Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 11 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 96 2019-04-16

Name

Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

Barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye urefu wa kilometa 123 inayounganisha nchi mbili za Tanzania na Msumbiji, bado haijaanza kujengwa kwa kiwango cha lami:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye urefu wa kilometa 123 ni barabara kuu inayounganisha nchi mbili za Tanzania na Msumbiji na inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii iliamua kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa lengo la kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, kazi ambayo ilikamilika mwaka 2013. Katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 shilingi bilioni 5.86 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa uchimbaji na usafirishaji wa makaa ya mawe katika Kijiji cha Muhukuru kilicho kilometa 74 kutokea Songea katika barabara hiyo, kumesababisha kuongezeka kwa magari mengi na mazito yanayobeba makaa ya mawe. Kufuatia hali hiyo, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) imeamua kufanya mapitio ya usanifu wa kina (Design Review) ili kukidhi mahitaji halisi yaliyojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kazi hiyo kukamilika, Serikali itaendelea kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.