Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Amb Dr. Diodorus Buberwa Kamala (17 total)

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri.
Kwa kuwa inaonekana hizi shilingi bilioni 2.5 zilizowekwa kwenye bajeti ya 2016/2017 zitalipwa tu pale uthamini utakapokamilika, sasa uthamini huo unatarajiwa kukamilika lini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa katika majibu Mheshimiwa Waziri amebainisha kwamba uwanja mpya utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege za Airbus pamoja na Boeing, na uwanja wa sasa wa Bukoba hauwezi kuhudumia ndege za Airbus na Boeing, si kweli kwamba sasa uwanja huu wa Bukoba umeshafikia ukomo sasa jitihada ziharakishwe ili ndani ya miaka mitano uwanja wa Omukajunguti uwe umejengwa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, tayari mthamini yuko pale kwa ajili ya kufanya uthamini tena na kazi hiyo imekamilika, na kesho anakwenda Dar es Salaam kumpelekea Chief Valuer thamani aliyoiona pale ili kazi ya ulipaji ianze mara moja.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, anauliza je, sasa anaona kwamba huo uwanja wa Bukoba uwezo wake utashindwa baada ya miaka mitatu. Naomba kujibu swali hili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uwanja wa Bukoba ulipojengwa design capacity yake (uwezo wake) ulikuwa ni kuchukua abiria 300,000 kwa mwaka, hivi sasa tunavyozungumza Uwanja wa Bukoba unachukua abiria 25,000 tu kwa mwaka. Kwa vile tunaamini hapo itakapofikia mahitaji ya uwanja huo wa kuchukua abiria wengi tutakwenda kujenga uwanja mpya huo ambao anauulizia Mheshimiwa Mbunge.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu lakini ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kipindi cha mpito kilimalizika mwaka 2010 na kwa kuwa tathmini ya uhakika ilitakiwa ifanyike ili kuweza kujua changamoto zilizotokana na kutekeleza utaratibu wa kodi kupungua taratibu, je, ni lini Tanzania ilifanya tathmini ya uhakika kujua changamoto hizo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Kanda ya Ziwa, Mwanza, Tanga na Arusha kuna viwanda vingi ambavyo vimelazimika kufungwa kwa sababu ya ushindani wa bidhaa kutoka Kenya; viwanda kama vya mafuta ya kula, maziwa, sabuni na vinginevyo, siwezi kutaja vyote. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inasaidia viwanda hivyo kufufuliwa kwa sababu kufa kwake kumetokana na utekelezaji wa sera ambazo hazikufanyiwa tathmini na kuzirekebisha ili viwanda vyetu visiweze kufungwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ambalo anataka kujua kwamba ni lini tathmini hiyo ilifanywa baada ya kipindi kile cha mpito cha kuanzia 2005 mpaka 2009, niseme tu maelezo niliyotoa yanatokana na tathmini ambayo ilitolewa katika tathmini ya mwaka 2015. Ndiyo maana unakuta katika maelezo yangu nimesema mbinu mbalimbali zimefanyika ili kuweza kuboresha viwanda vyetu na kuhamasisha wafanyabiashara wafanye kazi yao vizuri, kwa hiyo tathmini ilifanyika.
Mheshimiwa Spika, vilevile amezungumzia suala la kuhusu viwanda ambavyo baada ya kuruhusu Ushuru wa Forodha kufutwa katika bidhaa hizo zilizokuwa katika kundi „B‟, biashara nyingi au viwanda vingi vya Mikoa kama ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Tanga, Mwanza, Rukwa na hata Arusha viliathirika na najua kabisa na yeye pia anajua kwa sababu katika thesis yake aliyoiandikia Ph.D ilikuwa juu ya hiyo.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba Serikali inaendelea kufanya mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba inaboresha mazingira ya ufanyaji wa kazi katika viwanda na kuwajengea capacity. Kuna mikutano, semina na hata kuangalia vigezo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba viwanda vyetu vinafufuka.
Mheshimiwa Spika, mara zote hapa Waziri wa Viwanda na Biashara amekuwa akitoa mikakati mbalimbali ambayo Wizara yake inafanya ili kuhakikisha wafanyabiashara hao wenye viwanda waweze kufufua viwanda vyao. Moja ya mikakati ni kuweza kutambua viwanda gani ambavyo vimekufa na nani anavyo au kuna viwanda gani ambavyo vimeathirika na tatizo hilo la mambo ya ushuru ili viweze kuwezeshwa na kuanza kufunguliwa upya.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba katika kipindi hicho cha 2009 mpaka 2010, viwanda vinavyozalisha bidhaa kama za saruji vilikuwa vimekufa, lakini kwa sasa hivi tunaona kwamba sehemu kubwa ya viwanda vinavyofanya vizuri ni pamoja viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa za saruji pamoja na mafuta ya kupikia. Ahsante.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: MheshimiwaNaibu Spika, ahsante sana. Ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza, kwa kuwa Jumuiya ya Ulaya katika mpango wake wa miaka mitano au kwa lugha nyepesi Multiannual Financial Framework waliahidi kuisaidia Tanzania Euro milioni 629, kwa kuwa hii inaendana na mpango wa Agenda For Change ina dalili ya kupungua misaada hiyo.
Je, kwa Tanzania misaada hiyo itatoka kama walivyoahidi au inapungua kwa kuzingatia sera yao ya ajenda ya mabadiliko?
Swali la pili, kwa kuwa hivi sasa tunaandaa GSP,
Tanzania tumefanya uamuzi katika Bunge hili kwamba sasa EPA basi ikiwezekana, lakini sasa kwa uamuzi huo maana yake sasa tutafanya biashara ya kupitia GSP au DSP Plus.
Je, kulingana na hii ajenda ya mabadiliko tunajiandaaje sasa kuingia katika mlolongo huu?
NAIBU WAZIRI, MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuthibitisha au kusema kwamba ahadi ambayo ilifanywa na Jumuiya ya Ulaya ya kuahidi kuisaidia Tanzania Euro milioni 628 kwamba itabaki pale pale au itapungua au kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika vigezo ambavyo wao wameviweka kama framework ya kuweza kutoa misaada hiyo ni kuhakikisha kwamba nchi inaweza kuhakikisha inasimamia vizuri suala la la haki za binadamu na utawala bora, usawa wa jinsia, kuhakikisha kwamba vyama vya kiraia vinafanya kazi zake vizuri, kusimamia shughuli zinazofanywa na Serikali za Mitaa, kusimamia vizuri na kuhakikisha kwamba tunapambana na rushwa, kuhakikisha kwamba tunasimamia sera za usimamizi wa kodi na usimamizi wa sekta ya umma. Hivi vyote vinafanyika ndiyo maana unakuta kwamba mpaka sasa hivi hata World Bank wanaendelea kutupa misaada.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotakiwa kufanya
kama Watanzania ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuishi na kusimamia utawala bora na sekta ya umma inasimamiwa vizuri. Hilo ndiyo jibu langu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwamba katika
Bunge hili liliamua kwamba suala la kusaini mkataba wa EPA sasa basi, kwa hiyo, sasa Tanzania inafanyaje. Tanzania imejipanga vizuri kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi kuhakikisha kwamba inahamasisha sekta binafsi ifanye kazi pamoja na Serikali. Vilevile inahamasisha mashirika ya nje na nchi nyingine za nje kuja kuwekeza katika nchi yetu.
Wizara yangu imefanya kazi hiyo vizuri na mifano mmeiona. Vilevile kama nilivyosema kwamba diaspora tunaendelea kuwasimamia na kuwahamasisha katika Balozi zetu, Mabalozi wanafanya mikutano na hawa diaspora ili kuhakikisha kwamba wao pia wanatumia fursa ya kuwekeza katika nchi yetu. Katika mwelekeo huo tutakuwa tunalinda maslahi ya nchi yetu na siyo kuyapoteza.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, huo mpango unaoandaliwa ni jambo jema na kwa kuwa mpango huo utatusaidia vijiji vinavyozunguka maeneo hayo kupata asilimia 26, ni lini maandalizi ya mpango huo yatakamilika? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika kata hiyo ulipo Msitu wa Minziro kuna kitongoji kinaitwa Bulembe na kwa kuwa katika kijiji hicho kuna ngome zilizotumiwa na Wajerumani kupigana Vita ya Pili ya Dunia na kwa kuwa katika eneo hilo huwezi kwenda kwa sababu hakuna barabara isipokuwa uwe jasiri kutumia pikipiki au kutembea kwa miguu zaidi ya saa sita, je, Waziri au Naibu Waziri yuko tayari kuandamana nami kutembea zaidi ya saa sita kwenda kuona vivutio hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umesema kwa ufupi ni kwa ufupi kwa sababu na maswali yenyewe yalikuwa yanaelekeza kupata majibu kwa ufupi. Kuhusu swali lake la kwanza, lini mpango utakamilika, mpango huu utakamilika ndani ya mwaka wa fedha uliokwishaanza.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, je, Waziri au Naibu Waziri yuko tayari kuandamana naye kwenda kuona vivutio alivyovitaja ambavyo viko ndani ya msitu lakini pia ni vivutio vya malikale.
Mheshimiwa Spika, jibu lake ni kwamba mimi au Mheshimiwa Waziri wakati wowote ule tutakapokuwa tumepata fursa na hasa baada ya kikao hiki cha Bunge tutakuwa tayari kwenda kuona na tutaweza kuona namna gani tunaweza tukaondoa changamoto hiyo ya miundombinu ambayo ni mojawapo ya changamoto zinazosumbua kwenye sekta ya utalii.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu lakini ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa Kenya iliruhusiwa kuuza bidhaa zake zinazozalishwa EPZ asilimia 20 bila kodi jambo ambalo alitakiwi, lakini kwa nini wakati huo huo baada ya muda mfupi Kenya hiyo hiyo ikaruhusiwa mitumba inayotaka nje badala ya kutozwa senti 40 kwa kilo watoze senti 20 kwa kilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nchi za Ethiopia, Afrika ya Kusini, India, Morocco na nyinginezo zinatoa mkakati maalum wa kusaidia viwanda vya nguo na ngozi ili watu waweze kuwekeza kwenye sekta hizo kwa kutoa garantees walau ya miezi ya sita na baadaye Serikali inajiondoa na wazalishaji wanaendelea na kwa kufanya hivyo Ethiopia na nchi nyingine zimefanya vizuri Je, Tanzania tuko tayari walau kujifunza kidogo kutoka katika nchi hizo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza suala la nguo pamoja na mitumba ni suala ambalo ni nyeti na suala ambalo linahusu viwanda vyetu vya Afrika Mashariki kwa ujumla. Kimsingi ni kwamba kufuatia maombi hayo kumekuwa na mambo mengine ambayo yameendelea ambayo yameendelea kujadiliwa na nchi. Lakini kubwa zaidi ni kama nilivyosema awali kwamba swala hilo lilikuwa limejadiliwa na Wakuu wetu wananchi.
Kwa hiyo, mabadiliko mengine yoyote yale ni muhimu lazima yarudi tena kwa wakuu wetu wa nchi na misingi hiyo naamini kwamba Serikali kwa kushirikiana na nchi ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa ujumla wake tutapata ufumbuzi wa mambo ambayo yanayoonekana labda pengine yanakuja kuwa ni kikwazo hasa katika kuhakikisha kwamba bidhaa zinazotoka kwenye nchi zetu zinalindwa vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusiana na kujifunza kutoka nchi nyingine za Morocco na kadhalika. Kimsingi wajasiriamali hawa wawekezaji wanapokuja kwenye nchi wanakuja na mitaji lakini wanakutana na sheria mbalimbali ambazo kwa upande mmoja zinakuwa zinasaidia kuwezesha uwekezaji huo, lakini upande mwingine inaweza ikatokea kwamba kuna vikwazo na sisi tumekuwa tukiendelea kujifunza na kuona namna bora zaidi ya kuwasaidia wawekezaji wetu ili waweze kukua na kuendeleza viwanda vinavyowekezwa na ajira kwa ujumla.
Kwa hiyo, ni wazo jema tutaendelea kujifunza na vilevile kuona namna bora kadri inavyoonekana kila siku ya kuweza kuwasaidia wawekezaji wetu.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukiangalia majibu yaliyotolewa ni kwamba upembuzi unaendelea na gharama halisi zitajulikana Septemba.
Sasa hii inanipa wasiwasi kidogo kwa sababu kipindi hicho bajeti itakuwa imepitishwa, sasa wananchi wa Jimbo la Nkenge wawe na uhakika upi kwamba ni kweli mradi huu utaanza kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameeleza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, tufuatane twende katika Wilaya ya Misenyi tuweze kupokea na kuona changamoto mbalimbali tunazokumbananazo katika utekelezaji wa miradi ya maji. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, lakini nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza Balozi kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya katika kuwatetea wananchi wake waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata maji, na sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kwa wananchi wake katika kuhakikisha wanapata maji, siyo maji tu, ni kwa maana ya maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahikishie wananchi wa Mheshimiwa Dkt. Kamala kwamba sisi katika bajeti yetu kwa kuwa tumeshakuwa na upembuzi, inatupa estimation cost ya kuwaweka katika suala zima la bajeti ili mradi huu uweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la kwenda kufanya ziara, nipo tayari kwenda kutembelea, siyo kwenda kuona tu katika hali ya kwenda kutatua matatizo ya maji katika Jimbo lake. Ahsante sana.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki katika kushirikiana katika masuala ya chakula na mifugo, waliipitisha mpango kazi wa usalama wa chakula, je, utekelezaji wa mpango huo umefikia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wakuu wa nchi pia katika kikao chao walitoa mapendekezo ya kuanzisha ufugaji wa kisasa katika nchi za Afrika Mashariki, je, utekelezaji wake umefikia wapi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango kazi wa chakula na utekelezaji wa usalama wa chakula katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ulijadiliwa na wakuu wa nchi, kwa sasa hivi ni kwamba kwa utaratibu wa sheria na kanuni za Jumuiya ya Afrika Mashariki, nchi husika zinachukua uzoefu na makubaliano waliokuwa wamefikia wakuu wa nchi ili kutekeleza lile waliokubaliana nalo. Nafikiri katika suala hili Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo Wizara ya kisekta inaweza kuwa na jibu sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ufugaji wa kisasa zimechukuliwa jitihada za makusudi za kuhamasisha wakulima na wafugaji hasa wa kuku ili kuweza kujifunza kutoka kwenye nchi hizi za Jumuiya kuweza kupata uzoefu wenzao wanafanyaje ili kuweza kuendeleza area hii ya ufugaji wa kisasa. Wafugaji hawa ni wafanyabiashara wanaweza kuwa wakubwa na wadogo na wameweza kuwa wamejifunza katika mikutano ile ya wafanyabiashara ambayo huwa inaitwa katika East African Council katika jumuiya ili kuweza kupeana uzoefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutokana na mikutano hii wanaweza kujadili jinsi wenzao kwenye nchi zinazotoka kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki wanavyofanya basi na wao wanaweza kujifunza. Ninachoweza kusema kwamba Tanzania kama Tanzania wanafanya vizuri katika area hii ya ufugaji wa kisasa na hasa kuku.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na ukweli kwamba wakandarasi 13,000 ni kidogo sana ukilinganisha na idadi ya Watanzania, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kigezo kimoja wapo kinachotumika kutoa kazi wanaangalia uzoefu wa kufanya kazi hiyo hiyo kwa yule anayeomba na kwa kuwa tumekuwa tukisisitiza kutoa ajira kwa vijana wetu, graduates wanapo-graduate tunawaambia waanzishe makampuni.
Swali la kwanza, je, vijana hawa wanapo-graduate kwenye vyuo vikuu wakaanzisha kampuni, wakiomba kazi wataweza kupata kazi kwa utaratibu huu? (Makofi)
Swali la pili, ukiangalia sifa mojawapo inayotumika kazi ni kwamba uwezo wa kifedha wa Mkandarasi lakini uzoefu unaonyesha uwezo wa kifedha wa wakandarasi wetu ni mdogo, wengine wanafutiwa hata kwa kushindwa kulipa ada na wengine wanashindwa hata ku-access mabenki kwa sababu ya utaratibu mbovu wa mabenki tulionao.
Je, Serikali haioni wakati umefika wa kuanzisha Benki ya Wakandarasi na kuboresha taratibu ili kuwezesha Wakandarasi wetu waweze kujikomboa na kupambana na umaskini. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tunawahamasisha graduates wa fani ya uhandisi pamoja na ubunifu wa majenzi waanzishe kampuni na Serikali ina window maalum. Tumeweka window maalum ya kuhakikisha hawa watu tunawapa training, nadhani mfano utagundua pale Daraja la Mbutu tulifanya hivyo, hatukuzingatia uzoefu bali tulifanya pale ya majaribio, vilevile barabara ya kule Bunda kwenda Serengeti nayo vilevile kuna kilometa 50 tuliziweka kwa hawa Mbutu Joint Venture, tunaona kwamba kumbe hilo linawezekana na ndani yao ameshajitokeza mkandarasi mmoja sasa amepata uwezo mkubwa zaidi, Kampuni ya Mayanga ambayo sasa inajenga uwanja wa ndege wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutalifanya hilo na tutaendelea kulifanya lakini lazima tuzingatie sheria kwa sababu tukienda kinyume cha sheria tutakwenda kinyume na kile ambacho tulikubaliana humu Bungeni. Tutatafuta kila aina ya mwanya kujaribu suala hili za uzoefu lisitukwamishe sana kuhamasisha wakandarasi wa kizalendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uwezo wa kifedha ni suala la wakandarasi wenyewe na nadhani Mheshimiwa Balozi Buberwa Kamala unafahamu kwamba wakandarasi wana mpango huo wa kuanzisha benki yao na Serikali tutaendelea kuhamasisha mpango huo ukamilike.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa lengo la kutoa ajira kwa watu wenye ulemavu limekuwa likifuatiliwa na taasisi mbalimbali duniani, na kwa kuwa taasisi nyingi hupewa ulazima wa kutenga idadi ya walemavu watakaoajiriwa na kupewa incentives kwa walemavu wanaoajiriwa.
Je, Serikali yetu iko tayari kujifunza lolote kulingana na utaratibu huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 katika eneo la ajira, Sheria imetoa msisitizo kwamba kila mwajiri nchini ambaye atawaajiri watu kuanzia 20 na kuendelea lazima atenge 3% kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafuatilia kuhakikisha kwamba Sheria hii inatekelezeka.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa mwaka 1975 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kushirikiana na Shirika la SIDA alianzisha vyuo vya FDC kwa nia ya kutoa ujuzi kwa akina mama wajasiriamali na vijana ili waweze kuongezewa ujuzi na hivyo kuweza kujiajiri; na kwa kuwa Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nkenge imeandaa mpango mkubwa wa kutoa ujuzi kwa wajasiriamali akinamama na vijana, je, Wizara iko tayari kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Nkenge katika kutekeleza mpango huo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alitembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Gera na akakuta zaidi ya shilingi milioni 100 zilizotolewa kwa ajili ya kukarabati zilifanya kazi ndivyo sivyo; na kwa kuwa alitoa maelekezo palepale wale waliofanya kazi chini ya viwango warejee tena kwa gharama yao, je, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri yametekelezwa au imebaki kama ilivyokuwa kabla ya kutoa maelekezo yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kama tuko tayari kushirikiana na Ofisi ya Mbunge, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko tayari kushirikiana naye kwa sababu lengo letu ni moja, tunataka vile vyuo viweze kufanya kazi ili tuendelee kupata nguvukazi ya ufundi na stadi mbalimbali katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kuhusu maelekezo yaliyotolewa juu ya ukarabati uliofanyika ambao haujakwenda vizuri. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maelekezo na uamuzi wa Wizara uko palepale, tutaendelea kufuatilia kuhakikisha kwamba maelekezo yale yanatekelezwa.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri ambayo na mimi nakubaliana nayo, lakini mafanikio haya yapo hatarini kupotea kabisa ama wafanyabiashara wasio waaminifu wataendelea kungiza sukari nchini kama wanavyofanya hivi sasa na kufanya repackaging ya sukari hiyo kwenye mifuko wakisingizia kwamba imezalishwa hapa nchini wakati sio. Na hivyo kusababisha viwanda kukosa soko kama ambavyo inatokea kwa Kagera Sugar hivi sasa wamezalisha sukari, imejaa kwenye maghala, hawana sehemu ya kuiuza. Je, Serikali inalitambua hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kama Serikali inalitambua hilo ni hatua zipi inazichukua kuhakikisha usemi wa kwamba Tanzania tunajenga Tanzania ya viwanda, tujenge kweli Tanzania ya viwanda kwa kulinda viwanda vyetu, lakini si kusema tunasema tunajenga ya viwanda huku tukiruhusu wafanyabiashara wasio waaminifu wanaingiza sukari ndani ya nchi, na wanafanya repackaging wanaua viwanda vyetu?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunayo sukari nyingi kwenye viwanda vyetu. Kiwanda cha Kagera Sugar kina sukari na imerundikana nje kama ambavyo mmeona kwenye vyombo vya habari. Hali ni hiyo hiyo Kilombero na TPC. Kwa majibu ya swali la kwanza na la pili Serikali tunatambua na kikosi maalum cha Serikali kinafuatilia na kwa ruhusa yako ningeomba nisiende zaidi kwa sababu katika kinachofanyika kuna jinai ndani yake na vyombo vya dola vinafuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwambia wawekezaji wote wa viwanda vyetu Serikali inawafuatilia na itawalinda na wale wanaochezea viwanda vyetu nataka niwahakikishie uchunguzi ukikamilika tutachukua hatua kali. Fair Competition wako kazini, TFDA wako kazi, TAKUKURU wako kazini na watu wa TRA wako kazini. Ni timu makini na niwaeleze kwa utangulizi hili suala lina jinai na anayehusika atakiona cha moto. (Makofi)
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, haisikiki. Nashukuru sana. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Ukiangalia swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe angependa kujua hasa kwa Kata za Ilela na Ilunde nini kinafanyika? Sasa pamoja na kwamba Katavi imetajwa na mipango ipi, ni nini hasa kinaandaliwa kufanywa katika maeneo hayo na ni shilingi ngapi zimetengwa?
Swali la pili; kwa kuwa katika Wilaya ya Karagwe, Biharamulo, Ngara pamoja na Misenyi, TBC haisikiki na wananchi wangependa kuisikia, ni nini kinafanyika kuwezesha TBC kusikika katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO): Mheshimiwa Spika, nikianza na swali la kwanza; katika majibu yangu ya msingi, nimeuzungumzia Mkoa wa Katavi kwa ujumla ambao tafsiri yake ni kwamba itajumuisha pia Kata za Ilunde na Ilele ambazo ziko ndani ya Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha bajeti ya mwaka 2017/2018 Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo tumetengewa kiasi cha shilingi bilioni 33.2 ambapo mpango mkakati tulionao hivi sasa ni kuhakikisha kwamba tunaongeza zaidi usikivu kwa sababu ukiangalia katika mwaka 2016 TBC ilikuwa ina usikivu wa asilimia 54 tu nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, ndani ya miaka miwili baada ya bajeti hii kuongezeka, tumefikia usikivu wa asilimia 64. Mkakati uliopo ni kuyafikia maeneo mengi zaidi ili wananchi wapate fursa ya kupata habari kupitia TBC.
Mheshimiwa Spika, nikienda katika swali la pili la katika maeneo ya Misenyi, jibu langu ni hili hili la kwamba kwa mwaka huu wa fedha ambapo tuna kiasi cha fedha nilichokisema hapo tulichotengewa, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kufunga mitambo mingi zaidi ili wananchi wapate fursa ya kuweza kusikia TBC.
Mheshimiwa Spika, katika maeneo yale ya pembezoni tumeongeza usikivu kutoka kilowati 200 mpaka kilowati 1000 na ninaamini kabisa kwamba kwa mwaka huu wa fedha tutajipanga vizuri zaidi kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanaisikia TBC.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Ranchi ya Missenyi ni miongoni mwa ranchi za mifano na ina hekta 23,000 na ng’ombe 1,670. Je, Mheshimiwa Waziri anayo mambo mengine anayoweza kunieleza ili na mimi nianze kufikiria kama yeye kuiita Ranchi ya Missenyi ranchi ya mfano huku ikiwa na hekta 23,000 na ng’ombe 1,600? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa swali langu nimeuliza wananchi wanaozunguka Ranchi ya Missenyi wamepata faida zipi, sasa hii kusema mitamba 12 na mbuzi sita inanipa mashaka. Nimsaidie Mheshimiwa Waziri kwamba Kata ya Mabale ipo mbali, eneo tofauti kabisa na Ranchi ya Missenyi, Kata ya Mabale imezunguka Ranchi ya Mabale. Sasa yupo tayari kukubaliana na mimi kwamba waliomasidia kumtafutia majibu wamemdanganya na awawajibishe ili wasimdanganye tena? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimthibitishie kwamba ni kwa nini nimesema Ranchi ya Missenyi ni miongoni mwa ranchi za mfano katika nchi yetu. Nadhani yeye amechukulia kigezo cha idadi ya mifugo na ukubwa wa eneo pekee; lakini nataka nimwambie kwamba tuna sababu nyingine kadha wa kadha za kuifanya Ranchi ya Missenyi kuwa ni ranchi ya mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sababu hizo ni eneo la kijiografia (geographical location) yake Ranchi ya Missenyi yenyewe. Sisi sote tunafahamu kwamba ranchi hii ipo katika mpaka wetu na nchi kadhaa zinazozunguka nchi yetu. Kwa hiyo, sisi kama Taifa na hata ambao waliasisi ranchi hii walikuwa wanajua kwa sababu gani ambapo tumeenda kuiweka ranchi hii. Hii ndiyo maana kutokana na sifa zake kadha wa kadha ambazo ni pamoja na hii ya idadi ya mifugo na geographical location tunasema kwamba Ranchi ya Missenyi ni ranchi ya mfano na tutaendelea kuiboresha ili kuhakikisha kwamba tasnia ya mifugo katika nchi yetu inaendelea kuwa na kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amelieleza kuhusiana na Mabale kwamba haipo katika Ranchi ya Missenyi ama ipo mbali na Ranchi ya Missenyi na kwamba labda nimedanganywa na waandishi wangu wa majibu. Naomba nichukue maelezo haya ya Mheshimiwa Mbunge, na kama upo uboreshaji sisi tupo tayari kukosolewa maana kukosolewa ndiyo kuimarika pia, ahsante. (Makofi)
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na ninashukuru pia kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Waziri wake na Katibu Mkuu wake. Ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba alituma wataalam kule Kata ya Kanigo, Kata ya Kashenye, Kata ya Ishozi na Kata ya Ishunju kwa ajili ya maandalizi ya awali ya kutumia maji ya Ziwa Victoria. Je, yuko tayari kuharakisha jitihada hizo ili maji hayo yaanze kutumika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo la pili. Kwa kuwa Wilaya ya Misenyi tumebarikiwa kuwa na mito mingi; tunao Mto Kagera pamoja na Mto Nkenge na mingine: Je, mradi kama huu ambao uko mbioni kuanza kama Mheshimiwa alivyojibu katika maeneo ya Kyaka na Bunazi, atakuwa tayari kubuni mradi kama huo katika maeneo yaliyo karibu na Mto Nkenge?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya. Nilifika katika Jimbo lake, nimeona kazi kubwa zinazofanyika katika eneo lile. Kubwa ambalo ninalotaka nimhakikishie, sisi kama Wizara ya Maji ambayo siyo Wizara ya ukame, tumeona haja kwamba haina budi na kwamba haiwezekani tuone kabisa vijiji ama Miji ambayo iko karibu na mito mikubwa ama maziwa wakose maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tuna vyanzo vya uhakika, ndiyo maana tumewatuma wataalam wetu waweze kwenda katika eneo lile ili tuweze kubuni mradi na wananchi wake waweze kupata majisafi na salama na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la ku- design katika Mto Nkenge; uwepo wa chanzo unatupa nafasi kama Wizara ya Maji katika kuhakikisha tunabuni miradi mikubwa ili tuweze kuwapatia wananchi wake maji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kuanzisha mradi katika Mto Nkenge ili wananchi wake waweze kupata majisafi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na shukurani za dhati kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Misenyi na Jimbo la Nkenge kwa mradi mkubwa wa maji ambao kwa mara ya kwanza sasa unaanza kutekelezwa, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; pamoja na ukweli kwamba mradi huu ni mkubwa lakini majibu yanaonyesha utatekelezwa katika bajeti ya Mwaka 2019/2020. Sasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wanasubiri mradi huo mkubwa nini Serikali inafanya kuhakikisha maji yanaendelea kupatikana kwa uhakika ili wasipate tabu wakati wakisubiri mradi mkubwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili dogo; katika kikao changu cha wadau, wataalam waliniandalia taarifa nzuri na nikawaeleza wadau kuhusu Mradi wa aji ya Ruzinga lakini wadau wengi wakasema hapana Mheshimiwa unadanganywa, maji Ruzinga hayatoi.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kufuatana na mimi ili twende kati ya Ruzinga ili tuone hizi fedha nyingi tunazopeleka tunafikiri maji yanatoka na hayatoki ili isije ikafika wakati mwingine ambao siyo muafaka wa kuuliza maswali kama haya twende pamoja anisaidie kutoa maelekezo ya Muarobaini wa matatizo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kiukweli amekuwa akifanya kazi kubwa sana katika Jimbo lake. Kitu ambacho nimhakikishie; mimi ni Naibu Waziri wa Maji, faraja yangu ni kuona Wanankenge wanapata maji safi na salama. Sasa nataka nimhakikishie baada ya Bunge tutafika na tukiona mradi ule ambao tumetoa fedha maji hayatoki tutamchukulia hatua Mhandisi wa maji pamoja na Mkandarasi ambae amepewa sehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ambacho nataka kumweleza Mheshimiwa Mbunge ahadi ya utekelezaji wa mradi mkubwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na watalaam wetu wameshafanya usanifu ninachotaka kumhakikishia, katika kipindi hiki ili wananchi waweze kupata huduma ya maji timu yetu imegundua kisima kikubwa sana katika Kijiji cha Igayaza, tutatekeleza mradi wa haraka ili wananchi wake waweze kupata huduma hii muhimu sana ya maji. Maji ni uhai na sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji hatupo tayari kupoteza uhai wa Wanakyaka. Ahsante sana.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri na nichukue nafasi hii kumpongeza pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa uteuzi alioupata na kwa kazi nzuri ambayo anaifanya toka ameteuliwa. Pamoja na hayo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ukiangalia majibu yanayoonyesha kwamba NARCO walipewa ramani tarehe 20 Oktoba, 1969, yanathibitisha ukweli kwamba vijiji vya maeneo hayo vilikuwepo kabla ya ranchi. Kwa kuwa tulipokuwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa wa Kagera wa wakati huo na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, alioneshwa ramani ya NARCO ambayo ilionesha unapovuka Mto Kagera ukaenda mpaka wa Uganda hakuna kijiji, eneo lote ni la NARCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alishtuka na akaelekeza ramani hiyo siyo sahihi na akasema yeye alipokuwa askari alipigana vita na vijiji vilikuwepo na akaelekeza ramani hiyo irejeshwe kwake ili aweze kuipitia na ifutwe kwa sababu haitambui uwepo wa vijiji na toka wakati huo ramani hiyo imekuwa siri kubwa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kunionesha nakala ya NARCO wanayoitumia kugawa maeneo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo la pili, pamoja na majibu mazuri kwamba hekta 21,571 zimetolewa lakini nakuwa na wasiwasi kwa sababu katika eneo hilo inaonekana kuna viongozi wanaolipwa ili wasione na kwa kuwa bado wapo maamuzi haya mazuri huenda yasilete tija. Je, yuko tayari kuniambia haya maeneo yaliyoongezwa ni yaleyale yaliyokuwa ya vijiji au ni maeneo yaliyokuwa ya NARCO sasa vijiji vimeongezewa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Kamala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaozunguka mashamba ya NARCO katika Wilaya ya Misenyi wamekuwa na mgogoro na Serikali na NARCO kwa muda mrefu. Hatua zilizochukuliwa sasa ni kwamba mchakato wa kupitia upya mgongano wa ramani hizi umeshaanza katika ngazi ya wilaya na unaendelea katika ngazi ya mkoa. Wataalam kutoka TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi sasa hivi wameanza kupitia mipaka ili kuondoa tatizo hili la muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Balozi Dkt. Kamala achukue hatua tu kuwasilisha haya mawazo yake aliyoyasema na namna gani tunaweza kumaliza jambo hili kimaandishi Serikalini ili na yeye awe part ya mchakato huu wa kumaliza mgogoro wa mipaka katika vijiji hivi.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza. Utafiti uliofanywa na watafiti katika vyuo vikuu vya Tanzania umebainisha kwamba upungufu wa wahadhili katika vyuo vikuu kwa Tanzania ni asilimia 44, na umebainisha pia kwamba, chuo kama Muhimbili, kuna upungufu wa wahadhili asilimia 65, chuo kama cha Mbeya, kina upungufu wa wahadhili asilimia 54 na utafiti huo umebainisha pia, kati ya hao waliopo pamoja na upungufu huo, asilimia 53 tayari wameshastafu kwa sheria za sasa.

Je, Wizara iko tayari kutafakari upya uamuzi wa kwamba, wahadhili wakifikisha miaka 65 wastaafu na wasiongezewe mkataba?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa taasisi nyingi duniani zilishapandisha umri wa kustaafu, kwa mfano, Nairobi University umri wa kustaafu kwa maprofesa ni miaka 70 na baada ya hapo anaweza akaendelea kwa mkataba. Ujerumani hakuna neno kustaafu kwa maprofesa, ukistaafu unapewa cheo cha Emeritus Professor, unaendelea kufundisha na kutafiti mpaka pale utakaposema sasa umechoka, na Uingereza wamebadilisha sheria kabisa sheria ya Bunge, neno kusitaafu katika kufundisha vyuo vikuu limefutwa kabisa, kwa sababu wamegundua akistaafu mmoja leo, inawachukua miaka 40 kuweza kutengeneza mtu kama huyo.

Je, Wizara iko tayari kufikiria na kujifunza kutoka kwa wenzetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, Mheshimiwa Mbunge ametoa utafiti alioufanya na ninaomba niamini kwamba huyu ni Dokta na ni Balozi atakuwa amefanya utafiti wa kutosha, lakini tutaongezea kufanya ili kupata taarifa sahihi sana juu ya jambo hili. Lakini ni kweli kwamba wako wahadhili wengine wengi ambao wanastaafu wakiwa na umri wa kuweza kufanya kazi, hilo jambo ni ko wazi, hili jambo ni ushauri mzuri naomba tuupokee, tufanyie kazi tuone uwezo utakavyoruhusu, tutashauriana na tutaomba Mheshimiwa Mbunge kukutane zaidi katika jambo hili ili liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile, pamoja na kwamba tunataka maprofesa hawa na wataalamu wengine waongezewe muda wa kufanya kazi, lakini tunao mpango pia wa Serikali wa kuendelea kusomesha wataalamu wetu ndani na nje ya nchi. Kwa mfano sasa hivi tunavyozungumza tuna wataamu 65 kati yao ni wadhamivu wanasoma nje ya nchi na watatu wanasoma katika udhamili. Kwa hiyo, tutataangalia namna ya kuweza kuongezea muda wa kufundisha wale hasa wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo, na kwenye fani mahususi na jambo hili Serikali itakwenda kulifanyia kazi, ahsante sana.