Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 9 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Fedha 76 2019-04-12

Name

Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DAIMU I. MPAKATE (K.n.y. MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO) aliuliza:-

Idadi ya watu nchini inazidi kuongezeka sambamba na ongezeko la mahitaji ya ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji ili kuendeleza shughuli zao kwa tija na kuwaondolea adha wanazozipata?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu ufugaji bora na uzalishaji wa malisho kupitia mashamba darasa ili kuwajengea uwezo wa kufuga kwa tija pamoja na kuendeleza malisho katika maeneo yaliyotengwa. Lengo la kutoa elimu hii ni kuhakikisha wafugaji wanaachana na ufugaji wa kuhamahama na kutulia kwenye eneo moja lenye malisho yaliyoboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya mashamba darasa 265 yameanzishwa katika Halmashauri mbalimbali nchini ambapo wafugaji wanaweza kujifunza jinsi ya kuzalisha mbegu na malisho bora ya mifugo ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa mbegu na malisho ya mifugo. Aidha, katika mwaka wa 2018/2019, Serikali imeongeza hekta 2,500 katika mashamba yake kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu za malisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imepanga kutoa mafunzo rejea kwa wafugaji na Maafisa Ugani nchi nzima juu ya ufugaji bora unaozingatia ukubwa wa ardhi iliyopo. Mafunzo hayo tayari yameanza kutolewa katika Halmashauri ya Simanjiro, Mkoani Manyara na Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Mkoani Tabora na kuendelea kutolewa kwa awamu katika Halmashauri zote nchini. Aidha, Serikali imeendelea na juhudi za kuwasaidia wafugaji kukabiliana na tatizo la maji kwa ajili ya mifugo kwa kuchimba malambo 1,381 na visima virefu 103 katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Mawaziri nane iliyoundwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kutafuta suluhu ya migogoro ya matumizi ya ardhi iliyoko nchini tunaamini itakuja na mapendekezo chanya ambayo yatapelekea kuondoa migogoro na adha zinazowakabili wafugaji na wakulima nchini.