Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 14 Sitting 10 Water and Irrigation Maji na Umwagiliaji 120 2019-02-08

Name

Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMINA N. MAKILLAGI aliuliza:-

Tatizo la maji linaendelea kuwa kubwa siku hadi siku katika maeneo mbalimbali:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya majisafi na salama vijijini?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto kubwa ya upatikanaji wa fedha inayokabili ujenzi wa miundombinu ya maji katika maeneo mbalimbali nchini. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia programme ya maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya pili iliyoanza mwezi Julai, 2016, imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kutenga na kutoa fedha za kujenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji katika maeneo ya maji Vijijini, Miji Mikuu ya Mikoa, Miji Mikuu ya Wilaya, Miji midogo pamoja na Miji na Vijiji vinavyohudumiwa na miradi ya maji ya Kitaifa. Lengo ni kufikia asilimia 85 ya wananchi wanaopata huduma ya majisafi na salama katika maeneo ya vijijini na asilimia 95 kwa maji mijini ifikapo 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha fedha za ndani zinapatikana za kutosha na kwa wakati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, Serikali imeanzisha Mfuko wa Maji ambao umekuwa chanzo cha uhakika wa fedha kwa ajili ya miradi ya maji hususan vijijini. Kutokana na jitihada hizo za kutafuta fedha za miundombinu ya maji, hadi sasa huduma ya maji vijijini imefikia asilimia 64.8 na kwa upande wa mijini imefikia asilimia 80.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha miundombinu ya maji inajengwa katika maeneo mbalimbali na kutoa huduma ya maji kwa wananchi.