Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 9 Sitting 8 Water and Irrigation Maji na Umwagiliaji 101 2017-11-16

Name

Gibson Blasius Meiseyeki

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Magharibi

Primary Question

MHE. GIBSON B. MEISEYEKI aliuliza:-
Uhaba wa maji ni moja kati ya matatizo sugu katika Jimbo la Arumeru Magharibi ingawa maji yote yanayotumika katika Jiji la Arusha yanatokea kwenye Jimbo la Arumeru Magharibi:-
Je, ni nini mkakati wa haraka wa Serikali wa kutatua tatizo hilo la maji katika kata takribani 20 kati ya kata 27 za jimbo hilo?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gibson Blasius Meiseyeki, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli zaidi ya asilimia 65 ya maji yanayotumika Jiji la Arusha yanatoka katika vyanzo vilivyopo katika Halmshauri ya Arusha lilipo Jimbo la Arumeru Magharibi. Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) ni kuboresha huduma ya maji vijijini na mijini kwa kujenga miradi mipya, kupanua na kukarabati miundombinu ya maji.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali imekamilisha miradi mitatu katika Vijiji vya Ilkirevi, Oleigeruno na Nduruma na miradi mingine sita katika Vijiji vya Bwawani, Likamba, Ngaramtoni, Oloitushula, Nengun’gu na Loovilukuny ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Miradi yote hiyo ipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.
Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Kata za Moivo, Sokon II, Kiranyi, Bangata na Kiutu ambazo zipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha vinanufaika na huduma ya maji safi na salama yanayotumika katika Jiji la Arusha. Aidha, Kata tatu za Olturumet, Olmotony na Kimnyak ambazo pia zipo katika Halmashauri hiyo zitanufaika na mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa hivi sasa katika Jiji la Arusha.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/ 2018, Serikali imetenga shilingi bilioni tatu kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Arusha za kukamilisha miradi inayoendelea. Aidha, hivi sasa Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo (DFID) imetoa shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya usanifu wa mradi wa kuboresha huduma ya maji utakaohudumia Vijiji vya Lengijave, Olkokola, Ekenywa, Ngaramtoni na Seuri ambavyo pia vipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha. Usanifu wa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2018.