Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Albert Ntabaliba Obama (3 total)

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwanza nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Buhigwe, kupongeza Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi. Kwanza pongezi zimuendee Mheshimiwa Rais mwenyewe, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kuikazania barabara hii alipokuwa Waziri wa ujenzi. Lakini niendelee kupongeza Wizara ya TAMISEMI, nayo imechukua juhudi hiyo ili iweze kujengwa. Lakini naomba nimpongeze tena Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuiweka kwenye mpango barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali moja dogo la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye Jimbo letu na Wilaya yetu ya Buhigwe makao makuu ya Wilaya yamebadilika kutoka Kasulu kwenda Buhigwe lakini tunazo barabara nyingine ndani ya Halmashauri yetu ambazo inabidi zichongwe kwa ajili ya kufika makao makuu na kupunguza urefu wa kuzunguka. Tunazo barabara kama nane ambazo zinahitaji kama shilingi milioni 950. Naomba ushauri wako.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukiweka rekodi sawa, Mheshimwa Obama toka kipindi chote cha miaka mitano ambapo alikuwa kama partner wangu wa karibu zaidi alikuwa akizungumzia maeneo haya ya barabara zake na amefanikiwa kuhakikisha kwamba wamehamisha makao makuu. Lakini nikijua wazi kwamba Sera ya Barabara tunaanza kipaombele katika zile barabara za kwanza zilizokuwa bora zaidi. Maana sera ya barabara ndiyo ilivyo hivyo; zile barabara ambazo hazijafunguliwa zinapewa kipaumbele cha mwisho zaidi.
Mheshimiwa Mweyekiti, sasa kwa sababu barabara hii kwa jinsi Mheshimiwa Mbunge alivyouliza ni barabara mpya, lengo ni ku-connect vizuri, kurahisisha ule umbali uwe mfupi zaidi. Nimsihi Mheshimiwa Mbunge, hili ni jambo jema, wananchi lazima wapate huduma, lakini nipende kuwahamasisha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo mumuunge mkono Mbunge huyu sasa katika vile vipaumbele vya kufungua barabara hizo mpya; kwa sababu hii ni barabara ya ndani ya Halmashauri, jambo hili katika Kamati ya Uchumi hali kadhalika katika Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani muangalie jinsi gani sasa mtatumia own source japo angalau kuanza kulifungua. Ofisi ya Rais TAMISEMI katika suala zima la kufungua barabara zake za vikwazo tutaangalia jinsi gani kwa njia moja au nyingine zile Halmashauri za pembezoni zote ambazo zina changamoto kubwa za miundombinu ya barabara tutaziangalia kwa jicho la karibu ili wananchi waweze kupata huduma za kijamii katika maeneo yao.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza naomba nipongeze juhudi za Serikali katika kutatua tatizo la maji nchini, lakini namba mbili naomba niendelee kuipongeza Wizara ya maji kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata ya Mnanila, wananchi wa Kata ya Mwayaya na Kata Mkatanga katika majibu ya Waziri anasema utekelezaji wa maradi huu utaanza katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Maji, watu wale hawaelewi programu ya pili, ya tatu hawaelewi. Swali lao, je, mradi huu unaanza kutekelezwa lini?
Swali la pili Jimbo letu la Buhigwe bado lina vijiji na Kata ambazo kwa kweli bado tuna matatizo makubwa ya maji. Je, Waziri anaweza akatuma wataalamu wake kwenda kwenye Kata ya Rusaba Kibande, Kilelema, Mgera, Kibigwa na Nyaruboza ili kufanya tathimini ya gharama za kupeleka maji katika vijiji vile ili navyo tuweze kuviingiza kwenye programu hapa baadaye?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza hii Programu ya Pili ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inaanza lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Programu ya Kwanza ya Maendeleo ya Sekta ya Maji tuliianza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2006/2007 ambayo imekamilika mwaka 2015 Disemba na katika programu hiyo tulikuwa na wadau wanaotuchangia fedha pamoja na Serikali yenyewe nayo imekuwa inatoa fedha kwa ajili ya utekelezajiwa miradi ya maji. Katika programu hiyo Mheshimiwa Mbunge mwenyewe ni shahidi kwamba miradi ya Munzenze, Kirungu na Nyamgali, ilianza kutekelezwa na sasa hivi ina maendeleo mazuri tu katika hiyo programu ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa programu ya pili tumeianza mwezi Januari, 2016, inaendelea, nayo itadumu kwa muda wa miaka mitano na katika programu hiyo wadau wa maendeleo tayari wameshatoa ahadi ya kutuchangia dola bilioni tatu na nukta tatu. Lakini hiyo ni pamoja na Serikali nayo itaendelea kukusanya fedha na kuchangia kwenye utekelezaji wa miradi kwenye vijiji ambavyo bado havijapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna vijiji ambavyo bado havijafikiwa na hii programu na Mheshimiwa Mbunge ameomba kwamba je, tutatuma wataalam lini? Mheshimiwa Mbunge natambua kwamba unayo Halmashauri ya Buhigwe, lakini Halmashauri ya Buhigwe bado ni changa, tutakachofanya na ambacho tumeshaanza kufanya sasa hivi ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji, inaendelea kuajiri wataalam na kuwapeka katika Halmashauri yako na Halmashauri nyingine zote ambazo zina upungufu wa wataalam. Ili tuwe na wataalam maeneo husika kuliko kuwachukua wataalam kutoka Wizarani. Lakini pale inapohitajika kama utaalamu unahitajika zaidi basi tutakuwa tuko tayari Mheshimiwa Mbunge kuja kutoa utaalamu zaidi kwenye eneo lako.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niipongeze Wizara kwa majibu mazuri, baada ya hapo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ya Manyovu - Kasulu imekuwa ni kero kubwa sana hasa wakati huu wa mvua na sasa hivi nauli ya kutoka Manyovu - Kasulu imefikia mpaka shilingi 10,000; na tunayo barabara nyingi ya lami ya kutoka Kigoma mpaka Manyovu yenye urefu wa kilometa 60 ambayo nauli yake ni shilingi 3,000. Kwa hiyo, umuhimu wa kujenga barabara hii na kuianza mapema inajionyesha kwa vigezo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kujua, Wizara imekiri kwamba inafanya upembuzi yakifu, wananchi wa Buhigwe wanataka kujua upembuzi yakinifu unaisha lini na ujenzi unaanza lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Rais alipokuwa akijinadi tuliita vijiji vya Mlela, Buhigwe, Kavomo, Nyankoloko, Bwelanka na akaahidi kwamba atajenga barabara ya kilometa tano katika Wilaya ya Buhigwe, je, ni lini ahadi hiyo itatimizwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Ntabaliba kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufuatilia miradi mbalimbali ya Miundombinu katika Wilaya yake na Jimbo lake, nikupongeze sana. Mimi ninakuhakikishia kama ambavyo tumekuwa tukiwahikishia katika ofisi zetu mimi na Waziri wangu, kwamba tutashirikiana na wewe kuhakikisha mambo yote ambayo tuliyaahidi katika Wilaya yako yanatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu la msingi, ujenzi utaanza baada ya kukamilika upembuzi na usanifu wa kina, kwa maana unaofanywa na kufuatiliwa na wenzetu wa AfDB. Nikuombe tu kwa kuwa anayefanya si Serikali, kazi hii inafanya na AfDB chini ya Afrika Mashariki suala la lini ni gumu kukueleza isije ikaonekana tunasema uongo hapa Bungeni. Nikuhakikishie suala hili litakamilika katika kipindi kifupi kijacho na baada ya hapo shughuli za ujenzi zitaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, nimuhakikishie, kama ambavyo tulimuhakikishia ofisini, kwamba kilometa zake tano ambazo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliahidi zitatekelezwa mara baada ya masuala haya ya miradi ambayo ni kiporo yatakapokamilika; na uzuri wake sehemu kubwa za viporo zinakamilika mwaka huu ujao wa fedha baada ya hapo tutakamilisha ahadi zingine zote ambazo Mheshimiwa Rais aliziahidi hasa za kilometa tano, kilometa sita katika sehemu mbalimbali za Miji ya Tanzania hii.