Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako (20 total)

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru ingawa muda ni mchache niseme mawili tu ya haraka haraka.
Kwanza, Waheshimiwa Wabunge leo tuna taarifa hizi kumi na zote hizi zinazungumzia mapendekezo ya Bunge hili. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri ni vyema ungetuongoza kwamba kama walivyosema wenzetu kwenye Kamati ya Uwekezaji ukurasa wa 49 kwamba ni vyema maazimio haya, mengine ni mazito sana, kwa mfano mambo yaliyozungumzwa kuhusu Bandari ya Dar es Salaam kama ni ya kweli basi yataisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hiyo tu wewe mwenyewe kwa sababu ni mahiri kuongoza Bunge hili ningeomba sana haya yote maazimio Waheshimiwa Wabunge tukubaliane yasiachiwe kwa Katibu wa Bunge; sisi wenyewe Wabunge tuunde Kamati yetu ndogo ya kuratibu mambo haya ni mambo mazito sana, vinginevyo yatakuwa hayana maana haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukumbushane kidogo, Mabunge mengine yanafanya hivyo kwamba kazi hii tunayoifanya ni kazi muhimu ya Kikatiba; ni kazi yetu kabisa ya msingi ya kuishauri Serikali na kuisimamia, lazima mambo ya msingi yalimo humu pengine si yote, lakini yale ya msingi lazima yadadavuliwe, yaandikwe vizuri na Serikali tuitake ije na majibu na kalenda yake ya utekelezaji, vinginevyo itakuwa ni hadithi tu, mambo ni mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamezungumzwa humo ndani, ushauri wangu nakubaliana na wenzetu wa Kamati ya Uwekezaji kama walivyoainisha kwamba tuunde Kamati Ndogo na wewe Mheshimiwa Chenge utuongoze tuunde Kamati Ndogo itakayosimamia mambo haya kwa kuwa ni mambo makubwa na mazito sana ambayo haiwezi kuachiwa Ofisi ya Katibu peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa niliseme kwa muda uliobaki kidogo huu nizungumzie suala la PPP. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda anahangaika sana, hongera. Kaza buti, lazima ufanye promotion na lazima uendelee kufanya promotion.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ushauri wangu ni kwamba, ili upate pesa lazima utumie pesa; waswahili wanasema ili ule lazima uliwe, ndiyo maana yake. (Kicheko)
Kwa hiyo, nilikuwa naomba hii private sekta tuisaidie, yenyewe haiwezi kunyanyuka; private sector duniani kote inasaidiwa kukua ili hatimaye iweze kuzalisha wafanyabiashara na walipe kodi na hatimaye kodi hiyo ndio inakuja kusaidia Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa mambo mengine yanatisha ukiyasoma humu ndani, kwa mfano kama kesi imeamuliwa ni kwa nini wenzetu wa Maliasili hawatekelezi haya yaliyoamuliwa na Mahakama? Kwa nini Serikali hamfanyi? Tunapotaze shilingi bilioni 10 wakati kesi imeamuliwa na Serikali imeshinda? Hakafu wakati huo tunaambiwa fedha hazipo, fedha si ndizo hizi? Ten billion mnai-surrender namna gani wakati kuna court ruling? Wale matajiri kama hawataki kakamateni mali zao tupate ten billion yetu. Sasa mengine humu ndani yanazungumzwa kwa kweli yanatia uchungu sana. Tunatafuta fedha tuna shida ya fedha ya miradi ya maendeleo fedha zingine zimeachiwa kwa matajiri na sababu iliyotolewa humu kwamba eti hakuna Bodi ya Tanzania National Parks, alah! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi bodi hiyo iundwe haraka sana na ndio mambo ambayo sisi kama Bunge lazima tusimame kidete na tuitake Serikali iunde hiyo bodi tuokoe ten billion yetu na hilo linakuwa halina mjadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala mwisho ni la kilimo. Mimi tafsiri yangu ya viwanda ni viwanda vya kilimo, vya mifugo na vya sekta ya uvuvi. Hivi viwanda vya Wachina Waturuki, Waingereza na wengine wanakuja kutusaidia tu lakini the basic industry ni lazima itokane na kilimo chetu, kilimo, wafugaji na wavuvi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako nizungumzie habari ya wawekezaji; ndugu Mwijage tembea na wawekezaji mfukoni kama wapo walete kwetu tutawapa maeneo ya kufanya shughuli zao.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nikupe pole kwa yaliyotokea maana mimi nipo karibu nao hapa, nilisikia minong‟ono yao tangu mapema. Tunakushukuru kwa uvumilivu wako mkubwa maana kwa kweli waliamua kufanya vurugu ambayo wala haikuwa na msingi wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna moja nilitaka kulisema lakini lingenoga kama wangekuwepo. Nataka niwakumbushe Wabunge wa CCM kwamba hii Serikali ni yetu sisi na sisi ndiyo wenye ajenda, wao hawana cha kupoteza hawa. Nilikuwa nafikiri ni vyema na sisi tukalifahamu vizuri jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna Mbunge mmoja amezungumza ningependa angekuwepo rafiki yangu yule kwamba Wabunge wanajikombakomba, jambo hili limenikera sana. Hatuwezi kujikomba Serikali ni ya kwetu sisi. Rais huyu anatokana na Chama cha Mapinduzi ndiye anakuwa ni Rais wa Watanzania wote. Kwa hiyo, Serikali hii ni ya Chama cha Mapinduzi of course inafanya kazi kwa wananchi wote. Ndugu zangu Mawaziri mlioteuliwa na Mheshimiwa Magufuli msonge mbele kwani ajenda iliyopo mbele yetu ni kubwa na tusipepese macho. Twende kwa malengo yetu ili tuwe na cha kusema mwaka 2020 vinginevyo wenzetu hawa kwa msingi mkubwa hawana cha kupoteza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee naomba niwashukuru wananchi wa Kasulu Mjini kwa kuniamini, kwa kunituma kuja hapa na kwa kunirudisha Bungeni. Walinipeleka likizo lakini wameamua wao wenyewe kwa mapenzi yao nirudi hapa. Nami nawahakikishia kwamba sitawaangusha na nawashukuru wananchi wa Kasulu kwa kuchagua Madiwani wengi wa CCM na kura nyingi za Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hotuba hii kwa maoni yangu, ningeshauri sana hotuba hii iwe ni input kwenye Mpango wetu wa Maendeleo kwa sababu imegusa kila kitu ambacho wananchi wanakilalamikia. Ukurasa wa 6 Mheshimiwa Rais amezungumzia vitendo vya rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Ukienda ukurasa 12 anazungumza hayo hayo lakini anahitimisha ukurasa wa 25 ana-quote maneno ya Mwalimu Nyerere miaka ya 1980 ambaye alisema hivi:- “Rushwa na ufisadi havina budi kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini wakati wa amani, rushwa na ufisadi ni adui mkubwa wa ustawi wa jamii na ni adui mkubwa kuliko hata wakati wa vita.” Hayo ni maneno ya Mwalimu Nyerere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 6, 11, 12 na 25, Mheshimiwa Rais ameonekana kukerwa sana na vitendo vya rushwa na wizi. Lazima tumsaidie kwa nguvu zetu zote kupiga vita rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nitoe mfano tu, katika kipindi cha mwaka 2012 - 2015, miaka mitatu tu, sisi wenzenu wa Halmashauri ya Kasulu, kwa mujibu wa ripoti ya CAG, tuliibiwa fedha shilingi bilioni 5.9 na wakati huo, ndiyo nataka na rafiki zangu wangesikiliza, waliokuwa Wabunge wa Majimbo yote mawili, Jimbo la Kasulu Mjini na Jimbo la Vijijini walikuwa ni wapinzani hawa. Wizi uliopitiliza, wizi uliotamalaki umetokea wakati wapinzani hawa wanasimamia Halmashauri yetu ila kule tumewashinda, tumewashughulikia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Waziri wa TAMISEMI simuoni hapa, niombe kwa Waziri Mkuu, yale majizi yaliyotuibia kule Kasulu bado yapo. Wengine wamehamishwa, wengine wamestaafu na wengine eti wamepewa likizo za kustaafu. Tunaomba sana, Waziri Mkuu na Waziri wa TAMISEMI, bahati nzuri tumepata nyaraka muhimu sana za wote waliohusika, nitazipeleka kwa Waziri Mkuu ili majizi haya yashughulikiwe na mkondo wa sheria uchukue nafasi yake na yale yatakayotiwa hatiani hakika tuyapeleke jela pengine kule magereza ndipo ambapo wanastahili kuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nimefarijika Mwanasheria Mkuu wa Serikali amenidokeza kwamba kumbe sheria ya kufilisi mali bado iko, haya majizi yanayotuibia nafikiri wakati sasa umefika, kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali sheria hiyo isimamiwe vizuri haya majizi tuyafilisi jamani haya. Wanaiba, wanafungwa wanarudi, tuyafilisi majizi haya ili nchi yetu iendelee kuwa na ustawi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Rais amelizungumza na aliliona kama ni kero kote alikopita ni tatizo la maji. Maana ni ukweli usiopingika kwamba wanawake wa nchi hii ndiyo wametupa utawala huu na wanawake hawa ndiyo wanateka maji. Nafikiri wakati umefika kwa kweli wanawake hawa tuwape faraja ya kuwaondolea mzigo wa kuteka maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kule kwetu Kasulu sisi hatuna shida ya vyanzo vya maji na Waziri wa Maji analijua hili. Vyanzo tunavyo, shida ni kuviendeleza tu ili kuongeza mtandao wa maji katika Mji wa Kasulu ili hatimaye katika kata zinazozunguka Mji wa Kasulu ziweze kupata maji ya kutosha. Vyanzo tunavyo, tunahitaji fedha wala si nyingi sana ili tuweze kuwa na mtandao mkubwa wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 11 Mheshimiwa Rais amezungumzia na ametukumbusha juu ya nia na sera za CCM za kujenga barabara za lami kuunganisha mkoa na mkoa. Hili jambo ni la kisera wala siyo la utashi wa mtu, barabara ya kuunganisha mkoa na mkoa ni kipaumbele cha Serikali ya CCM. Waziri wa Fedha unalijua suala hili vizuri, sisi barabara ya Kigoma – Nyakanazi haina mbadala kwa sababu inatuunganisha na Mkoa wa Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga. Barabara hii kwetu haina mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilidokeze kidogo tu ni suala hili la ujenzi wa reli, tumeshalizungumza sana.
Mimi ni muumini katika uchumi wa reli, bila nchi kuwa na reli hakuna kitu kinachoitwa kukuza uchumi. Huwezi kukuza uchumi au ukafikiria kuingia katika uchumi wa kati kama huna railway system. Hilo naliamini kabisa kwa nguvu zangu zote na Waziri wa Fedha bila shaka na yeye anaamini hivyo. Tutizame reli ya kati kwa jicho la kwenda kubeba mzigo ulioko Kongo ya Mashariki. Kule Kongo ya Mashariki kuna tani milioni tatu za shaba zinataka kwenda Ulaya na njia muafaka na nyepesi ni kupita reli ya kati, bandari ya Dar es Salaam na mwisho kwenye masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni wakimbizi. Jambo la wakimbizi sisi kwetu ni jambo kubwa na sisi wenzenu wa Mkoa wa Kigoma tumebeba dhamana ya kubeba wakimbizi hawa. Tuna wakimbizi kutoka Kongo, Rwanda, Burundi na kusema kweli tuna wakimbizi kutoka Somalia. Wote hawa wako katika Mkoa wa Kigoma. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Rais kwa asilimia mia moja kwa mia moja. Nashukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DANIEL N. NSANZUGWAKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hoja ya Mapendekezo ya Mpango, nikisoma pamoja na mwongozo wake wa kuandaa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema katika Bunge hili kwamba katika utamaduni wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola, Muswada kuwasilishwa mezani au na Waziri wa Serikali au na Mbunge na Muswada huu au hoja hii ikatolewa ni jambo la kawaida sana, ni jambo ambalo ni la kawaida kabisa na wala hakuna kitu ambacho ni cha ajabu. Nataka tuweke rekodi hizo kwa sababu yaliyotokea katika siku mbili ilionekana kama ni kitu kikubwa, lakini kumbe ni jambo la kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitajikita katika mambo makubwa matatu, nitajielekeza katika miradi ya Kitaifa ya kimkakati. Bila shaka huwezi kuzungumzia kukuza uchumi kama huwezi ukazungumzia miradi ya kimkakati. Miradi ya kimkakati tafsiri yake ni kwamba ni miradi ambayo ikitekelezwa itausukuma uchumi ule uweze kuzalisha mambo mengi zaidi na uweze kuzalisha fedha ziweze kutekeleza mambo mengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika miradi ya kimkakati, kabla sijaendelea na jambo hilo naomba ukurasa wa tisa wa Mpango, tufanye marekebisho kidogo. Katika yale maeneo yanayolima kahawa, nimeona yametajwa pale katika ukurasa wa tisa, wamesema katika Wilaya za Moshi, Mbinga, Bukoba, Mbozi na Tarime, kana kwamba ndiyo zinalima kahawa peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuweke rekodi sawasawa, kwa takwimu za Tanzania Coffee Board, Mkoa ambao unatoa kahawa ya arabika bora katika nchi za Afrika Mashariki ni pamoja na Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, naomba katika mpango ule katika ile miche ya kahawa, ijumuishe pia Wilaya ya Kigoma na Wilaya ya Kasulu ambako tunalima arabika ya kiwango cha juu kabisa na zaidi ya hapo hata TaCRI wana kitalu kikubwa sana cha kuzalisha miche zaidi ya 1,000,000 pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya kimkakati, niungane na wasemaji waliopita kuzungumzia suala la reli ya kati. Naona kuna confusion kidogo hapa, hivi tukisema reli ya kati maana yake nini? Reli ya kati maana yake ni kutoka Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tabora, Kigoma na unakuja branch ya Tabora kwenda Mwanza ndiyo reli ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha wa Mpango huu, reli ya kati ni pamoja na mchepuko kutoka Isaka pale Kahama kwenda Keza, Keza iko kwenye mpaka wetu na Rwanda na pia mchepuko wa kutoka Uvinza kwenda Msongati ya Burundi na pia mchepuko wa Kaliua, Mpanda kwenda Kalema bandarini na mchepuko wa Dodoma kwenda Singida, hiyo ndiyo reli ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka tuwe na uchumi wa viwanda, kama kweli tunataka nchi yetu ibadilike ingie katika uchumi wa kati, lazima tujenge reli. Sasa shida inakuwa pesa tunapata wapi, gharama ni kubwa kwa awamu kwanza tunahitaji takriba dola bilioni 7.6. Hii siyo fedha nyingi, nchi hii ni kubwa, tunakwenda kukopa, tuna marafiki wetu wa maendeleo, kuna Wachina na Wajapani wanatuamini na sisi tunawaamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwamba hatuna fedha za kujenga reli, hatutaki kuisikia katika Bunge hili. Tunataka Serikali ije na mkakati mahsusi, mkakati wa msingi kabisa wa kwenda kukopa fedha hizi kwa Serikali ya Watu wa China, kwa Serikali ya Wajapani tujenge reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, bila ya kuwa na reli, tunacheza ngoma. Haiwezekani mizigo yote, makontena yote, mafuta yote yapite kwenye barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, ni nchi yetu pekee ambayo mizigo mizito inapita kwenye barabara. Matokeo yake barabara hizi zinaharibika sana, inajengwa barabara ya kukaa miaka 30, uhai wake unakuwa ni miaka mitatu, minne, barabara inakuwa imeharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tukubaliane, Waziri wa Fedha usipokuja na mkakati wa kujenga reli ya kati ikiwa na michepuko niliyoitaja, Isaka, Keza kwenda kubeba mzigo wa nickel, Uvinza - Msongati kwenda kwa ndugu zetu wa Burundi kuchukua mzigo wa Congo; mchepuko wa Kaliua, Mpanda - Kalema kwenda bandari ya Momba katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo kuchukua mzigo wa Lumbumbashi.
Tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, utakapokuja na Mpango huo bila hiyo reli ya kati hatuwezi kuelewana katika Bunge na nitaomba Waheshimiwa Wabunge tusimame kidete kumwambia arejeshe Mpango huo mpaka atuwekee reli ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani miaka zaidi ya ishirini tunazungumza reli ya kati, lakini haijengwi, haiwezekani? Wenzetu Kenya wameanza kujenga Mombasa kwenda Kigali, kwa nini sisi hatujengi, kwa nini hatuanzi, utasikia tumekarabati kilomita 176 za latiri 80, hatutaki kusikia lugha hiyo na nchi yetu si maskini, ina rasilimali za kutosha, tunaweza tukazikopea kujenga reli ya kati na michepuko niliyoitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya kati maana yake hizo reli zinakwenda kwenye mali, ukichepuka Isaka kwenda Keza, unakwenda kwenye nickel nyingi sana, tani milioni kwa mamilioni. Bandari ya Uvinza kwenda Msongati hiyo inapita Kasulu hiyo, Shunga - Kasulu, kwenda Burundi - Msongati maana yake ni madini ya nickel yaliyopo Burundi na mzigo ulioko Congo ya Mashariki. Isitoshe bila kujenga reli ya kati kwa standard gauge, tutaua bandari ya Dar es Salaam, bandari ya Dar es Salaam kwa miaka michache ijayo itakuwa haina mzigo, tutaua bandari ya Mwanza, tutaua bandari ya Kigoma na tutaua bandari ya Kalema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana, Waziri wa Fedha, bila kuja na mkakati mahususi wa reli hii, kwa tafsiri hiyo, tutashawishiana Wabunge wote tukuombe urudi tena mpaka uje na hoja mahususi ya kujenga reli ya kati. Bila reli ya kati hakuna uchumi wa viwanda, bila reli ya kati hakuna nchi kwenda kwenye pato la kati, kwa nini tuendelee kujiharibia wenyewe, wakati tunaweza tukatenda haya na yakafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie ni maeneo wezeshi kwa maendeleo ya viwanda. Soma kwenye Mpango hapa, tumezungumzia juu ya nishati, reli na barabara. Nimefurahi kusikia kwamba washirika wetu wa Maendeleo wametupatia fedha kwa ajili ya kujenga gridi ya Taifa kutoka Geita sasa kuja Nyakanazi, Kwilingi na Kakonko, Mkoa wa Kigoma. Ningefikiri kupitia kwa Washirika wetu wa Maendeleo hao hao, tungeendeleza hiyo grid sasa, ile western grid, ile corridor kutoka Kakonko iende Kibondo, Kasulu, Kigoma na Katavi. Hatimaye iweze kuja ku-link na Tabora, tuweze kuwa na umeme wa kutosha kwa ajili ya maendeleo ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la msingi sana na la kisera na liko kwenye Ilani yetu ni barabara ya Kigoma – Kidahwe - Nyakanazi. Hii barabara ni barabara ya kihistoria, imesemwa kwa miaka zaidi ya 20 sasa na bahati nzuri mkandarasi yuko site pale. Yule mkandarasi nimepata habari, alikuwa ananiambia Waziri wa Uchukuzi hapa kwamba wamempa fedha kidogo ili aendelee. Sasa tunaomba barabara hiyo ni barabara ya kimkakati kwa sababu inatuunganisha na mikoa mitano ya nchi hii; inatuunganisha Kigoma - Kagera, Kigoma - Mwanza, Kigoma - Geita, na Kigoma - Shinyanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo barabara ni muhimu sana. Tunamwomba Waziri wa Fedha, aje na mkakati sasa wa kuimalizia barabara hiyo. Na huyo mkandarasi ambaye yuko site, basi tunamwomba aendelee ili barabara hiyo ikamilike. Si hiyo tu, sisi tunaotoka Kigoma, hiyo barabara ndiyo siasa za Kigoma na tunasema barabara ya Nyakanazi kipindi hiki, ndio wakati wake na niseme tu kwamba tutaomba sana barabara hii ijengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza naipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya na hasa hii dhana ya kuwajibika Serikalini, ni dhana muhimu sana. Haya majitu yasiyowajibika wala msirudi nyuma, yaendelee kutumbuliwa ili yapotee kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, napenda nimrudishe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa ukurasa wa 28. Ukurasa wa 28 kuna mambo ya nyongeza ambayo Mheshimiwa Waziri ameyasoma, kwenye kitabu hayapo. Yapo kumi nimeyasikia; moja mpaka kumi. Ulikwenda moja, tisa, kumi. Naomba yale kumi ya namna ya utekelezaji wa mkakati, ayaandike tuyapate. Ni ya msingi sana, nilimsikia vizuri sana kwa sababu nilikuwa hapa. Hilo ni ombi katika hotuba hii nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili ya haraka haraka, la kwanza naomba nijielekeze ukurasa wa 15 ambapo Tanzania imekuwa ikipoteza uwezo wake wa kushindana kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia zile takwimu, zinatisha kidogo, kwamba kuanzia mwaka 2012 tumekuwa tunashindwa kuvutia mitaji ya ndani na ya nje na mbaya zaidi mwaka 2016 inatarajiwa tutakuwa nchi ya 139 katika nchi 186 katika kuvutia mitaji ya ndani na nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri, katika mkakati mzima wa kutekeleza Mpango wetu mzuri wa miaka mitano inayokuja, ni muhimu sasa Serikali na Wizara tukajua ni kwa nini hasa tumeshindwa kuvutia wawekezaji? Ni kwa nini hasa tumeshindwa kuvutia mitaji ya ndani? Tatizo ni nini? Ni urasimu kwenye vyombo vyetu huko TIC au tatizo ni nini hasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima iwepo sababu ambayo inafanya nchi yetu ishindwe. Katika nchi 186 kwa mujibu wa vigezo vya World Bank, tunapokuwa nchi ya 140, ni sawa na kuwa nyuma kabisa. Kwa hiyo, nawiwa kusema kwamba ni vyema Serikali yote ikae kuelewa kwa nini tumeshindwa kuvutia mitaji ya ndani na nje na ukizingatia mpango mzima kwa kiwango kikubwa, umetamka kwamba utashirikisha sekta binafsi?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ningependa kusema ni kilimo ambalo wenzangu wamelisemea, lakini niseme eneo dogo tu, kwenye Benki ya Kilimo. Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakubaliana nami kwamba kama kweli tunataka kuwa nchi ya viwanda kwa dhati kabisa, ni lazima tuweke nguvu kubwa sana kwenye Sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya nyenzo za kukuza Sekta ya Kilimo ni pamoja na Benki hii ya Kilimo. Kwa mujibu wa hotuba hii, Benki ya Kilimo haina mtaji na kama inao ni kidogo sana. Ina Shilingi bilioni 60 tu, ukiachilia mbali kwamba Benki hiyo iko Dar es Salaam na wamekuja kwenye Kamati yetu tumewashauri kwamba wajitofautishe ili ikibidi sasa wahamie katika maeneo ya uzalishaji ili iwe Benki ambayo kweli ni kioo, ni Benki ya Wakulima na hakika isiwe Benki iliyoko Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri mmoja kwa Serikali na hasa Wizara ya Fedha, hatuwezi kuendelea kama ilivyokuwa mwaka wa 2015 kwamba Benki ya Kilimo haina mtaji, lakini wenzao wa TIB, Alhamdullah wana angalau Shilingi bilioni 212. Benki ya Kilimo ambayo tunaitarajia isaidie wakulima ili wazalishe, hatimaye nchi iingie kwenye nchi ya viwanda na viwanda vingi viwe vya kuchakata mazao ya kilimo, bado Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kuna haja kubwa kama Serikali mwangalie namna nzuri ya kuwezesha Benki hii ya Kilimo iweze kufanya kazi zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo njia nyingi. Kwa mfano, kama wenzetu wa DANIDA waliweza ku-support CRDB na mnaona ilipofika, kama wenzetu wa DANIDA waliweza ku-support PASS kule Morogoro na mnaona PASS ilipofika, kwa nini Mashirika rafiki na nchi rafiki pengine zenye masharti rafiki msizihusishe katika mkakati mzima wa kuiwezesha Benki ya Kilimo kupata mtaji unaoeleweka? Nina hakika mkifanya hivyo Benki hii itasambaa katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niweke angalizo; hatuwezi kuzungumza nchi ya viwanda kama hatuwezi kuwezesha Sekta ya Kilimo. Hilo ni lazima tukubaliane kabisa na bado kuna matatizo makubwa hata kwenye bajeti ya Sekta ya Kilimo. Mheshimiwa Waziri unajua kwamba bajeti ya pembejeo iko chini sana. Sasa kama bajeti ya pembejeo ipo chini sana kwa maana ya mbolea, mbegu, viatilifu, tafsiri yake ni kwamba hiki kilimo tunachotaka baadaye iwe ndiyo nguvu ya kujenga viwanda vya ndani, hiyo azma inaweza ikashindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu sincerely kabisa ni kwamba lazima tuangalie namna nzuri ya kutoa fedha za kutosha kwenye eneo la pembejeo na hasa mbolea. Kwa takwimu za wenzetu wa Wizara ya Kilimo ni kwamba hata uzalishaji wa chakula mwaka 2015 ulishuka kwa takribani tani 500,000. Ni dhahiri tukienda katika mfumo huu ambapo hata fedha za pembejeo za kilimo zimeshuka, tafsiri yake ni kwamba uzalishaji wa mazao ya kilimo utakuwa chini and consequently itakuwa ni ngumu sana kupata mazao ya kutosha kumudu viwanda vyetu vya ndani na hatimaye tuweze kuboresha maisha ya watu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limenivutia sana ni hii miradi ya kipaumbele hasa reli ya kati. Naomba Serikali ifahamu kabisa tukisema reli ya kati, maana yake ni reli inayoanzia Kigoma inaishia Dar es Salaam, ndiyo reli ya kati na ndiyo jina lake. Mwanzo wa reli ni Kigoma na mwisho wa reli ni Dar es Salaam. Msingi wake ni mmoja tu, kwamba hii reli kule Kigoma itakuwa ni mkakati wa ku-tape kutoka nchi ya Kongo Mashariki ambako kuna shaba nyingi sana, zinc nyingi sana na mbao nyingi sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonesha kwamba mzigo ulioko Mashariki ya DRC ni takribani tani milioni nne na hizo zinaweza kufika kwenye bandari na kwenda kwenye masoko nje ya nchi kupitia reli ya kati. Reli ya kati maana yake ni Kigoma - Dar es Salaam. Matawi yake ndiyo Tabora - Mwanza, Tabora – Kaliua – Mpanda na sasa hii mpya ya Uvinza – Msongati.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo tafsiri ni muhimu sana ili tuelewane vizuri. Kwa sababu bila kuwa na tafsiri hiyo, tafsiri yake ni kwamba ule mkakati wa tani milioni nne za Kongo ya Mashariki, hautaweza kupita Bandari ya Dar es Salaam. Sincerely nashauri hata ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge uanzie Kigoma kwa ku-tape mali iliyoko DRC halafu reli hiyo itoke Kigoma ndiyo ijengwe kuelekea Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la mwisho ni utafiti. Nimesoma kwenye kitabu cha hotuba, Mheshimiwa Waziri wa Fedha umeanisha vizuri sana umuhimu wa utafiti, lakini liko jambo moja linahitaji uelewa tu wa jumla. Kwa nini Taasisi zetu za Utafiti, ili zipate fedha za Utafiti lazima eti zikashindanie COSTECH? Ni mambo ya ajabu kabisa haya! Nina hakika haya mambo ndiyo Mheshimiwa Magufuli hataki hata kuyasikia!
Mheshimiwa Naibu Spika, watafiti wako Ilonga, Uyole, Mlingano, lakini eti fedha za utafiti zinapelekwa COSTECH wakazishindanie ndiyo ziende kwenye Taasisi za Utafiti, kwa nini? Hivi unahitaji kwenda shule kulijua hili? Kwa nini pesa hizi zisiende kwenye utafiti moja kwa moja? Kwanza itapunguza urasimu na itapunguza muda wa fedha kutoka Hazina na kufikia Vyuo vya Utafiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nakualika Mheshimiwa Waziri wa Fedha, utembelee Kituo cha Utafiti cha Cholima kilichoko Dakawa. Hicho ndiyo kituo ambacho ni known kwa utafiti wa mpunga. Waheshimiwa Wabunge, kama tukiendelea hivi bila utafiti kwenye Kituo hicho nchi hii tutakosa mchele kwa miaka michache ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu tumekwenda pale, tumekuta mambo ya ajabu sana! Hawa watu wana miaka mitatu hawajapata fedha kwa ajili ya utafiti. Fedha kidogo waliyoipata, eti wanashindanishwa na COSTECH! Mimi sielewi! Wala haikuingia kwenye kichwa changu hata kidogo, kwamba watafiti, wasomi wazuri, Watanzania hawa wanaanza tenda, ku-lobby kule COSTECH ili wapate fedha kuendesha utafiti kwenye Vyuo vyao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali mjue wazi kabisa kwamba Vyuo vya Utafiti hasa kwa mazao ya kilimo vinajulikana; vipo Uyole, Naliendele, Ilonga, Ukiriguru, Mlingano, Seriani na kadhalika. Wapelekeeni fedha hao moja kwa moja, ni wataalam na wasomi wazuri katika jambo hili. Kupitisha hizi fedha COSTECH ni kupoteza wakati tu na kuweka urasimu ambao hauna sababu. (Makofi)
Mwisho kabisa naomba nami kwa namna ya pekee niwashukuru wapigakura wangu wa Kasulu Mjini kwa kuniwezesha kurudi Bungeni, maana haya mambo ni mazito!
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwashukuru, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja. Mkakati ni mzuri na msonge mbele. Ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL N. NSANZUNGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kwa namna ya pekee nikushukuru wewe mwenyewe binafsi kwa namna ambavyo unatuongoza katika kikao hiki kwamba Wabunge tunahitajiana na Muungano wetu huu ni muungano wa watu wa sehemu zote mbili na lazima wote tuvumiliane, tuheshimiane na tupendane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kusema ninachotaka kusema naomba kwanza nioneshe masikitiko yangu kabisa kwa Wizara hii. Mheshimiwa Waziri nilikuwa nasoma hotuba yako yote, katika maeneo yaliyoathirika na ujio wa Wakimbizi Mkoa wa Kigoma tangu mwaka 1958 tumepokea Wakimbizi, lakini hotuba yote hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais, hakuna hata sentensi moja inazungumzia uharibifu wa mazingira uliosababishwa na ujio wa Wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imenishangaza sana na Mheshimiwa Waziri sijui nina hakika ulisahau maana huwezi kufanya hivyo. Waheshimiwa Wabunge, Mkoa wa Kigoma tuna mazingira ya peke yetu kabisa, hayafanani na mahali pengine. Ujio wa Wakimbizi tumechukua dhima hii kwa niaba ya Taifa letu, lakini naona juhudi zinazofanywa na Serikali ni juhudi hafifu katika hatua zote za kukabiliana na uharibifu wa mazingira ambao umefanywa na ujio wa wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina haja ya kushika mshahara wa Waziri baadaye ingawaje nimejiandaa kuukamata, ningependa nipate maelezo ni kitu gani kama Serikali inafanya kwa mazingira ambayo yameharibika kwa miaka 40 iliyopita na iko mito ambayo iko mbioni kupotea, Mheshimiwa Waziri wewe unajua Mto Makere sasa hivi umepotea, ule mto hautumiki tena. Chepechepe ya Malagarasi ambayo ni ardhi oevu na imetamkwa na UNESCO iko katika hatari ya kupotea kwa sababu ya harakati za binadamu na nyingi zikisababishwa na wakimbizi.
Ningeomba Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha hotuba yako ili tusigombanie mshahara wako ueleze ni hatua gani za makusudi zimefanywa kwa Mkoa wa Kigoma, Mkoa wote tumeathirika katika jambo hili, uhalifu ni mwingi, ujambazi ni mwingi, maradhi ya kuambukiza ni mengi kwa sababu ya ujio wa wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni shahidi, juzi ulikuwa Kigoma umeona mambo ya ajabu katika makambi ya wakimbizi, tunaomba jambo hili Mheshimiwa Waziri utueleze hatua gani zimefanyika katika ku-mitigate janga na mazingira vis-a-vis ujio wa wakimbizi katika Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kwa ruhusa yako niliseme kidogo ni hili la Muungano. Hili jambo linazungmzwa, nina bahati nzuri nilishiriki katika harakati za muafaka tu, nilishiriki najua harakati zake. Mheshimiwa Waziri, CCM tumeshinda Uchaguzi Zanzibar, CCM tumeshinda Bara, lazima sasa wakati umefika Chama cha Mapinduzi na Serikali zetu mbili tufungue milango ya mazungumzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya kisiasa hayaondolewi na uchaguzi, migogoro ya Kijeshi haiondolewi na uchaguzi, migogoro ya kiusalama haiondolewi na uchaguzi, migogoro ya kiusalama ya kisiasa inaondolewa na mazungumzo. Tufungue milango tuzungumze. Sisi ndiyo wa kupoteza, wana CCM ndiyo wenye mali, hawa wenzetu hawana mali sisi ndiyo tuna dhima ya kulinda mali hii. Nina hakika na naamini bila kutia mashaka kabisa kwamba hatuwezi kuiacha Zanzibar kama ilivyo, lazima tuzungumze ili hatimaye Muungano huu uweze kuwa na hatima ambayo itatusaidia kusonga mbele. Muungano tunauhitaji sana, acha kunipotosha wewe hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa niliseme ni athari pana za mazingira. Nitoe ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, nchi yetu inakabiliwa na jangwa na wewe umeeleza vizuri kwenye kitabu chako. Nchi yetu inaathiriwa na kuzurura ovyo kwa mifugo kila pembe za nchi yetu. Wakati umefika jambo hili la uharibifu wa mazingira, jambo hili la nchi yetu kuingia katika athari na hatari ya jangwa haliwezi kuondolewa na Wizara moja, ni vizuri Ofisi ya Makamu wa Rais, iongoze harakati hizi za kukaa pamoja ili jambo hili lipate suluhu ya kudumu ili wakulima na wafugaji sasa watulie na athari hizi za tabianchi ziweze kutazamwa kwa ujumla wake kama Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ni makubwa sana kila mahali kuna shida, naamini kabisa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano mnaweza kuwa ndiyo vinara, mkasikia will kuhakikisha kwamba tatizo hili la mazingira mnatazama kwa ujumla wake kama Serikali na kamwe siyo Wizara moja moja kama ambavyo tunaiona inatokea sasa hivi, kuna migogoro katika maeneo mengi sana na yote inatishia uhai wa mazingira ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo umelizungumza katika ukurasa wa 41, Mheshimiwa Waziri umezungumza kwamba kuna mwongozo umeutoa wa elimu ya hifadhi ya mazingira, ingekuwa vizuri hizo nakala 1,050 ambazo umesema zimesambazwa basi nakala chache Wabunge tuko siyo chini ya 400, Wabunge wote tupate nakala ya huo mwongozo wa elimu ya mazingira kama ulivyoeleza kwamba mmeusambaza katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo muhimu sana ili na Waheshimiwa Wabunge waweze kufanya kazi hii katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niwaombe wenzetu wa NEMC, katika hotuba yako umezungumza majukumu makubwa sana ya NEMC, ukaguzi wa viwanda, ukaguzi wa majosho, ukaguzi katika hifadhi zetu za wanyama, ukaguzi wa mahoteli. Naomba kupitia kwako wawekezaji wengi wanalalamikia muda mwingi ambao unatumiwa na NEMC katika ukaguzi wao, matokeo yake wawekezaji wengi wamekuwa wakinung‟unika sana na manung‟uniko yao ni pamoja na urasimu usiokuwa na sababu kabisa za wenzetu wa NEMC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumza na wenzetu wa NEMC wako wasomi wazuri tu wakiongozwa na Dkt. Baya, ni wazuri sana, shida yao ni rasilimali fedha, rasilimali watu. Huwezi ukazungumzia uwekezaji wenye nguvu kama taasisi hizi zinazopaswa ku-facilitate uwekezaji bado ni dhaifu. Wenzetu wa NEMC wapeni nguvu, waongezeeni fedha ili kaguzi zao katika miradi mbalimbali ya uwekezaji uweze kwenda na iende kwa wakati. Kuchelewa unajua wawekezaji hawa lengo lao kubwa ni wakati, haiwezekani mtu anajenga kiwanda chake au hoteli anahitaji miezi mitatu ya ukaguzi, anawasubiri NEMC, anajenga service station anahitaji miezi mitatu, minne kusubiri NEMC haiwezekani! Tumezungumza nao wanasema shida yao kubwa ni resources, hawana fedha za kutosha na waongezewe wataalam wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nitaunga mkono hoja hii kama nitasikia hatua ambazo zinafanyika za ku-mitigate masuala ya wakimbizi katika Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, na-reserve jambo hili la kuunga mkono hoja hii mpaka nitakapopata maelezo mazuri kuhusu hatua ambazo zinafanyika kwa Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru na sina haja ya kugombana na Waziri kwenye mshahara wake, nitaunga mkono nitakaporidhika na maelezo yake. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kusema machache. Niseme kwamba niko kwenye Kamati ya Kilimo, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaendelea kukupa hongera kwa kazi yako nzuri na timu yako. Hata hivyo, nina machache ambayo ningependa tuweke record sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kitabu cha Mheshimiwa Waziri ni record, kina kumbukumbu, nimekisoma chote. Ukurasa wa 116 kinaainisha msaada wa chakula uliotolewa; ameainisha baadhi ya Wilaya. Kwa takwimu hizi, tafisiri yake ni kwamba, takriban asilimia 65 ya nchi yetu ina upungufu wa chakula. Kitu ambacho ningependa tuweke record sawasawa, humu ndani Mheshimiwa Waziri unasema kuna msaada wa chakula mmepeleka kwa Wakimbizi. Sasa nataka tuweke record sawasawa, siku hizi NFRA ndiyo inalisha wakimbizi wetu au ni suala la UNHCR? Naomba tuweke record vizuri kwenye vitabu vyetu hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia bullet inayofuata umesema tumetoa msaada wa chakula Southern Sudan. Sasa tumerudi kwenye enzi za Mzee Nyerere za ukombozi wa Bara la Afrika? Kwamba sisi tunaanza kuwalisha watu wa Southern Sudan?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilidhani kule Southern Sudan tunakwenda kuuza nafaka zetu, kwasababu kuna fedha za UNHCR! Nilihisi vilevile kwenye makambi ya wakimbizi NFRA inakwenda kuuza chakula kule ili tupate fedha, tena fedha za kigeni kwa sababu haya Mashirika ya Kimataifa yana fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuweke record sawasawa, huo msaada unaosema unapeleka Southern Sudan ni msaada wa namna gani? Hao wakimbizi to my knowledge ni kwamba hawahitaji NFRA, wao wanalishwa kupitia fedha za UNHCR. Pengine Mheshimiwa Waziri kwa taarifa yako tu, sisi kwenye RCC tumeshakubaliana kwamba RC atakuja kwako kuomba kibali ili Mashirika ya Wakimbizi yanunue chakula katika Mkoa wa Kigoma ambacho kinazalishwa na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo tumeshakubaliana kwenye RCC na nasikia eti mpaka waje waombe kibali kwa Waziri. Mahindi ya kwetu, kuyauza NHCR hatuwezi mpaka tuje tuombe kibali kwenye Wizara. Nadhani hayo ni baadhi ya mambo ambayo yanahitaji kurekebishwa katika mfumo wa huu utawala wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ningependa niliseme, Mheshimiwa Waziri tumeshazungumza suala la uzalishaji wa mbegu na suala la Bugaga. Nimekupa options mbili; hili shamba la Bugaga maarufu shamba la Wajapani; shamba la mbegu tulilitoa kwa ASA. Huu ni mwaka wa nane limeachwa kuwa shamba pori. Sisi tumewapa option tu, kama hili shamba hamlihitaji turudishieni Halmashauri. Turudishieni shamba letu! Haiwezekani! Uhaba wa kuzalisha mbegu ni mkubwa, lakini huu ni mwaka wa nane, shamba limekaa, lina miundombinu ya umwagiliaji lakini halitumiki! Kama wenzetu wa ASA wameshindwa Mheshimiwa Waziri na Wizara yako imeshindwa kulitumia, tunaomba shamba letu mturudishie. Wala hatuna ugomvi na hilo, tutalitumia wenyewe na tuna uwezo wa kulitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwa kweli ni kwamba na Waheshimiwa Wabunge wote mtuunge mkono, tumuunge mkono Waziri tuhakikishe fedha za pembejeo zinaongezeka. Hatuwezi kuzungumzia uchumi wa viwanda wakati hatujatafsiri kibajeti kusaidia Sekta ya Kilimo, haiwezekani! Naomba Waheshimiwa Wabunge wote tushikamane wakati utakapofika tuhakikishe sekta hii inaongezewa fedha; fedha za mbolea, fedha za madawa na kadhalika na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa niliseme ni mbolea hii ya Mijingu. Mheshimiwa Waziri kuna maeneo mengi, mbolea hii ya Mijingu ambayo inazalishwa katika nchi yetu, wananchi hawaelewi vizuri, wanailalamikia! Kwa nini Wizara msije clearly na wewe Mheshimiwa Waziri na watalaam wako mkaeleza exactly utajiri wa mbolea hii ili wananchi waelewe? Kwa sababu mbolea hii inazalishwa nchini, tungekuwa na fursa ya kuitumia zaidi. Ni muhimu kabisa wananchi hawa waelewe contents za mbolea hii na umuhimu wa mbolea hii. Maeneo mengine mbolea hii watu wanaikataa, lakini Serikali imekaa kimya haisemi jambo lolote. Tokeni nje muisemee mbolea hii kwa sababu inazalishwa hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni kumkumbusha tu Mheshimiwa Waziri na Watalaam wake wananisikia, kuna mtu mmoja amezunguza jambo hili; katika nchi yetu mikoa mitatu inayopata mvua za uhakiki inajulikana na ni Mikoa mitatu tu!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka 40 iliyopita mikoa yenye mvua za uhakika, udongo wa rutuba ni mikoa mitatu tu. Mkoa wa kwanza ni Kagera, hakuna uwekezaji wa maana umefanyika wa kilimo kule; Mkoa wa pili ni Kigoma, hakuna uwekezaji wa maana wa kilimo umefanyika kule; Mkoa wa tatu ni Katavi. Sasa mnahangaika, mnawekeza maeneo ambayo hayana mvua, hayana udongo wenye rutuba, ni kitu gani mnafanya Mheshimiwa Waziri? Mkae kama Serikali, hii Mikoa ambayo tuna comperative advantage, tuweze kuwekeza kwa nguvu zetu zote katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, pale Kasulu tuna Chuo cha Kilimo. Kile Chuo kilikuwa cha World Bank baadaye World Bank wakakiacha, sasa kimerudi. Tunaomba kupitia kwako Mheshimiwa Waziri na wananchi wa Kasulu wamenituma jambo hili, tunakiomba kiwe ni sehemu ya mlingano, sehemu ambayo…
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii lakini Mheshimiwa Mwigulu nadhani tumeelewana vizuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa namna ya pekee nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba kwanza nianze kwa kukupa hongera nyingi sana Profesa Ndalichako na timu yako, mnafanya kazi nzuri, hongereni sana. Hiyo ni tafsiri kabisa kwamba akina mama wenye ujuzi, mnaweza, hongereni sana! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii, niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri unafahamu kwamba asilimia 68 ya Civil Service ya nchi hii ni Walimu. Kwa hiyo, zaidi ya Watumishi wa Serikali hii ni Walimu. 68 percent ndiyo Civil Service ya nchi hii. Tafadhali sana! Wewe Mheshimiwa Waziri, Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Utumishi, kaeni pamoja kuhakikisha kwamba Walimu hawa tunawapa kipaumbele cha kwanza. Bila wao hakuna nchi hii. Sisi wote tuko hapa kwa sababu tulisoma, kwa sababu tulifundishwa na Walimu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila shaka kila mmoja anafahamu kwamba Walimu hawa wana changamoto nyingi sana. Shule zetu nyingi hazina nyumba za Walimu, shule nyingi hazina madarasa ya kutosha, Halmashauri zetu zinahangaika kushoto na kulia. Naomba, wakati umefika, Serikali yenyewe itafute fedha popote itakapopata fedha hizo, kujumuika na Halmashauri zetu ili miundombinu ya elimu iweze kuwa rafiki na hakika shule zetu ziweze kuboreka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ambalo napenda kulisema, ni hili jambo la ada elekezi. Mimi huwa sielewi vizuri, labda Mheshimiwa Waziri atanifafanulia. Hivi ada elekezi ambazo mng‟ang‟ana na hao wenye shule, hizi shule siyo mali ya Serikali! Hizi shule ni mali ya watu binafsi. Mmekaa nao? Mmezungumza nao? Mmelewana? Maana yake haya ni kama mtu mwenye mali yako, halafu anakuja mtu mwingine anasema basi weka ada elekezi. Kila mmoja anajua nchi hii, miaka ya 1980 na 1990, watoto wetu walikuwa wakienda Kenya, Uganda na Malawi kusoma. Sasa wenye mitaji yao wameanzisha shule hizi, tunaanza kuja na ada elekezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu na ushauri wangu kwa Serikali, kaeni na wamiliki wa shule hizi, ni mali zao, mwasikililize, Serikali ifanye facilitation tu. Hakuna sababu ya kugombana na hawa watu. Tunataka watoto wetu wakasome tena Kenya? Wakasome Uganda? Ni muhimu sana ada elekezi hizi mkubaliane na wamiliki wa shule, zile shule ni mali yao na kamwe siyo mali ya Serikali; na tumeshatoka huko ambako mali zilikuwa za Serikali, shule zilikuwa za Serikali; sasa shuke hizi ni za watu binafsi. Naomba sana jambo hili Mheshimiwa Waziri, wewe ni mahiri, wewe mwenyewe ni Mwalimu, mkae mliangalie vizuri mkubaliane na hawa wamiliki wa shule na muafaka upatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika mkizungumza na wamiliki wa shule, wana uelewa, wamewekeza fedha zao nina hakika mtafika mahali kwenye middle ground ambapo hata kama ni ada elekezi basi ni rafiki kwa wamiliki wa shule na kwamba pia watafanya biashara pamoja na kwamba elimu kwa kweli kwa kiwango kikubwa ni huduma zaidi kuliko biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda niliseme ni haya mafao na malipo ya Walimu, kwa mfano, Walimu katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Walimu katika Mkoa wa Kigoma, wamekuwa na malimbikizo mengi sana. Nimepata taarifa kwamba juzi wamelipwa, eti madai yao fedha iliyohakikiwa wameletewa asilimia 13 tu basi. Sasa anayefanya uhakiki ni nani huyo? Hawa Walimu ni kipaumbele. Naomba sana Walimu wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Walimu wa Kasulu Mjini na Halmashauri wahakikiwe vizuri. Unafanyaje uhakiki unakuja na ten percent ya uhakiki! Ni kitu ambacho hakikubaliki. Ingekuwa angalau 40 percent, 50 percent unaweza ukaelewa, ten percent, 13 percent ya madai yao yaliyohakikiwa, hilo ni dhahiri kabisa kwamba kuna mahali kuna tatizo na tatizo tusiliruhusu likachafua Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imeanza kwa matumaini makubwa kwa Watanzania hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda nilizungumze, sisi Mkoa wa Kigoma, tumeanza kujenga a grand High School, Shule ya Sayansi. Maana yake Waheshimiwa Wabunge mnafahamu kwamba Mwanasayansi aliyepata tuzo ya Nobel katika nchi hii, anatoka Mkoa wa Kigoma. Tumeanza kwa juhudi zetu wenyewe, tumejenga a ground high school, shule ya sayansi. Imejengwa pale Kasulu, tumejichangisha wenyewe, mkoa mzima tumepata karibu shilingi milioni 600 na tumeanza kujenga shule pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Wizara nayo, wewe Mheshimiwa Mama Ndalichako ni mdau, nawe kama Wizara na Serikali kwa ujumla mwangalie namna nzuri ya kusaidia juhudi za watu wa Kasulu na watu wa Kigoma ili hatimaye ile grand high school baadaye tuibadilishe iwe Chuo Kikuu. Kitakuwa Chuo Kikuu cha kwanza cha sayansi. Nina hakika kwa uwezo wa vijana wa Kigoma, kitatoa wanasayansi walio bora na walio mahiri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hiyo imeshaanza na wenzetu wa SUMA JKT wametupa ushirikiano mzuri sana, ndio wanatujengea eneo hili. Nasi Halmashauri ya Mji wa Kasulu tumetoa eneo bila fidia, eneo la ekari 115 nami Mbunge wao nimetumia kila lililokuwa ndani ya uwezo wangu, kuhakikisha kwamba eneo lile limepimwa na linamilikiwa kihalali sasa na Halmashauri na Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya ujenzi wa Grand High School. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nizungumzie ujenzi wa makitaba. Sisi pale katika Mji wa Kasulu tumejenga maktaba. Kipindi kile nikiwa Mbunge mwaka 2005 tulijenga maktaba kwa kushirikiana na wenzetu wa Tanzania National Parks. Tumejenga jingo kubwa, lina gorofa mbili. Jengo lile limegota, nafikiri ni wakati muafaka umefika sasa Wizara na Serikali mwingilie kati mtupe nguvu, mtusaidie ili jengo lile sasa lianze kufanya kazi. Malengo na madhumuni ni kufanya maktaba ile kiwe ni kituo cha elimu katika Mji wa Kasulu na ni mji ambao unakua kwa haraka sana kama miji mingine inavyokua katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nizungumzie suala la ukaguzi wa shule. Mheshimiwa Waziri, shule hazikaguliwi. Waheshimiwa Wabunge shule za Sekondri na za Msingi hazikaguliwi. Sasa shule hazikugaliwi…
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja hii, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii. Hata hivyo nianze na kuchangia machache katika sekta hii ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara na Serikali kuzifanya High Schools zote nchi nzima ziwe chini ya Wizara ya elimu na TAMISEMI ibaki na Primary Schools na „O‟ Level Secondary Schools tu. Hii itasaidia sana Halmashauri za Wilaya na Miji yetu kujikita zaidi kuboresha shule tajwa hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 2006/2007 Serikali iliamua kwa maksudi kusaidia Mikoa, ambayo ipo nyuma kielimu. Mikoa hiyo ni pamoja na Kigoma, Singida, Mtwara, Lindi na Katavi. Mikoa hii ilikuwa inapata fedha za ziada kila mwaka shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kusaidia kujenga madarasa, mabweni ya wasichana na nyumba za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zilisaidia sana na kwa Mkoa wa Kigoma hali ilianza kubadilika, ajabu ni kwamba, baadaye 2011/2012 fedha hizo zilisitishwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri sana fedha hiyo, irejeshwe ili Mikoa iliyobaki nyuma kielimu iweze angalau kupiga hatua. Huu ulikuwa mpango maalum ni lazima Serikali iangalie hali hii ili kuweka uwiano mzuri katika nchi yetu na baina ya Mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitengo cha Ukaguzi wa Shule; kitengo hiki kimezorota sana na sehemu nyingine shule za msingi na sekondari hazikaguliwi kabisa! Ni vizuri kitengo hiki kiwe kitengo huru na kisimamiwe na Wizara moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu malipo ya Walimu katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu; malipo ya walimu yahakikiwe vizuri na walipwe stahili zao za matibabu, likizo, likizo ya uzazi, kupanda vyeo na kadhalika. Walimu wengi wanalalamika sana, Wizara ya Elimu na TAMISEMI harakisheni uhakiki ili walimu hawa walipwe fedha zao mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Ujenzi wa Maktaba ya Wilaya Kasulu; Halmashauri ya Mji wa Kasulu tulijenga jengo la maktaba lenye ukubwa wa ghorofa mbili. Tulishirikisha wadau mbalimbali wa elimu kama vile TANAPA na UNHCR tukafika ujenzi wa asilimia 65. Tafadhali Wizara au Serikali saidieni juhudi za wananchi hawa, tupeni nguvu. Tukipata shilingi milioni 200 zitasaidia sana kukamilisha jengo hili na litaanza kutumika. Ni matarajio yetu mwaka 2016/2017, Wizara itaangalia namna njema ya kufanikisha na kukamilisha mradi huu muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ujenzi wa Kasulu Science Grand School; Mkoa wa Kigoma wenye Halmashauri Nane tumeanza mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari ya Sayansi. Mkoa wa Kigoma ulianza kazi hii kutuma Suma JKT, kazi imeanza na hadi sasa shilingi milioni 600 zimetumika. Tunaomba Serikali na Wizara ya Elimu isaidie mradi huu muhimu kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma. Tumeanza tusaidieni kukamilisha ndoto yetu ya kujenga shule hii muhimu ya sayansi. Matarajio yetu ni kwamba, shule hii baadaye tutaifanya ni Chuo Kikuu cha Sayansi na kitaitwa Kigoma University of Science and Technology.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Kasulu tumetoa eneo la ekari 115 kwa ajili ya ujenzi wa shule hii. Eneo hili limepimwa na sasa tuna – process hati ya kumiliki ardhi hiyo. Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Kigoma tumeanza, tunahitaji msaada wa Wizara ya Elimu ili ndoto yetu iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa namna ya pekee kabisa, naomba niwape hongera sana Mawaziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Simbachawene na Mheshimiwa Kairuki na Naibu Waziri, bado ni vijana na mna nguvu, tunataraji mtakimbia na kasi hii na mtafika. Pia kwa namna pekee naomba nimshukuru sana Katibu Mkuu wa Wizara yenu ni mtu msikivu sana, Alhaji Iyombe, kila ukienda ofisini kwake ni mtu wa msaada sana. Alhaji Iyombe kama unanisikia hongera sana kwa utulivu wako na utu uzima wako, endelea kulea vijana hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa na machache ya kuzungumzia. La kwanza ni utawala bora. Wakati Mheshimiwa Bashe anachangia alizungumzia habari ya majizi ambayo yanahama kutoka halmashauri moja kwenda nyingine. Mheshimiwa Waziri Mkuu maadam uko hapa nikukumbushe jambo moja kwamba moja ya majizi makubwa nililokuletea lilipelekwa Nzega kutoka Kasulu.
Mheshimiwa Simbachawene liko tatizo kubwa la wizi uliotokea pale Kasulu wa shilingi bilioni 5.9 kati ya mwaka 2013/2015 na haya majizi bado yanatembea tu na mengine yamehamishwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu katika yale majizi yaliyokubuhu, moja ya majizi yale lilitoka Kasulu likaenda Nzega na kule Nzega nimeambiwa amestaafu baada ya kutuibia pesa nyingi sana. Haiwezekani! Huyu mtu lazima atafutwe na afikishwe kwenye mikono ya sheria.
Kwa hiyo, kusema kwamba Nzega ilikuwa ni dumping ground nadhani ni kweli maana hata hilo jizi lililokubuhu lilitoka Kasulu likapelekwa Nzega. Mheshimiwa Waziri Mkuu mtusaidie majitu haya yakamatwe yafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo napenda kulizungumzia alilisema Mheshimiwa Makamba siku anachangia bajeti ya Waziri Mkuu, juu ya utawala bora. Mheshimiwa Simbachawene tuna Halmashauri zaidi ya 34 zinaongozwa na wapinzani wetu kwa maana kwamba baada ya matokeo ya uchaguzi walichaguliwa na wanaziongoza. Nawashauri sana, hizi Halmashauri ambazo zinaongozwa na wapinzani na hizi zinazoongozwa na wana CCM zenye wapinzani wengi vilevile, kuna haja kabisa ya kuzipangia mkakati wa mafunzo maalum vinginevyo hazitatawalika, wataishia kwenye ubishi tu, ndio ni zote, hazitatawalika hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku ile Mheshimiwa Makamba alisema jambo la msingi kwamba chama cha siasa kikishinda uchaguzi kinaunda Serikali, ni kweli na ndiyo utamaduni wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola. Siyo kuunda Serikali tu, kinaanza kutekeleza ilani yake ya uchaguzi na hakiishii hapo lazima kipate space ya kutawala na wapinzani wetu lazima watupe nafasi ya kutawala, hilo halina ubishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, equally the same, chama tawala nacho lazima kijue kwamba kuna nafasi ya wapinzani katika demokrasia na hiyo space lazima iwepo. Space hiyo Mheshimiwa Simbachawene haiwezi kutoka mbinguni lazima hawa watu wawe trained. Halmashauri 34 zinaongozwa na wapinzani per se lakini ziko nyingine kama 14 hivi zina wapinzani wengi kwa maana kwamba unakuta CCM tumezidi mmoja, wawili, watatu au wanne, kwa sababu ya dhana nzima ya utawala bora lazima kuwe na special program kupitia TAMISEMI kuwajengea uwezo vyama na Halmashauri zote hizi na hasa hizi ambazo zinaongozwa na CCM kwa wingi na hizi ambazo zinaongozwa na wapinzani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu wa Kambi ya Upinzani niwakumbushe kitu kimoja, opposition maana yake ni kuikumbusha Serikali ya siku isilale usingizi.
Ndiyo utamaduni huo lakini na ninyi kwa sababu mlishindwa uchaguzi mkuu lazima mtoe space ya kutawala kwa watu walioshinda na hilo hatubishani. Mimi sikuwepo siku mbili hizi nimeshukuru sana leo kuona wapinzani wanachangia ndiyo demokrasia hiyo. Ile kukimbia hupati kitu unaposema unatusaidia sisi tujue unachosema, unachofikiri lakini mkikaa kimya mlikuwa mnatunyima haki yetu.
MBUNGE FULANI: Eeeeh.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Ndiyo na mlikuwa mnafanya vibaya, lakini sasa nashukuru busara zimeingia, mmewasomesha wameelewa na tutakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo napenda nilizungumzie ni mipango miji. Mheshimiwa Simbachawene unazungumza kwenye hotuba yako upangaji wa miji na kwamba umeisha-identify miji 600, hiyo miji yenyewe iliyopo haina Maafisa wa Ardhi, Maafisa Mipango Miji na haina Valuers. Sasa niulize, hivi kuna tatizo gani la kuajiri moja kwa moja toka kwenye vyuo vyetu vya ardhi wataalam hawa wakaenda kwenye Halmashauri zetu ili kuzuia miji holela? Hili ni jambo muhimu sana, Waziri wa Ardhi uko hapa hebu mshirikiane na TAMISEMI muweze kuondoa tatizo hili. Huwezi kuzungumzia kupanga miji kama huwezi kuwa na wataalam ambao kazi yao ni kupanga miji hii. Jambo hili linawezekana na mnaweza mkalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne ni nyumba za walimu. Nadhani walimu wenzangu mtakubaliana na mimi kwamba kama kuna shida kubwa iliyopo kwenye halmashauri zetu ni nyumba za walimu jamani, walimu hawana nyumba za kukaa, kabisa. Unashangaa sasa kila Halmashauri inakuwa na utaratibu wake wa kuweka kwenye bajeti nyumba 5, 10, 12. Nilikuwa naangalia kwenye kitabu hiki cha TAMISEMI kwenye development, Mheshimiwa Simbachawene una karibu shilingi trilioni moja kwa ajili ya development. Hebu Mheshimiwa Simbachawene hizi fedha za development katika eneo la nyumba za walimu kwa nini ...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda umeisha.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia sekta hii muhimu sana ya uchukuzi, barabara, reli na kadhalika. Kwanza niwape hongera sana timu ya Profesa na mwenzake kwa kazi mnayoifanya.
Mheshimiwa Spika, nataka nijielekeze katika mambo matatu. Suala la kwanza ni suala la kisera. Tumeshakubaliana na kwa mujibu wa Sera za Chama cha Mapinduzi kwamba tutajenga barabara za lami kuunganisha mkoa na mkoa, ndivyo tulivyokubaliana. Nilikuwa najaribu kuangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, hiyo sera hamuizingatii. Mnaanza kuhamisha rasilimali na resources kuhangaika na barabara za Kata kwenda Kata na Wilaya kwenda Wilaya. Kwa nini tusianze kujenga barabara za kuunganisha mikoa kwa mikoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano sisi Mkoa wa Kigoma, nashukuru nimeona kuna juhudi inafanyika kwa barabara yetu ya Tabora – Kigoma kwamba kuna vipande vipande bado vinafanyiwa kazi na nimeona kuna mweleko mzuri. Hopefully flow ya fedha itakwenda vizuri ili barabara ile ikamilike; lakini bado sisi hatujaunganishwa na Tabora, hatujaunganishwa na Katavi, haijaunganishwa na Kagera, haijaunganishwa na Mwanza, haijaunganishwa na Shinyanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha anieleze, kwa nini wanatapanya resources wakati tumeshakubaliana kwamba mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano iunganishwe kwanza kabla ya maeneo mengine? Hilo ni jambo muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nizungumzie suala la uwiano. Jamani hii nchi ni yetu wote. Hakuna wa Tanzania bora kuliko Watanzania wengine, Watanzania wote ni sawasawa. Ukiangalia mtandao wa barabara za TANROADS na unaweza ukaenda tu ukapata picha ukurasa 279, ukiangalia zile barabara za changarawe kwa mfano, inakupa picha ya moja kwa moja kwamba kuna mikoa ambayo ina mtandao mkubwa kuliko mikoa mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, ni mpya katika awamu hii na bahati nzuri Jimbo lake ni Ikulu, hana Jimbo la uchaguzi, naomba waanze kwenda na utaratibu kuwe na uwiano, ikibidi wa-employ concept ya slow match na quick match. Wale waliotangulia sana, wasubiri wenzao. Haiwezekani unakuwa na mkoa una mtandao wa kilometa 300 wengine wana mtandao wa kilomita 600 wengine 900 wengine 800; that is very unfair. Twende kwa utaratibu mzuri (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo, sisi Mkoa wa Kigoma tumeomba barabara kupandishwa hadhi kutoka barabara za Wilaya, Halmashauri, kuwa barabara za Mkoa kwa maana ya TANROADS. Tunaomba Mheshimiwa Waziri alizingatie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano kule Kasulu kuna barabara muhimu sana, inatuunganisha kati ya Kasulu, Kabanga, Msambala, inakwenda Mwanga mpaka Wilaya mpya ya Buhigwe, kwenda border yetu na Burundi. Barabara hiyo tunaomba, Mheshimiwa Waziri kwa kibali chake tumeshapitisha kwenye RCC, inangoja timu yake ile na Kamati yake ili barabara hiyo waweze kuipandisha hadhi. Tutaomba sana! Siyo hiyo tu, ziko barabara tatu, nne za Mkoa wa Kigoma ambazo tumeomba zipandishwe hadhi na hiyo tafsiri yake itatuongezea mtandao wa barabara angalau za changarawe. Hilo lilikuwa la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, ni barababara yetu ya kihistoria ya muda mrefu nimeona imetengewa fedha, shilingi bilioni 70 Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi, Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 32 ameeleza vizuri kwamba kipande cha Kidahwe – Kasulu kuna mkandarasi yuko pale na kimetengewa fedha; na kipande cha Kabingo - Nyakanazi, nacho kimetengewa fedha, lakini hapo katikati, kuna kilometa zaidi ya 200 za Kabingo – Kibondo – Kasulu - Manyovu Border na Burundi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ameandika kwenye kitabu chake kwamba kilometa 258, amezungumza kwenye kitabu chake kwamba hiyo inafadhiliwa na fedha za African Development Bank. Sasa tungependa kujua, ameishia hapo tu na akaweka na nukta kubwa, maana yake nini? Hizo barabara zinaanza lini? Kwenye vitabu vyake vyote viwili haonyeshi bajeti au hizo fedha za ADB zitatoka lini na ni kiasi gani kwa barabara hiyo?
Mheshimiwa Spika, hiyo maana yake nini? Maana yake ni kwamba, hiyo barabara kubwa ya kihistoria ya Kigoma - Kidahwe - Nyakanazi itakuwa haijakamilika, kama hicho kipande hakijakamilika, sisi tunaotoka Kidahwe, Kasulu itakuwa imekamilika. Nilimshukuru Mheshimiwa Waziri, nilimwona akiwa Kijiji cha Kasangezi anahangaika na barabara ile. Yule Mkandarasi juzi nimemuuliza mwenyewe akaniambia amepewa fedha. Hiyo ni assuarance ya watu wa Kigoma, kwamba hiyo barabara ya kihistoria sasa inajengwa. Tunaomba flow ya fedha iendelee, barabara hiyo ni muhimu sana, kwa sababu ni barabara ya kihistoria na ni barabara ya siku nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo naomba pia nizungumzie barabara ambayo ameitaja kwenye kitabu chake, hii barabara ya Sumbawanga - Mpanda - Nyakanazi, shilingi bilioni 77. Sasa nataka kujua Mheshimiwa Waziri, hii barabara maana yake kutoka Sumbawanga ukaja mpaka Katavi - Mpanda, ukaja mpaka Uvinza - Border, ukaja mpaka Kanyani - Kasulu kwenda Nyakanazi, hiyo ni barabara ndefu sana. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri tuelewe, hizi fedha ambazo wamezitenga, shilingi bilioni 77 zinajenga sekta ipi? Maana yake ukitoka Mpanda mpaka Uvinza, unazungumza habari ya kilometa 600 ni mbali sana! Sasa napenda kujua, hizo shilingi bilioni 77.5 zinajenga sekta ipi katika barabara hiyo?
Mheshimiwa Spika, nakumbuka kulikuwa na mkakati wa kujenga barabara itoke Katavi kwa maana ya Mpanda kuja Uvinza border, ije mpaka Kanyani - Kasulu - Nyakanazi inakuwa ina-link ile barabara. Sasa tungependa kujua hizi fedha huyo mkandarasi atakuwa anaanzia wapi, anaanzia Kanyani kwenda Uvinza au anaanzia Uvinza kwenda Mpanda, kwa maana ya Mkoa wa Katavi? Mheshimiwa Waziri ningependa kuelewa kwa sababu hiyo ni barabara ndefu sana na inapewa jina refu sana, kilometa zaidi ya 600, ni barabara ndefu na ningeomba kupata maelezo ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine dogo tu, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 75 amezungumza ujenzi wa block train kwenda Kigoma na Mwanza kwa kuhudumia wafanyabiashara wa Kigoma – Mwanza – Tabora – DRC - Burundi - Uganda na kadhalika. Amezungumza habari ya vichwa vya treni, kuundwa. Yeye unajua Kiswahili; yeye ni mtu wa Zanzibar, kuundwa maana yake nini? Wanaunda vichwa vya treni au wananunua vichwa vya treni? Sijui kama ni lugha maana wanazungumza kuunda vichwa vya treni, sasa kuunda maana yake nini? Kama wanaviunda, basi napenda clarity tu, labda ni lugha, lakini ninachojua kama wanachozungumza ni kununua vichwa vya treni naweza nikaelewa. Naomba hilo jambo aliweke makini.
Mheshimiwa Spika, ukurasa 72 nafikiri nayo ni error, anazungumza habari ya ujenzi wa reli ya Arusha – Musoma, lakini anazungumza habari ya matawi yake ya Tabora – Mwanza. Mheshimiwa Waziri hiyo jiografia imekosewa; hakuna ujenzi wa reli ya Arusha – Musoma ukawa na matawi ya Tabora kwenda Mwanza. Halafu anazungumza habari ya tawi la kwenda Minjingu na matawi ya kwenda Engaruka, angalieni jiografia hiyo msije mkajichanganya katika utekelezaji wa miradii hii ya reli, hiyo iko ukurasa wa 72.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, juhudi ni nzuri, Mheshimiwa Waziri endelea, tuna matumaini makubwa na naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi na hongera kwa Waziri, Profesa Mbarawa na Naibu Waziri wake na timu nzima ya Wizara. Mmeanza vizuri, endeleeni kwa kasi hiyo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache kuhusu barabara ya Kidahwe - Kasulu kilometa 50, fedha shilingi bilioni 19.3. Kutoka Kidahwe hadi Kasulu Mjini ni kilometa 60; je, ina maana kilometa 10 zinazobakia zitajengwa lini? Ni vizuri barabara yote ya Kidahwe - Kasulu, kilometa 60, zikajengwa pamoja bila kuacha kiporo au kipande hicho; tafadhali Wizara angalieni jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kasulu – Kibondo – Kabingo na Kasulu – Manyovu, Mheshimiwa Waziri umesema itakuwa financed na ADB kama sehemu ya mkakati wa Sekretarieti ya EAC. Ni vizuri tukajua time frame ya ujenzi wa barabara hii, ni barabara ndefu, kilometa 2,258; tafadhali Wizara pamoja na Wizara ya Fedha muipe kipaumbele barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupandisha hadhi barabara za Mkoa wa Kigoma. Mheshimiwa Waziri, Mkoa wa Kigoma ni kati ya mikoa yenye mtandao mdogo kabisa wa barabara za mikoa (Regional Roads). Tafadhali, pandisha au toa idhini ya kupandishwa barabara zifuatazo kuwa barabara za mkoa:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kasulu – Kabanga – Msambara – Mwaufa – Mganza hadi Herujuu; barabara ya Nkundutsi – Malamba – Muhunga – Herujuu; barabara ya Buhigwe – Muyama – Kasumo – Mwanga – Mganza – Herujuu. Barabara hizi zina sifa na kitakuwa kichocheo za kukuza uchumi na zina sifa zote stahili kupandishwa hadhi kuwa Regional Roads.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii. Hata hivyo, nashauri niseme machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Wilaya ya Kasulu kuanzisha Baraza la Ardhi tangu mwezi Aprili, 2016. Nashauri basi wataalam hao wafike haraka Kasulu ili Baraza lianze kazi mara moja. Ni hatua nzuri yenye manufaa kwa Wilaya za Kasulu na Buhigwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo uhaba mkubwa sana wa Maafisa Ardhi na Maafisa Mpango Miji. Ni vizuri Serikali iliangalie jambo hili ili wahitimu wa vyuo vyetu vya ardhi waajiriwe moja kwa moja bila kusubiri nafasi hizo eti zitangazwe, ni jambo muhimu sana. Kama walimu wanaajiriwa moja kwa moja, kwa nini isiwe hivyo kwa wapimaji wa ardhi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara sasa iongeze hoja hii Serikalini ili mwaka huu shida hii kwenye Halmashauri, Wilaya, Manispaa na Miji imalizike. Kasulu Town Council ina uhaba mkubwa wa upimaji ardhi, valuers na Afisa Mipango miji yupo mmoja. Hatuna muda wa kusubiri, wakati ni sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu zoezi hili hati za ardhi za kimila limefanyika nchi nzima, Wilaya ya Kasulu na hasa vijiji vinavyounda Halmashauri ya Mji bado hati hazijatolewa, licha ya baadhi ya vijiji kupimwa. Ni muhimu sasa zoezi la kutoa hati za kimila lihamie Wilaya ya Kasulu na hasa vijiji vya Nyumbigwa, Mhunga, Malumba Herujuu, Karanga, Mpanza na Masambara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Kasulu (Kasulu Town Council) tumetenga ardhi, viwanja kwa ajili ya wawekezaji wa nyumba na hasa nyumba za gharama nafuu za NHC. Tafadhali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri, aagize NHC waje sasa Kasulu, soko ni zuri kwa sababu sasa Kasulu ina Halmashauri mbili; Kasulu DC na Kasulu TC, nyumba zinahitajika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mahitaji ya nyumba za walimu na waganga ni kubwa, mfano Wilaya ya Kasulu, Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Wilaya, mahitaji ya nyumba ni zaidi ya nyumba 2000. Kwa nini NHC wasiagizwe kufanya kazi hiyo badala ya Halmashauri ya Wilaya kujenga nyumba chache chache kwa kipindi kirefu? Hii inaweza kufanywa kwa uamuzi wa Serikali na hasa Wizara yako ili NHC wasijikite mijini tu na waelekezwe kupeleka nguvu maeneo ya vijijini wakajenge nyumba za gharama nafuu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa namna ya pekee naomba niwape hongera nyingi sana Waziri na Naibu Waziri na timu nzima ya wenzetu wa Wizara ya Maliasili. Naomba pia niwape hongera za dhati kabisa Mhifadhi Mkuu na Wahifadhi wa Gombe na Mahale National Parks kule Kigoma, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasema ninachotaka kusema, mimi hii Kampuni ya Green Miles naifahamu, nilikuwa kwenye Tume ya Wanyamapori. Kama haya yanayosemwa na Kambi ya Upinzani ni ya kweli, basi lipo tatizo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo kampuni ya Green Miles tulii-disqualify nikiwa kwenye Tume kwa sababu ilikosa sifa. Nafikiri ni mambo ambayo Wizara mnaweza mkakaa na wenzenu mkayafanyia kazi vizuri kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri. Moja ya disqualification yao waliidanganya Tume kipindi kile na kwa kweli tukawa-disqualify. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara na wataalam wenu mkae chini ikibidi mwende kule kwenye eneo lenyewe muweze kujiridhisha na hali halisi iliyopo pale. Maana yake nakumbuka Waziri wa Maliasili aliyepita hiyo kampuni aliinyang‟anya leseni kwa kukosa sifa. Sasa nasema haya mambo yako ndani ya Wizara, mnaweza mkaangalia namna ya kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie juu ya ikolojia ya Kigosi Moyowosi. Hii ikolojia Kigosi Moyowosi inaanzia Mkoa wa Shinyanga eneo la Bukombe inakuja Kibondo inakwenda Kasulu mpaka Uvinza. Naomba niseme eneo hili limevamiwa na mifugo wengi sana na kusema ukweli linatishia uhai wa Mto Malagarasi na siyo Mto Malagarasi tu inatishia hata chepechepe (wet land area) ya Mto Malagarasi na hakika inatishia uwepo wa Ziwa Tanganyika. Nadhani ni jambo muhimu sana Serikali ikae na kuangalia namna njema na nzuri ya kuwaondoa hawa wafugaji na kuwatafutia maeneo mengine ya kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme siyo jambo jema sana Mheshimiwa Waziri mkaanza kuwa na utamaduni wa kuua ng‟ombe kwa risasi, hilo jambo linatufedhehesha sana kwa kweli. Kama nchi kunakuwa na makosa yamefanyika basi nchi hii ni ya kiistaarabu yatatuliwe kistaarabu. Wafugaji hawa waelekezwe, waondoshwe kwenye hifadhi, wasiharibu mazingira yetu, lakini kitendo cha kuua ng‟ombe, kupiga risasi ng‟ombe kinaturudisha kwenye ujima kwa kweli siyo ustaarabu wa leo. Naomba hilo jambo lizingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ikolojia hiyo hiyo ya Moyowosi kuna msitu mashuhuri sana unaitwa Msitu wa Makere Kusini maarufu kama Pori la Kagera Nkanda. Hilo pori lilikuwa gazetted mwaka 1954, Septemba, nina hakika Wabunge wengi mlikuwa hamjazaliwa kwa sababu hata mimi mwenyewe nilikuwa sijazaliwa. Eneo hilo lilikuwa halina watu kipindi hicho lakini sasa hivi limejaa watu na kuna misuguano mikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia hotuba ya Waziri inazungumzia juu ya usimamizi wa misitu na Wakala kufanya mapitio, ukurasa wa 59 wa hotuba yake. Katika hilo eneo la Kagera Nkanda lenye wanavijiji wengi kuna migongano ya wakulima na hawa wenzetu wa TFS. Naomba mipaka ile ya mwaka 1954 iweze kuhuishwa hawa wakulima wapate maeneo yao ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda nimuarifu Profesa kwamba ikolojia ile haitishiwi na kilimo cha wananchi wale wa vijiji vya Wilaya ya Kasulu bali ikolojia ile inatishiwa na mifugo mingi toka nchi jirani na mifugo mingi inayoingia katika eneo lile bila utaratibu. Tafadhali sana, kama alivyobainisha ukurasa wa 59 wa hotuba yake, naomba mipaka ile ihuishwe vizuri, tena wametumia neno zuri soroveya. Tunaomba usoroveya huo mkaurudie upya ili yale maeneo ambayo wananchi wameyalima kwa muda mrefu waendelee kuyatumia bila kuwasumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wenzetu wa TFS wamekuwa ni walaji rushwa, wanasumbua watu wetu na kusema kweli hakuna tija hata kidogo. Mheshimiwa Waziri naomba hilo alizingatie na nimeshazungumza naye. Wananchi wetu wa vijiji vinavyozunguka pori lile wamekuwa wakilima pale kwa miaka 20 iliyopita na tumewazuia sisi kama Halmashauri wasikate miti wanalima kilimo rafiki. Kwa hiyo, ni muhimu sana Profesa akatoa maelekezo hawa watu wa TFS wasiwasumbue waendelee kujikimu kupata maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri ningeomba Sheria ya Misitu Na.14 itazamwe upya kwani imepitwa na wakati.
Nchi hii ina watu wengi sasa, kabla watu hawakuwa wengi kiasi hiki. Ni vyema sheria hii ingeangaliwa na kusema kweli yale maeneo ambayo yamekosa sifa, yako maeneo Profesa yamekosa sifa kwa mfano mapori ya akiba na open area wapewe wananchi wakiwemo wafugaji tupunguze migogoro hii ambayo kama Taifa inatufedhehesha kwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja mdogo, kwa mfano eneo la wazi la Wembere lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 10,000 limepoteza sifa, hakuna mnyama tena, wananchi wanakatakata mikaa mle lakini hawa watu wa maliasili wanazuia watu kufanya shughuli zao. Maeneo kama hayo mngeyahuisha tukapunguza migogoro hii ya wakulima na wafugaji ili watu wafanye shughuli zao kwa sababu yale maeneo hayana sifa tena ya uhifadhi na yako mengi tu mkifanya tathmini mtagundua hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda nilizungumzie ni kuhusu Sekta ya Utalii. Ukisoma hotuba ya Waziri ukurasa wa 81 unazungumza Wizara na World Bank kuandaa mpango mkakati wa kuendeleza utalii, ni jambo jema, lakini hawajaeleza time frame ya huo mpango mkakati wao. Ukurasa wa 89 umezungumzia kuainisha vivutio vya utalii nchini na wametaja Mikoa ya Mwanza, Mara, Kigoma, Geita na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Wizara, nilidhani kuanza kubainisha vivutio vya utalii pamoja na vivutio vya utamaduni ingekuwa ni input kwenye mpango mkakati wa Wizara. Kipi kinaanza, bila shaka unaanza mpango mkakati kabla ya kuzungumzia habari ya vivutio na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 81 na 89 wa hotuba ya Wizara, naomba wautazame upya ili kuleta maana zaidi kwamba lazima uanze na mpango mkakati halafu vivutio vya utalii katika Mikoa ya Kigoma, Mwanza, Mara na kadhalika pamoja na culture tourism ziwe ni input kwenye mpango mkakati wenu. Bila shaka kama mnafanya kazi hiyo na World Bank ingekuwa jambo la busara sana basi mpango mkakati huo uwe na time frame na mtueleze katika mpango mkakati huo mmeandaa kufanya mambo gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri baada ya mpango mkakati kukamilika, basi tu kwa mahusiano mema na Wabunge wenzake, Waziri atuletee mpango mkakati huo tuuone ili tuweze kuwasadia baadhi ya mambo ambayo tunafikiri yanafaa kuwemo katika mkakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo napenda niliseme kwa ujumla wake kwa Mheshimiwa Waziri, ni kutangaza utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo hasa Kagera Nkanda, naunga mkono hoja hii. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba kwa namna ya pekee nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niseme machache. Mengi yameshasemwa, nami nitakuwa na machache kabisa. Naomba pia, Waziri wa Fedha, Ndugu Mpango na Naibu wake na timu yake niwape hongera kwa kazi. Changamoto bado ni kubwa kwa sababu ndiyo tumeanza bajeti. Kwa hiyo, tumeanza vizuri, nina hakika tutakwenda katika muktadha huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabla sijaanza kusema ninayotaka kusema, nikuombe wewe mwenyewe kitu kimoja. Wewe Naibu Spika sasa hivi ndio mkubwa wa Bunge hili, nawe hakuna mashaka kabisa, uwezo wako tumeuona wote hauna mashaka hata chembe! Uwezo wako ni mkubwa, lakini wewe ni mkubwa wa taasisi hii sasa. Hivi Waheshimiwa Wabunge wa CCM naomba niwaulize swali moja, hivi sisi tukiwasamehe hawa tunakosa nini? Naomba mnisaidie tu, wewe ndio mkubwa wa mhimili huu; hivi Wapinzani hawa ambao wanakuonea wewe bila sababu, tukiwasamehe tunakosa kitu gani? Sisi ni Chama kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba, hatuna mashaka nawe, uwezo wako ni mkubwa, linda mhimili huu. Kamati ya Uongozi mkutane, Mama Naibu Spika una uwezo mkubwa, tuwahurumie hawa; wewe ni Mkristo, unasali; tuwahurumie hawa. Nami nina hakika, maana leo ukiwauliza kwa nini wametoka, sababu hawana, lakini na sisi tuulizane sisi tunapata faida gani wao kutoka hawa? Mnijibu swali, tunapata faida gani? (Kelele)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unilinde, hoja yangu mimi nasema, sisi ni Chama kikubwa, tuna maslahi mapana ya kufanya, tuna kazi ya kufanya. Nakuomba kama Mkuu wa mhimili huu, mkae tumalize stalemate hii, haitusaidii kama Chama. Hayo yalikuwa ni mawazo yangu mimi. (Kelele)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hata kama halipendezi, lazima lisemwe. (Kelele/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa niliseme, nataka nijielekeze kwenye kitabu hiki cha Kamati ya Mheshimiwa Mama Hawa, Kamati ya Bajeti. Waheshimiwa Wabunge, ukurasa wa 28 na 29 wa Kitabu hiki cha Kamati, Kamati ya wenzetu wa Bajeti wananung‟unika, wanasema Serikali haijasikiliza maoni ya Wabunge. Yameandikwa humu ndani, naomba ninukuu;
“Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa Kamati ya Bajeti katika utekelezaji wa bajeti hii kwa kiasi kikubwa Serikali haikuzingatia maoni na majukumu ya Kamati ya Bunge ya Bajeti. Masuala la kibajeti ambayo ni ya kisheria Kamati hii imeona Serikali inayapuuza. Bunge linataka kufanywa kama rubber stamp kwa kuidhinisha bajeti ya Serikali.”
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, narudia tena maneno yangu, wewe ni mkuu wa mhimili huu, linda hadhi ya Bunge. Kama liko tatizo limetokea kwenye Kamati ya Bajeti, ni vizuri kabisa Serikali wakae na Kamati ya Bajeti waelewane. Kwa sababu, Kamati ya Bajeti ndiyo inatusemea sisi Waheshimiwa Wabunge. Sisi wote hatuwezi kuwa kwenye Kamati ya Bajeti. Haiwezekani tuwe na Serikali ambayo haipokei ushauri wa Kamati ya Bajeti. Haiwezekani, mhimili huu tutauharibu, tutauvunjia heshima na Bunge ni chombo cha heshima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba, yako mambo mengi yamezungumzwa na wenzetu wa Kamati ya Bajeti, hayapendezi. Wanalalamika! Haiwezekani Bunge letu sisi wenyewe, Bunge la Chama cha Mapinduzi wasisikie maoni ya Kamati ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, haiwezekani! Nakuomba jambo hili ulichukulie kwa uzito unaofaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 29 wa maoni ya Kamati hii wanasema, utaratibu wa Kikanuni wa kupokea hoja wakati wa kujadili bajeti umekaa vibaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni mwanasheria mzuri, tafadhali tuongoze vizuri. Hii Kanuni kama imekaa vibaya, tuiangalie upya ili Bunge liwe na maana katika upitishaji wa bajeti ya Serikali, vinginevyo tutakuwa rubber stamp tu.

TAARIFA....

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe Taarifa kaka yangu Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko kwa kutumia Kanuni ya 68(7) kwamba humu ndani hakuna Mbunge wa Upinzani aliyefukuzwa na Naibu Spika. Kwa hiyo, kusema Naibu Spika uwasamehe, ni kuondoa ukweli kwamba walioadhibiwa wameadhibiwa na Bunge zima na siyo Naibu Spika. Hawa waliotoka, wameondolewa na Mwenyekiti wao wa Chama, nami wameniomba niwatetee na ndiyo maana nimesema pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ulinde muda wangu. Hiyo hoja anayoizungumza Mheshimiwa Lusinde naikubali, wala sina matatizo nayo. Hoja yangu ni kwamba, sisi ni Chama kikubwa, ndiyo chenye ajenda. Hata hao wakitoka mwaka mzima hawana cha kupoteza hawa. Sisi ndio tuna ajenda yetu, ndiyo hoja yangu tu iko hapo. (Kelele/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tafadhali muda wangu ulindwe. Nilikuwa nazungumzia juu ya Kanuni ambapo wewe ni Mtaalam, jambo hilo mlizingatie.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba pia nizungumzie makato ya pensheni. Nimesikiliza maoni yakitolewa hapa, lakini naomba tu niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge sio Watumishi wa Serikali. Sisi Wabunge hatuna pensheni. Hatuna hata Bima ya Afya, ukimaliza miaka mitano ndiyo imetoka, haupo tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sielewi hata kidogo msingi kabisa wa kukata pensheni ya Wabunge, siuoni hata kidogo. Sababu zitakuwa ni nyingi. Kwa mujibu wa utaratibu, pensheni yenyewe ni kama posho tu. Pensheni siyo malipo ya moja kwa moja, ni kale kapesa unapewa kwamba Mbunge wewe kajikimu baada ya kazi yako ya miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha anakakata panga, kama alivyosema kijana hapa ili iweje? Waheshimiwa Wabunge, jambo hili halikubaliki kwa sababu, kwanza ni la kibaguzi. Kama hoja ni hiyo, ili Wabunge tuwe fair kwa mujibu wa ile Sheria ya Mwaka 1999 ya Political Pensioners Act, basi wale wote waliotajwa kwenye Act ile waorodheshwe tulipe kodi kama tunataka kuwa fair. Kwa nini Serikali wana-single out Waheshimiwa Wabunge tu? Hakuna sababu ya msingi. Labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze hoja ya msingi, kwa nini wanafikiri ni Wabunge tu ndio wawe liable kwa kukatwa pesa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vinginevyo jambo hili mrudi kwenye Kamati ya Bajeti. Hata kwenye Kamati ya Bajeti nao wanashangaa, wanalilalamikia vilevile. Hatuwezi kuwa na Bunge ambalo Wabunge hawasikilizwi, haiwezekani; na sauti ya Wabunge iko kwenye Kamati zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili hata Mheshimiwa Mama Hawa Ghasia kasema kwenye kitabu chake; hata Kamati ya Bajeti hawalijui jambo hili, Serikali wanalitoa wapi? Kwa hiyo, bado naamini kabisa, kama walivyosema wenzangu, bado kukata posho ya Wabunge hawa wakimaliza miaka yao mitano siyo sahihi na ni jambo ambalo halikubaliki, wakalitazame upya kwenye Kamati ya Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa niliseme, limesemwa sana hili la biashara ya utalii. Mheshimiwa Waziri wala huhitaji mtu kwenda shule kuliona. Wapinzani wetu wakubwa wa biashara hii ni Kenya; wapinzani wetu wa biashara hii ni Rwanda; wapinzani wetu wa biashara hii ni Uganda; wote wameondoa VAT, wewe unaitoa wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, biashara hii tukiweka VAT maana yake watalii hawatakuja. Kama hawatakuja maana yake tutapata hasara. Tukipata hasara, hata hayo mapato ya Serikali yatashuka bila shaka. Kwa hiyo, naomba hii VAT kwenye biashara ya utalii ni jambo ambalo halikubaliki wala halina msingi wowote katika mazingira haya ya ushindani.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa niliseme ni hizi milioni 50 kwa kila kijiji. Ushauri wangu kwa Serikali, tujifunze kutokana na mamilioni ya JK. Tujifunze kutokana na experience ya mamilioni ya JK. Bahati nzuri kipindi kile nilikuwa Serikalini, zile fedha hazikuwa na impact yoyote, ni kwa sababu zilitumika vibaya. Sasa na hizi fedha shilingi milioni 50 kwa kila kijiji kwa muktadha huu kwamba tukafungue SACCOS ziende kwenye vijiji hazitakuwa na impact iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mmoja alizungumza jana jambo hili, ni vyema fedha hizi tukaangalia namna nzuri ya kuzitumia, hata kama maana yake ni kwenda ku-push on kwenye mbolea, kwenye viuatilifu na madawa ya mifugo ili wananchi hawa kama ni mkulima apate mbolea kwa bei ya Coca Cola. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi, vijiji viko vingi sana. Jimboni kwangu au Wilaya ya Kasulu kuna vijiji 108, mara milioni 50 ni takriban shilingi bilioni tano. Hizo shilingi bilioni tano ukizishusha kwenye pembejeo za kilimo, watu watakwenda kununua mbolea kama wanavyonunua Coca Cola na shida itakwisha. Tutakwenda kuwaeleza na jambo hili litakuwa na maana zaidi kuliko hivi tunavyofikiria eti kwenda kufungua SACCOS katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho nizungumzie miradi ya kipaumbele. Miradi ya kipaumbele ambayo imezungumzwa ni pamoja na barabara zetu muhimu; Bandari ya Dar es Salaam, Reli ya Kati, Barabara ya Kidahwe – Nyakanazi. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-wind up ningependa kuelewa vizuri status ya hii miradi ya East Africa; miradi hii ya Afrika Mashariki ambayo katika ile barabara ya Kidahwe – Nyakanazi kuna portion ya kwenda Manyovu na kuna portion ya Kabingo – Kasulu ambayo inakuwa financed na East Africa. Napenda kujua status yake ili tuweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ni dhahiri naunga mkono hoja kwa sababu ndiyo wanaanza, lakini mshirikiane na Kamati ya Bajeti. Serikali msiwe peke yenu. Nawashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba kwa namna ya pekee kabisa nikupe hongera sana Balozi Mahiga na Naibu wako. Na kweli tuwape hongera sana Mabalozi wetu wanaofanya kazi nchi za nje katika mazingira magumu. Wengine wanafanya kazi katika mazingira ambayo sio rafiki sana, hawana vitendea kazi, hawana staff wa kutosha, lakini wameendelea kufanya kazi kwa moyo mmoja, tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa naomba nianze na hili moja na Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba ulisikie hili. Lipo tatizo, nilikuwa nafikiri ni muhimu Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi, Wabunge wa Upinzani, tuwe na mafunzo maalum ya diplomasia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama ni ya siku mbili, siku tatu. Unajua Mheshimiwa Msigwa kuna mambo mengine hayasemwi hadharani. Kuna mambo mengine hayasemwi hadharani na kuna mambo mengine yanasemwa hadharani. Katika utamaduni wa diplomasia kuna mambo ambayo unaweza ukayasema tu hadharani na mengine yanazungumzwa ndani, under camera. Kwa hiyo, niombe, huko ndani nyuma kulikuwa na utamaduni huu kwamba Bunge linakaa, Balozi Mahiga na uzoefu wako unakuja na wenzako mnatupiga shule sawasawa, tunaelewa. Hata makatazo mnatueleza kwamba hiki usifanye na hiki ufanye. Maana haitoshi tu kwamba, wewe ni Mbunge unakwenda kukutana na Mabalozi, unakutana nao kuzungumza kitu gani? Kuna mambo mengine ambayo yanagusa uhai wa Taifa letu yana namna yake ya kuyazungumza na hata Bunge la mwaka 2005, Bunge la mwaka 2000 yote yalifanyika mafunzo yaliendeshwa na Wabunge walifundishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge kujifunza hakuishi, unaweza ukakaa unasema sema maneno hapa kwa sababu tu pengine hujui vizuri au unafikiri kila kitu lazima kisemwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Mheshimiwa Balozi nikurudishe kwenye kitabu chako ukurasa wa 118, nianze na kuzungumzia ujenzi wa Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja na pia nimeona imeambana na kipeperushi hiki hapa ambacho kinazungumzia Vituo vya Pamoja na Utoaji wa Huduma Mipakani. Naomba nikukumbushe tu, umeorodhesha vituo saba, lakini katika kipeperushi hiki umeongezea habari ya Vituo vya Kasumulu kule Songwe, Malawi na Mtambaswala na kwenye border ya Tanzania na Msumbiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nikukumbushe kitu kimoja kwamba kuna vituo muhimu sana umevisahau. Kuna kituo muhimu sana cha forodha, kiko kwenye mpaka wetu wa Burundi, sehemu ya Manyovu na Burundi, ni border post ya muda mrefu sana na Serikali ya Tanzania kimkakati ilishajenga barabara ya lami kutoka bandari ya Kigoma mpaka kwenye border na wenzetu wamejenga barabara ya lami kuanzia border pale kwenda Bujumbura. Sasa kituo kile ni cha siku nyingi sana, sasa katika orodha hii sikioni. Nilikuwa nafikiri kama sio oversight basi mkiongeze na kiweze kupewa fedha kikarabatiwe vizuri. Mpaka wa Manyovu ni mpaka wa siku nyingi na ni mpaka wa kihistoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kingine cha forodha, ambacho umekisahau Mheshimiwa Waziri ni Kituo cha Forodha cha Mabamba na Burundi ni Kituo cha Forodha cha muda mrefu, kiko katika Wilaya ya Kibondo, hiyo Manyovu iko Wilaya ya Buhigwe. Nilikuwa naomba katika vituo vile ambavyo vinahitajiwa kufanyiwa ukarabati, Mheshimiwa Waziri ni vyema mkavitazama vituo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba, swali langu la pili Mheshimiwa Waziri, naomba Balozi unisaidie utakapokuwa unahitimisha, ni vigezo gani mnavitumia tunapoanzisha Ubalozi mpya? Ningependa kujua vigezo, ambavyo vinatumika kwa mfano, mimi mpaka leo sielewi ni kwa nini hatuna Ubalozi Seoul - Korea ya Kusini? (Makofi)
Mheshmiwa Mwenyekiti, nchi ya Burundi ina Ubalozi pale, nchi ya Zambia ina Ubalozi pale. Niliishi pale Seoul, kwa nini sisi Tanzania hatuna Ubalozi pale? Na mnajua wenzetu Wakorea hawa na katika diplomasia ya kiuchumi ndiyo wametujengea Daraja la Malagarasi.
Mheshmiwa Mwenyekiti, mtu akikuuliza moja ya vitu halisi vya kuonyesha ni kwamba Daraja la Mto Malagarasi na viunga vyake limejengwa kwa sababu ya ushirikiano ulioanzia Foreing Affairs kwa kweli na ni jitihada za Mheshimiwa Kikwete akiwa Waziri wa Foreign Affairs, ambaye alizungumza na wenzetu wale, hatimaye tukapa daraja lile. Sielewi kwa nini hatuna Ubalozi pale. Seoul - Korea ya Kusini mnajua ni nchi, ambayo imepiga hatua kubwa katika TEHAMA, katika ujenzi, katika kilimo, ni muhimu Mheshimiwa Waziri utakapohitimisha unieleze ni kwa nini hatuna ofisi pale Seoul?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, ambalo ningependa niliseme ni kuhusu Wakimbizi. Sisi Mkoa wa Kigoma tumepokea wakimbizi tangu uhuru, lakini bado wakimbizi wanaingia katika nchi zetu. Nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri kupitia ofisi yako pale ofisini kwako kwenye Foreign Services anzisheni kitengo cha wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kitengo cha wakimbizi kilichopo Mambo ya Ndani kina deal na usalama zaidi wa wakimbizi. Lakini sisi ambao tumeathirika na ujio wa wakimbizi, ambao Mabalozi wengi wanakuja Kigoma pale, Mabalozi wengi wanakuja Kasulu pale, Mabalozi wengi wanakwenda Kibondo pale hatuna namna ambayo tuna kiunganishi cha kwamba Mabalozi hawa sasa wanaokuja kuhudumia wakimbizi kuwe na jitihada maalum hasa ya kusaidia maeneo, ambayo yameathirika na ujio wa wakimbizi.
Mheshimiwa Balozi, mwezi Januari nilibahatika kukutana na Mabalozi sita waliokuja kutembelea kambi za wakimbizi, tumezungumza mengi sana nikahisi ni wakati sasa kwenye ofisi yako au ofisi yako muwe na uhusianao wa karibu kati ya Kitengo cha Wakimbizi Mambo ya Ndani na Kitengo cha Wakimbizi katika ofisi zako ambacho kitakuwa kina-raise masuala haya na hasa huduma kwa maeneo ambayo yameathirika na ujio wa wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nizungumzie suala la migogoro. Alisema ndugu yangu mmoja suala la Kongo, Mheshimiwa Balozi Mahiga, lazima tuilinde Kongo ya Mashariki, lazima tuilinde DRC kimkakati, wale ni partners wetu katika biashara. Kwa sababu tuna askari wetu kule ambao wanafanya kazi nzuri sana na nimwombe Waziri wa Ulinzi wale askari wasitoke Kongo wanatufanyia kazi nzuri sana, naomba tuilinde DRC kimkakati kama partners wetu wa kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naunga mkono kwamba wakati umefika pale Lubumbashi angalau tuwe na Ofisi ndogo ya Kibalozi kwa ajili ya kulinda maslahi yetu kama nchi. Ile ni nchi kubwa, nchi yenye utajiri mkubwa na kusema kweli tunaweza tukanufaika nayo kwa msingi huo, naomba uyazingatie hayo.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Nsanzugwanko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii. Hata hivyo, niseme machache. Kwanza, nianze na suala la usalama. Katika nchi za maziwa makubwa hali ya usalama ni tete sana, hali siyo shwari katika nchi nyingi za majirani. Kenya hali siyo nzuri; Uchaguzi Mkuu wa mwaka kesho nchini humo inatia shaka kama usalama utakuwepo. Ukabila nchini Kenya sasa ni kidonda ndugu. Hatari iliyopo ni kutengeneza wakimbizi na wengi watakimbilia Tanzania. Tanzania ichukue jukumu la usuluhishi na upatanishi ili tuwe salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepeleka vijana (Askari) kurejesha amani Kongo; ni jambo jema sana. Tuilinde Kongo kimkakati kama mbia wetu wa biashara na Foreign Service. Anzisheni Ofisi ndogo ya biashara pale Lubumbashi ili tulinde maslahi yetu ya kiuchumi na kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu Mgogoro wa Burundi na Usuluhishi. Juhudi zinazoendelea pale Arusha ni njema sana. Ni vizuri katika usuluhishi ule pia, washirikishwe Viongozi wa Dini hasa Wakristo na Waislamu. Haya ni makundi mahususi ambayo yanaweza kusaidia kuwezesha mawasiliano na maelewano. Zaidi usuluhishi huo pia, ushirikishe Baraza la Wazee (Council of Elders) ambalo linaweza kuundwa na Elders waliopo katika Mkoa wa Kigoma na Wilaya za Biharamulo na Ngara. Tamaduni za maeneo hayo zinafanana sana na hali/mazingira yaliyopo Burundi, hata lugha yetu ni moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Kutangaza Lugha yetu ya Kiswahili kilichopo Addis Ababa, Ethiopia, kimeendelezwa kiasi gani? Kimeleta ajira ngapi kwa vijana wetu? Tunataka Kiswahili kiwe bidhaa tena bidhaa ambayo itatuongezea mapato kama Taifa. Kwa nini hadi sasa Kiswahili hakitumiki kama lugha rasmi ya EAC? Tatizo ni nini? We have to promote Kiswahili now.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni watumishi wangapi wa vyeo vya juu wameajiriwa pale Head Quarters iliyopo Arusha? Ni watumishi wangapi wa vyeo vya kati walioajiriwa na EAC Head Quarters pale Arusha? Watumishi wa vyeo vya chini/operating staff, wahudumu/drivers ni wangapi? Nataka kujua pia tunavyonufaika na EAC kuwapo katika ardhi ya Tanzania kiajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna protocol yoyote katika nchi wanachama za kuhakikisha demokrasia inakua na kustawi katika Jumuiya hii? Kitendo cha kung‟ang‟ania madaraka kwa Viongozi katika Jumuiya hii ni hatari sana, kitaua ustawi wa jamii na uhuru wa watu wetu. Tanzania must take lead; tuzungumze, tushauri na tuongoze juhudi hizi za kujenga demokrasia hii ambayo ni changa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono jitihada zinazofanyika katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa 2016/2017 hadi 2020/2021, mkakati ni mzuri uelekeo unatoa picha kubwa ya matumaini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza, Utekelezaji wa Miradi ya Kipaumbele kama Taifa; Ushauri, miradi ya kielelezo itekelezwe kwa umakini kama Taifa, we need action and not words. Miradi ya Reli ya Kati, Kanda Maalum za Kiuchumi, Bagamoyo, Kigoma, Mtwara na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Kidahwe-Nyakanazi na Manyovu, Kasulu; miradi hii ni muhimu sana itekelezwe hata kama ni kukopa fedha kutoka nje au ndani, imepangwa vizuri itekelezwe kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili, ukurasa wa 28; Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Kikosi Kazi cha Maboresho ya Kodi kiangalie vyanzo vipya vya mapato (New Tax Revenues) mfano, angalieni Economic za Uvuvi wa Bahari Kuu, tunaambiwa ni eneo lenye kuweza kuchangia pato kubwa la Taifa hili. Uzoefu wa nchi za Singapore, Thailand na Austria unatoa rejea sahihi kabisa. Tuwekeze huko, tununue meli ya uvuvi na tuboreshe gati namba Sita, ambayo imetolewa na Mamlaka ya Bandari (TPA), kama bandari yetu kituo cha kupokea mavuno hayo ya Bahari Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi za Umma ambazo Serikali inamiliki hisa zake ukurasa wa 43 hadi 44 wa hotuba ya Waziri; taasisi za Tipper, PUMA Energy, Kilombero Sugar ni taasisi ambazo Serikali yetu ina hisa, lazima tuwekeze huko. Taasisi za Tipper na PUMA Energy ambako Serikali ina asilimia 50 ni maeneo ambayo yakisimamiwa vema na Serikali kuweka nguvu yanaweza kuongeza pato la Taifa letu. Kampuni hizo zipewe support ili zizalishe mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushiriki wa sekta binafsi kupitia PPP; Mheshimiwa Waziri, dhana hii inafahamika vizuri Serikalini? Ipo wapi miradi ya PPP mfano, ujenzi wa barabara ya Chalinze- Dar es Salaam wako wapi sekta binafsi? Ushiriki mdogo wa sekta binafsi kutokana na Mazingira yasiyowezeshi ya uwekezaji, angalieni upya vikwazo vinavyokwamisha ushiriki wa private sector, tatizo lazima libainishwe na lipatiwe dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 40 kupitia upya ada, ushuru na tozo ili kuzirekebisha ziendane na maendeleo na ustawi wa jamii. Kikosi kazi kiangalie tozo kwenye pamba, kahawa, tumbaku, mkonge, chai na kadhalika ili mazao haya yalimwe kwa tija bora zaidi kuliko ilivyo sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru. Mimi nitakuwa na machache tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja nataka tuweke angalizo kuhusu hifadhi zetu na mifugo. Waheshimiwa Wabunge tusipokuwa makini baada ya miaka michache tutakuwa hakuna wildlife nchi hii. Hii ya wafugaji kung’ang’ania kwenye hifadhi zetu eti tu kwa sababu bwana mkubwa alisema msitoke, hii siyo sahihi jamani. This country tuta-wipe-up wildlife yote ya nchi hii. Nadhani hoja ya msingi ambayo nafikiri Serikali ingekwenda kuifanyia kazi ni ile Tume ya Waziri Mkuu ya zile Wizara tano ziharakishe kufanya zoezi lile ili yale maeneo ambayo yamekosa sifa ya uhifadhi ndiyo mifugo ihamishiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Ngorogoro hamjui mkakati uliopo wa Wakenya hapa, wanataka kui-suffocate Ngorongoro hatimaye tuiue Serengeti ili wabaki na advantage ya Masai Mara ya Kenya. Nilikuwa naweka tu angalizo ili tuweze kuelewana vizuri na watu wa maliasili nadhani jambo hili hatuwezi kulifumbia macho, tusipokuwa makini baada ya miaka michache nchi hii itakuwa haina maliasili wala haitakuwa na wanyamapori au watapungua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la tozo. Ukiangalia taarifa ya Kamati yetu ya Bajeti inazungumzia kwamba tozo hizi kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 kwamba hizi tozo zimeondolewa. Mimi nipo kwenye Kamati ya Kilimo na Mifugo, hizi tozo hazijaondolewa na taarifa niliyonayo ni kwamba Waziri wa Biashara anahangaika kutafuta namna gani ya kuziondoa, sasa hizi taarifa zingine zinakuwa hazina uhalisia. Tozo za mazao, tozo ya Bodi ya Pamba, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Korosho kidogo wameangalia, lakini Bodi ya Chai bado na mazao mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri nikikubaliana na mapendekezo ya Kamati hii ya kilimo madam tunakwenda kwenye bajeti tunaomba tozo hizi Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hizi tozo futeni. Waziri Mramba alizifuta hizi sijui kwa nini zinarudishwa. Wale wenye kumbukumbu tozo hizi ziliitwa kodi za kero, kodi za mazao na zikaondolewa, sasa leo kwa nini zishiondolewe? Nafikiri hilo ni jambo muhimu kwa sababu tunajenga na tunakwenda kwenye bajeti ni vema tozo za mazao ya biashara zikaondolewa ili wakulima waweze kuuza mazao yao na hatimaye wapate kipato chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalopenda kuzungumzia ni upatikanaji wa mbegu, Waziri wa Kilimo unajua kwamba nchi hii hatuna mbegu, hata mbegu za mazao ya chakula zinazozalishwa nchini ni asilimia 35 mpaka asilimia 40, mbegu nyingi zinatoka nje ya nchi yetu. Zinatoka Zimbabwe na Kenya. Ushauri wangu kwa Serikali kama tulivyosema kwenye Kamati yetu ya Kilimo haiwezekani tuzungumzie uchumi wa viwanda wakati hatuna hata mbegu za mazao yetu wenyewe ambayo hatimaye ndiyo zitatengeneza hivi viwanda vya agro industries. Sasa suala la mbegu ni la msingi sana na nilikuwa naomba wenzetu wa Serikali mkaliangalie hasa kwa sababu tunajenga upya bajeti yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upatikanaji wa mbolea limezungumzwa. Labda niseme Waheshimiwa Wabunge wananchi wetu wengi wanaishi vijijini na wananchi wetu wengi ni wakulima. Hawa wananchi wetu bado kuna shida ya upatikanaji wa mbolea. Kwa mfano, takwimu za mwaka jana huu mwaka tunaoumaliza sasa, ni kaya 378 tu ambazo zimepata pembejeo nchi nzima ambayo ni sawa sawa na asilimia 0.06 ya wakulima, sasa huu kama siyo mchezo wa kuigiza ni kitu gani? Hatuna mbolea, hakuna mbegu halafu unakuja kuzungumzia uchumi wa viwanda, viwanda vipi hivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda tunavyovifikiria lazima viwe ni viwanda ambavyo vitaajiri watu wetu wengi vijijini na viwanda hivyo ni viwanda vya mazao ya kilimo pamoja na michikichi. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo ni jambo la msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la uzalishaji wa mbegu Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Waziri wa Uwekezaji na Waziri wa Mambo ya Ndani jengeni mkakati wa kuzalisha mbegu kupitia Magereza yetu. Jeshi la Magereza Waziri wa Mambo ya Ndani jana umelisema vizuri tu, nina hakika wenzetu wa Magereza wana mashamba makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mkakati maalum ambao umejengwa kibajeti, nina hakika tunaweza tukazalisha mbegu zetu wenyewe na zikatosheleza. Maeneo kama Magereza, JKT na hata watu binafsi wanaweza wakafanya kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho ni hii food for thought wenzetu wa Serikali mkalitizame. Kwa maoni yangu na maoni ya watu wengi kwenye Kamati yetu ya Kilimo jamani hii Wizara ya Kilimo ni kubwa sana, hii Wizara ina vitu vingi sana. Ushauri wangu kwa Serikali muangalie namna nzuri ya kumshauri bwana mkubwa hii Wizara muundo wake utazamwe upya. Maana yake una mifugo una kilimo, uvuvi, ushirika, masoko na taasisi zaidi ya 60 chini ya Wizara moja.
Kwa hiyo, nilikuwa nashauri sincerely kabisa, wenzetu wa Serikali mkakae mliangalie hili mumshauri bwana mkubwa namna anavyoweza kuhuisha huu muundo ili uweze kuwa na tija kwa sababu Wizara hii kwa kweli ni Wizara mama. Wizara hii ndiyo roho ya Taifa letu kwa sababu ndiyo inaajiri watu wengi na ni tegemeo la maisha ya Watanzania walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni huu Mfuko wa Maji ambao umesemwa sana na kwenye Kamati tulikwenda mbali zaidi tukasema ni vizuri hata hizo fedha zinazotolewa tuwe tunajua ni kiasi gani cha mafuta yameuzwa. Kwa sababu msingi wa Mfuko wa Maji ni hizi fedha zimezungushiwa wigo wake ili zikaondoe tatizo la maji katika maeneo yetu vijijini. Kumekuwa na kuchechemea kidogo kwa Serikali. Tunataka kujua exactly ni kiasi gani ambacho Mfuko wa Maji unapaswa kupata, siyo ku-remit kwenda Wizarani. Mapato halisi ya Mfuko wa Maji lazima yajulikane kwa sababu ni kauli ya Bunge hili, tuli- ring fence zile fedha kwa ajili ya kwenda kuondoa matatizo ya maji katika maeneo yetu ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine nimeyasema jana, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimwa Mwenyekiti ahsante, ningejua kama Mheshimiwa Zitto ana utamu huu ningempa hizo dakika tatu lakini ngoja niendelee. Hilo la mwendelezo ni la msingi sana kwamba amemteua Kamishna na mimi nimesikia kwenye redio wakati nakuja, ni jambo jema kwamba sasa kuna chombo maalum kinashughulikia dawa za kulevya ni jambo jema sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo mawili tu ya kwa haraka. La kwanza, ukurasa wa 35 wa kitabu hiki cha repoti kinazungumzia Sera ya Mambo ya Nchi za Nje kwamba mpaka sasa tunavyozungumza Sera ya Mambo ya Nchi za Nje inayotumika ni sera ya mwaka 2001. Nafikiri wasemeji waliopita akiwemo Mheshimiwa Zitto nimemsikia na Mheshimiwa Bashe akizungumza shida iko hapo. Kwa mujibu wa repoti hiyo ukurasa wa 35 wanasema sera mpya na mapitio ya sera hiyo ya mambo ya nchi za nje inayozingatia diplomasia ya kiuchumi na mapana yake bado haijafanyiwa kazi. Mimi nilikuwa nafikiria Waheshimiwa Wabunge hapo ndipo kwenye shida. Tuiombe Serikali kama ni kalenda ya miezi sita, ya mwaka mmoja basi wenzetu wa Mambo ya Nchi za Nje wawe wametuletea sera hiyo ambayo inafanyiwa mapitio tangu mwaka 2001, haiwezekani sera ifanyiwe mapitio tangu mwaka 2001 mpaka leo. Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala haya ya kuzingatia diplomasia ya uchumi ndiyo masuala ya msingi ya sera mpya ambayo kila siku tunaisema lakini kwa mujibu wa taarifa ya wenzetu wa Kamati na ndugu yangu Mheshimiwa Balozi Adadi mmefanya kazi nzuri sana kuikumbusha Serikali kwamba lazima tuipe time frame. Kama ni miezi sita, kama ni mwaka mmoja watuletee sera hiyo ambayo imefanyiwa mapitio inayozingatia diplomasia ya kiuchumi. Hoja yangu ya pili nimeshangaa kidogo na Waziri wa Ulinzi uko hapa nimeshangaa kidogo. Ukurasa wa 30 wa repoti hii wanasema, hatuna Sera ya Ulinzi, hilo jambo limenishtua Waheshimiwa Wabunge, kama hatuna sera ya ulinzi tumepelekaje askari wetu Congo, Darfur, Lebanon na kwingineko? Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nipate maelezo wakati Mwenyekiti unahitimisha ni kwa nini hakuna sera...
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa muda wako umeisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kabla sijasema mengi, kwanza niunge mkono hoja hii ambayo imeletwa mbele yetu toka Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na machache sana, lakini moja kubwa naomba tu kwa namna ya pekee niwapongeze wenzetu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri na watendaji wake, timu nzima ya Serikali, mmefanya kazi nzuri sana na hasa hii kazi ya kurejesha nidhamu Serikalini,
hongereni sana. Hili ni jambo jema na kila mmoja anaona tofauti iliyokuwepo siku za nyuma na siku za sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niendelee kuwashauri, kama ilivyo kazi yetu Wabunge ni kuwashauri Serikali, kwamba tunaomba utaratibu huu wa nidhamu ya watumishi wa Serikali ujikite katika kulinda misingi ya sheria. Tafadhalini sana, endelezeni nidhamu ya watumishi wa umma, tuwaheshimu watumishi wa umma kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa namna ya pekee naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kumaliza ligi hii ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya ya kuwaweka ndani watumishi wa umma hovyo hovyo. Kwa kweli juhudi zimekuwa nzuri, sasa tunaona mashindano haya hayapo tena, maana huko nyuma ilikuwa Mkuu wa Mkoa akijisikia, Mkuu wa Wilaya akijisikia anaweza kumweka ndani ofisa yeyote wa Serikali bila utaratibu. Tunashukuru sana, jambo hili wenzetu wa Utumishi, TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu mmelisimamia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee, Mheshimiwa Simbachawene najua amefanya vizuri katika jambo hili, na tunakupongeza sana kwa kazi nzuri anayoifanya. Lazima Wakuu wetu wa Wilaya na Mikoa wafuate sheria kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda nilisemee limeainishwa ukurasa wa 31 na 32 wa hotuba ya Waziri Mkuu ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Tunaishukuru sana Serikali kwa jitihada hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe, Mheshimiwa Jenista, reli ya kati tafsiri yake ni reli inayotoka Kigoma kwenda Dar es Salaam ikiwa na matawi ya kutoka Tabora kwenda Mwanza na matawi kutoka Kaliua kwenda Mpanda, ndiyo reli ya kati hiyo. Sasa nimeona kwenye kitabu cha Waziri Mkuu, kuna juhudi kubwa zimefanyika katika ujenzi wa reli ya kati na hususan kuanza kufanya feasibility studies katika matawi haya ya reli ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashauri kwamba ili reli hii iweze kuwa ya kiuchumi, maadamu inaanza kujengwa kwa kiwango cha standard gauge ni vizuri reli hii ikatoka Dar es Salaam ikaenda Kigoma kwa sababu ya mzigo mkubwa, tani milioni nne zilizoko katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo ambayo zinahitaji njia kwenda kwenye masoko ya Kimataifa. Tusipofanya hivyo, tutajikuta mbele ya safari, hii reli haitakuwa na faida za kiuchumi mbali na kusafirisha abiria peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda niliseme ni uwiano wa maendeleo katika Mikoa yetu. Waheshimiwa Mawaziri mlioko hapa nadhani Waziri wa TAMISEMI unanisikia, nchi yetu hii ina mikoa takribani 25.
Uwiano wa Mikoa hii umetofautiana katika sekta mbalimbali, ni vyema sasa Serikali yenyewe kama ambavyo mwaka wa 2016 mlitupa takwimu za hali ya umaskini katika nchi yetu tukawa na utaratibu wa kuiinua mikoa ambayo iko nyuma, mikoa hiyo iko nyuma kwa sababu za kihistoria tu. Mikoa kama Kigoma, Dodoma, Singida, Katavi, iko nyuma kwa sababu za kihistoria. Ni jukumu la Serikali kuweka uwiano sawa wa mikoa hii katika sekta mbalimbali kama elimu, maji, afya, kilimo, barabara na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengine yana nafuu kidogo na maeneo mengine yana shida kubwa sana na wananchi wote hawa ni Watanzania hawa hawa.
Kwa mfano, Mkoa wetu wa Kigoma mpaka leo bado ni mkoa haujaunganishwa na Tabora kikamilifu, haujaunganishwa na Katavi, haujaunganishwa na Geita, haujaunganishwa na Kagera, haujaunganishwa na Shinyanga, hali ni mbaya sana.
Sasa naomba sana TAMISEMI mko hapa, Ofisi ya Waziri Mkuu, angalieni uwiano ambao una afya katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania hawa wana haki sawa. Maeneo mengine yana unafuu na mengine yana shida kubwa. Kwa hiyo, naomba kama ushauri Serikalini kwamba ni muhimu sana kuweka uwiano wa maendeleo katika mikoa ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa niishauri Serikali ni suala la kilimo. Katika nchi yetu kuna maeneo yanapata mvua, Mwenyezi Mungu ameyabariki tu, yanapata mvua za kutosha na tunalo tatizo kubwa sana hata la kuzalisha mbegu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu kwa kweli kwa miaka yote hii, miaka 50 ya uhuru sasa hatuwezei kujitosheleza hata kwa mbegu za mazao ya nafaka. Nilikuwa nafikiri ni wakati muafaka wenzetu wa kilimo na Serikali, yale maeneo yanayopata mvua za kutosha kwa mwaka mzima tuyape kipaumbele ili tuweze kuzalisha mbegu za kutosha ili tujitosheleze kwa mbegu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kwamba mpaka sasa nchi yetu tunazalisha mbegu asilimia 40 ya mbegu zilizobaki zinatoka nchi jirani kama Kenya, Zimbabwe na mataifa mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nizungumzie juu ya umeme wa Malagarasi. Niwapongeze wenzetu wa nishati wamefanya kazi kubwa na taarifa niliyonayo ni kwamba wenzetu wa Benki ya Dunia na African Development Bank wametoa fedha kwa ajili ya kuanza kujenga umeme wa
Malagarasi. Huo umeme ni muhimu sana kwa maendeleo ya watu wa Kigoma na ni dhahiri umeme huo utaingizwa pia kwenye Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa nizungumzie suala la maji, maji ni uhai na ni dhahiri kwamba maeneo yenye vyanzo vya maji vingi na mikoa ambayo ina vyanzo vya maji vingi tu sasa kwa sababu ya matatizo ya tabia ya nchi, uharibifu wa mazingira, naishauri Serikali
kwamba wakati umefika maeneo yenye vyanzo vya maji tuyalinde, kuwe na mkakati wa kitaifa wa kulinda vyanzo vya maji. Kwa mfano, katika Mkoa wa Kigoma, katika Wilaya ya Kasulu peke yake tuna vyanzo vya maji takribani 600 ambavyo havikatiki mwaka mzima. Vyanzo hivi vinapeleka maji yake katika Mto Malagarasi kwa kiwango kikubwa na maji hayo hatimaye yanakwenda kwenye Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu mpango kabambe wa kupeleka maji Malagarasi, Urambo, Kaliua na kwingineko kama hakuna mkakati endelevu wa Serikali nina hakika tutafika mahali maji ya Mto Malagarasi yatakuwa hayatutoshi, hayataweza kuzalisha umeme na kufanya
shughuli za kilimo. Kwa hiyo, nashauri strongly kabisa kwamba wenzetu wa Serikali hata kama ni mwakani tuleteeni a comprehensive plan ya kulinda vyanzo vya maji. Iko mikoa yenye vyanzo vingi, Morogoro wana vyanzo vingi, Katavi wana vyanzo vingi tuwe na mpango mkakati kabisa kitaifa wa kulinda vyanzo vya maji katika maeneo ambayo maji hayakauki mwaka mzima. Ni kweli yako maeneo yenye shida lakini tukiwa na mkakati endelevu nina hakika maji haya hatimaye yatatusaidia sisi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, Mheshimiwa Simbachawene ulitembelea Kigoma, ulitumwa na Mheshimiwa Rais kule Kigoma…
Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.