Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 10 Sitting 5 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 61 2018-02-05

Name

Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Primary Question

MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Serikali imefanya kazi kubwa kujenga mtandao wa barabara za kiwango cha lami nchini, kipindi cha nyuma
barabara kuu zilikuwa zinawekwa matuta ili kudhibiti ajali, lakini hivi karibuni Serikali imefuta utaratibu wa kuweka matuta kwenye barabara hizo na hivyo kuwa chanzo kikubwa cha ajali zinazosababisha majeruhi, ulemavu na vifo. Kwa mfano, eneo la Buigiri, Wilaya Chamwino lina ajali nyingi kutokana na barabara kukosa matuta.
(a) Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kurejesha utaratibu wa kuweka matuta kwenye barabara?
(b) Kama utaratibu wa matuta hauwezekani, je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kuyaondoa matuta yote kwenye barabara kuu ili kuondoa malalamiko ya wananchi kwa viongozi wao kwenye maeneo ambayo hayana matuta?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Mwakanyaga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijatoa majibu ya swali namba 61 la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga Mbunge wa Chilonwa, lenye sehemu (a) na (b) napenda kutoa maelezo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuboresha usalama barabara na kurekebisha sehemu hatarishi kwenye barabara kuu na barabara za mikoa nchi nzima ikiwemo barabara ya Morogoro - Dodoma eneo la Buigiri ili kupunguza ajali za barabarani. Hatua zilizochukuliwa na Serikali kupunguza ajali za barabarani ni pamoja na kuweka au kurudisha alama zote muhimu za barabarani ikiwemo za kudhibiti mwendo, kuweka michoro ya barabarani na kurekebisha kingo za madaraja zilizoharibika, uwekaji wa matuta na kadhalika kama ilivyokuwa ikifanya kipindi kilichopita.
Katika mwaka wa fedha 2017/2018 TANROADS itaendelea kuweka vivuko vya watembea kwa miguu (zebra crossing) na alama zote muhimu nchini pale tutakapohitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa maelezo ya awali napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga Mbunge wa Chilonwa, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ajali za barabarani zina sababisha majeruhi, ulemavu na vifo kwa watu wetu ikiwa ni pamoja na kusababisha hasara kubwa kiuchumi kwa Taifa letu. Moja ya njia ambayo Serikali imekuwa ikitumia kupunguza ajali kwenye baadhi ya sehemu ni kuweka matuta ya barabarani. Hata hivyo, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa, kiutaalam hairuhusiwi kuweka matuta kwenye barabara kuu. Aidha, matuta yaliyowekwa katika barabara kuu yaliwekwa kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani kama njia ya mpito. Wizara inafanya utafiti kupata njia mbadala ya kupunguza ajali kabla ya uondoshaji wa matuta hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mpito, Serikali inaendelea kurekebisha matuta ambayo yalijengwa bila kuzingatia viwango vilivyomo kwenye Mwongozo wa Wizara wa Usanifu wa Barabara (Road Geomentric Manual ya 2011) kulingana na upatikanaji wa fedha.
Aidha, inapobainika kuwa kuna haja ya kuweka matuta kwenye barabara, matuta hayo yatawekwa kulingana na viwango vilivyoainishwa kwenye mwongozo huu.