Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye (12 total)

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba miaka ya 1990 tulipokea wakimbizi kutoka Burundi na wakawekwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nduta. Baada ya hali ya amani kurejea, ile kambi ilifungwa, Serikali ikawapatia wananchi kuanzisha kijiji cha mfano cha Nduta.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakimbizi hali ya amani iliyokuwa siyo nzuri tena Burundi, wakimbizi tena walirejea na Serikali ikawaomba wale wananchi waondoke kwa ahadi kwamba itawalipa fidia. Sasa ni lini wananchi hao watalipwa fidia yao? Swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ujio wa wakimbizi mara nyingi pamoja na mambo mengine huwa ina athari za kimazingira na kimiundombinu hasa barabara na maji. Kuna ombi ambalo Kiwilaya tulitoa na Serikali ya Mkoa ikatuunga mkono kuhusu miundombinu ya maji kwa kuwa ujio wao umesababisha kuongezeka kwa watu wanaotumia miundombinu ile ile ya maji na barabara…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa naomba uulize swali tafadhali.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri anajua, juzi juzi alikuwa Kibondo na akajua kwamba tumepeleka ombo UNHCR kwa ajili ya kupata maji.
Je, Serikali imefanya msukumo gani hadi sasa hivi ili tuweze kupatiwa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilifanya ziara hivi karibuni huko kwenye kambi za wakimbizi na katika ziara hiyo pia tulikutana na maandamano ya wananchi ambao walikuwa wana madai ambayo Mheshimiwa Mbunge ameeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatua ambayo tumechukua ni kuweza kuzungumza na UNHCR ili waangalie uwezekano wa kuwalipa; siyo fidia lakini ni kama kifuta machozi. Kwa sababu kwa mujibu wa taratibu, wale wananchi waliruhusiwa kulima pale, lakini eneo lile ni miliki ya Serikali na limetengwa maalum kwa ajili ya kuhifadhi wakimbizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Engineer Nditiye kwamba mazungumzo ambayo tumefanya na UNHCR yameonekana kuzaa matunda na tunatarajia kwamba wananchi hawa wanaweza wakapatiwa kifuta jasho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la huduma za jamii, moja katika mikakati mikubwa ya Serikali ambayo hata Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya Ziara katika maeneo hayo, alitoa msisitizo muhimu wa maeneo ambayo wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka kambi za wakimbizi kuweza kufaidika na huduma mbalimbali za kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Nduta, kwa mfano sasa hivi UNHCR wamekubali kutoa nusu ya mahitaji ya madawati yanayohitajika katika maeneo hayo, lakini pia tumefanya nao mazungumzo kuhakikisha kwamba katika maeneo ya huduma za maji na afya wanaweza kutoa michango yao ili wananchi waweze kufaidika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani kabisa kwamba baada ya mazungumzo hayo tunaweza kuona mafanikio kuhusiana na miradi ya maji katika maeneo hayo.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Mimi nilitaka kujua kuhusu kipande cha barabara kutoka Kibondo kwenda Mabamba kilometa 45 ambacho Mheshimiwa Waziri alizungumza kwamba kitajengwa kwa kiwango cha Lami. Lakini katika vitabu vyake vya bajeti imetengewa milioni 80, hiyo ni kwa ajili gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Kibondo hadi Mabamba ilitolewa ahadi na viongozi wetu, ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Na mimi naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi hii tutaitekeleza na wala asiwe na wasiwasi. Fedha tulizozitenga za shilingi milioni 80 anazoziongelea ni kwa ajili ya ukarabati mdogo mdogo si kuanza ujenzi. Ujenzi wa kipande hiki tutaufanya kadri uwezo wa kifedha tutakapokuwa tunajaliwa.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Ninaamini Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba zahanati karibu nane zimekwishapata umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Kwanza na ya Pili, lakini hazijaunganishwa.
Je, ni lini Wizara ina mpango wa kuunganisha umeme kwenye Zahanati hizo nane?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa hospitali alizotaja za Kibondo na Kasulu zote zimeunganishwa na umeme lakini hazijawashwa. Utaratibu wa kuwasha hospitali zote za Mkoa wa Kigoma na Mikoa mingine ya jirani zinafanyika mwezi wa 11 na 12 mwaka huu wa 2016.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kujua, kwa kuwa sekondari nyingi sasa zina maabara na baadhi ya sekondari hizo kata zake zimekwishapitiwa na umeme, lakini Sekondari hazina umeme ni jukumu la Wizara au ni nani mwenye jukumu la kuingiza umeme kwenye shule hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge juu ya mchakato wa shule hizi za sekondari ambazo zina maabara. Ni kwamba katika mchakato wa utengenezaji wa bajeti za Halmashauri, Halmashauri inatakiwa itenge bajeti ya kutosha kwa ajili ya uwekaji wa umeme katika shule hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo Waziri wa Nishati na Madini wiki iliyopita alizungumza wazi kwamba tutaweka kipaumbele kwa kupitia Wizara ya Nishati na Madini, kuhakikisha kwamba Halmashauri zinafanya hivyo. Pia Wizara ya Nishati na Madini itaweka kipaumbele ili shule hizi zote ziwe na umeme katika nchi yetu.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Katika Wilaya yangu ya Kibondo, Jimbo la Muhambwe, kuna Chuo cha MCH ambacho kwa muda mrefu sasa karibu miaka mitano wamejaribu kujenga maabara, wamekwishafikia mpaka ngazi ya kupaua, wamekwishaweka mbao mwaka wa pili na nusu sasa na hakijapauliwa. Ni lini Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya kupaua jengo hilo la maabara?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini? Ni pale ambapo uwezo wetu wa kibajeti utaruhusu.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya kutia moyo ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa migogoro ya ardhi katika Halmashauri zetu na hasa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo imekuwa mingi sana, je, Serikali ina mpango gani wa kuziwezesha ofisi za Kanda ku-speed up utoaji wa hati ili kupunguza migogoro ya ardhi? (Makofi)
Sehemu ya pili, moja kati ya vitu vinavyosababisha migogoro mikubwa sana ya ardhi, hasa mijini ni uwepo wa baadhi ya watumishi wa Idara ya Ardhi wasiokuwa waaminifu katika Halmashauri zetu, watumishi hawa wamekuwa wakikaa muda mrefu sana sehemu moja ya kituo cha kazi. Je, Serikali ina mpango wowote wa kuwabadilisha mara kwa mara ili kujenga mahusiano mazuri kati ya wananchi na watumishi hao wa Idara ya Ardhi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikiwezesha Ofisi za Kanda na tuna Kanda nane na zote zinafanya kazi hiyo ya usajili kama alivyosema, pengine labda kama kuna eneo ambalo lina upungufu na kazi hazifanyiki vizuri tungeomba kufahamu, kwa sababu ninavyofahamu mimi Kanda zote nane zinafanya kazi ya usajili na ndiyo maana tumefanya hivyo ili kurahisisha usajili katika maeneo hayo. Kwa hiyo, kama kuna sehemu kuna tatizo basi ni vizuri tukafahamu maaana lengo la Serikali ni kurahisisha na kupunguza ule muda wa kusubiri, kwa sababu sasa hivi ndani ya mwezi mmoja tunasema hati inakuwa imeshasajiliwa. Lakini kama lengo letu halifikiwi maana yake kuna tatizo mahali fulani, sasa nitashukuru sana Mheshimiwa Mbunge kama atatuambia kwamba pengine kanda hiyo ambayo anatoka yeye hakuna ufanisi mzuri katika suala zima la usajili.
Mheshimiwa Spika, swali la pili anasema uwepo wa watumishi wasio waaminifu na wa kukaa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, nadhani ni azma ya Serikali kuona kwamba watumishi wanapokuwa katika maeneo wanafanya kazi zao kwa uadilifu na weledi mkubwa kama ambavyo dhamana hiyo wamepewa. Lakini pale inapotokea pengine mtumishi amekaa eneo moja muda mrefu na amekuwa mzoefu kawa kama ni mwanakijiji katika eneo lile au ni mwanamji wa pale na ameshindwa kufanya kazi aliyoifanya, basi tutawasiliana na Wizara husika ili tuweze kuona nini cha kufanya. Kwa sababu kumhamisha pale kama ameshindwa kufanya kazi na kumpeleka eneo lingine unakuwa hujamsaidia, kama ana tatizo kubwa basi tujue tatizo lake ni nini ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa. Pengine kuwahamisha tu inaweza ikawa siyo solution, lakini kikubwa ni kujua madhaifu yake ni nini ili tuweze kuona hatua za kinidhamu kuweza kumchukulia mtumishi kama huyo.
MHE. ENG. ATASHASTA J.NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru sana, jina langu ni Atashasta Justus Nditiye au Engineer Nditiye inatosha. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wazawa Green Field Plantations walianza mchakato wa kufuatilia eneo hilo toka mwezi wa pili mwaka jana na tuliwapa ushirikiano namshukuru sana Mkuu wa Wilaya pamoja na wananchi wa Jimbo la Muhambwe, lakini ilipofika mwezi wa nane ameondoka mpaka sasa hivi ninapoongea hajarudi. Tunadhani ni muhimu sana tupate mwekezaji competitor kwa ajili ya ku-speed up suala la yeye kuja kufanya shughuli za uwekezaji kama tunavyotarajia ili wananchi wasije wakakata tamaa. Ni lini Serikali inafikiria kutafuta mwekezaji mwingine ikiwezekana hata wa kutoka nje ili kuweza kuwekeza katika Kiwanda cha sukari? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika kuelekea kwenye sera ya viwanda katika nchi yetu tuna wabunifu wengi sana na katika Wilaya yetu ya Kibondo kwa mfano, kuna kijana amebuni magodoro yanayotumia mifuko ya plastic na kila alipojaribu kuwasiliana na COSTECH kwa ajili ya ushauri wamekuwa hawampi ushirikiano wa kutosha. Ni lini Serikali inajipanga kuwaongezea uwezo COSTECH ili wanapopata maswali kutoka kwa wabunifu wadogo wadogo waweze kuwatembelea na kuwapa ushauri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata taarifa kwamba hapa mwekezaji aliondoka na hajarejea na kama alivyosema Serikali yetu ya Awamu ya Tano ni Serikali ya viwanda. Tutamleta mwekezaji mwingine kama alivyosema na siyo mmoja bali wawili, watatu kuongeza competition na ufanisi hilo nimelichukua na Serikali inalifanyia kazi, watakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ubunifu na COSTECH; kwanza nikiri kwamba huyo mwanafunzi na nimwambie Mheshimiwa Mbunge mwanafunzi huyo ni mwanafunzi wangu niliyemfundisha Masters Chuo Kikuu Mzumbe. Namfahamu na tulimfundisha na sasa anaendelea na ubunifu huo na COSTECH pamoja na Chuo Kikuu Mzumbe tumepanga kumuendeleza mwanafunzi huyo pamoja na wabunifu wote wanaoibuka ndani ya Nchi yetu.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Gereza kuu la Wilaya ya Kibondo pamoja na kuhudumia Watanzania na mahabusu kwa wafungwa, linahudumia vile vile mahabusu na wafungwa kutoka nchi jirani ya Burundi kwa maana ya Wakimbizi kwa wingi sana. Lina upungufu mkubwa sana wa maji na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la UNHCR liliahidi kwamba litasaidia kuleta mradi wa maji kwa Gereza lile na taarifa tulishazitoa mpaka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Je, Srikali imefikia hatua gani kuwalazimisha sasa wale watu wa UNHCR walete maji katika Gereza hilo la Kibondo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nampongeza Mheshimiwa Nditiye kwa kufuatilia jambo hili na mara kwa mara tukionana, amekuwa akinikumbushia jambo hili hili. Nimwambie tu kwamba, kati ya wiki hii mpaka wiki ijayo, timu ya Wawakilishi wa Shirika la Wakimbizi Duniani hapa kwetu nchini, pamoja na wadau wanaoshughulikia masuala ya wakimbizi, watazungukia Mkoa wa Kigoma, watazungukia makazi likiwemo Gereza hilo na moja ya ajenda kubwa wanayokwenda kufanya ni kuangalia miundombinu jinsi inavyoweza kusaidia uwepo wa watu wengi katika Makambi pamoja na Magareza kama hilo ambalo amelitaja.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo ndiyo hospitali vilevile inayotumika kama Hospitali ya Rufaa kwa Wilaya ya Kakonko, lakini inatumika kama Hospitali ya Rufaa kwa wakazi kutoka nchini Burundi, kwa maana ya wakimbizi wapatao laki mbili. Serikali ina mpango gani wa kuongeza majengo kwenye hospitali hiyo ambayo hayajawahi kuongezwa kutoka mwaka 1971?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa sababu hiyo hiyo Serikali ina mpango gani wa kuongeza mgawo wa dawa ili kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi wa Wilaya ya Kibondo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hospitali ya Mheshimiwa Mbunge ya kama Kibondo, ni kweli na mimi nilifika tulienda kukagua hospitali ile, kuna changamoto ya miundombinu pale na hata wenzetu wa Kakonko kwa mwalimu wangu pale, mara nyingi sana wanatumia kama ndio referral hospital yao katika eneo lile, changamoto hizo tumeziona. Siku ile nilivyokuwa pale site niliwaambia waangalie upungufu uliokuwepo (needs assessment) maana hata vifaa tiba na X-Ray lilikuwa ni changamoto na nilitoa maelekezo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, imani yangu ni kwamba wenzetu pale Halmashauri watafanya hiyo needs assessment ambapo mchakato utaanza katika vikao vya Halmashauri, tutaangalia nini kwa pamoja kitafanyika kwa ajili ya kuboresha hospitali ile kwa sababu idadi ya wagonjwa niliyoikuta pale ni kubwa sana na ni kweli anachosema Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, Serikali inasubiri jinsi gani michakato itawekwa katika kipaumbele cha Halmashauri yenyewe na sisi tutaweka nguvu kwa kadri iwezekanavyo ili hospitali ile iweze kutoa huduma vizuri.
MHE. MHANDISI ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba tu kwanza nimpe taarifa tu kwamba maji yalitoka ndani ya miezi sita tu kama na siku nane halafu mpaka sasa hivi toka 2010 lile gereza halina maji ya uhakika na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati huu mradi unatengenezwa kipindi kile tulikuwa hatuna wakimbizi sasa hivi ninapoongea 2015 tumepokea wakimbizi 120,000 na kati ya hao kuna wahalifu mbalimbali ambao nao wanatumia gereza hilo hilo ambalo kipindi hicho kulikuwa na upungufu wa lita 39,000. Tunapozungumzia kwamba maji ni uhai na kwa kuwa na idadi ya wafungwa sasa imeongezeka, Serikali ina mpango gani wa dharura hata wa kuwashirikisha UNHCR ambao ndiyo wana dhamana ya wakimbizi katika kutatua tatizo hilo? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sheria inawapa kinga wafungwa wa kisiasa na wafungwa wengi ambao wanatoka kwa wakimbizi siyo wa kisiasa, ni wafungwa wa makosa ya kawaida na kwa kuwa sasa wameanza kurudishwa makwao, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuwarudisha wale wafungwa ambao wako kwenye gereza ili kupunguza idadi ya wafungwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kuhusu ushauri wake wa kulichukulia kwa uzito unaostahili tatizo hilo ambalo yeye kwa kuwa ni Mbunge amekuwa karibu na gereza na ameona shida hiyo inaathiri vilevile wananchi la kuhusisha UNHCR ni wazo zuri na tutalichukua. Tumekuwa tukishirikiana na UNHCR kwa miradi mbalimbali ya maendeleo hasa katika maeneo ambayo wilaya/majimbo/vijiji vilivyopo karibu na maeneo ya wakimbizi ikiwemo maji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatuoni kwa nini tusichukue na hili jambo tukaliingiza katika mpango huu hasa ukitilia maanani ni juzi tu Mheshimiwa Makamu wa Rais amezindua mpango kabambe ambao utaweza kuwanufaisha zaidi wananchi wanaohusika katika maeneo ambayo wakimbizi wanaishi. Kwa hiyo, ni wazo zuri ambalo tumelichukua kwa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja yake ya wafungwa ambao wamefungwa kwenye magereza, tuna utaratibu wa kubadilishana wafungwa katika nchi mbalimbali ambao upo kabisa kisheria na kupitia utaratibu huo hilo jambo linafanyika. Kwa hiyo, siyo jambo geni limekuwa likifanyika miaka yote tu.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa miaka mingi sana hadi mwaka jana mwanzoni, wananchi waliruhusiwa kufanya shughuli za uvuvi ndani ya hifadhi pamoja na ufugaji nyuki. Lakini toka mwaka jana mwanzoni Serikali ilipiga marufuku na wananchi wakiingia kule wananyanyaswa sana ikiwa ni pamoja na kupigwa na wafanyakazi wa Idara ya Wanyamapori na Wahifadhi.
Je, ni lini Serikali itaruhusu wananchi, waendelee kufanya shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, itajenga mahusiano mazuri kati ya Serikali na wananchi?
Swali la pili, sehemu kubwa ya hifadhi hiyo ya Moyowosi haina alama kwenye mipaka yake na kwa kuwa wananchi wanakuwa wakinyanyaswa sana kwa ajili ya kufanya shughuli zao ambazo walikuwa wamekwisharuhusiwa na Serikali, ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuweka alama hizo za mipaka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza wakati Serikali imetoa ruhusa ya kufanya shughuli zile za uvuvi na ufugaji nyuki, ruhusa ile ilizingatia masharti ya kitaalam kwamba shughuli hizi za kibinadamu kwa kiwango hicho ambacho kiliruhusiwa kilikuwa hakiathiri shughuli za uhifadhi katika eneo linalohusika na kwamba utaratibu huo, utaendelea kutumika pale itakapoonekana kwamba kuna umuhimu wa kufanya hivyo kwa ushauri wa wataalam.
Hivyo basi, ningeweza kusema kwamba tutakwenda kuangalia eneo hili specifically sasa hivi, mahsusi lakini kwa kuwa nimeishatangulia kusema kwamba Serikali tayari inao mpango wa kushughulikia masuala haya kimkakati zaidi, basi nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira kidogo, twende tukayaangalie yote hayo kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya swali lake, kuhusiana na kwamba eneo kubwa au sehemu kubwa haina alama, hii ni mojawapo ya changamoto ambayo inasumbua masuala ya uhifadhi kwenye maeneo yetu kwamba maeneo mengi alama zake ziko kwenye kumbukumbu za kitaalam, unazungumzia coordinates kwa mfano. Coordinates kwa mtumiaji wa kawaida mwanakijiji ambaye anapakana na eneo hilo si alama ya kutosha kuweza kumfanya mwananchi huyo aweze kutii Sheria vizuri zaidi.
Kwa hiyo, tunaposema tunakwenda kushughulikia kimkakati zaidi, ni pamoja na kwenda kuweka alama za kudumu lakini zinazoonekana vile vile. Lakini pia zitakazoshirikisha wananchi wanaoishi au jamii zinazoishi kwenye maeneo hayo, ili tukubaliane kwamba kuanzia hapo sasa huo ndio mpaka, na mpaka huo utakuwa unaonekana vizuri, na kila mmoja atalazimika kuuheshimu.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mepesi mepesi ya ndugu yangu Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, inaonyesha jinsi ambavyo mtiririko wa project management engineering pattern usivyokuwepo katika majibu yake ya swali ya msingi. Haiwezekani leo Serikali inapanga kuchukua kufanya usanifu wa kina na kuandaa vitabu vya zabuni halafu wakati huo huo mtaalam mshauri anaendelea na usanifu ambao unatakiwa kwisha mwezi Julai, 2017, wakati mtu wa Environmental Impact Assessment hajafanya kazi yake. Hiyo inanipa mashaka kama kweli huu mradi upo au haupo. Sasa naomba Serikali itoe tamko kama kweli huu mradi upo na utaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, amezungumzia kiasi cha shilingi milioni 300 zilizotolewa kwa ajili ya Mji wa Kibondo kupanua miundombinu. Hata hivyo, ninayo uhakika na yeye Mheshimiwa Naibu Waziri niliwasiliana naye mwezi wa Aprili mwanzoni, kwamba kuna milioni 300 zilizotolewa kwa ajili ya Mji wa Kibondo toka mwaka jana bajeti iliyopita hii tunayoimalizia, lakini ziliendelea kuchezewa chezewa pale Mkoani mpaka sasa hivi tunavyoongea pesa haijaenda Kibondo. Lakini tunaambiwa tuna milioni 300 zina…

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nijue hiyo milioni 300 anayoizungumza kwamba itatolewa mwaka huu ni ile tuliyodhulumiwa Kibondo mwaka jana au inakuwa carried forward au ni ya mwaka huu? Naomba kujibiwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa amesema majibu ni mapesi, mtiririko wa mipango hauonekani vizuri ni kweli. Moja, tunataka kwanza tuwe na chanzo na chanzo ni Malagalarasi. Usanifu unaofanyika ni wa kutoa maji mto Malagalarasi kuleta Kaliua, Urambo na Tabora. Chanzo hicho hicho kikishakamilika ndiyo kitachukua maji kupeleka katika Jimbo lake ndiyo maana kidogo inamchanganya Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba mradi upo tukishakuwa na chanzo cha maji tayari kitakachobaki ni kuweka fedha kufanya utafiti mdogo wa kuyatoa maji kwenye chanzo ambacho kipo na kuendelea kukipeleka katika Jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na shilingi milioni 300, ni kweli, tulishaliongea hili nje na Mheshimiwa Mbunge, nikajaribu kufuatilia nikakosa majibu na juzi nilikuwa Kigoma. Hata hivyo, nimhakikishie kwamba sasa tutaunda Tume ndogo ili kuweza kuangalia kuhusu hizi shilingi milioni 300, moja je, ni kweli zilitolewa, na kama zilitolewa ziko wapi? Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge hapa hakiliwi kitu, kama kuna mtu atakuwa amefanya fujo, taratibu na Sheria za Kiserikali zipo atashughulikiwa. (Makofi)