingine nyingi tu, ambazo sheria inazitambua. Zipo taratibu kama vile restricted system, shopping, single source, direct contracting, minor value sasa zote hizi zinatambulika. Ukisema by tender maana yake hizi nyingine zote zinazotambuliwa na sheria umeziweka pembeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo ningependa iangaliwe, ukienda katika kifungu cha 6(c) replace monitor and evaluate with advice with on performance, sheria inashauri tuweke maneno advice on performance na tuondoe monitor and evaluate katika kifungu 6(c).
Mheshimiwa Naibu Spika, ambacho ningependa kusema hapa ni kwamba hiki kifungu nashauri chote kifutwe, kwa sababu masuala ya advice and performance tayari sheria inatambua yako kwenye sheria na yanasimamiwa na PPRA. Sasa masuala ya advice and performance tayari tumeshaweka utaratibu mzuri wa kuyashughulikia na sheria inatambua kuwepo kwa PPRA; kwa hiyo tutakuwa tunarejesha kazi ambazo tayari tulishawapa PPRA zinarejeshwa kwenye taasisi zingine jamba ambalo litaleta mgongano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma ukurasa namba 3 wa Mheshimiwa Waziri alipokuwa akiwasilisha hoja ya mapendekezo, nikaangalia wadau wakubwa waliokutana na Wizara nikaona kuna TANESCO, TANROADS na taasisi zingine, lakini kwa masikitiko makubwa sikuona National Board of Materials Management watu ambao ndio muhimu, ndio wataalamu wanaotakiwa kuongoza katika masuala ya procurement. Sasa sijui ni kwa bahati mbaya Mheshimiwa Waziri alisahau au hawakuwa consulted au wao wenyewe walishindwa kutoa ushauri wao. Lakini sababu hiyo iliyosababisha hawa National Board of Materials Management wasio consulted, inapelekea wanaopanza kutaja sifa za Mkurugenzi Mkuu wa PPRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kifungu 23 kinataja sifa za Mkurugenzi Mkuu wa PPRA. Lazima tukubali katika dunia hii, kwa mfano mimi kama mchumi siwezi kuomba hata siku moja kuwa Mkurugenzi Mkuu wa PPRA. Waliosomea mambo hayo watanishangaa na watanidharau.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hiki kifungu kinachopendekezwa kinasema mwanasheria, mchumi, mwanamuziki anaweza kuwa. Sasa hii sikubaliani nayo ushauri wangu ni kwamba lazima tuheshimu profession za wataalam. Tunayo Board ya Materials Managementi na wataalam walio bobea katika masuala ya procurement, basi ni vizuri sifa hizi hata tunapozitaja, tuanze kutaja. Hapa Tanzania tuna bodi nyingi, kwa mfano tuna Professional Board ya Madaktari, huwezi ukakuta kule mwanasheria eti ndio anakuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, ukienda kwa wakandarasi, utakuta kuwa Mwenyekiti wa hiyo Bodi au Mtendaji Mkuu lazima awe mkadarasi aliyesomea, ukienda kwa wahasibu kule, ili uweze ku-add ile professional body lazima uwe mtaalamu wa Uhasibu. Lakini unapokuja kwenye Materials Management inakuwa tofauti; naomba niseme tunalo tatizo katika nchi hii ambapo kila mtu anafikiri anaweza kufanya kazi za procurement hiyo siyo sawa.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia haraka haraka kuna utaratibu wa kuweka lots unapo-advertise tender, kama tender ni bilioni 40, 50 ni vizuri kuweka lots ili upate watu wengi wanaoweza kufanya kazi hiyo na ifanyike kwa haraka. Najua hapa Tanzania kuna taasisi moja ilijaribu kufanya hivyo, tulipongeza kwa hatua hizo lakini tulikuwa tunapongeza hatua ambazo walifanya kwa ubunifu wa watu waliokuwepo wakati huo siyo utaratibu ambao sheria ilikuwa inaruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo ningependa nishauri ukienda kifungu kinachozungumzia suala la kwamba tender board ikutane mara moja kwa quarterly. Lakini Sheria ya Manunuzi ukiiangalia inaitaka Procurement Management Unit (PMU) wakutane kila mwezi na taarifa yao waiande kwaajili ya kuiwasilisha kwenye tender board na PMU lazima wakutane na wanashughuli nyingi za kufanya, lakini wakati huo huo tumeamua sasa kwamba tender board ikutane mara moja kwa miezi minne ili kubana matumizi. Maana yake ni kwamba ule urasimu tunaoukwepa tunarejea kwenye urasimu huo huo kwa sababu PMU itakaa kulingana sheria inavyotaka, lakini haitaweza ku-reporti kwenye tender board mpaka baada ya miezi minne ambapo sasa tender board ndipo inapokaa. Kwa hiyo tunaondoa urasimu mmoja, tunarejesha urasimu wa aina nyingine
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa hili ni la kisheria zaidi, nitaomba Serikali ilitizame tunawataja katika sheria hii kwamba kifungu cha 83, tunapendekeza kufungua kampuni itakayojihusisha na rushwa si chini ya miaka kumi; ukishasema itapewa adhabu si chini ya miaka kumi maana yake itategemea siku hiyo Hakimu ameamkaje, anaweza akatoa hata miaka 50, hata 100. Sasa hilo kwangu ni changamoto. Lakini pia nchi hii, tunazo sheria nyingine zinazoshughulikia masuala ya rushwa, juzi tumepitisha mabadiliko hapa, tumeanzisha na mahakama ya kushughulikia masuala ya uhujumu uchumi. Kama kuna sheria nyingine zinazoshughulika na masuala ya rushwa kwa nini basi tusiache sheria hizo zikafanya kazi kuliko kufanya mabadiliko hapa, ambayo tunampa Hakimu uamuzi ambao ni pendulous box huwezi kujua anachukua hatua zipi? Lakini kwa sisi ambao siyo wanasheria tunajua kwamba pale inapotokea kuna sheria iliyotungwa awali inashughulikia jambo hilo hilo; unapokuwa unatunga sheria mpya lazima uhakikishe sheria hiyo unayotunga isigongane na zile sheria nyingine ambazo tayari zipo. Mimi nadhani wanasheria wanalielewa hili na wataweza kulifanya kazi kwa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, la mwisho kabisa ni dogo tu, ukiangalia corruption mult-practice ni ipi kuna sehemu wametoa definition hawakuweka comma wamesema giving receiving sasa nimejaribu kutafuta kwenye dictionary zote za kiingereza nini maana ya giving receiving nimekuta hana maana, kwa hiyo ninashauri koma iongezwe pale, giving ni jambo moja na receiving ni jambo lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia Muswada huu muhimu ulio mbele yetu. Ni Muswada muhimu kwa sababu bajeti tuliyopitisha na miongozo mingine inayoendana na hiyo bajeti, utekelezaji wake utategemea nguvu za kisheria za sheria ambayo tutaipitisha leo na ambayo naiunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini gazeti la Citizen la leo limeandika habari ambayo sitatumia muda mrefu kuisoma. Kuna wakati nilishazungumza hapa Bungeni kwamba suala la mitumba linapoelekea litatuletea changamoto kubwa. Kwa sababu kuna petition imepitishwa kule Amerika ambayo sasa inalenga kuzuia biashara kati ya nchi za Afrika Mashariki na Amerika na kuondoa kabisa nchi za Rwanda, Tanzania na Uganda na nchi nyinginezo katika list ya AGOA.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni jambo kubwa hilo, kwa sababu tunapojenga Tanzania ya viwanda na yote mengine tuliyopitisha, tunapoondolewa kwenye orodha ya AGOA maana yake sasa kutakuwa na mtikisiko lakini hata bajeti yetu ambayo tulitarajia kuna baadhi ya kodi tutakusanya, hatutazikusanya. Kwa hiyo, ni jambo ambalo nitaomba wahusika walitazame na waone ni hatua zipi zinaweza zikachukuliwa na kama kuna lolote tunaweza tukafanya, basi tulifanye ili kuweka mambo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda nilisema na hili ni la jumla, mwaka 2007 nchi za Afrika Mashariki tulikubaliana kwamba bajeti ya nchi za Afrika Mashariki itasomwa siku moja na wakati wa kuisoma ni uleule. Lengo ni kwamba tulipooanza kutekeleza Customs Union asilimia kubwa ya maamuzi ya kibajeti yanafanyika katika vikao vya Afrika Mashariki. Maana yake ni kwamba muda mwingi tunaoutumia hapa tunazungumza kodi zile tu ambazo tunakuwa hatuamui sisi wenyewe na zilizo nyingi zinaamuliwa katika ngazi ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulikubaliana iwe siku moja, lakini kinachoendelea kutokea hivi sasa ni kwamba baadhi ya nchi zinaamua kusoma bajeti zinavyotaka. Nyote mnafahamu na mnatambua kwamba bajeti ya mwaka huu ni kwamba Rwanda, Uganda na Tanzania ndiyo pekee tulisoma kwa siku moja waliobaki hawakuweza kusoma kwa siku moja kwa sababu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lina implication kwenye masuala ya sera. Jambo hili lina implication kwamba mambo yote unayokuwa unayatoa kisera hapa ya kodi na hatua wengine wenye akili wanakuwa wameshajipanga kwenye magodauni yao ili kufanya mambo ambayo yata- sabotage kile ambacho unajipanga. Kwa hiyo, nimeona niliseme hilo kwa sababu lina implication kubwa kisera na kwenye utekelezaji wa bajeti siyo baadaye tunalaumia tu, haitekelezeki lakini kumbe kuna mambo ambayo tungeweza kuyajua na tukayafanyia kazi yangetusaidia kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho la jumla ni kwamba ukiisoma hii amendment, mimi siyo mwanasheria nitangaze hiyo interest siyo mtaalam wa sheria, nilipoitwa kusoma na nikapewa nafasi kabisa kwa bahati mbaya niliitwa sehemu nyingine na nikapewa offer kubwa zaidi kwa hiyo nikaachana na sheria. Nilipewa offer kubwa zaidi kwamba niende sehemu nisome digrii ya kwanza na nikimaliza pengine nisome ya pili na nisome ya tatu na nipate na ajira. Kwa hiyo, nikaamua kuachana na haya mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ambacho nakisema na naomba wataalam wetu waandishi wa sheria watusaidie, ni la jumla hili tuone kama inawezekana, unaposoma hizi amendments zote kwa mfano amendment of section 63, huu ni mfano tu, inasema:-

“The Principal Act is amended in section 63 by- (a) deleting paraghaph (d)”.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili kwa wanasheria waliobobea ni jambo jema kwao na kwa wale ambao wana ofisi zao Wabunge zenye nyaraka zote, maana ofisi ya Mbunge ni kwamba unakuwa na wasaidizi, unakuwa na nyaraka zote na kila kitu, kwa hiyo ukitaka kitu chochote unapata. Hata hivyo, sisi hapa sote hakuna mwenye ofisi hapa Dodoma na sote hapa hakuna ambaye anaweza akasema anajua hiyo Principal Act inasema nini, inabidi uende library utafute uiangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, najaribu kushauri kwamba kama itawezekana wataalam wetu wa kuandika sheria pale wanapotaja kifungu kinachoondolewa wakitaje chote pale ili ninapopitisha hapa nijue kinachoondoka ni hiki na kinachowekwa ni hiki vinginevyo ni jambo gumu kueleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni mtaalam wa sheria unajua kwamba inakuwa ngumu sana unapokuwa unapitisha amendment lakini unachopitisha hukijui. Ni kama unafanya mchezo tu lakini waliobobea wao wanajua na wenye nyaraka zote na wanaotunza hivi vitu wanakuwanavyo. Mwingine anaweza kusema nyie Wabunge mnakuwa wazembe, lakini hali halisi ndiyo hiyo, hivyo, inabidi tuangalie tuone tunafanyaje kurekebisha hali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kulichangia kwa haraka ni kwamba ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha kuna kitu kinaitwa stay of application. Stay of application unakuta mtu anaomba na tunakubaliana ndani ya Afrika Mashariki kwamba fulani anaruhusiwa asitekeleze jambo fulani, wanakubaliana kwamba fulani ameruhusiwa asitekeleze hili kwa muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kingine wataalam wanaita duty remission wanakwambia hiyo kodi uikusanye au kama huikusanyi itakusanywa baadaye irejeshwe. Hata hivyo, uzoefu umeonesha hata zile kodi zinazosemwa zitakusanywa, Waziri wa Fedha atakuwa anaelewa wala hawazikusanyi tena, ikishatoka imetoka, hazitakusanywa na wala hazitarejeshwa. Mambo haya ukiyatazama maana yake ni kwamba tuna tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunaelewa na Waziri wa Fedha anaelewa kuna kitu kinaitwa Uganda list ambapo Uganda tuliipa msamaha mkubwa sana wa kodi na matokeo yake ni kwamba kuna vitu vingi vinaingia Uganda na vinatakiwa viuzwe Uganda tu lakini vinaishia kuja hata Tanzania. Unapokuwa unafanya hivyo maana yake huku tunapoimba wimbo wa kujenga viwanda tutakuwa hatuwezi kuvijenga kwa sababu mtu atakwambia kuna vitu vya gharama nafuu vinakuja. Kwa hiyo, ni eneo la kuangalia, sijui tutafanyaje lakini ni eneo gumu sana ambalo nimeona niliseme hapa ili tuone tunajipanga namna gani, kwa sababu vinginevyo tutaishia kusema bajeti haitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano mmoja. Tunataka kujenga mtambo mzuri wa liquid gas cylinder, lakini wakati tunakubaliana kufanya hivi na hapa Tanzania kuna watu wameshawekeza wanazalisha hizi cylinder, kuna nchi moja sitaitaja kidiplomasia yenyewe imeamua kufuta asilimia 25 ya kodi imeweka zero. Maana yake yenyewe inataka hizi cylinder zisitoke ndani ya East Africa maana yake zisitoke Tanzania, maana yake initiative zetu za kuwezesha kuwa na viwanda ndani ya Tanzania hazitawezekana, sasa hii inaleta tabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwenye sekta ya chuma. Hapa Tanzania kuna viwanda vingi vimewekeza kwenye chuma lakini wakati tunasema ukitoa chuma kilichokuwa processed kutoka nje basi tulipe asilimia 10 na tumeeleza kwenye sera zetu za kodi lakini wengine wao wanasema ni sifuri. Wanaweka sifuri kwa sababu wana interest ya kuvitoa nje, wakivitoa nje wakaleta kwao maana yake viwanda vya chuma vilivyopo Tanzania havitaendelea, maana yake hata hiyo Mchuchuma tunayozungumza, hata hao wawekezaji hatutawapata. Haya ni mambo ambayo lazima tujiulize mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma yako mambo mengi hayaishii tu kwenye bidhaa za chuma yanaenda kwenye textile, ngozi, garments na vitu vingine vingi. Kwa hiyo, hii ni changamoto kubwa ambapo tusipoitazama, tukachukua juhudi za makusudi, basi hatutaweza kujenga uchumi wetu kama tunavyotarajia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia utalii ni jambo muhimu na tumechukua measures za kusaidia kuboresha utalii lakini nadhani katika bajeti ijayo pia tujipange kuchukua hatua kubwa zaidi. Kwa sababu ukiangalia hapa Tanzania tuna changamoto ya kuwa na taasisi nyingi zinazoshughulikia ku- regulate utalii. Wenzetu Kenya wao wameanza kuwa na taasisi moja tu inayoshughulika utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukiangalia tumetenga shilingi ngapi za kusaidia utalii, sioni ikijitokeza moja kwa moja lakini ukiangalia kwa wenzetu unakuta wao wametenga kwa mfano shilingi bilioni moja kwa ajili ya tourism recovery, wametenga pia shilingi bilioni nyingine moja kwa ajili ya kutunza yale masoko ya zamani yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja nilishangazwa na wataalam wetu wa utalii walikuja na mkakati wao wa kutangaza utalii pale Brussels nikauliza mbona Ubelgiji haimo? Wakasema hii haipo kwa sababu hapa utalii tulishaanza tunaenda sehemu mpya. Nikawaambia usiende tu sehemu mpya ukasahau ya zamani, ya zamani kama unayo mfano Uingereza, Ujerumani lazima uendelee kuwatunza, usiache tu ukakimbilia pengine. Haya nayasema tu kwa sababu pamoja na kwamba bajeti yetu tumeiweka vizuri, lakini najua lazima tujipange kuweka vizuri zaidi katika bajeti ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa muda ulionipa na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2017
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja muhimu iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na naunga mkono mapendekezo ya Serikali ya kufuta RUBADA, kwa sababu kama ilivyoelezwa katika ukurasa wa 13 ni kwamba uendeshaji wa taasisi hiyo na uwepo wa taasisi hiyo unaongeza gharama zisizokuwa za lazima za uendeshaji wa Serikali kama ilivyoelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kama mnavyofahamu tulipopitisha bajeti hapa tulipitisha pamoja na mambo mengine, trilioni 9.2 kwa ajili ya mishahara peke yake. Sasa kama tunatumia trilioni 9.2 kwa ajili ya mishahara peke yake, maana yake sehemu kubwa ya bajeti inaelekezwa huko, maana yake sasa ukubwa wa Serikali umepanuka mno, ndiyo maana jitihada nyingi ambazo zimefanyika za kuondoa wafanyakazi hewa na mambo mengine, lakini bado tu tunajikuta tunahitaji trilioni 7.2 huenda ikaongezeka siku hadi siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo uamuzi huu wa Serikali wa kuondoa RUBADA kwa sababu taasisi nyingine zilizopo za Kiserikali zinaweza kufanya kazi hii iliyokuwa ikifanywa na RUBADA ni vizuri tukamulika na maeneo mengine. Kwa leo sitapenda kuyagusia hayo kwa sababu sote tunayafahamu. Kuna suala la utitiri wa taasisi zinazofanya mambo yanayofanana, kuna changamoto za masuala ya Wakala, yote haya yaangaliwe kwa upana wake ili tuone zile taasisi ambazo zipo lakini hazina tija basi tuziondoe na shughuli hizo ziweze kuendelea kufanywa na Serikali, tupunguze matumizi yasiyokuwa ya lazima. Kwa hiyo, naunga mkono uamuzi wa kuondoa RUBADA sina shaka shughuli hizo zitaweza kufanywa na watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, angalizo tu ni kwamba, tunapoondoa RUBADA zile mali zilizokuwa chini ya RUBADA lazima tuwe makini ili isije ikawa RUBADA imeondoka na mali zikaondoka, kwa sababu kwenye transition ya kipi kilikuwa chini ya RUBADA sasa kitaenda wapi, tusipoangalia basi mambo mengi yanaweza yakaendelea hapo katikati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni kuhusu kumpa uwezo Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuhusu masuala ya kutoa misamaha hasa kwa miradi ambayo tunapata fedha ya wahisani na makubaliano kati ya Serikali yetu na wahisani mbalimbali. Ni jambo muhimu kwa sababu, unaposema mradi fulani ulipe kodi lakini fedha hizo ni za mradi ama tumepata sehemu ya fedha hizo kutoka kwa wahisani maana yake unawatoza walipa kodi wa ile nchi ambayo umepata fedha hizo kwa ajili ya miradi yako ya maendeleo, si jambo jema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo uamuzi wa Serikali wa kuliona hilo ni jambo jema, tumerudi kwenye mstari. Kwa hiyo naunga mkono hoja hiyo kwa sababu itasaidia kuongeza moyo wa wahisani kutusaidia, lakini pia itapunguza gharama za miradi, pia itaharakisha utekelezaji wa miradi yetu ya maendeleo na tutaweza kuelekea kwenye Tanzania ya viwanda kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja kama ilivyowasilishwa.