Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 18 Sitting 9 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 111 2020-02-07

Name

Salum Mwinyi Rehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Primary Question

MHE. SALUM MWINYI REHANI aliuliza:-

(a) Je, ni lini Mamlaka ya Hali ya Hewa itakuwa inatoa taarifa sahihi na za wakati kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini?

(b) Je, ni lini Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kushirikiana na Idara ya Earthy Warming watakuwa wanatoa taarifa za hali ya upatikanaji wa mvua na ukame ili kuwaepusha wakulima wengi kulima na kupata hasara kwa kukosa mvua wakati wao wanajua hali itakavyokuwa?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salum Mwinyi Rehani, Mbunge wa Uzini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imeendelea kuboresha usahihi wa taarifa za hali ya hewa kwa kuhakikisha uwepo wa vifaa muhimu katika vituo vya utabiri wa hali ya hewa nchini. Kwa sasa usahihi wa taarifa zinazotolewa umefikia asilimia 87.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, TMA imeanzisha Jarida la Klimatolojia ambalo hutolewa kila mwaka kuhusu tathmini ya viashiria vya mabadiliko ya hali ya hewa nchini. Pia, mwaka 2015, Mamlaka iliandaa taarifa inayoonesha mwelekeo wa mabadiliko ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na mwelekeo wa unyeshaji mvua na joto kwa miaka 30 ijayo. Kimsingi tangu mwaka 2015, kiwango cha usahihi katika tabiri za hali ya hewa kimekuwa zaidi ya 80% ambacho ni kiwango cha chini kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, TMA hutoa taarifa mbalimbali za hali ya hewa kwa umma ikijumuisha zile za utabiri wa kila siku, misimu ya mvua na tahadhari ya hali mbaya ya hewa nchini. Taarifa zinazotolewa zinajumuisha ushauri na tahadhari pale inapoona dalili za kuwepo kwa matukio ya mafuriko au ukame wakati wa misimu ya mvua. Aidha, TMA inashirikiana na vyombo mbalimbali vya habari na Serikali ikiwemo Wizara ya Kilimo (Idara ya Usalama wa Chakula, Kitengo cha Early Warning) ili kuhakikisha kwamba taarifa za hali ya hewa zinawafikia Maafisa Ugani na watumiaji kwa wakati. Taarifa hizi pia husambazwa kupitia ofisi zote za hali ya hewa nchini.

Mheshimiwa Spika, katika taarifa zinazotolewa, wakulima hushauriwa kupata ushauri kutoka kwa wataalam mbalimbali wakiwemo Maafisa Ugani. Mamlaka ya Hali ya Hewa pia imeanzisha mfumo wa kusambaza Taarifa za Hali ya Hewa kwa wakulima kupitia njia ya ujumbe katika simu za viganjani (farm sms).