Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako (12 total)

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kuwa na vijana wengi wanamichezo na wasanii mfano Shaaban Robert, Diamond, Ali Kiba, Banana Zoro, Linex, Mrisho Mpoto na kadhalika:-
(a) Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika Mkoa wa Kigoma kwa kujenga Jumba la Sanaa (Theater Centre) ili vijana wa aina hii wawe na sehemu nzuri ya kuendesha shughuli zao?
(b) Kama Serikali inakubaliana na hoja hiyo, kituo hicho kitaanza kujengwa lini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatambua mchango mkubwa wa wasanii mashuhuri wenye asili ya Mkoa wa Kigoma kama vile Diamond, Ali Kiba, Banana Zoro, Mrisho Mpoto japokuwa nimepata taarifa kwamba huyu Mrisho Mpoto origin yake ni Mkoa wa Ruvuma na wengine ambao wameiletea sifa na kuitambulisha nchi yetu katika fani ya muziki na sanaa.
Mheshimiwa Spika, katika Sera ya Utamaduni ya mwaka 1999, Sura ya 4, kipengele Na.4.1.9 inasema, Serikali itahakikisha kuwa panakuwa na jengo la kisasa la sanaa za maonesho katika ngazi ya Taifa. Aidha, wananchi watahamasishwa kuhakikisha kwamba wanatenga maeneo ya maonesho.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kuhimiza Halmashauri na Manispaa zote nchini kutenga maeneo ya kujenga vivutio vya sanaa. Kuhusu Mkoa wa Kigoma, tunashauri Serikali ya Mkoa kwa kushirikisha Halmashauri zote za Mkoa huo ione umuhimu na namna bora ya kupanga na kutekeleza ujenzi wa Jumba la Sanaa. Aidha, tunatoa wito kwa Halmashauri zote nchini zione umuhimu wa kujenga majengo hayo.
(b) Mheshimiwa Spika, kazi ya kujenga miundombinu katika Halmashauri mbalimbali nchini ni jukumu la Halmashauri husika. Hivyo kila Halmashauri inashauriwa kutenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya Maendeleo ya Sanaa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Mkoa wa Kigoma ni kati ya Mikoa mitatu inayopata mvua nyingi katika nchi yetu kwa wastani na takribani milimita 1,300 kwa mwaka ikifuatiwa na Mkoa wa Katavi.
(a) Je, ni kwanini Serikali haifanyi jitihada ya kuwekeza katika kilimo ili kunufaika na uwepo mzuri wa hali ya hewa?
(b) Je, ni kwanini Mkoa wa Kigoma uliondolewa katika Mikoa na yenye uzalishaji mkubwa na kupata mgao mdogo wa pembejeo?
(c) Je, ni kwanini kituo cha Mbegu cha Bugaga kilichopo Wilaya ya Kasulu kimetekelezwa.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ningependa kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa kwa siku za nyuma Mikoa ya pembezoni ukiwepo Mkoa wa Kigoma imekuwa na changamoto nyingi za kimaendeleo kutokana na kukosekana kwa miundombinu muhimu kwa maendeleo. Serikali imefanya jitihada kubwa kuwezesha uwekezaji katika Mikoa hii ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa miundombinu muhimu kama barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa katika Mkoa wa Kigoma, zinaendelea tafiti mbalimbali za kilimo kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile kampuni ya Kigoma Sugar kwa zao la Miwa, na Belgium Technical Cooperation kwa zao la chai kabla ya kuanza kuhamasisha sekta binafsi kwa uzalishaji mkubwa. Aidha, Mkoa wa Kigoma uko katika mpango wa BRN katika kilimo cha miwa (Sugarcane Cluster) ambapo katika mpango huo, mashamba makubwa mawili yameshatambuliwa na wawekezaji kama vile Kigoma Sugar wameshaonyesha nia ya kuzalisha sukari kwa kushirikiana na wakulima wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kigoma umepewa kipaumbele kwa upande wa ruzuku ya pembejeo ambapo ni kati ya Mikoa mitano iliyopewa ruzuku kubwa ya pembejeo kwa msimu wa 2015/2016 kati ya Mikoa 24 Nchini. Hii ni kutokana na umuhimu wake katika uzalishaji mkubwa wa chakula hasa mahindi hapa Nchini. Idadi ya kaya zilizopata ruzuku ya pembejeo za kilimo katika Mkoa wa Kigoma imeongezeka kutoka kaya 60,239 msimu wa 2013/2014 na kufikia kaya 74,000 msimu wa 2015/2016. Aidha, mgao mdogo wa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima kila Mkoa ikilinganishwa na mahitaji hutokana na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba la kuzalisha mbegu la Bugaga lenye ukubwa wa hekta 336.906 limekaa muda mrefu bila kuzalisha mbegu kutokana na ufinyu wa fedha. Wizara imeweka mkakati wa kulifufua shamba hilo katika msimu wa 2016/2017 ili liweze kuzalisha mbegu kwa wingi kwa ajili ya wakulima wa Kanda ya Magharibi ikiwemo Wilaya ya Kasulu. Aidha, Serikali inahimiza makampuni na vikundi mbalimbali Mkoani Kigoma kushirikiana na ASA katika shughuli za uzalishaji mbegu za mazao mbalimbali ili kuchangia maendeleo ya kilimo katika Mkoa wa Kigoma.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Mji wa Kasulu ni Mji wa siku nyingi sana tangu enzi za Wajerumani lakini hauna mtandao wa maji unaokidhi mahitaji ya wakazi wa mji huo:-
(a) Je, ni lini Serikali itakarabati vyanzo vya maji vilivyopo ili maji yafike katika mitaa ya Kata za Mrusi, Mwilavya na Kidyama?
(b) Je, ni kwanini Serikali haitoi fedha ili kujenga tenki la kusafisha maji kwa sababu maji yaliyopo ni machafu?
(c) Je, ni kwanini Serikali haitoi pesa ili chanzo kingine kilichoainishwa kijengwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, lenye sehemu(a) (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya mtandao wa maji inayoukabili Mji wa Kasulu. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kupanua mfumo wa usambazaji maji katika Mji huo. Fedha hizi zitatumika kwa ajili ya kuboresha hali ya huduma ya maji ikiwemo kuongeza mtandao wa maji Mjini Kasulu ambapo pia Kata za Mrusi, Mwilavya na Kidyama zitapata huduma ya maji safi na salama.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imekamilisha usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi wa maji safi Mjini Kasulu. Usanifu huo pia umehusisha chujio la kutibu maji katika Mji wa Kasulu. Kwa sasa andiko la mradi limewasilishwa Tume ya Mipango kwa ajili ya kuombea ufadhili kutoka Serikali ya India. Gharama za mradi huo ni kiasi cha Dola za Marekani shilingi milioni 9.89.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika kipengele (b) hapo juu, Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi wa mradi huo kupitia ufadhili au mkopo nafuu kutoka Serikali ya India. Fedha hizi zikipatikana, ujenzi wa chanzo kingine utafanyika.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITILE (K.n.y MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO) aliuliza:-
Miji mingi nchini inakabiliwa sana na uhaba wa Maafisa Ardhi na Maafisa Mipango Miji.
(a) Je, ni kwa nini Serikali isianzishe utaratibu wa kuajiri Maafisa hawa moja kwa moja wanapohitimu Vyuo Vikuu?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isichukue jukumu la kununua vifaa vya kupimia ardhi kama vile darubini, GPS na kadhalika na kuvisambaza kwenye Miji yetu ikiwemo Mji wa Kasulu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna upungufu mkubwa wa wataalam katika sekta ya ardhi na tafiti zinaonesha kwamba hadi kufikia Machi, 2016 idadi ya wataalam wa sekta ya ardhi kwa maana ya Maafisa Ardhi, Mipango Miji na Wapima Ardhi, Wathamini na Mafundi Sanifu katika Halmashauri 161 ilikuwa ni 1,087 ukilinganisha na mahitaji ya wataalam 3,040. Idadi hii ni sawa na asilimia 36 ya mahitaji kamili ya watumishi hao. Tafsiri ya mapungufu haya imekuwa ikionekana katika kiwango kidogo cha upangaji, upimaji na umilikishwaji wa ardhi iliyopimwa mijini na vijijini.
(a) Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu wa kuajiri maafisa moja kwa moja wanapohitimu Vyuo Vikuu, Serikali imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo. Mathalani katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2016/2017 Wizara yangu imeomba kibali cha kuajiri watumishi wapya 252 katika sekta ya ardhi. Kama kibali hicho cha kuajiri kitapatikana basi nina uhakika pengo litapungua ingawa ni kwa kiasi kidogo.
Hata hivyo nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuliona hili na nimwahidi kuwa Serikali imechukua wazo lake na pia itaendelea kulifanyia kazi.
(b) Mheshimiwa Spika, kuhusu ununuzi wa vifaa vya upimaji, Wizara yangu tayari imetenga kiasi cha shilingi bilioni nane katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kununua vifaa vya upimaji ambavyo vitasambazwa katika ofisi zetu za Kanda na hata hivyo Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji ndizo zenye dhamana ya kusimamia upimaji wa ardhi kwenye maeneo yao, hivyo zinapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya upimaji. Aidha, katika kukabiliana na upungufu wa vifaa vya upimaji, Wizara imekuwa ikinunua vifaa vya kupimia ardhi na kuvisambaza kwenye Halmashauri kila fedha zinapopatikana.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Katika Mto Malagarasi iko miradi mikubwa mitatu ambayo ni mradi wa kutoa maji Mto Malagarasi kwenda katika vijiji 69 vilivyopo Wilaya ya Urambo, uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji wa miwa na mradi wa uzalishaji wa umeme wa megawati 44.5.
(a) Je, Mto Malagarasi una ujazo gani wakati wa masika na kiangazi?
(b) Je, maji ya mto huo yanatosheleza mahitaji ya miradi hiyo mitatu?
(c) Je, Serikali imefanya utafiti wa kiufundi kujua bajeti ya maji katika mto huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia Mto Malagarasi, ikiwemo mradi wa maji kwa ajili ya Miji ya Urambo na Kaliua, kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji umeme wa megawati 44.5. Wakati wa masika mto huu unakuwa na maji yanayotiririka kwa mita za ujazo 55 kwa sekunde; na wakati wa kiangazi unakuwa na mita za ujazo 40 kwa sekunde.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Kwanza imekamilisha mipango ya pamoja ya uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za maji katika Bonde la Ziwa Tanganyika ambako Mto Malagarasi unapatikana. Hii ni sehemu ya utafiti wa kiufundi wa kujua wingi na ubora wa maji pamoja na mgawanyo sawia wa matumizi ya maji katika Bonde dogo la Mto Malagarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utafiti huo, umeonesha ya kuwa Mto Malagarasi una maji ya kutosha kwa miradi mbalimbali itakayoibuliwa ikiwemo miradi mitatu iliyotajwa na bado yatabaki kuelekea yakitiririka kwenda Ziwa Tanganyika.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO (K.n.y MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO) aliuliza:-
Hivi sasa yapata miaka 11 utafiti wa mafuta na gesi katika mwambao wa Ziwa Tanganyika kwenye maeneo ya Kigoma, Rukwa na Katavi umefanyika au unaendelea kufanyika.
(a) Je, ni nini hali ya utafiti huo?
(b) Bonde la Mto Malagarasi nalo limefanyiwa utafiti
wa mafuta na gesi; je, hali ya utafiti huo ikoje?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodem Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Kabwe Zuberi Zitto, Mbunge wa Kigoma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya Beach Petroleum
ya nchini Australia ilianza kufanya utafiti wa mafuta na gesi Kusini mwa Ziwa Tanzanyika tangu mwaka, 2010. Kampuni hiyo ilifanya utafiti na kukusanya data ambazo kimsingi ziliwezesha kupatikana taarifa za uchunguzi pamoja na utafiti. Kampuni hiyo imeshindwa kuanza kuchimba gesi kwa sababu zifuatazo:-
Kwanza kabisa ni kwa sababu ya kupanda kwa gharama za uwekezaji, lakini pia kupanda na kushuka kwa bei za mafuta duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 10 Oktoba, 2016, Serikali za Tanzania na DRC ziliingia makubaliano ya (MoU) ya kufanya utafiti wa mafuta na gesi pamoja katika Ziwa Tanganyika. Maeneo makubwa ambayo yamekubalika kufanyiwa kazi ni pamoja na kutathmini kwa pamoja data za kijiolojia pamoja na kijiofizikia ili kutambua ukubwa wa mashapo ambayo yatavuka mpaka, vilevile kuandaa jinsi zitakavyofanya kazi kwa ushirikiano. Nchi za Burundi na Zambia nazo zimeomba kuingizwa katika makubaliano hayo ili kufanya utafiti katika ziwa lote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Motherland Industries ya nchini India iliingia ubia na Serikali kupitia TPDC kufanya utafiti wa mafuta na gesi asilia katika eneo la Bonde la Mto Malagarasi mwaka 2012. Kufuatia kushuka kwa bei ya mafuta duniani tangu wakati huo, kampuni imeshindwa kukamilisha majukumu yake ya kazi kama ilivyokubalika kwenye mkataba wa Production Sharing Agreement, kutokana na hatua hiyo, Serikali inakusudia sasa kurudisha eneo hilo kwa ajili ya utangazaji na wawekezaji wengine wapya.
MHE. PETER J. SERUKAMBA (K.n.y. MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO) aliuliza:-
Athari za mazingira ni kubwa na vyanzo vingi vya mito (water sources) vimeathirika sana (mfano Mto Makere):-
Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi na mrefu wa kukabili hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako, napenda nichukue fursa hii ya mwanzo kabisa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kuniteua kwenye Baraza lake. Nishukuru pia Wabunge wenzangu ambao wamenipa ushirikiano na wewe mwenyewe Mwenyekiti ulikuwa mjumbe mwenzangu wa Tume kwenye Utumishi wa Bunge, nakushukuru sana kwa ushirikiano ulionipa. Niwashukuru wananchi wa Mwibara pia kwa kunifanya Mbunge wao na Rais akaniona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwako, Mbunge wa Kasulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji, Serikali ilipitisha Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji wa mwaka 2006. Mkakati huu umeainisha hatua za muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu za kukabiliana na uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji. Aidha, mwaka 2008, Serikali iliandaa Mkakati wa Hatua za Haraka za Kuhifadhi Mazingira ya Bahari, Maziwa, Mabwawa na Mito ili kuhifadhi maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2012, Serikali ilipitisha kwa ajili utekelezaji Mkakati wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Aidha, mwaka 2016, Serikali ilielekeza utekelezaji wa Programu ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na pia Serikali inakusudia kuzuia matumizi ya kuni kwenye taasisi za umma ili zianze kutumia nishati mbadala. Mikakati yote hii inalenga kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mfupi zilizoainishwa na mkakati wa mwaka 2006 ni pamoja na kuwaondoa wafugaji waliovamia mabonde na maeneo ya vyanzo vya maji; kusimamisha shughuli zote za kilimo na kuwaondoa wavamizi kwenye maeneo yaliyoharibika sana; kuzitaka taasisi na watumiaji wengine wakubwa wa miti, kuni na mkaa kuwa na mshamba yao ya miti; kudhibiti shughuli za umwagiliaji usio endelevu na kuzitaka wilaya zote kubainisha vyanzo vya maji na kufanya tathmini ya hali ya mazingira yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zingine ni kudhibiti matukio ya uchomaji moto wa misitu; kupiga marufuku upandaji wa miti isiyofaa katika maeneo ya vyanzo vya maji; kuendeleza Kampeni ya Taifa na Kupanda na Kutunza Miti; Kuendeleza Program ya Kitaifa ya Elimu ya Mazingira kwa Umma; kuwa na programu za hifadhi ya mazingira na mipango shirikishi ya matumizi bora ya ardhi kwa kila wilaya na kutekeleza na kupiga marufuku uchimbaji holela wa madini kwenye vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda wa kati ni pamoja na kujenga na kuendeleza malambo, visima na mabwawa katika maeneo ya wafugaji na wakulima; kuhuisha na kusambaza kwa mpango kabambe wa matumizi ya ardhi ili uanze kutumika mara moja na kuianisha na kuondoa miti isiyofaa kwenye vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mrefu ni pamoja na kuendeleza teknolojia sahihi za kuvuna, kuhifadhi na kusambaza maji ya mvua na ya ardhini, kuharakisha matumizi ya njia mbadala za kuzalisha umeme ili kupunguza gharama za umeme kwa watumiaji na hatimaye kupunguza mahitaji ya kuni na mkaa. Aidha, Serikali imeanzisha Tuzo ya Rais ya Kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Kupanda na Kutunza Miti. Lengo la tuzo hii ni kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuhifadhi mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji. Tuzo hii hutolewa kila baada ya miaka miwili.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA (K.n.y. MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO) aliuliza:-
Ibara ya 89 hadi 101 ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inazitaka nchi wanachama wa Afrika Mashariki kubadilishana uzoefu (exchange of information on technological development and research findings).
(a) Je, ni taarifa zipi kiutafiti ambazo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeshirikiana?
(b) Je, ni taarifa zipi za sekta ya kilimo na mifugo ambazo nchi zimeshirikiana?
(c) Je, ni watumishi wangapi waandamizi kutoka Tanzania ambao wamepata ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzungwanko, Mbunge wa Kasulu, lenye vipengele (a), (b) na (c), naomba kutoa maelezo mafupi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 89 hadi ya 101 ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inazitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika uendelezaji wa sekta ya uchukuzi kwa maana ya barabara, reli, bandari, usafiri wa anga na majini, taratibu za usafirishaji wa shehena, huduma za posta na simu, mawasiliano, hali ya hewa na nishati. Aidha, Ibara ya 103 ya Mkataba huo imeweka misingi ya ushirikiano kwenye sayansi na teknolojia ikiwemo kubadilishana taarifa za utafiti wa kisayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya mafupi, naomba kujibu swali sasa la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsazungwanko, Mbunge wa Kasulu, lenye vipengele (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinashirikiana katika kuandaa taarifa za kitafiti hususani katika hatua za upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya kikanda inayotekelezwa kwa pamoja miongoni mwao kama vile Mpango wa Uendelezaji wa Mtandao wa Barabara na Reli wa Afrika Mashariki.
Aidha, nchi wanachama zinashirikiana kwenye tafiti za kuandaa sera, mikakati, sheria za Jumuiya ili kupata matokeo tarajiwa. Vilevile nchi wanachama zimeanzisha Kamisheni ya Pamoja ijulikanayo kama Kamisheni ya Afrika Mashariki ya Sayansi na Teknolojia ambapo makao yake makuu yapo Jijini Kigali, Rwanda. Uwepo wa Kamisheni hii utaiwezesha nchi wanachama kufanya utafiti kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na hata kunufaika pamoja kutokana na matokeo ya tafiti hizo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 105 ya Mkataba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inazitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana katika sekta ya kilimo na mifugo. Katika eneo hili nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeendelea kushirikiana katika masuala yanayohusu mbegu, madawa ya mimea na mifugo, usalama wa chakula na udhibiti wa magonjwa ya wanyama na mimea.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na muundo wa utumishi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ina nafasi tano za Maafisa Waandamizi Wateule ambapo Tanzania inashikilia nafasi mbili ambazo ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Mipango na Miundombinu na Mwakilishi wa Majeshi. Kwa upande wa nafasi zinazojazwa kupitia ushindani ambazo ni Wakuu wa Taasisi za Jumuiya katika nafasi saba Tanzania ina nafasi mbili ambazo ni Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Utafiti wa Afya na Naibu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi wa Ziwa Victoria. Kwa upande wa nafasi za Wakurugenzi, kati ya nafasi 12 katika Jumuiya Tanzania ina nafasi nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo hayo tuna jumla ya Watanzania nane wanaoshikilia nafasi ya watumishi waandamizi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi zake.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Mahakama ya Wilaya ya Kasulu ni ya zamani sana, ni chakavu sana na wakati mwingine huduma hazitolewi kabisa.
• Je, ni kwa nini Serikali imeitelekeza Wilaya ya Kasulu?
• Je, mahakama hiyo itajengwa lini?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzungwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kasulu ni chakavu. Hata hivyo, mpango wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ilikuwa ni kujenga upya jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kasulu ambapo hadi sasa mkandarasi wa ujenzi huo ameshapatikana na anategemea kuingia makubaliano ya ujenzi huo mwishoni mwa mwezi huu wa Juni, 2017. Hivyo napenda kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Mahakama itaanza utetelezaji wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Kasulu.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Katika nchi yetu suala la usawa na haki kwa wananchi wetu ni jambo linalozingatiwa sana na utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano; taarifa ya hali ya umaskini nchini imebainisha kwamba ipo mikoa minne ambayo kiwango cha umaskini kipo juu sana na mojawapo ya mikoa hiyo ni Kigoma.
Je, ni hatua zipi za makusudi (kibajeti) zinazochukuliwa ili Mkoa wa Kigoma ujinasue na hali ya umaskini ambayo kwa kiasi cha asilimia 80 umesababishwa na madhila ya kihistoria (historical injustices) na Serikali kuacha au kushindwa kujenga miundombinu ya maendeleo kama barabara, vituo vya afya na kadhalika?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 Wizara ya Fedha na Mipango, Idara ya Kuondoa Umaskini kwa kushirikiana na REPOA ilifanya uchambuzi wa kina wa hali ya umaskini kwa lengo la kupata takwimu za hali ya umaskini katika ngazi ya Mikoa na Wilaya (poverty mapping). Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana, Mkoa wa Kigoma ulikuwa na kiwango kikubwa cha watu wanaoishi chini ya mstari wa umaskini cha asilimia 48.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba siyo kweli kwamba Serikali iliacha au kushindwa kujenga miundombinu ya maendeleo kama barabara, vituo vya afya na kadhalika katika Mkoa wa Kigoma na hivyo kusababisha watu wa Kigoma kuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali katika Mkoa wa Kigoma ni pamoja na Daraja la Jakaya Kikwete katika Mto Malagarasi, Kivuko cha MV Malagarasi, barabara ya Kidahwe hadi Uvinza, Kigoma – Kidahwe na Mwandiga – Manyovu. Aidha, miradi ya barabara inayoendelea ni pamoja na Kidahwe – Kasulu, Kibondo – Nyakanazi na Kibondo – Mabamba mpaka mpakani mwa Burundi. Miradi mingine ni kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya kitega uchumi ya NSSF na NHC, miradi ya umeme vijijini na uwanja wa ndege Kigoma awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii yote imelenga kufungua fursa za kiuchumi kwa Mkoa wa Kigoma na hivyo kuongeza kasi ya kupunguza umasikini wa kipato kwa wananchi wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2016/2017 hadi 2020/2021), Serikali imepanga kuendeleza eneo maalum la uwekezaji Kigoma, upanuzi na uboreshaji wa bandari ya Kigoma, ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma, ujenzi wa mradi wa kuzalisha megawati 44.7 za umeme wa maji kutoka mto Malagarasi na kuunganishwa na Gridi ya Taifa ifikapo mwaka 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imepanga kujenga reli ya Kisasa na kuimarisha reli ya zamani na kununua vichwa 63 vya treni na mabehewa ya mizigo 1,960 kwa ajili ya kuimarisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa watu, bidhaa na huduma ifikapo mwaka 2020. Ni matarajio yetu kuwa kukamilika kwa miradi niliyoitaja kutafungua fursa za kiuchumi, kuongeza ajira na kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa katika Mkoa wa Kigoma.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-
Takwimu za Mpango wa Maendeleo 2016/2017 zimeonesha kuwa Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa mitano (5) iliyo maskini zaidi nchini:-
• Je, Serikali inafanya nini kuhakikisha Mikoa hiyo inapata rasilimali fedha na watu ili iweze kuondokana na hali hiyo ya umaskini?
• Je, nini kifanyike kwa Mkoa wa Kigoma ili kujenga ulinganifu katika maendeleo?
• Je, kwa nini Serikali isitenge shilingi bilioni 5 kwa kila mwaka kwa kila Mkoa ili kuondoa kitisho cha Mikoa hiyo kuachwa nyuma kimaendeleo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel N. Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasuli Mjini, lenye vipengele (a), (b), (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali yetu huzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na mwaka mmoja mmoja pamoja na Mwongozo wa Bajeti kugawa rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na changamoto za umaskini. Aidha, mgawanyo wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo huenda sambamba na mgawanyo wa rasilimali watu kwa ajili ya utekelezaji, usimamizi, uperembaji na kutoa huduma kulingana na aina ya miradi.
(b) Mheshimiwa Spika, katika kujenga ulinganifu wa maendeleo katika Mkoa wa Kigoma, Serikali imebainisha maeneo na miradi ya kimkakati kwa ajili ya utekelezaji ili kufungua fursa za kiuchumi. Miongoni mwa maeneo ya kimkakati yaliyobainishwa na kuanza kutekelezwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/ 2017 – 2020/2021 ni Mradi wa Upanuzi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma; Mradi wa Uzalishaji wa Umeme wa Maji katika maporomoko ya Mto Malagarasi MW 44.7; kuanzisha na kuendeleza Eneo la Uwekezaji Kigoma (Special Economic Zone); Mradi wa Gridi ya Kaskazini Magharibi KV400; na ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa.
(c) Mheshimiwa Spika, mgawanyo wa rasilimali fedha huainishwa kwenye Mwongozo wa Bajeti ya Serikali kwa kila mwaka ambao huandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Dira ya Taifa; na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala. Hoja ya kutenga shilingi bilioni 5 kwa kila Mkoa, kila mwaka ni lazima ifungamanishwe na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala. Hivyo basi, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, kwa sasa Serikali haina Sera wala Mwongozo wa kutenga shilingi bilioni 5 kwa kila mwaka, kwa kila Mkoa ili kukabiliana na changamoto za umaskini.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE (K.n.y. MHE. DANIEL NSANZUGWANKO) aliuliza:-
Mkoa wa Kigoma hususan Wilaya za Kasulu na Kibondo zimekuwa makazi ya wakimbizi kwa muda mrefu sana.
Je, ni lini Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNHCR itakuja na mpango kabambe wa kusaidia maeneo yaliyoathiriwa na ujio wa wakimbizi hao (a comprehensive plan and support for refugee affected areas)?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli baadhi ya maeneo ambayo hupokea wakimbizi nchini hupata athari mbalimbali ikiwemo uharibifu wa mazingira. Hata hivyo, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) inatekeleza mipango mbalimbali inayolenga kuboresha huduma kwenye jamii katika Wilaya zinazohifadhi wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya za Kibondo na Kasulu huduma ambazo zimekuwa zikiboreshwa ni pamoja na afya, elimu, kilimo, masoko, ujasiriamali pamoja na hifadhi ya mazingira.