Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- (a) Je, bado kuna faida kwa Watanzania kuendelea kukimbiza Mwenge wa Uhuru kila mwaka, kama zipo ni faida gani? (b) Kama hakuna faida, je, ni lini Mwenge huo wa Uhuru utasitishwa?

Supplementary Question 1

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Swali la kwanza, malengo, dhamira ya kuanzishwa Mwenge wa Uhuru yameonekana kutotimizwa ikiwemo badala ya kueneza upendo Mwenge wa Uhuru umekuwa unaeneza chuki. Mfano, katika Mkoa wa Rukwa hivi karibuni Wenyeviti na Watendaji waliwekwa ndani kwa kosa la kutochangisha wananchi kuhudumia Mwenge wa Uhuru.
Je, kama ni mfano wa kuigwa na katika Afrika na Dunia hakuna nchi iliyotuigiza wakakimbiza Mwenge huu hamuoni kwamba kukimbiza Mwenge sio kuleta maendeleo katika nchi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali pili, nataka nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu Mwenge wa Uhuru historia yake ni kuupamba Uhuru wa Tanganyika na Zanzibar ina historia yake ya kupata Uhuru kutokana na Mapinduzi. Kwa sababu Mwenge sio jambo la Muungano, hamuoni sasa iko haja ya kuacha kuuleta Mwenge huu kule Zanzibar ambapo hatuoni maana yake yoyote?

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango, uratibu na utekelezaji wa kimfumo na wa kifalsafa wa ukimbizaji wa mbio za Mwenge, huratibiwa kwa kufuata kanuni na utaratibu wa maandalizi uliowekwa kwa nchi nzima ya Tanzania. Hivyo basi, kama ziko dosari ambazo zimekuwa zikijitokeza eneo moja hadi lingine hazitaki kumaanisha kwamba historia ya falsafa ya Mwenge ile ambayo imejengwa katika misingi ya uhuru wa nchi yetu, eti sasa ndiyo iondolewe kwa sababu ya dosari hizo ndogo zinazojitokeza. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali kwenye dosari ndogo tutaendelea kuzipitia na kuziondoa ili falsafa ya Mwenge wa Uhuru iendelee kubaki kama ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mheshimiwa Mbunge anasema Zanzibar si sehemu ya Mwenge huu wa Uhuru. Nataka kumkumbusha Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya matunda mema ambayo yalizaliwa kwa sababu ya falsafa ya Mwenge wa Uhuru ni pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Azimo la Arusha na ukombozi wa Bara la Afrika. Hivyo, kwa sababu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni matunda ya Mwenge wa Uhuru, Mwenge huu utaendelea kukimbizwa Bara na Visiwani na utaendelea kuenziwa na Watanzania wote Bara na Visiwani ukiwemo wewe Mheshimiwa Mbunge Haji kutoka Visiwani kama Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo linaenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru.

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- (a) Je, bado kuna faida kwa Watanzania kuendelea kukimbiza Mwenge wa Uhuru kila mwaka, kama zipo ni faida gani? (b) Kama hakuna faida, je, ni lini Mwenge huo wa Uhuru utasitishwa?

Supplementary Question 2

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi nataka kuuliza kwa mtu ambaye ni Mtanzania aliyezaliwa katika nchi yetu, anayehoji juu ya Mwenge…
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Badala ya kuhoji juu ya mambo mabaya yanayotokea kwenye Mwenge, anayehoji juu ya Mwenge unafanya nini huyu unaweza kumkabidhi hii nchi akaendelea kukaa nayo? Nataka tu kupata ufafanuzi huo.

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri ambalo linaonyesha jinsi alivyokomaa katika kujua historia ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niwaambie Watanzania, falsafa ya Uhuru wa nchi yetu ya Tanzania haiwezi kutenganishwa na Mwenge wa Uhuru. Naomba niwakumbushe, wakati wa Uhuru tarehe 9 Desemba 1961, Marehemu Baba wa Taifa alisema, sisi tutawasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike ndani na nje ya mipaka yetu ulete amani, tumaini, upendo, uondoe chuki na dhuluma, sasa jambo hili si dogo. Kwa Mtanzania anayemuenzi Marehemu Baba wa Taifa itashangaza sana kama hatataka kuenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda tu kuwaomba Watanzania kwa kweli hatuna haja ya kuchukuliana hatua ya namna moja au nyingine lakini wote tutambue Mwenge wa Uhuru ni tunu kubwa ya Uhuru wa nchi yetu na unapaswa kuenziwa na Watanzania wote.

Name

Dr. Ally Yusuf Suleiman

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mgogoni

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- (a) Je, bado kuna faida kwa Watanzania kuendelea kukimbiza Mwenge wa Uhuru kila mwaka, kama zipo ni faida gani? (b) Kama hakuna faida, je, ni lini Mwenge huo wa Uhuru utasitishwa?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kama ziko dosari katika kukimbiza Mwenge basi zitarekebishwa. Mimi nachotaka kumwambia hakuna dosari, dosari ni huu Mwenge wenyewe. Kwa sababu kwanza unapoteza fedha nyingi kupita kiasi na wakati na kwa kule kwetu tunaamini kukimbiza Mwenge ni ibada. Kwa nini tuendelee kulazimishwa kuabudu moto?
Swali langu ni hilo kwa nini tulazimishwe kuabudu moto? Sisi tunaamini ni ibada ya moto hiyo.

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimia Mwenyekiti, labda tu nianze kwa kumnukuu mwanafalsafa mmoja ambaye nilimsoma anasema, vipo vitu vingine vinahesabika lakini huwezi kuvihesabu. Unaweza ukawa na vitu vinavyohesabika lakini ukashindwa kuvihesabu na nataka nikuambie hata wewe unaweza kuwa na mtazamo ambao ni hasi kuhusu Mwenge wa Uhuru lakini utashindwa kutekeleza mtizamo huo wa kuufuta Mwenge wa Uhuru katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nakuambia hivi Mheshimiwa Mbunge, mwaka jana wakati tunahitimisha mbio za Mwenge Mkoani Simiyu, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Simiyu, kwa kutumia Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Simiyu umeweza kuzindua viwanda vitatu ambavyo vimeongeza maendeleo ya kiuchumi na vimeongeza ajira kwa Watanzania. Kwa hiyo, ukiangalia faida za Mwenge huu ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu tumezindua
mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Katavi. Mkoa wa Katavi haukuwa na uwanja mkubwa wa michezo wa Mkoa. Nje ya bajeti ya maendeleo ya mkoa, Mkoa wa Katavi umeweza kuanza ujenzi mkubwa wa kiwanja cha mpira katika mkoa huo. Nimeeleza hapa miradi ya kujitegemea ambayo imebuniwa na wananchi ambayo imeongeza chachu ya maendeleo na uchumi wa wananchi katika Tanzania nzima. Mwenge wa Uhuru utadumu, utaendelea kusimama kama tunu ya nchi yetu ya Tanzania.

Name

Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- (a) Je, bado kuna faida kwa Watanzania kuendelea kukimbiza Mwenge wa Uhuru kila mwaka, kama zipo ni faida gani? (b) Kama hakuna faida, je, ni lini Mwenge huo wa Uhuru utasitishwa?

Supplementary Question 4

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mwaka jana Mwenge ulizimwa Simiyu, Mtukufu Rais John Pombe Magufuli alizuia misafara ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na baadhi ya Wakurugenzi na kuokoa kiasi cha pesa sijui zaidi ya shilingi bilioni sita.
Nataka kujua kwa mwaka mzima kukimbiza Mwenge wa Uhuru kunagharimu Taifa hili shilingi ngapi? (Makofi)

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Keissy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimwa Keissy kwa kutambua namna ambavyo Mwenge huu wa Uhuru kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais uliweza kuokoa fedha nyingi sana ambazo zilikuwa zikitumiwa na Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine kuhudhuria katika mbio hizo za Mwenge. Tumekubaliana kwamba ni lazima tuendelee kuthamini namna nzuri ya matumizi ya fedha katika kukimbiza Mwenge wa Uhuru. Kwa hiyo, hilo halina shaka Mheshimiwa Keissy na sisi tunalisimamia vizuri kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Mwenge wa Uhuru ambayo Mheshimiwa Keissy anataka kujua ni kiasi gani zimekuwa zikiandaliwa kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine. Hivyo kama anataka kujua ni kiasi gani bajeti zinatumika katika kila Halmashauri moja kwenda nyingine nitamuomba aonane na mimi na tutawasiliana na hizo Halmashauri.