Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye (19 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kwa jina naitwa Engineer Nditiye, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua nafasi hii kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniteua kugombea nafasi hii. Vilevile nawashukuru wananchi wa Jimbo la Muhambwe kwa kuniamini na kuona sasa maneno maneno Bungeni hayatakiwi, inatakiwa Kazi tu! Nawaahidi kwa moyo wa dhati kabisa kwamba Engineer Nditiye, nimekuja kufanya kazi wala siwezi kuwa na maneno maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ndugu yangu Mheshimiwa Mpango. Kwanza namsifu sana kwa hotuba yake nzuri sana na mipango yake mizuri sana. Vile vile nashukuru hotuba ya Mheshimiwa Rais, ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango mipango yake mingi ime-base kwenye hotuba ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na suala la elimu; ili tuingize nchi yetu katika uchumi wa viwanda, tunahitaji tuboreshe sana suala letu la elimu. Ni lazima tujikite sana katika kuhakikisha kuanzia shule za msingi, wanafunzi wanapenda masomo kama hesabu na sayansi ili hata hivyo viwanda vitakapoanzishwa tuweze kupata watu sahihi, kwa ajili ya kuviongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimkubushe Waziri wangu wa Nishati, Profesa Muhongo kwamba ili ku-achieve mipango yetu, tunahitaji tupate umeme kwa sababu, Serikali yetu ilitushauri kwamba kila Kata iwe na sekondari, na wananchi waliitikia huo mwito, kila Kata ina sekondari.
Vilevile Serikali yetu ilituambia kwamba kila sekondari ya Kata sasa iwe na maabara. Nikuhakikishie kwamba katika Jimbo langu la Muhambwe, karibu sekondari zote za Kata zimekwisha jenga maabara na tumekwishafikia asilimia 80, tunasubiri tu hatua ndogo ndogo ili maabara zianze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyoko ni kwamba, katika Jimbo langu lenye Kata 19, ni Kata tatu tu ambazo zina umeme; na maabara yoyote ile sidhani kama inaweza kuendeshwa kama hakuna umeme. Kwa hiyo, ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Muhongo pamoja na kazi nzuri unayoifanya, nakuomba sana ufikirie hilo Jimbo la Muhambwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la reli. Sidhani kama kuna Mbunge yeyote ambaye atasimama hapa aache kuizungumzia reli ya kati, kwa sababu inahudumia mikoa zaidi ya 13.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile reli ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Hilo liko wazi, tunaomba sana, kwenye mipango yako utueleze in detail. Siyo kueleza juu juu tu kwamba kilometa ngapi zitakarabatiwa; tunataka utueleze za wapi na wapi na kivipi? Tunataka reli yote ikarabatiwe kwa sababu umuhimu wa reli hiyo hauna maswali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa ni Mbunge wa kutoka Mkoa wa Kigoma siwezi kumaliza bila kuzungumzia barabara ya kutoka Nyakanazi mpaka Kigoma, nimeiona hapa kwenye ukurasa wa 11 imewekwa, naomba sana na tutakuwa makini kweli kuhakikisha hiyo barabara ambayo kwetu sisi ni ya muhimu kutuunganisha na Mikoa mingine inapewa kipaumbele na ijengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la miundombinu ya maji. Kama nilivyozungumza hapo awali, Wilaya yangu ya Kibondo ina Kata 19, lakini Kibondo Mjini kwenyewe hatuna maji ya uhakika wala hayako salama haya yanayotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba Wizara ya Maji ihakikishe inatafuta chanzo kingine, kwa sababu chanzo kilichokuwepo kimeshavamiwa na shughuli za kibinadamu na hakifai tena; hakitoa maji; na kama Wilaya unaweza ukakaa hata siku nne bila kuwa na maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Waziri wa Maji katika mipango yetu hii ahakikishe kwamba wananchi wanapata maji safi na salama ili waweze kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la maliasili. Katika Jimbo langu nina Kata zaidi ya sita ambazo zinapakana na Hifadhi ya Moyowose, Kata za Busunzu, Busagara, Lusohoko, Kitahana, Kata ya Mulungu na vijiji vyake. Kwa muda mrefu sana tumekuwa tukiomba Serikali irekebishe mpaka ili wananchi wapate sehemu ya Kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba Vijiji hivi ni vya muda mrefu na wakati huo wananchi hawakuwa wengi, sasa wameshaongezeka na wanahitaji sehemu zaidi ya kulima.
Kwa hiyo, nashukuru sana kwa waraka uliopitishwa na Mheshimiwa Waziri wa Ardhi kuorodhesha vijiji vyote ambavyo vinapakana na mpaka ili waweze kuongezewa sehemu ya kulima. Nashukuru sana, nami nitashirikiana na wewe kwa karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa haraka haraka. Kwenye kampeni za Mheshimiwa Rais, alipopita Jimboni kwangu pale, aliahidi kuhusu suala la pensheni kwa wazee wote, awe mtumishi, mkulima au mfugaji na wavuvi aliahidi pensheni kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hilo suala litekelezwe na liwekwe kwenye mpango imara ambao utatekelezeka ikiwezekana kuanzia mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, michezo. Nimefurahi sana kwamba hivi karibuni tumetoa product moja Tanzania ambayo imesikika moja kwa moja. Huyu anaitwa Mbwana Samatta. Tukumbuke kwamba michezo ni chanzo kizuri sana cha mapato kwa nchi. Angalia nchi kama Brazil, asilimia kadhaa ya uchumi wake wanategemea sana wanamichezo ambao wanaenda kucheza nchi za nje, wanaleta uchumi nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhakikishe sasa tunaanza kuwekeza hasa kwenye Mikoa ile ambayo ni vyanzo vya sanaa na michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia Mkoa wa Kigoma, Tanga kidogo na Morogoro kwenye football huwezi ku-doubt. Vilevile kwenye sanaa ya muziki, hata maigizo; Mkoa wa Kigoma una mchango mkubwa sana.
Naomba sana Serikali ijikite sana katika kuwekeza katika Mkoa wetu kuhusu suala la michezo na sanaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami vilevile nianze kwanza kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mbalimbali kwenye taarifa yetu.
Nitoe shukrani vilevile kwa Wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambao tulifaya kazi bega kwa bega bila kuchoka. Vilevile nitoe shukrani kwa michango iliyotoka kwa Mawaziri kuhusu kuboresha taarifa yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ilishindwa kutekeleza baadhi ya majukumu kama ulivyosikia michango mbalimbali ya Wajumbe kutokana na ufinyu wa bajeti uliokuwepo. Kuna baadhi ya michango ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wameitoa lakini haimo ndani ya taarifa yetu mfano mdogo ni suala la RUBADA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la RUBADA kwenye mipango ya Kamati yetu ya Utekelezaji ya mwaka 2016 tulitakiwa twende RUBADA kuangalia na kufanya kazi lakini pesa haikuwepo kwa hiyo tulishindwa kwenda kule na ndiyo maana hata kwenye taarifa yetu suala la RUBADA halikuwepo. Nipende tu kulitaarifu Bunge lako kwamba siku pesa itakapopatikana tutakwenda na tutakuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kuweza kuishauri Serikali yetu nini cha kufanya kuhusu RUBADA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea michango kwa maneno ya Waheshimiwa Wabunge 22 lakini nimepokea ya maandishi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge 16. Nashukuru sana kwa michango yao yote, michango ambayo ilijaa uzalendo wa hali ya juu na uchungu wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upimaji na urasimishaji wa ardhi lilizungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi sana, ni kweli kwamba sehemu nyingi sana za miji yetu haijapimwa na hiyo ni changamoto ambayo Serikali inatakiwa iangalie kwa makini. Kamati inaishauri Serikali itenge pesa za kutosha kuwezesha upimaji na urasimishaji wa ardhi kwa wananchi wetu wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kitu cha ajabu, juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwamba Wizara ya Maliasili iende ikatambue mipaka ya baadhi ya hifadhi. Sisi kama Kamati tulishangaa, tuliamini kwamba ilitakiwa na Wizara ya Ardhi nayo ishirikishwe katika kutambua mipaka ya hifadhi za maliasili, lakini hatuoni kama hilo lilitendeka na tuna wasiwasi kama kweli hilo zoezi litaweza kufanyika kwa Wizara ya Maliasili peke yake bila kushirikisha Wizara ya Ardhi. Kama Kamati tunaishauri Serikali Wizara zishirikiane katika kufanya kazi ili kuleta tija katika mambo mbalimbali ambayo wanaelekezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea mchango kutoka kwa baadhi ya Wabunge kuhusu ile Kamati ya Wizara Tano inayoshughulikia migogoro. Sisi kama Kamati tumeipokea na tunazidi kuisisitiza Serikali ihakikishe kwamba ile Kamati inaleta ripoti yake kwa wakati ili tuweze kupunguza kama sio kuondoa kabisa migogoro kati ya hifadhi na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Ngorongoro vilevile hatukuweza kuliingiza kwenye taarifa ya Kamati yetu kwa sababu tuliliweka kwenye ratiba ya kwenda kutembelea Ngorongoro ili tuweze kuishauri vizuri Serikali, lakini kama kawaida tuliambiwa bajeti haitoshi tukashindwa kwenda. Ni ngumu sana kutoa taarifa na kuzungumzia kitu ambacho hujawahi kukiona. Tunachelea kuzungumza taarifa ya sehemu muhimu kama Ngorongoro kwa kutegemea makaratasi tuliyoletewa mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mjumbe mmoja wa Kamati yangu vilevile ameulizia kuhusu suala la Faru John. Nilitegemea suala hili lingeulizwa na Wajumbe wengi kweli, lakini nashukuru kwamba wengi walielewa kwamba hili suala lipo kwenye uchunguzi, liko chini ya Waziri Mkuu kuna tume imeundwa kulichunguza. Tunaamini tume hiyo itatuletea ripoti baada ya hapo tutaanza kulijadili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la askari wa wanyamapori. Kwa ujumla kama Kamati hata sisi tunasikitishwa sana na baadhi ya askari wa wanyamapori ambao wanaamua kuchukua sheria mkononi na kuua Watanzania wenzetu. Kwa hiyo, kama Kamati tunashauri Wizara ya Maliasili na Utalii iongeze mafunzo kwa askari wetu, lakini vilevile tuishauri Serikali kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu hifadhi zetu kwa sababu bila wananchi kupata uelewa wa kutosha migogoro kati ya askari na wananchi itaendelea kuwepo na hatupendezwi na madhara yanayotokana na vifo vya Watanzania wanaoingia kwenye hifadhi zetu. Kuna njia rahisi zinaweza kutumika ambazo haziwezi kuleta madhara sana kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ongezeko la VAT kwenye suala letu la utalii. Wakati tunaandaa ripoti yetu tulikutana na Wizara nayo ikatuahidi kwamba mwisho wa mwaka wa fedha watakuwa na taarifa kamili ya hali ya utalii. Kwa hiyo, naomba kama Kamati na Bunge tuvumilie, tusubiri Wizara ituletee taarifa hiyo na kama kutakuwa na upungufu tutaangalia namna ya kuboresha zaidi ili hifadhi na utalii wa nchi yetu uendelee kukua na utuletee tija katika mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye suala la National Housing. Wabunge wengi sana wameongelea sana suala la National Housing. Kama mapendekezo ya Kamati yalivyojionyesha ni kweli kwamba maeneo mengi ambayo National Housing wanakwenda kujenga wanalazimika kununua ardhi, halafu wakishajenga wanalazimika kuleta miundombinu ya barabara, wanaleta umeme na maji. Wakati mwingine National Housing wanapata viwanja sehemu ya mbali na maeneo ambako hivyo vyanzo vipo na wao wanalazimika kuchukua hizo gharama na kuzigawa kwa kila nyumba moja moja. Hali hiyo inasababisha nyumba za National Housing zisionekane ni za gharama nafuu kwa sababu ukishalipia vitu vyote hivyo huwezi kupata gharama nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikuwa natamani sasa Serikali ishirikiane, taasisi zote zinazohusika zishirikiane. Haiwezekani National Housing wagharamie suala la maji halafu Mamlaka za Maji ndiyo ziende zisome bili na kupata pesa kama zenyewe, hiyo ni kumbebesha mwananchi mzigo usikuwa na tija. Vilevile kwa masuala ya umeme, haiwezekani National Housing wasafirishe nguzo hamsini kupeleka kwenye destination ya site halafu TANESCO waje wachukue bili kwa sababu tu umeme ni wa kwao. Naamini TANESCO wakichukua jukumu lao na Mamlaka za Maji zikichukua jukumu lao pamoja na Halmashauri zetu zikichukua jukumu la kupeleka miundombinu ya barabara nyumba zetu za NationalHousing zitakuwa za gharama nafuu na sisi kama Kamati tunalitetea Shirika letu la National Housing liweze kuendelea kufanya kazi zake za kuwahudumia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea amendment kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kuhusu suala la Kigamboni Development Agency. Kamati inakubaliana nayo na tutaomba iingizwe kwenye taarifa yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na hifadhi zetu. Kwenye taarifa yetu tumeiweka wazi kwamba kuna mifugo ambayo ipo ndani ya hifadhi zetu. Bado tunasisitiza kwamba kikanuni na kisheria mifugo hairuhusiwi kuwemo ndani ya hifadhi. Tuwashauri Waheshimiwa Wabunge wawaeleweshe wananchi. Nilifurahishwa sana na Mheshimiwa Sannda ambaye alichukua jukumu la kuwaelimisha wananchi na wanaheshimu hifadhi na hawaingilii hifadhi. Hizi hifadhi kama zikivurugika, nchi yetu itakuwa jangwa na hatutapona. Hiyo mifugo tunayoitetea leo na yenyewe itakufa. Kwa hiyo, tujitahidi tushirikiane tuhifadhi misitu yetu ili kuhifadhi mazingira yetu yasiharibike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nitaongelea suala la mashamba makubwa yaliyotelekezwa. Kamati yetu imependekeza Serikali ifanye uhakiki wa haraka mashamba yote makubwa yaliyotelekezwa yachukuliwe yapangwe na yagawiwe kwa wananchi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Vilevile kama itawezekana na Serikali tunatamani iwe na land bank ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya viwanda kwa sababu tunakwenda kwenye dunia ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la shoroba, siwezi nikazungumza moja kwa moja migogoro ya tembo na wananchi inayotokea sehemu mbalimbali hasa Mkoa wa Mara. Nachelea ku-confirm moja kwa moja kwamba inawezekana shoroba zimeingiliwa, inawezekana zimeingiliwa au hazijaingiliwa. Hata hivyo, natamani Serikali sasa iamke na iende kutambua shoroba zote ambazo zimeingiliwa kwa sababu baadhi ya shoroba Halmashauri imejenga, baadhi ya shoroba kuna shule zimejengwa na hizo zote ni za Serikali. Kwa hiyo, ushirikiano kati ya Wizara mbalimbali ni muhimu sana kuhakikisha tunalinda shoroba zetu na zile ambazo kweli kabisa taasisi za Serikali zimejenga basi Serikali iangalie namna ya kufidia ziondolewe ili wanyama wapate mahali pa kupita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo sehemu aliyopita miaka hamsini iliyopita habadilishi anapita palepale. Kwa hiyo, ukijenga aki-escape lazima atadhuru mifugo na mazao ya wananchi kwa sababu sehemu anakopita ni palepale hata miaka mia inayokuja. Kwa hiyo, tulinde shoroba zetu ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata changamoto kidogo kutoka kwa Mheshimiwa Kanyasu kuhusu pori la Geita kuvamiwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Kanyasu kwa kuonesha uchungu wa kutaka kuhifadhi pori letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba kutoa hoja kwamba Bunge sasa lipokee na kukubali taarifa ya Kamati pamoja na maoni na maendekezo yalimo katika taarifa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja!
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa jitihada zake mbalimbali za kuisogeza nchi yetu katika uchumi wa kati. Nampongeza vilevile Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwa mpango mzuri sana aliouleta, ambao ni mpango endelevu kwa ajili ya Serikali, unaolenga Mpango wa Serikali wa miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii vilevile kuwashukuru wachangiaji mbalimbali Waheshimiwa Wabunge waliochangia Mpango huu kwa nia njema kabisa, lakini niwashukuru kipekee wale waliochangia kwenye sekta ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.

Mheshimwa Mwenyekiti, kipekee kabisa napenda niongelee masuala makuu manne, nitaongelea masuala ya reli, nitaongelea masuala ya barabara, nitaongelea masuala ya bandari na mwisho nitagusia kidogo masuala ya viwanja vya ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango mkubwa sana wa ujenzi wa reli mpya kwa kiwango cha standard gauge, kila Mbunge anajua na kila mwananchi anafahamu. Serikali ya Awamu ya Tano inatarajia kujenga jumla ya kilometa 4,886 ambazo kiujumla kabisa zitajumuisha kanda kuu tatu, tutakuwa na Ukanda wa Kati ambao utajumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Isaka, Mwanza ambayo ni kilometa 1,219 lakini vilevile tutakuwa na Ukanda wa Kaskazini ambao tutakuwa na reli ya kutoka Tanga, itapita Arusha mpaka Musoma, hizo ni kilometa 1,233 na vilevile tutakuwa na Ukanda wa Kusini ambao ni wa kilometa 1,092 ambao utatoka Mtwara – Mbamba Bay na matawi yake ambayo ni ya Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia na reli ya kati, tumeshaanza ujenzi wa kiwango cha standard gauge kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, kilometa 300 ambazo zitajumlisha njia ya reli ya kawaida pamoja na trunks zake na sliding, mkandarasi mpaka sasahivi yuko site anaendelea na kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwishapata mkandarasi vilevile kwa ajili ya kipande cha Morogoro mpaka Makutupora kilometa 422 sasa hivi yuko kwenye mobilization, wakati wowote ule ataanza kazi, sehemu nyingine zote zinaendelea na utaratibu wa upembuzi yakinifu na taratibu nyingine kwa ajili ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya gharama itakayotumika kwa ajili ya mradi huu wa standard gauge kwa nchi yetu itakuwa ni dola za Kimarekani bilioni 3.17. Tunategemea itakapokwisha itakuwa na uwezo wa kwenda speed ya kilometa 160 kwa saa, vilevile itabeba tani milioni 17 kwa mwaka. Hiyo ni miradi kwa upande wa reli ambayo inaendelea na tumeona jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba hiyo reli inajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa bandari tulikuwa na wachangiaji kadhaa ambao walizungumzia sana masuala ya bandari. Serikali imekuwa na mpango mzuri sana wa kuboresha bandari yetu kwanza ya Dar es Salaam kwa geti namba moja mpaka geti namba saba, ambapo moja ya shughuli zitakazofanyika itakuwa ni kuongeza kina cha bandari kwa mita 15 deep sea, halafu kuna sehemu ya meli kugeuzia na yenyewe inapanuliwa kwa kiwango kizuri kabisa cha kimataifa, vilevile tunaongeza sehemu ya dragging and channel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Bandari ya Dar es Salaam itaenda kuboreshwa kwa kipindi kifupi kinachokuja kuhakikisha kwamba inaweza kuhudumia meli nyingi kwa wakati mmoja kwa kiwango cha kimataifa na gharama zitakazohusika katika mradi huo ni shilingi za Kitanzania bilioni 335.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna uboreshaji wa Bandari ya Mtwara ambapo zimetengwa jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 186. Tunatengeneza gati mpya pale kwa ajili ya kufungua lango la Kusini kusafirisha na kupokea mizigo. Tunajua jinsi ambavyo kuna mabadiliko makubwa sana katika Ukanda wetu wa Kusini, kuna viwanda vinaanzishwa vikubwa, tunategemea tuweze kupata mizigo ya kutosha kwa ajili ya kuhudumia bandari ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mamlaka ya Bandari Tanzania inaendelea kulipa fidia kwa wananchi kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo baada ya malipo kukamilika tunategemea kwamba ardhi itakayokuwa imepatikana sasa atapewa mwekezaji ambaye tunaendelea na mawasiliano naye kwa ajili ya kujenga bandari hiyo ambayo itasaidia sana katika kufungua lango upande wa Mashariki wa nchi yetu. Ni matumaini yetu kwamba, wananchi ambao wako maeneo ya Bagamoyo ambayo yako karibu na sehemu tutakakojenga bandari watatoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Serikali kuhakikisha kwamba tunapata eneo hilo kwa ajili ya kujenga bandari mpya pale Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna suala la viwanja vya ndege. Ni kweli kwamba Serikali imenunua jumla ya ndege sita, tunazo Bombadier Q400 ziko tatu ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 76 na ndege mbili tayari ziko hapa nchini na moja itakuja hivi karibuni. Tunayo ndege ya Q Series au Q300 ambayo inabeba abiria 150 mpaka 176 na yenyewe iko kwenye hatua za mwisho kabla haijaja nchini na tumekwishafanya malipo ya mwanzo kwa ajili ya kupata Boeing 787 ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 262. Ndege hizo zote ni kwa ajili ya kurahisisha huduma ya usafiri kwa njia ya anga ili nchi yetu iweze kupata maendeleo yanayotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeendelea kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya upanuzi wa viwanja mbalimbali hapa nchini. Tuna viwanja 11 ambavyo tayari matengenezo yameshaanza kwa ajili ya kuvipanua, kupanua run ways, kuna sehemu kwa ajili ya apron, kwa ajili ya sehemu za kugeuzia ndege na ku-park, lakini vilevile tumeendelea kujenga majengo ya abiria kwa ajili ya kuhudumia abiria wanaofika kwenye viwanja hivyo husika vya ndege. Kwa kutaja tu, kuna uwanja wa ndege wa Kigoma tumeshatangaza tender kwa ajili ya kutafuta mkandarasi wa kupanua uwanja huo, kuna uwanja wa ndege wa Sumbawanga tumeshatangaza tender vilevile, kuna viwanja vingine mbalimbali kama Mbeya, Tabora na uwanja wa ndege wa Geita. Kwa hiyo, kuna maendeleo makubwa ambayo Serikali inayafanya kwa ajili ya kuhakikisha kwamba viwanja vyetu vinakuwa vya ubora wa kisasa kabisa kwa ajili ya kuhudumia abiria mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kwa haraka tu upande wa barabara. Waheshimiwa Wabunge wote wanaelewa wazi kwamba kuna miradi mikubwa tunaendelea nayo ya ujenzi wa barabara. Kuna barabara ya TAZARA flyovers inaendelea, mkandarasi yuko pale na tunategemea muda sio mrefu barabara itakuwa iko tayari kwa ajili ya matumizi, vilevile kuna Ubungo Interchange ambayo tayari maandalizi ya ujenzi yameshaanza, mkandarasi yuko kwenye site kwa ajili ya kufanya mobilization na shughuli mbalimbali za kuhakikisha kwamba ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeendelea na mpango wa kuhakikisha kwamba kila Mkoa katika nchi yetu ya Tanzania unaunganishwa kwa kiwango cha lami. Sehemu zile chache zilizobakia ambazo bado hazijapata mkandarasi tunaendelea kutangaza tenda ili mkandarasi apatikane kwa ajili ya kuweza kuunganisha Mikoa yetu kwa kiwango cha lami, lakini vilevile tunaunganisha Wilaya zetu ndani ya Mikoa mbalimbali kwa kiwango cha lami na hatua kadhaa mbalimbali zimeshaendelea kutekelezwa. Tunashukuru sana kwa michango ya Waheshimiwa Wabunge na tunawaahidi tutaendelea kuhakikisha kwamba tunayachukua mawazo yao na kuyafanyia kazi kwa kadri itakavyowezekana, ili nchi yetu iweze kuwa na mtandao wa barabara nchi nzima ambao unapitika mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwapongeza vilevile Waheshimiwa Wabunge ambao wametuletea michango kwa njia mbalimbali na kwa sekta yetu ya uchukuzi, mawasiliano na ujenzi tunawaahidi kwamba, tutafanya nao kazi kwa karibu sana, lakini tukiwakumbusha kwamba ujenzi au uinuaji wa kiwango cha barabara unategemea kwanza vikao ndani ya Halmashauri husika, baada ya hapo inekwenda kwenye RCC, baada ya hapo ndiyo inakuja kwenye bajeti kuu na kutengewa pesa kwa ajli ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mwasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kunifanya niweze kusimama mbele ya Bunge lako tukufu. Lakini nichukue nafasi hii vilevile kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua niweze kumsaidia katika nafasi aliyonipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa namshukuru Waziri wangu Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Mbunge) kwa ushirikiano na muongozo anaonipatia mara kwa mara katika utendaji wa shughuli zangu. Nawashukuru vilevile watendaji, Dkt. Leonard Chamuriho - Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Engineer Nyamuhanga - Katibu Mkuu wa Ujenzi na Dkt. Maria Sasabo - Katibu Mkuu wa Mawasiliano pamoja na Engineer Madete - Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano kwa ushauri wanaonipatia katika kutenda majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii vilevile kuwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Muhambwe ambao najua kabisa kwamba sasa hivi wanani-miss, lakini niwahakikishie kwamba niko nao katika majukumu yote ya Jimbo vilevile pamoja na kwamba siendi mara kwa mara. Naishukuru vilevile na familia yangu. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, nitachangia kuhusu sekta ya mawasiliano pamoja na sekta ya uchukuzi kwa haraka haraka. Nimepata concern nyingi sana za Waheshimiwa Wabunge kuhusu masuala ya mawasiliano kwenye maeneo yao. Ni kweli kabisa kwamba takwimu za kiserikali zinaonesha kwamba nchi yetu tunawasiliana kwa asilimia 94, nitafafanua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaposema kwamba tunawasiliana kwa asilimia 94 ni kwamba karibu maeneo mengi sana ya nchi yetu yanapata mtandao wa mawasiliano ya simu isipokuwa baadhi ya maeneo wanakuwa wako selective wanataka labda wapate na Vodacom, Tigo, Airtel pamoja na Halotel sasa Kiserikali hiyo hatuizuii ni kitu kizuri lakini sisi tunachosema kwamba eneo likipata huduma ya mawasiliano kama ni Halotel tunatia tiki kwamba hapo wanaweza wakawasiliana na kwa kweli katika hali ya kawaida kama kuna dharura yoyote wanaweza wakapata mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unaitwa UCSAF ambao kazi yake kubwa unapeleka mawasiliano sehemu zile ambazo hakuna mvuto wa kibiashara. Tukumbuke siku za nyuma tulikuwa tunategemea sana hizi Kampuni za Simu kupeleka mawasiliano au minara sehemu ambazo wao wanaona kwamba zinafaa na zitawapatia faida katika majukumu yao ya kibiashara, lakini kutokana na hilo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kabisa kwamba tuunde Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ambao sehemu ambazo hazina mvuto wa kibiashara basi wale UCSAF wataweza kupeleka mawasiliano. Hii ndiyo kazi maalum kwa ajili ya kupeleka mawasiliano kwa Watanzania wote.

Kwa hiyo majuku yake makubwa kwanza ni kupeleka mawasiliano sehemu ambazo hakuna mvuto wa kibiashara na ambako hakuna kabisa mawasiliano na hilo jukumu limeendeelea kufanyika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Tumegundua sehemu nyingi sana zimeshapelekewa minara hasa ya Halotel na hawa UCSAF wameingia mkataba na Halotel kwa ajili ya kupeleka mawasiliano sehemu hizo ambazo hakuna mvuto wa kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile kuna maeneo ya mipakani, Wabunge wengi sana waliochangia hasa wanaokaa maeneo ya mipakani kama mimi wamezungumzia kwa kirefu sana kwamba kuna maeneo ambayo wakiingia mtandao unaosoma ni wa nchi jirani. Hilo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeliona, lakini kwa kushirikiana na TCRA kuna mpango mkakati unafanywa kuhakikisha tunapeleka minara yenye nguvu lakini na kuangalia masafa yanayozingatiwa ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata mawasiliano ya Tanzania na hao wengine wanaendelea kupata mawasiliano ambayo yanawahusu kwa nchi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile eneo la tatu ambalo linasumbua ni minara iliyopo sasa hivi kutokuwa na nguvu, ni kweli kabsia maeneo mengi ya nchi yetu baadhi hayajapata huduma za umeme na ndiyo maana kupitia mpango wa umeme wa vijijini Awamu ya Tatu (REA III) tuna uhakika kwamba matatizo yatapungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kushirikiana na TCRA na UCSAF wameendelea kupeleka ujumbe kwa makampuni hayo ya simu yale ambayo yamepeleka solar waongeze nguvu ya hizo solar energy ili at least mawasiliano yaweze kupatikana masaa yote. Kwa sababu tumegundua kabisa ni kweli kwamba kama siku mvua imekuwa ikinyesha labda toka asubuhi mpaka mchana zile solar zinakuwa haziwezi ku-charge kwa sababu jua hakuna matokeo yake ikifika saa 12 jioni mawasiliano ya simu maeneo hayo yanakuwa hayapatikani.

Kwa hiyo, tumewashauri haya makampuni ya simu wamepele aidha, generator na hasa hasa wapeleke generator au waongeze nguvu ya zile solar kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tunaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo hayana mawasiliano yanapelekewa mawasiliano na hivi karibuni nimekuwa nikiongea na Wabunge na niliwaeleza waniletee tu maeneo ambayo wana uhakika kabisa hakuna mawasiliano ili kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote tuweze kuwapeleka minara waweze kupata mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea kiasi kwa haraka haraka kuhusu TCRA na majukumu yake. Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wameizungumzia sana TCRA na ninashukuru sana kwa pongezi mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge mmezitoa kwa TCRA, kwa kweli tunazipokea na tunashukuru sana kwamba TCRA inaendelea kufanya kazi nzuri sana. Lakini niwakumbushe tu Wabunge kwamba pamoja na majukumu mbalimbali, TCRA vilevile inaendelea kuhakikisha tunadhibiti usalama wa mitandao yetu na tunasimamia masafa ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata faida kutojua na masafa ambayo ilipangiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile, TCRA imeendelea kusimamia upatikanaji wa mapato stahiki ya Serikali kutokana na matumizi ya mawasiliano na hasa kwa kutumia ule mtambo wetu ambao tumeufunga wa TTMS ambapo kwa kupitia TTMS tunapata telecommunication trafficking yote ya ndani na ya nje kwamba mtu anapopiga simu kutoka nje na watu wanaopiga simu kutoka ndani tunaona wametumia dakika ngapi, wametumia shilingi ngapi kwa hiyo stahiki ya Serikali ni kiasi gani na stahii ya hayo makampuni y simu ni kiasi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia hiyo nina uhakika kabisa TCRA wameendelea kuisaidia Seriakli na wananchi kwa ujumla lakini vievile wameendelea kuhakikisha kwamba wanapunguza matukio ya uhalifu kwenye mitandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni kutokana na mtandao kukua sana tumekuwa na changamoto mbalimbali za matumizi mabaya mitandao yetu ambako hata viongozi wamekuwa wakitukanwa, sisi wenyewe Wabunge tumekuwa tukidhalilishwa hapa na pale, lakini kupitia TCRA wametengeneza muundo ambao tunaendelea kuwadhibiti hawa wahalifu wa mitandao na hasa wale ambao wanaleta lugha ambazo hazina maadili kwenye nchi yetu kuhakikisha kwamba tunashirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Cybercrime kuhakikisha kwamba tunawadhibiti na matukio hayo kiasi fulani kwa kweli yamepungua na hata yanatokea mara nyingi tunao uwezo wa kuyafutailia na kuwakamata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kwa haraka haraka kuhusu Data Centre, tunacho kituo cha Data Centre, kuna baadhi ya Wabunge wameliongelea. Kituo hiki kinaendelea kutumika vizuri ambapo hadi sasa tunavyoongea taasisi za Serikali 41 tayari zinakitumia kituo hiki na taasisi 11 za binafsi na zenywe zinakitumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa kituo hiki ni kuhakiakisha kwamba matumizi yote yale yanayofanywa kwa transaction, wka mfano, unapohamisha pesa kutoka kampuni ya simu kwenda benki, benki kwenda kampuni ya simu au unapolipia EWURA, unapolipia TANESCO na mambo mbalimbali kuna tozo zile za Kiserikali ambazo zinatakiwa zirudi Serikalini. Kwa kutumia Data Centre ni rahisi sana kwa TRA kuweza kuona mapato hayo na kweza kuyadai kutoka kwenye taasisi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie tu kwamba kituo kinafanya vizuri na ninatoa wito kwa Makapuni mbalimbali kuendelea kujiunga na Data Centre ili kujiridhisha na kuhakikishiwa kwamba wanapata pesa na tender nyingi kutoka Serikalini kwa sababu Serikali inahitaji kuona pesa inayoitoa ione matumizi yake lakini ipate stahiki kutokana na pesa inayoitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kwa haraka haraka kuhusu sekta ya uchukuzi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi aliyotupatia kukutana mahali hapa kwa ajili ya kujadili mambo muhimu yanahusu nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pili, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa majukumu mengi sana anayofanya kwa ajili ya nchi yetu. Nimpongeze vilevile kwa majukumu mengi anayoendelea nayo na nashukuru kwa kuniamini niweze kumsaidia.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee kabisa, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa support kubwa anayonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza sana na kumshukuru pacha wangu Naibu Waziri wa Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayehusika na Ujenzi, Mheshimiwa Eliasi John Kwandikwa bila kuwasahau watendaji wote nikianza na Mhandisi Dkt. Chamuriho (Katibu Mkuu wa Uchukuzi), Mhandisi Dkt. Maria Sasabo (Katibu Mkuu wa Mawasiliano) na Arch. Mwakalinga (Katibu Mkuu wa Ujenzi).

Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa maelekezo na misaada mbalimbali wanayoipatia Wizara yetu katika kutekeleza majukumu yake. Nichukue nafasi hii niwashukuru Wabunge wote kwa ushirikiano, urafiki na ukarimu ambao wanaitendea Wizara yetu katika kutekeleza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Muhambwe lililoko Mkoa wa Kigoma, Wilaya ya Kibondo. Vilevile naishukuru familia yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Kwa sababu ya muda nitajaribu kujieleza kwa baadhi ya hoja chache tu, kwa upande wa uchukuzi nitagusia masuala ya hali ya hewa lakini nitagusia miradi miwili mikubwa ya kimkakati ya reli ya kutoka Tanga - Musoma na Mtwara - Mbambabay. Nikipata nafasi nzuri nitagusia masuala mazima ya ATCL lakini kwenye mawasiliano nitazungumzia suala la usajili wa laini za simu pamoja na utendaji wa UCSAF.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee, kwanza, nitoe pole kwa Watanzania wenzetu ambao wamepata madhara sehemu mbalimbali kutokana na mvua nyingi na kubwa zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Sasa hivi Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo kadhaa ya Pwani yame-experience mafuriko ambayo yanaendelea, tunaona kwenye mitandao ya kijamii na sehemu mbalimbali na tunapigiwa simu hata na ndugu zetu kwamba hali si nzuri sana kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, niipongeze Mamlaka ya Hali ya Hewa imekuwa ikifanya kazi nzuri sana ya kuwaelimisha Watanzania juu ya athari ambazo zitatokea kwa siku zijazo kutokana na vifaa vya kisasa wanavyovitumia. Itakumbukwa kwamba tarehe 21 Aprili, 2019, Mamlaka ya Hali ya Hewa walitoa tahadhari kwamba Mikoa ya Kusini Lindi na Mtwara ingekumbwa na kimbunga cha Kenneth. Bahati nzuri tuliendelea sana kuhakikisha kwamba tunatoa tahadhari kwa wananchi lakini Mungu akatuepushia mbali kile kimbunga hakikuweza kutoa athari kubwa. Ilipofika tarehe 24 tuliwatahadharisha tena hata wenzetu wa Mikoa ya Simiyu na Shinyanga kwamba kuna kimbunga ambacho kingetokea kutokea misitu ya Congo kingeweza kuathiri maeneo ya Kahama na tulishuhudia kwamba kulikuwa na mafuriko yaliyotokea.

Mheshimiwa Spika, hili najaribu kuwaelezea baadhi ya Wabunge ambao walithubutu kusema kwamba Mamlaka ya Hali ya Hewa inafanya utabiri kama waganga wa kienyeji, hiyo sio kweli. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sasa hivi inafanya utabiri wake kwa asilimia 87.8. Katika hali ya kawaida tungepaswa hata kuondoa lile neno utabiri tuwe tunasema tu hali ya hewa kama mataifa yaliyoendelea yanavyofanya. Wakisema kitu kinatokea na sisi kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa tukisema kitu kinatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Mkoani Dar es Salaam na maeneo ya Pwani ni sehemu ya mvua za masika. Nitoe wito kwa Watanzania wenzetu kwamba mvua hizi ni kubwa na zitaendelea kuwepo kwa kipindi chote mpaka mwisho wa mwezi huu. Tunaomba wachukue tahadhari na waendelee kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa. Tumejipanga kuhakikisha kwamba tunawahabarisha Watanzania ili wachukue tahadhari mbalimbali kujiepusha na uharibifu wa mali zao lakini pia na maisha yao.

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa kutoa utabiri wa viwango vya kimataifa, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba mamlaka ina wataalam waliobobea katika masuala ya Hali ya Hewa. Aidha, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa Mamlaka inakuwa na vifaa vya kisasa vya kufanya uangazi (observation) na utabiri.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Serikali imeingia mkataba wa ununuzi wa rada tatu za kisasa za hali ya hewa ambazo zitafungwa katika Mikoa ya Mtwara, Mbeya na Kigoma. Rada itakayofungwa Mtwara itasaidia kufuatilia vimbunga katika bahari ya Hindi, rada itakayofungwa Mbeya itasaidia kuhudumia wakulima kwenye mikoa inayozalisha chakula kwa wingi lakini na rada itakayofungwa Kigoma itasaidia katika kufuatilia na kutoa tahadhari ya matukio ya radi na taarifa muhimu kwa wananchi wanaofanya shughuli zao katika Kanda ya Ziwa Tanganyika na mwambao wa ziwa hilo. Ununuzi wa rada hizo tatu utaifanya Tanzania kuwa na jumla ya rada tano ikijumuisha na rada zilizofungwa Dar es Salaam na Mwanza.

Mheshimiwa Spika, nitaongelea kiasi fulani suala la ujenzi wa reli kati ya Tanga - Musoma. Hatua tuliyofika mpaka sasa hivi kwa upande wa Serikali ni kufanya upembuzi yakinifu lakini tumekwishafanya usanifu wa awali na wa kina, tumekwishajua gharama zinazopaswa. Hatua iliyoko sasa hivi ni kutafuta mwekezaji ambaye ataingia mkataba na Serikali kufanya mradi huo kwa njia ya PPP.

Mheshimiwa Spika, katika kufikia hatua hiyo kuna kitengo ambacho kiko Wizara ya Fedha ambacho ndiyo kinashughulika na mikataba hiyo. Watu wa Wizara ya Fedha wanatusaidia katika kuhakikisha kwamba mikataba itakayoingia na mwekezaji mbia inakuwa na tija kwa nchi yetu. Hatuko tayari kuona kwamba nchi yetu inaingia kwenye mikataba ambayo haina tija kwa wananchi. Sisi tumejipanga kuhakikisha kwamba mikataba yote tutakayoingia inakuwa na tija lakini inawasaidia wananchi kwa kizazi cha sasa, cha kesho na kinachokuja.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna wabia wamekuwa wakijitokeza mara kwa mara kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutaka kuwekeza kwa njia ya PPP kwa reli ya Tanga – Musoma lakini pia kwa reli ya Mtwara - Mbambabay. Hata hivyo, masharti yao wakati mwingine yanakuwa ni magumu sana kutekelezeka na tumekuwa tukiendelea na mazungumzo nao kuhakikisha kwamba mkataba kati yetu sisi Serikali na wao basi unakuwa na tija kwa nchi yetu. Tusiumie lakini na wao wasiumie wapate faida kwa sababu tunategemea waingize hela zao katika shughuli hizo.

Mheshimiwa Spika, vipande vya reli kutoka Tanga - Musoma na kipande cha reli kutoka Mtwara - Mbambabay na matawi yake ya Mchuchuma na Liganga bado yako kwenye mazungumzo na yako mahali pazuri. Itakapofikia mahali muafaka tutawaelewesha Watanzania kwamba sasa tunaingia mkataba kwa ajili kutengeneza reli hizo.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo suala la ndege zetu za ATCL. Serikali imenunua ndege hizo na kuwapatia ATCL ili wazifanyie biashara warudishe pesa kwa Serikali. Hivi karibuni kumetokea maneno ya manung’uniko kidogo kutoka kwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kwamba nauli za ATCL zimekuwa kubwa. Ukweli ni kwamba si sahihi, nauli za ATCL bado zimeendelea kuwa ni nafuu kabisa na ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wengi huwa wanakuwa na option namba mbili baada kukosa tiketi za ATCL, ni kwa sababu huduma ni nzuri na nauli zao ni nyepesi.

Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida tunakubali kuwa na ushindani, kuna ndege nyingine za Precision, ziko ndege za aina mbalimbali na zenyewe zinatoa huduma kwenye njia ambazo ATCL wanafanya kazi. Huwa wanaanza kwa bei nafuu lakini mwisho wa siku wanaenda kuwa na gharama kubwa sana ambazo wateja wao huwa wanakimbilia ATCL. Nakuomba sana tuwashawishi Wabunge waiunge mkono ATCL, ni shirika letu la ndege ili liweze kuendelea kutoa huduma nzuri na za uhakika na ndege zetu ni za uhakika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo nikiri changamoto ya kuwepo kwa delay za ndege zetu. Nikiri changamoto ya kuwa na cancellation kwenye baadhi ya route. Hilo ni la kweli tumekwishalishuhudia na sisi kama Serikali tumeshatoa maelekezo kwa ATCL kwamba kuanzia sasa hivi ndege yoyote ambayo itakuwa na delay zaidi ya nusu saa tunahitaji tupate maelezo ya maandishi yakiambatana na vielelezo. Kama ni hali ya hewa basi tupate na taarifa ya hali ya hewa ambayo imeambatanishwa ku-justify maelezo ya delay ya safari husika. Hilo tumekwishaongea na watu wa ATCL na wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba safari zote za ndege haziwi na changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, niongelee kwa harakaharaka masuala ya mawasiliano, kuna suala la usajili wa laini za simu. Ni kweli kuanzia tarehe 1 Mei, Serikali kupitia TCRA imeamua Watanzania wasajili laini zao za simu kupitia alama za vidole zikiambatana na kitambulisho cha NIDA.

Mheshimiwa Spika, kwanza nifafanue ni laini moja kwa kila mtandao. Kama una mitandao ya Tigo, Voda, Halotel, Airtel na TTCL unaruhusiwa kuwa na laini moja moja. Endapo utahitaji laini ya pili eleza tutakusajili.

Mheshimiwa Spika, nia ya kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba kwa kiasi kikubwa tunayadhibiti matumizi mabaya ya mtandao. Ukisajili laini zako tatu za Voda tukajua kabisa ni wewe umesajili maana yake ikitumika vibaya basi tutakuchukua halafu tutakupeleka kwa upole kabisa ili uweze kwenda kuwasaidia Polisi kutoa maelezo ya hicho kilichokufanya utumie mtandao vibaya, hatuna lengo baya.

Mheshimiwa Spika, suala la vitambulisho tumeamua kuchagua kitambulisho cha NIDA kwa sababu moja tu kwamba ni kitambulisho ambacho kinavuka mipaka yote Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Kitambulisho cha Mkazi wa Zanzibar tunakikubali, ni halali na kizuri na hakina tatizo lakini tunachokiona ni kwamba kile kinatumika kwa Mzanzibar, kikija huku Bara hakitumiki, kwa hiyo, hakiwezi kutumika kwa Bara lakini mitandao ya simu kama Halotel, Tigo na kadhalika inatumika Bara na Visiwani. Tukichukua kitambulisho cha kule peke yake hakitatusaidia kudhibiti uhalifu.

Mheshimiwa Spika, pia leseni za magari siyo kila Mtanzania aliyetimiza miaka 18 ni lazima awe na leseni ya gari. Kuna wengine hawana leseni ya gari, wale ambao hawana leseni ya gari wanahitaji kuwa na mawasiliano ya simu. Kwa hiyo, tumeona kwamba kitambulisho cha NIDA kitawasaidia kwa sababu kile ni kitambulisho ambacho kinamhusu Mtanzania yeyote aliyetimiza miaka 18.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi nipende kutoa taarifa kwamba kwa Zanzibar taarifa za NIDA zinasema zaidi ya asilimia 90 wameshapewa namba ya usajili wa vitambulisho vya NIDA. Masuala ya kupata kitambulisho yanaendelea taratibu lakini namba za usajili wamekwishapata. Kwa hiyo, tuna uhakika kwamba wataweza kusajili bila tatizo lolote.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tanzania Bara tuko kwenye Watanzania milioni 16. Kwa hiyo, ukichanganya tuko mahali pazuri na bado tunaamini kwamba kwa miezi nane tuliyoitoa, Watanzania wengi watakuwa wameshasajili na wataweza kutumia huduma vizuri kwa usalama wao lakini kwa uchumi vilevile kuona kwamba zile message za tafadhali nitumie pesa kwa namba hii zinadhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, Kuna Mheshimiwa Mbunge alizungumza kuhusu masuala ya picha za ajabu ajabu. Ni ngumu sana kama Serikali kumdhibiti mtu yuko chumbani kwake akaamua kujipiga hizo picha akaangalia mwenyewe. Huwezi kumzuia mtu kama huyo apige picha aangalie chumbani kwake afurahi kama inaweza ikamsaidia lakini anapoitoa nje ya chumba chake ikaanza kusambaa tutamkamata yule wa mwisho mpaka yule wa kwanza aliyejipiga zile picha akazituma kule. Nia na madhumuni ni kwamba mitandao ya mawasiliano itumike kwa faida kwa Watanzania wote bila kuathiri mtu mwingine yeyote ambaye hataki taarifa ambazo wewe unazo. Tumejipanga kuhakikisha kwamba tunadhibiti uhalifu wa kimtandao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa kuna suala la UCSAF na minara ya mawasiliano. Niliwahi kuzungumza kwamba tunafahamu changamoto ya minara ya mawasiliano kwa Waheshimiwa Wabunge na tumeendelea kufanya kazi kwa bidii sana kuhakikisha kwamba eneo kubwa sana la nchi yetu linapata mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi asilimia 94 ya Watanzania wanawasiliana. Tunachokiangalia ni kwamba kuna mawasiliano eneo fulani. Changamoto ndogo sana tunayoipata sasa hivi ni kwamba kama kuna mawasiliano ya Halotel kuna Watanzania wanataka Voda au Tigo lakini sisi Kiserikali tunasema eneo fulani Kongwa wana mawasiliano kwa sababu wana mtandao wa Halotel labda na TTCL. Wakipata dharura watapiga simu, wakitaka kuuza mazao watapiga simu, wakitaka kufanya miamala kutoka Benki kwenda mitandao hiyo au kutoka mtandao kwa mtandao watafanya miamala. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba kila watu wanawasiliana na kwa hilo asilimia 94 ya Watanzania wanawasiliana na hizi asilimia 6 zilizobakia mpaka inapofika katikati ya mwaka ujao tunakwenda kutangaza mwezi huu vijiji 689 tutakavyovipelekea minara ya mawasiliano ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanaendelea kuwasiliana.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza hayo, naunga mkono hoja asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nichukue nafasi hii kwa mara nyingine tena kuendelea kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Muhambwe kwa kunipa kura za kutosha kuweza kuja kuwahudumia kama Mbunge wa jimbo lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia maeneo mawili; Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utawala Bora na nitaanza na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kuna mamlaka ambayo inaruhusu kuanzishwa kwa vijiji vipya. Katika Jimbo langu kuna Vijiji vipya vimeanzishwa kama vitano lakini bahati mbaya vimeanzishwa bila kuwepo miundombinu ambayo inawezesha wananchi wa sehemu hiyo kuweza kuishi kwa amani sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vilivyoanzishwa vyote vitano havina shule, havina zahanati lakini vilevile havina miundombinu ya barabara wala maji. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri anayehusika ili nisishikilie mshahara wake ahakikishe kwamba, vijiji vilianzishwa kwa ridhaa yake anaviangalia kwa jicho la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna suala la afya ya mama na mtoto, tunayo changamoto kubwa sana na hata kwenye mapendekezo ya Bajeti ya Serikali ilionyesha kwamba, kweli bado tuna tatizo la vifo vya mama na mtoto. Hilo suala katika majimbo binafsi linatugusa sana lakini zaidi tunaguswa sana na suala la michango ya Bima ya Afya ile CHF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejitahidi sana kwa kadiri tunavyoweza tumehamasisha wananchi wanachangia Bima za Afya lakini wanakata tamaa wanapokwenda hospitali halafu tena wanaandikiwa wakanunue dawa. Wananchi wanakata tamaa na wanachoka kweli kweli. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali ijizatiti katika eneo hilo, mwananchi anapolipa Bima ya Afya yaani CHF akienda hospitali amkute Daktari halafu apewe dawa asilazimike kwenda kununua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaingia kidogo kwenye suala la elimu; tuendelee kuishukuru Serikali kwa mpango wake wa kuanzisha maabara katika sekondari zote za Kata. Maabara zimejengwa kwa mfano, katika Jimbo langu maabara zimejengwa karibu kata zote 19 zinakaribia kumalizika, tumeshajenga kwa asilimia 70, asilimia 30 bado kumalizia finishing.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini changamoto tuliyonayo ni suala la umeme; hakuna maabara yeyote duniani inayoweza kuendeshwa bila umeme. Naomba sana Serikali iliangalie hilo ili hizo maabara tunazozijenga watoto wetu waweze kuzitumia kwa maana ya kufanya practicles ambazo zitawaletea tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la makusanyo ya ushuru au vyanzo vya mapato vya Halmashauri zetu; najua kwamba, kila Halmashauri ina mbinu zake za kuandaa na kutekeleza vyanzo vyake vya mapato kwa ajili ya kuongeza mapato. Katika Jimbo langu bahati nzuri tunapakana na nchi jirani ya Burundi kwa sehemu kubwa sana, tumeweka masoko kama mawili yamepakana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tuna changamoto, soko moja ambalo lipo sehemu ya Kibuye, kipindi kama hiki cha mvua halifanyi kazi yoyote kwa sababu linahitaji daraja na daraja hakuna. Kwa hiyo, hata wale ndugu zetu wa nchi jirani wanashindwa kuvuka kuja kufanya biashara na kile kilikuwa ni chanzo kizuri sana cha mapato. Hawa watu wa nchi jirani wanategemea sana Tanzania katika kufanya matumizi mbalimbali; kwa hiyo wanatuletea sana pesa. Tunaomba sana Serikali iangalie suala la daraja katika soko la ujirani mwema la Kibuye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa vilevile kuongelea hizi pesa shilingi milioni 50 kwa kila Kijiji, tunaomba sana hizi pesa Serikali itupe mwongozo. Kiukweli ni kwamba, kila wakati ninapokwenda jimboni, kila ukienda kusalimia wananchi wanakuuliza swali hilo hilo. Mheshimiwa pesa ile milioni 50 imeshafika? Kila kijiji unachokwenda kusalimia wanakuuliza hilo swali. Tunajua kwamba, hazijafika lakini sasa kumbe tunahitaji mwongozo wa namna ya kuzigawa na mwongozo uwe wazi kweli kweli, vinginevyo itatuletea sana shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Ofisi ya Rais, Utawala Bora; Ofisi ya Rais, Utawala Bora wameanzisha Bodi ya Mishahara na Maslahi katika Utumishi wa Umma. Nakiri kwamba, hicho ni kitu kizuri sana kwa sababu kimeanzishwa muda kidogo lakini ukweli ni kwamba, bado maslahi na mishahara ya watumishi wengi bado ni duni. Wakati mwingine ndiyo inasababisha hata watumishi washindwe kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuingia hata kwenye tamaa za kudai rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana hii Bodi ya Mishahara na Maslahi katika Utumishi wa Umma iwezeshwe sana ili iweze kufanya kazi zake za kuhudumia watumishi ili waepukane na tamaa ambazo zinaweza zikawaingiza katika matatizo, lakini vilevile wajiepushe na tamaa ambazo zitaliingiza Taifa katika hasara kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ofisi ya Rais, Utawala Bora vilevile tunapata shida sana na TASAF. Nikiri ukweli kabisa kwamba, wakati wa kampeni mimi nilipata shida sana, wiki mbili za mwisho zile pesa zilitoka kwa wananchi. Wakati fulani wa kampeni kuna mwananchi amekuja amelewa anasifia kweli Serikali kwa kugawa hizo pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla hata sijamaliza hizo kampeni akatokea mwananchi unamwona kabisa hali yake ni duni amefika pale analalamika kwamba, yeye hajapewa pesa, ilikuwa ni mtihani mkubwa sana lakini nashukuru Mungu kwamba, yale yalipita. Tunaomba sana TASAF watusaidie sana kurekebisha hilo suala. Wanaostahili kupewa kaya zile maskini ndiyo zipewe hiyo pesa ya kuwawezesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niongelee suala lile la TAKUKURU, hii ni taasisi ambayo katika hali ya kawaida inatakiwa iwe rafiki sana na wananchi ili iweze kutekeleza majukumu yake. Inapotekeleza majukumu yake sio rahisi kwamba, itafurahisha watu wote, kuna wakati mwingine hawawafurahishi watu wote, kwa hiyo wanajenga urafiki lakini wakati huo huo wanajenga uadui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ufanyike utaratibu hawa Maofisa wa TAKUKURU kila baada ya miaka mitatu basi wawe wanabadilishwa vituo ili wasichukiwe sana na wananchi wakatengeneza uadui lakini vilevile wasizoeane sana na wananchi wakashindwa kufanya kazi yao ya kupambana na rushwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri iliyogusa karibu sehemu nyingi, hasa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara. Hata hivyo, nitapenda kupata ufafanuzi katika maeneo muhimu mawili kuhusu miundombinu ya barabara katika Jimbo langu la Muhambwe lililoko Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake ametaja kuwa kuna pesa imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami (Nyakanazi – Kibondo, kilometa 50, shilingi 17,400,000); angalia katika kitabu ukurasa wa 227.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kupata ufafanuzi ili kuondoa mkanganyiko pale Waziri anaposema Nyakazi - Kibondo, kilometa 50.
Wananchi hawaelewi kwani kipande hicho kinaishia Kabingo ambayo iko Wilaya ya Kakonko, Nyakanazi - Kibondo ni kilometa 91. Vilevile naomba commitment ya Waziri kuhusu hiyo pesa inayotegemewa kutoka ADB itapatikana lini na ujenzi utaanza lini kwa kipande kutoka Kabingo - Kakonko - Kibondo - Kasulu - Manyovu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye mapendekezo ya RCC iliyofanyika Februari, 2016 tulipendekeza baadhi ya barabara katika Majimbo ya Muhambwe, Kibondo, zipandishwe hadhi kutoka Wilaya kwenda Mkoa (Kitahama - Mabamba) na kutoka Mkoa kwenda Taifa (Kifura – Kichananga – Mabamba) kutokana na umuhimu kiuchumi na kiusalama kwa nchi yetu. Sijaona kwenye hotuba hii, naomba ziingiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kutenga pesa kwa ajili ya barabara ya Kibondo – Mabamba, (Page 255(281). Kwenye hotuba ilisema itajengwa kwa kiwango cha lami (kilometa 45), nimeona imetengewa shilingi milioni 80; tafadhali angalia suala hili kwani nyumba zinaendelea kuwekewa alama za “X”.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii adhimu kabisa. Mimi nitaongelea masuala matatu, suala la kwanza nitaanza na suala la Hifadhi yetu ya Taifa ya Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba tunawashukuru sana wananchi ambao wanaishi maeneo ya Ngorongoro kwa kutulindia Hifadhi yetu ya Ngorongoro ambayo ni alama ya Kimataifa, kwa maana ya urithi wa Kimataifa. Ni wazi kwamba sasa Sheria Namba 284 iliyoanzisha Ngorongoro imepitwa na wakati. Sheria ile wakati inaanzishwa mwaka 1959 ilihusu kuwahudumia wakazi 8,000 waliokuwa wanaishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, lakini kwa sasa hivi tunavyozungumza watu wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wamezidi 87,000. Ni wazi kwamba Ngorongoro Conservation Area hawawezi tena kuwahudumia wananchi wanaoishi mle na matokeo yake tunashuhudia migogoro ya kila siku kati ya wananchi wanaoishi eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba sana Serikali, Mheshimiwa Waziri ulete Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro tuihuishe, ili iende na wakati. Ngorongoro hawana uwezo tena wa kuwanunulia chakula wananchi wanaoishi mle, hawana uwezo tena wa kuendelea kuwahudumia huduma
za afya, zaidi ni migogoro ya kila siku tunayoishuhudia na kuiona kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Ngorongoro licha ya kwamba inahudumiwa kwa maana ya wananchi kwa sheria iliyopo, lakini kuna Baraza la Wafugaji. Juzi wakati tunatembelea Ngorongoro na Loliondo, Baraza lilikuja na ajenda kwamba, hela wanayopewa haitoshi. Kusema ule ukweli Wajumbe wa Kamati wengi walishangaa kwamba kuna Baraza tu la Wafugaji ambalo linapewa 2.7 billion shillings kuhudumia wananchi wa Ngorongoro ambao ni Wilaya inayojitegemea ambayo Serikali inapeleka pesa kwa ajili ya kuwahudumia. (Makofi)

Kwa hiyo, ndiyo umuhimu wa kuitaka Wizara ilete Sheria ya Ngorongoro tuiangalie upya, tuifanyie marekebisho kwa kuwa mmeshindwa kuwahudumia wananchi wanaoishi mle ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la hifadhi zetu, TANAPA. Kwa upande wangu naona kwamba, kazi zinazofanywa na TANAPA na kazi zinazofanywa na Ngorongoro, ukiondoa lile suala la uhifadhi mseto, zinafanana. Vilevile kuna ile Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA). Kazi zinazofanywa na TAWA, TANAPA na Ngorongoro zote zinafanana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara iangalie namna ya kuzijumlisha hizi taasisi zote tatu kiwe kitu kimoja kikubwa kiweze kuwa manageable kirahisi kuliko migogoro ambayo tunaishuhudia kila siku katika taasisi hizo. Wakati fulani nimewahi kwenda kule Pori la Moyowosi, katika hali ya kawaida wale watu walikuwa hawajui majukumu yao na majukumu ya TANAPA ni yapi na majukumu ya TFS ni yapi. Ukimuuliza suala hili huyu, anakwambia hili ni suala la TFS, ukimuuliza huyu anakwambia hili la TAWA, ukiwauliza hawa wanasema kama TANAPA wangekuwepo hapa, hili lingekuwa limepatiwa ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu ni kwamba Mheshimiwa Waziri, angalia namna ya kuunganisha hizi taasisi tatu ambazo zote zinafanya kazi ya aina moja kwa lengo moja, ziwe kitu kimoja ambacho kitakuwa na bodi moja na tutakuwa tumemsaidia Rais katika kupunguza hata baadhi ya matumizi yasiyokuwa ya lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nitaongelea kidogo hii migogoro ya mifugo na hifadhi zetu. Hakuna asiyekubaliana kati ya Wabunge kwamba, umuhimu wa kuhifadhi hifadhi zetu ni mkubwa sana. Kila Mbunge ninaamini anakubaliana kwamba lazima hifadhi zetu zihifadhiwe, tumezikuta kutoka kwa babu zetu ni vizuri tukubaliane kwamba tunaziacha kwa wajukuu zetu wazione na waziendeleze, nina mashaka na seriousness ya Wizara.
Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba unisaidie niweze kutumia dakika zilizobaki za Mheshimiwa Ester Mahawe halafu na za kwangu niendelee kuzitumia. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nianze kwanza na suala zima la uhifadhi wa misitu yetu. Mimi wakati mwingine huwa nashangaa sana. Sijabahatika wala sikufanikiwa kuwa mmoja wa waongeaji wa jazba sana; ndivyo nilivyoumbwa, halafu sioni ubaya. Lakini ninajaribu kuona namna ya kuwashawishi na kuwashauri Wabunge wenzangu, sisi ni viongozi, kuna mambo mengi sana yanaudhi, wala haina siri, lakini ukishakuwa kiongozi lazima uwe na kifua cha kuweza kumeza mambo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si swali la kujiuliza sana, ni kitu cha kawaida kabisa kwamba hakuna hata mmoja wetu hapa ambaye hajui umuhimu wa kutunza misitu yetu. Ni jambo lililo wazi kabisa kwamba mifugo ina faida kubwa sana kwa nchi yetu, lakini nakuhakikishia, mifugo haiwezi kuwepo kama tutaruhusu hii misitu yetu inayotuletea mvua ili misitu ichipuke na wanyama wapate mahala pa kulishwa, kama itateketea. Nchi itakuwa jangwa kama tukiruhusu mifugo iingie kwenye hifadhi na kuanza kulisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanaotoka mikoa ya wafugaji wanajaribu kujenga hoja tu kwamba ng‟ombe hawana tofauti na nyati. Hebu wajaribu kufuatilia vizuri, wana tofauti kubwa sana na nyati. Miaka 30 iliyopita kwenye miaka ya 1980 Shinyanga ilivyo leo haikuwa hivyo na mifugo ilikuwepo na hakukuwa na contradiction yoyote na misitu nayo ilikuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba sana, Waheshimiwa Wabunge tuuone ukweli, nchi yetu itageuka kuwa jangwa na hii mifugo tunayoitetea leo haitakuwa salama wala haitakuwa hai kama nchi yetu itakuwa jangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache siasa, tuwaambie wananchi wetu ukweli. Kwenye kampeni watu wote tumezungumza mambo mengi, lakini sasa turudi tuwaambie ukweli kwamba tukiruhusu sasa mifugo ikaenda kulisha kwenye misitu yetu nchi itakuwa jangwa, kwa hiyo, hata hiyo mifugo nayo itakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko ninakotoka Wilayani kwangu Kibondo ukihesabu mifugo ya wananchi wa Wilaya ya Kibondo, naomba nisizungumze kama mbaguzi, haizidi 60,000, lakini kwenye Pori la Moyowosi tuna ng‟ombe zaidi ya 300,000, kila siku ni ugomvi, kisingizio ni kwamba wanakwenda kunywa maji Mto Malagarasi, sasa hivi kina cha Mto Malagarasi kimeshuka, nchi inakwenda kuwa jangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kuchangia kuhusu suala la wanyamapori na uhifadhi na nitaongelea Pori la Moyowosi au Kigosi. Suala la ujangili linaendelea kutetemesha sana nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kibondo kuna ofisi kubwa sana ya Moyowosi, nilifanikiwa kwenda kutembelea pale, nikaongea na wafanyakazi kama mwanakamati wa Kamati ya Maliasili na Utalii. Nilipata changamoto zao nyingi sana, Mheshimiwa Waziri naomba uzishike. Pale kwenye ile ofisi wana magari matatu mazuri kabisa, lakini OC haifiki, matokeo yake wanaweza wakasikia bunduki ya kuua mnyama imelia somewhere lakini mafuta ni mpaka waombe kwa wale waliomiliki vitalu, hiyo ni aibu. Naomba sana hilo Serikali ilitilie umuhimu na iwasaidie sana wale wahifadhi waweze kufanya kazi zao bila matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nitakwenda kwenye sekta ya utalii. Si siri ndiyo sekta ambayo inaingiza fedha nyingi sana za kigeni kwa Taifa letu. Ina-contribute 25 percent ya fedha za kigeni katika uchumi wa nchi yetu, lakini sekta hii bado haijapewa kipaumbele cha kutosha, tunaomba sana Serikali sasa igeuze macho, iangalie sekta ya utalii. Tukiwa kama nchi ya pili kwa vivutio vingi vya utalii baada ya Brazil hatustahili kuwa hapa tulipo. Tunatamani nchi yetu i-contribute hata 50 percent ya Pato la Taifa kupitia utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo litawezekana tu kama tutawezesha Bodi ya Utalii kufanya matangazo stahiki. Bodi ya Utalii ya Tanzania kwenye bajeti iliyopita haikufikia hata Shilingi bilioni tatu ilizopewa kwa ajili ya kufanya matangozo ya utalii. Matokeo yake Bodi ya Utalii ya nchi jirani ya Kenya ilipewa zaidi ya bilioni 50 kufanya matangazo ya utalii kwa ajili ya nchi ya Kenya, ambayo unaweza ukaenda kwenye mbuga mojawapo ya kwao ukazunguka kilometa sita ukaona swali mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutokana na matangazo wanayoyafanya watalii wengi wanashuka Kenya, wanadanganywa danganywa, uongo uongo weanakuja kuangalia wanyama kwetu halafu wanarudi Kenya wanaingiza pesa nyingi sana Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wala sishangai sana kuona kwamba hata Mlima Kilimanjaro, Kenya ndio wanaoutangaza zaidi kuliko Tanzania, hiyo ni aibu.
Ninaomba sana Bodi ya Utalii iwezeshwe, ipangiwe fungu kubwa la pesa ili iweze kutangaza utalii wetu na nchi iweze kufaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mali kale. Nilipata mshituko mkubwa sana, kama miezi miwili iliyopita nilipomuona binti mmoja wa Kikenya akiitangazia dunia kwamba Olduvai Gorge iko Kenya na kwamba sasa dunia iende ikaangalie unyayo wa mtu wa kale kabisa duniani ambao unapatikana Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, Serikali ilichukua jukumu la kukemea na wale wakakanusha. Lakini kusema kweli tayari damage iliyofanyika kwa yale maelezo ya yule binti ni kubwa sana hayawezi kukanushwa tu kirahisi rahisi kama vile na ikaweza kuleta impact kwa uchumi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali ichukue juhudi za makusudi za kuhakikisha vivutio vyetu vinatangazwa na TANAPA, TTB pamoja na Ngorongoro. Bila kufanya hivyo wenzetu wataendelea kuchukua advantage ya sisi kukaa kimya na tutaendelea kupata shida ya kutopata mapato stahiki kutokana na vivutio ambavyo Mungu ametujalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa TDL. Ninazo taarifa kama Mwenyekiti wa Kamati ni-declare interest kwamba kuna three percent ya gross ambayo inatakiwa iende kuimarisha Chuo Cha Utalii, iimarishe TTB na shughuli za ku-promote utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mashaka kama hiyo pesa kweli inafika, naomba sana hili lifuailiwe ili TTB ipate nguvu, lakini na Chuo chetu cha Utalii ambacho kwa hapa Afrika ya Mashariki ni chuo cha kipekee sana kiweze kupata facilities za kuwafanya vijana wetu waweze kujifunza utalii, na ajira nyingi kwenye hoteli zetu zichukuliwe na Watanzania badala ya kuchukuliwa na watu kutoka nchi jirani zinazotuzunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nizungumzie Chuo cha Misitu cha Olumotonyi. Wakati tunafanya ziara ya kamati tulizungukia chuo kile, kila hali mbaya sana. Tunaiomba sana Serikali, ukitaka kupata faida lazima uwekeze. Huwezi kutegemea kuvuna kama hujalima na kupanda. Kinachoonekana sasa hivi Serikali inataka ivune mahala ambapo haikupanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Misitu ni chuo muhimu sana kwa maendeleo ya Tanzania, ni chuo cha kipekee kwa Afrika Mashariki na Kati kinachofundisha watu uhifadhi wa misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana kipewe kipaumbele, kiwezeshwe fedha, kiongezewe bajeti ili kiweze kutufundishia vijana wetu tuweze kupata tija kutokana na chuo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote nianze kumshukuru Mungu kwa nafasi hii, lakini vile vile niendelee kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Muhambwe kwa kunituma kuja kuwatumikia kama Mbunge wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitamani sana nizungumze kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Pamoja na mambo mazuri yaliyoongelewa kwenye hotuba yake, lakini nina ushauri mdogo sana ambao ningependa niutoe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la Private Public Partnership (PPP); nitaongelea hasa kwa Jiji la Dar es Salaam kama ushauri. Naamini Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi itaupokea. Kuna suala la ujenzi wa kipande cha barabara kutoka Dar es Salaam mpaka Chalinze, sina tatizo na hiyo; na kuna kipande cha barabara kutoka Oysterbay ambacho kitakwenda mpaka Ocean Road. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri mdogo tu kwa Serikali yangu kuhusu kipande cha barabara ya kutoka Oysterbay mpaka Ocean Road. Ni kweli kwamba kile kipande kinajengwa kwa ajili ya kusaidia kupunguza foleni katika Jiji la Dar es Salaam, lakini kwa maamuzi ya Serikali ya
kuhamisha Makao Makuu kuja Dodoma, naona uwezekano wa foleni hasa kipande cha kutoka maeneo ya Bunju mpaka Mjini ikiwa inapungua. Nilikuwa Dar es Salaam juzi nimeona kabisa kwamba foleni inapungua na hapa wamehama wafanyakazi wachache sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini watakapohama kabisa, kile kipande cha barabara kutoka Oysterbay kwenda Ocean Road ambacho kikimalizika itatakiwa watu wawe wanalipia ili kufika mjini, kinaweza kukosa pesa ya kurudisha kwa ajili ya kuwalipa wale private na hivyo tukaiingiza Serikali kwenye gharama ya kulipia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba kama kuna uwezekano, kama hatujafika mbali sana kwenye hatua hiyo, basi Serikali iangalie namna ya kuzitoa hizo pesa zije huku Dodoma zijenge miundombinu tutanue mji wetu ambao hakika sasa hivi tunaanza kuiona foleni hapa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ushauri huo, niingie kwenye hotuba ya TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utawala Bora. Kwanza nawashukuru sana Ofisi ya TAMISEMI; Mheshimiwa Waziri Simbachawene na Msaidizi wake Mheshimiwa Jaffo kwa kazi nzuri sana wanayoifanya.
Wamekwishatembelea sana sehemu mbalimbali za nchi yetu na kwangu Wilaya ya Kibondo wameshafika. Nashukuru sana kwa shughuli mbalimbali wanazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea sana Kituo cha Afya cha Kifura katika Wilaya yangu ya Kibondo. Kituo hiki cha Afya kimesahauliwa sana kwa muda mrefu.
Miundombinu yake imekuwa chakavu, lakini hicho kituo kimezidiwa kiasi ambacho kinasababisha hata Hospitali ya Wilaya nayo izidiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke tu hii hospitali ya Wilaya ya Kibondo inatumika kama Hospitali ya Rufaa kwa Hospitali ya Kakonko kwa jirani yangu Mheshimiwa Bilago.
Wale pale hawajawa na Hospitali ya Wilaya inayoitwa Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, rufaa zao zote wanazileta Kibondo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya yangu ya Kibondo pale, kwa takwimu za mwaka 2012 ina watu 290,000. Kwa sasa hivi lazima watakuwa wameshazidi, lakini tuna Kambi ya Wakimbizi ya Nduta ambayo Hospitali yao ya Rufaa na wao ni Hospitali ya Wilaya ya Kibondo, ambayo miundombinu yake bado ni ya mwaka 1969. Naomba sana Serikali iangalie hilo iweze kupanua miundombinu katika hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile miundombinu ya maji katika Wilaya yetu ya Kibondo ambayo ni ya toka mwaka 1973, bado inaendelea kutumika mpaka sasa hivi.
Kumbuka mwaka 1973 tulikuwa na wakazi wasiozidi 64,000, sasa hivi tuna watu zaidi ya 290,000 ukiondoa watumishi wanaokuja kuhudumia wakimbizi ambao tunao wengi sana; kwa hiyo, huduma ya maji ni ya kiwango cha chini sana katika Wilaya yetu ya Kibondo. Tunaomba sana Serikali iliangalie hilo tuweze kupata miundombinu ya maji ya kuweza kutosheleza watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulijaribu kuongea hata na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani asaidie kuhusu suala la kuwabana UNHCR ambao ndio wameleta wakimbizi pale wasaidie katika suala hilo. Naamini Waziri wa Mambo ya Ndani bado analishughulikia suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe shukrani ya dhati kwa Wizara ya Afya kwa kutuletea gari moja ya kuhudumia wagonjwa (ambulance). Gari hiyo imekuwa ni ya msaada mkubwa sana kwa akinamama na watoto ambao walikuwa wanapata shida sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie kwenye suala la ahadi za Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais wakati anafanya kampeni zake, mwaka juzi, 2015 alipita pale Wilayani Kibondo akaahidi ujenzi wa kipande cha lami cha kilometa sita. Kila nikienda kule, huwa nadaiwa. Naomba sana, TAMISEMI waangalie namna ya kuweka kwenye mahesabu yao, hicho kipande cha barabara kiweze kujengwa, kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo aliwaahidi wananchi wa Wilaya ya Kibondo na Wilaya ya jirani ya Kakonko, nakumbuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine aliloliahidi Mheshimiwa Rais ambalo natamani sana lifanyiwe kazi ni suala la pensheni kwa wazee. Mheshimiwa Rais akiwa jukwaani aliahidi wazee wote ambao hata kama siyo wafanyakazi, wafugaji, wakulima, anapotimiza miaka 60
watapewa pensheni ya kila mwezi. Naomba sana hilo suala lifuatiliwe na lianze kutekelezwa. Japo nimeangalia katika bajeti sioni utaratibu wowote ambao umesababisha hili suala liweze kuwa la kutekelezeka. Naomba sana Serikali iliangalie hili suala ili tusipate shida sana na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la TASAF. Mpaka sasa hivi, katika Wilaya yangu ya Kibondo kiujumla bado naona lina utata mkubwa sana. Ni kweli kwamba kuna baadhi ya watu walipewa hizo fedha, lakini hawakuwa wanastahili; nashukuru kwamba kuna baadhi
wameondolewa; lakini utekelezaji wa suala hilo umewagusa hata wale ambao walikuwa wanahusika katika kupewa hiyo pesa ya TASAF. Wameondolewa bila utaratibu maalum. Sijajua utaratibu uliotumika kuwaondoa baadhi ya watu ambao wanastahili kabisa kuwemo katika utaratibu wa TASAF. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, Serikali iangalie tena upya wale ambao wanastahili kuwemo kwenye utaratibu wa kulipwa na TASAF, waendelee kulipwa bila kubaguliwa na wale ambao hawastahili waondolewe kweli. Natamani sana watumike viongozi wa Serikali za Vijiji, lakini
huu utaratibu naona TASAF kwenye Ofisi za Wilaya kule wanaamua wenyewe wanavyotaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kidogo kuhusu suala la usambazaji umeme kwenye taasisi za umma. Tunashukuru sana Serikali kwamba imekuja na REA awamu ya tatu, tunaamini watasambaza umeme katika vijiji vyote. Utaratibu wa REA, wanapitia kwenye barabara kuu na kwamba watakwenda kushoto na kulia kilometa isiyozidi moja na nusu kusambaza umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muktadha huo, umeme unapita karibu na shule au zahanati, sijaona kama Wilaya zile ambazo kipato chake ni kidogo, zimesaidiwaje kuhakikisha kwamba shule za sekondari, msingi na zahanati zinaingiziwa umeme kwenye Taasisi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali ihakikishe kwamba shule za sekondari hasa zile za kata zinaingiziwa umeme ili kutupunguzia mzigo sisi Wawakilishi kwa kuwa tunadaiwa kila tunapokwenda, tuingize umeme na kufanya wiring moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna upungufu wa Walimu katika sekondari zetu; hilo najua limeshapigiwa kelele sana na Waheshimiwa Wabunge, naamini Serikali italifanyia kazi, mimi nitaongelea sana kuhusu suala la wahudumu wa afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna changamoto kubwa sana. Nalipigia sana kelele hili kwa sababu katika Wilaya ya Kibondo kuna ongezeko la watu zaidi ya 200,000 ambao tunalazimika kuwahudumia katika suala la…
NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya miundombinu. Kwanza nachukua nafasi hii kuwashukuru sana Wajumbe wote wa Kamati ya Miundombinu kwa taarifa yao nzuri kabisa ambayo imetupa mwongozo kama Serikali katika kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Wajumbe wote kwa ushauri mbalimbali ambao mmeendelea kutupatia ambao umetuimarisha katika kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda wenyewe siyo rafiki sana, nitajikita moja kwa moja kwenye suala la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege. Tulipata maelekezo na ushauri mzuri sana kutoka kwa Kamati kuhusu namna ya kuweka mipaka kwenye viwanja vyetu ambavyo kwa kweli vinavamiwa. Nakiri ukweli kwamba viwanja vyetu vingi sana vinavamiwa na Watanzania aidha, kwa kujua au wakati mwingine kwa kutojua. Tumeendelea kuwasiliana na mamlaka zinazohusika kuhakikisha kwamba viwanja vyetu vinabaki salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwashauri Watanzania, kabla hawajafanya maendelezo ya sehemu yoyote waliyopata nafasi ya kiwanja karibu na Taasisi za Kiserikali ni vizuri sana wakawasiliana na mamlaka zinazohusika kabla ya kuweka maendelezo ya kudumu. Kwa upande wetu Serikali, sasa hivi tunajiandaa na tunatengeneza Kitengo maalum cha Real Estate kwa mamlaka ya viwanja vya ndege ambacho kitafanya kazi ya kufuatilia viwanja vyetu vyote kubaini mipaka yetu yote na kufuatilia kupata hati. Kwa sababu bila kutengeneza Kitengo hicho cha Real Estate tutapata matatizo kidogo katika kufuatilia hizo hati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo kuhusu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Nashukuru sana kwa pongezi ambazo Kamati wametupatia, tunazipokea kama Serikali na tunakiri kwamba TCRA kwa kweli inafanya kazi nzuri sana kuhakikisha kwamba ina-regulate masuala ya mawasiliano hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuishauri TCRA na tunaielekeza kabisa kwamba wale wamiliki wa ving’amuzi binafsi ambao wanatakiwa watoe channel za bure kwa Watanzania watekeleze. Kama hawatatekeleza kwa wakati unaotakiwa, basi TCRA ijipange kuwachukulia hatua stahiki ili Watanzania waendelee kupata huduma za free chanel kama leseni ya wale watoa huduma inavyowataka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita vilevile kwa suala la TTCL. Kwanza nitoe shukrani za dhati kwa ushauri wa kuimarisha TTCL ambao umetolewa na Kamati. Tunawashukuru kwanza kwa hatua mliyoichukua ya kui- support Serikali katika uanzishaji wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL). Tunawashukuru kwa jinsi ambavyo mmeendelea kuipigania iweze kuwa imara. Huo ni moyo wa kizalendo ambao kwa kweli sisi Serikali tunaunga mkono; na tunaishukuru sana Kamati kwa jinsi ambavyo mnaipambania TTCL.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi TTCL inatengeneza muundo wa shirika. Baada ya hapo shirika limeshafunguliwa kama Shirika la Umma. Hivi sasa inaendelea na shughuli za kimkakati. Kwa mfano, sasa hivi ninayo furaha kueleza Bunge lako Tukufu kwamba kuna mkakati ambao TTCL unaendelea nao wakishirikiana na TANROAD wa kuhakikisha mizani yote Tanzania inawekewa vifaa maalum au inaunganishwa na mkongo wa Taifa kuhakikisha kwamba malipo yote yanayofanyika magari yote yanayopita yanaonekana kuanzia Makao Makuu ya TANROAD na hata Wizarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi huu tunategemea kutekeleza kwa awamu mbili. Awamu ya Kwanza tumeanza na Vituo 19. Mpaka sasa hivi ninapoongea Vituo 14 vimeshaunganishwa na mkongo wa Taifa, ambapo kila gari inayopita inaonekana lakini ina uzito unaoongezeka unaonekana. Kwa maana hiyo, hata charge wanayochangiwa kikawaida inaonekana moja kwa moja kwenye mitandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea kwa kutekeleza mradi huu, mapato ya Serikali hayatapotea, lakini ile human intervention tutaipunguza kwa kiwango kikubwa sana. Kwa sababu ni kweli kwamba kupitia kwenye mizani Serikali tumekuwa tukipoteza mapato. Njia rahisi kabisa ambayo tumeona ni ya kutufaa ni kuanzisha hii system ambapo TTCL wameonesha uwezo mkubwa sana katika kuitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mfumo huu utaweza ku-share na mifumo mingine ya TANROADS ambapo ni mifumo kama ya fedha, mifumo ya emails, hata rasilmali watu. Kati ya vituo hivyo tunaamini kabisa tutakapoingia awamu ya pili tutatekeleza na vituo vingine vitakavyofuata ili kuhakikisha kwamba mapato yote ya Serikali hayapotei kupitia mizani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri pamoja na wasaidizi wake wote. Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mbalimbali iliyoelekezwa sana kwenye Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la SGR liliongelewa sana, napenda tu kutoa taarifa kwamba mpaka sasa hivi kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro tumekwishafikia asilimia 48. Kazi kubwa ya kujenga tuta kuanzia Dar es Salaam mpaka Morogoro imekamilika kwa asilimia 98. Imebakia kulaza reli na kuweka miundombinu ya umeme kusubiri uanzaji wa safari ambapo mwezi Novemba tuna hakika safari za kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa njia ya SGR zitakuwa zimeanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba transfer of knowledge tunaifanya kwa umakini wa hali ya juu sana. Kuna vijana wetu wengi sana ambao tumewa-attach kwenye mradi mzima lakini kuna wengine ambao tunawapeleka nje ya nchi kuwasomesha kwa awamu. Kwa hiyo, watakapoondoka hawa wakandarasi tutakuwa na timu nzuri kabisa ya kuweza kuendeleza mradi wetu kwa mapana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi waliongelea sana kuhusu meli kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika. Nitoe tu taarifa kwamba tayari tumekwishasaini mkataba wa kutengeneza meli moja Ziwa Victoria lakini tunakarabati meli ya MV Victoria na MV Butiama kwenye Ziwa Victoria. Vilevile tumeshaingia mkataba wa kutengeneza meli moja mpya kwenye Ziwa Tanganyika pamoja na kukarabati MV Liemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi walizotupatia kwa uanzaji na kuimarisha Shirika letu la Ndege la ATCL. Michango yao mingi tumeipokea na tumeendelea kurekebisha hata ratiba ambapo sasa tunaweza ku-move sehemu mbalimbali kurahisisha usafiri wa Watanzania.

Sasa hivi kwa Dodoma siku nne tunasafiri asubuhi na jioni na tunaendelea kuimarisha na tutakwenda na ratiba nyingine mpya huku tukiendelea kukaribisha hata wawekezaji wengine kwa ajili ya kurahisisha usafiri wa anga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imeendelea kuimarisha viwanja vyetu vya ndege sehemu mbalimbali. Mpaka sasa kuna viwanja 11 ambavyo wakandarasi wako katika hatua mbalimbali ya kuvipanua kwa ajili ya kuweza kuhudumia ndege zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kuelezea masuala ya mawasiliano, Serikali yetu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeendelea kupeleka mawasiliano maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Mpaka sasa hivi nchi yetu tunawasiliana kwa asilimia 94 na hizo asilimia 6 zilizobakia tunaendelea kuzifanyia kazi kwa sababu nyingine ziko kwenye maeneo ambayo jiografia yake ni ngumu kidogo kupeleka mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, barabara za Mikoa zinaendelea kuunganishwa. Tunaamini hivi karibuni nchi yetu mikoa yote itakuwa imeshaunganishwa kwa lami, hasa kwa ile mikoa michache iliyobakia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu. Nichukue nafasi kuwapongeza sana Kamati yetu ya miundombinu kwa taarifa yao ambayo ni nzuri sana, taarifa ambayo kwa kweli kwa ujumla ilikuwa na maelekezo mazuri sana kwa upande wetu sisi Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kwa haraka sana suala la bandari nitaongelea kidogo na TASAC lakini pia nitaongelea masuala ya usajili wa line kwa alama za vidole. Ni kweli kwamba tumeendelea kufanya maboresho ya makusudi kabisa kwenye bandari yetu ili kuongeza mzigo na kuweza kuuhudumia kama ipasavyo. Tumeendelea kufanya mchakato wa kupanua bandari kwenye gati mbalimbali lakini pia tumeagiza vifaa mbalimbali vya kufanyia kazi ya kupakua mzigo wetu ili tuweze kufanya kazi usiku na mchana pia tuweze kupakua mzigo mwingi kama inavyopaswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba changamoto za hapa na pale zipo na sisi kama Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari tumeendelea kuwasiliana na wadau mbalimbali na tumekuwa tukifanya vikao mbalimbali kuhakikisha kwamba changamoto za hapa na pale ambazo zipo zinatatuliwa kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kuhusu suala la TASAC; limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge. TASAC ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 14 ya mwaka 2017 na katika sheria hiyo kipengele cha 7(1)(a) kinairuhusu TASAC kufanya kazi ya ku-clear na ku- forward mizigo ambayo ni mahususi exclusivity mandate. Ni kweli kwamba sio kila mzigo unaweza ukawa cleared na kila mtu au kila kampuni, kuna mizigo mbalimbali ambayo kwa kweli iko kiusalama zaidi, ni lazima ichukue wajibu wake wa kulinda hiyo mzigo kuweza kuisafirisha na kuigomboa. Pia ni lazima vilevile tutengeneze mazingira ambapo meli inayokuja ni lazima tujue imeleta mzigo gani kutoka huko ilikotoka na umefikaje hapa ili tuweze kutengeneza utaratibu wa kupeleka maelezo kwa taasisi zinazohusika na bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni lazima vilevile tutengeneze mazingira ambapo meli inayokuja ni lazima tujue imeleta mzigo gani kutoka huko ilikofika na umefikaje hapa, ili tuweze kutengeneza utaratibu wa kupeleka maelezo kwa taasisi zinazohusika na bandari. Hatuna nia mbaya na wala wale ma-shipping agency hatujawazuwia wanaendelea kufanya kazi zao kama kawaida, hata wale ma-clearing and forwarding wanaendelea kufanya kazi zao kama kawaida na shughuli bandarini zinzendelea kama kawaida. TASAC haijaja kuuwa sekta binafsi isipokuwa imekuja kuimarisha sekta binafsi, lakini pia kulinda rasilimali za Serikali ambazo ni muhimu zilindwe na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwa harakaharaka suala la mawasiliano. Ni kweli kwamba, kuanzia tarehe 01Mei, 2019 Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano tulikubaliana kwamba, Watanzania sasa waanze kutumia line zao za simu kwa kusajili kwa alama ya kidole kupitia kitambulisho cha Taifa cha NIDA. Na kwa kweli, mpaka sasa hivi ninapoongea na Bunge lako Tukufu line milioni 31 kati ya line milioni 43 tayari zimekwishasajiliwa kwa alama za vidole kwa kutumia vitambulisho vya NIDA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia line ambazo tayari tumekwishazizima mpaka sasa hivi ni line 6,211,000 na tunaendelea kuzima kwa awamu. Awamu inayofuata wiki ijayo kuanzia Jumatatu ni kuzima line milioni 12 ambazo Watanzania walionazo bado hawajasajili kwa alama za vidole. Tunafanya hivyo kwa lengo zuri la kuhakikisha kwamba, tunawalinda watumiaji wa mawasiliano wawe salama wanapofanya mawasiliano yao au wanapofanya transactions mbalimbali kupitia mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshtushwa kidogo na maelezo yaliyotolewa na Mbunge mmojawapo wa Mtwara hapo kwamba, yeye ameibiwa kupitia Kampuni ya Simu ya Vodacom:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maelezo kidogo; tunapotumia hizi simu janja za sasa hivi kuna vitu mbalimbali ambavyo vinatusaidia na vinatuletea manufaa katika kutumia hizo simu janja. Watu wanajifunza, watu wanapakuwa document mbalimbali, sasa unapofanya transactions hizo ujue kwamba, kama umeishiwa bundle halafu hujatoka kwenye download hicho kitu unapoweka bundle upya lazima litaendelea kuliwa. Wakati mwingine watu wanapata changamoto kutokana na hivyo, lakini watu wenye zile simu za kawaida walio wengi hatujawahi kusikia changamoto kama hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba sana Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla unapotumia simu janja na unaweka bundle likiisha uhakikishe vile vitu ambavyo umeshaanza ku-download unaviondoa kwenye mfumo wa kuwa-downloaded, ili unapoweka bundle lingine lisiishe kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunashukuru sana… ahsante sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Engineer Nditiye.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwepo kwenye Bunge letu Tukufu. Pia nawashukuru wapiga kura wa Jimbo la Muhambwe kwa kuniwezesha kurudi kwa mara ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye kitu kimoja tu ambacho napenda nikichangie kama kuisaidia Serikali yetu katika kuinua kipato. Hivi karibuni kwenye hotuba hii ambayo mimi binafsi naiona ni nzuri sana, kumekuwa na maelezo mengi sana ya Waheshimiwa Wajumbe na Wabunge kwa ujumla ya kuelezea jinsi ambavyo hawaridhiki na fedha iliyotengwa kwa ajili ya TARURA na wakawa wanapendekeza kwamba sasa tuangalie uwezekano wa kuhakikisha kwamba tutachukua pesa kutoka TANROADS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe ushauri. Kwanza kabisa, hakuna kosa kubwa tutakalofanya kama tutakapojaribu kuondoa hiki kidogo ambacho wanacho TANROADS kwa njia yoyote ile. Isipokuwa kitu ambacho tunaweza kufanya ni kuhakikisha tunatafuta vyanzo vizuri na sahihi kwa ajili ya TARURA. Tunajua umuhimu wa TARURA kwa barabara zetu kuanzia vijijini mpaka barabara kuu na tunajua jinsi ambavyo wana-struggle, ukweli ni kwamba bajeti yao huwa ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nije tu na mpango na niutoe kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha auangalie kama utaweza kufaa. Mwaka 2020 kwenye kipindi kama hiki niliweza kuhudhuria kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti na nikaitoa kama proposal, ni jinsi gani tunaweza tukatumia sekta ya mawasiliano kuhakikisha kwamba tunapata fedha za kutosha kwa ajili ya kuwasaidia TARURA kuweza kufanya shughuli zao kwa ajili ya wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hicho ambacho bado nasimamia kwenye wazo langu hilo, tuliwapendekezea watu wa Wizara ya Fedha kwamba tuongee na makampuni ya simu, tuweke tozo kidogo kabisa ambayo itawezesha TARURA kupata fedha. Tukawapa pendekezo; na nitaomba mnisikilize kwa makini, tuliwaelekeza tukawaambia bwana, tukiweka senti 25 kwa kila megabyte moja; sasa hivi Watanzania waliosajiliwa kwa kutumia line za simu wako milioni 50; na kati ya watu milioni 50, watu milioni 24 imesomeka kwamba wanatumia mitandao ya internet kwa njia mbalimbali na shughuli mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema tuchukue tu sample ya watu milioni 10, tusichukue yote milioni 24, tuchukue watu milioni 10 ambao wanatumia internet, nikasema tuweke tozo ya senti 25, isifike hata shilingi moja, tuweke senti 25 kwa kila megabyte moja. Nikasema kwamba kwa gigabyte moja ambayo ni megabyte 1,000, tukiweka hapo kwa senti 25, tutakuwa tumechangia Serikali shilingi 250 kwa gigabyte moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilienda mbali zaidi na nitaleta hiki kitu kwa maandishi kwa sababu najua itaisaidia Serikali. Kwanza kabisa, niwahakikishie Serikali, tusiwe waoga, hayo makampuni ya simu yamekuwa na ushirikiano mzuri sana na Serikali na yamekuwa yanachangia sana kwenye Serikali na hawawezi ku-complain. Isitoshe hakuna bei elekezi ya mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine katika kutoa huduma kwa wateja wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitumia watu milioni 10 ambapo kila mmoja anatoa shilingi 250, let’s say kwa wiki moja, tuchukulie tu kwamba kwa wiki moja mtu atatumia gigabyte moja, tutakuwa tumetengeneza shilingi bilioni 2.5. Uki-manipulate hiyo hesabu kwa muda wa mwezi ni shilingi bilioni 10 na kwa mwaka mzima ni shilingi bilioni 120 kwa bajeti ya shilingi bilioni 273 ya TARURA tutakuwa tumewaongezea kiasi cha pesa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Sawa. Mheshimiwa kengele imegonga lakini tufafanulie jambo moja. Hiyo senti 25 inalipa kampuni kwa ile gigabyte iliyoniuzia mimi au unapendekeza nikatwe mimi halafu kampuni ya simu ikusaidie kukusanya?

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza mteja ndiyo akatwe senti 25 kwa megabyte moja halafu zile kampuni wazipeleke Serikalini kama fedha ya Serikali. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya, ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, MAWASILIANO NA UCHUKUZI (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa
Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada wetu huu muhimu sana, lakini namshukuru vilevile Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri sana ambayo wameendelea kuifanya.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii vilevile kuishukuru Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya Profesa Norman Sigalla King kwa ushauri mzuri sana waliokuwa wametupa na ushirikiano mzuri kabisa waliotupatia wakati wote tulipokuwa kwenye mchakato wa kuandaa na kusogeza Muswada huu mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii vilevile kuwashukuru sana Wabunge wote wa Bunge lako Tukufu, zaidi kipekee nitoe shukurani zangu za dhati kwa wale wote ambao wamechangia katika Muswada wetu huu. Michango yote ni mizuri, naamini imetolewa kwa lengo zuri kabisa la kutunga sheria ambayo itasababisha Wakala wa Meli ufanye kazi nzuri kwa ajili ya manufaa ya nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna suala ambalo lilijitokeza kwa baadhi ya wachangiaji walitaka kujua mifano tuliyochukua katika kuanzisha hili Shirika la NASACO. Ni kweli kwamba walitaka kujua tumechukua mfano kutoka kwenye nchi gani? Walifikia mpaka mahali wakasema kwamba tulitakiwa tufikirie kwa nchi kama Marekani wanafanyaje, Uingereza wanafanyaje, lakini wakaja wakasema Kenya wanafanyaje; Beilla, Msumbiji wanafanyaje. Ni kweli kwamba tulitoa majibu yetu kama Serikali na bado tunaendelea kusisitiza kwamba practice ambayo inatumika Marekani na practice ambayo inatumika nchi za ulaya kwa ujumla wake kwa kiasi kikubwa sana ni tofauti sana na jinsi tunavyoweza kufanya hapa Tanzania kwa mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Spika, nchi kama Marekani iko very well centralized kwa system zao za computerization, kila kitu kinachofanyika kinajulikana wakati huohuo, hata ukiingia kwenye nchi hizo ile ukiingia tu zile registration zinakufanya ujulikane hata unakokwenda kulala na kuishi kwa hizo system zao zile zinawasababisha watu wanapofanya shughuli za bandarini kila kitu wanachogusa kionekane kwenye system na kodi stahiki ni lazima ilipwe kwa wakati muafaka. Sisi kwetu system hiyo bado haijafika japo lengo la Serikali ni kufika huko.

Mheshimiwa Spika, kwa nchi kama Kenya niliambie Bunge lako Tukufu kwamba siku ya Jumapili iliyopita huu Muswada wameshaanza kwenda kwenye mchakato kama sisi tunavyoupitisha na wao wamekiri kabisa kwamba kuna mapato yanapotea kwenye tasnia ya bandari na mambo ya maritime na kwamba wameona na wanafikiri kuja
kujifunza kutoka kwetu kama tutaridhia Muswada huu upite. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Muswada huu ukipita tutafanya udhibiti mkubwa sana, hatutategemea tena kwamba mwenye meli awe ndio wakala wa kuhudumia meli yake. Kwa kufanya hivyo tutaamini kabisa kwamba tutaongeza hata ajira kwa Watanzania ambao tumewalenga katika kuhakikisha kwamba wanaanzisha hizo wakala za kuhudumia meli.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala lingine la kilichoiua NASACO na kwa nini tumeanzisha kitu kama NASACO. Labda nirudi kidogo kwenye historia, mnamo mwaka 1999 tuliamua kubinafsisha hii sekta ya huduma za bandari kupitia NASACO. Shirika lile tuliligawa katika division nne, tukaliingiza kwenye ushindani na sekta binafsi. Wakati tunafanya hivyo tukiri kwamba hatukuweka kanuni za kutosha za kuwadhibiti wenye meli ambao matokeo yake waliamua kuanzisha wakala wa kuhudumia meli zao. Mwisho wa siku NASACO na division zake zote nne zilikosa kazi ya kufanya kwamba hazikuwa na meli za kupakua au kupakia mizigo na kusafirisha, kwa hiyo, zikafa. Hilo ni suala ambalo lililosababisha NASACO ikafa.

Mheshimiwa Spika, la pili, wale Wakala binafsi walio wengi lobbying zao ni tofauti kabisa na lobbying za mashirika ya umma. Shirika la umma linapofanya lobbying kuna system zake za Kiserikali na wala halitakiwi kwanza hata hivyo kufanya lobbying, lakini wale wenzetu watu binafsi huwezi kushindana nao, wale kuna namna wanakwenda kuongea na wateja tofauti na taasisi za Serikali zinavyokwenda kuongea na wateja. Matokeo yake wale wateja mara nyingi wanawapa kipaumbele hizi sekta binafsi. Hiyo ilkuwa ni sababu nyingine ya pili ya kusababisha mashirika yalioanzishwa kutoka kwenye NASACO yashindwe kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini hili la sasa hivi tumeliweka katika hali ambayo itaweza kuisaidia nchi yetu kiuchumi lakini zaidi kiusalama. Tunahitaji sana nchi yetu ifaidike na shughuli na rasilimali mbalimbali ambazo zinafanyika kwenye nchi yetu, huduma ya bandari ni huduma nyeti sana ambayo inahudumia asilimia 95% ya mizigo yote inayotoka nje ya nchi kwa maana ya biashara. Tunahitaji tulianzishe shirika letu hili ili liweze kudhibiti na kusogeza huduma zaidi kwa wananchi. Hata hivyo, hiki sio kitu cha kwanza kufanya shughuli ya regulation at the sametime wanafanya shughuli za operation, mfano mzuri ni VETA.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi sana wanafahamu kuhusu VETA, wale ni regulator, VETA ndio wanaotoa leseni au vyeti kwenye VETA ndogondogo za watu binafsi na hata zile za Serikali, lakini VETA haohao wanafanya shughuli ya kufundisha mafunzo ya ufundi lakini wanaosimamia hata wale ambao wanatoa mafunzo ya ufundi kwa maana ya kuwapa mitihani na kuwasimamia na kutoa vyeti. Kwa hiyo, hii NASACO haitakuwa kitu cha kwanza kufanya kazi za regulation at the sametime kufanya kazi za operation. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunategemea shirika letu hili litakuwa linapokea nyaraka, linazichakata lenyewe kisha wanawapatia mawakala kwa ajili ya ku-clear mizigo. Hakutakuwa na ucheleweshaji kwa sababu shughuli zote tunategemea zitafanyika electronically na tumejipanga kuhakikisha kwamba hakutakuwa na urasimu wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi kwa kumalizia kuendelea kutoa shukrani za dhati kwa ushirikiano mkubwa sana tuliopata kutoka kwa Wabunge. Kuna wengine ambao kwa kweli walikuwa wanakuja kutupa ushauri hata nje ya muda ambao tuko hapa Bungeni. Tuliendelea kushukuru sana kwa sababu inaonesha kwamba Wabunge walio wengi wanaridhika na uanzishwaji wa Muswada huu. Wabunge walio wengi wanakubaliana kabisa kwamba ni lazima tudhibiti hii sekta ya maritime kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE - NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama kwa mara nyingine mbele yenu kwa ajili ya kuchangia hoja yetu hii ya Shirika la Mawasiliano Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nianze kwa kuwashauri Waheshimiwa Wabunge wenzangu, hakuna mahali hata sehemu moja ambako Serikali imezuia au inawatisha wawekezaji kutoka sekta binafsi kuja kuwekeza katika sekta hii maalum kabisa ya mawasiliano. Kumekuwa na maelezo mengi sana kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na hasa wa upande wa pili kwamba kitendo kinachofanywa na Serikali kinakusudia kuwatisha wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mashirika, tunazo hizi sekta binafsi, kampuni ambazo zinaendesha huduma za mawasiliano kama Tigo, Vodacom na Halotel, tunafanya nazo kazi vizuri kabisa na tunazipatia ushirikiano wa kutosha na bado tunaendelea kuwashawishi na kuwakaribisha sana wawekezaji wengine waje kuwekeza kwenye sekta hii ya mawasiliano kwa sababu nafasi zipo na uwanja mpana upo kwa ajili ya kuwekeza. Hatuwezi kumtisha mtu na hatuna nia hiyo wala hatutakuja kuwa na nia hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri hawa wenzetu wanapokuwa wanasifia Mataifa mengine wajue kwamba nchi kama Marekani wana shirika imara kabisa la simu linaitwa AT&T. Hilo ni mali ya Serikali asilimia 100 na linaendeshwa na Serikali na ndilo linalofanya kazi nzuri sana kwenye soko la mawasiliano katika nchi ya Marekani. Hiyo ni nchi ambayo mara zote wanafanya mfano wake; lakini vile vile tuna British Telecommunication inamilikiwa kwa asilimia 100 na inafanya kazi nzuri sana katika sekta ya mawasiliano ya simu kwenye nchi ya Uingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Serikali tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaliwezesha shirika letu hili jipya la simu kwa kila hatua kuhakikisha kwamba linakamata soko na hao wengine waje washindane wala sisi hatuwezi kuwazuia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Waheshimiwa Wabunge kadhaa ambao walizungumzia kuhusu gharama za mitandao ya simu na hasa za kwenda nje. Nieleze tu ukweli Waheshimiwa Wabunge lazima wafikirie na wakubaliane na sisi, kwamba miaka 10 iliyopita gharama za simu hazikuwa hivyo. Nashukuru Mungu kwamba kuna Mbunge mmojawapo ameeleza kabisa kwamba Shirika la Simu lilivyokuwepo kipindi hicho yeye hakuwepo, kwa hiyo hajui lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimfahamishe tu na nimpe faida kidogo, kwamba wakati hizi huduma za simu zinaanza tulianza na shirika linaitwa Tritel, wakati ule ukipiga unachajiwa na ukipigiwa unachajiwa; na kwa kuwa haukuwepo siwezi kukulaumu. Naomba akamuulize hata kaka yake, baba yake mdogo na vitu kama hivyo atamweleza kwamba hizo huduma zilikuwa ghali sana tofauti na sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutahakikisha kwamba huduma zinaendelea kuwa nafuu kwa sababu kutokana na competition iliyopo, mashirika yenyewe na hizi kampuni binafsi zina-regulate bei zao kuvutia watumiaji. Vile vile kuwepo kwa mkongo wa Taifa kutalisaidia Shirika letu la TTCL kuhakikisha kwamba linakuwa na gharama nafuu sana kwenye ushindani uliopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu waliuliza sana kwamba kwa nini Kampuni ya TTCL tumeifuta na kwa nini tunaleta hii mpya. Naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wezangu; miaka ya mwanzoni ya 1990 wakati tunafanya ubinafsishaji, wakati wa wimbi la ubinafsishaji tulibinafsisha mashirika mengi sana na moja kati ya vitu tulivyofanya kosa tukabinafsisha ni Benki yetu ya NBC. Ninyi ni mashahidi, wachache mlikuwepo, wengine najua hamkuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ile benki yetu ambayo ilikuwa imara kabisa tulilazimishwa kwa ulaghai ambao ninyi wengine mnauunga mkono, kwamba tuigawe kwenye taasisi tatu na matokeo yake tumeendelea kuyumba sana. Kwa sababu hiyo, sasa hivi Serikali imejipanga kutokurudia makosa hayo. Ni lazima wanaotaka kuja kushindana kwenye sekta mbalimbali waje wakiwa wamejipanga, wakute kwamba sisi tuko imara na tunaendesha shughuli zetu bila kuwategemea wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili Shirika la Mawasiliano (TTCL), tumelianzisha kwa sababu lililokuwepo lilikuwa limeanza kufanya vibaya baada ya kuamini kwamba tukichanganya na sekta binafsi mambo yanaweza yakaenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze tu Waheshimiwa Wabunge; ni lazima wakubaliane na Muswada wetu kwa sababu hatimaye Shirika letu hili la Mawasiliano litawatumikia wananchi wa Tanzania na ni mali ya wananchi wa Tanzania. Linafanya kazi kwa ajili ya wananchi wa Tanzania wote. Pia ni shirika ambalo linatulinda kiusalama na mwisho wa siku faida itakayopatikana itaingizwa katika Hazina Kuu ya Serikali kwa ajili ya kugawiwa tujengewe barabara, hospitali na zahanati ambazo Waheshimiwa Wabunge wote tunahitaji kwenye majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliomba sana TTCL ijiorodheshe kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (The Dar es Salaam Stock Exchange Market). Kama nilivyozungumza hapo awali, hili shirika ni mali ya Serikali, Shirika hili la Mawasiliano Tanzania lipo kwa ajili ya Watanzania, ni kwa maslahi mapana ya nchi, hatutegemei kulipeleka kwenye soko la hisa kwa muda huu kwa sababu tunategemea lilinde maslahi mazima ya nchi kiuchumi, kiusalama na kijamii. Kwa hiyo tunategemea kuendelea kulilinda kwa hali yoyote ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema hapo awali, tutaendelea kuliwezesha na tutaendelea kuhakikisha kwamba linapata management stahiki bila kujali mapendekezo mengi ambayo yanakuja kinyume na Muswada tuliouleta. Kwa sababu shirika hili likiyumba ni sisi Waheshimiwa Wabunge tutaingia huku tena kuanza kulaumu. Sisi tumepanga majukumu ya watendaji wa shirika hili, tumepanga kwa kuangalia maslahi ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kabisa kwamba kuna suala zima la experience ya atakayeliongoza shirika. Hili suala limejikita zaidi kwenye kanuni za mashirika ya umma. Kwenye taratibu za ajira kwa mashirika ya umma kuna vigezo ambavyo vinazingatiwa, na kigezo kimojawapo cha kuwa mtendaji mkuu wa shirika ni lazima uwe na experience ya kutosha kwenye tasnia hiyo au zinazofanana na hiyo. Naisi tumezingatia hilo katika kuhakikisha kwamba shirika letu linapata uongozi ulio imara, uongozi bora ambao utatusogeza mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na ndugu yangu Mheshimiwa Anthony Mavunde kwamba pamoja na mipango mbalimbali ya Serikali ya Mkoa wa Dodoma kuhakikisha barabara zinapitika lakini Wizara yangu kupitia bajeti ya Serikali Kuu iliyopitishwa mwezi wa Sita, vilevile tuna mipango yetu ya kuhakikisha kwamba barabara nyingi sana, zile za inner and outer ring roads zinarekebishwa. Natoa shukrani za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge hasa wale wote ambao walisema ndiyo kwa bajeti ya Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge ambao kwa kweli kwa wingi wao wote, karibu wote hawana doubt wala kipingamizi na Makao Makuu kuhamishiwa hapa kwamba sisi kama Serikali kwa upande wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano tumejipanga vizuri sana kuhakikisha kwamba barabara zetu zote zitakuwa imara na zinapitika wakati wote katika Jiji letu hili la Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuwatoa hofu hasa Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa kutoka maeneo ya Zanzibar kwamba Wizara yangu kupitia Sekta ya Uchukuzi tumeendelea kufanya utaratibu wa kuhakikisha kwamba Shirika letu la Ndege sasa linakuwa na safari za mara kwa mara kutoka Zanzibar kupitia Dar es Salaam mpaka Dodoma na maeneo mengine tena ya nchi kuhakikisha kwamba mji wetu unafikika kwa urahisi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunapozungumza, kuna taratibu za mwisho mwisho kabisa zinaendelea kukamilishwa na Shirika letu la Ndege kuhakikisha kwamba kwa kuanzia mwisho wa mwezi huu kutakuwa na safari ya kutoka Zanzibar kupitia Dar es Salaam mpaka Dodoma. Ndege hiyo itaungana na ndege nyingine ambayo itakuwa iko Dar es Salaam kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma siku za Jumatatu asubuhi. Hata hivyo, Ijumaa jioni pia tunaendelea kufanya utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na ndege mbili ambazo zitakuwa zinatoka Dodoma kwenda Dar es Salaam mpaka Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala lililoongelewa na ndugu yangu Mbunge wa Bahi ambaye alizungumzia uboreshaji wa uwanja wetu huu uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie pamoja na Wabunge wenzangu kwamba uwanja wetu huu uliopo mpaka sasa hivi kuna shilingi bilioni 3,700 ambazo Serikali kupitia TAA wametoa kwa ajili ya kulipa fidia tuweze kupanua uwanja wetu kwa mita 150 zaidi ili huo uwanja sasa uweze kutumika masaa 24. Kabla ya wiki mbili tuna hakika hizo pesa zitakuwa zimelipwa kwa wananchi ili angalau waweze kupisha upanuzi wa uwanja huo tuweze kuruka masaa 24. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ili niokoe muda, tayari taratibu mbalimbali za ujenzi wa uwanja mpya wa Msalato zimeanza. Marejeo ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tayari yamekamilika kwa asilimia mia moja na sasa hivi kinachomalizika ni michoro, lakini tuna uhakika wa kupata fedha kwa sababu tupo kwenye mazungumzo ya mwisho kabisa na African Development Bank kwa ajili ya mkopo rahisi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini baada ya hapo tutapata huo mkopo na tutatangaza tenda kwa ajili ya kupata Wakandarasi makini na wazuri ambao watatujengea uwanja mkubwa na wa kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nichangie hayo kuhusu upande wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa niweke wazi naunga mkono Miswada yote miwili na nampongeza sana Mwenyekiti wa Kamati yetu na Kamati nzima ya Miundombinu kwa ushirikiano mkubwa sana waliotupatia. Ninayo machache tu sana yatakayohusu sana Sheria hii ya TMA, ambayo imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge. Nitaongea kwa ufupi sana suala la kwa nini tunataka mtu mwenye PhD ndiyo awe ni Mtendaji wa Mamlaka. Ni takwa la Shirika la Duniani la Metrological (WMO), kuwataka Watendaji wote wa nchi mbalimbali ambazo ni wanachama wa WMO wawe na elimu ya kutosha kwa ngazi ya PhD. Bahati nzuri mpaka sasa tunapokwenda kuibadilisha hii Sheria hata Mtendaji wetu wa TMA ana elimu ya PhD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri vilevile hata kwenye mamlaka hii ambayo tunakwenda kuifanyia kazi TMA tunao graduate watu ambao wana PhD kama 15 na kuna sera nzuri sana ya mamlaka ya kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanapelekwa kuongeza elimu kuweza kupata elimu ya kutosha kuhakikisha kwamba tunakuwa na Wataalam wabobevu wengi zaidi kwenye Mamlaka yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea tena kwa kidogo sana kuhusu suala zima la experience. Hatuna shida sana na experience ya miaka hata mitatu, lakini hii ni Taasisi kubwa sana ambayo inashughulika na maisha ya watu na vitu, sisi kama Serikali mwanzo tulipeleka miaka ndiyo ile experience ya mtu kuweza kukamata nafasi ya kuwa Managing Director. Hata hivyo, tukasikiliza maoni na ushauri wa Kamati ambao wao walitaka miaka mitano, lakini mwisho wa siku tulikubaliana kwamba tuweke angalau miaka nane, kwa sababu mtu mwenye PhD mwenye uzoefu wa miaka mitano bado hajawa na uzoefu wa kutosha sana kwa mujibu wa standard za WMO kuweza kukamata nafasi kama hiyo. Tunakubaliana kabisa kwamba mtu hata wa miaka mitatu ana uzoefu mzuri na degree yake hata degree ya pili ana uzoefu mzuri; lakini tunafuata takwa mahususi la WMO katika kuendesha hizi Taasisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la fidia, nashukuru hata Mwenyekiti wa Kamati amekubaliana kwamba Serikali tuliliona na tukakubaliana kwamba utungaji wa sheria kama hizi huwa unaenda sambamba na sheria zingine. Katika kutekeleza majukumu haya tunakwenda sambamba na Sheria ya Ardhi namba (4) ambayo itakuwa inatu-guide katika kufanya mambo hayo. Hatuwezi kufanya bila kushirikisha sheria nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Mheshimiwa Ramo kuhusu suala zima la utaalam kuzingatiwa. Haya ni masuala ambayo yanagusa sana maisha ya watu, hatuwezi tukakubaliana mtu yeyote azungumze lolote wakati wowote na masuala wa waganga kama Serikali hatuwezi kuyazingatia sisi tunakwenda kwa masuala ya kisayansi. Tunakumbuka na tunajua si ajabu kuna baadhi ya maeneo mtu anaweza akasema leo mvua itanyesha, labda ikanyesha kwa bahati, lakini siyo vitu vya uhakika. Sisi katika Sheria hii tunataka mamlaka ndiyo iwe mdhibiti wa kuhakikisha kwamba kinachozungumzwa ndiyo kinachukuliwa na wananchi wote na hatuzungumzi bila kuwasiliana na dunia inavyotaka, ndiyo maana kila baada ya dakika 15 sheria inataka tutoe taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya wananchi kuweza kujua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo, nashukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini wa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa niweke wazi naunga mkono Miswada yote miwili na nampongeza sana Mwenyekiti wa Kamati yetu na Kamati nzima ya Miundombinu kwa ushirikiano mkubwa sana waliotupatia. Ninayo machache tu sana yatakayohusu sana Sheria hii ya TMA, ambayo imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge. Nitaongea kwa ufupi sana suala la kwa nini tunataka mtu mwenye PhD ndiyo awe ni Mtendaji wa Mamlaka. Ni takwa la Shirika la Duniani la Metrological (WMO), kuwataka Watendaji wote wa nchi mbalimbali ambazo ni wanachama wa WMO wawe na elimu ya kutosha kwa ngazi ya PhD. Bahati nzuri mpaka sasa tunapokwenda kuibadilisha hii Sheria hata Mtendaji wetu wa TMA ana elimu ya PhD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri vilevile hata kwenye mamlaka hii ambayo tunakwenda kuifanyia kazi TMA tunao graduate watu ambao wana PhD kama 15 na kuna sera nzuri sana ya mamlaka ya kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanapelekwa kuongeza elimu kuweza kupata elimu ya kutosha kuhakikisha kwamba tunakuwa na Wataalam wabobevu wengi zaidi kwenye Mamlaka yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea tena kwa kidogo sana kuhusu suala zima la experience. Hatuna shida sana na experience ya miaka hata mitatu, lakini hii ni Taasisi kubwa sana ambayo inashughulika na maisha ya watu na vitu, sisi kama Serikali mwanzo tulipeleka miaka ndiyo ile experience ya mtu kuweza kukamata nafasi ya kuwa Managing Director. Hata hivyo, tukasikiliza maoni na ushauri wa Kamati ambao wao walitaka miaka mitano, lakini mwisho wa siku tulikubaliana kwamba tuweke angalau miaka nane, kwa sababu mtu mwenye PhD mwenye uzoefu wa miaka mitano bado hajawa na uzoefu wa kutosha sana kwa mujibu wa standard za WMO kuweza kukamata nafasi kama hiyo. Tunakubaliana kabisa kwamba mtu hata wa miaka mitatu ana uzoefu mzuri na degree yake hata degree ya pili ana uzoefu mzuri; lakini tunafuata takwa mahususi la WMO katika kuendesha hizi Taasisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la fidia, nashukuru hata Mwenyekiti wa Kamati amekubaliana kwamba Serikali tuliliona na tukakubaliana kwamba utungaji wa sheria kama hizi huwa unaenda sambamba na sheria zingine. Katika kutekeleza majukumu haya tunakwenda sambamba na Sheria ya Ardhi namba (4) ambayo itakuwa inatu-guide katika kufanya mambo hayo. Hatuwezi kufanya bila kushirikisha sheria nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Mheshimiwa Ramo kuhusu suala zima la utaalam kuzingatiwa. Haya ni masuala ambayo yanagusa sana maisha ya watu, hatuwezi tukakubaliana mtu yeyote azungumze lolote wakati wowote na masuala wa waganga kama Serikali hatuwezi kuyazingatia sisi tunakwenda kwa masuala ya kisayansi. Tunakumbuka na tunajua si ajabu kuna baadhi ya maeneo mtu anaweza akasema leo mvua itanyesha, labda ikanyesha kwa bahati, lakini siyo vitu vya uhakika. Sisi katika Sheria hii tunataka mamlaka ndiyo iwe mdhibiti wa kuhakikisha kwamba kinachozungumzwa ndiyo kinachukuliwa na wananchi wote na hatuzungumzi bila kuwasiliana na dunia inavyotaka, ndiyo maana kila baada ya dakika 15 sheria inataka tutoe taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya wananchi kuweza kujua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo, nashukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)