Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima (5 total)

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naomba pia niulize swali; kwa kuwa Jimbo la Kigoma Kusini kwenye Ukanda wa Ziwa Tanganyika tunatumia meli ya Liemba, lakini kwa bahati mbaya gati karibu tano kwa muda mrefu sasa hazijajengwa na wala hazijakamilika.
Swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri; je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuwapunguzia adha wananchi wanaotumia meli ya Liemba kwa kujenga Gati ya Kirando, Mgambo, Sibwesa na Gati ya Kalia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, hizi gati anazoziongelea katika mwambao wa Ziwa Tanganyika ni gati muhimu sana kwa sababu tuna vilevile tatizo la barabara. Kwa hiyo, usafiri wa ile meli ni muhimu sana kabla hatujafungua usafiri wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulishawaagiza Tanzania Ports Authority kwamba katika mwaka huu wa fedha lazima ahadi ambazo viongozi wetu walizitoa kuanzia Serikali ya Awamu Nne na hii Serikali ya Awamu ya Tano, ni lazima tulitekeleze katika eneo hili kwa sababu mateso yaliyoko katika eneo hilo kwa kweli ni makubwa.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia mwaka huu wa fedha na katika miaka hii mitano ikikamilika ahadi zile tutakuwa tumezikamilisha, ikiwa ni pamoja na kuimarisha gati ya Kirado, Simbwesa na hizo zingine ambazo Mheshimiwa Mbungu amezitaja.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini nitake tu kumhakikishia kuwa eneo hilo la ekari 10,760 na hizo ekari 5,760 ambazo yeye amezitolea majibu kwamba zinatumika kwa ajili ya mifugo na kilimo, nimhakikishie tu kwamba eneo kubwa halijaendelezwa kwa miaka mingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna zadi ya ekari 4,500 hazijaendelezwa kwenye kitu chochote. Gereza hawajalima wala hawana mifugo. Wananchi wa vijiji vitatu, kijiji cha Kabeba, Ilagala na Sambala hawana maeneo ya kulima na historia inaonesha walichukua zaidi ya ekari 4,000 bila makubaliano na vijiji hivi vitatu.
Swali langu je, ni kwanini Mheshimiwa Waziri asielekeze gereza litoe angalau ekari 1,500 ili na hawa wananchi wa Jijiji vitatu wapate maeneo ya kulima? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kumekuwa na tabia ya baadhi ya Maafisa Magereza kuwakamata wananchi wa vijiji hivi vitatu kuwapiga, kuwanyang‟anya zana zao za kilimo, lakini pia kuwafungulia kesi na kuwapeleka mahakamani. Je, Mheshimiwa Waziri, kama Serikali anatoa tamko gani kwa wananchi wa vijiji hivyo vitatu ambao wamekuwa harassed na Maafisa wa Gereza la Ilagala? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Hasna Mwilima kwa jinsi anavyofuatilia mambo ambayo wananchi wake wamemtuma na kwa kweli yeye ni Mbunge makini, hata juzi nilipita kule wakasema hata uchaguzi ungefanyika leo, angeshinda kwa kiwango kikubwa kuliko kilichopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwenye suala hili alilolisemea, ni kweli kuna ekari ambazo hazijaendelezwa, lakini kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, zile zilizoachwa ni zile ambazo zimewekwa kwa sababu ziko kwenye chanzo cha maji ambayo yanatumika siyo tu kwa gereza, yanatumika hata kwa wananchi wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu wa malengo mapana ya taasisi zetu hizi za magereza ni hasara kuwa na wafungwa wanaolishwa kwa kodi za walipakodi halafu wakawa hawana kazi ya kufanya. Kwa hiyo, hicho tunachosema hata eneo lile lililopo halijatosheleza tunamaanisha malengo marefu ya kuweza kuwatumia wafungwa wanaoweza kufanya kazi ikiwa ni sehemu ya kuwarekebisha ili magereza yetu yaweze kujiendesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu tamko la Serikali kwa wale wananchi ambao wananyang‟anywa vifaa; moja niseme Serikali ya Wilaya ambako ndiko na Jimbo lilipo ni vizuri wakapanga matumizi bora ya ardhi na wanaweza hata wakawasiliana na Wizara ya Ardhi ili kuwatafutia wananchi maeneo mbadala ya kufanya kazi hizo ili wasiingie bila ruhusa katika maeneo ya Magereza na hivyo kusababisha mgongano huu ambao unasababisha wao kukamatwa. Lakini maeneo yote ambayo yana Magereza, tunaendelea kuhimiza mahusiano bora kati ya Taasisi hizo za Serikali pamoja na wananchi wanaozunguka maeneo husika.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, tarehe 16 Desemba 2016, wadau wote wa zao la tumbaku walikuwa na mkutano Morogoro na mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Dkt. Tizeba. Katika mkutano huo vyama vililalamika kuhusiana na kuwa na madeni ya muda mrefu yanayowasababishia kukosa mikopo ya pembejeo kwenye mabenki. Mheshimiwa Waziri alitoa tamko kwenye mkutano huo hapo Morogoro kwamba mabenki sasa wachukue yale madeni ya muda mrefu badala ya kuvibebesha mizigo vyama vya msingi yapelekwe moja kwa moja kwa mwanachama au mkulima mmoja mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kwa msimu huu, mabenki hayajatekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri kutaka madeni yale yaelekezwe kwa mtu mmoja mmoja badala ya vyama. Je, nini kauli ya Serikali kwa wakulima wa vyama vya msingi kwenye zao hili la tumbaku waliokosa mkopo wa pembejeo kwenye msimu huu wa 2016? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kilimo cha tumbaku kinahitaji utunzaji wa mazingira na kwa mujibu wa kanuni ya zao hili kila mkulima anatakiwa kwenye hekta moja anayopanda tumbaku apande miti 150 na miti 200 apande kwenye mashamba yanayomilikiwa na vyama vya msingi. Kwenye Halmashauri yetu ya Uvinza vyama vya msingi tulivyonavyo vinahitaji jumla ya hekta 240 sawa na hekari 600. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvisaidia vyama vya msingi vya zao la tumbaku kupata maeneo ya kupanda miti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama alivyoeleza kwamba mwaka jana Mheshimiwa Waziri alitoa kauli ya kuelekeza namna bora ya kulipa madeni ya muda mrefu yanayovikabili vyama vya msingi na alielekeza kwamba ufanyike utaratibu ili madeni yale yaweze vilevile kulipwa na wale wanaodaiwa moja kwa moja badala ya kuleta mzigo kwenye chama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado huu ndiyo msimamo wa Serikali. Serikali itaendelea kufuatilia kwamba kwa nini hili halijatokea kama ilivyotakiwa kwa sababu tunaamini kuendelea kuvibebesha vyama vya msingi mzigo ndiyo chanzo cha vyama hivyo kuporomoka na hatimaye zao la tumbaku kuanguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utunzaji wa mazingira, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge ana uelewa mzuri sana kuhusu namna zao la tumbaku linavyotakiwa kuendeshwa kwamba ili uweze kuzalisha tumbaku ambayo ina vigezo vya kimataifa lazima iwe environmentally compliant (ikidhi vigezo vya mazingira) na ndiyo maana kuna hitaji la kupanda miti. Nitaongea na Mheshimiwa Mbunge ili niangalie namna ya kuongea na Halmashauri za Mkoa wake kuhusu namna ya kupata ardhi kwa ajili ya kupanda miti hiyo ambayo inatakiwa kwa ajili ya zao la tumbaku.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nina masikitiko makubwa sana, itabidi Naibu Waziri anipe uhakika wa hao wafanyakazi 389 walilipwa lini na wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapoongea hivi nina ushahidi, suala hili hata Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali analifahamu. Lilifanyiwa uhakiki, watu walitumwa kutoka Hazina wakaja Uvinza wakafanya uhakiki, wakaona kweli wafanyakazi hawa wana haki hawakulipwa mshahara wao wa mwisho na hawakulipwa nauli.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumefanyiwa uhakiki Mwanasheria Mkuu wa Serikali analifahamu bahati mbaya leo hayupo hapa, lakini analifahamu, alihakikisha na akatoa ushauri kwamba hawa wafanyakazi walipwe, wanadai zaidi ya shilingi milioni 320.9; je, Waziri yupo tayari kuniletea ushahidi kwamba walilipwa lini na nani, kwa sababu ninavyofahamu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha anayo haya madai juu ya meza yake?
Swali langu la pili, Kiwanda cha Chumvi hivi tunavyoongea wamiliki wameuza kila kitu, wameuza vifaa vyote, wameuza vyuma, wameuza magari, wameuza matofali, kila kitu. Tunajua kabisa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuimarisha viwanda, vilivyopo na kufufua vingine na kuhamasisha vingine ili viweze kujengwa. Swali langu ni kwa nini, kama dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuendeleza viwanda, leo tunaachia kiwanda kama kile cha chumvi ambacho wananchi wa Uvinza akina mama.....
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu kwa nini wanaachia wamiliki wanaoendesha kiwanda hiki kufunga kiwanda kinyume na utaratibu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kuhusu kuleta orodha, jambo ambalo linaweza kufanyika hapa ambalo ni rahisi la kuweza kuwasaidia wafanyakazi wetu, katika majibu yangu ya msingi nilisema kama wako wale ambao wanahisi kwamba madai yao hayakulipwa ipasavyo na bado wana malalamiko, mimi na Mheshimiwa Mbunge tunaweza kuchukua hizi taarifa zote mbili tukazioanisha ili tupate muafaka wa kuweza kuwasaidia wafanyakazi hawa wa Kiwanda cha Chumvi.
Kwa hiyo, nimuondoe hofu tu Dada yangu Mheshimiwa Mwilima kwamba nalichukua jambo lako kwa uzito mkubwa sana, na kwa namna alivyozungumza kwa masikitiko makubwa, na mimi niungane nae kwamba tutakwenda pamoja wote kuangalia arodha hii ili kama bado kuna mapungufu tutafanya kazi ya kushughulikia pamoja na taasisi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili kuhusu kufunga viwanda na wakati tunasema nchi yetu ni ya uchumi na viwanda. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hata hili nalo pia linahitaji kuweza kufahamu hasa changamoto ambazo zimepelekea jambo hili kutokea, lakini nimuahidi tu kwamba chini ya Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tunashughulikia masuala ya kazi na ajira na mategemeo yetu na matazamio yetu makubwa ni kuona kwamba viwanda vingi vinakuwepo, uwepo wa viwanda ndipo ajira zinatengenezwa.
Mheshimiwa Mbunge hata katika taarifa ya ILO ya mwaka 2014 ya The Global Employment Trend inasema ya kwamba ili kuendelea kuongeza nafasi za ajira hasa kwa vijana ni vema tuwe na viwanda vingi zaidi. Ninakachokisema hapa ni kwamba, nakwenda kufuatilia kufahamu changamoto na tatizo ambalo limepelekea kiwanda hiki kufungwa ili tuweze kupata suluhisho la kudumu, vijana wa Kigoma waweze kupata ajira.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Posho ya Wenyeviti wa Serikali za Vijiji kwenye Halmashauri zingine hawalipwi kabisa. Sasa nataka niulize tu swali kwa nini Wizara ya TAMISEMI isitoe Waraka Maalum kwenda chini kwa Wakurugenzi wote kuwaelekeza kwamba katika own source za Halmashauri wawe wanatoa kiasi fulani kwa ajili ya Wenyeviti wa Vijiji huku tukijua hao ndiyo wanaotusaidia kufanya kazi kubwa za maendeleo kwa niaba ya Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) : Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, huo Waraka ambao Mheshimiwa Mbunge anaupendekeza ulitolewa mwaka 2003, lakini kwa sababu umekuwa ni wa muda mrefu pengine labda baadhi ya wenzetu wanaanza kuusahau, basi tutachukua ushauri wake ili tutoe maelekezo tena.
Mheshimiwa Spika, msisitizo ni kwamba lazima Halmashauri zote zifanye mapitio ya vyanzo vyao vya mapato, waongeze mbinu za ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kusudi wawe na uwezo mzuri wa kuweza kulipa. Hii ni kwa sababu hata taarifa za CAG zinaonesha kwamba ile asilimia 20 katika baadhi ya Halmashauri imekuwa hairudi kule kwenye vijiji kwa sababu tu ya malalamiko kwamba wamekusanya kidogo sana. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.