Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako (43 total)

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nipende kumkumbusha kwamba tunasema wasanii na wanamichezo wenye asili ya Kigoma, siyo wakazi wa Kigoma. Mrisho Mpoto mimi nazungumza naye, asili yake ni Kigoma ila amehamia Songea. Hata akina Diamond nao ni watu wa Kigoma lakini wanaishi Dar es Salaam. Nilitaka tuweke rekodi sawasawa maana huwezi kuwa msanii mzuri kama asili yako siyo Kigoma.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, hii Sera ya mwaka 1999 ambayo inatamka dhahiri kwamba hizi Theater Centers zitajengwa Makao Makuu ya nchi, je, Mheshimiwa Waziri huoni kwamba sera hiyo imepitwa na wakati kwamba vijana wengi wako kwenye Majiji, Halmashauri na Manispaa zetu? Ni lini Serikali itaiangalia upya sera hiyo ambayo kusema kweli imepitwa na wakati kabisa hasa Sura ile ya Nne ambayo inasisitiza kwamba hizi Theater Centers zitajengwa katika Makao Makuu ya nchi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, niendelee kushukuru kwamba Mheshimiwa Waziri amekiri Kigoma imetoa mchango mkubwa na kwa kweli wasanii wale wengi wao wanatoka Kigoma, Kibondo na Uvinza. Napenda kujua ni kwa nini basi Wizara isitoe mwongozo technical kwa Wakuu wetu wa Mikoa na Ma-RAS wetu ili wajue kwamba sasa wakati umefika hizi Theater Centers zijengwe katika Halmashauri na Manispaa zetu zote katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Nsanzugwanko kwa jinsi anavyoshirikiana vizuri na wasanii. Vile vile tunathamini mchango mkubwa wa Waheshimiwa Wabunge wote katika kuitetea na kuwa mstari wa mbele kuboresha tasnia ya sanaa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ambalo linasema kwamba sera hii imepitwa na wakati, ni kweli tunakubali kabisa kwamba sera hii kwa namna moja au nyingine imepitwa na wakati. Kwa hiyo, kwa hivi sasa napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu imeshaandaa Rasimu ya Utamaduni na imeshaiwasilisha katika ngazi za juu za maamuzi.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inapongeza sana kazi za wasanii na hasa kwa jinsi wanavyojishughulisha na masuala ya kijamii. Tumekuwa tukiwaona wasanii kama Mrisho Mpoto na wenzake wakijishughulisha na kampeni za kuhamasisha usafi katika Majiji yetu. Kwa sababu hiyo basi tumeona pia kuna umuhimu wa kufanya maandalizi ya Sera ya Sanaa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ambalo linataka Serikali itoe mwongozo kwa mikoa, tunakubaliana nalo kabisa kwamba tutatoa mwongozo huu. Pia napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kupitia Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Wizara inaendelea kutoa wataalam waliokamilika katika fani za sanaa na utamaduni ikiwemo utaalam wa uandaaji wa Majumba ya Sanaa. Hata hivyo, Wizara hii pia ipo katika mazungumzo na TaSUBa ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza kutoa mafunzo nje ya kituo hiki.
Mheshimiwa Spika, napenda nichukue nafasi hii kuziomba Halmashauri zote ziajiri Maafisa Utamaduni. Ahsante.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Pamoja na majibu mazuri yenye matumaini ya Naibu Waziri kwa wananchi wa Mji wa Kasulu, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali langu la kwanza nataka kujua, hilo andiko la mradi kama Naibu Waziri anaweza akakumbuka, ni lini limepelekwa Tume ya Mipango ili tuweze kuwa na comfort kwamba jambo hili linashughulikiwa? Kama atakumbuka!
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, napenda kujua, naona fedha hizi shilingi bilioni 9.89 takriban shilingi bilioni 10 sasa, zinaombwa toka ufadhili wa Serikali ya India. Sasa kwa sababu zinaombwa toka Serikali ya India, napenda kujua kupitia kwako: Je, Serikali ina fallback yoyote endapo Serikali ya India haitatoa fedha hizi? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia masuala ya maji katika Mji wa Kasulu. Ni kwamba andiko hili tulishalipeleka Serikali ya India, kwenye Tume ya Mipango ilishapita, tumeshalipeleka tayari na muda siyo mrefu tunategema kwamba tuta-sign mkataba wa makubaliano ya kutekeleza mradi huu. Kwa hiyo, hali ni nzuri. Kama kutatokea kwamba kutakuwa vinginevyo, Serikali ipo. Serikali ya Awamu ya Tano katika vitu vyote ambavyo tayari tumeshavipanga, tutaweza kutumia fedha za ndani, kuweza kutekeleza mradi wa Kasulu.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii, ninapenda kuuliza swali dogo la nyongeza.
TRA wanafanya kazi nzuri, lakini katika baadhi ya maeneo TRA hawa hawana ofisi; kwa mfano katika Wilaya ya Kasulu, Wilaya kubwa ya kibiashara, Wilaya ya mpakani TRA haina ofisi. Sasa ningependa kujua kupitia kwako je, wenzetu wa Wizara ya Fedha mna sera ipi ya kujenga ofisi za TRA katika maeneo hasa yale ya kibiashara ili mapato ya Serikali yaendelee kuongezeka.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, TRA imekuwa ikifanya uchambuzi wa mwenendo wa biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika Wilaya na Mikoa ya nchi yetu ili kuweza kuamua mahali ambapo panatakiwa patangulie katika kujenga ofisi za Mamlaka ya Mapato, ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Kasulu ambapo tumekuwa na mazungumzo na Mheshimiwa Nsanzugwanko na yeye ametuahidi kwamba atatupatia hata kiwanja. Tumemuahidi kwamba tupo tayari sasa kujenga Ofisi ya TRA katika Mji wa Kasulu. Vivyo hivyo kwa Wilaya nyingine tunaendelea taratibu, tutaanza na zile ambazo gharama zetu za kupata mapato zinakuwa ni ndogo zaidi kulinganisha na mapato. Lakini dhamira yetu ni kuwa na Ofisi ya TRA katika nchi nzima.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWAKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Naomba niulize swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, muuliza swali msingi wake ulikuwa ni udanganyifu mkubwa uliotokea katika Mkoa wa Kigoma hasa katika Mfuko huu wa TASAF, sasa nilikuwa naomba Waziri anipe comfort hapa kwamba je, haoni kwamba kuna haja ya kufanya uhakiki maalum kwa Mkoa wa Kigoma kama ambavyo Mheshimiwa Sabreena alijielekeza kwenye swali lake?
Mheshimiwa Naibu Spika, udanganyifu kwa Mkoa wa Kigoma ulikuwa ni mkubwa sana katika Wilaya ya Kasulu na Kibondo katika Mfuko huu wa TASAF.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ni kweli kwamba msingi wa swali ilikuwa hasa ni kujua udanganyifu uliotekea Kigoma; na tunapojibu swali hapa kwa sababu linagusa karibu programu hii ambayo ni ya Wilaya ambapo tumeanza kwa Tanzania Bara karibu Wilaya 151, ni dhahiri kwamba tungepata maswali mengi na ndiyo maana tumekuja na jibu la jumla kwamba yale yaliyotokea Kigoma yametokea pia na maeneo mengine; na udanganyifu umekuwepo na hatua hizo hizo zitakazochukuliwa Kigoma ndizo zitakazochukuliwa na huko sehemu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa tu ni kwamba kwa utafiti tuliofanya Kigoma ni kwamba kaya ambazo zinaonekana zimefanyiwa udanganyifu ni takribani kaya 1,020 na hizo tumeshaziondoa kwenye orodha na wale watumishi waliofanya udanganyifu huo wanaendelea kuchukuliwa hatua, lakini pia kuna wale wengine ambao ni wa kuchaguliwa maana unavyojua lile zoezi linashirikisha wale Wenyeviti wa Vijiji pale, Mtaa na nini na nini. Sasa unamkuta Mwenyekiti wa Kijiji au Mwenyekiti wa Kitongoji amemweka mke wake au unamkuta mwingine ni mtumishi, ni mwalimu naye yupo kwenye mpango huu. Hao wote tumewaondoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama ni kuchua hatua za kinidhamu dhidi yao pamoja na ile benefit of doubt ya watu kutokufahamu; wengine wamefanya siyo kwa makusudi, lakini kwa wale waliofanya makusudi kusema ukweli hatua zitachukuliwa na kazi hiyo kwa maana ya Mkoa wa Kigoma, tumeifanya vizuri labda tu hapa tuendelee kuchukua hatua ili jambo hili lisijirudie tena. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Tunaendelea. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, swali lake litaulizwa na Mheshimiwa Abdallah Chikota.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya kiufundi yaliyotolewa na Naibu Waziri, nina maswali madogo tu ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ikolojia ya Mto Malagarasi ina athari ya moja kwa moja kwa maji katika Mji wa Kasulu, nilitaka kufahamu ule mradi mkubwa unaofadhiliwa na Serikali ya India kwa takriban shilingi bilioni 9.89, ni lini mradi huo sasa utaanza kutekelezwa katika Mji wa Kasulu ili Kasulu yote na viunga vyake na miji midogo inayozunguka Mji wa Kasulu iweze kupata maji ya uhakika?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka kujua mkandarasi aliyekuwa anashughulikia mradi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika kuyaleta katika Mji wa Kigoma amefilisika, na mmetangaza kwamba sasa anatafutwa mkandarasi mwingine, napenda pia kujua juhudi za kumpata mkandarasi mwingine badala ya huyu aliyefilisika kwa mradi wa Kigoma Mjini zimefikia wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, ahsante.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, majibu.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, suala la miradi kwa ufadhili wa Serikali ya India, hatua tuliyoifikia sasa tunafanya shortlisting kupata mhandisi mshauri atakayefanya usanifu wa kina kuweza kujua ni shughuli zipi zitafanyika katika Mji wa Kasulu, ndiyo fedha ziweze kutoka. Kwa hiyo, tupo kwenye hatua hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusu mkandarasi ambaye ana mradi mkubwa wa maji pale Kigoma Mjini, naomba nisiseme kwamba tunatafuta mkandarasi mwingine kwa sasa, kwa sababu bado hiyo kandarasi haijafutwa.
Kwa hiyo, hayo ni mambo ambayo tunafikiria may be tunaweza tukafanya, lakini tukisema sasa, inaweza ikaathiri utekelezaji wa mradi huu. Serikali itahakikisha kabisa kwamba mkataba uliyokuwepo utakamilisha ili wananchi wetu wa Kigoma waweze kupata maji.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Niongezee kwa hoja ya msingi iliyozungumzwa. Mwekezaji huyo katika Bonde la Malagarasi aliyeko Muhambwe pia yuko mwekezaji mwingine anaitwa Kigoma Sugar yuko Bonde la Malagarasi upande wa Wilaya ya Kasulu. Wote hawa inaonekana wameshindwa na kama sisi Kasulu tunataka ardhi yetu ekari 100,000 tumnyang‟anye sasa tuweze kutafuta mwekezaji mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa naomba basi juhudi hizo za kutafuta mwekezaji zifanyike kote Muhambwe na Wilaya ya Kasulu kwa sababu wote wako kwenye Bonde hilo la Malagarasi. Kwa hiyo, swali langu ni kuomba tu Serikali wawekezaji wote hao wa zamani wameshindwa, hawapo.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme siyo kwa Wilaya ya Muhambwe na Kasulu tu, niseme kwa Wilaya zote na maeneo yote ya uwekezaji na hasa uwekezaji kwa ajili ya kilimo cha miwa pamoja na viwanda vya sukari. Naomba tupatiwe taarifa ili Serikali tuchukue hatua mara moja kama walipewa ardhi basi naamini Waziri wa Ardhi yupo makini tutaichukua ardhi hiyo na kumpa mwekezaji mwingine.
Kwa hiyo, niombe Waheshimiwa Wabunge tupate taarifa ya wawekezaji wote wanaonekana ni wababaishaji na wameshindwa kufanya kazi, tushirikiane na Tanzania ya viwanda inawezekana.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Katika Sekta ya Gesi utafiti wa gesi na mafuta katika Bonde la Ziwa Tanganyika pamoja na Chepechepe na Bonde la Mto Malagarasi, tungependa kujua utafiti huo umefikia wapi?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa majibu mazuri, niongezee lile swali la awali; matumizi ya gesi na mambo ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba sasa hivi Mikocheni na nyumba za TPDC 70 wanatumia gesi, wana mabomba mawili mle ndani; bomba la maji na bomba la gesi. Matumizi yake kwa mwezi hawajavuka sh. 25,000/= hata wakipika vyakula kama maharage, makongoro, ni sh. 25,000. Hiyo tumefanya. Halafu kuna viwanda 37 vinatumia gesi. Hili jana liliongelewa. Tumepata fedha dola milioni 150 kutoka African Development Bank kwa ajili ya kusambaza gesi Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.
Waheshimiwa Wabunge, maana ya uchumi wa gesi ni kwamba hii gesi ni lazima tujenge mabomba mengi. Sasa hivi bomba kubwa la Mtwara – Dar es Salaam liko kwenye asilimia 10 lakini likijaa kabisa gesi, ni mita za ujazo milioni 784 (784 million cubic feet of natural gas) ndiyo inapaswa kupita mle kwa siku. Sasa hivi bado tuko ten percent, lakini ikishafika pale Kinyerezi, ni lazima tujenge mabomba kwenda Morogoro, Dodoma, kila mahali, mpaka Mbeya. Hiyo ndiyo maana ya uchumi wa gesi na ndiyo maana tunasema hii nchi lazima tujenge mabomba mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ya matumizi ni kwamba elimu itakayotolewa Mheshimiwa Mbunge, nadhani siyo muhimu. Gesi ya zamani ndiyo ilikuwa inalipuka, lakini gesi ya kisasa hailipuki. Hii gesi ni CNG (Compressed Natural Gas). Kwa hiyo, ukweli ni kwamba huenda hata elimu haihitajiki, ni kununua unakwenda kutumia tu na ndiyo inaingia kwenye magari. Kwa hiyo, hatuwezi kuweka gesi kwenye gari halafu tena inalipuka. Kituo cha kwanza cha gesi kiko pale Ubungo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye swali lako Mheshimiwa Nsanzugwanko, ni kwamba mkutano wa kwanza, tena nilikuwa sijamweleza Naibu Waziri, naye itabidi aniwakilishe, mzee niwakilishe; kikao cha kwanza kitafanyika Kalemee wiki ijayo cha exploration kwenye Ziwa Tanganyika. Ni kwamba Congo, Tanzania, Burundi na Zambia ni lazima tukae chini; tunajua kwamba kuna gesi na mafuta. Hiyo tunaweza kujua kwa sababu ya ugunduzi kule kaskazini Lake Kivu. Kabla hatujaanza kuzozana, ni afadhali tuanze majadiliano kwamba gesi na mafuta yakipatikana tutakuja kugawana kiasi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, exploration ile tunaifanya pamoja na Mto Malagarasi, tunajua dalili kwamba kuna ama gesi au mafuta, lakini huku gesi tumeshaiona huku Kipili kusini mwa Ziwa Tanganyika huku, ipo. Sasa tunataka kujua ni kiasi gani na ni mafuta kiasi gani.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi nauliza kwa kifupi tu. Barabara hii aliyouliza Mheshimiwa Malocha, mimi na yeye tumekuwa tukiiuliza kila mwaka na huu ni mwaka wetu wa saba hapa Bungeni na ni commitment ya Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Kikwete aliyepita na Rais wa sasa aliyeko madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha kwenye barabara hii, lakini zimekuwa hazitoki na mwaka huu tumeona pamoja na lile daraja. Sasa nataka commitment yake, endapo na mwaka huu stori zitakuwa zilezile za miaka saba iliyopita, ni hatua gani atachukua kama Waziri ili hii barabara ikamilike?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Silinde amekuwa akiuliza mara nyingi na jibu letu muda wote limekuwa hilo hilo, kwamba tutajenga daraja hilo, lakini ameona mwaka huu tumetenga fedha na mwaka ujao na ameshiriki kuzipitisha, nikupongeze pamoja na Wabunge wote. Namuahidi kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano daraja hili litajengwa, lisipojengwa kwa kweli nitamruhusu anikate kichwa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara ya Makambako - Songea imefanana sana na barabara ya Manyovu - Kasulu - Kibondo hadi Kabingo na bahati nzuri barabara hiyo Naibu Waziri ameitembelea. Ni kwa nini sasa barabara hiyo wasiingie kwenye ule mtindo wa kusanifu na kujenga (design and build) wakati usanifu unachukua muda mrefu kufika mpaka Kabingo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara anayoongelea ni karibu unakamilika, kwa hiyo, nadhani kubadilisha mfumo kwa sasa haina sababu sana. Mfumo wa jenga sanifu tunapenda kuutumia lakini tunajua gharama yake ni kubwa kidogo ukilinganisha na tukifanya usanifu wenyewe na baadaye tunatoa tender.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nimuombe tu, tuhakikishe tunakamilisha kazi hii inayokamilika sasa hivi na baada ya hapo tuanze kutenga fedha za kujenga barabara hiyo. Kwa sababu lengo lako ni kuhakikisha barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami na inajengwa haraka iwezekanavyo.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Huu mradi wa umwagiliaji wa Mto Luiche umefanana sana na mradi wa umwagiliaji wa Bonde la Titye na Bonde la Rungwe Mpya. Sasa ningependa kujua, miradi yote hii miwili kwa kweli inasuasua sana, imeshaanza lakini uendelezaji wake wa kujenga mifereji umekwama sana. Nilitaka kujua ni lini sasa Wizara hii itaangalia scheme hizo mbili ambazo zimeshaanza kufanya kazi lakini shida imekuwa ni mifereji ya kupeleka maji kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Nsanzugwanko kuhusiana na miradi miwili kwenye jimbo lake ambayo anadai kwamba ilishaanza kufanyiwa kazi lakini kuna mambo ambayo hayajakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba katika ziara nilizozifanya kwenye maeneo mengi ya umwagiliaji ni kweli kabisa hoja ya Mheshimiwa Nsanzugwanko, kwamba unakuta miradi kwenye vyanzo yale mabanio yameshajengwa, mifereji mikubwa imejengwa lakini midogo ya kusambaza maji kupeleka kwenye mashamba bado. Hata hivyo kuna miradi mingine ambayo imesanifiwa vizuri na imejengwa vyanzo vya maji kutokana na uharibifu wa mazingira vimekauka na ile miradi haifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndio maana sasa Serikali ya Japan imetusaidia fedha na mshauri ameanza kufanya kazi, ili kupitia miradi yote hii tuweze kubaini changamoto na aweze kuainisha zile hekta 1,000,000 tulizoahidi kuzijenga katika hiki kipindi cha miaka mitano. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba timu iliyopo itafika mpaka kwako ili kubaini changamoto gani imefanya hiyo miradi isikamilike, kuna shida gani baada ya hapo tunaweka fedha kuhakikisha tunakamilisha ili wananchi waweze kulima na tuwe na uhakika wa chakula.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Mji wa Mkwajuni hauna tofauti na Mji wa Kasulu. Mji wa Kasulu sisi tuna maji mengi tu, tatizo letu ni maji machafu yanayotoka kwenye bomba. Sasa Mheshimiwa Waziri, ni lini atatujengea treatment plant ili tupate maji masafi kama sera za nchi yetu na Sera za CCM zinavyoagiza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kama anavyosema kwamba Mji wa Kasulu unapata maji ambayo ni machafu, lakini mkakati wa Serikali tumeshatoa maelekezo kwamba kuanzia sasa hatutatoa maji ambayo si salama kwa wananchi. Kwa hiyo, kitu cha kwanza tutaanza na mitambo midogo ya kuweka dawa, lakini jinsi hali ya uchumi inavyoboreka, tutapeleka mitambo ya kuweza kusafisha maji kubadilisha rangi kuwa rangi ya tope yawe maji meupe. Kwa hiyo, huu ndio mkakati wa Serikali katika kuhakikisha wananchi wetu wanapata maji safi na salama na ni meupe, mazuri.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina swali dogo tu, najua kuna juhudi nzuri sana za kufufua Shirika letu la Ndege hili la ATCL, lakini lipo tatizo kubwa la wafanyakazi wasiokuwa na tija. Ndege hizo mbili zinazotarajiwa kununuliwa kuna wafanyakazi zaidi ya 200, ni lini sasa au mna mkakati gani wa kupunguza wafanyakazi wasiokuwa na tija ili hizo ndege mbili zitakazonunuliwa ziwe na manufaa kwa Shirika la ATCL?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli ATCL kuna wafanyakazi takribani 200 na sasa hivi kuna ndege moja, tunalolifanya sasa hivi ni kuhakikisha wafanyakazi wote tunawaajiri upya kuhakikisha tunakuwa na wafanyakazi ambao wanaendana na ndege zilizopo. Hatutaki kuchukua watu ambao wanakaa wanapiga maneno, lakini hakuna kazi ambayo inafanywa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, shida iliyoko huko Njombe inafanana sana na iliyoko huko Kigoma. Mkoa wa Kigoma tuna mkandarasi ambaye ana mgogoro, sasa mgogoro huu umeendelea kati ya REA na Wizara ya Ujenzi. Tungependa kujua kwa Wilaya za Kigoma, Buhigwe, Uvinza na Kasulu, mgogoro kati ya mkandarasi na Wizara unamalizika lini ili mradi wa REA Awamu ya Tatu uweze kuanza? Nakushukuru.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara nyingine tena ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Nsanzugwanko anavyofatilia masuala ya umeme katika Mkoa wa Kigoma kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwa upande wa Mkoa wa Kigoma, Mkandarasi kwa ajili ya kutekeleza mradi wa REA Awamu ya Tatu mchakato umekuwa ukiendelea, lakini nitumie nafasi hii kusema kuwa, kweli wakandarasi walishtakiana, shitaka linaendelea mahakamani na kwa taratibu za Kisheria, jambo linapokuwa mahakamani huwezi kuliingilia kwa sababu ni muhimili mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa taarifa tu kwamba Serikali imeshaanza kuwapelekea umeme wananchi wa Kigoma, wiki iliyopita tulizindua mradi wa utekelezaji wa umeme vijijini katika Wilaya ya Kibondo na tayari mkandarasi ameshawasha Kijiji cha Mabamba. Lakini katika Jimbo la Kakonko pia tumeshazindua, mkandarasi ameshawasha umeme katika Kijiji cha Katale na ataendelea Nyamtukuza. Niwape taarifa wananchi wa Kigoma kwamba mara baada ya taratibu za kimahakama kukamilika vijiji vyote 120 vilivyobaki vitapelekewa umeme.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri mafupi ya Mheshimiwa Waziri Profesa Kabudi. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri kwa kuwa Mahakama hiyo tumeisubiri kwa muda mrefu na umekiri kwamba mkandarasi amepatikana, je mkandarasi huyo anaitwa nani? Na mkandarasi huyo atajenga kwa gharama gani, kwa maana kama amepatikana atakuwa anajulikana na gharama ya ujenzi inajulikana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo la pili; pale pale Kasulu kilomita kama 10 hivi kuna Mahakama ya mwanzo ya Heru Juu, na bahati nzuri mimi kule Heru Juu ndiko ninakozaliwa, Mahakama ile iliangukiwa na mti mwaka 2010 na bahati nzuri Mtendaji Mkuu wa Mahakama alifika pale akaiona. Je, hiyo Mahakama ya mwanzo ya Helujuu ni lini itakarabatiwa, maana haijengwi, inakarabatiwa, ili wananchi waendelee kupata huduma za Mahakama ya Mwanzo katika Mahakama ile? Ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi ambaye atajenga Mahakama ya Wilaya ya Kasulu anaitwa Morad Tanzania Ltd. ambaye pia ndiye amejenga Mahakama ya Kibaha. Gharama ya ujenzi wa mahakama hiyo nitamuomba Mheshimwa Mbunge baadaye nimpe ili ajue ni kiasi gani. Hata hivyo haitazidi gharama ambayo imetumika kwa ile Mahakama ya Kibaha na kama umeona kitabu cha bajeti ya mwaka huu kule nyuma Mahakama ile ya Kibaha umeiona na ndivyo itakavyokuwa Mahakama ya Kasulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mahakama ya Mwanzo ya Heru Juu, kijiji ambacho na mimi nimewahi kufika na nimekipenda sana, napenda nikuarifu kwamba Mahakama ya Mwanzo ya Heru Juu itaanza kujengwa katika mwaka wa 2017/2018.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Nina swali dogo tu la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Ulipaji wa kodi unategemea uwepo wa ofisi za TRA katika maeneo mbalimbali. Nimekuwa nikiuliza zaidi ya mara mbili, sisi Halmashauri ya Mji wa Kasulu tumeshatoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za TRA na tumewapa bure. Swali langu, kwa sababu bajeti imepita kwa kishindo, ni lini ofisi ya TRA itajengwa katika Mji wa Kasulu ili kuhudumia Wilaya nne zilizopo katika Mkoa wa Kigoma za Kakonko, Kibondo, Buhigwe na Uvinza? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza yeye pamoja na Halmashauri yake kwa kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za TRA katika Wilaya ya Kasulu, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niseme Mheshimiwa Waziri wa Fedha alitoa commitment kwamba ofisi hizi zitajengwa na nirudie kusema na niagize ofisi yetu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania wahakikishe ndani ya mwaka huu wa fedha 2017/2018, ofisi hizi zinajengwa katika Wilaya ya Kasulu ili kusogeza karibu huduma hizi kwa wananchi wetu.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Swali hili lina umuhimu wa pekee kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma na napenda nimuulize swali moja dogo Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Bandari za Ujiji na Kibirizi unakwenda sambamba na ujenzi wa Bandari ya Nchi Kavu ya Katosho ambayo tayari Serikali imeshalipa fidia kwa wananchi wale. Napenda kujua, je, ujenzi wa Bandari ya Nchi Kavu ambayo tayari Serikali imeshalipa fidia wananchi wale unaanza lini maana sasa ni takribani mwaka mmoja tangu wananchi wale wamelipwa fidia? Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe shukurani za dhati kwa jinsi anavyojitahidi kupigania bandari za mkoa ambao anatokea. Ni kweli kwamba wakati huu mchakato wa usanifu wa kina na upembuzi yakinifu ukiwa unaendelea tayari Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari imekwishatangaza tenda kwa ajili ya kuanza ukarabati wa gati katika eneo la Kibirizi na Ujiji pamoja na Ofisi ya Meneja wa Mkoa wa TPA ili vyote viende sambamba kwa tenda moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Katosho nalo limeingizwa katika package ya peke yake ya kuanza kujenga sakafu kubwa ili treni inapopita pale kabla ya kufika kituo cha mwisho cha Kigoma iweze kuanza kushusha mizigo ambayo itakuwa inaweza kusafirishwa kwenye nchi jirani na maeneo ya mikoa ya jirani ikiwemo Kigoma. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. DANIEL N. NSWAZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo tu; barabara ya Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi, ni barabara ya muda mrefu sana; na kipande cha Kidahwe – Kasulu kina mkandarasi, lakini mkandarasi huyo amekuwa kazini kwa miaka kumi akijenga kilometa 50. Swali langu kwa Waziri ni kwamba ni kwa nini mkandarasi huyu halipwi madeni yake ili barabara hiyo ikamilike? Kwa nini barabara ya kilometa 50/0 aijenge kwa miaka 10 wakati hana fedha? Barabara hii mkandarasi yupo kwenye site.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kipande cha kutoka Kidahwe kuja mpaka Kasulu kina mkandarasi. Nimhakikishie Mheshimiwa Nsanzugwanko kwamba mkandarasi huyo ameshalipwa malipo yake, lakini sasa hivi kuna mvua nyingi sana zinaendelea pale Mkoani Kigoma, tena mkoa mzima na hivyo kusababisha ucheleweshaji kidogo wa kumalizia. Kuna hatua za awali ambazo zimeshaendelea na yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge anajua, kipande cha kilometa karibu 20 kitawekwa lami mara mvua zitakapopungua. Kwa sababu mambo mengine ni ya kitaalam, huwezi kuweka lami wakati kuna mvua inanyesha kila siku. Mvua za Mkoa wa Kigoma bahati nzuri anazifahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kipande cha kutoka Kibondo mpaka Nyakanazi kupitia Kakonko na kutoka Kasulu, tender itatangazwa hivi punde. Ahsante sana.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina swali dogo kwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ya Morogoro inafanana sana na shida iliyoko Kigoma ambapo Mkoa wa Kigoma tuna mradi wa maji wa Ubelgiji ambao fedha zake zimeshasainiwa. Katika Mji wa Kasulu vijiji vya Nyansha, Nyantale na Kibondo vina shilingi bilioni mbuili katika mradi huo. Hata hivyo tangu fedha zimesainiwa kati ya Waziri wa Fedha na Balozi wa Ubelgiji mpaka sasa hakuna kazi yoyote iliyofanyika.
Mheshimiwa Mwneyekiti, ni kwa nini Wizara haifuatilii mradi huu ambao tayari una fedha zake; lakini bado haujaanza kwa sababu ya urasimu tu? Nilikuwa naomba majibu katika swali hilo.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Nsanzugwanko kuhusiana na shilingi bilioni 18 kutoka Ubelgiji ambazo zimeelekezwa moja kwa moja Kigoma kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kwenye eneo lake la Kasulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi una hatua zake. Hatua ya kwanza, kusaini mkataba wa kifedha, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameshasaini. Hatua ya pili sasa hivi Katibu Tawala wa Mkoa anaendelea na kufanya manunuzi kwa ajili ya kupata wakandarasi. Baada ya kukamilisha hayo manunuzi basi utaratibu wa utekelezaji wa miradi utaanza.
MHE. DANIEL N. NSWANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri barabara ya Kidawe - Kasulu kilometa 63 tumezungumza na wewe na nikakujulisha kwamba mkandarasi hafanyi kazi sasa, anafanya kazi ndogon dogo tu kwa sababu hajalipwa fedha zake, barabara hiyo sasa ni miaka 12 inajengwa, ni kwa nini mkandarasi hapewi fedha zake akamaliza barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge najua tumeongea mara nyingi sana kuhusu barabara za Kigoma, lakini niseme tu kwa wananchi wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla, Serikali imejipanga vizuri sana kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara kwa sababu kipaumbele chetu ni kuunganisha Mikoa yetu ya jirani na nchi za jirani. Kwa hiyo Mheshimiwa Nswanzugwanko unafahamu Kidahwe kwenda Kasulu kilometa 63 yuko mkandarasi pale, lakini kwa sasa kutokana na hali ya hewa kuna kazi ambazo zinafanyika wakati wa kipindi cha mvua, pamoja na kuwa tuna deni na mkandarasi yule upande wa Wizara tunafanya kila juhudi tuweze kuhakikisha kwamba tutapeleka fedha ili mvua zitakapopungua speed iwe kubwa.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa barabara zote ukianzia Nyakanazi kuja Kakonko; kutoka Kankonko kuja Kibondo na kuja kuunganika Kigoma kuna juhudi nzuri na hatua nzuri tumefikia kwa ajili ya kutengeneza mikataba kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ili pamoja na viungo vyake kutoka Kasulu kwenda Manyovu pale border ziko kilometa 58 hivi lakini zipo tena kutoka Kakonko kwenda Mabamba na wewe unafahamu.
Kwa mkoa huu ambao ulikuwa umechelewa kufanya matengenezo ya barabara kiwango cha lami kwamba sasa ziko fedha ambazo harakati zinaendelea, kwa hiyo, Kigoma itafunguka na itaungana na mikoa mingine. Mheshimiwa Nswanzugwanko na wananchi wa Kigoma naomba wavute subira na tutaendelea kukupa feedback kujua hatua nzuri zinazoendelea kule Kigoma. Ahsante.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri ingawa maelezo yenyewe yanajikanganya sana. Msingi wa swali ni hatua za makusudi za kibajeti, kwa sababu Mkoa wa Kigoma kama ilivyo mikoa mingine unapata bajeti kwa mujibu wa ceiling. Sasa nina maswali mawili madogo tu ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo barabara anazozizungumza, zimesimama kujengwa. Zimeanza kujengwa tangu mwaka 2006. Barabara hizo hazijengwi tena na Wizara ya Fedha nyie ndiyo mnatoa fedha. Ni lini sasa kwa makusudi mtatoa fedha ili barabara hizi ziweze kukamilika baada ya kukaa kwa miaka 12 hazijakamilika? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni dhahiri kabisa kukamilika kwa majengo ya NSSF na National Housing hakuwezi kuondoa umaskini wa watu wa Kigoma. Hoja ya msingi ni kwamba tunataka kuwe na special strategy ya mikoa hii minne ambayo iko nyuma, ndiyo hoja ya msingi iko hapo. Majengo haya yapo tu! Kwa hiyo, msingi wa hoja yangu ni kwamba Mheshimiwa Waziri atueleze ni mkakati upi wa kuiondoa mikoa hii minne katika lindi la umasikini kuweka katika mikoa ambayo ni bora zaidi kama ilivyo mikoa mingine? Hiyo ndiyo hoja ya msingi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeonesha dhahiri miradi inayotekelezwa ili kuweza kuwaondoa wananchi wa Kigoma kutoka kwenye lindi la umaskini. Huwezi kuwaondoa wananchi katika lindi la umaskini bila kuwa na miundombinu ambayo nimeionesha. Ndiyo msingi wa jibu langu la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara zilizosimama, Wizara tupo katika majadiliano, tulimaliza uhakiki na sasa tunaelekea kulipa na barabara hizi zitaendelea kujengwa kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anauliza kuhusu special strategy, napenda kuliambia Bunge lako tukufu kwamba special strategy ipo na tumeanza kuitekeleza kwa mikoa yote. Kwa Mkoa wa Kigoma aliouliza, mfano wa special strategy ni upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma ambapo ndege kubwa zilikuwa hazitui na sasa ndege kubwa zinatua, watalii wanafika kwa wakati, wawekezaji wanafika kwa wakati, wafanyabiashara wanafika kwa wakati na tunafungua uchumi wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekamilisha kwa asilimia 100 ujenzi wa magati mawili; Gati la Kagunga limekamilika kwa asilimia 100, Gati la Kibwesa limekamilika kwa asilimia 80. Hii ni kuufanya Mkoa wa Kigoma uwe ni hub ya biashara kwa landlocked countries zinazotutegemea sisi Tanzania ili tuweze kufungua uchumi wa watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Mbunge pamoja na ndugu zangu wote wa Kigoma, Serikali yao ipo makini. Tunaelewa kulikuwa na shida ya bottleneck inflation na sasa tunafungua kwa kukamilisha miradi hii, ndio maana reli yetu ya kuwa kiwango cha kisasa tunakwenda kuikamilisha kufungua mikoa yetu hii. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nami nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugawaji wa maeneo ya utawala ngazi ya kata, tarafa na mitaa yaliyokosewa sana au kusahaulika katika Wilaya ya Kasulu. Unakuta kijiji kimoja chenye wakazi 10,000 ni mtaa mmoja, kijiji chenye wakazi 12,000 ni mtaa mmoja. Nina mifano halisi, kwa mfano wa Kijiji cha Nyantale ni kimoja na mtaa ni huo huo. Je, maeneo yaliyokosewa na kusahaulika ni lini sasa TAMISEMI wanakwenda kurekebisha kasoro hizo kwa sababu hazihitaji miundombinu wala uwekezaji wowote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba kuna baadhi ya maeneo wakati wa kutenga maeneo hayo yaliyokosewa, vigezo havikuangaliwa vizuri. Kwa sasa hivi kulingana na payroll iliyopo Serikalini ambayo bado tunaendelea kuirekebisha itakuwa vigumu sana ndani ya miaka hii miwili kumuahidi kwamba tutarekebisha mwaka ujao au mwaka 2020. Naomba sana wananchi katika maeneo hayo waweze kuwa na uvumilivu, kwa nchi nzima zoezi hilo litafanyika baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru mimi nina swali dogo la nyongeza. Tarafa ya Herujuu huko Kasulu tunalima Kahawa nyingi na hasa Kata ya Herujuu, Kata ya Muhunga na Kata ya Muganza lakini eneo hilo halina Chama cha Ushirika na Chama cha Ushirika kiko Buhigwe kilometa 45. Ni kwa nini Mheshimiwa Waziri asitoe ruhusa sasa wakulima hawa wakauza kwa watu binafsi?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuwaruhusu kuuza kwa watu binafsi kwa sababu tutakuwa tume-distort mfumo tunaojaribu kuujenga. Tunajaribu kujenga mfumo hapa ambao tukiruhusu hicho anachokisema tutakuwa tumeuvuruga tena wenyewe wakati tunajaribu kutengeneza.
Mheshimiwa Spika, mimi binafsi Jimboni kwangu tunalima kahawa, lakini wale wakulima wa kwangu tumewaunganisha na vyama vingine ambavyo vina uwezo wa kufika sokoni na sisi tunaendelea tu kumshauri Mheshimiwa Nsanzugwanko kufanya namna hiyo. Jambo muhimu hapa ni kuangalia uwezekano wa wao wenyewe kuwa na AMCOS yao; na AMCOS zinaruhusiwa kufikisha Kahawa kwenye soko kule Moshi.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, naomba kwa ruhusa yako kabla sijauliza maswali yangu mawili madogo ya nyongeza, kwanza niwashukuru timu ya kampeni iliyotoka Kakonko, uniruhusu niwapongeze Wabunge wote wa CCM na Upinzani waliokuja Kakonko kwa kampeni. Tunasema tunashukuru sana kwa changamoto mlizotupa na tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Chiza kwa ushindi mnono alioupata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno machache ya utangulizi, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, msingi wa swali langu ni mikoa ile mitano ambayo iko nyuma, ndiyo msingi wa hoja na si suala la Ilani ya Uchaguzi ya CCM, si suala la Mpango wa Miaka Mitano. Hoja ni mikoa mitano iliyoko nyuma ambayo inahitaji kupata special attention, inahitaji equalization ili iweze kulingana na mikoa mingine ndiyo msingi wa swali.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la nyongeza ni kwamba miradi yote aliyoitaja ukiacha ujenzi wa reli ya kati, hiyo miradi haijatekelezwa na mingine ina miaka 20. Hiyo mikoa mitano iliyoko nyuma inahitaji kubebwa, kusaidiwa itoke katika maeneo yale ili iweze kuwa sawa sawa na mikoa mingine. Je, ni nini mkakati wa Serikali kwa mikoa hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza ni kwamba hiki kinachoitwa North-West Grid, ni mradi ambao una urefu wa kilometa 2,500 kutoka Tunduma – Nyakanazi kupitia Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Kasulu – Kibondo mpaka Nyakanazi. Je, mradi huu utakapoanza kutekelezwa kwa nini usiwe na wakandarasi zaidi ya watatu ili uishe kwa haraka ili wananchi tupate umeme katika maeneo haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza amesema msingi wa swali lake ni mikoa mitano maskini, lakini alikwenda specific na kuutaja Mkoa wa Kigoma na ndiyo maana na mimi nilijibu specifically kwa Mkoa wa Kigoma, nini ambacho Serikali yetu inafanya.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba kupitia miradi ya maendeleo kama nilivyoitaja ndiyo fursa a kiuchumi hufunguliwa kwa ajili ya wananchi wetu kwenye mikoa husika. Kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo, mpango wa maendeleo wa mwaka mmoja mmoja, Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ndiko vipaumbele huwekwa kulingana na geographical location ya mikoa yetu na aina ya umaskini. Kwa hiyo, miradi hupangwa kulingana na miongozo hiyo niliyoitaja. Kwa hiyo, naomba tu Mheshimiwa Daniel akubaliane na jibu hili kwamba hatuwezi kupanga bajeti nje ya miongozo na mipango inayotuongoza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ametoa pendekezo, tutakaa kama Serikali na Wizara ya Nishati kuona jinsi gani mradi huu wa North – West Grid utatekelezwa kwa haraka ili kurahisisha maendeleo ambayo tunayataka yafike kwa wananchi wetu.
MHE. DANIEL N. NSWAZUNGWAKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi nina swali dogo la nyongeza kwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Scheme ya Umwagiliaji ya Msambala katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu ni scheme ambayo imetelekezwa, ina chanzo cha uhakika cha maji, lakini haipati fedha. Napenda kujua toka kwenye Wizara, ni kwa nini mradi huu muhimu umetelekezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Nia yetu sisi kama Serikali hatuna haja ya kutelekeza miradi, ila tumeona haja sasa ya kuunda Tume kubaini miradi ambayo itakuwa na tija kwa nchi yetu katika kuhakikisha tunaipelekea fedha ili iweze kuwa na tija kwa wananchi. Ahsante sana.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nami naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kigoma tuko off grid, kuna mradi wetu mkubwa sana wa Malagarasi ambao tuliambiwa ungeanza quarter hii ya kwanza ya financial year hii. Ningependa kujua kutoka kwa Waziri ni lini mradi sasa wa Malagarasi mini-hydro utaanza ili tuanze kuwa na chanzo cha uhakika cha umeme katika Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ameuliza ni lini mradi huu wa Malagarasi utaanza. Kama ambavyo tuliwasilisha kwenye bajeti yetu ya Bunge hili na ikaidhinishwa na Bunge lako tukufu kwamba mradi huu utaanza kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019, lakini jambo kubwa hapa amelizungumzia kwamba Mkoa huu upo off grid, naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu, hivi karibuni Benki ya Dunia imetoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa line inayotoka Iringa – Mbeya - Sumbawanga lakini pia kipande cha Nyakanazi - Kigoma kimepata ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, kwa hiyo, kwa vyovyote vile Mkoa huu tunaanza kuingia kwenye gridi kutokana na miradi hiyo, wananchi wa Kigoma niwathibitishie kwamba kwa kweli Serikali ya Awamu ya Tano inafanyakazi kuhakikisha Mkoa huu unaingia kwenye Gridi ya Taifa. Ahsante. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mji wa Kasulu ni kati ya miji ambayo inasubiri kwa hamu sana fedha za mkopo wa India katika ile miji 17. Hii ni kwa sababu Mji wa Kasulu unakabiliwa na tatizo la maji na hata machache yaliyopo ni machafu, kwa hiyo, kutibu tatizo hilo ni fedha za Mfuko wa India. Sasa niapenda kujua miradi hiyo 17 inaanza lini ikiwa ni pamoja na Mji wa Kasulu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kasulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tuna mradi mkubwa wa India ambapo siyo miji 17 sasa itakuwa miji 25 na mradi huo utagharimu shilingi za Kitanzania trilioni 1.2. Tenda ya kwanza ilitangazwa tarehe 17 Agosti, kwa ajili ya pre- qualification na consultancy na itafunguliwa tarehe 17 Septemba. Kwa Mheshimiwa Mbunge yeyote anayehitaji kujua information za mradi huu anaweza kupata kwenye website ya Benki ya Exim ya India. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma ni mkoa ambao huduma za afya zipo chini sana. Katika mikoa mitano ambayo huduma za afya ziko chini ni pamoja na Mkoa wa Kigoma.
Sasa ningependa kumuuliza Waziri, ni kwa nini Mkoa wa Kigoma haupewi kipaumbele (priority) ikiwa hali ya akina mama na vifo vya watoto ni kubwa sana? Hata ambulance tu kwenye Hospitali ya Wilaya hatuna, naomba commitment ya Wizara.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si kweli kwamba Mkoa wa Kigoma haupewi kipaumbele katika utoaji wa huduma za afya. Hata hivyo ni kweli kwamba Mkoa wa Kigoma ni mmojawapo ya mikoa ambayo yaani viashiria vya afya hasa afya ya mama na mtoto ni mbaya, iko duni. Kwa hiyo, Serikali ina mpango tunaita result based finance (lipa malipo kwa ufanisi). Kwa hiyo Mkoa wa Kigoma ni moja ya mikoa nane ambayo tunaipatia fedha mahsusi kila zahanati, kila kituo cha afya, kila hospitali Kigoma tunaipa fedha kwa ajili ya kuhakikisha akina mama na watoto wajawazito wanapata huduma bora. Tanga haipati, Dodoma haipati na Rukwa haipati. Kwa hiyo, utakavyoona Kigoma tunaipendelea, I mean siyo tunaipendelea tunaipa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumegawa magari ya wagonjwa sita katika Mkoa wa Kigoma, hatukugawa katika mikoa mingine. Kwa hiyo, nachotaka kumuomba Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Nsanzugwanko unafanya kazi nzuri Kasulu endelea kushirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Serikali kwa ujumla katika kuimarisha huduma za afya ikiwemo afya ya mama na mtoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mengine ni masuala ya uelewa/attitude. Ameongea Naibu Waziri, wanawake kuhudhuria kliniki wanajivuta. Kwa nini wanawake wa Kilimanjaro wengi wanahudhuria kliniki na si wanawake wa Kigoma? Kwa hiyo, tumeona tunakuja na kampeni ya kitaifa tunaita Jiongeze Tuwavushe Salama; ataizindua Mama Samia Suluhu Hassan. Tunataka wanawake wa Kigoma wajiongeze kwenda kliniki kabla ya kuanza kulaumu mambo mengine. Wakijiongeza na sisi Serikali tutajiongeza tutawapa 25,000 kila mama anayejifungulia I mean Kituo cha Afya kitalipwa 25,000 kwa kila mama anayejifungulia katika Kituo cha Afya cha Kigoma. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kukushukuru.
(Makofi)
MHE. DANIEL K. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwulize Mheshimkiwa Waziri, Mikoa ya Katavi na Kigoma, REA III haijaanza kwa sababu ya migogoro iliyoko Mahakamani, lakini taarifa tulizonazo ni kwamba ruling imeshatoka. Ni lini sasa mkandarasi ataanza kazi katika Mikoa ya Kigoma na Katavi?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Nzanzugwanko. Ni kweli kabisa Mikoa miwili ya Katavi na Kigoma ilikuwa na migogoro katika Mahakama zetu. Napenda kutoa taarifa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba mgogoro huo kimsingi kwa upande wa Ujiji umetatuliwa, mgogoro uliobaki ni ile kesi ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe taarifa tu kwa upande wa Mkoa wa Kigoma, namshukuru sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ijumaa ametupa mwelekeo na sisi kuanzia Jumatano ijao, mkandarasi tunamkabidhi rasmi mkoa nzima wa Kigoma. Mkandarasi kwa upande wa Katavi tunakamilisha maandalizi ya manunuzi ili mwisho wa mwezi huu naye akabidhiwe. Ufikapo mwezi Julai, utekelezaji wa REA III kwa mikoa miwili ya Katavi na Kigoma utakuwa umeshaanza na tayari kukabidhiwa kwa wananchi.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi narudi kwenye swali la msingi. Ikolojia ya Kigosi Moyowosi inategemea sana uwepo wa Mto Malagarasi. Mto huu uko kwenye kitisho kikubwa cha kukauka kwa sababu mifugo imekuwa ni mingi. (Makofi)
Je, Wizara mnafanya nini kuokoa chepechepe (wetland) ya Mto Malagarasi ambayo imevamiwa na ng’ombe wengi na mpaka leo kuna ng’ombe zaidi ya 100,000 kwenye wetland ya Mto Malagarasi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa swali la Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko. Naomba nimhakikishie tu kwamba katika lile eneo la Mto Malagarasi ni eneo muhimu sana kwa ajili kutoa maji na kusambaza katika maeneo muhimu kama ulivyokuwa umesema wewe mwenyewe. Ni kweli kabisa sasa hivi tunaweka jitihada, limevamiwa lile pori, kuna wanyama wengi, kuna mifugo mingi emeenda katika lile eneo, lakini lile eneo ni mojawapo ya maeneo ambayo yako kwenye Ramsar sites.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hivi sasa tunakuja na mkakati wa kutosha kabisa wa kuweza kuhakikisha kwamba hatua ya kwanza ilikuwa ni kuweka vigingi katika mipaka yetu ile Ramsar site. Bado zoezi halijakamilika, litakapokamilika naamini kabisa tutakuwa tumekuja na ufumbuzi kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili, nitumie fursa hii kabisa kwamba mifugo hairuhusiwi katika maeneo ya hifadhi zozote kwa mujibu wa sheria. Ndiyo maana tukikamata hiyo mifugo, kwa kweli tunaipeleka mahakamani na hatua kali zitachukuliwa kwa watu wa namna hiyo.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutachukua hatua za makusudi za kuhakikisha kwamba mifugo yote katika eneo hilo inaondolewa mara ili kuhakikisha huo mto unaendelea kuwepo na uendelee kutusaidia katika matumizi mbalimbali.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Swali la kwanza la Mheshimiwa Gashaza lilikuwa ni Ngara kuanzishiwa Kanda Maalum ya Kipolisi na Wilaya ya Ngara, Kakonko, Kibondo, Kasulu na Kigoma ni maeneo ambayo yanapakana na nchi nne yaani Burundi, Rwanda, Congo na Zambia kwa upande wa majini Kusini. Ni kwanini Serikali isione umuhimu wa kuanzisha kanda maalum kwa sababu zone ile ndiyo zone inayopitisha silaha ambazo hatimaye zinakuja kutushambulia katikati ya nchi yetu. Ni kwa nini Serikali isione umuhimu wa wilaya hizo tano kuanzishiwa Kanda Maalum ya Kipolisi ili kudhibiti uingizaji wa silaha katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba kuna jitihada kadhaa ambazo tumezichukua za kuimarisha hali ya usalama katika maeneo ya Mkoa wa Kigoma kwa ujumla wake ikiwemo hasa maeneo ya Wilaya ya Ngara. Kutokana na jitihada hizo imepelekea kwamba eneo hilo kwa sasa hivi kukosa vigezo vya kuweza kuanzisha ama umuhimu wa kuanzisha Kanda Maalum. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aridhike kwamba kwa sasa hivi akubaliane na sisi kwamba eneo la Ngara bado halijakidhi vigezo hivyo kutokana na kuimarika kwa hali ya usalama katika maeneo hayo.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, runway ya uwanja wa ndege au uwanja wa ndege wa Kigoma ni uwanja wa kimkakati kiuchumi ukizingatia mali iliyopo katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na majirani zetu. Sasa mgogoro uliokuwepo wafidia kwa wananchi umekwisha, sasa ni lini Serikali na European Investment Bank ambao ndiyo finance wa mradi ule sasa watakaa pamoja ili uwanja wa ndege ule uweze kupanuliwa na kutujengea jumba la wageni na maegesho ya ndege?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Nsanzugwanko na jibu lake ni fupi, mazungumzo kati ya Serikali na European Investment Bank yamekamilika tunachosubiri watuletee no objection ili tusaini mkataba mkandarasi aendelee na kazi.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa hoja ni Serikali ianze mchakato wa kimkataba wa makubaliano, ndiyo msingi wa hoja. Kama kubadilishana wafungwa kunaongozwa na mkataba, ni lini Serikali yetu itaanza mchakato huo kati ya nchi ya DRC na Burundi ambazo zina wafungwa wengi Kasulu na Kigoma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri anataka kuniambia wale wafungwa wa Kongo na Burundi waliopo Kibondo, Kasulu na Kigoma kwa ujumla wanatoka Taifa gani kama siyo wakimbizi toka nchi hizo nilizozisema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daniel Nsanzungwanko, Mbunge wa Kasulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni ushauri ambao tumeuchukuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kweli wale ni wakimbizi lakini kwa maana ya tafsiri ya kisheria wamefanya makosa wamekuwa ni wafungwa. Kwa hiyo, kimsingi kwa tafsiri ya kisheria wale ni wafungwa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nina swali fupi sana la nyongeza kuhusu huu mradi wa Northwest Grid kutoka Mbeya – Tunduma mpaka Nyakanazi. Bunge hili tulishauri kwamba kwa sababu njia ni ndefu, takribani kilometa 2500, tulishauri kwamba angalau mkandarasi awe zaidi ya mmoja ili mmoja aweze kuanzia Kigoma kwenda Nyakanazi wakati mwingine anatoka Tunduma kuja Mpanda mpaka Kigoma. Maadam fedha zimepatikana sasa, je, ushauri huo umezingatiwa? Vinginevyo kitakachotokea ni kwamba itakuwa ni kazi ya muda mrefu kwa sababu njia ni ndefu sana. Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Nsanzugwanko kwa swali hili muhimu sana katika ukanda wa Kusini na hasa Magharibi mwa upande wa Kigoma, Katavi pamoja na Iringa.
Mheshimiwa Spika, kwanza katika mradi huu ni kweli kwamba tumepata fedha kutoka Benki ya Dunia jumla dola milioni 455 ambayo itatekeleza mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa kilovott 400 kutoka Iringa kupita Mbeya hadi Sumbawanga. Taratibu za kuanza mradi katika portion hii zimeshaanza, ujenzi rasmi utaanza mwezi Machi mwakani.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo wanashauri Waheshimiwa Wabunge, na yeye akiwemo, mradi huu ni mrefu sana, una umbali wa kilometa 2872 ambapo tumeugawa katika portion tatu. Kutoka Iringa, Sumbawanga hadi Tunduma ni portion moja ambayo tutaanza mwezi Machi na kuanzia Mei utaanza kuanzia Sumbawanga hadi Mpanda na kutoka Mpanda hadi Nyakanazi.
Mheshimiwa Spika, lakini mbali na mradi huo, tumeona wananchi wa Katavi na Kigoma watachelewa sana kupata umeme wa gridi tumeanza kujenga mradi mwingine wa kutoka Ipole, Sikonge kupeleka kilovott 132 Katavi ili kurahisisha wananchi wa maeneo ya katikati kupata umeme wa grid mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Spika, lakini vile vile mradi mwingine wa nne unaopeleka umeme wa grid katika Mkoa wa Kigoma ni pamoja na ule wa kutoka Tabora kupita Urambo hadi Kaliua umbali wa kilometa 370 nao uaanza kujengwa mwezi Februari mwaka ujao. Kwa hiyo ni matumaini yetu wananchi wa Katavi na Kigoma wataanza kupata umeme wa grid kuanzia mwezi Oktoba mwakani.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina swali dogo la nyongeza; tatizo la Baraza la Ardhi kwa Mkoa wa Kigoma ni tatizo sugu na mashauri mengi ya ardhi katika Mkoa wa Kigoma yapo katika Wilaya ya Kasulu, wameshafanya utafiti wa kuanzisha baraza pale lakini huu ni mwaka na nusu sasa. Je, ni lini wanatuanzishia Baraza la Ardhi Kasulu ili kupunguza matatizo ya ardhi na watu wasiende Kigoma na wengine kutoka Kibondo kwenda Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika mabaraza mapya ambayo yameanzishwa nadhani na Kasulu limo kama kumbukumbu zangu ziko vizuri. Kwa hiyo nasema tutafika tuweze kuona eneo ambalo limeandaliwa kwa ajili ya baraza kwa sababu katika yale yaliyoongezeka nadhani na Kasulu imo. Ahsante.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na maelezo mazuri ya Naibu Waziri, napenda niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, swali langu la (b) linauliza ni kesi ngapi DPP amezuia majalada hayo ya watuhumiwa, ndiyo msingi wa swali. Kwa maoni yangu swali hilo naomba lijibiwe sasa kwa sababu halikujibiwa katika maelezo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Halmashauri ya Mji wa Kasulu tuliibiwa fedha takribani shilingi bilioni 5.9 ingawa baadaye nasikia uhakiki ulibainisha kwamba takribani shilingi bilioni 2 zilikuwa zimeibiwa. Washtakiwa wale walisimamishwa kazi, wakahojiwa na TAKUKURU lakini cha ajabu ni kwamba watuhumiwa hawa hawajafikishwa Mahakamani eti kwa sababu DPP hajatoa kibali. Ni kitu gani hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa kaka yangu Nsanzugwanko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana masuala ya watumishi wa Jimbo lake la Kasulu ambao wanategemewa kutoa huduma kwa wapiga kura wake ambao pia ni wapiga kura wake. Jambo la kwanza, kwenye majibu yangu ya msingi hapa nimesema DPP ni Ofisi inayojitegemea na ipo kwa mujibu wa Katiba. Kwa maana hiyo, siyo kwanza amezuia isipokuwa majalada haya yamechelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, Kasulu siyo kwamba kulikuwa na ubadhirifu wa shilingi bilioni
5.9 bali ni ubadhirifu wa shilingi bilioni 1.6 na kulikuwa na kesi 12. Katika kesi hizo 12 aliyekuwa DT wa Halmashauri hiyo ya Kasulu anahusika kwenye hiyo kesi moja lakini kesi sita zenyewe zilifutwa kwa sababu zilikosa ushahidi na kesi tano zinasuasua kwa sababu kuna mashahidi wengine wanaogopa kutoa vielelezo. Kwa hiyo, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu na kuwaasa Watanzania wote kwamba wawe na kiu ya kutoa ushirikiano na Taasisi yetu ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa sababu rushwa ni adui wa haki. Nakushukuru.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee kidogo maelezo kwa kuelezea mamlaka ya DPP kwa mujibu wa Katiba ambapo ni Ibara ya 59B(2) ambayo inampa Mkurugenzi wa Mashtaka uwezo wa kufungua, kuendesha na kusimamia mashtaka yote nchini. Kwa hiyo, ana mamlaka ya kufungua au kuendesha lakini kama haendeshi anasimamia mashtaka yote yanayohusu makosa ya jinai nchini. Hata Ibara ndogo ya (3) inaeleza vizuri kwamba mamlaka hayo anaweza kuyatekeleza yeye mwenyewe au mtu mwingine kwa maelekezo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la DPP ama anazuia au hazuii ma-file kwenda kwenye mashtaka, Mheshimiwa DPP hazuii bali anatoa kibali au hatoi kibali. Pia hafanyi hivihivi, anachopaswa kufanya DPP kwa sababu yeye siyo Mamlaka ya Uchunguzi bali ni mamlaka ya mashtaka, kwa hiyo ni lazima apime ushahidi ulioletwa kutoka kwenye Mamlaka ya Uchunguzi kama unajitosheleza kuweza kufungua mashtaka. Kama anaona kwamba ushahidi ulioletwa kutoka kwenye mamlaka ya uchunguzi haujitoshelezi kufungua mashtaka hatatoa kibali cha kufungua mashtaka, mpaka pale atakapojiridhisha kwamba ushahidi unajitosheleza. Ahsante.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya kutoka Tabora kwenda Kigoma ambayo inatuunganisha na Tabora bado haijakamilika; na kipande cha kutoka Malagarasi mpaka Uvinza ambacho kilikuwa na Mkandarasi wa Abu Dhabi Fund tumesikia kuna matatizo ya kiufundi: Je, Mheshimiwa Waziri unasema nini juu ya jambo hilo? Vinginevyo barabara hii haitakamilika mpaka tufike mwaka 2020.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nsanzugwanko anafahamu, tumezungumza mara nyingi sana juu ya barabara hizi. Niseme tu kwa ufupi, Chagu – Kazilambwa pamoja na barabara ya Malagarasi – Uvinza zitakamilisha mtandao wa barabara kutoka Tabora kwenda Kigoma tukikamilisha vipande hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutazungumza tu na Mheshimiwa Mbunge tuone kama kuna changamoto, basi tujue nini kinachoendelea. Kwa kifupi tunakwenda kujenga barabara hii.
MHE. DANIEL N. NSANZUKWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya matawi ya reli ya SGR ni kujenga reli kutoka Uvinza – Kasulu - Msongati nchini Burundi. Je, mchakato wa kuanza upembuzi yakinifu umefikia hatua gani?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, niomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Mbunge Nsanzugwanko ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati yangu ya Miundombinu na yeye pia najua anafahamu, kwa hiyo, tutoe muda kidogo, ni dakika chache zimebaki ili nitoe hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano halafu mambo mengine yatafuata, tusiwahishe shughuli, dakika bado ni chache.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWAKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusikiliza majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza lilikuwa ni mahususi kwa Kasulu Mjini ambapo timu ya watalaam wa NEMC na Wizara ya Maji wakiwa tisa walikuja kufanya survey pale mwaka 2018 na wakaandika ripoti nzuri sana, wakati huo alikuwa Waziri Makamba. Hiyo ripoti iko ofisini kwako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ile ripoti ifanyiwe kazi kwa sababu ilikuwa mahususi kwa ajili ya Mji wa Kasulu na Kasulu Vijijini ambako mito zaidi ya 50 ilibainika pale na moja ya chanjo kipo shambani kwangu, nami ndio nakilinda kwa gharama kubwa ili kisiharibike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni la Kitaifa zaidi. Nimekubaliana naye na sasa napenda nipate time line: Je, huo mradi wa urejeshaji wa ikolojia ya Mto Malagalasi unaanza lini kwa maana ya vijiji vya Buhoro, Busunzu, Msambala na Kabanga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu amesema ni mradi wa Kitaifa, napenda kujua time line ya huo mradi wa kurejesha ikolojia ya Mto Malagarasi ambayo imeharibika sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko kwa juhudi zake kubwa za kuhifadhi mazingira na ametupa ushirikiano wa kutosha tangu wataalam wamekuja na leo anaikumbuka ile taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba taarifa hiyo sasa nitakwenda kuisoma vizuri na nitakushirikisha kabla Bunge hili halijaisha, ni hatua gani ambazo tutaanza kuzichukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na swali la pili, kwamba hatua gani mbadala na kwa wakati gani? Naomba pia kabla hatujamaliza shughuli zetu za Bunge leo, pia nitakupa taarifa hizi nikiwa nimeshawasiliana na watalaam kwamba wakati gani tunaweza kuanza kazi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nianze kwa kumpongeza Naibu Waziri huyu kwa kuteuliwa. Nina swali dogo la nyongeza:

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma haujafanyiwa soil profiling na Mkoa wa Kigoma una Chuo chake cha Kilimo cha Mbondo ni kwa nini sasa Serikali na hii tumeshaiomba huko nyuma, kwa nini sasa Chuo cha Mbondo kilichopo Kasulu kisifanywe ni Chuo Dada cha TARI kwa ajili ya profiling ya udongo katika Mkoa wa Kigoma, Mkoa ambao unapata mvua nyingi kuliko Mikoa mingine yote katika nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme kitu kimoja; tumetenga mwaka huu Shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuwekeza katika Chuo hicho kilichoko Kigoma, na specifically Kigoma itakuwa ni moja ya eneo la kimkakati la Wizara ya Kilimo kwa sababu ya Palm na tuna mpango wa UNIDO na FAO ambao tutawekeza fedha nyingi kwa ajili ya uzalishaji wa Palm Oil ili iwe ni solution ya kuondokana na kuagiza mafuta katika nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ombi ulilosema kwamba iwe ni Chuo sehemu ya TARI itakuwa chini ya TARI na itapewa hadhi kama vyuo vingine center za utafiti ambazo ziko chini ya TARI. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona nina swali la nyongeza, shida iliyoko Kalenga inafanana sana na shida iliyoko katika Mkoa wa Kigoma. Barabara ya Uvinza – Malagarasi ni ahadi ya muda mrefu na tumeambiwa huu ni mwaka wanne kwamba kuna fedha za Abu Dhabi Fund.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kujua hizo fedha Abu Dhabi Fund zipo kweli au hazipo ili tujue kwamba barabara hiyo haitajengwa.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, fedha zipo.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nimesikia maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ambayo kwa ujumla wake swali langu la msingi halijajibiwa. Swali langu la msingi naulizia utoshelevu wa mbegu za mahindi na maharage kwa sababu ni mbegu ambao ni chakula. Je, kama nchi tunajitosheleza mbegu za mahindi na maharage kwa asilimia ngapi? Ndiyo msingi wa swali langu. Hii habari ya mtama, ufuta na ngano haikuwa msingi wa swali.

Mheshimiwa Spika, swali la pili nina hakika kuna uhaba mkubwa sana wa uzalishaji wa mbegu. Ni lini Wizara ya Kilimo sasa itakuja na mkakati unaoeleweka wa namna ya kukabiliana na tatizo hili na hasa ukizingatia kwamba Jeshi la Magereza na JKT kuna nguvukazi kubwa ambayo wanaweza kushirikiana na Wizara wakaja na mkakati wa kuondoa tatizo la mbegu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, tunataka majibu siyo maelezo tafadhali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Spika, mahitaji (potential demand) ya nchi ni metric tons 120,000 kwa mwaka. Asilimia 70 ya mahitaji haya ni mbegu za mazao ya nafaka ikiwemo mahindi. Ni ukweli usiopingika kwamba kama nchi tunajitosheleza kwa asilimia 40 tu ya mahitaji yetu ya mbegu ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, huu ndiyo ukweli na ndiyo status kwamba kama nchi tuna uwezo wa kuzalisha asilimia 40 ya tani 120,000 za mbegu ya mazao yote ndani ya nchi, kwa hiyo tuna upungufu wa asilimia 60 katika suala la uzalishaji kama nchi. Sasa hivi Wizara inafanya programu na siku ya Jumapili ya wiki hii taasisi zote zinazohusika na suala la uzalishaji wa mbegu za umma na binafsi tunafanya kikao Morogoro kwa ajili ya kutengeneza master plan ya miaka mitatu ili tuondokane na tatizo la import za mbegu na gap iliyopo katika suala la mbegu katika nchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuhusisha Taasisi za Umma kama JKT, Magereza katika grand plan ya miaka mitatu ya Wizara ya kufanya seed production, research na seed multiplication na soil profiling, JKT na Jeshi la Magereza ni sehemu ya mkakati wetu. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko kwamba kama Wizara tunafahamu upungufu na kama Wizara tumeamua kimkakati uwekezaji wa development partners wote tutaupeleka kwenye seed production, research na seed multiplication kwa kutumia irrigation ili tuondokane na suala la uzalishaji wa mbegu wakati wa msimu wa mvua. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza. Jeshi la Magereza ni kati ya taasisi ambazo zilipewa kazi maalum ya kuzalisha mbegu na hasa mbegu za nafaka. Ni kwa nini hadi sasa Jeshi la Magereza pamoja na JKT hawafanyi kazi hiyo na tatizo la mbegu ni kubwa na Wizara ya Kilimo wamekiri kwamba jambo hili limekuwa ni zito sana kwao. Ni kwa nini Jeshi la Magereza halifanyi kazi hiyo kikamilifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango mkakati wetu wa kujitosheleza na kilimo ambao nimezungumza kwamba tumeuandaa na tunauboresha kwa mwaka huu umegusia maeneo mengi. Nimesema kwamba katika mkakati huo kuna malengo ya kuhakikisha kwamba tuna magereza 10 ya kimkakati ya kilimo ambayo yatakuwa yanazalisha chakula cha kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika kutimiza azma hiyo tunabidi tuliwezeshe Jeshi letu la Magereza kifedha ili liweze kutimiza malengo haya na ndiyo maana tunavyozungumza tayari tuna mazungumzo na Benki ya TIB, na TID kwa ajili ya kuweza kupata fedha kwa ajili ya shughuli hizo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba katika mkakati huo, umeangalia maeneo mengi sio tu katika maeneo ya uzalishaji lakini unapozungumzia uzalishaji pamoja na zana za vitendea kazi, upatikanaji wa matrekta na ongezeko la idadi ya wafungwa katika magereza hayo ya kimkakati lakini pia na maeneo maalum ya kuweza kuhakikisha kwamba tunazalisha mbegu kwa ajili ya uzalishaji. Na hilo tutalianza katika gereza Kitwanga kule Kigoma kwenye Mkoa ambao Mheshimiwa Nsanzugwanko anatoka ili kuweza kwenda sambamba na ile dhana ya Serikali ya kuhakikisha kwamba zao la mchikichi linachukua nafasi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wazo lake ni zuri lakini ni sehemu ya mipango ambayo tunayo na mipango hii ambayo tunadhani kwamba ni muhimu sana na imetiliwa mkazo sana na Serikali hii kwa pamoja tukishirikiana tutafanikiwa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwanza sijui kama wewe kwako kule Kongwa umesalimika. Miji mingi inageuka kuwa Miji holela, kuwa squarter kwa sababu haipimwi, haipangwi na halmashauri nyingi hazina fedha ya kufanyakazi hiyo, ndiyo ulikuwa msingi wangu wa swali sasa nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hii interim plan ya Kasulu ya 2008 mpaka 2018 mwenyewe kwenye jibu lake Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba iliishia njiani haikukamilika na taarifa nilizonazo ni kwamba mpango huu haukukamilika, sasa swali la kwanza; Je, sasa Mheshimiwa Waziri madam wewe mwenyewe uko hapo Je, ni lini sasa mtakuja kukamilisha hiyo Land use planning ya Kasulu ili ikamilike? Maana iliisha tu 2018 haikukamilika 2018.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Miji 18 ambayo Waziri umeitaja Je, katika Miji hiyo ambayo itakuwa katika hiyo program ya kuendeleza na kupanga Miji Je, Mji wa Kasulu umo? Na kama Mji wa Kasulu haumo ni lini utakuwemo kwenye program hiyo? Suala la miji ni suala kubwa sana, kubwa sana vinginevyo Miji itakuwa squarter yote katika nchi yetu. Ahsante sana.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, namshauri Mheshimiwa Nsanzugwanko aongee na Halmashauri ya Kasulu ili waonesha mahitaji ya master plan maana yake ukihitaji unaanza kwenye Kamati ya Mipango Miji na halmashauri yenyewe ya Wilaya inaonesha uhitaji wa kuwa na master plan ya Wilaya yake. Wakishaazimia hivyo, basi waweke bajeti kwenye halmashauri yao ya kufanya master plan ya Mji wao wa Kasulu na Miji yote.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara, wenye Miji yao maana mamlaka ya upangaji kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji ni wenye Wilaya (halmashauri) ambao ni Madiwani. Sisi kama Wizara hatuwezi ku-dectate, hata matumzi ya ardhi wanaosimamia zaidi ni halmashauri yenyewe kwahiyo wakishaazimia kwamba sasa wanafikiri ni wakati muafaka watengeneze master plan basi waazimie vilevile na kuweka bajeti.

Mheshimiwa Spika, tunajua liko tatizo la wataalam wa halmashauri, hatuna wataalam wa kutosha wa Mipango Miji lakini serikali imechukua jitihada ya kutambua weledi na utaalam uliko Nchi hii kwa hiyo tumeanzisha Makapuni chini ya Bodi ya Mipango Miji Makampuni ambayo ya Watanzania wenye weledi na utaalam mkubwa wa kufanya hizi master plan ambayo Halmashauri zinaweza zikawatumia.

Mheshimiwa Spika, lakini halmashauri ambayo haina uwezo huo, Wizara inaweza kusaidia wataalam wa Wizara tulionao wachache kuja kushirikiana na halmashauri ile katika kutoa usimamizi wa utayarishaji wa master plan. Kwa hiyo, nakushauri Mheshimiwa Nsanzugwanko utakapokuwa tayari Manispaa ya Kasulu basi tushirikishe na sisi lakini kama hujui mahali pakuanzia tuzungumze mimi na wewe naweza nikamtuma mtaalam mmoja kule Kasulu akawaeleze wale Madiwani namna master plan inavyoweza kuandaliwa.

Mheshimiwa Spika, lakini katika mipango hii ya hizi master plan 18 zinazoandaliwa naomba Mheshimiwa Nsanzugwanko nimuombe nitamtajia Wilaya zote ambazo ziko kwenye huu mpango wa master plan kwenye bajeti yangu ijumaa na Waheshimiwa Wabunge wote watasoma lakini ijumaa nitawapeni pia nafasi ya kujua pamoja na Miji hii ya Wilaya mnayoijua, lakini viko vijiji vyenu wengine hamvijui vimeshaiva sasa ili kuzuia hizo squatter, vijiji vingine Wilaya imeshaamua kuvitangaza vimeletwa kwangu na nimeshavitangaza na vyenyewe vipangwe kimji ili watu wanaoishi katika vijiji hivyo wapangwe, wapimiwe na wapewe hati kama za Mjini navyo nitawapa jedwali ili Waheshimiwa Wabunge wote mjue vijiji vyenu ambavyo vina hadhi ya kimji ambavyo tumeshavitangaza Tanzania nitawapeni ijumaa nakushukuru. (Makofi)