Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima (5 total)

MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-
Gereza la Ilagala limehodhi eneo kubwa la shamba na kufanya wananchi wa Kata ya Ilagala kukosa maeneo ya kulima.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa sehemu ya eneo kwa ajili ya wananchi wa Ilagala ili na wao waweze kupata maeneo ya kulima?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Gereza la Ilagala ni gereza la kilimo na mifugo ambapo linamiliki jumla ya ekari 10,760 na kati ya ekari hizo, ekari 4,500 ziko katika milima na mabonde ambapo zimehifadhiwa kwani ni vyanzo vya mito katika eneo hilo. Ekari 3,000 zimetengwa na zinatumika kwa ajili ya ufugaji wa ng‟ombe, mbuzi na kondoo; na ekari 5,000 kwa ajili ya makazi na ekari 2,760 ni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya mahindi; mahindi ya mbegu, michikichi, mihogo, mbaazi, mboga pamoja na matunda. Hata hivyo, pamoja na shughuli tajwa hapo juu, eneo hilo bado halitoshelezi kwa ajili ya mahitaji yaliyokusudiwa.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-

Tarafa ya Nguruka na Uvinza zinalima zao la tumbaku na kuiingizia Halmashauri ya Uvinza fedha nyingi kwenye makusanyo ya ndani lakini wamekuwa wakinyonywa kwenye bei ya uuzaji na upangaji wa viwango vya pamoja vya soko:-
Je, ni lini Serikali itawatumbua wakulima wa tumbaku wa Uvinza ili nao wapate chama kikuu ndani ya Mkoa wa Kigoma na kuwapunguzia gharama za usafirishaji kwenda hadi Tabora?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa wakulima wa tumbaku kuendelea kunufaika na huduma zitolewazo kupitia vyama vya ushirika. Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 na Kanuni za mwaka 2015 ili chama cha ushirika kiweze kusajiliwa kinapaswa, pamoja na kutimiza masharti mengine, kikidhi kigezo cha kuwa na uhai wa kiuchumi katika maana ya economic viability.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa chama kikuu kuanzishwa, uhai wa kiuchumi unazingatia viwango vya uzalishaji kwa mwaka wa vyama vya msingi vinavyohudumiwa na chama kikuu hicho na ufanisi wa mfumo wake wa masoko. Kwa mujibu wa matakwa hayo ya kisheria ili chama kikuu cha ushirika wa tumbaku kiweze kusajiliwa kinapaswa kiwe kinazalisha na kuuza angalau kilogramu milioni kumi za tumbaku kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa katika Mkoa wa Kigoma kipo chama kikuu kiitwacho Kigoma Tobacco Growers Cooperative Union (KITCU). Chama kikuu hicho kinahudumia Wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu na Uvinza. Takwimu zinaonesha kuwa kutokana na wanunuzi wa tumbaku kupunguza mahitaji ya tumbaku kwa mwaka, uzalishaji wa chama kikuu hicho umepungua hadi kufikia wastani wa kilogramu milioni nane kwa mwaka. Wilaya ya Uvinza ambayo inajumuisha Tarafa za Nguruka na Uvinza inazalisha takriban 55% ya tumbaku yote ya KITCU, ambazo ni takriban kilogramu milioni 4.5. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wilaya hiyo imezalisha kilogramu 3,586,175 za tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na taarifa hiyo na umuhimu wa kuzingatia Sheria ya Ushirika katika kuanzisha vyama vya ushirika, kwa sasa chama kikuu kingine cha ushirika kinachojishughulisha na zao la tumbaku katika Mkoa wa Kigoma hakiwezi kuanzishwa. Badala yake Serikali inajielekeza katika kuimarisha nguvu za uzalishaji za KITCU, chama ambacho makao yake makuu yako Nguruka katika Wilaya ya Uvinza ili kiweze kukidhi vigezo vya kiuchumi na kisheria na hivyo kuendelea kuwahudumia wanachama wake kwa ufanisi zaidi, wakiwemo wananchi wa Wilaya ya Uvinza.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-
(a) Je, Serikali inawaeleza nini wafanyakazi wa Kiwanda cha Chumvi ambao walistaafishwa bila malipo ya kiinua mgongo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwabana wamiliki wa kiwanda hicho ili waboreshe mazingira ya kiwanda pamoja na mazingira ya wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wafanyakazi wa Kiwanda cha Chumvi ambao walistaafishwa bila malipo ya kiinua mgongo lilishashughulikiwa, ambapo wafanyakazi husika walilipwa mafao yao kwa mujibu wa sheria ikiwemo kiinua mgongo. Aidha, kwa kuzingatia Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2016 yaliyopitishwa na Bunge lako Tukufu wakati wa Kikao cha Bajeti, kama kuna mfanyakazi au wafanyakazi wanaoona kuwa hawakulipwa stahiki zao za kupunguzwa kazi ipasavyo, wanayo fursa ya kuwasilisha moja kwa moja madai yao kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi pasipo kupitishia kwa Kamishna wa Kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kuimarisha mikakati na huduma za usimamizi na ukaguzi kazi kwa kuchukua hatua stahiki kwa waajiri wanokiuka sheria ili kuboresha mazingira ya kiwanda na mazingira ya wafanyakazi. Aidha, kupitia Marekebisho ya Sheria za Kazi ya mwaka 2016, Maafisa Kazi wamepewa mamlaka ya kuwatoza faini za papo kwa papo waajiri wanaokiuka sheria. Kanuni kwa sasa zinaandaliwa ili kuweka mwongozo na utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nivisihi vyama vya wafanyakazi nchini, navyo vitimize wajibu wao wa kutetea na kusimamia haki za wafanyakazi pamoja na kukuza tija na uzalishaji sehemu za kazi.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA (K.n.y MHE. HASNA S. K. MWILIMA) aliuliza:-
Shughuli kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika ni uvuvi lakini nyavu zimekuwa zikikamatwa na kuchomwa moto.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia wavuvi hao nyenzo au vifaa vya kisasa vya uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi ili kuwawezesha wavuvi wakiwemo wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika kufanya uvuvi endelevu na wenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeondoa kodi kwenye zana na malighafi za uvuvi zikiwemo engine za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio kupitia Sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2007. Aidha, kupitia Umoja wa Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (The East African Community Common External Tariff) engine za uvuvi na malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake kwa maana ya fishing gear accessories 10% na outboard engine 0%) zimepewa punguzo la kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo inatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wananchi wakiwemo wavuvi ili waweze kununua zana bora za uvuvi. Hivyo wavuvi wahamasishwe kujiunga katika Vyama vya Ushirika ili kuwawezesha kupata mikopo hiyo.
Vilevile Serikali inatekeleza mpango wa kutoa ruzuku ya zana za uvuvi, ambapo wavuvi wenyewe huchangia 60% na 40% iliyobaki ya gharama huchangiawa na Serikali. Hadi sasa engine 73 zimenunuliwa kupitia mpango huu, nakati ya hizo engine 49 zimelipiwa na kuchukuliwa na vikundi vya wavuvi vilivyokidhi vigezo vikiwemo vitatu kutoka katika Wilaya ya Kalambo na kimoja kutoka katika Wilaya ya Sumbawanga.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE (K.n.y. MHE. HASNA S. K. MWILIMA) aliuliza:-
Kituo cha Afya cha Nguruka kinahudumia Wakazi wa Kata Nne za Tarafa ya Nguruka pamoja na wananchi wa Usinge katika Wilaya ya Kaliua.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi kituo hicho kwa kuongeza miundombinu na kumalizia ukarabati wa jengo la Mama na Mtoto ambalo limeachwa bila kukarabatiwa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Nguruka kinahudumia watu wapatao 108,330 wa Kata nne za Tarafa ya Nguruka na majirani Wakazi wa Tarafa Usinge Wilaya ya Kaliua, Mkoani Tabora kama kituo cha rufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona haja ya kukiboresha Kituo cha Afya cha Nguruka ili kiweze kutoa huduma bora kwa wananchi ikizingatiwa kwamba Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Magufuli alitoa ahadi ya kukiboresha kituo hicho alipokuwa katika kampeni za uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha azma hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imetenga shilingi milioni
• katika mwaka wa fedha 2017/2018 ili kuongeza miundombinu ikiwemo wodi ya akinamama wajawazito na watoto, ujenzi wa uzio, ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti, mfumo wa maji taka na ukarabati wa nyumba ya watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuimarisha na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha huduma za afya hapa nchini.