Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 16 Sitting 7 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 88 2019-09-11

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. PASCAL Y. HAONGA (K.n.y. MHE. DAVID E. SILINDE) Aliuliza:-

Je, ni lini barabara ya Mlowo – Kamsamba – Kiliyamatundu – Kibaoni itajengwa kwa kiwango cha lami?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mlowo – Kamsamba – Kiliyamatundu – Kibaoni yenye urefu wa kilometa 369 ni barabara ya Mkoa na inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha ujenzi wa Daraja la Momba lenye urefu wa mita 84 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inaendelea kwa barabara kuanzia Kamsamba hadi Mlowo, kilometa 130.14 na barabara ya mchepuo kwa kuingia Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, kilometa 15, kwa gharama ya shilingi milioni 765.46. Kazi hii imefikia asilimia 75.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 180 kwa ajili ya kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara na kuijenga kwa kiwango cha lami sehemu ya barabara hii kuanzia Kiliyamatundu hadi Kasansa (sehemu ya Kilyamatundu – Muze (km 142) na Ntendo – Muze (km 37.04), taratibu za kumpata Mshauri Elekezi wa kufanya kazi hiyo zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sehemu ya barabara kutoka Kasansa hadi Kibaoni (km 60), sehemu ya kuanzia Kibaoni hadi Majimoto (km 34) ipo kwenye hatua za manunuzi ya kumpata mshauri elekezi kwa ajili ya kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Kibaoni – Majimoto – Inyonga (km 162). Aidha, sehemu iliyobaki kuanzia Muze – Mamba – Majimoto (km 55) Serikali inatafuta fedha ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kwa ajili ya usafiri wa wananchi na usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara yanayozalishwa na wananchi wa maeneo ya Kata za Igamba, Hulungu, Itaka, Nambinzo hadi Kamsamba pamoja na maeneo ya Kiliyamatundu, Muze, Kasansa, Majimoto hadi Kibaoni, Serikali inaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka na mara tu usanifu wa kina utakapokamilika, ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hii utafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.