Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye (169 total)

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniamsha mara ya pili. Swali langu la nyongeza, je, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha kwamba huduma hii haijurudii baada ya kupata usafiri endelevu, ili kadhia hii isiweze kujirudia tena? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali inafanya miradi mitatu ya kuhakikisha kwamba meli tatu katika Ziwa Victoria zinafanya kazi kwa pamoja. Kwa hiyo, tuna uhakika kabisa kwamba hata itakapotokea meli moja imepata hitilafu kutakuwa na meli mbili ambazo zinaendelea kufanya kazi kwa pamoja. Ahsante.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba wananchi hawa watabomolewa nyumba zao na Serikali haitalipa fidia na tafsiri yake ni kwamba wananchi hawa wamevunja sheria.
Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Oktoba, 2017 Rais alipokuwa Mwanza, alizuia wananchi wa Mwanza kubomolewa makazi yao. Je, kauli hii ililenga Ukanda wa Mwanza peke yake au ni Tanzania nzima? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, imekuwa ni kawaida kwa Serikali hii ya CCM kuendelea kupeleka huduma za kijamii katika maeneo hayo ambayo wananchi wanabomolewa ikiwepo kata ya Tambukareli, Msasani pamoja na Ilemo, huduma za maji, umeme pamoja na vituo vya kupigia kura lakini leo hii mnakwenda kuwabomolea. Je, ni kwa nini Serikali haina mkakati wa kuhakikisha sasa inazuia huduma hizo katika maeneo hayo kwa sababu hayajapimwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, wakati mwingine ni lazima Waheshimiwa Wabunge tushirikiane na Serikali na tufuatilie taarifa rasmi zinazotolewa na Serikali. Mheshimiwa Rais kauli yake haikumaanisha waliovamia hifadhi ya reli.

Mheshimiwa Spika, wale ambao wamevamia hifadhi nya reli ambapo vipimo vyake vipo kabla ya mwaka 1904 wataondolewa bila kulipwa fidia yoyote na wale ambao reli itawafuata kwenye maeneo yao utaratibu wa fidia unaendelea kupangwa na watalipwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linauliza kuhusu huduma zinazoendelea kupelekwa. Kiukweli ni kwamba sehemu nyingi sana ambazo ni maeneo ya hifadhi ya reli baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu wameendelea kuwapimia viwanja wananchi. Wale tulikwishaongea na kwamba Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na TAMISEMI watawachukuliwa hatua watumishi wasiokuwa waaminifu lakini bado nina hakika wananchi walikuwa wanajua kwamba wanapimiwa maeneo ambayo si sahihi kwao kwenda kujenga kwa sababu yanaeleweka wazi.
Mheshimiwa Spika, labda nitoe mfano kidogo, maeneo yaliyopita umeme mkubwa wa Gridi ya Taifa yako wazi na wananchi hawaendi kujenga kule, lakini wao hawalalamikiwi isipokuwa sehemu ya reli ambayo ni muhimu sana kwa Taifa letu watu wanaivamia na hawaulizwi. Kwa hiyo, ukweli kwamba huduma zilizopelekwa zitaondolewa uko palepale kwa sababu hata waliojenga mabondeni nao huduma zinaondolewa ili kupisha huduma za kijamii, ahsante.
MHE. KEPT. ABBAS ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa makampuni yanayotengeneza aina hizo za ndege yamesitisha utengenezaji, sasa je, Serikali haioni itakumbwa na changamoto za upatikanaji wa vipuri? Hilo ni swali la kwanza.
Swali la pili, je, lini hasa uboreshaji wa karakana hiyo utaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Abbas Ali Mwinyi kwa uzalendo wake mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba viongozi wetu wa kitaifa wanasafiri katika hali ya usalama mkubwa. Vilevile nikusifu kwa kutumia utaalamu wako mzuri kama rubani mzoefu wa kuhakikisha kwamba ndege zetu zinakuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Abbas kwa kuwa ni kweli kwamba Serikali inafahamu hilo; lakini nimhakikishie kwamba vipuri hivyo bado vinatengenezwa na kampuni hiyo hiyo ya Uholanzi ambayo ndiyo mtengenezaji mkubwa wa ndege za Fokker ambako vipuri hivyo vinapatikana kwenye unit yao iliyopo nchini Malyasia.
Mheshimiwa Spika, vilevile huko nchini Malyasia ambako ndiko vipuri vinapotengenezwa kuna unit yao ya mafunzo (training center) ambako wanafanya re-validation ya licence na kwa ndege hizo marubani wetu wote huwa wanakwenda kule kwa ajili ya ku-review leseni zao. Nimhakikishie Mheshimiwa Abbas kwamba vipuri vipo vinapatikana kwenye unit yao hiyo na tutaendelea kuvitumia na tunaendelea kuwasiliana kwa ajili ya matengenezo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ni kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi. Mara TGFA watakapotuletea makadirio basi Serikali itatenga pesa kwa ajili ya matengenezo ya hanga hilo la ndege, ahsante sana.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Bado niko kwenye aircraft, kwenye tiketi za ATCL kuna picha ya ndege aina ya Embraer ambayo inabeba abiria 105 ambayo kimsingi bado haipo nchini, lakini kwenye tiketi za ATCL wameweka picha ambayo inaonekana kama ndege ipo na ukinunua ile tiketi unaweza ukafikiri kwamba unaenda kupanda aircraft hiyo ya abiria 105 lakini ukienda kule unakuta na bombardier ya abiria 70.
Sasa kwa nini Serikali inafanya udanganyifu? Haihofii kwamba iko siku atatoka mtu mwenye upeo wake akaenda pale akakuta anapandishwa ndege ambayo haipo picha kwenye tiketi alafu aka-sue ndege ikakamatwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwenye tiketi alizozizungumza hiyo picha bado ipo, lakini yale ni matoleo ya tu ya kawaida ambayo kikawaida kibiashara hayawezi kuathiri kabisa shughuli za utaratibu wa biashara ya usafishaji wa abiria kwa njia ya ndege. Hata hivyo, tutaliangalia na kuangalia namna ya kuweza kulirekebisha katika muda mfupi ujao. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kwa kuwa Serikai imesema kwamba inafanya tathmini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ili kuingiza Vijiji vya Mhezi, Msindo, Mshewa, Vuudee, Tae, Gavao na Saweni lakini mara nyingi imejitokeza kwamba mfuko huu hauna fedha za kutosha kutekeleza miradi. Je, Serikali iko tayari kutafuta namna nyingine ili kuwezesha vijiji hivi vipate mawasiliano? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tatizo la Same Magharibi linafanana kwa kiasi fulani na maeneo kadhaa ya Jimbo la Mafinga Mjini hasa katika Vijiji vya Kisada, Ulole, Bumilayinga na Maduma. Je, Serikali iko tayari kutia msisitizo ili Kampuni ya Viettel ambayo wanaendesha mtandao wa Halotel wakafunge mitambo ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kupata mawasiliano ya uhakika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba vijiji vingi sana bado vinahitaji huduma ya mawasiliano. Takwimu zilizopo ni kwamba tuna jumla ya kata 3,381 na kati ya hizo ni kata 443 ambazo tayari zimekwishafikiwa na mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu unaofanywa kupitia Mfuko wa Mawasiliano ni kuangalia asilimia ngapi eneo husika halina huduma ya mawasiliano kwa kutumia prediction map kutoka makampuni ya simu ambayo yanatoa huduma za mawasiliano. Nimepokea maombi mengi sana kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge mbalimbali ambao wamepita pale ofisini kwa ajili ya kutaka huduma za mawasiliano zifike kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitambue kupokea maombi kutoka kwa Mheshimiwa Cosato Chumi ambaye alifika sana ofisini kwangu, Mheshimiwa Edwin Sannda, Mheshimiwa Venance Mwamoto wa Kilolo, Mheshimiwa Deo Ngalawa na Mheshimiwa Mwakibete wa Busokelo. Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha kwamba huduma ya mawasiliano inafika kwenye sehemu zote ambazo zinahitaji huduma ya mawasiliano kwa sababu sasa hivi mawasiliano ni nyenzo muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa ajili ya usalama wa nchi kwa kawaida viwanja vya ndege vinatakiwa viendeshwe na Agency za Serikali ambazo ni TCAA na TAA pamoja na Taasisi ya Meteorological . Taasisi hii ya KADCO ni kampuni, sasa swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, Kampuni ya KADCO itaunganishwaje na TAA kama alivyoeleza kwenye majibu yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini ndege za Bombardier zitashuka Wilayani Mpanda, Mkoani Katavi maana tunazihitaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, katika jibu langu la msingi nimeeleza tu kwamba, KADCO ni Shirika la Umma ambalo linamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo, siyo kitu cha ajabu kuunganisha KADCO na TAA kwa sababu zote zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, zote ni taasisi za Serikali na zikiunganishwa tutapata uongozi wa aina moja na bodi ya aina moja ambayo itarahisisha sana menejimenti ya viwanja vya ndege kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, tuko kwenye harakati za kupanua uwanja wa ndege wa eneo hilo. Kwa hiyo, tutakapopanua uwanja wa ndege wa eneo hilo Mheshimiwa Mbunge, ndege za Bombardier zitaanza kushuka. Tuna lengo la kuhakikisha kwamba viwanja vyetu vyote vya ndege vinaongezwa ubora wake na ukubwa ili ndege zote ambazo zina ukubwa wa kutosha ziweze kutua kwa ajili ya kuhudumia Watanzania. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kati ya mambo yanayosababisha Uwanja wa Ndege wa Mpanda usifanye kazi ni kutokuwepo kwa huduma ya zimamoto. Ni lini Serikali itatusaidia kuhakikisha huduma ya zimamoto inakuwepo kwenye Uwanja huo wa Mpanda?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza nampongeza sana wewe na Wabunge wenzako wote wa Mpanda kwa jinsi mnavyoshughulikia masuala ya huduma za usafiri wa anga kwa ajili ya mkoa wenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, sasa hivi gari linalotoa huduma ya zimamoto kwenye uwanja ule limepata hitilafu na Serikali kupitia TAA tunaendelea kushughulikia kuhakikisha kwamba, uwanja ule unapata hiyo huduma ya zimamoto na hivi karibuni tumeendelea kuwasiliana na watu wa kule Mpanda ili walete makadirio yatakayowezesha hiyo huduma irudi katika hali yake ya kawaida.
MHE. JAKU HASHIM AYUBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza mnyonge mnyongeni, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kitendo alichoonyesha asubuhi hii leo cha uungwana na ungwana ni vitendo. Nikupongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa masikitiko makubwa, tena makubwa, tena makubwa kwa mara ya tatu. Wizara yake anayoiongoza Mheshimiwa Waziri imekuwa ikiwaonea wananchi wa Zanzibar, Unguja na Pemba. Nipo tayari kumthibitishia hilo kwani mafuta yanayouzwa Zanzibar sasa hivi ni ghali kuliko hapa Dar es Salaam. Nimwombe tu kwa unyenyekevu, ni lini atakaa na watu wa upande wa Zanzibar kutatua tatizo hili? Kama anavyojua mafuta ni nguzo muhimu. Mafuta Zanzibar yanauzwa ghali, kodi zimekuwa nyingi na amekiri, nimpongeze kuwa Zanzibar wamechaji Dola 10, wakaiacha Rwanda Dola tatu, Zambia Dola tatu Burundi Dola tatu, kwa nini wanaionea Zanzibar kwa Dola 10? Mawaziri wengi husema Muungano huu wetu …
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima ujenge hoja kwanza. Bila kujenga hoja hawezi kuja kufahamu Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri, nimwombe ni lini atakaa na upande wa Zanzibar maana kuna barua mpaka leo Katibu wake Mkuu hajawajibu Wazanzibari, je, kalamu ya kuandikia hana au anaandika spelling moja moja? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni uonevu, mafuta Zanzibar yanauzwa ghali, sisi tunaumia. Mafuta ni nguzo muhimu …
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana. Kwanza nikiri kweli kwamba kuna changamoto katika hizi tozo ambazo zinatozwa na bandari, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Jaku kwamba tupo tayari kama Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi ya Zanzibar lakini vilevile na Mamlaka ya Mapato kukaa na kuangalia hizi tozo ambazo ni kero sana kwa wananchi wetu wa Tanzania, tuweze kuzitatua kwa pamoja. Katika hilo, nitamkaribisha Mheshimiwa Jaku tukae pamoja tulijadili kwa kina tuliondoe tatizo hilo ambalo linasumbua wananchi kwa njia moja au nyingine. Hili linatatulika kwa mustakabali wa nchi yetu ya Tanzania. Ahsante.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Hata hivyo ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mheshimiwa Waziri kujibu swali hili na kunihakikishia/kukiri kwamba yapo baadhi ya maeneo Kisiwani Pemba ambayo yanapata shida ya mawasiliano, hata hivyo ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo la mawasiliano Kisiwani Pemba katika maeneo ya Makangale, Kipange, Tumbe Kiungoni, Mtambwe, Gando na maeneo mengine yaliyopo Kaskazini na Kusini Pemba na kupelekea wananchi wa mikoa hiyo kupata usumbufu wa mawasiliano hasa katika kipindi cha dharura…
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali kupitia Wizara hii inawaambia nini tena wananchi kuhusu kutatua changamoto hii ambayo imekuwa ikiwaletea shida muda mrefu na wakati mwingine wananchi hulazima kupanda kwenye miti mirefu kutafuta mawasiliano? (Makofi)
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuongozana na wataalamu wake kwenda Pemba kutafuta maeneo na vijiji mbalimbali kuweka minara ili kuwatatulia matatizo wananchi wa Pemba? (Makofi
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi nimeeleza kwamba kuna uwezekano pamoja na Kata nyingi nilizozitaja kwamba zina mawasiliano, kuna sehemu nyingine baadhi ya vijiji havina mawasiliano kutokana na jiografia ya Pemba ikiwemo Matangale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge aniorodheshee majina ya vijiji vyote ambavyo mpaka sasa hivi havipati mawasiliano ili tuwatume watu wetu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote watembelee sehemu ile ili kuweza kuleta mawasiliano kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lengo la Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ya nchi yetu wananchi wanawasiliana. Napenda nichukue nafasi hii kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba mpaka sasa hivi kwa takwimu tulizonazo kutoka Mfuko wa Mawasiliano wa Wote Watanzania asilimia 94 wanawasiliana. Kwa hiyo, asilimia sita iliyobakia inawezekana ni baadhi ya vijiji ambavyo amezungumza Mheshimiwa Mbunge; na ninamkaribisha Ofisini aje atuletee majina ya vijiji ambavyo hawawasiliani ili tuweze kutatua changamoto hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kwa ruhusa yako, mimi niko tayari kuongozana naye mpaka Pemba ili tuweze kwenda kuangalia hizo sehemu ambazo zina changamoto. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nipate kuuliza swali la nyongeza.
Matatizo ya mawasiliano katika Halimashauri ya Wilaya ya Liwale na Wilaya nzima ile ni makubwa sana na ujio wa Kampuni ya Halotel pamoja na TTCL tuliona kwamba inaweza kuwa kama mkombozi kwa ajili ya mawasiliano katika Halmashauri ile. Kwa bahati mbaya zaidi, miradi ambayo ilikuwa tayari wananchi wametoa maeneo yao kwa ajili ya kujenga minara katika Kata za Mirui, Ngongowele, Mpigamiti, Mkutano, Ndapata na Igombe na Mtunguni miradi ile yote imesimama hatuwaoni tena wale Halotel…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli ya Serikali juu ya kukwama kwa miradi hii katika hizo Kata nilizozitaja?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna baadhi ya sehemu ambazo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na watoa huduma za mawasiliano wameendelea kupata changamoto mbalimbali katika kutekeleza miradi ya kuweka mawasiliano kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumeendelea kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali katika sehemu mbalimbali kuhakikisha kwamba mawasiliano yanawafikia wananchi kwa wakati. Kwa hiyo, namwakikishia Mheshimiwa Kuchauka kwamba hiyo miradi ambayo imekwama tunaifahamu na tunaifuatilia tutahakikisha kabla ya mwisho wa mwezi wa Juni, 2018 tutawatembelea sehemu hizo ili watu waweze kuwasiliana. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mawasiliano katika Kisiwa cha Pemba ni sawa kabisa na Wilaya ya Kilindi, baadhi ya maeneo hayana mawasiliano kabisa. Nini kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu wananchi wa Kata ya Saunyi, Kata ya Loane na baadhi ya maeneo ya Kata ya Kimbya ambao hawana mawasiliano kabisa katika Wilaya yangu ya Kilindi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejikita kupeleka mawasiliano sehemu zote ambazo hazina mawasiliano kabisa. Tunapata changamoto kwa baadhi ya vijiji ambavyo vina mawasiliano, lakini wananchi wanataka kutafuta mawasiliano ya ziada. Katika maeneo hayo, mipango ipo, lakini siyo ya haraka.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mgumba nafahamu kwenye Kata ya pili uliyoitaja baada ya Saunyi, kuna mawasiliano ya aina moja na wananchi wanataka mawasiliano ya aina nyingine. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuwasiliana na watoa huduma za mawasiliano, watakapoona kuna faida kwao, watapeleka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumejikita kupeleka vile vijiji ambavyo wale watoa huduma lazima tuwashawishi kupeleka huduma za mawasiliano. Sile sehemu ambazo hakuna mawasiliano kabisa, hizo ndiyo tumejikita kama Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wa eneo hilo, wanawasiliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndani ya vijiji hivi ambavyo nimevitaja, kama sehemu mojawapo ambako vinasomeka, tutahakikisha tunapeleka mawasiliano ili wananchi wa Tanzania wote wawasiliane.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kabla sijauliza swali langu la nyongeza kwanza niipongeze timu yangu ya Coastal Union ya Tanga ambayo imepanda daraja mwaka huu, lakini pia niwapongeze timu ya African Sports kwa kubakia katika ligi daraja la kwanza. Maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo:- (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia ukarabati unaofanywa na ambao ulishawahi kufanywa uwanja wa ndege wa Tanga, katika eneo la Magomeni kuna nyumba zaidi ya 228 ambazo zilifanyiwa evaluation mwaka 2008 lakini mpaka leo hawajalipwa. Lakini pia kuna nyumba nyingine 802 ambazo nazo zinahitajiwa kuvunjwa ili kupanua uwanja ule wa ndege.
Sasa je, nataka kujua, Serikali ni lini itawalipa Wananchi wale fidia ili kuweza kufanya ukarabati huu mkubwa unaotakiwa kufanywa kufuatia ufadhili wa Benki ya Dunia?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, kwa kuwa Jiji la Tanga sasa hivi route za ndege zimeongezeka na kuna shughuli nyingi za mipango ya kiuchumi amabzo zinafanyika. Je, ni lini Bombadier itaanza kwenda Tanga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba zote ambazo zilifanyiwa evaluation kwa ajili ya malipo ya fidia, shughuli za fidia zinafanyika na evaluation imekwishafanyika na tunafahamu idadi ya pesa zinazodaiwa lakini tuko kwemnye uhakiki kupitia Wizara ya Fedha ya kulipa fidia hiyo, kwa hiyo, wakati Wizara ya Fedha itakapomaliza kupitia fidia hiyo, malipo yatafanyika kwa watu ambao wataathirika na upanuzi wa uwanja wa ndege huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Bombadier itaanza lini safari za kwenda Tanga, kiutaratibu Bombadier wanafanya biashara pamoja na kutoa huduma kama mashirika mengine ya ndege kwa hiyo, hilo tutalichukua, tutawapelekea ATCL basi waje wafanye tathmini ya masuala ya soko, usalama na mambo mengine ambayo yanahusika kabla ya kupeleka ndege kufanya shughuli za safari za uwanja huo wa Tanga, ahsante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Kata ya Makole, Manispaa ya Dodoma walisitishiwa uendelezaji wa nyumba zao kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege ulioko hapa wakati huo kuna wananchi wa Kata ya Msalato 89 wanaidai Serikali tangu mwaka 2005.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kujua wananchi wa Msalato watalipwa lini lakini pili wananchi wa Makole waliositishiwa uendelezaji wa nyumba zao…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwepo na upanuzi wa uwanja wa ndege au tutautumia sasa hivi hapa Dodoma na wananchi wa Makole madai yao ya fidia yanashughulikiwa kupitia Wizara ya Fedha na sasa hivi Wizara ya Fedha wako kwenye uhakiki wa kuhakikisha kwamba wanalipa hayo madai yao wakati watakapomaliza uhakiki.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nilitaka nimuulize Mheshimiwa Waziri kutokana na tamko lake la juzi, Jimbo la Segerea katika Kata ya Kipawa kuna wananchi 1,800 wanasubiri malipo tangu mwaka 1992 na juzi alisema kwamba waondoke. Sasa nilitaka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini sasa atawafanyia malipo yao watu wa Kata ya Kipawa, Mtaa wa Kipunguni na wanahusika vipi kuondoka kabla hawajalipwa malipo yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna wananchi wanatakiwa wapishe eneo la uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere International Airport ambao walivamia miaka ya nyuma, lakini Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kwamba walipwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya hao kuna wananchi 59 ambao tayari wamekwishapokea malipo yao kwa ajili ya kupisha upanuzi wa uwanja huo. Tunaowazungumza na ambao nilitoa agizo waondoke ni hao wananchi 59 na bado naendelea kusisitiza kwamba hao wananchi 59 ambao tayari wamekwishakupokea malipo yao ya fidia, wanatakiwa waondoke wapishe upanuzi wa uwanja wetu wa ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikiri kwamba kuna baadhi ya wananchi ambao hawajalipwa kwa sababu mbalimbali, kuna baadhi walifungua kesi na kuna wengine ambao hawajafungua kesi lakini hawakuridhika na fidia, hao bado tunaendelea kutafuta utaratibu mwingine wa kuwashawishi kwa njia moja au nyingine ili waweze kupisha upanuzi wa uwanja huo wa ndege.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mkoa wa Mara una shughuli nyingi sana ambazo zingeweza kuliongezea Taifa letu uchumi kwa maana ya utalii, tuna Ziwa Victoria lakini pia makumbusho ya Baba wa Taifa. Katika majibu yake Naibu Waziri ametueleza kwamba wamefanya usanifu pia kwenye uwanja wa ndege wa Musoma, ningependa kujua uwanja wa ndege wa Musoma na wenyewe upo kati ya viwanja vilivyopewa priority maana yake umetaja Tanga tu kama ndiyo umepewa kipaumbele na unaanza kukarabatiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Kwenye jibu langu la msingi wakati najibu kuhusu uwanja wa ndege wa Tanga nilieleza viwanja 11 ambavyo vimeshafanyiwa Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na uwanja wa Musoma ukiwemo. Ni kweli kwamba viwanja vyote vimepewa kipaumbele kinacholingana na pesa itakapopatikana kama nilivyoeleza tutafuta mkopo kutoka Benki ya Dunia, pesa itakapopatikana basi viwanja vyote vitapewa kipaumbele kujengwa kwa sababu tunahitaji viwanka vyote vya Mikao viwe na kiwango kizuri ambacho ndege yoyote inaweza ikashuka, ahsante.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri, lakini pamoja na majibu hayo mazuri naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Buigiri ni eneo linalojulikana kwamba kuna Shule ya Watoto Wasiona kabisa na wengine wana uono hafifu. Je, Serikali haioni kwamba kuna kila sababu ya kulishughulikia suala hili la usalama barabarani katika eneo la Buigiri kwa umuhimu na haraka ili kuondokana na tatizo la ajali pale Buigiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna kituo kwa ajili ya wasioona sehemu za Buigiri kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge. Kiutaratibu tunategemea sehemu zenye mahitaji maalum kama hayo kuwe na watu ambao wanawaongoza wanaovuka barabara ili wasiweze kupata ajali. Lakini hata hivyo, nimshauri na kumueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tutaendelea kutafuta utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba watu wenye mahitaji maalum kama hao wanapokuwa wanavuka na kutumia barabara zetu wanasaidiwa ili wasiweze kupata madhara.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsantekwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Naomba nimuulize Waziri, kwa vile imethibitika kwamba baadhi ya ajali zinazotokea barabarani au zinasababishwa na ubovu wa barabara, au zinasababishwa na ukosefu wa alama mahususi za barabarani jukumu ambalo amekebidhiwa wakala wa barabara yaani TANROADS. Je, Serikali ina mpango gani wa kuiwajibisha TANROADS pale ambapo sababu ya ajali inaonekana ni kutotekeleza wajibu wa wakala huyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna ubovu wa barabara na Serikali imekuwa ikiendelea kufanya jitihada za kurekebisha ubovu huo kuhakikisha kwamba barabara zetu kuu na barabara za mikoa zimapitika kila wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito tu kwa Watanzania wenzetu, kumetokea tabia ya hivi karibuni wananchi kuchukua hatua wenyewe ya kuweka matuta barabarani na hicho kimekuwa ni chanzo kimojawapo cha ajali mbalimbali kwa sababu wanapoweka matuta bila kuwashauri au bila kuwaambia TANROADS ina maana yale matuta yanakuwa hayana alama na magari yanapokuja yanafika, yanavamia yale matuta na kusababisha ajali. Niwashauri Watanzania, tunawaomba wasiweke matuta barabarani bila kuviambia vyombo husika vinavyohusika na barabara ili kuweka alama kuwaonyesha madereva kwamba kuna tuta mbele wanakokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge Ndugu yangu Joseph Mhagama kwamba TANROADS wanajitahidi sana kufanya kazi zao kwa uadilifu na kwa umakini wa hali ya juu kuzingatia usalama wa Watanzania. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii kuweza kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na tatizo la uwekaji kiholela wa matuta kwenye baadhi ya barabara za mitaani na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa vyombo vya moto na ikizingatiwa kwamba wananchi hawa hawana utalaam wowote. Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na kadhia hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokuwa namueleza Mheshimiwa Joseph Mhagama, ninatoa wito kwa Watanzania, barabara hizi zinajengwa kwa gharama kubwa sana ya pesa za Watanzania. Tunapoweka matuta bila vyombo vinavyohusika hasa TANROADS kufahamu tunaharibu barabara zetu ambazo tumezijenga kwa gharama kubwa sana. Kitu ambacho Serikali tunakifanya, tunapanga mkakati wa kuwasiliana na Wizara ya mambo ya ndani kitengo cha usalama barabarani kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi namna ya matumizi bora ya barabara bila kuleta ajali kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba sana Watanzania wasijichukulie maamuzi ya kuweka matuta barabarani hata kwa kugongwa kwa mbuzi tu isipokuwa wawasiliane na taasisi zinazohusika tusaidie kama kuna umuhimu wa kuweka matuta tutaweka, lakini kwa utaratibu ambao unaeleweka.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi hii kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa baadhi ya majibu yake yamekuwa mazuri, lakini katika majibu yake anasema kutokana na usafiri huu hautoshelezi, bado wananchi wetu wanapata taabu sana kupatikana usafiri huu wa kwenda Pemba. Wananchi wetu wanafika kulala bandarini kusubiri meli ya kwenda Pemba. Sasa ni kwa nini Serikali isitenge bajeti mahususi kwa ajili ya kununua meli ili iweze kufanya kazi hizi kuwahudumia wasafiri wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, bado usafiri huu ni ghali sana kwenda Zanzibar na kwingineko, sasa ni kwa nini Serikali isiingize mkono wake kuzisaidia kampuni hizi kwa wakati huu ili bei ya tiketi zishuke zisiwe hapa zilipo? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyokiri katika swali la msingi kwamba usafiri wa majini kuelekea visiwa vya Pemba na Unguja hautoshelezi. Na ndiyo maana nikatoa wito kwa wawekezaji wengine wanaoweza kutoa huduma hizo wajitokeze kwa wingi washirikiane na Serikali katika kutoa huduma hiyo. Naamini watakapofanya hivyo matatizo yatapungua kwa kuwa ni kweli kabisa tunakiri kwamba bado kuna changamoto ya usafiri wa majini kwa ajili ya kutoka Dar es Salaam au Tanga kwenda visiwa vya Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu gharama; kwanza kabisa, Serikali inazo meli mbili; kuna MV Maendeleo halafu MV Mapinduzi, zote zilinunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, lakini bahati mbaya sasa hivi zipo kwenye matengenezo na marekebisho mbalimbali. Ninaamini zitakapokuwa katika hali yake ya kawaida zitasaidia katika kutoa huduma kwa wananchi wa visiwa vya Pemba na Unguja na bei itapungua. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba bandari hii au mradi huu ni wa muhimu na utaleta nafuu kubwa sana kwa wananchi wa Kigoma, naomba Serikali iwaambie watu wa Kigoma, kwa kuwa mradi huu umeshachelewa sana, imetenga kiasi gani kwa bajeti inayokuja kwa ajili ya kuhakikisha sasa mradi huu unaanza mara moja? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kule Moshi tuna tatizo kama hili la Kigoma, tuna Stendi ya Kimataifa inapaswa kujengwa pale na Benki ya Dunia iko tayari kutoa fedha. Nataka nijue kutoka Serikalini, ni lini kibali kitatoka kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hiyo li tuweze kunufaika na huo msaada kutoka World Bank?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inayofanyika sasa hivi kama nilivyoeleza katika jibu la msingi ni kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kazi hiyo ikishakamilika wale ndiyo watatupa gharama zinazostahili kufanya kazi husika na ndipo tutakapojua tunatumia gharama gani katika ujenzi wa hiyo sehemu ambayo Mheshimiwa Mbunge anaifuatilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili kuhusu stendi, nikiri kwamba umuhimu wa kuwekwa stendi hiyo ni mkubwa sana kwa sababu ni kweli Benki ya Dunia imeonesha nia ya kufadhili. Hata hivyo, bado Serikali inaendelea na majadiliano na Benki ya Dunia kuangalia namna nzuri itakayofanya ili kuhakikisha ujenzi wa stendi hiyo unafanyika. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Swali hili lina umuhimu wa pekee kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma na napenda nimuulize swali moja dogo Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Bandari za Ujiji na Kibirizi unakwenda sambamba na ujenzi wa Bandari ya Nchi Kavu ya Katosho ambayo tayari Serikali imeshalipa fidia kwa wananchi wale. Napenda kujua, je, ujenzi wa Bandari ya Nchi Kavu ambayo tayari Serikali imeshalipa fidia wananchi wale unaanza lini maana sasa ni takribani mwaka mmoja tangu wananchi wale wamelipwa fidia? Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe shukurani za dhati kwa jinsi anavyojitahidi kupigania bandari za mkoa ambao anatokea. Ni kweli kwamba wakati huu mchakato wa usanifu wa kina na upembuzi yakinifu ukiwa unaendelea tayari Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari imekwishatangaza tenda kwa ajili ya kuanza ukarabati wa gati katika eneo la Kibirizi na Ujiji pamoja na Ofisi ya Meneja wa Mkoa wa TPA ili vyote viende sambamba kwa tenda moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Katosho nalo limeingizwa katika package ya peke yake ya kuanza kujenga sakafu kubwa ili treni inapopita pale kabla ya kufika kituo cha mwisho cha Kigoma iweze kuanza kushusha mizigo ambayo itakuwa inaweza kusafirishwa kwenye nchi jirani na maeneo ya mikoa ya jirani ikiwemo Kigoma. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Tarehe 5 Agosti, 2017 wakati Rais alipokuja kuweka jiwe la msingi la bomba la mafuta pale Chongoleani-Tanga, tarehe 6 alizundua Kiwanda kipya cha Saruji cha Kilimanjaro na alinipa nafasi ya kuongea kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimtaka Mheshimiwa Rais kupitia Serikali ya Awamu ya Tano kufanya categories za mizigo katika bandari zetu. Nataka kujua, mpango ule umeishia wapi kwa sababu Bandari ya Tanga sasa hivi inafanya kazi chini ya kiwango na hata vifaa vya kisasa vya kuteremsha makontena ya fourty feet hakuna, Waziri ananiambiaje?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, CHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Mbunge ni mfuatiliaji mzuri nadhani atakuwa shahidi kwamba sasa hivi Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari imekwishaanza marekebisho na matayarisho ya kupanua Bandari ya Tanga. Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba Bandari ile ya Tanga inakwenda sambamba na wingi wa mizigo ambayo inategemewa kuanza kupatikana kupitia ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima. Kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge asiwe na mashaka kuna utekelezaji wa upanuzi wa Bandari ya Tanga unaoendelea na wakandarasi wako pale wameshaanza kazi hiyo. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi pamoja na majibu ya kukatisha tamaa ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. (Kicheko)
Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba barabara hii ni muhimu sana katika eneo hili na ametueleza kwamba katika bajeti ya mwaka 2018/2019 wametenga kujenga kilometa tano tu katika barabara ambayo anasema ina urefu wa zaidi ya kilometa tisini na kitu.
Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba kuendelea kutenga kilometa tano zitawafanya wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini na Mkoa wa Singida na Manyara kusubiri ujenzi huu kwa zaidi ya miaka 19 ijayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii imekuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na imetusumbua sana wakati wa uchaguzi kila mara.
Je, Serikali sasa ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 15 zilizosalia katika kufika katika mji wa Ilongero ili kusudi kuwaondolea walau kuwapunguzia wananchi adha hii wanayoipata kwa sasa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara au ujenzi wowote ule unahitaji kupata pesa ya kutosha. Ninamwomba tu Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba nchi yetu ni kubwa na kila sehemu inahitaji ipate huduma kutokana na mfuko na kipato cha Serikali kilichopo na sio kwamba tuna-concentrate na barabara moja tu. Tunakiri kwamba kweli barabara ile ni muhimu lakini Tanzania ni kubwa na yote inahitaji pesa kutoka Wizara hiyo hiyo moja.
Kwa hiyo, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kupata kilometa tano ni mwanzo, lakini pesa itakapopatikana tunaweza tukajenga hata kilometa nyingi lakini angalau hizo tano zilizopatikana ni muhimu azipokee na ashukuru kwamba tunafanya jitihada kama Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni kweli barabara hii ipo kwenye ahadi na hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi barabara hii inasomeka, lakini siyo hiyo tu peke yake ni barabara ambayo inatoka kuanzia Karatu ambayo ipo Arusha, inapitia Mbulu inakuja mpaka hapo tunapopazungumza Haydom inakwenda mpaka Simiyu. Pesa zitakapopatikana na tukumbuke kwamba tuna ahadi mpaka mwaka 2020, pesa itakapopatikana hizi barabara zote zitajengwa kwa kiwango cha lami. Tuna nia nzuri kama Serikali kuhakikisha kwamba Wananchi wanapata huduma nzuri za barabara.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, wananchi wa Busekelo kwa kushirikiana na mimi nikiwa Mbunge wao tumeamua kulima barabara inayounganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa Mbeya kwa kutumia zana za jembe la mkono.
Je, ni lini Serikali itatupa support ili tuweze kukamilisha barabara hii ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Busekelo na Makete na ukizingatia kwamba…
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana kwa jinsi anavyopigania wananchi wa jimbo la Busokelo katika kuhakikisha kwamba wanapata huduma nzuri za barabara. Ni kweli nakiri kwamba nilimwona juzi kwenye vyombo vya habari akihamasisha na kufanya kazi sambamba na wananchi kuhakikisha kwamba barabara inapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii imo kwenye Ilani, Serikali inalitambua na tumeona jitihada za Mbunge na kwenye bajeti yetu ya mwaka huu imesomeka kwenye hatua za upembuzi yakinifu na details design. Kwa hiyo, tutalishughulia.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa. Na mimi nilitaka niulize kuhusu barabara ya kutoka Mtwara – Pachani - Mkongo – Gulioni – Ligera - Lusewa inaenda Magazine - Likusenguse hadi Tunduru ambayo ina urefu wa kilometa 300 iliyoahidiwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Awamu ya Nne, ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kipande hicho cha barabara kimekuwa kikisumbua kwa muda mrefu na kwa kweli tumekuwa tukipata mawasiliano mazuri sana na Mbunge akiwa anatetea kipande hicho cha barabara. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo suala tunalo na tunalifanyia kazi; tunawasiliana mara kwa mara na Meneja wa TANROADS wa Mkoa kuhakikisha kwamba inaingizwa kwenye utaratibu ambapo tutaanza kuifanyia matengenezo makubwa. Ahsante.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nichukue nafasi hii kumwuliza swali dogo Mheshimiwa Naibu Waziri; ni nini kauli ya Serikali juu ya kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Masasi - Nachingwea - Nanganga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali ni kwamba pesa inatafutwa, kwa sababu hatua za awali za ujenzi wa kipande hicho cha barabara zilishaandaliwa na zinatekelezwa. Pesa itakapopatikana, barabara hiyo itaingizwa kwenye mpango ianze kutengenezwa kwa kiwango cha lami.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya mwezi Desemba, 2017 kuhusu barabara ya Nyakahura - Murugarama ilieleza kwamba iko kwenye hatua ya mchakato wa manunuzi, ni lini sasa mchakato huo wa manunuzi utakamilika ili barabara hii yenye urefu wa kilometa 85 iweze kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya kumpata mkandarasi shughuli za ujenzi wa kipande hicho cha barabara zitaanza mara moja.
MHE. DANIEL N. NSWAZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo tu; barabara ya Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi, ni barabara ya muda mrefu sana; na kipande cha Kidahwe – Kasulu kina mkandarasi, lakini mkandarasi huyo amekuwa kazini kwa miaka kumi akijenga kilometa 50. Swali langu kwa Waziri ni kwamba ni kwa nini mkandarasi huyu halipwi madeni yake ili barabara hiyo ikamilike? Kwa nini barabara ya kilometa 50/0 aijenge kwa miaka 10 wakati hana fedha? Barabara hii mkandarasi yupo kwenye site.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kipande cha kutoka Kidahwe kuja mpaka Kasulu kina mkandarasi. Nimhakikishie Mheshimiwa Nsanzugwanko kwamba mkandarasi huyo ameshalipwa malipo yake, lakini sasa hivi kuna mvua nyingi sana zinaendelea pale Mkoani Kigoma, tena mkoa mzima na hivyo kusababisha ucheleweshaji kidogo wa kumalizia. Kuna hatua za awali ambazo zimeshaendelea na yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge anajua, kipande cha kilometa karibu 20 kitawekwa lami mara mvua zitakapopungua. Kwa sababu mambo mengine ni ya kitaalam, huwezi kuweka lami wakati kuna mvua inanyesha kila siku. Mvua za Mkoa wa Kigoma bahati nzuri anazifahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kipande cha kutoka Kibondo mpaka Nyakanazi kupitia Kakonko na kutoka Kasulu, tender itatangazwa hivi punde. Ahsante sana.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Mbozi na Wilaya ya Songwe hazijaunganishwa kwa barabara licha ya kwamba Wilaya ya Mbozi ni Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe, lakini wananchi wa kutoka Wilaya ya Songwe kwenda Makao Makuu ya Mkoa ambayo yako Mbozi wanalazimika kupita mkoa mwingine ambao ni Mkoa wa Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize sasa, ni lini barabara ya kutoka Kata ya Magamba ambayo inapitia Kata ya Magamba Wilaya ya Mbozi; na hili niliweke vizuri, Magamba hiyo inapatikana Songwe, lakini Magamba nyingine pia inapatikana Mbozi. Kuna uwezekano wa kutengeneza njia kwenda Makao Makuu ya Mkoa kutoka Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini barabara hii itatengenezwa licha ya kwamba Naibu Waziri wa Ujenzi alisema kwamba angeweza kuja Mbozi kuangalia uwezekano na hadi sasa amewadanganya wananchi wa Mbozi, hajafika. Naomba sasa jibu la Serikali.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaunga mkono kabisa mambo ambayo yanaendelea hapa Bungeni, kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge katika kuuliza maswali. Nadhani wakati mwingine ni vizuri tuwe tunawasiliana kimkoa kwanza kujua status ya mambo ambayo tunakuja kuyauliza huku Bungeni. Siyo kitu kibaya wananchi wakifahamu kwamba umekuja kuuliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba kuna taratibu za ujenzi wa barabara ambazo zinaendelea kupitia TANROADS Mkoa wa Songwe. Ninaamini kama Mbunge angewasiliana na Meneja wa TANROADS Mkoa, asingekuja kuuliza swali kama alilouliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Haonga kwamba detailed design tayari, sasa hivi tunafanya utaratibu baada ya kupitia hizo details kuanza kutafuta Mkandarasi wa kujenga hicho kipande cha barabara kutoka Mbozi kwenda Songwe. (Makofi)
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Napenda kumuuliza swali la nyongeza kwamba wakati utaratibu wa kumpata Mkandarasi wa kutengeneza uwanja huo unaendelea, kwa nini huduma ya ndege isiendelee? Maana yake hivi sasa huduma ya ndege imesitishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa nini huduma za ndege katika Uwanja wa Songea ambazo zinawasaidia wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe zisiendelee wakati Mkandarasi anaendelea kutafutwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tumesimamisha kwa muda huduma za usafiri wa ndege katika kiwanja hicho ili kupisha marekebisho yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kuongeza tabaka la lami, kwa sababu sasa hivi ndege ikitua na kuondoka inapeperusha changarawe ambapo tuna wasiwasi zinaweza zikaingia kwenye propeller zikahatarisha usalama wa abiria, lakini na ndege vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunafanya ukarabati wa uwanja kwa kuondoa mashimo ambayo yako kwenye uwanja ule ili tuepushe ajali. Hata hivyo, tunahakikisha kwamba huduma zitarudi hivi karibuni baada ya kuwasiliana na TAA kwamba wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba hizo changamoto zilizoko katika uwanja huo zinarekebishwa.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, naomba nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pamoja na hayo naomba nitumie nafasi hii kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, ni muda mrefu sasa toka fedha hii shilingi bilioni moja itengwe na barabara ambayo imetajwa imefanyiwa sehemu tu ya matengenezo naomba kupata kauli ya Serikali, hizi kilometa 12 zilizobaki ni wakati gani zitamaliziwa kwa fedha ambayo imetengwa?
Swali la pili, naomba kuuliza Serikali imekuwa na kipaumbele cha kuunganisha barabara za Mikoa kama ambavyo jibu la msingi linavyojieleza. Nini mpango wa Serikali wa kukamilisha au kuanza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Masasi kwenda Nachingwea, Nachingwea kwenda Nanganga ikiwa ni ahadi ambayo imetolewa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna kiasi cha fedha kilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii na ilikuwa ni mkakati wa Serikali kulipa madeni. Katika kipindi hiki hadi Desemba Serikali ime-clear madeni kwa makandarasi zaidi ya shilingi trilioni 1.385 kwa maana hiyo hii ni fursa inatosha sasa kuanza kuendelea kutoa sasa mikataba kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge hizi kilometa 12 zitatangazwa na kuanza kutengenezwa wakati wowote.
Mheshimiwa Spika, pia niseme tu ni mpango wa Serikali kuunganisha Mikoa kama nilivyojibu katika jibu la msingi na Mheshimiwa Mwalimu Masala unakumbuka kwamba katika mpango ambao unaendelea kwa ajili ya ujenzi wa barabara kile kipande cha Nachingwea kwenda Nanganga kilometa 46 kitatangazwa wakati wowote, kipo kipande kingine cha Nachingwea - Ruangwa kilometa 45, lakini kuna kipande cha Ruangwa - Nanganga kilometa 58. Pia unatambua kwamba kuna ujenzi wa daraja kule kwenye Mto Lukuledi hii ni dhamira ya Serikali kuweza kuunganisha maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, baada ya eneo hili kuwa limekamilishwa itakuwa ni sehemu ya kuunganisha Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Ruvuma kwa maana kuwa unatambua kwamba ukitokea Nachingwea kwenda Kilimarondo utakuwa unaelekea kule Mindu upande wa Tunduru tutakuwa tunaunganika na wenzetu wa upande wa Ruvuma. Upande wa Morogoro pia kilometa 129 ukitokea Nachingwea kuelekea Liwale naona Mheshimiwa Kuchauka ananitazama hapa ni kwamba barabara hii sasa tutakapokuja kuanza kutengeneza itakuwa ni sehemu ya barabara ya kuunganisha upande wa Lindi kuelekea Mahenge kule Morogoro.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge nikuombe tu uvute subira ni mpango mzuri wa Serikali kuhakikisha kwamba tunaweza kutengeneza barabara hizi kuunganisha Mikoa na hii itatupa fursa sasa ya kuunganisha barabara ambazo zinakwenda kwenye Wilaya. Kwa hiyo tuvute subira na wananchi wajue Serikali inafanya kazi kubwa kulipa madeni na kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza nataka niweke kumbukumbu sahihi kwamba mimi ni Mbunge wa Busokelo ambayo iko ndani ya Wilaya ya Rungwe.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba kuna sera, kuna miongozo kuna vitengo mbalimbali vya kufuatilia forensic wizi wa mitandaoni, lakini bado wizi unaendelea; Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuwatumia wataalam wetu wa ndani kushirikiana na nchi ambazo zimefanikiwa kutatua tatizo hili la wizi wa mtandaoni ikiwemo Israel ama India?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, sekta ya mawasiliano inachangia asilimia 13 ya pato la Taifa. Kwa msingi huo sekta hii ni muhimu sana, lakini Serikali bado haijaanzisha Bodi ya TEHAMA. Nchi ambazo zimefanikiwa katika TEHAMA kwa mfano Finland wamefanikiwa kugundua Nokia ukienda Korea Kusini kuna Samsung, ukienda Marekani akina Job Steve - Apple na Mataifa mengine mbalimbali. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha hii Bodi ya TEHAMA ili professionals ambao wamesoma hii TEHAMA waweze kutambulikana na kuongeza Pato la Taifa zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni kweli kwamba wizi au uhalifu wa kimatandao bado unaendelea na kwa msingi huo Serikali tumejipanga kwamba tutawashirikisha wataalam wetu wa ndani.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nitambue kwamba Mheshimiwa Mwakibete ni mtaalam sana wa mambo ya ICT na TEHAMA ambaye amefanya kazi maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi na hasa nchi za Ulaya ili kutengeneza software au programs ambazo zinaweza kupunguza au kumaliza kabisa tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa-support wataalam wetu kwenda kujifunza nje ya nchi kwa nchi ambazo zimefanikiwa tatua tatizo hili, nchi kama Israel, India na Marekani. Tutambue tu kwamba uhalifu wa mtandao ni kitu ambacho kipo dunia nzima na jinsia ambavyo siku zinakwenda watu wanagundua njia mpya na Serikali tunawa-support wananchi na wataalam mbalimbali kuhakikisha kwamba wanatafuta programs za kuzuia uhalifu huo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kweli kwamba kumekuwa na utitiri wa watu wengi sana wanaojifanya kwamba ni wataalam wa TEHAMA na kwa sasa kuna umuhimu kama Serikali wa kuunda bodi ya kusimamia wataalam wa TEHAMA.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo kupitia Kamisheni ya TEHAMA ambayo ilitangwazwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2015 tunaamini ndani yake tutaunda Bodi ambayo itawatambua wataalam wa TEHAMA kwa elimu zao, lakini tutahakikisha vilevile wanafanya mitihani ili kuwa competitive katika masuala mazima ya TEHAMA kama ilivyo Bodi ya Uhasibu NBAA au Bodi ya Wahandisi ya ERB.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza, naomba tufanye marekebisho kidogo kwenye majina ya vijiji, kijiji kinaitwa Ichemba na wala siyo Lihemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile minara hii inajengwa kwa umbali mrefu karibu kilometa 30 kwenda mnara mwingine, je, Serikali kwa kushirikiana na makampuni haya iko tayari kuongeza minara mingine katikati ili kuongeza upatikanaji wa mawasiliano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwenye jibu ametaja mchakato wa ujenzi au kutengeneza minara katika Vijiji vya Ichemba, Kanoge, Busanda na Igombemkulu utafanyika siku za usoni. Kwa Kiswahili rahisi ukisema siku za usoni maana yake haijulikani ni hata baada ya miaka 10, 15 ni siku za usoni. Je, Serikali sasa iko tayari kueleza muda maalum badala ya kutuambia habari za siku za usoni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Kadutu kwa sababu pamoja na mambo mengine tumekwishawasiliana kuhusu masuala ya mawasiliano kwenye jimbo lake na nilimweleza vizuri tu hatua mbalimbali ambazo Serikali imeendelea kuzichukua. Kawaida umbali kati ya mnara na mnara katika eneo ambalo halina milima mingi sana ni radiance ya kilometa 80.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imeendelea kuweka umbali wa radiance ya kilometa 60 kwa sababu umbali huo unarahisisha kuweka mnara mwingine umbali wa kilometa hata 60 kama hakuna milima. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Kadutu kwamba umbali wa minara kama yeye anapata kwa kilometa 30 ni kwa sababu maeneo yaliyopo yana milima milima na tutajitahidi kuangalia sehemu zote ambazo hazipati mawasiliano tusogeze minara mingine ili wananchi waweze kupatiwa mawasiliano kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini miradi kwenye vijiji vilivyotajwa pale itapatiwa mawasiliano. Kwa sasa hivi tunaorodhesha vijiji na kata mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya nchini mwetu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Hivi ninavyoongea tumepanga tufanye ratiba ndefu ya miezi miwili baada ya Bunge la Bajeti kwa ajili ya kupima kwa kutumia GPS na kuweka alama ni wapi tutaweka minara kwa ajili ya kuwezesha wananchi wa Tanzania wote waweze kupata mawasiliano.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kuna mwingiliano mkubwa wa njia za mawasiliano hasa SafariCom kwenye Jimbo la Vunjo, Rombo na maeneo yanayozunguka mipakani. Serikali ina mkakati gani, labda washauriane ili kuweza kuona mwingiliano huu unaondoka namna gani kwa sababu wewe mtumiaji unalazimika kuingia kwenye roaming bila wewe mwenyewe kutaka na inasababisha gharama kubwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli maeneo mengi sana ya nchi yetu hasa yale ya mipakani kumekuwa na mwingiliano mkubwa sana wa mawasiliano kati ya hizo nchi jirani na Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na TCRA tumeendelea kuyaainisha maeneo hayo kwa ajili ya kuongeza nguvu minara yetu na kuzuia frequency ambazo ni mtambuka kutoka nchi moja kwenda nyingine kuhakikisha tunazidhibiti ili Watanzania wapate mawasiliano ya Tanzania na nchi jirani ziendelee kupata mawasiliano kutoka nchi hizo.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Igunga kama lilivyo Jimbo la Ulyankulu, tuna kata kadhaa ambazo bado hazina mawasiliano. Kata hizo ni pamoja na Kiningila, Isakamaliwa, Mwamashiga, Mtunguru na Kata ya Mwashiku Jimbo la Manonga. Ni lini basi Serikali itasaidia ili wananchi hawa waweze kupata mawasiliano? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Dalaly kwa sababu mara nyingi sana tumekuwa tukikutana ofisini kwa ajili ya kuongelea kata zake hizo alizozitaja ambazo ni kweli hazina mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru vilevile kwamba ameshatuandikia hata kwa maandishi na hii taarifa yake tayari iko kwa watu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ambao tumekubaliana kwamba mwezi saba mpaka wa tisa tutakuwa na ziara nchi nzima kuhakikisha tunaweka mawasiliano ya eneo hilo. Namhakikishia tu Mheshimiwa Dkt. Kafumu kwamba nitakapokuwa nakwenda maeneo ya Igunga nitamtaarifu ili tuwe wote kutembelea maeneo haya. Ahsante.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza kabisa nimshukuru Naibu Waziri, Mheshimiwa Nditiye kwa kutuma wataalam wake kwenda kubaini maeneo ambayo hayana minara katika Jimbo la Lushoto. Je, ni lini sasa utekelezaji utaanza ili wananchi wa Lushoto waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwenye swali la msingi na kama nilivyoeleza kwenye maswali mengine ya nyongeza, Mheshimiwa Shekilindi kuanzia mwezi wa Saba baada ya Bunge la Bajeti nitafanya ziara ndefu sana ya kutembelea maeneo yote yenye changamoto za mawasiliano nikiambatana na timu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika nitafika jimboni kwake na pia nitafika kwa Mheshimiwa Nape naye ambaye najua kabisa anasumbuka sana kuhakikisha tu kwamba mawasiliano kwa nchi yetu yote yanapatikana bila tatizo.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Tatizo hili linafafana kabisa na tatizo la Kijiji cha Ngarasero katika Jimbo la Ngorongoro, Mkoa wa Arusha. Je, ni lini Serikali itapeleka minara katika eneo hilo ili wananchi waweze kupata mawasiliano katika Kijiji cha Ngarasero?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Ngorongoro ni moja kati ya maeneo ambayo nayo yana changamoto ya mawasiliano. Kwa baadhi ya sehemu ambazo zina changamoto, tayari tumekwishatuma watu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwenda kufanya tathmini ya mahali gani panatakiwa kwenda kuwekwa minara kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pindi watakapotuletea taarifa, tutatangaza tenda ili makampuni mbalimbali ya simu yajitokeze kwa ajili ya kujenga minara ili kutatua changamoto hiyo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyeki, ahsante kwa majibu mazuri. Nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa usumbufu umekuwepo kwa watumiaji wa hizi cable hasa hii Cable ya Dodoma, mtu ushaharibikiwa inabidi uende trip mara mbili, mara tatu kuripoti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu aliyonijibu Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba inabidi uende tena Ofisi ya Mamlaka ya Mawasiliano ukatoe ripoti, hizo ni gharama na ni usumbufu. Kwa nini Serikali isiweke kitu kama hotline ikiwa mtu unaposumbuliwa na mambo kama hayo unapiga ukapata ripoti ili kuhakikisha kwamba mtumiaji anapata haki kwa ile pesa yake aliyoitoa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyeki, swali langu lingine ni vile unavyokwenda kutaka kujiunga na hizi cable unaahidiwa utapata channel kama 200 au 300. Inapokuja kwenye hali halisi ukijaribu kutafuta channel nyingi unaambiwa access denied, sasa huu kweli si wizi wa kiwaziwazi? Je, Serikali inadhibiti vipi kuhakikisha kwamba mtumiaji anapata haki yake kwa pesa aliyoilipia? Nahisi bado Mamlaka ya Mawasiliano inatakiwa izidishe udhibiti kwenye vyombo hivi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyeki, napenda kumtaarifu tu Mheshimiwa Asha kwamba huwa zipo hotline lakini kwa kweli sasa hivi sipo nazo kichwani. Baada ya muda tukikuta tu hata pale canteen nitakuwa nimeshazipata kutoka kwa watu wa TCRA CCC na kumpatia ili kuweza kuwasiliana na watu ambao wako pale kwa ajili kuhudumia wateja.
Mheshimiwa Mwenyeki, swali lake la pili ni kuhusu channel chache kuliko zinavyopaswa, hiyo inahusika na masuala ya ving’amuzi. Nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Asha kwamba Serikali kupia TCRA tunaendelea kuwahakiki hawa wanaotoa huduma za TV. Kuna leseni mbalimbali, leseni kama DSTV wale wako wazi kabisa kwamba channel za bure ni mbili au tatu lakini kwa mfano hivi ving’amuzi vingine kama Dodoma Cable, sijapata uhakika Mheshimiwa Asha wana channel za bure ngapi na kwa zipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakapopata uhakika nitakuwa na nafasi nzuri sana ya kukujibu lakini tuna uhakika na kama Serikali tunafahamu kwamba kuna baadhi ya cables ambazo zinatakiwa zitoe channel za bure na zile ambazo hazitoi channel za bure tunazifuatilia kwa karibu ili tuweze kuzifungia kama zinakiuka masharti.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyeki, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kirefu cha LUKU ni Lipia Umeme Kadri Utumiavyo. Kwenye ving’amuzi kwa nini Serikali isikae na watoa huduma ili mtumiaji alipie kadri anavyotumia badala ya kulipia kwa mwezi awe ametumia au hajatumia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya makampuni yanayotoa huduma za cable kwa ufupi huwa yanafanya biashara na huwa yanalenga katika kupata faida. Nimhakikishie Mheshimiwa kwamba tumelipokea wazo lake hilo na tutalifanyia kazi kama Serikali tuone namna nzuri ya kulitekeleza.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia ya leo ya utandawazi mawasiliano ni uchumi, ni kilimo, ni kila kitu. Maeneo yote ambayo nimeyataja Mpanda Mlohoka, Usinga, Kombe, Shela, Mwamashimba, Ibumba, Mkuyuni na vingine vingi ni maeneo ambayo wanalima sana zao la tumbaku ambalo linaingiza kipato kikubwa. Serikali imekuwa na speed ndogo sana ya kupeleka mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu lake hapa la msingi anasema kwamba kuna baadhi ya maeneo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali, kwenye jibu la swali la msingi Mheshimiwa Waziri anasema maeneo mengine itategemea upatikanaji wa fedha, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali, kwa kuwa kuna makampuni ambayo pia yanapeleka mawasiliano maeneo ya Vijijini, wakati wanasubiri kupata fedha Serikali kwenye mpango wa Serikali wanaweza kuongea na haya makampuni ili baadhi yaanze kupeleka mawasiliano maeneo hayo kuliko kusubiri mpaka Serikali ipate fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwepo na migongano mikubwa kwenye masuala ya ulipaji wa minara ya simu kwenye maeneo mbalimbali ya vijijini, Serikali za Vijiji zikiona kwamba minara ile ni vipato kwa ajili ya Serikali lakini pia wananchi ambao wametoa yale maeneo wakiona ni haki yao wao kulipwa. Serikali inasemaje juu ya minara ambayo imewekwa vijijini ambapo imeleta migongano hawajui kwamba hela ziende wapi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Magdalena Sakaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ni taasisi ya Serikali ambayo inahusika kupeleka mawasiliano katika vijiji vyote au sehemu zote ambazo hazina mvuto wa kibiashara. Haya makampuni ya simu yanafanya biashara, ili yaweze kuweka mnara sehemu mojawapo ni lazima pawe na mvuto wa kibiashara. Kuepuka hilo, ndiyo maana Serikali ilianzisha Mfuko wa Mawasialiano kwa Wote kuhakikisha kwamba hata zile sehemu ambazo hazina mvuto wa kibiashara zinapata mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na vijiji vya Mheshimiwa Sakaya, nashukuru sana kwamba kuna barua yake ambayo imeanisha vyote hivyo na nimeshaipokea pamoja na barua za Wabunge wengine wengi tu. Namuahidi baada ya kipindi cha Bunge hili la bajeti nitafanya ziara ya mwezi mzima na wataalam wangu kutoka TCRA na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuhakikisha tunaanisha maeneo yote nchi nzima ambayo hayana mvuto wa kibiashara tutangaze tenda ili makampuni ya simu yaweze kuweka minara wananchi waweze kuwasiliana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu malipo, kwanza kabisa kuna masuala kama mawili. Suala la kwanza ni malipo kwa mtu ambaye anatoa eneo lake mnara uwekwe, mara nyingi huwa ni mapatano kati ya mwenye ardhi na makampuni ambayo yanaweka mnara. Wakati mwingine tunashauri sana vijiji ndio viwe vinatoa maeneo kwa ajili ya kuweka mnara ili kuhakikisha kwamba pesa inarudi kwa wananchi lakini inapotokea kwamba ni mtu binafsi amepata hiyo fursa hatuwezi kumuingilia sana japo tunatamani sana halmashauri iweze kuwa inaingilia. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni kama alivyosema Naibu Waziri yanafanya biashara lakini kuna maeneo ambayo yana mahitaji makubwa na biashara ipo lakini hayajawahi kupata huduma za mawasiliano kwa muda mrefu. Naomba kujua ni lini Vijiji vya Nyangere, Nyaburundu, Nyabuzume, Tiling’ati, Tingilima na Kibara Ginnery zipata mawasiliano? Kwa mfano Kibara Ginnery ina kiwanda muda mrefu lakini hakuna mawasiliano, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Getere, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Getere na nimpongeze kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana suala la mawasiliano hasa kwenye hii Kibara Ginnery. Vilevile nimshukuru kwamba ni mmoja kati ya Wabunge ambao wameleta maombi yao ofisini kwangu kwa ajili ya kwenda kuwekewa minara kwenye maeneo yote ambayo hayana mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niamuahidi kama nilivyozungumza wakati najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sakaya kwamba baada ya Bunge hili nitafanya ziara karibu nchi nzima, specifically kwa wale Waheshimiwa Wabunge wote ambao wameleta barua ofisini kuomba mawasiliano. Nitafanya ziara, tutaanisha maeneo, tutatangaza tenda kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, tutafungua tenda kabla ya mwezi Oktoba, minara itaanza kujengwa maeneo mbalimbali. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo Kaliua linafanana na maeneo yangu ya Wilaya ya Nachingwea katika Kata za Kilimarondo, Mbondo, Mateko pamoja na Kiegei. Naomba kupata majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri nini mkakati wao juu ya kutatua tatizo hili.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Masala, DC wangu mstaafu wa Wilaya ya Kibondo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Masala ni mmoja kati ya Waheshimiwa Wabunge ambao wameleta barua zao za maombi ya minara kwa ajili ya mawasiliano kwenye eneo la Nachingwea. Vijiji vyote alivyovitaja, namuahidi kwamba nitakwenda kule na nitakapokuwa nakwenda kule nitamtafuta ili tuwe naye hata kama kuna maeneo mengine ambayo yana changamoto ya mawasiliano tuweze kuyaona na tuyafanyie kazi ili tuhakikishe kwamba inapofika mwishoni mwa mwaka huu Tanzania inawasiliana kwa asilimia 100. (Makofi)
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza.La kwanza, kwa wananchi wa Bukoba Town na Kagera kwa ujumla usafiri wa meli ni ajira, usafiri wa meli ni usafiri wenye nafuu na wenye kuaminika na usafiri wa meli unatoa unafuu wa bidhaa mbalimbali zinazokwenda Mkoa wa Kagera kuliko ilivyo sasa. Sasa miaka 22 tangu MV Bukoba izame na ahadi za kupata meli mpya zianze kutolewa tangu awamu ya Mheshimiwa Mkapa ni miaka mingi; je, wananchi wa Bukoba na Kagera kwa ujumla wakijenga hisia kuwa wanatengwa watakuwa wanakosea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nini kimekuwa chanzo cha mazungumzo baina ya Serikali na makampuni kutofikia makubaliano ili meli mpya ijengwe na wananchi wa Kagera ambao wanaadhimisha mwezi Mei huu kukumbuka waliotwaliwa ili waweze kuwa na matumaini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. Eng.ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi wananchi watakuwa wanafanya kosa kubwa sana kuona kwamba wanatengwa kwa sababu hatua mbalimbali za Serikali zimekwishaanza kuchukuliwa na nimeeleza wazi kwamba tayari kuna Mkandarasi ambaye amekuja kwa ajili ya kuingia mkataba wa kujenga meli hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi hasa tumeshindwa kuingia nao mkataba kwa sababu hatupendi tuwadanganye wananchi na vilevile hatupendi Serikali yetu iingie kwenye gharama zisizokuwa na sababu kutokana na kuingia mikataba ambayo siyo ya uhakika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili tumeshindwa kuingia mkataba nao kwa sababu kuna vigezo mbalimbali vya kiufundi na kiutaalam ambavyo walitakiwa waviingize katika mkataba wao, wao walivisahau. Sasa hivi nimhakikishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wameviingiza na wao tena wameomba tender katika kuhakikisha kwamba wanatengeza hiyo meli mpya, tunahakikisha kwamba tukishapatana nao vizuri meli itajenga na inawezekana wakapata wao au wakapata watu wengine. (Makofi)
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba katika majibu yake wajipange sana katika mikakati yao kwa sababu Shirika la Anga la Kenya bado wanatufilisi kwa kuchukua mapato ya nchi. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2015/2016 TCAA iliingia mkataba na Kampuni ya COMSOFT GMBH ya Ujerumani. Kwa kuweka mitambo ya kisasa ya kuongozea ndege na kufuatilia safari za ndege yenye thamani ya shilingi bilioni 3.4. Kwa sababu mkandarasi huyu hakuweka dhamana katika kazi, yake mnamo mwaka 2014/2015 mzabuni alitangaza kufilisika.
Kwa kuwa shirika liko kimya kuhusu suala hili Mheshimiwa Waziri naomba kukuuliza, ni kwa kiwango gani shirika limeweza kuokoa fedha hii ya walipa kodi zilizopotea? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali namba mbili, Mheshimiwa Waziri, Mamlaka ilipokutana na Kamati ya PIC ilikuwa na kilio kwamba wana ukosefu wa wataalam wenye sifa katika usafiri wa anga. Katika hotuba yako uliyoiwakilisha muda mchache tu mwaka huu ulisema kwamba Chuo cha Usafiri wa Anga Dar es Salaam kinatoa wataalam wa mafunzo tofauti na wenye viwango vya kimataifa wa ndani na nje ya Tanzania. Je, Mheshimiwa Waziri wataalam hawa…
...wataalam hawa wanaomaliza chuo unawapeleka wapi?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, kwanza nimuhakikishie tu kwamba kwa ufungaji wa rada nne hizo ambazo Mheshimiwa Rais amezindua tarehe 2 Aprili, tuna hakika anga letu lote tutalimiliki sisi kwa maana ya kuhakikisha usalama wake. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi kwamba nchi jirani zitafanya hicho kitu badala yetu. Lakini nikijibu swali lake la kwanza nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha iliyolipwa na Serikali haijapotea bado ipo na sasa hivi kuna taratibu zinafanyika kuhakikisha kwamba pesa yetu inarudishwa kwa wananchi walipa kodi wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu ukosefu wa wataalam nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna wataalam 40 ambao wamepelekwa kusoma ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanaiendesha mitambo yetu hii ya rada ambayo inafungwa kwa ufanisi wa kutosha.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nasikitika Waziri anavyojibu, anaingiza suala la Mbunge wa Jimbo wakati mimi niliuliza swali langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, majibu ya Waziri hayajaniridhisha kabisa. Kuna vijiji vya Kimala, Idete, Uluti, Nyamuhanga, Ibofwee na Itimb. na vingine ambavyo sijavitaja wanajihusisha sana na kilimo kwa ajili ya biashara pamoja na kuzalisha zao la mbao, ambayo yote haya yanahitaji mawasiliano kwa ajili ya kupata soko. Je, ni lini Serikali itahakikisha kuwa wananchi hawa wanapata mawasiliano ili waweze kuuza mazao yao na kupata masoko wanayoyahitaji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Waziri amesema minara hiyo imejengwa na inatoa huduma kama kawaida, yuko tayari twende akaone hiyo minara anayosema inatoa huduma ili ahakikishe mwenyewe kwamba huduma hiyo haipatikani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASIALIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Tendega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuondoe masikitiko kwa sababu hizi shughuli tunazifanya kwa kuwa tunazijua na tumeshatembelea na kufanya survey ya kutosha nchi nzima kujua maeneo gani yana shida ya mawasiliano critical na eneo gani ambalo lina shida ya mawasiliano ya kawaida ambayo yanahitaji kuongezewa coverage na ni maeneo gani ambayo yana shida za mawasiliano kwa vipindi tu vifupi kutokana na kufungiwa solar badala ya umeme wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kujibu maswali yake kuhusu eneo la Kimala, Kidete na vijiji vinavyohusiana, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafanya ziara baada ya Bunge hili la bajeti kwenye maeneo yote pamoja na maeneo ya Kata nzima ya Kising’a najua kuna changamoto za mawasiliano, lakini nitafanya ziara kwenye Kata ya Mahenge, maeneo ya Magana na Ilindi ambako kuna shida kabisa ya mawasiliano, vilevile nitafanya ziara kwenye Kata ya Ibumu kwenye Kijiji cha Ilambo kuangalia kuhusu changamoto ya mawasiliano ya simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nitakuwa tayari kuongozana naye pamoja na Mbunge wa Jimbo kuangalia maeneo hayo. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema mkataba ukisainiwa utachukua miezi sita mpaka mnara ujengwe. Nina minara mitatu ambayo kimsingi imejengwa miaka miwili mpaka sasa haijamalizika, kwa mfano; mnara wa Airtel ambao uko Maga, mnara wa Halotel ambao upo Gidilim na mnara wa Halotel mwingine ambao upo Tumati haujakamilika. Je, Mheshimiwa Waziri atasaidiaje minara hii ikamilike kwa sababu Serikali imeweka fedha nyingi ili wananchi wa Mbulu vijijini wapate mawasiliano?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vijiji ni vingi ambavyo havina mawasiliano, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuja kuonja taste ya kukaa nje ya mawasiliano? Kwa mfano; Getereri, Mewadan, Migo, Harbaghe, Endadug, Eshkesh, Endamasaak, Gorad na Endamilai, yuko tayari sasa kuja ili uone hali ya mawasiliano ilivyo vibaya Mbulu Vijijini ili akatupangia vijiji hivi kupata minara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. Eng. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna minara mitatu ambayo imefungwa muda mrefu na mpaka sasa haifanyi kazi ipasavyo. Kuna mnara wa Maga ambao ulijengwa na Airtel, kuna matatizo yaliyotokea kati ya wakandarasi na jamii inayozunguka eneo hilo iliyosababisha mpaka sasa hivi mgogoro ambao unaendelea kutatuliwa kwa ngazi ya kata.
Mheshimiwa Spika, nahakikisha kwamba naendelea kuwafuatilia hawa watu wa Airtel kwa sababu wao waliingia mkataba na UCSAF kwa ajili ya kupeleka mawasiliano. Masuala ya mgogoro kati ya Airtel na Kata yanatakiwa yatatuliwe miongoni mwao lakini mawasiliano ya wananchi wa maeneo ya Maga yapatikane.
Mheshimiwa Spika, vilevile eneo la Gidilim ambako Halotel wamejenga mnara kuna kama miaka miwili haujaanza kufanya kazi kutoka na Mkandarasi kutopata vifaa vya kutosha kupeleka maeneo hayo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafuatilia yote hayo pamoja na Yaeda, Ampa ambako Halotel vile vile wamefunga ili kuhakikisha kwamba hiyo minara inaanza kufanyakazi kwa haraka sana.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kuhusu kuambatana na yeye kuona maeneo hayo aliyoyataja. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Massay, kwa kweli anafanya kazi kwa bidii sana. Muda mwingi sana huwa tunawasiliana kuhusu masuala ya mawasiliano; na mimi kama mwenye dhamana ya mawasiliano namhakikishia kwamba Serikali tunajua umuhimu wa kuwa na mawasiliano kwa wote kwa sababu mpaka sasa hivi tuna asilimia 94 ya Watanzania wanawasiliana. Hatutaki wabaki hata kidogo inapofika mwisho wa mwaka huu, tunataka Watanzania wote wawe wanawasiliana. Ahsante sana.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini napenda kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza, upanuzi wa Bandari hii ya Kigoma unakwenda sambamba na Bandari Ndogo za Ujiji na Kibirizi ni lini sasa Serikali watakamilisha ujenzi wa Bandari ya Ujiji na Kibirizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mwezi wa Nne Mheshimiwa Zitto aliuliza kuhusu Azimio la Mawaziri wa Maziwa haya Makuu ambapo walikubaliana Kigoma kuwa Bandari ya mwisho katika usafirishaji wa mizigo kwenda Mashariki ya Congo na Burundi. Je, Serikali wamefikia wapi katika utekelezaji wa azimio hili na lini watakamilisha ujenzi wa Bandari Kavu ya Katosho Kigoma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Bandari Ndogo za Ujiji na Kibirizi ni moja kati ya Bandari za kipaumbele ambazo zinatafutiwa pesa ya ujenzi na Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi ninavyoongea Mheshimiwa Mbunge nikutaarifu tu kwamba Bandari ndogo ya Ujiji na Kibirizi ziko kwenye lot moja na zilishatangazwa tenda ya kutafuta mkandarasi wa kujenga na tenda hiyo ilifunguliwa tangu tarehe 28 Agosti na sasa hivi taratibu za kumpata mnunuzi wa kuendelea kuzijenga na kusanifu zinaendelea, na tutakapopata tutamtaarifu lini hizo Bandari zitaanza makandarasi na kuanza kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Mayeye, ni kweli kwamba kulikuwa na changamoto ya kulipa fidia kwa wananchi ambao wako eneo la pale Katosho na wananchi walishalipwa na walishaachia sehemu kwa ajili ya kujenga Bandari kavu ya Katosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizofanyika mpaka sasa hivi ni kusafisha eneo lote kuona mipaka, lakini vilevile tumetangaza tenda kwa ajili ya kumpata mtu wa ku-design na kujenga majengo mbalimbali ndani ya eneo hilo na tenda inategemewa kufunguliwa katikati ya mwezi huu.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa swali la nyongeza. Kwa kuwa Bandari Ndogo za Kirando, Lukoma, Mgambo na Sibwesa hazijakamilika na kwa vile wafanyabiashara wa Jimbo langu la Kigoma Kusini kwenye kata zinazopakana na nchi za DRC, Burundi na Zambia hufanya biashara zao na kupitishia mizigo kwenye Bandari hii ya Kigoma. Swali langu; kwa kuwa wafanyabiashara hawa hutumia magari makubwa na wanapitia kwenye kivuko cha Ilagala na kivuko hiki hakina uwezo wa kubeba magari makubwa, je, kwa nini sasa tenda ya kutangazwa ujenzi wa Daraja la Ilagala haijatangazwa mpaka leo ilhali tumepitisha pesa kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) inayo mpango wa kujenga Bandari ndogo katika eneo la Kilando na Sibwesa. Mpaka sasa hivi Bandari ya Sibwesa imeshakamilika kwa asilimia 93, tunasubiri tu taratibu mbalimbali za kikandarasi na za kiufundi kwa ajili ya kwenda kuifungua hiyo Bandari ya Sibwesa ianze kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Kilando utaratibu wa kumpata mkandarasi unaendelea, tayari watu wameshafanya design; tunasubiri tu taratibu zikikamilika tutangaza tenda kwa ajili ya kumpata mtu wa kufanya ukarabati na ujenzi wa Bandari hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa Daraja la Ilagala nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari taratibu za mwanzo zimeshaanza za upembuzi yakinifu. Baada ya hapo tutafanya usanifu wa kina ili kupata gharama tutangaze tenda kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa kujenga daraja hilo. Ahsante. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Gati la Kilindoni lilipo Wilayani Mafia lipo katika hali mbaya sana. Mbao zake zimechakaa, ngazi imekatika na lile tishali ambalo abiria pale wanapandia limekaa vibaya kiasi kwamba wakati wowote inaweza ikatokea ajali. Sasa Mheshimiwa Waziri ningependa atufafanulie, kwamba imekuwaje, ni lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa wa gati la Kilindoni ukizingatia kwamba ile boti ya DMY itaanza kazi mwezi wa 10? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba gati la Kilindoni lipo katika hali isiyoridhisha kwa matumizi ya abira. Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania pamoja na wataalam kutoka TEMESA na DMY wameshatumwa maeneo yale kwa ajili ya kwenda kufanya ukaguzi na kuleta gharama ambazo zitatumika kutengeneza BOQ kwa ajili ya kufanya marekebisho makubwa ambayo tunakiri yanahitajika katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru tena. Nianze kwa kumshukuru sana Naibu Waziri aliyepata muda wa kuitembelea barabara hiyo na Mheshimiwa Anne Kilango mnamo tarehe 8 Agosti. Mheshimiwa Anne Kilango anatuma salamu na anasema ahsante sana na nadhani aliiona kazi kubwa hiyo. Pamoja na shukurani hizo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maji ni adui mkubwa sana wa barabara ya lami na baada ya mvua kila wakati vile vipande vya lami vilivyojengwa katika eneo husika zikiwemo zile kilomita tatu Kihurio, kilomita tano kisiwani, kilomita tano Ndungu zinaendelea kumomonyoka kila wakati. Je, Serikali haioni sasa kuna kila sababu ya kufanya haraka kuunganisha vipande hivyo ili lami ile iliyowahi isifagiliwe kabisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wote wa Kilimanjaro ilionekana wazi kwamba katika vikao vya RCC Same iko nyuma sana kwenye miundombinu ya barabara na barabara iliyotajwa hapa ni barabara muhimu ambayo pia ina Mbuga za Wanyama. Je, ni lini sasa, baada ya upembuzi yakinifu Serikali iko tayari kupeleka hela hiyo mapema ili zoezi hili lifanyike kwa sababu hii ni ahadi ya Waheshimiwa wagombea Marais toka Awamu ya Nne na Awamu ya Tano? Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza kwa jinsi ambavyo anafanya kazi zake kutetea Mkoa wa Kilimanjaro na wananchi wake kwa ujumla. Swali lake la kwanza ni kweli kwamba mvua au maji ni adui mkubwa sana wa barabara zetu na hasa zile za lami na hata zile ambazo si za lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyoeleza katika majibu ya swali la awali, kwamba baada ya usanifu wa kina kukamilika na kujua gharama tutatangaza tena tutampata mkandarasi, tukishampata mkandarasi hatua za haraka za kutafuta pesa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hiyo zitaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, sisi tunasubiri taarifa za kitaalam, zitakapokuwa tayari na kujua gharama hatutachukua muda mrefu kama Serikali kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami na tutaendelea kuilinda hiyo barabara kwa pesa tulioitenga kwenye bajeti ya mwaka huu. Ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza katika majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba watajitahidi kukwepa hii reli mpya watakwepa Mto Mkondoa na Mto Kinyasungwi na hii mito ndiyo yenye maji mengi yanayosababisha mafuriko maeneo ya Gulwe mpaka Godegode.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, kwa kuwa maji haya huwa yanasambaa kilometa tatu na yeye anasema atajenga kukwepa kilometa mbili, Je, itawezekana? Mafuriko siyataendelea na reli itaharibika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili; eneo la Gulwe kuna makorongo makubwa sana. Mwaka 1996 tulipata mtaalam Johnson kutoka Marekani alijenga ma- gabion makubwa sana lakini mvua moja tu ma-gabion yote yalikwenda. Sasa una maelezo gani Mheshimiwa Naibu Waziri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana kwa jinsi anavyofuatilia na mara kadhaa amekuwa akifika hata ofisini kwa ajili ya kuangalia kwamba eneo lenye matatizo ya mafuriko ya mara kwa mara linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumtaarifu tu kwamba ni kweli maji huwa yanasambaa mpaka kilometa moja, lakini kama atavuta kumbukumbu vizuri mwezi wa pili mwishoni nilitembelea eneo la mafuriko na nikatoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya wa eneo hilo pamoja na kuwasihi wananchi kwamba eneo la reli kwa upande ule ni mita 60 kwa upande wa kushoto na mita 60 upande wa kulia, hawatakiwi wafanye shughuli zozote za kibinadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za kibinadamu ni moja kati ya sababu kubwa zinzosababisha reli yetu kufurikishwa na maji kwa sababu ukishaanza kulima kando kando ya reli unasababisha ule udongo unakuwa tifutifu, ukisababisha udongo kuwa tifutifu maji yakija ni lazima yatabomoa ile reli, lakini kama hakuna shughuli za kibinadamu maana yake ile miti itaendelea kuota na kuzuia. Ile reli haikujengwa kwa bahati mbaya, ilifanyika utafiti ndiyo ikajengwa maeneo yale, lakini niendele kutoa msisitizo kwa wananchi kwamba wasivamie maeneo ya reli na wakae mbali mita 60 kutoka kwenye reli ilipo upande wa kushoto na kulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili; ni kweli kwamba hiyo gabion ilijengwa kubwa na kutatua hilo ni ile njia yetu ya pili kwamba reli itajengwa ndani ya mahandaki mbali kilometa mbili kutoka reli ilipo. Tutajenga meter gauge pamoja na standard gauge ili kuhakikisha kwamba hayo maji sasa hayaji na wananchi tuna uhakika hawatakuja kutuvamia kule kwenye milima ambapo tunajenga reli yetu.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali moja tu la nyongeza; Makao Makuu ya Shirika la Reli Tanzania pale Dar es Salaam hasa Ofisi ambako wanachapisha tiketi za Nchi nzima jengo lile lipo kwenye hali mabaya mno.
Je, Serikali haioni kwamba upo umuhimu sasa wa kulikarabati jengo lile ili wafanyakazi wanaofanyakazi mle ndani na wao wajione ni sehemu ya matunda ya Taifa hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba jengo la Makao Makuu wa Shirika la Reli Tanzania pale Dar es Salaam linahitaji ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge siyo jengo lile tu peke yake, ni majengo mengi sana ya vituo vya Mikoa ambayo kwa kweli hali zake ziyo nzuri na kupitia Shirika la Reli Tanzania tumekwishatoa maelekezo kama Serikali wapitie maeneo yote yale na sasa hivi kuna timu ya wataalam ambao wanapitia kila eneo la majengo ya reli na kuhakikisha kwamba wanaleta gharama nzima pamoja na vile vituo ambavyo vinaitwa gangs na vyenyewe viweze kurekebishwa ili viendane na wakati na wafanyakazi wafanye kazi katika mazingira mazuri.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Kumekuwa na ahadi ya Serikali ya kujenga reli ya standard gauge kutoka Mbambabay - Mchuchuma - Songea mpaka Mtwara. Je, ni lini Serikali itajenga reli hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko kwenye mchakato wa kuhakikisha reli ya Kaskazini ya kutoka Tanga mpaka Musoma na reli ya Kusini kuanzia Masasi mpaka Mbambabay inajengwa kwa kiwango cha kisasa na mpaka sasa hivi ninavyoongea tayari Serikali ilikwishamaliza usanifu wa kina pamoja na upembuzi yakinifu na sasa hivi tuko kwenye hatua za kutafuta mshauri muelekezi wa masuala ya kifedha kwa ajili ya kumpata mwekezaji under PPP tukayeshirikiana na Serikali kujenga reli hizo.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya TAZARA ni reli ambayo ingeweza kusaidia sana kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam na kupeleka nchi za Congo, Zambia na Zimbabwe na kuepusha uharibufu mkubwa wa barabara ambao umekuwa ukitokea kutoka Dar es Salaam kwenda Tunduma. Tumeshangaa kwamba mizigo mingi wanatumia malori kusafirisha badala ya reli ya TAZARA. Je, kuna changamoto gani ambazo Serikali imezigundua kutokana na wafanyabiashara wengi kutokutumia reli hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli yetu ya TAZARA imekuwa ikifanyakazi kwa muda mrefu sana na imekuwa ikihudumia mizigo pamoja na abiria kutoka Dar es Salaam mpaka Kapirimposhi nchini Zambia na kusema kweli Shirika letu hilo la TAZARA limekuwa likifanyakazi nzuri sana katika huduma hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hivi karibuni kumejitokeza baadhi ya wafanyakazi wasiokuwa waaminifu ambao walikuwa wanaishauri vibaya Serikali kitendo kilichosababisha sasa tuanze kukosa mizigo kutoka kwa wateja wetu ambao ni muhimu sana ikiwemo kile kiwanda cha kutengeneza saruji ambacho kiko Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hivi karibuni nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imekwishalifanyia kazi na kuna timu ya wataalam inafuatilia kuhakikisha wateja wetu wote ambao walipotea wanarudishwa. Na sasa hivi nimhakikishie tu Mheshimiwa Mwakajoka kwamba wateja wale wakubwa tumekwishaanza kuwarudisha na TAZARA sasa inafanyakazi nzuri sana. Tuna uhakika ndani ya mwaka mmoja huu wateja wote watakuwa wamesharudi kwa sababau hakuna njia nyepesi na nzuri na salama ya kusafirisha mizigo na abiria kama reli zetu kupitia TAZARA na TRC.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu uhuru barabara hii ni ya vumbi, lakini pia wananchi hawa ni wakulima wakubwa wa kahawa ambao wamekuwa wakichangia katika uchumi katika nchi yetu, lakini pia inashangaza ni namna gani Serikali inawaza zaidi nchi jirani kuliko watu wake ambao wanaendelea kupita katika barabara mbovu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize Serikali kwa sababu miaka ya uhuru ni zaidi ya miaka 50 wananchi wa eneo hili wasubiri sasa miaka mingapi ili barabara hii iweze kutengenezwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili nimeuliza swali langu kuhusu daraja la Kalebe lakini Serikali imekwepa kabisa kugusia daraja hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja hili linasaidia sana wanafanyabiashara na linabeba mizigo ya tani na linapitisha mizigo ya tani 10 badala ya 40 na kuna biashara kubwa ya mbao ambayo wananchi wanahangaika kupitia kutoka Bukoba Vijijini kwenda Kyaka na baadae kurudi Bukoba Mjini na hatimaye sasa kwenda Mwanza, kwa hiyo wanachukua muda mrefu.
Je, kwa sababu mmenionyesha dhamira ya kutokuweza kujenga barabara hii na ndio maana mmepuuza Daraja la Kalebe, sasa naomba nimuulize Waziri daraja hili sasa lina muda upi wa maisha kwa maana ya life span linaweza kudumu kwa muda gani ili kabla ya kufanyiwa matengenezo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeeleza vipaumbele vya Serikali ambavyo nina hakika hata Mheshimiwa Mbunge naye anakubaliana navyo. Tumejipanga kuunganisha mikoa pamoja na nchi jirani, kisha baada ya hapo tutaenda kwenye barabara za mikoa kuunganisha sehemu mbalimbali na barabara yake hiyo ya Kyaka ikiwemo. Hatuna nia ya kuipuuza barabara hiyo na ndio maana kupitia bajeti ya mwaka huu ambayo bahati nzuri kabisa mwenzangu yule hakuiunga mkono tumetenga shilingi milioni 411 kwa ajili ya ukarabati ili njia hiyo iendelee kupitika mwaka mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili la Daraja la Kalebe ninaomba tuwasiliane naye twende tukaangalie status kwa sababu siwezi kumpa majibu ambayo ni nusu nusu ambayo sina uhakika nayo. Ahsante.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa, barabara ya Rasimkumbi mpaka Kilindoni kilometa 55 katika kisiwa cha Mafia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na imo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Lakini mpaka sasa hata usanifu haujaanza.
Swali, je, ni lini Mheshimiwa Waziri barabara hii usanifu utaanza na hatimaye kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Dau, Mbunge wa Mafia kwamba barabara ya Rasimkumbi hadi Kilindoni upembuzi yakinifu tayari umekwishaanza, tukishapata taarifa ya upembuzi yakinifu tutakwenda kufanya usanifu wa kina kwa ajili sasa ya kutafuta pesa kwa ajili ya kujenga eneo hilo. Kwa hiyo, tunaomba avute subira kazi zinaendelea tumekwisha jipanga kwa ajili ya kutekeleza.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipatia swali la nyongeza.
Je,ni lini Serikali itaendeleza ujenzi wa barabara ya Ludewa - Kilosa - Mikumi kwa kiwango cha lami? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabra aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge tayari ilikwishafanyiwa upembuzi yakinifu na ikafanyiwa usanifu wa kina na hivi karibuni tumekwishapata fedha ambayo itaanza kutekeleza mradi huo awamu kwa awamu. Kwa hiyo, tunamuomba Mheshimiwa Mbunge na ninamshukuru sana kwa kufuatilia sana barabara za Mkoa wa Morogoro ambazo zinaunganisha avute subira ataona wakandarasi wakiwa eneo la kazi kwa ajili kutekeleza barabara hiyo muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu.
MHE.DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Barabara ya Bagamoyo hadi Mlandizi ni barabara wezeshi kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.
Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba, Je, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami na wananchi wake kuweza kulipwa fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imekwishafanya upembuzi yakinifu wa barabara aliyoitaja kutoka Bagamoyo mpaka Mlandizi, na sasa hivi hatua za usanifu wa kina zinaendelea ili kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami. Lakini mpaka sasa hivi kuna pesa ambayo imetengwa kwa ajili ya kui-mantain barabara hiyo iweze kupitika mwaka mzima. Kwa hiyo, usanifu wa kina utakapokamilika barabara hiyo itaanza kutafutiwa pesa kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.Nilishauliza mara kadhaa kuhusu barabara hii ya Dumila- Kilosa – Mikumi na Serikali ilikuwa ikitoa majibu haya haya kuhusu upembuzi yakinifu. Barabara hii ni muhimu sana na hata mwaka jana tulitengea bajeti kuhusu ujenzi wa kipande hiki cha kilometa 21 kutoka Ludewa kwenda Kilosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningependa nipate majibu ya Serikali, je, ni lini hasa wananchi wanataka kujua ni lini hasa kazi ya ujenzi wa barabara ya kipande hicho cha kilometa 21 Ludewa –Kilosa utakamilika na then tutaanza lini ujenzi wa kutoka pale Kilosa kuelekea Mikumi ili wananchi wa Mikumi waweze kufaidi matunda ya Serikali yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Mbunge amekuwa akisikia mara kwa mara kwamba upembuzi yakinifu tayari, usanifu wa kina tayari. Nimtaarifa tu kwamba hatua hizo mbili zilishafanyika, hatua inayofuata ni kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo. Fedha ilikwisha tengwa na hivi karibuni tunaamini katika bajeti ya mwaka huu kipande hicho cha barabara kitaweza kujengwa ili tuwaunganishe watu wa Morogoro na Ludewa, ahsante.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Barabara ya kutoka Iguguno mpaka Bukundi ambayo ni Mkoa wa Simiyu inaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu, na tunaona sasa daraja la Sibiti linaendelea vizuri kwa ujenzi wake. Ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza kwa jitihada zake mbalimbali anazozifanya katika kuhakikisha kwamba barabara za Jimboni kwake zinapitika muda wote. Na kwa kweli hata wananchi ambao anawawakilisha wanakiri hilo kwa sababu nilipotembelea kule mara ya mwisho waliniambia jitihada zake anazozifanya na nikawaeleza wananchi wa pale jinsi ambavyo anafika ofisini mara kwa mara kuhakikisha kwamba barabara zinapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namshukuru vilevile kwa jinsi alivyotambua jitihada za Serikali za kuhakikisha lile daraja sasa limekwisha kuwa tayari na linapitika. Lakini wale wakandarasi waliotengeneza lile daraja bado wapo eneo la site na ni hao ambao tutawatumia kuhakikisha hicho kipande alichokitaja Mheshimiwa Mbunge kinatengenezwa na kipitike kwa kiwango cha lami.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. pamoja na jibu la Mheshimiwa Waziri lakini zipo tafiti kadhaa na nyingi ambazo kimsingi zinaonesha kwamba bado kuna madhara makubwa ya watu kuumwa na kichwa na hata kupoteza kumbukumbu kutokana na mionzi inayotokana na minara hii ya simu.
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja hasa ya kufanya tafiti za kina zaidi ili kubaini kwamba madhara haya yapo na namna gani Serikali itatumia njia ili kuyaondoa madhara hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, minara hii imejengwa na imo ndani ya Halmashauri, sasa kimsingi kuna malalamiko makubwa kwa wananchi ambao wamo ndani ya Halmashauri hizo ambazo minara hii imejengwa kwamba hawafaidiki na uwepo wa minara hii ingawa minara hii ipo kibiashara. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja sasa kuandaa utaratibu maalum ili kuona kwamba wananchi na Halmashauri ambazo minara hii ipo zinafaidika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASIALIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tafiti zilizofanyika na Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU) kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi siyo kwamba madhara hakuna kabisa, madhara yapo na hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na makampuni ya simu kwa kuzungushia uzio eneo ambalo wamefunga mnara. Katika kufanya hivyo tunaamini kwa ule upungufu madhara wa mara 1,000 kwa kila mita moja kutoka kwenye mnara hakuna mtu anayeweza kudhurika. Hayo madhara mengine yanayotokana na mtu kuumwa kichwa ni yale ambayo siyo ajabu inawezekana hayatokani na matatizo ya mnara kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya wale ambao minara imefungwa kwenye maeneo yao na kutopata chochote kutokana na hilo na hilo limekuwa likishughulikiwa. Tumekuwa tukipata changamoto kama Wizara kwamba tunapowapa kazi wale watoa huduma labda Tigo, Vodacom, Airtel na kadhalika wanakwenda kwanza kuongea na wananchi kule vijijini. Kwa hiyo, wakishaongea nao wananunua maeneo yao kwa hiyo mwananchi wa kijijini kwanza anakuwa anapokea rent, lakini kunakuwa na tozo ya Halmashauri ambayo huwa inatoa kutokana na vikao walivyokaa Madiwani husika.
Kwa hiyo, hilo linakuwa ni gumu sana sisi kama Serikali kuendelea kuliingilia lakini nimuahidi Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba tunaendelea kulifuatilia kuhakikisha kwamba Serikali kupitia Halmashauri inapata tozo ambazo ni stahiki. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii nimpongeze Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambazo anazifanya. Kwa kuwa wananchi wa Kilolo bado hawajaanza kupata athari yoyote ya minara hii sasa naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu nimekuwa nikiulizia swali la kupata mawasiliano ambayo hayapo kabisa katika vijiji vya Imalutwa, Mazombe, Isele, Kising’a, Mahenge, Maganailindi na Ilambo. Je, Serikali sasa safari hii itakuwa tayari hasa Mheshimiwa Waziri na ulitoa ahadi kwamba utafika ili wananchi hawa waweze kupata mawasiliano ili waendane na sera ya viwanda kwenye nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASIALIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Venance kwa jinsi anavyofuatilia sana suala la wananchi wake kupata mawasiliano katika shughuli zao, kwa kweli amefuatilia sana na katika awamu hii ambapo tumetenga kata 173 za kupelekewa mawasiliano kuna Kata zake nafikiri tatu ambazo tayari tumeshazitengea kwenda kupata mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuahidi tu kwamba hizo kata nyingine ambazo hazijapatiwa mwisho wa mwezi huu kuna kata nyingine 205 ambazo tunategemea zitaingizwa kwenye mpango wa kupelekewa mawasiliano ya simu. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifanya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma na wananchi ambao wanaishi karibu na uwanja ule nyumba zao ziliwekwa alama ya “X” kwa maana kwamba zile nyumba zitavunjwa kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege. Hata hivyo baadhi ya wananchi wamelipwa na baadhi ya wananchi hawalipwa fidia kutokana na nyumba zao kuwekwa alama “X”. Naomba kujua ni lini wananchi ambao hawalipwa watalipwa fidia ili waende wakayafanye maendele ya ujenzi wa nyumba kwenye maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimtaharifu Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia kesho hao wananchi ambao wanadai fidia zao wataanza kulipwa kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza nimuambie tu Mheshimiwa Waziri hatuna kata ya singena tuna kata ya Singe. Lakini pia swali langu la msingi niliuliza vijiji vitatu ikiwemo Kijiji cha Chemchem Kata ya Mutuka ambayo pia haina mawasiliano.
Mheshimiwa Waziri swali la kwanza kama Halotel wameshindwa kwa nini sasa Wizara yako isifuatilie Kampuni nyingine weather Airtel au Vodacom waje waweke minara hiyo kwasababu mazungumzo haya ya Halotel ni tangu mwaka jana na hakuna kazi inayofanyika na hivi vijiji havina mawasiliano. Kwa nini usifuatilie hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Serikali miaka iliyopita mwaka juzi na mwaka jana wali-centralize makusanyo yanayotokana na makampuni haya ya simu ya service levy mwanzo halmashauri zilikuwa zinalipwa moja kwa moja tulikuwa tunakusanya Halmashauri lakini Serikali ilivyo-centralize makusanyo hayo walisema watatuletea kwenye Halmashauri zetu hadi hivi ninavyoongea Halmashauri zetu hawapati service levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba ni lini Serikali watarudisha makusanyo hayo kwenye Halmashauri zetu maana wao ndio wanakusanya sasa halmashauri hatukusanyi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi nimemuelekeza Mheshimiwa Gekul kwamba tumeunda timu ya wataalam kuchunguza minara yote ya simu wala sio ya kampuni moja wapo ya Halotel au Tigo au Vodacom kuangalia uhakika wa mawasiliano kwa maeneo husika ambako imewekwa minara hiyo. Kwa hiyo, hii timu itakapotuletea taarifa tutaweza kujua tufanye vitu gani kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata mawasiliano ya kutosha. Namshauri Mheshimiwa Mbunge awe mvumilivu hiyo timu itatuletea majibu ambako tutaweza kupata mahala pa kuanzia kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala lake la pili kuhusu service levy haya masuala bado kwanza yanaanzia kwenye Halmashauri zetu ambapo sisi Wabunge ni Madiwani huwa mapato yakipatikana huwa yanapelekwa accordingly kutokana na mapatano kati ya halmashauri zetu na makampuni ya simu.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Ulanga ya sasa hivi tumeanza uchimbaji wa graphite ambayo tutakuwa tunasafirisha tani 350,000 hadi 500,000 kwa mwaka wastani wa malori 150 hadi 170 kwa siku kwa barabara ya vumbi hatuwezi Serikali peke yake itapata kodi ya mrahaba bilioni 61 hadi 100 kwa mwaka lakini bila barabara ya lami biashara hii hatuwezi kuifanya.
Sasa basi maswali yangu je, Serikali haioni umuhimu wa kukamilisha barabara hii haraka kabla ya mwaka 2020 ili tusizikose hela hizi ambazo tunazihitaji sana kwa sasa hivi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili Serikali ipo tayari kushirikiana na Mbunge kutafuta wafadhili mbalimbali kwa ajili ya kuangalia ni namba gani wataharakisha ujenzi wa barabara hii unafanyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi nimeeleza hatua ambazo tumekwishaanza kuzifanya kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hizo hatua zitakapokamilika ujenzi wa kipande hicho cha barabara utaaanza mara moja kutegemeana na upatikanaji wa pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili ninazo taarifa kwamba tarehe 16 Juni, 2018 kutakuwa na kikao kati ya wadau mbalimbali wanaotaka kushirikiana na Serikali katika kujenga kipande hicho cha barabara ambako Mheshimiwa Mbunge naye atakuwepo kwa hiyo tutasikiliza mapendekezo yao kama Serikali kama yana tija kwa ajili ya nchi tutayapokea, lakini ninaamini kwamba Serikali ina mpango madhubuti wa kuhakikisha kwamba kisehemu hicho kinajengwa kutokana na hali ya uchumi iliyoko maeneo hayo. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya swali hilo, nina maswali mawili ya nyongeza.
(i) Wananchi wa Nyamisati walipisha ujenzi huo lakini sehemu waliyopelekwa miundombinu yao imekuwa siyo rafiki. Mfano hakuna choo, banda la abiria ni kifusi katika hilo gati la muda. Je, lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi huo?
(ii) Vijana wa maeneo hayo wamejiunga na vikundi vyao vya ujasiriamali kama mkombozi. Je, sasa Serikali ina mpango gani wa kuwapa kipaumbele katika ujenzi huo ili vijana hao wafaidike, wapate vibarua ukizingatia watu wa Pwani wanasema mgeni njoo mwenyeji apone? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Ungando kwa jinsi alivyofuatilia kwa muda mrefu sana ujenzi wa gati hili la Nyamisati. Ninakumbuka kuna kipindi fulani tuliwahi kwenda naye mpaka kufanya kikao na watu wa TPA kwa ajili ya kufuatilia kwa ukaribu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kujibu swali lake la kwanza, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, tayari TPA wanamtafuta mkandarasi kwa ajili ya kujenga choo cha umma pamoja na sehemu ya kupumzikia kwa maeneo ambako wananchi wamepisha ujenzi wa gati uendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo, tutakapopata mkandarasi hilo eneo litajengwa kwa ajili ya wananchi kupumzika vilevile kutakuwa na maeneo rafiki kwa ajili ya wananchi ambao watakuwa wanasubiri huduma za gati hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu la swali lake la pili, ninaielekeza TPA, ninajua kwamba kwenye mkataba ambao wameingia na hawa wakandarasi wawili kuna kipengele ambacho kinawataka wakandarasi wawachukue wazawa katika shughuli zile ambazo siyo za kitaalam kuweza kufanya kazi kama vibarua na vitu kama hivyo. Ninawaagiza TPA wahakikishe wanafanya kazi kama walivyoingia mkataba na wakandarasi kutumia wazawa katika shughuli ambazo siyo za kitaalam. Ahsante. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukweli kwamba mkandarasi yupo site, lakini kasi ya mobilization na vifaa duni anavyovitumia vinatia mashaka sana kama mkandarasi anaweza akamaliza kazi hii katika muda uliotajwa.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari baada ya kikao hiki cha bajeti, mimi, Mheshimiwa Ungando, Mbunge wa Kibiti na mama yetu Mheshimiwa Salma Kikwete ambaye ni mdau mkubwa sana wa Gati la Nyamisati, tufanye ziara ya pamoja ili kuhakikisha kwamba gati hili linakwisha kwa muda uliopangwa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba kati ya Wabunge ambao wamekuwa wakifuatilia suala la Gati hili la Nyamisati ni pamoja na Mheshimiwa Dau na Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, wote kwa pamoja wamekuwa wakifuatilia na wakitaka kujua hatua mbalimbali ambazo zinaendelea katika ujenzi wa gati hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vifaa wakandarasi wanavyo, bado wanaendelea kukusanya, kama nilivyozungumza kwenye majibu ya awali kwamba wako kwenye mobilization kwa hiyo vifaa bado vinaendelea kuletwa na wana vifaa vya kutosha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo, ndiyo maana tumeweka deadline, huu mradi utakabidhiwa mwezi mapema Machi mwakani. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba vifaa vitafika kwa wakati na nipo tayari kwenda nao Waheshimiwa Wabunge wote kwa ajili ya kwenda kuukagua mradi huo.(Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kisiwa cha Izumacheri hawana usafiri tofauti na usafiri wa Meli ya MV Chato, leo ni mwaka wa tatu toka tumeingia Bungeni Mheshimiwa Rais aliahidi, meli hiyo inapaki juu ya jiwe, na ni mwaka wa pili tunaahidiwa kuletewa pesa kwa ajili ya ujenzi wa gati.
Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kuambatana nami baada ya Bunge kwenda kuona adha ya meli inayo-park juu ya jiwe ili uweze kuachia pesa kwa ajili ya ujenzi wa gati hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Rais aliahidi ujenzi wa gati kwa eneo hilo na bado Serikali inatambua na inaendelea kufuatilia namna ya utekelezaji wa ahadi hiyo ya Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaagiza TPA toka mwaka jana mwanzoni, wanaendelea na utaratibu wa kutuletea gharama halisi za kutengeneza gati eneo hilo ili wananchi waweze kupata huduma kwa usahihi. Nieleze tu kwamba niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Musukuma kwenda kuangalia eneo hilo kwa ajili ya kuweka gati. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa na mimi fursa ya kuuliza swali la nyongeza:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vivuko vya Kigamboni vimekuwa vikiharibika mara kwa mara; je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha inavitengeneza vivuko hivi ili kuondosha maafa yasitokee kwa wananchi ambao wanavitumia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia TEMESA Serikali imeendelea kuvihudumia vivuko mbalimbali vilivyopo nchini kwetu kuhakikisha vinafanya kazi kama vinavyotakiwa.
Mimi nina taarifa kwamba hicho kivuko kilikuwa na hitilafu kidogo na ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kufuatilia baada ya muda, hata tukitoka nje tutawasiliana na watu wa TEMESA kuona kuna changamoto gani kwenye hicho kivuko ili ziweze kutatuliwa. Ahsante.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali kwa kutupatia Kivuko cha Msinjahili, Kitumbikwera kule Lindi. Je, ni lini Serikali itakamilisha eneo la kituo cha kupumzikia wasafiri au cha kusubiria wasafiri kati ya Msinjahili na upande wa Kitumbikwera? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Ni kweli kwamba tumerekebisha kivuko alichozungumza Mheshimiwa Mbunge na kwa kweli sasa hivi kimeshaanza kutumika. Kwenye package ya tenda aliyopata mkandarasi wa kujenga kivuko kile, tulimwambia aweke na sehemu ambako wananchi watapumzika. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafuatilia kuona kwamba sehemu ya kupumzika inatengenezwa.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ndogo ili niweze kuuliza swali ndogo la nyongeza. Matatizo ya meli pamoja na barabara yaliyopo Ludewa yanafanana sana na matatizo yaliyopo Mtwara, Lindi hadi Dar es Salaam. Shehena kubwa ya saruji kutoka Dangote huwa inasafirishwa kwa barabara hadi kufika Dar es Salaam, vilevile shehena kubwa ya mawe kutoka Kilwa huwa inasafirishwa hadi kufika Dar es Salaam kwa njia ya barabara, tatizo ambalo lingeweza kutatuliwa kwa kutengeneza zile meli za MS Mtwara pamoja na MV Lindi. Ni lini sasa Serikali itatengeneza meli zile za MS Mtwara na MV Lindi ili barabara ile kati ya Dar es Salaam hadi Mtwara isiharibike na shehena hiyo kubwa iweze kusafirishwa na meli hizo mbili? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba zile meli alizozizungumza Mheshimiwa Mbunge zina hitilafu, lakini tayari tumeshatuma mafundi na wataalam kwa ajili ya kwenda kuangalia gharama ambazo zinahusika kwa ajili ya matengenezo ya meli hizo. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati muafaka ukifika zitatengenezwa ili wananchi wa eneo hilo wapate huduma. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa umbali wa kutokea Ubena Zomozi mpaka Ngerengere ni kilomita 18 na kati ya hizo kilomita 11 zimetengewa kujengwa kwa kiwango cha lami katika Bajeti ya 2018/2019 na zimebaki kilomita saba tu; na kwa kuwa barabara hiyo inaunganisha majeshi yetu mawili kati ya Kizuka mpaka Sangasanga. Je, Serikali haioni umuhimu wa kumalizia hizo kilomita saba kwa kiwango cha lami ili barabara hii ifike Ngerengere Mjini na kule kwenye Kambi yetu ya Jeshi ya Sangasanga?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ahadi kama hii ilitolewa na Rais wa Awamu ya Nne tangu 2010 na Rais wa Awamu ya Tano 2015 katika barabara ya Bigwa – Mvuha kujengwa kwa kiwango cha lami; na kwa kuwa barabara hii iko kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulishamalizika muda mrefu. Ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami ukizingatia tumebakiza miaka miwili kwenda kwenye uchaguzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kipande cha barabara kati ya Ubena hadi Kizuka chenye urefu wa kilometa 11 kimewekewa lami na kipande cha kilometa saba kati ya Kizuka mpaka Ngerengere bado ni cha vumbi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mgumba ambaye kwa kweli Mheshimiwa Mwenyekiti nikiri kwamba ni Mbunge ambaye anafuatilia sana suala la barabara hii kwamba tunafahamu umuhimu na unyeti wa kipande cha barabara kutoka Kizuka kwenda Ngerengere cha kilometa saba, lakini vilevile kutoka Ngerengere kwenda Sangasanga cha kilometa sita na kipande cha kutoka Sangasanga kwenda Mdaula, tunajua umuhimu wa eneo hilo na unyeti wa eneo hilo. Namuomba Mheshimiwa Mbunge tutakapotoka hapa twende Wizarani tukamwoneshe taratibu na hatua ambazo tumekwishafikia kuhakikisha kipande hicho chote ambacho kina mzunguko kinawekewa lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili; ni kweli kwamba kuna ahadi mbalimbali zilishatolewa na viongozi wetu wakuu kuweka barabara kwa kiwango cha lami kutoka Bigwa kuja Mvuha mpaka Kisaki. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba mipango ipo, bahati nzuri upembuzi yakinifu ulishafanyika na usanifu wa kina tayari, kinachosubiriwa sasa ni upatikanaji wa pesa ili tuweze kutangaza tender, kumpata mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kuna utaratibu wa kuunganisha wilaya kwa wilaya. Wilaya ya Bukoba Vijijini inapakana na Wilaya ya Misenyi kutoka katika Kijiji cha Msira kwenda katika Kijiji cha Bulembo, pale katikati kuna mto na watu wanaoishi pale wengi ni wakulima wa zao la kahawa. Je, ni lini Serikali itaamua kuunganisha vijiji hivi kwa kujenga barabara ili kuwarahisishia wakulima hawa wa zao la kahawa usafiri wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunafahamu umuhimu wa kuunganisha wilaya kwa wilaya kwa kiwango cha lami na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mipango ipo kwa ajili ya kuunganisha Wilaya ya Bukoba Vijijini na Misenyi na taratibu mbalimbali za kiuhandisi zimeshaanza kuhakikisha kwamba kiwango hicho kinawekwa hivi karibuni pesa zitakapopatikana.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kuna barabara ya kutoka Nyororo mpaka Mtwango kilimeta 40, barabara ya kutoka Mafinga mpaka Mgololo kilometa 84 na upembuzi yakinifu Serikali ilishafanya miaka miwili iliyopita. Sasa ni lini itaanza kujenga ile barabara kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kigola kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina nia na lengo la kuunganisha kwanza mikoa kwa kiwango cha lami. Hatua zitakazofuata baada ya kuunganisha mikoa yote kwa kiwango cha lami, tutaunganisha wilaya zote kwa kiwango cha lami. Namwomba sana Mheshimiwa Mbunge awe na subira, tunafahamu suala lake na siyo la kwake peke yake, wilaya nyingi sana Tanzania hazijaunganishwa kwa kiwango cha lami. Tutakapofikia mahali pa kuunganisha kwa kiwango cha lami wilaya zote tutafahamishana na tutaanza taratibu hizo mara moja. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali ina wajibu wa kulinda mipaka yake yote ya nchi hii kwa ajili ya kujilinda na maadui mbalimbali wanaovamia ndani ya nchi yetu na ili uweze kulinda mipaka ni lazima kuwe na barabara kwenye mipaka yote, barabara ambazo zinapitika kwa muda wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa kusini unaoanzia Mtwara Mjini kupita Mahurunga – Kitaya – Tandahimba – Newala mpaka Ruvuma, hii barabara ilipandishwa hadhi kwa muda mrefu sasa na inaitwa Barabara ya Ulinzi. Mpaka leo Serikali inasuasua kujenga. Naomba kujua ni lini barabara hii ya ulinzi ambayo nimeitaja itajengwa kwa kiwango cha lami ili kulinda mpaka wa kusini sawasawa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara zote za mipakani ndani ya nchi yetu ziko kwenye mpango wa kutengenezwa kwa kiwango cha lami na barabara hiyo aliyoitaja Mheshimiwa Maftaha ikiwemo. Nimhakikishie Mheshimiwa Maftaha kwamba upembuzi yakinifu umeshafanyika na usanifu wa kina tayari umekwishafanyika. Sasa hivi tuko kwenye taratibu za kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara husika.
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa swali la msingi linafanana na hoja nitakayoitoa na kwa kuwa ujenzi wa barabara ni kiungo muhimu kwa ajili ya maendeleo na pia kuboresha hali halisi ya mwananchi; na kwa kuwa Serikali iliahidi kutoka kwenye Ilani yake ya 2005, 2010 na 2015 ujenzi wa barabara kutoka Makofia kwenda Mlandizi, kutoka Mlandizi kwenda Mzenga, kutoka Mzenga kwenda Vikumburu na Manerumango; na kwa kuwa hadi leo barabara hiyo haijajengwa kwa kiwango cha lami. Je, Serikali itaanza lini ujenzi angalau, narudia tena angalau kwa kiwango cha changarawe ili kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo kupata usafiri mzuri na hali kadhalika ukizingatia Mkoa wa Pwani tunaongoza kwa viwanda vya uchumi? Naomba kauli ya Serikali tumesubiri mpaka leo haijajengwa, ni lini Serikali italisimamia jambo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba Mheshimiwa Zaynab Vullu ni Mbunge ambaye amekuwa akifuatilia sana barabara nyingi sana za Mkoa wa Pwani ambazo ziko kwenye ahadi ya Serikali ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Nampongeza sana kwa jitihada zake hizo, naamini kwamba Serikali tumeshasikia na nimhakikishie Mheshimiwa Vullu kwamba mpaka sasa hivi kuna pesa imekwishapitishwa kwenye bajeti hii ya Wizara yetu kutengeneza barabara husika kwa kiwango cha changarawe. Taratibu zinaendelea kufanyika ili pesa itakapopatikana wakati mwingine ujao tujenge kwa kiwango cha lami.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize swali Mheshimiwa Waziri; barabara ya kutoka Mwanza kwenda Shinyanga Boarder yenye urefu wa kilometa 102 iliyojengwa mwaka 1994 -1998 ni mbaya sana kwa sasa, ina zaidi ya mashimo 3,032 na imekuwa ikifanyiwa utengenezwaji wa mara kwa mara. Je, Serikali inaweza sasa kusema ni lini barabara hii itajengwa upya?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri Serikali tunafahamu ubovu wa barabara aliyoitaja Mheshimiwa na kwa kweli ina mashimo mengi na ni kero sana kwa wapitaji na watumiaji wa barabara ile. Nimhakikishie Mheshimiwa Ndassa kwamba Serikali iko kwenye mpango wa kufanya ukarabati mkubwa kwenye barabara ile na hali ya kifedha itakapoimarika Mheshimiwa Ndassa atatuona tukiwa maeneo yale na wataalam kwa ajili ya kurekebisha kipande hicho cha barabara.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri na yenye kuleta matumaini. Pia niipongeze Serikali bila hata kumung’unya maneno kwa namna ambayo kutokana na ujenzi wa barabara ya lami iliyounganisha Wilaya ya Tunduru na wilaya zingine na kuufanya Mkoa wa Ruvuma vilevile uweze kuungana na mikoa mingine kwa barabara ya lami. Wananchi wa Wilaya ya Tunduru kwa ujumla wanaipongeza na kuishukuru sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kuwa miundombinu ya usafirishaji inafanya kazi kwa kutegemeana, kusaidiana na kwa kushirikiana; baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara tumepanua fursa na kuweka mazingira ya kiuchumi na kijamii kuwa bora zaidi kwa maana ya kuvutia wawekezaji, lakini pia kuwahamasisha wananchi katika eneo hili. Sasa Uwanja wa Ndege wa Tunduru unauona umuhimu wake sasa zaidi kuliko hata ilivyokuwa hapo kabla. Je, Serikali itaingiza lini kwenye mipango ya ujenzi wa viwanja vya ndege, Uwanja wa Tunduru ukawa ni mmojawapo? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, lakini kwa kuwa Serikali pia imekiri kwamba uwanja uliopo haujafungwa rasmi na unaweza ukaendelea kutumika na sisi tunahitaji utumike kwa kuwa mahitaji ni makubwa, wawekezaji wanashindwa kusafiri umbali mrefu sana kwa kutumia njia ya usafiri wa barabara. Je, uboreshaji wa kiwanja kilichopo ambacho kwa sasa hivi hali yake ni mbaya hakiwezi kutumika utafanyika lini kwa maana ya kwamba si uzio tu peke yake, runway na taxiway zinatakiwa kufanyiwa marekebisho lakini pia hata kibanda kwa ajili ya kupokea na kuruhusu abiria kuondoka?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Engineer Ramo Makani kwa jinsi ambavyo mara nyingi sana anafuatilia masuala mbalimbali yanayohusu ujenzi, uchukuzi na mawasiliano kwa Jimbo lake la Tunduru Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna mradi wa ujenzi wa uwanja mpya kwa eneo ambalo tumeoneshwa na watu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduru, lakini bado kuna masuala ya fidia ndogo ndogo kwa wananchi. TAA ambao ni Wakala wa Viwanja vya Ndege wanaendelea kufanya tathmini ya malipo kwa wananchi ambao wanadai fidia zao kwa maeneo ambayo tutayachukua kwenye huu uwanja mpya ambao tunategemea kuujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nimhakikishie Mheshimiwa Ramo Makani kwamba taratibu za ulipaji wa fidia kwa wananchi hao zitakapokamilika tutahitaji sasa tupate hati ya kumiliki uwanja huo kabla ya kuanza mradi wa ujenzi wa uwanja huo. Taratibu nyingine zote zitafuata baada ya kupata taratibu muhimu kutoka Halmashauri ya Mji wa Tunduru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anauliza lini uboreshaji wa uwanja utaanza. Nimhakikishie Mheshimiwa Ramo Makani kwamba tayari timu ya wataalam kutoka TAA imekwishatembelea pale kama nilivyoeleza kwenye swali la msingi tangu mwaka jana mwezi wa Nne na wameshaona eneo la uwanja huo. Mahitaji muhimu kwa ajili ya kuboresha uwanja huo yameshaainishwa sasa hivi tupo kwenye taratibu za manunuzi kwa ajili ya kwenda kuuboresha uwanja huo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Swali la kwanza, kiuchumi kukamilika kwa reli hii kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma itakuwa hakuna tija kama kipande cha kutoka Dodoma kwenda Mwanza na kutoka Dodoma kwenda Mpanda na Kigoma kitakuwa haijakamilika. Tumeshuhudia uwekaji wa saini mikataba hapa karibuni kwa vipande hivi viwili. Sasa ni lini mikataba hii ya kipande kinachoanzia hapa kwenda Mwanza, Kigoma na Mpanda itasainiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, moja ya sababu ya bidhaa za viwandani kuwa bei kubwa sana katika Mikoa ya Geita na Kagera ni kwa kuwa usafirishaji katika maeneo haya unategemea barabara. Kwa kuwa kipande cha Isaka kwenda Kigali kitakamilika, ni upi mpango wa Serikali kujenga reli ya kutoka kwenye chanzo chochote kwenda Geita na Kagera?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imeshaanza ujenzi wa kipande cha kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na Morogoro mpaka Makutupora. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari taratibu za kuanza mchakato wa ujenzi wa kipande cha kutoka Makutupora mpaka Tabora umeshaanza. Tayari upembuzi yakinifu umekamilika na usanifu wa kina tayari umekamilika, tunatafuta pesa kama Serikali kwa ajili ya kuanza mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, tunao mpango wa kujenga kipande cha Geita – Lusahunga mpaka Uganda na taratibu zitakapokamilika, Mheshimiwa Mbunge atataarifiwa kama inavyopaswa. Ahsante. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali ina mpango gani wa kiuchumi wa kuimarisha barabara za vijijini katika mikoa ambayo haijapitiwa na lami ili kwenda sambamba kiuwiano kiuchumi tunapokwenda kwenye Serikali ya viwanda na uchumi wa kati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la ndugu yangu Mheshimiwa Malocha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara za vijijini kikawaida unaratibiwa na TARURA. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tunaendelea na michakato, lakini mapendekezo ya ujenzi wa barabara zote za vijijini kama nilivyozungumza huwa unaanzia kwenye Mabaraza ya Madiwani, inakwenda kwenye RCC kisha kama Wizara tunapatiwa. Kama linatuhusu Wizara ya Ujenzi, tunalishughulikia kama ipasavyo lakini kama inahusu TARURA, basi wenzetu wa Wizara ya TAMISEMI nao wanashughulikia kama inavyopaswa. Ahsante.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kutia moyo lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kuna minara imejengwa katika Kata ya Mapanda, Kijiji cha Mapanda na Kata ya Ikweha Kijiji cha Ikweha, lakini mpaka nauliza swali hili hakuna mawasiliano na Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa ameonana na Mheshimiwa Waziri wa Mawasiliano. Je, ni lini watapata mawasiliano katika kata hizo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya Bunge hili yuko tayari kwenda katika Kata ya Mapanda, Ikweha, Mpangatazara, Ihanu kujionea mwenyewe matatizo ya mawasiliano yanayowapata wananchi wa maeneo hayo? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khadija, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba kuna baadhi ya minara ambayo imewekwa lakini haijaanza kutoa mawasiliano kutokana na sababu mbalimbali. Sababu ya kwanza inaweza ikawa kutokuwepo umeme eneo hilo na wakategemea kutumia solar ambapo kama kunatokea hali ya mawingu, basi zile solar haziwezei kupeleka umeme wa kutosha kwenye minara na hivyo kusababisha wananchi kutokuwa na mawasiliano. Sababu nyingine ni za kijiografia. Hivyo, nawaelekeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote watembelee eneo alilolitaja Mbunge kuhakikisha kwamba wanatambua chanzo cha sababu ya minara hiyo kuwepo lakini haitoi mawasiliano. Nami nitafutilia kuhakikisha kwamba minara yote ambayo imewekwa na haina mawasiliano basi inaanza kupeleka mawaliano kwa wananchi kwa kuwa ndiyo lengo kuu la Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, niko tayari baada ya Bunge hili na nimeshaahidi hata Wabunge wengine kwamba nitafanya ziara ya miezi miwili na timu yangu ya watu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuhakikisha tunatambua maeneo yote ambayo hayana mawasiliano tuweze kuyapatia mawasiliano. (Makofi)
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kweli Wilaya ya Mufindi tuna tatizo kubwa sana la mawasiliano na Mheshimiwa Naibu Waziri amesema ni kutokana na jiografia ilivyo. Vijiji vya Idete, Kasanga, Ihowanza, ni sehemu kubwa sana hawana mawasiliano kabisa na amesema kwamba atakuja na timu yake, je, yuko tayari sasa timu hiyo iende ikafanye survey kwenye vijiji hivi ili wananchi wale waweze kupewa mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Kigola, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi, niko tayari kwenda naye kuangalia maeneo hayo. Ahsante.
MHE MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Serengeti, Kata za Ikoma hususani ndani ya hifadhi maeneo ya Robo, Kata za Sedeko, Nyansurura na Nyambureti, hakuna mawaliano ya simu. Mheshimiwa Naibu Waziri anasema nini kuhusu kupeleka minara katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe maelezo kwa ujumla tu kwamba tunayo changamoto kwenye maeneo ambayo yanapakana na Hifadhi ya Taifa na tuko kwenye mawasiliano mazuri sana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yako kwenye hifadhi tunaweka minara kwa mapatano maalum. Tunapata changamoto kwa sababu wanaohudumia ile minara hatuwezi kuwa na control nao ya moja kwa moja. Tunajipanga kuhakikisha kwamba tunakuwa na control nao ya moja kwa moja ili hata mnara unapowekwa kwenye hifadhi, basi usalama wa hifadhi zetu unaendelea kuzingatiwa lakini wakati huo huo wananchi wanapata huduma ya mawasiliano bila kukwamishwa. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya mpya ya Songwe maeneo ya Rukwa, Udinde, Guwa na Some hayana kabisa mawasiliano. Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akanihakikishia ni lini Serikali itaweka mawasiiano katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la ndugu yangu Mheshimiwa Mulugo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukurani za dhati kwa Mheshimiwa Mulugo kwa jinsi ambavyo anapambana kwa ajili ya Jimbo lake na wananchi wa eneo lake. Nashukuru vilevile kwa kuwa ameshaniletea barua ya maombi ya kuimarisha masuala ya mawasiliano kwenye maeneo aliyoyataja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mulugo kwamba tutafanya ziara baada ya Bunge hili kuhakikisha maeneo yake na maeneo mengine yote ambako Waheshimiwa Wabunge wameandika barua kuomba mawasiliano tunayatembelea na kuhakikisha tunaingiza kwenye bajeti ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ambao tutaanza kuutekeleza kuanzia mwezi Septemba, 2018. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kata ya Mchauru, Kata ya Sindano na maeneo ya Njawara na Ntona yako mpakani mwa Tanzania na Msumbiji na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ulithibitisha kwamba pembezoni au kwenye mipaka ya nchi yetu watahakikisha minara inajengwa. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atahakikisha kwamba wananchi wale wanapatiwa mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bwanausi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Bwanausi kwamba kati ya Waheshimiwa Wabunge walioleta barua zao mwanzoni kabisa kuhusu masuala ya mawasiliano alikuwa ni yeye. Namshukuru Mungu vilevile kwamba tumeendelea kupokea barua kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wengine wanaoeleza changamoto ya mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Bwanausi na wananchi wa Jimbo lake kwamba tutafanya ziara pale, tutaainisha maeneo ambayo tunaweza tukaweka minara kwa sababu siyo lazima ukiomba minara mitano uwekewe mitano. Unaweza ukaomba minara mitano, ukawekewa miwili na ikaweza ku-cover eneo kubwa sana; lakini unaweza ukaomba minara mitatu ukawekewa hata mitano kutokana na jiografia. Ndiyo maana naeleza kwamba ni lazima twende tukajiridhishe tukiwa na timu ya wataalam kuhakikisha kwamba tunaweka mawasiliano ambayo yatahakikisha yanawafaidisha wananchi kwa ujumla wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya mipakani vilevile kuna programu maalum ambapo tunashirikiana Mfuko wa Mawasiliano na TCRA kuhakikisha mawasiliano yanayohusu Watanzania yanabaki kuwa ya Watanzania na yanayohusu nchi nyingine yanaendelea kuwahusu wao.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naamini kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri kwa maneno yake ya mwisho amekubaliana na mimi kwamba vipo vyombo ambavyo vinatumia bandari bubu na havijafanyiwa usajili na wala havikaguliwi mzigo yake. Sasa kama wanavyosema watu nywele nyeupe ni sababu ya kuwa na busara zaidi. Sasa je, atakubaliana na mimi kwamba sasa Serikali ipo haja ya kuhakikisha hata hivi vyombo vinavyotumia bandari bubu sasa vinakuwa na vyombo/zana za uokoaji kama life jacket na vitu vingine? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza la pili ni kwamba, kwa nini kuna bandari bubu ni kwa sababu kuna tozo na kodi za kuudhi kwa watu wanaotoka Zanzibar na maeneo mengine katika bandari zetu ndiyo maana wanatumia bandari bubu. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuondoa hizi kodi kama kwenye TV moja, redio moja au nguo chache kwa watu wanaotoka Zanzibar na Pemba wanaokuja maeneo ya Tanga. Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kama nilivyoeleza mwanzo, umuhimu wa kutumia bandari rasmi tunapata data na kuhakikisha uimara na utayari wa chombo husika kusafirisha abiria kwa usalama zaidi. Kama Serikali, hatuwezi kuruhusu bandari bubu zitumike.
Mheshimiwa Spika, suala la tozo nikijibu swali lake la pili, tozo zinazotozwa kwenye vyombo vya baharini na maziwa makuu siyo kubwa sana kiasi cha kuruhusu watu waendelee kutumia bandari bubu. Namwomba Mheshimiwa Mbunge akubaliane na Serikali kwamba tozo zinazotozwa na affordable kabisa na zinatumika na watu ambao wanataka kufanya kazi kwa uhakika na kwa usalama zaidi kwa ajili ya abiria wao.
MHE. ZAYNABU M. VULLU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, bandari ya Nyamisati na bandari ya Kilindoni zimekidhi kigezo cha Serikali; na kwa kuwa wananchi wa kutoka Nyamisati kwenda Mafia au kutoka Mafia kwenye Nyamisati wanapata shida ya usafiri, uwezo wa majahazi yao hauzidi abiria 50 pamoja na mizigo yao. Je, ni lini Serikali itaondoa kadhia hiyo kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo kwa kuwapelekea boti ambayo itakuwa salama na uhakika wa kusafirisha, ukizingatia kunakuwa na wazee, akinamama wajawazito, watoto, wanaokaa sana bandarini na kukosa usafiri wa uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi anavyofuatilia hasa Bandari ya Nyamisati mpaka nimeshaizowea kuisikia kutoka kwake na Mheshimiwa Dau na wadau wote ambao wako Mkoa wa Pwani bila kumsahau Makamu Mwenyekiti wa Kamati yangu Mheshimiwa Hawa Mchafu.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna vyombo vinafanya kazi maeneo yale, lakini niwapongeze sana Wabunge wa eneo lile kwa sababu vyombo karibu vyote vinavyofanya safari kati ya Mafia na Nyamisati vimesajiliwa na ndiyo maana hata ikitokea ajali, huwa kuna utaratibu maalum ambao tunaweza kupata taarifa rasmi za ajali hiyo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali ina mpango wa kupeleka boti muda huu wakati tunaendelea na utengenezaji wa land craft kubwa tumewapatia TEMESA Sh.3,800,000,000 kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Spika, hivyo nawaomba Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Pwani wasiwe na wasiwasi Serikali ina utaratibu wa kutengeneza kivuko kile pamoja na boat la kuwasafirisha abiria. (Makofi)
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Serikali imebaini kuwa kuna bandari bubu na haziepukiki bandari bubu hizo. Je Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha hizi bandari bubu, wenye vyombo katika bandari bubu wanasajiliwa ili kuepusha ajali za mara kwa mara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna changamoto ya bandari bubu na kama Serikali tumekuwa tukiendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuzirasimisha bandari hizo kwa msaada mkubwa sana wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuwasiliana na wadau ambao wanaendesha bandari bubu. Kwa sababu nyingine huwa zinakuwa zinachangamka kabisa na zinatakiwa zipewe miundombinu mbalimbali ya Kiserikali ili ziwe salama kwa ajili ya Watanzania. Nimhakikishie tu kwamba tutaendelea kuzitembelea na kuwapa elimu na inapotakiwa tutaendelea kuzirasimisha ili kuokoa maisha ya Watanzania waweze kusafiri salama. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Toka asili bandari bubu ndiyo msaada mkubwa kwa wananchi hususani wa Visiwani baina ya Zanzibar na Mwambao wote huu wa Bahari ya Hindi. Linapokuja suala la bandari bubu na vyombo hivi mara nyingi vinaangaliwa vyombo vya baharini na vyombo vya maziwa vinakuwa vinaachiwa huru. Nataka kujua ni kwa nini bandari bubu ambazo wanazisema lakini zinakidhi viwango mfano Kipumbwi, Kigombe Tanga ambazo zinakidhi viwango hawazirasimishi haraka na kufanya kazi wananchi wakapata tija kwa safari zao?
NAIBU WAZIRI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, bandari bubu ni bandari bubu tu, hakuna namna ambavyo unaweza ukaifanya ikawa rasmi kwa kuibadilisha kwa maneno. Ni lazima taratibu za Kiserikali na Sheria zifuatwe kuifanya bandari bubu iweze kuwa rasmi. Nimewahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba bandari bubu zote ambazo zinakidhi vigezo tumekuwa tukizitembelea na kutoa elimu na kuwapa mapendekezo mbalimbali Kiserikali ambayo yatasababisha ziweze kuwa bandari rasmi.
Mheshimiwa Spika, Serikali haiwezi kufurahia kuendelea kuwa na bandari bubu na wala hatuwezi kuruhusu bandari bubu ziwepo, kikawaida bandari bubu zote hatuziruhusu. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba, hizo bandari alizozitaja tutazitembelea, tutaongea na wadau, tukiona zinakidhi vigezo tutazisajili halafu zitakuwa bandari rasmi. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kabla ya Mkongo wa Taifa ilikuwa ukinunua GB10 ni Sh.10,000 lakini baada ya Mkongo wa Taifa gharama imeongezeka sasa ukinunua GB10 ni Sh.35,000. Nilitaka kupata maoni ya Mheshimiwa Naibu Waziri anaposema gharama imeshuka kwenye data ana maana gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, wakati wa Mkongo wa Taifa unapigiwa debe, tuliambiwa utakwenda katika kila halmashauri na taasisi za umma ili kusaidia taasisi hizo kwanza kuwa informed na information system lakini kusaidia katika shughuli mbalimbali. Ni kwa kiwango gani agizo hili limetekelezwa katika taasisi za umma na halmashauri zote nchini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Constatine John Kanyansu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utafuatilia jibu langu la msingi, nimeeleza kwa ujumla jinsi ambavyo Mkongo umesaidia kupunguza gharama za matumizi na kuhakikisha kwamba Watanzania wengi wanapata huduma za mtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la Mheshimiwa Kanyasu linahusu kwa nini kabla ya Mkongo kulikuwa na huduma ambazo ni nafuu, kwa jinsi anavyoona yeye. Tukumbuke kwamba kabla ya Mkongo watumiaji walikuwa wachache sana sasa hivi napozungumza, huduma zimeendelea kushuka. Hiyo gharama aliyoisema ni ya kujiunga na vifurushi, kama hujiungi na vifurushi, ukiweza kupata Sh.10,000 peke yake unaweza ukapata GB nyingi za kutosha kutegemeana na aina ya mtandao ambao unautumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uunganishwaji wa taasisi mbalimbali, napenda nimweleweshe Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka sasa hivi tumeunganisha taasisi za Serikali na Agency zake jumla 72, Local Government Authorities nazo tumeunganisha 77, taasisi mbalimbali kama vyuo na watafiti, RITA na huduma za afya tumeunganisha jumla 207.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha imetengwa kimawasiliano kwa muda mrefu sana, hata imefikia stage Mkurugenzi wa Halmashauri anashindwa kuwasiliana kwa njia ya email katika shughuli zake za kikazi. Je, ni lini Serikali itaunganisha Wilaya ya Ngorongoro na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Catherine Magige kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana huduma mbalimbali zinazotakiwa kupatikana katika mkoa wake na hasa eneo alilolitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna baadhi ya wilaya hapa nchini bado hazijaunganishwa lakini ni chache. Kati ya Wilaya 187 bado hatujaunganisha Wilaya 16 na tumeshawaelekeza TTCL waende wakaunganishe Mkongo ili huduma hizo ziweze kupatikana. Ahsante.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kumekuwa na wimbi sasa limeibuka la wizi wa kutumia mitandao ya simu, wakiwa wanatuma message kwamba umeshinda Tatu Mzuka, umeshinda Tigo, tuma pesa kwenye namba hii; kumekuwa na desturi hiyo sasa hivi. Nilitaka kupata majibu kutoka kwa Waziri, TCRA imechukua juhudi gani kuhakikisha kwamba wizi wa mitandao kwa kutumia simu unakomeshwa na wahusika wanakamatwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bobali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa na matukio ya Watanzania mbalimbali kutumiwa message ambazo zinaonyesha na kuashiria kwamba kuna utapeli unaoendelea katika huduma za mawasiliano. Kwa kutumia Sheria ya Mitandao ya 2015, TCRA kwa kushirikiana na Polisi wameendelea kufanya kazi kwa karibu kuhakikisha kwamba wote wanaosambaza ujumbe huo, wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa mawasiliano unazidi kupanda kwa huduma za jamii na kiuchumi. Wananchi wa Kata ya Ninde na Kata ya Kala katika Ziwa Tanganyika ndiyo pekee hawana mtandao wa simu. Nimechukua hatua kama Mbunge kuandika barua kuleta Wizarani na kumfuata Mheshimiwa Waziri kumueleza juu ya tatizo hili. Je, wananchi watapata lini huduma hii muhimu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mipata, kama ifuatavyo:-
Mheshimwia Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna baadhi ya maeneo machache ya nchi yetu huduma za mawasiliano ya simu ni duni. Kwanza nimpongeze kwa jinsi anavyofuatilia; ameshakuja mara nyingi sana ofisini kufuatilia huduma za mawasiliano kwa eneo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, tenda imetangazwa na hivi karibuni tutawapa watoa huduma ambao wataenda kuweka minara sehemu mbalimbali ambazo mpaka sasa hivi hazina huduma za mawasilinao. Baada ya kufanya hivyo, basi huduma hiyo itaanza kupatikana kama kawaida kwa wananchi wake. (Makofi) Ahsante. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia nashukuru kwa majibu hayo yaliyotolewa na Serikali na kwa kuwa bado stesheni zetu nyingi hasa ikiwemo hii ya Makao Makuu bado hazina sura ya kuvutia na kwa kuwa huduma za vyoo na maji ni muhimu sana kwa afya, majibu ya Serikali yameeleza kwamba itategemea upatikanaji na vyanzo vya ndani, ambavyo vinaweza vipatikane au visipatikane au vitengwe au visitengwe. Je, ni kwa nini Serikali isitenge ikahaulisha kwenye mafungu mengine kufanyia matengenezo huduma hizi muhimu kwa afya ya wananchi wengi hasa wenye uwezo mdogo ambao wanatumia reli hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa watoaji wa huduma wengi kwenye reli hii ni wajasiriamali wadogo akinababa lishe, akinamama lishe na vijana. Kwa nini Serikali isiwafanyie utaratibu wa kujenga sheds au miavuli iliyopangika kwa utaratibu unaolekeweka wakafanya shughuli zao kuliko kutawanya masufuria, majungu, majiko, kuni along the railway lane? Na kwa nini Serikali…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO – (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hali ya Shirika la Reli Tanzania halijaimarika sana; lakini tukumbuke tu kwamba Shirika la Reli nalo linafanya biashara na linao wajibu na jukumu la kuhudumia wateja wake. Pale watakapoona kwamba wameshindwa tutataarifiana ndani ya Wizara halafu tutajua namna ya kuwasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, ni kweli kwamba wajasiriamali wapo wengi kwenye station zetu mbalimbali hapa nchini na wamekuwa wakifanya shughuli pamoja na Shirika letu la Reli. Ni jukumu sasa la Shirika la Reli wakae na hao wajasiriamali waweze kuwatengenezea mazingira wezeshi ya kufanya shughuli zao.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Watumishi wanaofanya kazi kwenye njia ya reli kwenye vituo vidogo (gangs) wanafanya kazi ngumu, kwenye mazingira magumu, lakini wamekuwa hawalipwi fedha zao kwa wakati. Kwanza ni vibarua lakini kuna wakati wanakaa wanapewa baada ya miezi miwili mitatu, wanaishi katika hali ngumu sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanalipwa fedha zao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Magdalena Sakaya kwa sababu ni mdau mkubwa sana wa reli, amekuwa akiitumia miaka mingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba gangs zetu nyingi sana zimekuwa chakavu na nyingine tumezifunga kutokana na uchakavu huo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Shirika la Reli lipo kwenye mchakato wa kuanza kuzirekebisha gangs zote nchini, kwa sababu kutokuwepo kwa gangs kumesababisha hata hujuma mbalimbali kwenye reli yetu na kusababisha upotevu wa mali na wakati mwingine hata maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tutahakikisha kwanza tunazirekebisha gangs zetu, lakini tumeomba kibali kwa ajili ya kufanya ajira nyingine zaidi kwa sababu hata waliokuwepo wameshafikia umri wa kustaafu lakini tumeamua kuwa-hold. Tutakapofikia hatua hiyo hali itabadilika na utaona kabisa kwamba wale nao wataanza kulipwa kwa wakati. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. MWANNE I. NCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa station hizo zina Vituo vya Polisi na kwa kuwa kwa muda mrefu sana Vituo hivyo vya Polisi havija pata msaada wa kukarabatiwa, pamoja na nyumba zao ni chakavu, mbovu, hazifai. Je Serikali iko tayari sasa kutenga fedha rasmi kwa ajili ya ukarabati wa Vituo hivyo vya Polisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO – (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye program ambayo imewekwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na ukarabati wa station watakarabati na Vituo vya Polisi ambavyo vipo kwenye station mbalimbali. Kwa hiyo tunamwomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati mchakato huo utakapoanza hivi karibuni hivyo vituo navyo vitakarabatiwa.
MHE. MARIAM KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na juhudi za Serikali ya Chama cha Mapinduzi kutekeleza Irani ya Chama cha Mapinduzi, kujenga reli ya kisasa ya Standard Gauge ambayo naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi; matatizo ya vituo vidogo vidogo pia yanawapata wakazi wa Dar es Salaam katika Treni yao ya station kwenda Pugu. Hakuna vituo vidogo vya kushushia abiria katika treni hiyo inayotoka station pale mjini kwenda Pugu. Treni inasimama tu na watu wanashuka shuka tu. Je Serikali ina mpango gani wa kuboresha vituo vya treni hiyo ambayo ni muhimu sana kwa wakazi wa Pugu, Ukonga, Kiwalani, Kipawa, Yombo na Vituka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO – (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana na nimpongeze Mheshimiwa Mariam Kisangi kwa jinsi anavyofuatilia sana ile reli ambayo imebatizwa jina la Reli ya Mwakyembe. Ni reli muhimu sana kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na imekuwa ikitoa huduma mbalimbali za kusaidia usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, vituo vilivyopangwa kwa ajili ya kuhudumia reli hiyo ambayo inaitwa kwa jina la Mwakyembe ni vile ambavyo vilikuwa vinatumika kwenye reli ile ya toka mwanzo; na hatuna mpango mpaka sasa hivi wa kubadilisha. Nawaomba Watanzania na wakazi hasa wa Dar es Salaam wasishuke kama treni haijasimama, ni lazima waendelee kuheshimu kwamba treni ina vituo vyake maalum na ikisimama ndio mtu ashuke au kupanda, wasipandie njiani kwa sababu wanaweza kupata ajali.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu hivyo vijiji alivyovitaja nilizunguka naye kuanzia kijiji kimoja mpaka cha mwisho. Kwa hiyo, anaelewa vizuri umbali wa bandari kutoka bandari moja kwenda bandari nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na azma nzuri ya Serikali ya kujenga gati katika eneo la Wilaya ya Ludewa, Mwambao wa Ziwa Nyasa, je, ni lini hasa hivyo vijiji alivyovitaja kwa maana ya Yigha, Makonde, Nsele, Chanjale, na Nkanda vitapata huduma hiyo ya kupakia na kushusha abiria?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa sababu tulikuwa naye Mheshimiwa Naibu Waziri katika ziara ile na ameona malalamiko na usumbufu ambao watu wanaupata. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia na kuhakikisha kwamba wanaondokana na kero hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Deogratias Ngalawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba nilifanya ziara ya Mwambao wa Ziwa Nyasa, Tarafa ya Mwambao tukiwa na Mheshimiwa Deogratias Ngalawa ambapo nilipata nafasi ya kupitia vijiji vyote alivyovitaja. Nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri sana na kubwa anayoifanya kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya meli katika eneo lile ambalo lina changamaoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mbunge kwamba baada ya mchakato wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao utajumuisha pamoja na mambo mengine kulipa fidia, ambayo nichukue tena nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Deo Ngalawa kwa jinsi anavyoishi vizuri na wananchi wake na wanavyotoa ushikiano kwa TPA, tuna hakika baada ya taratibu hizo ujenzi utaanza mara moja. Nimhakikishie tu kwamba kabla ya Juni, 2019 lazima baadhi gati zitaanza kutumika na wananchi wataanza kupata huduma hiyo.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niulize swali dogo tu, ni lini ujenzi wa Bandari Kavu utaanza ya Mbeya ambayo ni ya kimkakati kwa ajili ya kuhudumia mizigo ya nchi jirani za Zambia, Malawi na DRC? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunalo eneo ambalo tumelichukua kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa ajili ya kuweka Bandari Kavu katika Mkoa wa Mbeya. Sasa hivi utaratibu unaoendelea ni kuhakikisha tunalipa fidia kwa wananchi kwa eneo lile ambalo kwa kweli nikiri kwamba ni la kimkakati kwa ajili ya kuhudumia mizigo ya Zambia, Malawi na hata DRC. Tukishamaliza mchakato wa kulipa fidia kwa wananchi, tutaweka mipaka na kutengeneza ramani kwa ajili ya kutengeneza bandari hiyo kavu ili iweze kutoa huduma hizo.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikipata takribani shilingi bilioni 5 kutokana na meli za nje zinazoingia Tanzania kwa ajili ya kufanya uvuvi mkubwa. Je, Serikali sasa na hasa Wizara hii iko tayari kuanzisha bandari maalum ya uvuvi kwenye Bahari ya Hindi ambayo itakuwa inasaidia meli kubwa kutoka nje zinazokuja kwa ajili ya uvuvi ziweze kufanya kazi ili Serikali iweze kupata faida? Kwa sababu sasa hivi meli hizi kubwa zimekuwa zinapata takribani shilingi bilioni 500 na nchi yetu imekuwa ikipata shilingi bilioni 5 tu. Je, Serikali iko tayari kuchukua wazo hili kuanzisha bandari hiyo ili nchi yetu iweze kufaidika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tuko tayari kuchukua wazo hilo na tutashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Uvuvi na Mifugo kuhakikisha kwamba wanatuonesha maeneo stahiki kwa ajili ya kujenga bandari hizo.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kwa dhati kabisa kumshukuru Naibu Waziri huyu ambaye amekuwa akishughulika sana kwa suala la Muungano, mara utamkuta Pemba mara Unguja na mambo mengi ni sare ya Muungano anaileta Baraza la Wawakilishi, ni Waziri Naibu wa pekee na niombe Manaibu Mawaziri wengine mfuate nyayo zake huyu bwana na hana kiburi hata kidogo. Mheshimiwa Naibu Waziri sikusifu kwa kuwa upo mbele yangu lakini kiburi huna na Manaibu Waziri na Mawaziri wafuate nyayo zake.

Mheshimiwa Spika, katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema ndege kuondoka kule Ijumaa na Jumapili nimwambie kuwa ndege kule inaondoka saa mbili na kufika hapa 2.30 kutoka saa tatu mpaka saa 10 jioni huoni ni fatigue na ni adhabu hii kwa Wazanzibari: Sasa, swali la kwanza, je, ni lini atafanya utaratibu huu wa kujipanga upya kuona Zanzibar ni haki yao ya msingi katika Shirika hili la Ndege la Air Tanzania na hii Tanzania ni mmiliki kutokana na muungano wa Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania?

Mheshimiwa Spika, ATCL tokea mwaka 2007 inadaiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar shilingi milioni 241 na amekiri humu ndani kuwa watalipa na mpaka hii leo ikiwa mimi ni mjumbe wa Kamati hii hawajalipa deni hili? Pia je, ni sababu gani zilizopelekea Wajumbe wa Bodi ya ATCL hata upande mmoja…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba abiria wa kutoka Zanzibar kuja Dodoma wakipitia Dar es Salaam huwa wanachukua muda mrefu sana wakisubiri ndege ya kuwaunganisha, hilo tumeliona na kwa kweli tunalifanyia kazi, kama mnakumbuka juzi wakati tunapokea ndege yetu nyingine tumeahidiwa na Mheshimiwa Rais kuwa tutakuwa na ndege za Viongozi ili tuziweke kwenye ATCL ili tuweze kuhudumia.

Mheshimiwa Spika, lengo la ATCL ni kuhudumia Watanzania wote bila usumbufu wowote. Kwa hiyo, tukapozipata hizo tutahakikisha wasafiri wa Zanzibar kuja Dodoma hawachukui muda mrefu sana pale uwanja wa ndege.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Jaku ameuliza kuhusu deni la shilingi milioni 241 ambayo ATCL inadaiwa kama landing fee na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar. Ni kweli hilo deni tunalikumbuka na tunalifahamu na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kuwa linafanyiwa kazi na Mamlaka za Ukaguzi; tukishalihakiki tutalipa. Tunaendelea kulipa madeni kwasababu ATCL ina madeni mengi na inaendelea kuyalipa baada ya kuyahakiki.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jibu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa Mkakati wa East African Community ni kuhakikisha wanaondoa umaskini si kwa Kagera tu bali na mikoa mingine. Tatizo kubwa la Mkoa wa Kagera pamoja na kuwa na viwanda vingi ni barabara zao kutopitika kwa muda mrefu na kusababisha viwanda vyao visifikiwe kwa wakati na kusafirisha mali nje. Je, Serikali ina mkakati gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna baadhi ya mikoa ambayo pia imekuwa ina tatizo ambalo linafanana ikiwepo Mkoa wa Iringa tuna uwanja wa ndege, pamoja na kuwa kuna mazao mengi ambayo yanatoka na yanafika nchi za Afrika Mashariki lakini Serikali imekuwa ikisuasua katika ujenzi wa uwanja ule.

Ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba ule uwanja wa ndege unamalizika ili tupate na watalii wa kutosha waweze kwenda Ruaha National Park kwenye Jimbo la Ismani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambako maswali ya Mheshimiwa Mwamoto yamelenga, naomba kuyajibu maswali yake mawili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba hapo katikati kulikuwa na changamoto ya barabara, baadhi ya barabara kwa kweli zimekuwa na hali mbaya lakini Serikali imekwishapeleka fedha na kuna tangazo la kutafuta wakandarasi kwa ajili ya kurekebisha barabara za Bukoba na maeneo mengine mbalimbali ya nchi yetu ili ziweze kupitika kupeleka mazao sehemu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, tumekwisha tangaza tenda na kuna mkandarasi ambaye yuko tayari kwenye Uwanja wa Ndege wa Iringa, tunasubiri taratibu za mwisho za kuwalipa ili waweze kufanya ukarabati unaostahili. Ahsante sana.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza, napenda kuishukuru Serikali kwa namna ambavyo imeweza kutekeleza upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo tajwa kwa wakati kwa sababu hatua mbalimbali zinaonekana zinaendelea kufanyika. Kwa hiyo, niiombe tu Serikali iongeze speed katika yale maeneo ambayo mradi huu unatekelezwa katika kata hizo.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali katika hizo Kata ambazo tumezitaja kwa maana ya Uswaya, Tambarale, Mwamala ni maeneo ambayo yana watu wengi sana, kwa sababu Serikali ilikuwa imeweka mpango huu katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 na bajeti hii sasa inaelekea mwishoni, je, haioni sasa umuhimu wa kuweka katika mpango wa bajeti wa mwaka 2019/2020?

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwa ruhusa yako, kwanza nitoe pole kwako Mheshimiwa Spika lakini pia kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Zungu na wengine wote wadau kwa yale ambayo yametokea kule Misri. Sisi tunawaombea muendelee vizuri yasitokee tena kama yalitokea kule Misri. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata mawasiliano ya uhakika kwa asilimia 100. Hadi sasa hivi tunapoongea Watanzania kwa record za Serikali wanawasiliana kwa asilimia 94.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba mwezi Aprili, kuna orodha ya vijiji na kata nyingine itakayotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ambazo zitakuwa zimependekezwa kwa ajili ya miradi ya mawasiliano. Asiwe na wasiwasi, tumejipanga kutekeleza kuhakikisha kwamba Watanzania wanawasiliana.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa, hili swali limekuwa la muda mrefu na maeneo mengi ya Tabora Mjini zikiwemo Kata za Itetemya maeneo ya Kipalapala, lakini pia maeneo ya Ndevelwa, Ikomwa, Kakola, Uyui na mengine bado yana matatizo mengi sana ya mawasiliano ya simu. Namuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa hili Bunge lina muda mrefu na tutakuwa na siku za katikati za mapumziko ya wiki, ni lini atakuwa tayari kuongozana na mimi angalau tukakague pamoja miradi hii aweze kuona shida ya wananchi wa sehemu hizo kwenye mambo ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Adam Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwakasaka kwa juhudi nyingi sana anazozifanya katika kushughulikia kero za wananchi katika Jimbo la Tabora Mjini. Mwenyewe nimekwishafika pale, Mheshimiwa Mwakasaka na unakumbuka tulikuwa wote tukazungukia baadhi ya maeneo niliyozungumza yamefungiwa minara na nakuhakikishia kwamba niko tayari wakati wowote twende kutembelea maeneo mengine na nitaambatana na timu ya watalaam kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, ahsante.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Katika Jimbo la Nkasi Kusini vipo vijiji kadhaa ambavyo havina mawasiliano ya simu na nimefanya juhudi sana kumtembelea Mheshimiwa Waziri, mara tatu hivi na kumuandikia barua, vipo Vijiji vya Kasapa, Msamba, Mlalambo, Ng’undwe na vinginevyo. Je, ni lini sasa vijiji hivi vitapata mawasiliano ya simu ambayo ni muhimu sana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba amekwishafika Ofisini kwangu mara tatu, kwa ajili ya kufuatilia changamoto ya mawasiliano katika Jimbo lake la Nkasi Kusini. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari orodha ya vijiji ulivyoniandikia kikiwemo Kasapa, Msamba na Mlalambo vimekwishaorodheshwa kwa ajili ya kutangaziwa tenda hivi karibuni kabla ya mwezi Mei ili viweze kuingizwa kwenye mpango wa kupewa minara ya mawasiliano.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Urambo haikutokea katika orodha ya kwanza iliyotolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa maeneo ambayo hayana usikivu mzuri wa simu, je, kwa kuwa yuko tayari kwenda kwa Mheshimiwa Mwakasaka Tabora Mjini, hawezi pia kupitiliza kuja Urambo ili ajionee mwenyewe maeneo yasiyokuwa na usikivu wa simu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali la mama yangu, Mheshimiwa Margaret Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mwezi Agosti, 2018 tulitangaza orodha ya kata 273 zinazopelekewa minara kwa ajili ya kusambaza mawasiliano na bahati mbaya Jimbo la Urambo halikupata. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vijiji ambavyo aliniletea barua ofisini kwangu, vijiji vya Urambo vitaingizwa kwenye mpango wa mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Namhakikishia nitakapokwenda kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mwakasaka basi nitapitia mpaka Urambo kuangalia changamoto za mawasiliano, kama kuna jipya tutaweza kuongeza zaidi.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mwaka 2016, Serikali ilitutaka sisi Wabunge kuorodhesha vijiji, vitongoji pamoja na mitaa yote ambayo haina mawasiliano na sisi Wabunge tulifanya hivyo, tukaorodhesha vijiji vyetu vingi sana. Jimbo langu la Mbozi niliorodhesha vijiji vingi sana kikiwepo Kijiji cha Mbozi Mission ambacho kina hospitali kubwa na taasisi nyingi kama vyuo, hakina mawasiliano, Kijiji cha Maninga, vijiji vingi sana Jimbo la Mbozi havina mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nijue kwa nini Serikali ilituambia sisi Wabunge tupeleke orodha ya vijiji na maeneo ambayo hayana mawasiliano lakini mpaka sasa maeneo hayo hatujapata mawasiliano. Je, Serikali ilikuwa inadanganya Wabunge?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Haonga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mwaka 2016 tuliwaomba Waheshimiwa Wabunge waorodheshe maeneo mbalimbali ya majimbo yao ambayo hayana mawasiliano. Kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tulifanyia kazi maeneo mengi sana na ndiyo maana mpaka sasa hivi kwa mawasiliano takwimu zinasema Watanzania tunawasiliana kwa asilimia 94. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yake ya Mbozi Mission na mengine aliyoyazungumza inawezekana kabisa kwenye orodha ambayo tunategemea kuitangaza mwisho wa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi wa tano yakawemo na hivyo atapata mawasiliano. Hiyo ndiyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo lililoko Tabora Mjini kwa watoto wetu ni sawasawa na tatizo lililoko Pemba kwa wazazi wao, tatizo la mawasiliano. Mheshimiwa Waziri swali hili uliulizwa mwaka jana na Wabunge wawili na ukaahidi kuja Pemba na ukaja Pemba wewe mwenyewe ukaona tatizo lililopo, hususan kwa Mheshimiwa Maida na Mheshimiwa Bi. Mgeni lakini hadi leo tatizo liko vilevile halijatatuka hakuna mawasiliano katika maeneo hayo. Sasa nini impact ya safari yako kuja Pemba zaidi ya marashi ya karafuu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Yussuf, rafiki yangu sana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilikwenda Pemba mwezi Januari kwa ajili ya kukagua hali ya mawasiliano ya Kisiwa cha Pemba na ni kweli nilikuta hali si nzuri sana. Nikuhakikishie tu Mheshimiwa Yussuf kwamba impact ya safari yangu pamoja na marashi ya Pemba vilevile ni kuhakikisha tunawaletea mawasiliano ili wananchi wa Pemba waweze kuwasiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tuliyoikuta kule ni kwamba kuna hali ya kijiografia ya mabonde na milima, halafu ina minazi mingi sana. Kwa hiyo, badala ya kuweka mnara mmoja u-supply radius ya kilometa 15 kama kawaida ina supply radius isiyozidi kilometa 4, kwa hiyo, inahitaji minara mingi sana. Kama unavyojua mnara mmoja ni shilingi milioni 300 mpaka 600, kwa hiyo, ni lazima tuwe na uwekezaji wa kutosha. Nakuhakikishia kwamba tutaweka uwekezaji huo kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ili wananchi wa Pemba na hasa kwenye kihoteli kile cha chini ya bahari waweze kupata mawasiliano.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongezea Serikali kwa kazi ambayo imefanywa kwenye barabara hii. Kimsingi wakati naandika swali hili, kuliwa hakuna kazi yoyote ambayo imefanyika, lakini sasa hivi nakubaliana kabisa na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Mshauri Mhandishi NIMETA Consult ameshaanza kazi, nami mwenyewe ni shuhuda nimemwona akifanya kazi hii ya usanifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba kwa kuwa Serikali imesema kazi ya usanifu wa kina inaisha mwezi Juni, 2019 na hii barabara ni ahadi ya Rais na pia ni jambo ambalo lipo kwenye ilani:-

Je, Serikali inaweza ikatoa kauli hapa kwamba barabara hii kwa kuwa usanifu utakuwa umekamilika mwezi Juni, sasa kwenye bajeti ijayo itatengewa fedha ili Mkandarasi wa kuanza kujenga aanze kazi kabla ya Awamu hii ya Tano haijamaliza muda wake?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunapokea pongezi kwa moya wa dhati kabisa lakini napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Selemani Zedi kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana kipande cha barabara hii iliyotajwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mpango wa Serikali na nia ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara zote nchini kwanza zimepitika na pili zinaunganishwa kwa kiwango cha lami. Nimhakikishie Mheshimiwa Zedi kwamba barabara yake kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kama ahadi ya Mheshimiwa Rais, tutaijenga kwa kiwango cha lami kabla ya mwaka 2020 kwisha.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama ilivyo ahadi kwa Jimbo la Bukene, Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni zake na hata Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga barabara ya Tarime Mugumu ambayo ni kilometa 89 kwa kiwango cha lami; na kwa kuwa hii barabara ikijengwa itakuza uchumi siyo tu wa Tarime au Mara, bali wa Taifa, maana yake watalii watakao toka Kenya wataweza kupita kwenye njia ile:-

Ni lini sasa hii ahadi ya Mheshimiwa Rais itatimilika kwa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Tarime Mugumu almaarufu kama Nyabwaga Road?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali iliahidi kujenga kipande cha kilometa 44 kutoka Tarime mpaka Mugumu kwa kiwango cha lami. Naamini hata Mheshimiwa Mbunge anajua kwamba upembuzi yakinifu ulishafanyika, usanifu wa awali ulishafanyika na usanifu wa kina ulishafanyika. Sasa hivi tunatafuta pesa kwa ajili ya kumpa Mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekitik, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo, tutajenda hiyo barabara kwa sababu ya umuhimu wa utalii wa nchi yetu kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Magufuli kwa uzinduzi wa barabara ya kutoka Makambako mpaka Mufindi jana. Naomba niulize swali moja. Katika ujenzi wa barabara ya kutoka Dodoma - Mtera mpaka Iringa, pale katika kona za Nyang’holo huwa kunakuwa na maporomoko makubwa sana ambayo huwa yanajitokeza hasa wakati wa mvua:-

Je, Serikali inatusaidiaje? Maana kutakuja kutokea ajali kubwa sana, hata jana nimepita pale. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tayari ameshafika ofisini zaidi ya mara tatu akifuatilia kipande cha barabara hii ya kutoka Mtera - Iringa hasa kwenye kona zile za Nyang’holo ambazo ni korofi kabisa. Tunakiri na bahati nzuri nimeshamwelekeza Meneja wa TANROAD Mkoa kufuatilia eneo hilo ili tuanze tararibu za kulirekebisha kwa ajili ya usalama wa Watanzania.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mji wa Mwanza unaendelea kukua kila siku na miundombinu ya barabara hasa barabara ya Kinyata inayotoka Mwanza Mjini kwenda Usagara hali yake kimsongamano siyo nzuri; na leo nauliza karibia mara ya nne:-

Ni lini sasa Wizara itakuwa tayari kuhakikisha barabara inayotoka Mwanza Mjini kupitia Igogo - Mkuyuni na Butimba - Nyegezi mpaka Buhongwa, inapanuliwa kwa njia nne sasa na kuweza kuwa barabara inayofanana na maziringira halisi ya mji wenyewe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Jiji la Mwanza linapanuka kwa kasi sana na ni mipango ya Serikali kuhakikisha kwamba Jiji hilo linaundiwa program maalum ya kupanua barabara zake kupunguza msongamano. Namshauri Mheshimiwa Mbunge, baada ya kikao hiki, baada ya kipindi cha Maswali na Majibu, tuambatane naye mpaka Wizarani akaone mipango ya Serikali kuhusu Jiji la Mwenza kurekebisha barabara zake.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Mhandisi Mshauri yupo site kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara ya Nyakahura - Lulenge – Mulugarama; na kwa kuwa barabara hii ni ya muda mrefu.

Ni lini sasa ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Gashaza, ni kwa muda mrefu sana amekuwa akifuatilia hii barabara ambayo naomba niitamke kwa ladha yake; inaitwa Nyakahuura – Kumubuga, inapatia Murusangamba - Lulenge mpaka Murugarama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri anakiri kwamba Mshauri Mwelekezi yupo pale kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na baada ya kumaliza zoezi hilo atafanya usanifu wa awali kisha usanifu wa kina kupata michoro kwa ajili kutambua gharama za ujenzi. Hatua zinakwenda vizuri mpaka sasa hivi. Namshauri Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo. Tukishapata nyaraka zote hizo husika, hiyo barabara itaanza kurekebishwa tena kwa kiwango cha lami.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Lulindi. Swali langu la kwanza; Serikali iliahidi miaka miwili iliyopita kwamba itahakikisha inajenga minara katika mipaka yetu yote ya nchi, ikiwemo mpaka wa Tanzania na Msumbiji, lakini vijiji ambavyo viko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ujenzi wake umekuwa ukisuasua sana, hivyo kuwafanya wananchi wa Jimbo la Lulindi kutumia minara iliyoko Msumbiji.

Je, Mheshimiwa Waziri atawaambia ni lini maeneo ya Namtona na Chikolopola yatawekewa minara?

Swali la pili; vibali vya ujenzi kutoka NEMC kuchukua muda mrefu sana kuvipata: Je, Wizara inashirikiana vipi na Wizara inayohusika na NEMC ili kuhakikisha NEMC hawakamishi ujenzi wa minara hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kwamba tuna changamoto kubwa sana kwenye mipaka ya nchi yetu kutokana na mwingiliano wa mawasiliano kutoka nchi za jirani. Hivi karibuni kilifanyika kikao kikubwa sana cha East African Communication (EACO) pale Arusha, ambako wataalam wa Mamlaka za Mawasiliano za nchi za Afrika Mashariki walijadili kwa kina namna ya kuondoa changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mbunge kwamba changamoto hizo zinakwenda kutatuliwa na mpaka sasa hivi baadhi ya Makampuni ya simu tumeshaanza kuyaelekeza yaende yakafanye tathmini ya kiufundi namna ya kuondoa mwingiliano wa mawasiliano kutoka nchi nyingine. Kwamba ni lini tutapeleka mawasiliano; wakati wowote. Kama nilivyojibu katika swali langu la msingi tayari mkandarasi yupo, ameshajulikana ni Tigo na atapeleka mawasiliano kabla ya mwezi Januari mwaka 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, ameuliza kwa nini vibali vya ujenzi kutoka NEMC vinachelewa? Ukweli ni kwamba katika taratibu za ujenzi wowote lazima taratibu zifuatwe. Moja kati ya taratibu ni kupata kibali kutoka NEMC. Wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana ndugu zetu wa NEMC wa kuhakikisha kwamba minara inakopelekwa lazima kusiwe na madhara kwa binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kushirikiana nao katika hali ambayo tunaamini kuwa hakuna ucheleweshaji mkubwa sana. Panapokuwa na ucheleweshaji mkubwa, huwa tunawashauri Wakandarasi wale au watoa huduma watafute eneo lingine ambalo haliwezi kuwa na changamoto kwa wananchi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Changamoto ya minara inayokabili Jimbo la Lulindi, inafanana na ile ya Jimbo la Nanyamba. Unapozungumzia mpaka wa Tanzania na Msumbiji ni pamoja na Kata ya Kitaya na Kilomba iliyopo katika Jimbo la Nanyamba; na Kampuni ya TTCL imepewa dhamana ya kujenga minara minane, katika Jimbo langu la Nanyamba; sasa nataka nipate kauli ya Serikali.

Je, ujenzi huo utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwenye Kata ya Kitaya na Kilomba Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) ilipewa tenda ya kufunga minara maeneo yale. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mkandarasi tayari ameshaanza kukusanya vifaa kwa ajili ya kuvipeleka pale na hivi karibuni kazi itaanza; na ametuhakikishia kwamba ndani ya miezi sita, pale minara itakuwa imeshawekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni sambasamba na kwa Mheshimiwa Nape Nnauye kule Chiuta ambako wanahitaji mnara ili wananchi wa kule na wenyewe wawekewe mawasiliano.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo lililopo katika Mkoa wa Dodoma kama alivyouliza Mbunge aliyepita, nami tatizo hilo hilo katika Jimbo langu la Mgogoni. Jimbo hilo lina sekta muhimu sana kama Polisi na kadhalika, lakini bado mawasiliano ni tatizo:-

Je, ni lini, utajengwa mnara katika Jimbo hilo Kijiji cha Finya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli eneo alilolitaja lina changamoto ya mawasiliano. Nakiri kwamba nimeshawahi kutembelea eneo lile na tumeshachukua coordinates kwa ajili ya kutangaza tenda ambazo zinatangazwa mapema mwezi wa tano kwa ajili ya kusambaza mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo hilo litazingatiwa kwa sababu kuna taasisi za kijamii ambazo ziko maeneo ya pale. Itakapotangazwa tukapata mkandarasi kazi zitaanza na kumalizika mara moja. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yaliyoko Lulindi ni sawa kabisa na matatizo yaliyoko Jimbo la Ilemela, hasa kwenye Kata za Sangabuye ambapo kuna Kituo kikubwa cha Afya na upatikanaji wa mawasiliano umekuwa ni adimu sana, sambasamba na Kisiwa cha Bezi ambako hakuna kabisa mawasiliano na kuna wakazi wengi sana na Mheshimiwa Naibu Waziri ameshapata nafasi ya kutembelea kule; anawaambia nini wakazi wa Bezi na wakazi wa Sangabuye ni lini watapata mawasiliano ili na wao wawasiliane ukizingatia pale kuna Kituo cha Afya ambacho watu wengi wanaweza kupoteza maisha kwa kukosa mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli nilitembelea Kata ya Ilemela kwa Mheshimiwa Angelina Mabula, Naibu Waziri wa Ardhi na nilionyeshwa mpaka eneo la Bezi ambako kunahitaji mawasiliano. Nakiri kwamba kuna changamoto ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tu kwamba maeneo mengi ya nchi yetu Waheshimiwa Wabunge wengi sana minara yao ya mawasiliano haifanyi kazi vizuri. Tunakwenda kutuma timu ya wataalamu kwa ajili ya kurekebisha minara hiyo ya mawasiliano ili iweze kutoa mawasiliano vizuri kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Bezi tumeshafanya tathmini, tumeshatuma mafundi na wataalam kwa ajili ya ukaguzi. Hivi karibuni tutatangaza tenda na Kisiwa cha Bezi kitakuwemo kwa ajili ya kupelekewa mawasiliano. Ahsante.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Tatizo la mwingiliano wa mawasiliano ni kubwa sana katika Wilaya ya Rombo. Karibu nusu ya vijiji tunatumia lines za simu za Safaricom, tunasikiliza redio KBC na televisheni ya KTN ya Kenya. Hii ni hatari sana kwa usalama wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikiuliza hili swali tangu Mheshimiwa Makamba akiwa Waziri mhusika.

MWENYEKITI: Swali sasa Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali; Serikali ituambie sisi watu wa mpakani ni lini tatizo hili litatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili la nyongeza nililoulizwa na Mheshimiwa Bwanausi, niliezea Bunge lako Tukufu kwamba tayari tumeshakaa vikao, wataalamu wa Mamlaka za Mawasiliano za nchi za Afrika Mashariki kutathmini na kuzungumzia kuhusu suala la mwingiliano wa mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote wanaokaa maeneo ya mipakani nikiwemo hata mimi mwenyewe kwamba suala hili la mwingiliano wa mawasiliano kutoka nchi jirani linashughulikiwa.

Mheshimiwa Mwenyektii, hata juzi nimepita pale Tarime, mwenyewe nikiwa pale pale Tarime, nilikaribishwa karibu Kenya Safaricom nikashangaa, lakini ndiyo hivyo mwingiliano wa mawasiliano upo na tumekwishakaa kuanzia mwezi wa Pili tulikaa; na juzi nimemtuma Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano kwenda ku-cement kitu kilichoongelewa mwezi wa Pili na watu wa EACO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa mipakani kwamba hili linashughulikiwa na tunahakika kabla ya mwezi wa Kumi litakuwa limeshafanyiwa kazi, kwa sababu maeneo mbalimbali tayari hatua mbalimbali zimeshaanza kufanyika.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tatizo la Lulindi linafanana sana na Jimbo la Mikumi ambapo kwenye maeneo ya Vidunda, Uleli Ng’ombe, Kisanga, Tindiga na maeneo ya barabara ya kuu ya Tanzania; na Zambia maeneo ya Msimba, Mbamba pamoja na kwenye Hifadhi ya Mikumi, kuna tatizo kubwa sana la mawasiliano:-

Je, ni lini Serikali itawapatia mawasiliano wananchi wa Mikumi wa maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mikumi lina changamoto moja ya kupeleka mawasiliano kwa uhakika, lile Jimbo liko linapakana sana na Hifadhi yetu ya Mikumi na utaratibu wa kuweka minara kule lazima upate kibali kutoka Wizara nyingine. Wasiwasi uliopo ni kwamba tukiweka mnara, watakaohudumia ule mnara watakuwa ni waaminifu wasilete hujuma. Kwa hiyo, tumekuwa tukipata changamoto mbalimbali za namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa eneo kubwa sana, wananchi wa Mikumi wanapata mawasiliano. Vijiji alivyovitaja, kimojawapo kinapata mawasiliano ya Halotel, isipokuwa nilipotembelea pale wananchi walitaka wapate na vodacom, kwa maana ya M-pesa na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashauri na kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge kwamba lengo la Serikali kwa hatua hii, ni kuhakikisha tunapeleka mawasiliano maeneo yale ambayo hakuna mawasiliano kabisa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale maeneo ambayo tayari yana mawasiliano yanataka option nyingine, watusubiri kidogo na ndiyo maana tunapeleka mawasiliano kule ambako hakuna mawasiliano ili Makampuni mengine yavutike kwenda kuwekeza pale, kwa sababu mwisho wa siku ni makampuni ambayo yanakwenda kupata faida na wananchi vilevile. Kwa hiyo, nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge...

MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanaridhisha lakini ahakikishe kweli, maana yake vijiji hivi vimekaa porini sana, havina mawasiliano, tena kwenye mbuga za wanyama mtu akijeruhiwa inakuwa taabu hata mawasiliano ya gari kuja kuwachukua.

Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza; katika Kijiji cha Kizi ambapo kuna mkongo wa mawasiliano umejengwa na Serikali lakini kijiji hakina mawasiliano, je, Mheshimiwa Waziri, nimemfuata ofisini kwake zaidi ya mara kumi kuhusu Kijiji cha Kizi, vipi anaoneje hilo swali langu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Keissy kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ametaka nimhakikishie kwamba eneo hilo ambalo limetajwa nitafikisha mawasiliano. Kama nilivyomhakikishia ni kwamba vifaa viko bandarini, sasa hivi tulikuwa tunafanya clearance kwa ajili ya kuvipeleka sehemu husika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutapeleka hayo mawasiliano kabla ya mwisho wa mwezi wa Sita kama nilivyoahidi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Kijiji cha Kizi; tayari nimekwishatembelea kijiji hicho na tulikuwa na Mheshimiwa Mbunge. Kwanza nimpongeze kwa jinsi anavyofuatilia masuala ya mawasiliano, katika majimbo mengi sana hapa nchini, jimbo lake lina asilimia 93 ya kupatikana kwa mawasiliano, nimhakikishie tu kwamba hicho kijiji chake kilichobakia tutakwenda tutashughulikia na tutakiingiza kwenye Mpango wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu yake mazuri, yeye mwenyewe anajua kwamba minara ya Waheshimiwa Wabunge wengi haifanyi kazi ikiwemo mnara wa kwangu Kilolo na ameahidi mara nyingi kufika kuhakikisha kwamba minara inafanya kazi. Sasa je, atakuwa tayari kwenda kabla ya Bunge hili, kufika Kilolo na kuhakikisha kwamba mnara ule unafanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, niwe mkweli, Mheshimiwa Mwamoto amekuwa akifika mara nyingi sana ofisini kufuatilia masuala ya minara kwenye jimbo lake. Ni kweli pia kuna minara kama mitatu, minne hivi ambayo haipeleki mawasiliano vizuri sehemu kubwa, nadhani ni kwa sababu ya watumiaji wengi sana, kwa hiyo, inakuwa na uhafifu. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutapeleka timu ya wataalam waende wakaiongezee nguvu minara kwenye maeneo yake ili iweze kuwahudumia wananchi kwa ukaribu zaidi.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tatizo lililoko Babati Vijijini ni tatizo pia lililoko Kiteto, Vijiji vya Makame, Ishkribo, Asamatwa, Ngaboro, ni lini sasa vijiji hivi vitaunganishwa pamoja na hivi Vijiji vya Endagwe, Hoshan, kwa ajili ya kufanya tathmini ili wananchi wapate huduma ya mawasiliano?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kijiji cha Landanai kilichoko Simanjiro na Kijiji cha Ngage, ni vijiji ambavyo vina idadi kubwa ya watu lakini mpaka sasa vijiji hivi havijafanyiwa uthamini kwa ajili ya kupata mawasiliano hayo. Ni lini sasa Serikali itapeleka huduma hii Landanai?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Gidarya, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Kiteto alivyovitaja, bahati nzuri vimekwishaletwa mezani kwangu na Mbunge wa Kiteto, kupitia Chama cha Mapinduzi kwamba havina mawasiliano na tumekwishaviingiza kwenye orodha ya vijiji vitakavyopelekewa huduma ya mawasiliano na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namshauri tu Mheshimiwa asiwe na wasiwasi vijiji alivyovitaja vitapepelekewa mawasiliano na vijiji vingine hivyo vyote alivyoviulizia Mheshimiwa Mbunge, tayari ninayo orodha yake nililetewa na Mbunge wa jimbo husika. Nimhakikishie tu Mheshimiwa tukitoka hapa tunaweza kuwasiliana ukaangalia orodha ya vijiji hivyo kuona kama vimeshaingizwa au la, kwa sababu nina hakika vyote vimeshaingizwa.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kabla sijauliza swali naomba nikutakie heri ya Pasaka kwa niaba ya Warombo wenzangu wote.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amenukuliwa katika vyombo vya habari akisema kwamba kuanzia tarehe 1 Mei, 2019 kutakuwa na usajili mpya wa laini zote kwa kutumia alama za vidole. Ameendelea zaidi kusema kwamba hakutakuwa na ruhusa ya kumiliki zaidi ya laini mbili mpaka ruhusa maalumu ya maandishi. Mheshimiwa Waziri anafahamu kuna maeneo mengine laini hazipatikani, kuna maeneo Vodacom ipo lakini Airtel haipo. Sasa mkifanya hivyo hamtaona kwamba mtawatesa wananchi ambao huduma za baadhi ya laini hazipatikani katika maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selasini, Mbunge wa Rombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la usajili kuanzia tarehe 1 Mei, 2019. Ni kweli tumezielekeza kampuni za huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi kuanza sasa utekelezaji wa kusajili kwa kutumia alama za vidole na zoezi hilo litaanza kuanzia tarehe 1 Mei, 2019.

Mheshimiwa Spika, kwa ruksa yako tutaomba sasa Bunge lituruhusu tulete Madawati Maalumu ya watoa huduma ili Waheshimiwa Wabunge wafanye usajili wao wakiwa humu ndani.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine wote kwamba hakuna sehemu ambako nilizungumza kwamba kila Mtanzania atakuwa na laini moja tu ya simu, hapana. Kilichozungumzwa na nilichokizungumza na walikuja kufafanua wenyewe baadaye ni kwamba tunatamani kila Mtanzania awe na laini moja ya simu kwa mtandao mmoja, akitaka laini nyingine, kwa sababu possibility ipo, mtu unaweza ukawa unatumia Tigo lakini ukataka Ipad yako itumie Vodacom, tunaruhusu, useme, lakini tunaepuka utitiri wa laini nyingi.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wenyewe ni mashahidi mnaombwa fedha kila siku, tuma kwa namba hii, tuma kwa namba hii, hizo ni laini ambazo hazina tija na zinatuumiza sana Watanzania. Tulizungumza kwamba mtu awe na laini moja kwa mtandao mmoja, Vodacom moja, Tigo moja, Airtel moja na kadhalika.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, naomba nirejee katika swali la msingi, siko katika mambo ya laini ya Mheshimiwa Selasini.

SPIKA: Uliza, uliza.

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo Babati Vijijini yanafanana moja kwa moja na yaliyopo katika Halmashauri ya Chalize. Nimemwandikia sana Mheshimiwa Waziri na Wizara yake lakini utekelezaji umekuwa ni wa taratibu sana. Sasa kwa kuwa jambo hili nimeshamwandikia Mheshimiwa Waziri, naomba anijibu wamefikia wapi juu ya matatizo ya mawasiliano katika Kata ya Kiwangwa, Msata na Lugoba kama ambavyo tumeelekezana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Chalinze, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Vijiji vya Kiwangwa katika baadhi ya maeneo yana tatizo la huduma ya mawasiliano lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo lake analolitaja la Kiwangwa linahitaji kuongezewa nguvu kwenye mnara wa mawasiliano ulioko pale. Kwa hiyo, namshauri aje tuonane baadaye tuangalie vijiji vingine ambavyo tumeviingiza kwenye mpango wa kupelekewa huduma na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi nina swali moja tu la nyongeza. Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Shirika letu la Ndege la Taifa, kumekuwepo na malalamiko makubwa ya wananchi hususan kuhusu bei za tiketi. Ni kwa nini Serikali isione kuna umuhimu wa kupunguza gharama hizi za tiketi ili wananchi wengi waweze kumudu usafiri huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, itapelekea shirika kuongeza routes badala ya kuwa na route moja kwa siku wanaweza kuwa na route mbili mpaka tatu. Mfano Dodoma – Dar es Salaam kuna route moja...

MWENYEKITI: Ahsante sana, umeeleweka.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Halima Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei za safari za ndege za ATCL huwa zinapangwa kutokana na hali ya soko. Ni ukweli usiopingika kwamba ATCL wako kwenye ushindani na sisi Serikali tunaendelea kuwa-encourage na watu wengine waendelee kutumia usafiri wa anga kupeleka ndege zao maeneo mbalimbali. Sasa hivi wanashindana na watu kama Precision na mashirika mengine, kwa hiyo, hayo mashirika mengine kutokana na ushindani huo ndiyo bei inajipanga yenyewe, huwa inapangwa kutokana na market force.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa safari za ndani za ATCL hakuna mkoa wowote unaoishinda Pemba kwa biashara ya ndege. Mheshimiwa Waziri ulituita mbele ya wadau ukatuahidi kwamba ikifika Novemba/Desemba, 2018 ATCL itaanza safari za Pemba. Hadi leo mwezi Aprili, 2019 haijaanza safari kuelekea Pemba, nini kauli yako Mheshimiwa Naibu Waziri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mwaka jana tuliongea na baadhi ya Waheshimiwa kutoka Pemba kuhusu uwezekano wa ATCL kupeleka ndege yao Pemba. Mpaka sasa hivi hatupingi kwamba kuna abiria wa kutosha Pemba lakini ndege zenyewe siyo nyingi kiasi hicho. Naomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine wote waendelee kuvuta subira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Mheshimiwa Rais ametupatia ndege mbili za Serikali, tunaendelea kuzipaka rangi ili zianze kutumika kwa ajili ya abiria. Kwa hiyo, naamini hata Pemba tutawapelekea ndege moja na sehemu nyingine mbalimbali tutaendelea kupanua wigo wa kusafirisha watu kwa usafiri wa anga.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Wananchi wa Kahama wamekuwa wakiulizia usafiri wa ndege kwa Mkoa wa Shinyanga. Kwa sababu Uwanja wa Ndege wa Shinyanga bado unafanyiwa matengenezo, ni lini ATCL itaanza kutua Kahama?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Maige, Mbunge wa Kahama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalo ni eneo lingine ambalo Serikali inakiri kwamba kuna abiria wa kutosha hata ATCL inafahamu hivyo lakini bado kuna changamoto kidogo ya uwanja, tunaendelea kurekebisha runway iweze kukidhi mahitaji ambapo ndege zetu za ATCL zitaweza kushuka. Tayari tumeshamu-assign TANROADS kwa ajili ya kufanya BOQ ya kurekebisha uwanja huo. Ukisharekebishwa vizuri tutaanza kutua kwa sababu pale abiria na soko la kutosha lipo.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba wake wa Wabunge ama waume wa Wabunge wana haki mbalimbali za kupata huduma kama vile kupita njia za VIP lakini cha ajabu ni kwamba wake zetu wanapata shida sana upande wa VIP. Je, wana haki ama hawana haki ya kupata huduma upande wa VIP, kama vile kwenye feri na viwanja vya ndege?

MWENYEKITI: Kwenye viwanja vya ndege?

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano viwanja vya ndege pamoja na feri.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la ndugu yangu wa Nyang’wale, Mbunge mahiri sana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli ulio wazi kwamba wake au waume au wenza wa Wabunge wanayo haki yote ya kutumia VIP na sijawahi kuona hilo tatizo ninapotembelea viwanja mbalimbali vya ndege. Kwa hiyo, Mheshimiwa kama lilikutokea tunaomba radhi lakini siyo kitu cha kawaida, wenza wa Wabunge huwa wanapata huduma zote stahiki za VIP.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa ndege zetu za Air Tanzania zimekuwa zikishindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Arusha kwa kuwa kiwanja hiki ni kidogo na tunaelewa kabisa Arusha ni kitovu cha utalii na nimekuwa nikiongea kila mara na…

MWENYEKITI: Uliza swali.

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Serikali imekuwa ikiniahidi lakini haitimizi, mpaka sasa hivi nimechoka kufuatilia. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kupanua Kiwanja cha Ndege cha Arusha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Catherine Magige, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Arusha, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri ukweli kwamba Mheshimiwa Catherine Magige amekuwa akifuatilia sana suala la upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Arusha na nimpongeze kwa sababu kwa kupitia juhudi zake nimtaarifu rasmi kwamba TANROADS sasa hivi wanaandaa BOQ kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo kwa mita 200 zaidi lakini pia wanashirikiana na TAA katika kuhakikisha kwamba uwanja huo unaendelea kupanuliwa pamoja na kuwekewa apron nyingine mpya. Hivi karibuni mkandarasi ataingia site kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo ili ndege kubwa ziweze kuanza kuruka.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika marekebisho ya Uwanja wa Ndege wa Musoma, nakumbuka Mheshimiwa Rais amefika pale mara mbili na mara zote ameahidi uwanja huo ujengwe kwa kiwango cha lami na uthamini umefanyika, sasa ni zaidi ya miezi sita. Nataka kupata kauli ya Serikali baada ya kuwa kuna sintofahamu, je, mpango wa kujenga uwanja huo upo au haupo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Manyinyi, Mbunge wa Musoma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Ndege wa Musoma uko kwenye mipango ya kupanuliwa na kuwekewa runway kwa kiwango cha lami na TAA. Hivi karibuni nilifanya ziara Mjini Musoma tukakuta kuna changamoto ya fidia ambapo kulikuwa kuna mvutano wa hapa na pale lakini kuna timu ya wataalam imetumwa pale kwa ajili ya kwenda kuhakikisha ile changamoto ya fidia ya shilingi bilioni tatu na milioni mia saba inatatuliwa ili tuweze kulipa fidia na upanuzi uweze kuendelea.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya kutia matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kama nakumbuka Wizara iliahidi kutoa orodha ya vijiji vyote vitakavyotagazwa na kufunga minara katika majimbo yetu nchi nzima. Swali langu ni lini orodha hii tutapatiwa Waheshimiwa Wabunge ili tuwe na nafasi ya kushauri yale maeneo ambayo tunadhani ni muhimu zaidi kupata mawasiliano? Hapo ikiwemo na Bariadi katika Jimbo unalotoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, maeneo mengi service provider hawa wanapenda kujazana katika maeneo ya centers tu, wanakimbia kupeleka minara katika maeneo ya vijiji vyetu ambako ndiyo kuna shida kubwa ya mawasiliano na population ni kubwa sana. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwalazimisha service providers kwenda kuweka minara katika maeneo yetu ya vijijini ili wananchi wetu waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyoshughulika kuhakikisha jimbo lake wananchi wanapata huduma ya mawasiliano. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine wote kwamba Serikali inahakikisha kwamba mawasiliano yanapatikana kwa uhakika katika majimbo yote nchi nzima. Hivi navyozungumza nimekwishazungumza tena mara nyingine kwamba tumefikia asilimia 94 ya wananchi kuwasiliana na tutahakikisha kabla ya mwaka ujao kuisha asilimia 100 ya wananchi wa Tanzania wanapata mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, Mheshimiwa Mbunge orodha ya mwanzo nitaitoa kesho ya vijiji zaidi ya 600 ambavyo tunategemea kupeleka minara ya mawasialiano kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anataka kujua kwa nini watoa huduma wanarundikana sehemu moja. Kama nilivyowahi kuzungumza hapo awali hawa watoa huduma za mawasiliano ni wafanyabiashara na mfanyabiashara kawaida anatafuta sehemu ambako atapata biashara nzuri, hawawezi kupeleka sehemu ambako hakuna mvuto au ambako wakiwekeza pesa yao haitarudi. Ndiyo maana Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imekuwa ikitoa ruzuku kwa haya makampuni waweze kupeleka mawasiliano mpaka vijijini ambako kabisa wananchi hawawezi kununua huduma za mawasiliano kwa jinsi ambavyo watoa huduma wanataka. Ndiyo maana sasa tumeanzisha Mfuko wa Wawasiliano kwa Wote ili uweze kuziba hilo gap na kufanya wananchi waweze kuwasiliana nchi nzima.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama ilivyo Igalula kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini hususan kwenye Kata za Kizara, Makumba, Kalalani, Mkalamo, Elewa na Lutindi na Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu changamoto hizi. Ni lini Serikali itatoa utatuzi wa changamoto hizi zinazowakabili watu wa Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba nilishatembelea Korogwe Vijijini na hilo eneo alilolitaja Mheshimiwa Mbunge nililiona, ni kweli kwamba kuna mnara wa mawasiliano lakini hauna nguvu ya kutosha. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitatuma wataalam kwanza wakaongeze nguvu kwenye hicho kijiji cha kwanza alichokitaja halafu na nitatoa orodha nyingine kesho aangalie vijiji vingine ambavyo tumeviorodhesha kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano maeneo hayo.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo Igalula, Jimbo la Ludewa lina eneo kubwa sana ambalo halina mawasiliano ya simu. Hivi karibuni imejengwa minara katika Tarafa ya Mwambao lakini minara ile toka ilipowashwa imeongea kwa siku tatu tu. Sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri kuna tatizo gani minara imejengwa imewashwa siku mbili na baada ya hapo mawasiliano hakuna pamoja na ujenzi wa Kijiji cha Ibumi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwishatembelea Kata ya Mwambao ambayo iko mwambao wa Ziwa Nyasa na nimekwishavitembelea vijiji mbalimbali kuanzia Lupingu, Higa, Makonde ambako kweli kabisa kulikuwa kuna tatizo kubwa sana la mawasiliano. Mheshimiwa Deo ambaye ni mfuatiliaji mkubwa sana wa suala la mawasiliano ni shahidi kwamba ndani ya miezi mitano toka nimetembelea eneo hilo tumekwishaweka minara tisa (9) ya mawasiliano kwa ajili ya wananchi wa eneo la Mwambao. Minara mitatu (3) ambayo sasa hivi haifanyi kazi ilipata hitilafu kidogo na hivi sasa tunapozungumza tumetuma wataalam kutoka Halotel wanakwenda kurekebisha hitilafu hiyo ili wananchi waweze kuendelea kupata mawasiliano.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba niulize swali kwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Rombo limekuwa na tatizo kubwa sana la mawasiliano hasa katika kata zilizoko mpakani na ukanda wa juu na Mbunge wa Jimbo hili amekuwa akiuliza maswali mara kwa mara. Je, ni lini tatizo hili litamalizika katika Jimbo hilo la Rombo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace Kiwelu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo Jimbo la Rombo tu maeneo ya mpakani ni karibu majimbo yote ambayo yako mipakani Tanzania kuna tatizo la mwingiliano wa mawasiliano ya simu kutoka nchi jirani. Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekwishawaagiza watoa huduma kwanza kwenda kuongea na majirani zao watoa huduma wa nchi jirani kurekebisha changamoto iliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kulikuwa na utaratibu ambao wenzetu nchi jirani walikuwa wameukiuka ambapo tunaendelea kuufanyia kazi. Sasa hivi eneo la Rombo wako Vodacom na Halotel kwa ajili ya kurekebisha tatizo hil. Eneo la Musoma (Tarime) tumewapeleka Airtel na Tigo kwa ajili ya kurekebisha tatizo hilo. Maeneo ya Bukoba na Kigoma tumewapeleka tena watoa huduma wengine kwa ajili ya kurekebisha tatizo hilo.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa daraja, imekuwa ni faraja kubwa kwa kweli kwa wananchi, tunaipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu hayo, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa barabara hiyo na imekubali kuanza kutenga fedha kwa ajili ya usanifu kwa maana ya kuweka lami lakini bado katika barabara hiyo yapo maeneo korofi ambayo yanasababisha magari kukwama wakati wa masika. Je, kwa nini Serikali isitenge fedha za kutosha kutatua tatizo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kipande cha barabara ya Ntendo - Muze chenye kilometa 37.07 ni barabara inayotegemewa na wananchi wa Bonde la Ziwa Rukwa katika kupeleka mazao Mji wa Sumbawanga; na kwa kuwa barabara hiyo ina changamoto nyingi sana ya kukwamisha magari.

Mheshimiwa Mwwenyekiti, mwaka 2017/2018 Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kuweka lami kilometa 2 jambo ambalo linaweza likachukua miaka 18 kumaliza barabara hiyo. Kwa nini Serikali isiongeze fedha zaidi kuhakikisha barabara ile inakamilika ili kutoa huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya mwanzo nimeeleza tu kwamba kwenye mwaka huu wa fedha 2019/ 2020 tutakuja kuliomba Bunge lako Tukufu litupitishie bajeti yetu ili tuweze kutatua changamoto mbalimbali za barabara zetu hapa nchini ambazo zina mtandao mrefu sana na ambao kwa ujumla kabisa tayari upembuzi yakinifu ulishafanyika na tunaendelea na usanifu wa kina kwa maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, jibu lake la kwanza ni kweli kwamba mwaka huu tutatenga fedha nyingi kwa maeneo korofi ambayo yako kwenye barabara niliyoitaja hapo juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwenye barabara ya Ntendo – Muze kwanza kuna milima mikali sana, na kwa kweli barabara ile ni mbovu na ina changamoto na ndiyo barabara ambayo tunategemea kupata mazao mengi kutoka maeneo hayo. Kuna fedha ambayo tumetenga kupitia TANROAD kwa ajili kwenda kurekebisha maeneo korofi ili barabara iweze kupitika mwaka mzima.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara hii ya kutoka Kibaoni mpaka Mlowo imekuwa ikitajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na pia imekuwa ikitajwa kwenye kila bajeti inayopitishwa na Bunge hili. Je, kutokana na majibu aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, barabara imekwisha fanyiwa upembuzi yakinifu? Hivyo basi wanatafuta fedha ili kuja kuiwekea lami.

Je, Serikali haioni sasa kwamba ni hasara kuifanyia barabara upembuzi yakinifu na baadaye kuja kuitafutia fedha kwa ajili ya kuweka lami jambo ambalo utasababisha tena kuja kufanya upembuzi yakinifu mwingine?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi kabisa Serikali ikishafanya upembuzi yakinifu na ikafanya usanifu wa kina huwa hakuna gharama tena ya kurudia zoezi hilo kwa miaka ijayo hata miaka sita, lakini baada ya hapo ndiyo unaweza kufanya tena feasibility study upya baada ya kujiridhisha kwamba kuna mazingira ya kijiografia yaliyosababisha eneo hilo kubadilika, lakini ni ndani ya miaka mitano tunakuwa tumeshaanza kufanya utekelezaji wa miradi mbalimbali baada ya upembuzi yakinifu.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya wananchi wa Momba na wananchi wa Kwela kwa ndugu yangu Malocha tunashukuru sana kwa ujenzi wa daraja bora kabisa ambalo nafikiri wananchi tutakavyo kwenda kulizindua wataona kazi ambayo tumeifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja hili ni muunganisho wa hiyo Mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe lakini barabara inayozungumzwa inatokea kwenye Jimbo la Malocha inapitia Jimbo langu halafu inakwenda mpaka katika halmashauri ya Wilaya ya Mbozi. Ni barabara ndefu zaidi ya kilomita mia mbili na kitu, na barabara hii inajumuiya ya watu wasiopungua zaidi ya 150000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoomba ni commitment ya Serikali ni lini itakwenda kuanza ujenzi ili wananchi hawa sasa wapate barabara ya lami kama ambavyo ahadi ya Mheshimiwa Rais Kikwete na ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufu itekelezwe kabla ya kumaliza mwaka huu wa uchaguzi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli eneo lile lina watu wengi lakini kwa kweli ni eneo la kimkakati kwa sababu kuna uzalishaji mzuri sana wa mazao mbalimbali ambayo yanasaidia kwenye uchumi wa nchi. Kama nilivyozungumza hapa awali tunaleta bajeti yetu hivi karibuni, tunaliomba sana Bunge lako Tukutu litupitishie bajeti yetu halafu tuanze ujenzi baada ya kupata fedha mara moja.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Tunayo barabara ya kutoka Mbalizi kwenda Wilaya ya Songwe, Mbalizi ni Mkoa wa Mbeya na Songwe ni Mkoa wa Songwe na TANROADS Mbeya, TANROADS Songwe tayari kuna mgawanyiko wa kugawana hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani na kwenye agizo la Mheshimiwa Rais barabara hiyo yenye kilometa 91 na ilishafanyiwa tayari upembuzi kilometa 56 kutoka Mbalizi mpaka Galula ili iweze kupata lami, lakini mpaka leo kupo kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iniambie ni lini watafanya upembuzi yakinifu ili tuweze kupata lami kutoka Mbalizi mpaka Mkwajuni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amekiri kabisa kwamba kuna kipande cha barabara kutoka Mbalizi mpaka Songwe ambacho upande mmoja tayari umekwisha fanyiwa upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatafuta fedha hivi karibuni TANROADS upande mwingine wa pili wataanza kufanya upembuzi yakinifu ili tuwe na upembuzi yakinifu wa jumla wa kilomita 91 kwa ajili ya kuingiza kwenye mipango ya kuanza kufanya utekelezaji wa kujenga kwa kiwango cha lami.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Kata ya Izumacheli inaundwa na Vijiji vitatu, Kijiji cha Izumacheli, Kijiji cha Butwa na Kijiji cha Runazi na ina takriban wakazi kama elfu 40 wako katikati ya ziwa. Tunaishukuru pia Serikali ilituletea meli ya MV Chato ambayo inapita pale mara mbili kwa wiki. Swali langu, meli hii haina sehemu ya kupaki, inapaki juu ya jiwe, kitendo ambacho ni hatari sana kwa maisha ya Wananchi wa Izumacheli.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni nini kauli ya Serikali kulichukulia hili suala serious, ili kuwaepusha wananchi wale wasipate matatizo katika maisha yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, wananchi hawa tumewaahidi sana zaidi ya mara tatu sasa kwamba, daraja litatengenezwa, gati itatengenezwa na Mheshimiwa Naibu Waziri na Serikali imeonesha nia ya kuweza kuwasaidia wananchi hawa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa baada ya Bunge hili kwenda kujionea sehemu ambayo meli inaendelea kupaki kupakia abiria mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Joseph Musukuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Musukuma kwa jitihada kubwa mbalimbali anazozifanya katika kuwatetea na kuwapigania wananchi wa Jimbo la Geita Vijijini ambako yeye ni Mbunge mahiri. Sasa naomba nijibu maswali yake kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ni kweli kwamba, tumekwishaanza mchakato karibu miaka miwili iliyopita ambapo upembuzi yakinifu umefanyika na usanifu wa kina umeshafanyika kwa ajili ya kujenga gati eneo la Izumacheli, lakini pia tumeshatoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya hatua za mwanzo za kuanza ujenzi wa gati hiyo. Kwenye bajeti ya mwaka huu kama Mheshimiwa atapigana ipitishwe tunategemea kutenga pesa nyingine zaidi kwa ajili sasa ya kuendelea kwa kasi kubwa sana ili wananchi wa Izumacheli na maeneo ya Butwa, Ilasi na vijiji vinavyozunguka waweze kupata huduma ya kivuko.

Mheshimia Naibu Spika, swali la pili, mimi niko tayari baada ya kipindi hiki cha Bunge kwenda na Mheshimiwa Musukuma kutembelea maeneo ambayo yana changamoto ya usafiri.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Baada ya ajali ya Kivuko cha MV Nyerere tarehe 20 Septemba, mwaka jana pale Ukala, Serikali iliahidi kutengeneza kivuko kipya kwa ajili ya kusaidia wananchi eneo lile. Hivi sasa kuna kivuko cha muda cha MV Sabasaba ambacho kimekuwa na changamoto nyingi sana. Nataka kujua kutoka Wizara, ni hatua ipi imefikiwa ya ujenzi wa kivuko kipya kitakachofanya kazi kati ya Bugolora na Ukara? Nashukuru.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ile ajali Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeshatangaza tenda na Mkandarasi amepatikana na mkataba umeshasainiwa na sasa hivi tunaendelea kununua engine haraka ili kitakapokamilika kifungwe, lakini pamoja na Kivuko cha Nyamisati, Mafia.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kivuko cha Nyamisati, Kilindoni mpaka leo bado hakijakamilika. Ningependa kusikia kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini kivuko hiki kitakamilika?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetoka kumwambia Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ukerewe ni kwamba hivi vivuko viwili manunuzi yamekamilika na sasa hivi mkandarasi ameanza kazi na tunanunua engine haraka ili baada ya matengenezo sasa vivuko hivyo vianze kufanya kazi. Tulikuwa hatuna kivuko ambacho kilikuwa kinaenda Nyamisati na Mafia, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wapiga kura wake ni kwamba, Serikali imeshachukua hatua, tunajenga kivuko kipya ambacho kita-operate kati ya Nyamisati na Mafia.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ujenzi huu wa reli utakuwa na maana sana endapo upanuzi wa Bandari yetu ya Mtwara utakuwa umekamilika. Kwa sasa hivi mpango ulikuwa ni kujenga gati tatu lakini kinachoendelea sasa hivi Bandari ya Mtwara ni ujenzi wa gati moja tu. Je, hizo gati mbili zilizobaki ujenzi wake utaanza lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ili reli hii itumike vizuri, tunatarajia hata Mkoa wa Lindi utumie vizuri Bandari ya Mtwara lakini barabara ya kutoka Mtwara hadi Mnazi Mmoja imejengwa miaka 50 iliyopita. Je, Serikali ina mpango gani wa ujenzi mpya siyo ukarabati wa kuweka viraka viraka kutoka Mtwara hadi Mnazi Mmoja?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Chikota, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunashukuru kwa pongezi alizotupatia kutokana na jitihada mbalimbali ambazo Serikali inafanya kuhusu ujenzi wa reli kutoka Mtwara mpaka Mbambabay. Tunajua kwamba ili ujenzi wa reli hiyo uwe na tija, ni lazima tuanzie Mtwara kwenye bandari yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sasa hivi tumekwishaanza utekelezaji wa upanuzi wa Bandari ya Mtwara kwa awamu ya kwanza na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea na awamu ya pili na ya awamu ya tatu mpaka tutakapokamilisha upanuzi wa Bandari yetu ya Mtwara ili iwe ya kisasa kuweza kuhudumia mzigo mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kujua kuhusu upanuzi wa barabara ya Mtwara mpaka Mnazi Mmoja. Jibu lake ni kwamba mpaka sasa hivi tayari taratibu zote za kuanza ukarabati mkubwa wa barabara hiyo zimeshakamilika na tumekwishatangaza tenda hivi karibuni mkandarasi ataingia kazini kwa ajili ya kurekebisha barabara hiyo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 18(d) haki ya kupata taarifa ni haki ya msingi kabisa na imetajwa kwenye Katiba na Tanzania siyo kisiwa kwa maana kwamba tunatakiwa na sisi mambo yetu yafahamike kimataifa.

Je, Serikali haioni kwamba kuzizuia hasa Azam kuonesha matangazo haya ni kunyima fursa ya habari za ndani kujulikana kimataifa?

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima kuwa wazalendo ni kupenda vya nyumbani na hawa Azam tumeona wakifanya kazi kubwa sana ya kuelimisha Taifa na kutoa taarifa mbalimbali za kijamii na mara nyingi hata matangazo ya Live ya Mheshimiwa Rais yanaonekana kupitia Azam.

Sasa Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kuangalia hizi sheria na kanuni ili kuweza kuruhusu Azam TV iweze kuruka ndani na kuweza kuonekana katika ving’amuzi hivi tupate taarifa za channel zote za ndani zionekane katika Azam TV.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Shangazi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana kwa kuwa amekuwa ni mmoja kati ya wadau wa tasnia ya habari kwa jinsi anavyofuatilia masuala haya ya visimbusi au ving’amuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujibu maswali yake mawili ni kwamba ni kweli tunakiri kwamba kila Mtanzania anayo haki ya kupata habari na ndiyo maana kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania tulitengeneza utaratibu wa kutoa leseni za aina mbalimbali kwa watoa huduma za matangazo kuweza ku-apply. Watu wa StarTimes, Ting na Continental wali-apply leseni ambazo zinawawezesha kuonesha free to air channels lakini Azam, Zuku na wengine wali-apply leseni ambazo zinawaruhusu kuonesha matangazo kwa njia ya kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Serikali tuliwaambia kabisa madhara au faida ya kuchukua leseni za aina hiyo ambazo hata gharama ya ulipiaji kwa mwaka ni tofauti. Azam waliamua kuchukua ile ya kimataifa kwa sababu walitaka mtu anayetaka kuona habari kupitia Azam aweze kulipia; kitendo cha wao kuanza kuonyesha channels za free to air, zile ambazo zinamruhusu mwananchi yeyote hata kama hela imeisha kwenye king’amuzi aone, haikuwa ni sehemu ya masharti ya leseni yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa swali lake la pili, nimuondoe wasiwasi kwamba kati ya watu walio-apply leseni za kuonesha na free to air channel Azam wapo na nimuondoe wasiwasi kwamba jana wamepokea hiyo leseni na wametuhakikishia kama Serikali kwamba ndani ya miezi saba watakuwa wameshajenga DDT eneo lote la nchi yetu kwa ajili ya kurusha hizo channels za bure.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Gati hili la Bukondo siyo kwamba ni jipya, lipo, ila tu limeharibika kiasi kwamba meli zinapotua pale kwenye gati zinashindwa kutua vizuri, wananchi ni lazima wakanyage maji ndio wanaingia kwenye ferry. Kwa hiyo, siyo kwamba gati halipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti za Serikali kila mwaka huwa naiona inawekwa kwenye lakini utekelezaji tu wa ujenzi sijaona ukifanyika. Napenda kujua sasa, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa lile gati kwa sababu tayari lipo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa kuna barabara ambazo huwawezesha wananchi kufika kwenye gati hilo; barabara hizo nazo hazipitiki vizuri hasa katika kipindi hiki cha mvua; napenda kujua hatima ya hizi barabara. Kuna barabara ya kutokea Katoro - Inyara kwenda mpaka Bukondo; pia kuna barabara ya kutoka Nyarugusu kwenda Rwamgasa mpaka Katoro na nyingine ya kutokea Kahama ambayo tayari Serikali imeshaiweka kwenye bajeti ya kuweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami; napenda kujua hizo barabara zitatengenezwa lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya awali nimeeleza kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ina mpango wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga magati kwenye maziwa yote makuu. Kwa kusema hivyo siyo kwamba hatujui kwamba kuna gati katika eneo hilo. Gati katika eneo hilo lipo na gati hilo mpaka sasa hivi linamilikiwa na Halmashauri pamoja na GGM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu gati hilo kwamba linatakiwa kupata matengenezo na usimamizi maalum na ndiyo maana kwa ridhaa ya Bunge tulifanya marekebisho ya sheria kwenye Bunge lililopita kuhakikisha sasa kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari inaweza kumiliki bandari zote ambazo ziko kwenye maziwa makuu na eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zinaendelea na upembuzi yakinifu unafanyika, siyo kwa eneo hilo peke yake, ni kwa maeneo yote nchi nzima; maeneo ya bahari pamoja na maziwa makuu. Tutakapokuwa tumekamilisha huo upembuzi yakinifu, basi tutaichukua na bandari hiyo tutairekebisha ili kuiwekea miundombinu stahiki ya kuweza kuirekebisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili ameulizia kuhusu ujenzi wa kurekebisha barabara ambazo zinaingia kwenye eneo hilo la gati. Ni kweli katika mvua hizi zinazoendelea kumekuwa na uharibifu mkubwa sana wa miundombinu hasa ya barabara maeneo mbalimbali. Eneo hilo tunalifahamu na limeshatengewa katika zile shilingi bilioni tisa ambazo zimetengwa za dharura na lenyewe litazingatiwa kwa ajili ya kurekebishwa.
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Huko katika Ziwa Victoria kutokana na mvua nyingi zinazonyesha msimu huu, magati mengi yamemezwa na maji katika hili pamoja na gati alilolisema Mheshimiwa Bukwimba lakini Gati la Kisiwani Maisome na Gati la kule Bugorora Ukerewe na yenyewe yamezama, wananchi wanaingia kwenye vivuko kwa kuvua nguo. Tunaomba Serikali itupe kauli kwamba itashughulikia vipi kwa haraka magati haya ili wananchi wasiendelee kupata aibu na usumbufu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimia Dkt. Charles Tizeba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua kwamba kutokana na mvua hizi zilizonyesha magati mengi yamepata changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoweza kupitika vizuri baada ya kuwa yamejaa maji. Tumeendelea kufanya utafiti wa kina kwa kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari. Tukumbuke tu kwamba magati mengi ambayo yapo nchini bado yanamilikiwa na Halmashauri.

Kwa hiyo lazima kuwepo vikao vingi vya kukubaliana namna ya kuyachukua magati yale na kuyaendesha, kwa sababu sheria ilikuwa haijapitishwa na kwa kuwa sasa sheria imepitishwa ni lazima sasa tunakwenda hatua kwa hatua kuhakikisha kwamba yale magati yote ambayo yako chini ya kiwango yaliyokuwa yanamilikiwa na Halmashauri sehemu mbalimbali nchini yanarekebishwa kwa kiwango ambacho kinakidhi standard za kuendeshwa na Mamlaka ya Bandari.

Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba atuvumilie kidogo, tunakwenda kufanya utafiti wa kina na kuyarekebisha magati yote nchi nzima yaweze kupitika kwa kiwango na yaweze kuhudumia wananchi.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri na jitihada za Serikali, bado maeneo mengi ya Mkoa wa Manyara yana tatizo kubwa la mtandao. Ukiacha upatikanaji wa sauti, lakini bado kuna shida kubwa katika upatikanaji wa internet, kwa hiyo shughuli nyingi za Serikali zikiwemo hospitali, shule na ofisi mbalimbali zinashindwa kufanyika ipasavyo kutokana na ukosefu huo wa mtandao. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha data zinaweza kupatikana katika Mkoa wa Manyara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni stendi ya Mji wa Babati ilihamia nje kidogo ya mji na tuna tatizo kubwa sana la mtandao katika stendi hiyo. Ni mtandao wa tigo peke yake ndiyo unaopatikana na kama tunavyofahamu shughuli zilizoko stendi ni nyingi na abiria ni wengi wanaotumia mitandao mbalimbali.

Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba mtandao unapatikana katika stendi ya Mji wa Babati na ni lini labda pia Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kuona tatizo hili kubwa katika Mkoa mzima wa Manyara. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Ester Mahawe kwa jinsi anavyofuatilia Mkoa wake mzima suala la upatikanaji wa mawasiliano. Ni kweli kwamba maeneo mengi ambayo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ulikuwa unatoa pesa kwa ajili ya kujenga minara ya mawasiliano, walikuwa wanapeleka minara ambayo ina- supply 2G ambayo inahudumia voice na data kwa maana ya text peke yake lakini internet hakuna. Kuanzia tenda iliyotangazwa na kusainiwa Desemba, 2018, tulizielekeza kampuni zote kwamba sasa hivi kuanzia 2019 minara yote itakayojengwa iwe na access ya 3G ili wananchi wa maeneo hayo waweze kutumia data na mpaka sasa hivi minara inayoendelea kujengwa ambayo tunategemea itakamilika Juni, 2020, mingi sana itakuwa na huduma ya data kwa maana ya 3G, 4G na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili ni kweli kwamba stendi ya Babati ina mawasilino ya tigo peke yake. Niyashauri makampuni mbalimbali yanayotoa huduma za mawasiliano nchini yachukue nafasi hii kuona fursa ya kuweka minara hiyo katika maeneo ya stendi ya mabati kwa sababu kuna mkusanyiko mkubwa wa watu, kuna uchumi mwingi, kwa hiyo wakiweka mawasiliano pale itasaidia sana kuhakikisha kwamba wananchi wa Babati kwenye stendi pale wanaweza kupata huduma ya mawasiliano kutoka kwenye makampuni mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa mimi niko tayari kuongozana na tutatembea na maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Manyara na Mheshimiwa Ester Mahawe kwa ruhusa yako. (Makofi)
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kata ya Ibumi katika Jimbo la Ludewa ni kata pekee ambayo haina mawasiliano kabisa na bahati nzuri yupo mzabuni TTCL ameanza kujenga, lakini toka alipojenga ule mnara mpaka leo hii hatujui kinachoendelea. Naomba kauli ya Serikali sasa kujua ni lini wananchi wa Kata ya Ibumi watapata mawasiliano ya simu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Ngalawa, Mbunge wa Ludewa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kampuni ya mawasiliano Tanzania (TTCL) ilipewa zabuni ya kujenga mnara wa mawasilinao kwenye Kata ya Ibumi. Mpaka sasahivi ninavyoongea na Waheshimiwa Waunge, mnara huo ulikwishajengwa lakini bado haujawashwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulitokea tatizo la kiufundi katika kuwasha mnara huo, ambapo tatizo hilo sasa limerekebishwa na nimhakikishie Mbunge kwamba ndani ya siku 30, Mamlaka ya Mawasiliano pamoja na TTCL watashirikiana kuhakikisha kwamba changamoto hiyo iliyojitokeza inatatuliwa na watu wa Ibumi wataendelea kupata mawasiliano.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Wilaya ya Kwimba, Kata za Bugando, Mkalalo na Mwabomba kumekuwa na tatizo kubwa sana la mawasiliano na ni la muda mrefu. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka mawasiliano kwenye Kata hizo za Wilaya ya Kwimba ili wananchi hao waweze kufaidika na mawasiliano ya nchi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kemilembe, Mbunge wa Viti Maalum, Mwanza, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Kemilembe kwa jinsi anavyofuatilia masuala ya mawasiliano kwa Mkoa Mzima wa Mwanza ambapo kwa kweli muda mwingi sana amekuwa akifuatilia maeneo mbalimbali ya Mkoa huo. Kuhusu Wilaya ya kwimba ni kweli Mheshimiwa Kemilembe alikuja akaniletea barua kuhusu kata ambazo alizitaja. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Kemilembe na Mbunge wa Kwimba kwamba tayari zabuni kuhusu kata alizozizungumza zimewekwa kwenye kitabu maalum ambapo anaweza akaja mezani kwangu kuangalia. Awamu ya tano tutahakikisha kata zote zilizobakia ambazo hazijapata mawasiliano zinapata mawasiliano.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Bunge la Kumi na hata Bunge hili nimekuwa nikiiomba Serikali irekebishe tatizo la mwingiliano wa simu wa mitandao ya nchi jirani ya Kenya na Tanzania ambayo yanasumbua sana wananchi wangu katika Jimbo la Rombo kiasi kwamba wanajikuta wanatumia huduma za roaming na hivyo kuwa na gharama kubwa sana ya simu bila sababu yoyote. Nimekuwa nikipata ahadi nzuri sana kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba kuuliza, ule mkakati ambao Mheshimiwa Naibu Waziri alikuwa ananiahidi na ameliahidi Bunge, unaendelea na umefikia wapi ili kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA UCHUKUZI (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Selasini, Mbunge wa Rombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumekuwa tukiwasiliana mara nyingi sana kuhusu mwingiliano wa mawasiliano kati ya nchi ya Kenya na nchi ya Tanzania kwa upande wa eneo la Rombo. Sio huyo tu, nimekuwa nikiwasiliana na Wabunge kutoka maeneo mbalimbali ambayo yako mipakani. Tunavyo vikao vya kikanda vinavyohusu masuala ya mawasiliano kwamba Mamlaka za Mawasiliano za nchi mbalimbali katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati huwa yanakutana mara nyingi kujadili masuala hayo ya mwingiliano. Pia kwenye mikutano ya Kimataifa ya ITU pia suala la mwingiliano wa mawasiliano huwa linajadiliwa mara nyingi sana.

Ni kweli kwamba mpaka sasa hivi Mheshimiwa Selasini atakuwa shahidi yangu kwamba upande wa line za Voda kuna marekebisho makubwa sana yanaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna changamoto moja kwamba wenzetu hawaweki minara kilometa tano away from the border, sisi tunaweka kilometa tano away from the border, hilo limeendelea kuongelewa na hivi mwezi wa Pili kuna kikao kingine kikubwa cha kufuatilia utekelezaji wa kampuni za simu kupeleka minara kilometa tano kutoka mpaka ulipo ili angalau mawasiliano yale yaweze kuwahusu watu wanaohusika na nchi tofauti. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Selasini kwamba, tunaendelea na tukimaliza Vodacom pia tutakwenda na tigo, pia tutakwenda na Airtel ili kuhakikisha kwamba wanarekebisha hata zile frequency zao zisielekee nchi jirani ila ziwahudumie Watanzania.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika Mtaa wa Kalimaji, Kata ya Moshono, katika Jiji la Arusha kuna tatizo la mawasiliano ya tigo, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha mawasiliano hayo yanapatikana kwa vile wananchi wanayakosa hayo mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nuru Bafadhili, Mbunge wa Viti Maalum na Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri tumekwishaongea sana na Mheshimiwa Nuru Bafadhili kuhusu suala hilo na bahati nzuri nimekwishamuonesha kwenye vitabu jinsi ambavyo maeneo aliyoyataja tulivyoyaweka na nimpongeze sana kwa jinsi alivyofuatilia maeneo yale mpaka tumeyaingiza kwenye tenda ya awamu ya tano. Nimhakikishie tu kwamba kuanzia mwezi wa Tatu tutatangaza tenda ili makampuni ya simu yaweze kuchukua kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi hiyo na wananchi wa maeneo yale waweze kupata mawasiliano. (Makofi)
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa moja ya vitu ambavyo nchi hii inatakiwa kuwa navyo ni iwe inaelewa mambo mengi yanayohusiana na hali ya hewa kwa sababu tuna vifaa ambavyo vimeunganishwa na satellite duniani lakini kinachosikitisha ni kwamba mara nyingi matukio mengi ambayo yanatakiwa yatolewe kwa tahadhari, kwa mfano tuna tishio la nzige sasa hivi, lakini tuna tishio la kweleakwelea na viwavi jeshi, kwa hali ya hewa inavyoonesha na hali ya hewa ya mvua hicho kitu time yoyote kinaweza kutokea katika maeneo yetu. Sasa matatizo haya huwa yanatokea katika maeneo mengi na hakuna taarifa zinazotolewa. Je, ni lini Serikali itakuwa ina utaratibu wa kuweza kutujulisha kama nchi, yale matukio ya hatari kama haya yanavyoweza kutokea na kuweza kujilinda na kuwa tayari kuweza kukabiliana nayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tumekuwa tukiwasiliana na wenzetu duniani kwa kutumia taaluma ya satellite na ndiyo maana hivi karibuni Serikali imeendelea kuwekeza katika vifaa vya kisasa kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sakata la nzige na masakata mengine ambayo yanatokea huwa tunayaona na bahati nzuri huwa tunatoa taarifa kwenye vyombo mbalimbali vya habari. Hata taarifa zinapokuja huwa zimeanzia kwanza Mamlaka ya Hali ya Hewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taarifa huwa tunakuwa nazo na tunazitoa mapema kabla. Ni vyema niwashauri Waheshimiwa Wabunge kwamba kabla ya kufanya kitu chochote baada ya taarifa ya habari wawe na muda mzuri wa kuangalia taarifa za hali ya hewa ambazo huwa zinatolewa kwa usahihi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya hizo nilizozitaja, vipo vijiji ambavyo ukipiga simu mawasiliano unayoyapata ni ya nchi jirani ya Burundi siyo Tanzania. Kwa mfano, katika Wilaya ya Kakonko ipo Kata ya Mgunzu, kipo Kijiji cha Kigra na Chulazo ambavyo mawasiliano yake ni ya shida. Hata katika wilaya nilizozitaja viko vijiji ambavyo havikuweza kutajwa kwenye jibu la Waziri ambavyo mawasiliano yake bado ya wasiwasi. Je, Serikali iko tayari kuendelea kuhamasisha makampuni kujenga minara katika maeneo hayo ili wananchi waweze kupata mawasiliano ya uhakikika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza Mheshimiwa Josephine Gezabuke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Josephine Gezabuke kwa jinsi anavyopambana kuhakikisha kwamba wananchi katika maeneo mbalimbali hasa ya Mkoa wa Kigoma na maeneo mengine ambayo yapo mpakani ya nchi yetu yanapata mawasiliano ya uhakika bila muingiliano kutoka nchi nyingine za jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kujibu swali lake, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tumeendelea kuwasiliana na nchi jirani ili sheria iliyowekwa kutokana na Mkataba wa East Africa Communication uwe unaweza kutekelezwa vizuri. Utaratibu unataka mnara wa mawasiliano uwekwe kilometa 5 toka eneo la mpaka kwa kila nchi ili wananchi wanaohusika waweze kupata mawasiliano kutoka nchi husika lakini kuna maeneo ambayo kwa nchi za wenzetu wamekiuka utaratibu huo. Katika kikao kinachotegemewa kukaa mwezi Februari, 2020 tunategemea East African Communication wata-resolve suala hilo kwa sababu kuanzia Julai limekuwa likijadiliwa ili kuhakikisha wananchi ambao wanapaswa kupata mawasiliano ya nchi husika wanaendelea kupata bila kuingiliana na watu wengine. Hilo linahusu vilevile na muingiliano wa masuala ya redio. Ahsante.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru Serikali kwa majibu yake mazuri na ya kupendeza. Mheshimiwa Waziri katika jibu lake la msingi amesema kwamba kabla ya kutekeleza suala hili kwanza watafanya utaalam. Je, tathmini hii ya kitaalam itafanyika lini katika kisiwa hiki cha Tumbatu ili kuwapa wananchi manufaa zaidi. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hija, Mbunge wa Tumbatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya kitaalam ambayo tunategemea kuifanya eneo la kisiwa alichokitaja Mheshimiwa Mbunge litakuwa ni sambamba pamoja na tathmini ya kitaalam ya maeneo yote ya mipakani nchini kwetu Tanzania pamoja na visiwa vyote ambavyo vinahitaji kupata mawasiliano. Tathmini hiyo tunategemea kuifanya kuanzia tarehe Mosi mwezi wa kwanza mpaka 2020 katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuhakikisha kwamba maeneo hayo ambayo ni muhimu kwa nchi yetu yote yanapelekwa huduma za mawasiliano.
MHE. ZACHARIA P. ISSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Mwaka 2018/2019, Serikali kupitia Mpango wake wa Bajeti ilipanga minara minne katika Jimbo la Mbulu Mji, katika Kata za Murray, Nahasey, Masqaroda na Gunyoda. Hadi sasa ni mnara mmoja kule Murray umeanza kujengwa. Je, ni lini Serikali itajenga minara mitatu iliyobaki kwenye Kata za Masqaroda, Nahasey na Gunyoda?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mimi mwenyewe nimewahi kutembelea Mbulu Mjini na nikaona maeneo mbalimbali ambayo yana changamoto ya mawasiliano na hasa eneo la Masqaroda, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lile eneo kuanzia mwezi Februari mwanzoni minara itaanza kusimikwa kama tulivyopanga kwa sababu wakandarasi tuliowapatia kazi hiyo wameshatuhakikishia kama Serikali kwamba wameshajipanga kwa ajili ya kuanza kutekeleza kuanzia mwezi Desemba, mwezi Januari na mwezi Februari katika maeneo mbalimbali nchini.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na Serikali kuonesha ina nia ya kusaidia kwenye masuala ya mawasiliano, lakini sote tunafahamu sasa hivi kuna zoezi la usajili wa namba za simu kwa alama za vidole na zoezi hilo linahitaji kuwepo au kuwa na kitambulisho cha Taifa na ukomo wa zoezi hilo ni tarehe 31 Desemba, 2019. Je, Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ina mkakati gani wa kuhakikisha wale ambao hawajapatiwa vitambulisho vya NIDA hasa hasa wananchi wa Mkoa wa Kigoma wanapatiwa hivyo vitambulisho vya NIDA ili itakapofika tarehe 31 Desemba, 2019 Watanzania wote wapate haki ya kuendelea kufanya mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimbaa, Mbunge, Kundi la Vijana kutoka Mkoani Kigoma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Zainab Katimba kwa jinsi anavyopambana kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Zainab kwamba tumejipanga kama Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wanawasiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujibu swali lake, ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ndogo za mwanzo wakati tunaanza zoezi hili tarehe Mosi, Mei, 2019 kuhusu suala la upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA na sisi kwa upande wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, hatuhitaji kitambulisho cha NIDA, tunahitaji namba ya NIDA kwamba unapokwenda kusajili pale unapewa namba maalum. Kitambulisho kinaweza kikachelewa kwa njia moja au nyingine, lakini sisi tunachohitaji ni namba, ukishapata ile namba unakwenda kwa watoa huduma za mawasiliano unasajili kwa alama za vidole. Ni kweli kwamba sehemu mbalimbali watu wamekwishaenda kujisajili na namba zinaendelea kutolewa mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ninavyoongea Watanzania milioni 12,783,000 tayari wameshasajili kati ya watu milioni 44 ambao kwa takwimu za Serikali zinaonesha kwamba wana line za simu. Kwa hiyo naendelea kuwasisitiza na kuwaomba Watanzania tusisubiri mpaka mwisho, mtu mwenye namba ya kitambulisho aende akasajili kwa alama za vidole ili angalau itakapofika tarehe 31 Desemba, tutakapokuwa tumeizima mitambo yetu yeye asikose mawasiliano.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Matatizo yaliyoko huko Tumbatu yako pia katika Jimbo la Manyoni Magharibi, maeneo ya Kintanula, Kalangali, Mnazi Mmoja, Tulieni, Mbugani na baadhi ya maeneo ya Jimbo langu hayana mawasiliano mazuri ikiwemo Itagata na Lulanga. Je, Mheshimiwa Waziri anawahakikishiaje wananchi hao wa Jimbo la Manyoni Magharibi mawasiliano yatapatikana hasa katika Kijiji cha Kintanula lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Massare na Waheshimiwa Wabunge wengine wote ambao wana changamoto za mawasiliano kwenye majimbo yao kwamba kuna tenda ambazo tulitangaza, tenda kwa ajili ya kata 521 nchi nzima ambazo zitategemewa kuhudumia vijiji 122 na hizo tender zilifungua tarehe 3 Oktoba na sasa hivi tuko kwenye taratibu za kuwa wa-award tender kutoka kwa watoa huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Massare na Waheshimiwa Wabunge wengine wote ambao wana changamoto za mawasiliano kwenye majimbo yao kwamba kuna tenda ambazo tulitangaza, tenda kwa ajili ya kata 521 nchi nzima ambazo zitategemewa kuhudumia Vijiji 122 na hizo tenda zilifungua tarehe 3 mwezi wa 10 na sasa hivi tuko kwenye taratibu za kuwa wa-award tenda kutoka kwa watoa huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Massare na Waheshimiwa Wabunge wengine tunaweza kukaonana wakati wowote mezani kwangu pale nikawaonyesha Vijiji ambavyo tayari vimeshakuwa awarded, vile ambavyo bado havijawa awarded kwa ajili ya kwenda kuwekewa huduma za mawasiliano tunategemea mwezi wa kwanza kutakuwa na awamu nyingine kwa ajili ya kumalizia Vijiji vichache vitakavyokuwa vimebakia.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza; kabla sijauliza swali niruhusu nimshukuru Mheshimiwa Spika na Wabunge kwa ujumla kwa namna ya kipekee walivyonifariji mara baada ya kumpoteza mama yangu duniani, nawashukuru sana Waheshimiwa, nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa faraja yako. Swali langu ninalopenda kumuuliza Naibu Waziri changamoto ya mawasiliano ilipo kwenye visiwa vidogo vya Tumbatu inafafana kabisa na visiwa vya delta Wilayani Kibiti.

Je, ni upi mpango wa Serikali kuhakikisha wananchi wa delta Kibiti wanawasiliana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli changamoto ta mawasiliano katika visiwa vya delta inafahamika na kwa kule tumeunda kikosi maalum kwa ajili ya kwenda kutembela maeneo yote ya visiwa vidogo vidogo ambavyo havina huduma ya umeme, pia kufika kwake kuna changamoto. Tumeunda kikosi maalum kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, lakini kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kwenda kutembelea maeneo hayo kwa ajili ya kuangalia namna nzuri ya kufikisha umeme, kwa sababu tumegundua kwamba ukifikisha mawasiliano kama hakuna umeme kunakuwa na changamoto kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunapelekaga kule solar ambazo sio za kufanya kazi muda mrefu. Kwa hiyo, tunaendelea kufanya tathimini ya kina ya kiufundi kuhakikisha kwamba sehemu hizo zinakuwa na huduma nzuri ya mawasiliano. Nikuhakikishie kwamba mwezi wa kwanza mwaka huu sehemu mbalimbali za visiwa na sehemu maalm za Kanda ambazo ni za mipakani zote zitashugulikiwa ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata mawasiliano.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini imekuwa ni kawaida ya Serikali kutupa matumaini halafu masuala haya yanachukua muda mrefu sana. Na ni ukweli usiofichika kwamba bandari hizi zinatumika na bidhaa zinazotoka Zanzibar mara nyingi zinapitia katika bandari hizi. Sasa ninataka kujua, je, kwa nini bidhaa hizi zinapopita kutoka Zanzibar zikipita katika bandari hizi zinatozwa ushuru mara ya pili?

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, ni kusema kwamba kwa kutumia bandari hizi, kwa kuzirasimisha, tutakuwa tunaongeza mapato ya Serikali lakini pia ajira kwa watu wetu zitaongezeka lakini vilevile pia ajali zitapungua. Sasa ni lini ujenzi wa hiyo gati aliyosema Mheshimiwa Waziri na kujenga hivi vituo vya forodha utaanza rasmi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, kwenye majibu yangu ya msingi nimeeleza changamoto iliyopo kwenye bandari bubu na sisi kama Serikali tunaitambua changamoto iliyopo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna majahazi huwa yanachukua bidhaa kutoka upande wa pili wa Jamhuri yetu kuleta upande wa Tanzania Bara, na Serikali kupitia Jeshi la Polisi wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha kwamba biashara hiyo haifanyiki, na sina taarifa za moja kwa moja kwamba huwa wanatozwa ushuru kwa sababu wanatumia bandari bubu ambapo hatuna vituo vyetu vya forodha. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuzidhibiti hizo bandari bubu na tunaendelea kuzidhibiti kuhakikisha kwamba hazileti bidhaa ambazo si rasmi.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili; nimekwishaeleza kwamba kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha tutakuwa tumeshapanga mikakati yote na mwaka ujao wa fedha tutaanza sasa kutengeneza magati kwa sababu ni bajeti kubwa inayotumika katika kutengeneza magati ya kurasimisha hizo bandari bubu.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana. Watanzania wengi wanapata hasara kubwa sana katika hili suala abiria akichelewa boti tu tiketi yake imekufa kabisa hawezi kutumia kwa wakati mwingine wowote inasababisha kadhia kubwa kwa Watanzania wetu.

Hakuna Shirika lolote la Ndege duniani ambalo ukichelewa tiketi yake inakuwa imekufa, unalipa kiwango cha fedha kama ni dola 50 tiketi yako inaweza kuendelea kufanya kazi, hata Shirika letu hili la Tanzania pia hata ukichelewa unaweza kupanda ndege kwa wakati mwingine lakini Kampuni hii ya Azam Marine ukichelewa tiketi imekufa kabisa wala huwezi kutumia tena ni jambo la ajabu sana. Sasa ni lini Serikali itaondosha kadhia hii ili hawa abiria wetu wapate maslahi makubwa kutumia vyombo hivi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, kwanza siyo kweli kwamba mashirika yote ya ndege huwa tiketi yake ukichelewa yanarudishwa kuna zile Easy Jets ambazo kwa mfano Fastjet ukichelewa tiketi huwa haurudishiwi wala haupangiwi safari siku nyingine kwahiyo siyo kwamba ni mashirika yote ya ndege.

Mheshimiwa Spika, pia najaribu kuwashauri hata Watanzania wenzetu unapokuwa umepanga safari basi ujue kwamba kuna muda wa kuondoka na muda wa kufika. Haiwezekani tuwe tuna panga safari halafu unafanya mambo mengine tofauti na safari yako.

Katika majibu yangu ya msingi nimeeleza tu kwamba Shirika la Azam Marine huwa lina utaratibu ukitoa taarifa mapema tena waliandika kwenye tiketi yao nyuma ukitoa taarifa mapema kabla ya safari kwamba hutasafiri wana utaratibu wa kuiuza hiyo tiketi kwa watu wengine ili wewe wakupangie wakati mwingine, lakini sasa muuliza swali Mheshimiwa Mbunge yeye nafikiri anafikiri kwamba akishachelewa bila kutoa taarifa anaweza akapewa, sasa yeye Azam Marine atakuwa ameingia hasara kitu ambacho siyo kweli.

Mheshimiwa Spika, nawashauri Watanzania tupange safari zetu tuwe na uhakika wa kusafiri siku husika, tujiandae, halafu tuweze kuwahi ili tusipate matatizo kama hayo. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Serikali imekuwa ikitoa utaratibu elekezi wa kibei kwa maeneo mengi ya usafiri wa umma kwa wenzetu wenye mahitaji maalum na wanafunzi. Ni upi utaratibu uliowekwa kwenye usafiri wa maji kwa wenzetu hawa wenye mahitaji maalum? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Khadija Nassir kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa vyombo vya Serikali utaratibu upo tunazo meli za MSCL ambao kwa kweli utaratibu wa nauli huwa upo na uko wazi, lakini kwa vile vyombo ambavyo ni vya binafsi ambavyo vinasaidiana na Serikali katika kuhudumia wananchi, huwa tunaacha soko lijipeleke lenyewe, lijiendeshe. Kwa hiyo wale watu wanaomiliki vyombo vya usafiri wa majini huwa wanapanga bei kutokana na faida wanahisi wataipata pamoja na huduma ambazo wanaweza wakawasaidia wananchi.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kutambua jitihada za Serikali katika kuboresha mawasiliano na uchukuzi katika nchi yetu na hasa maboresho yaliyofanyika katika Shirika la Ndege la Tanzania sasa hivi kumeanza kujitokeza tatizo la ucheleweshaji wa ndege. Kila mara unaposafiri ndege inasogezwa, inasogezwa, inasogezwa na hili jambo linakera sana. Chanzo cha tatizo hili ni nini na Serikali mnachukua hatua gani kurekebisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika siku za karibuni kumetokea changamoto ya uchelewaji (cancelation) kwa Shirika letu la Ndege la Tanzania. Tatizo hili limetokana na sababu mbalimbali za kiufundi ambazo zimerekebishwa.

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya kuhitimisha bajeti yetu tulitoa maelekezo Menejimenti na Bodi ya ATCL kwamba kama kutakuwa na cancelation yoyote au delay ya zaidi ya nusu saa tupate taarifa ya maandishi ya sababu zilizobabisha hiyo ndege ichelewe kuondoka kwa zaidi ya nusu saa. Hilo limeshaanza kufanyika na huwa tanapata taarifa.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuwasisitiza ATCL kwamba wateja ndiyo watu wa thamani sana. Kwa hiyo, delay ambazo hazina sababu ya msingi ziepukwe sana.

Mheshimiwa Spika, nikutaarifu wewe na Bunge lako kwamba sasa hivi marekebisho yameshaanza kufanyika. Sasa hivi ATCL wameshaanza kwenda vizuri, delay na cancelation ambazo sio technical hazitokei tena.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Adhabu ya kaburi aijuaye maiti. Sisi tunaosafiri na Azam ndiyo tunafahamu adha yake.

Mheshimiwa Spika, hata ukisafiri na ile charter ya abiria 11 mzigo wa kilo 15 - 20 hulipishwi lakini ndani ya boti ya Azam unalipishwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri achukue mfuko mmoja wa mchele tuliogawiwa asafiri nao aone kama hatalipishwa. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ifuatilie suala hili na itupatie ufumbuzi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, suala la huduma ya safari za majini mara nyingi ni kati ya abiria na mwenye mali. Ukifugua nyuma ya tiketi ile kuna masharti ambayo yanaandikwa kwa uwazi na kwa lugha nyepesi kabisa. Ninawashauri sana Watanzania tuwe tunasoma masharti yale ili kama ukiona hayakidhi mahitaji yako basi usiende. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nyuma tiketi ya Azam kuna maelezo yanayoeleza mpaka kiwango cha mzigo unachotakiwa kwenda nacho ndani ya meli. Sasa anayepima ni yule mwenye meli kama imezidi anaruhusiwa kukukatalia kwa sababu ndiyo mkataba ulioingia wewe abiria na yule mwenye meli. Kwa hiyo, nawashauri Watanzania tuwe tunasoma vigezo na masharti vya kuingia kwenye huduma hizo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Tabora kuna karakana kubwa ambayo ipo tangu wakati wa mkoloni na kwa kuwa sasa kuna ujenzi wa standard gauge. Je, Serikali iko tayari sasa kuboresha karakana hiyo kupeleka mitambo ya kisasa ili iendane na treni hiyo ambayo ni ya kisasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunayo karakana kubwa kabisa ya matengenezo ya vichwa vya treni maeneo ya Tabora na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia TRC bado ina mpango wa kuendelea kuirekebisha karakana ile na tunamhakikishia kwamba tutaongeza vifaa na iko kwenye mpango ambao tunakwenda kuutekeleza kuanzia mwakani mwezi wa pili.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, mbali na Isaka kuwa dry port, stesheni ya Bukwimba ambayo iko Wilaya ya Kwimba tulishaomba kupitia TPA/kupitia TRL. Tunataka kujua sasa Mpango ni lini sasa mpango huo wa kuweka dry port katika Stesheni ya Bukwimba utafanyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, ahsante, Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Ndassa, Seneta, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara nzima kwa ujumla, naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Ndassa kwa jinsi anavyofuatilia masuala ya miundombinu katika Jimbo lake na nchi nzima kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipende tu kumjibu Mheshimiwa Ndassa kwamba eneo la Bukwimba lipo kwenye mipango ya Shirika la Reli pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kwa ajili ya kujenga bandari kavu, sasa hivi tunachosubiri ni ile layout plan ya watu wa Wilaya ya Bukwimba ambayo tukishaipata tutaweka layout plan yetu tena ndani ya eneo hilo kwa ajili ya kujenga hiyo dry port.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu yaliyokuwa na uhakika kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo mawili.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hapo zamani stesheni ndogo ndogo za reli zilikuwa zina stawi sana miji yake kutokana na kwamba reli zilikuwa zinasimama kwa mfano Stesheni ya Mpiji na Stesheni ya Kikongo na nyinginezo hadi Mwanza, Kigoma na Tabora na kwa kuwa ujenzi huu wa reli sasa hivi hakuonyeshi dalili ya kwamba kutakuwa na treni itasimama.

Je, kuna mpango gani na mkakati gani angalau kwa Stesheni ya Kikongo ambayo stesheni hiyo inaunganisha barabara inayotoka Makofia hadi Mlandizi, Mlandizi hadi Mzenga, Mzenga hadi Mwanarumango, Serikali haioni kwamba barabara hii na stesheni hii ikiboreshwa na treni zikasimama itasaidia kusafirisha abiria na mizigo ambayo wananchi wanataka kuipeleka kokote kule? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali na ninaishukuru na kuipongeza, imepanga Stesheni ya Soga na Kwala kuwa stesheni kubwa; je, Serikali haioni sasa kuna haja na umuhimu wa Halmashauri hizo kupewa ardhi, ardhi hiyo ikapimwa, ikagaiwa kwa wananchi, wananchi hao wakajenga na wakawa na miradi ambayo itaendeleza ule mji na wao kuwapatia kipato? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ametaka kujua status ya vituo vya zamani kupitia meter gauge. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro ambako tunapitia Mkoa wa Pwani kuna vituo vya zamani 14. Nimhakikishie tu kwamba vile vituo vitaendelea kuboreshwa kupitia mradi wa TIRP ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa dola milioni 300 na mpaka sasa hivi vimekwishaanza kurekebishwa na kuwekwa katika hali nzuri. Reli itakapokuwa inapita ile meter gauge itahudumia vituo vyote vile 14 kati ya Dar es Salaam mpaka Morogoro.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa SGR kuna vituo sita, Dar es Salaam mpaka Morogoro kuna vituo sita, vinne viko katikati na kimoja ni cha Dar es Salaam na kingine ni cha Morogoro. Vinne kuna Kwala, Soga, Kingolwira na Ngerengere. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kuunganisha vituo hivyo na vile vituo vya zamani unaendelea vizuri na reli ya kisasa inayojengwa kwa asilimia 70 itakwenda na ile reli ya zamani ya meter gauge.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili, Mheshimiwa alitaka kujua suala la upimaji wa ardhi kwa ajili ya maeneo yale. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mamlaka ya Mji wa Kibaha kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi wamekwishaendelea kupanga mji ule wa maeneo ya Kwala, Soga na Kingolwira kwa ajili ya kuwa-accommodate watu watakapata viwanja pale. Kwa sababu vituo vile vitakuwa ni vya kisasa ambavyo vitakuwa na huduma zote za kijamii na tunategemea hata wananchi nao waende wakae pale maeneo yao kwa ajili ya kufanya shughuli za kijamii.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ujenzi wa reli uendane sambamba na ujenzi wa barabara hasa kwa maeneo yenye misongamano mkubwa wa abiria na mizigo. Kwa mfano barabara ya Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro, ile barabara ina hali mbaya sana, ina msongamano mkubwa wa magari na inatumia masaa matano hadi sita kwa basi la abiria. Serikali ilikuwa na mpango wa kujenga barabara (highway) barabara sita, kutoka Dar es Salaam mpaka Chalinze – Morogoro na sasa hivi imesitisha.

Sasa nataka kusikia kauli ya Serikali, je, lini itafufua tena mpango huu wa ujenzi wa hii barabara ili kuondoa kadhia hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, Serikali haijasitisha ujenzi wa barabara njia sita ya kutoka Dar es Salaam kuja Chalinze, isipokuwa ujenzi unaendelea kwa hatua na hata juzi tu nimefanya ukaguzi wa barabara. Ile barabara ya kutoka Kimara kuja Kibaha sasa tuko 28% na mkandarasi anaendelea kulipwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Mlinga uvute tu subira kwamba tumejipanga vizuri kadri tunavyopata fedha, tunaendelea na harakati za ujenzi wa barabara hiyo. Hata hivyo, tunaendelea kufanya maboresho mbalimbali maeneo ambayo yanakuwa na uharibifu kwa sababu ni kawaida maeneo ambayo yanaharibika Serikali tunaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanya maboresho mbalimbali ili barabara ipitike wakati tunaendelea na hatua upanuzi wa barabara.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na malalamiko makubwa ya wamiliki wa mabasi juu ya upatikanaji wa mkandarasi aliyefunga mfumo huu lakini wenye mabasi wanalipia kwa kila basi tozo ya Sh.60, 000 kwa mwezi kwa kila basi, tofauti na wenzetu nchi jirani ambao wanalipia Sh.120,000 kwa kampuni nzima. Swali langu, Serikali inanufaika vipi na tozo hii ya kinyonyaji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inasimamia maeneo mengi ambayo fedha za Serikali zinaingia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba imedhibiti upatikanaji wa maduhuli ya Serikali. Ni kwa nini Serikali isihamishie mfumo huu Police Traffic ili wakauendesha na Serikali ikawa na uhakika wa kupata hayo maduhuli yake yote kuliko kwa njia hizi za panya na malalamiko kama ilivyo sasa hivi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Selasini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tozo zinazotozwa kwa ajili ya kufanya service ya VTS kwa mabasi mbalimbali ilikuwa ni kikao kati ya wamiliki pamoja na wakandarasi mbalimbali ambapo wamiliki waliwapendekeza kwa SUMATRA kwa ajili ya kufanya service hiyo. Kwa hiyo, pale SUMATRA haikuingilia mapatano kati ya wenye mabasi na wamiliki. Hata hivyo, kama kutakuwa na mapendekezo ya wenye mabasi kutaka aina nyingine ya mfumo wa kufanya service ya vifaa hivyo sisi kama Serikali tuko tayari kupokea na tutawashauri SUMATRA waweze kutekeleza.

Mheshimiwa naibu Spika, kwenye swali lake la pili, Serikali inaendelea kudhibiti mapato kupitia vyanzo mbalimbali lakini inaendelea kutengeneza wigo mpana wa kushirikisha hata sekta binafsi nazo kuweza kufanya shughuli kama hizo.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na sasa naomba kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa bado kuna vijiji ambavyo havijaweza kupata minara ya mawasiliano kama vile Kijiji cha Kititiza, Kikoi, Mkalinza Kata ya Mabawe na maeneo mengine ya Jimbo la Ngara, ni lini Serikali itaweza kuwezesha ujenzi wa minara katika maeneo hayo yaliyobaki? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, baadhi ya maeneo hususan katika Kata za mipakani kama vile Kata ya Kabanga, Mabawe, Rusumo, Kata ya Kasulu, Kata za Mipakani zinazotokana na nchi ya Burundi na Rwanda, usikivu umekuwa ni hafifu na hata kuwepo na mwingiliano wa mitandao ya nchi jirani. Je, Serikali ina mkakati gani kumaliza tatizo hili la mwingiliano wa mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Gashaza kwa ajinsi anavyofanya bidii kubwa sana kushughulikia wananchi wake kupata mawasiliano. Nikianza na swali lake la kwanza Vijiji vya Mabawe, Kititiza na Kigoi tunategemea kuviingiza kwenye mpango wa vijiji 811 ambavyo tunategemea kuvitangaza hivi karibuni kwa ajili ya kupatiwa huduma ya mawasiliano kabla ya mwezi wa tatu mwakani. Kwa hiyo, namuomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira vijiji hivyo vitapatiwa mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, ni kweli kwamba bado tuna changamoto kubwa kwenye maeneo ya mipakani ambapo mawasiliano yamekuwa yakiingiliana kati ya nchi jirani na nchi yetu. Hata hivyo, tumechukua hatua za dharura kwa kuwaelekeza TCRA washirikiane na mamlaka za mawasiliano za nchi jirani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mwingiliano huo unapunguzwa au kuondolewa kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huo umefanyika Mjini Arusha mwezi wa Nne kupitia kikao chao cha East African Communication (EACO) ambapo umeshaweka mkakati na kwa kuanzia maeneo ya mikoa ya Moshi na Kagera Vodacom wameshaanza kurekebisha mwingiliano wa mawasiliano ili kuhakikisha kwamba kila nchi inapata mawasiliano ambayo anahusika nayo badala ya kufanya roaming.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali lakini kwa umuhimu wa kipekee wa biashara ya bandari yetu na nchi jirani naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni bandari shindani na bandari yetu ya Dar es Salaam zimekuwa zikiongeza jitihada za kuhakikisha kuwa wanafikisha huduma kwenye maeneo ambayo yalikuwa ni miliki ya bandari yetu ya Dar es Salaam hada DRC Katanga, Zambia na Malawi. Kutokana na ushindani huo biashara yetu ya shehena kwenda maeneo hayo kwa Zambia imepungua mpaka asilimia 25 sasa hivi, na vilevile kwa DRC Katanga nako ni chini ya silimia 25; ni asilimia 21 kutoka asilimia 40. Sasa swali langu nauliza, pamoja nakuboresha na ujenzi wa Bandari Kavu ya Inyala;

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga sasa barabara ya kutoka Mbalizi – Shigamba – Isongole ambayo inapitia katika eneo la Bonde la Songwe na kwenda mpakani na Malawi?

Ni lini itajenga reli ya TAZARA kutoka Tunduma kwenda Bandari za Ziwa Tanganyika kwa ajili ya biashara yetu na DRC Katanga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Oran Njeza kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala ya kimkakati ya eneo lake. Ni kweli kwamba wananchi wa Mbeya Vijijini wamepata Mbunge jembe ambaye sidhani kama atakuwa na mpinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ametaka kujua mpango wa Serikali wa kuimarisha barabara ya kutoka Mbalizi – Shigamba kwenda Isongelo ambayo itaunganisha na Wilaya ya Ilenye ukoje. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kwa mwaka ujao wa fedha tumeshatenga fedha kwa ajili ya kufanya upembezi yakinifu, kisha tutafanya na usanifu wa kina kwa ajili ya kuiimarisha barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Kwa sababu tunajua kwamba kujenga Bandari ya Inyala bila ya kuwa na barabara ambayo ni imara itakuwa haiwezi kusaidia, kwa hiyo tunamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaijenga kipande hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye swali lake la pili anataka kujua kipande cha reli kitakachojengwa kutoka Tunduma hadi Bandari ya Kasanga Ziwa Tanganyika. Ni kweli kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania wanashirikiana na TAZARA kuhakikisha wanaweka miundombinu itakayokuwa wezeshi na rahisi kidogo kufikia Bandari ya Kasanga, Hivyo, kwa sasa wameshaanza upembuzi yakinifu wa kuhakikisha kwamba kipande cha reli kinatandikwa na watakapomaliza upembuzi yakinifu watafanya usanifu wa kina kupata gharama kwa ajili ya kupanga bajeti sasa ya kutekeleza mradi huo. (Makofi)