Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Gibson Blasius Meiseyeki

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Magharibi

Primary Question

MHE. GIBSON B. OLE-MEISEYEKI aliuliza:- PPRA na TEMESA vimekuwa vyombo vinavyoisababishia Halmashauri zetu hasara kubwa katika utekelezaji wa miradi katika utengenezaji magari na mitambo badala ya kusaidia Serikali katika kutimiza majukumu yake kwa bei nafuu:- Je, Serikali haioni umefika wakati wa kuvifuta vyombo hivyo au kuvibadilishia utaratibu wake wa kufanya kazi ili viweze kuwa na tija kwa Taifa letu?

Supplementary Question 1

MHE. GIBSON B. OLE-MEISEYEKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matokeo ya utekelezaji kazi wa Wakala hawa wa Serikali imekuwa tofauti kabisa na makusudio ya uundwaji wa sheria hizi, nikiwa na maana kwamba vyombo hivi vinaisababishia Halmashauri na Taasisi za Serikali usumbufu mkubwa wa ucheleweshaji wa utengenezaji wa mitambo lakini pia gharama kubwa za utengenezaji wa mitambo hiyo ukilinganisha na bei zilizoko kwenye masoko ya kawaida. Kwa mfano, TEMESA haina kabisa karakana na wataalam wa kutengeneza mitambo yetu hii, kwa maana hiyo Wakala hawa wamekuwa kama kupe wa kufyonza fedha za Serikali badala ya kuisaidia Serikali kuweza kutengeneza miradi kwa gharama nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliuliza kwenye swali langu la msingi kwa nini isifanyiwe marekebisho ya utekelezaji wao wa kazi ili sasa iweze kuleta tija na maendeleo ya haraka katika maeneo yetu badala ya kuweka vyombo ambavyo vinasababisha gharama kubwa katika utekelezaji wake wa kazi. Kwa hiyo, swali langu linabaki pale pale, kwa nini Serikali isibadilishe utaratibu wa utekelezaji kazi wa mamlaka hizi ili kuweza kuleta tija na ku-save fedha badala ya kusababisha gharama kubwa mara mbili, tatu ya gharama sahihi zilizoko mitaani? Kwa nini utaratibu wa utekelezaji wake wa kazi usibadilishwe? Ahsante (Makofi)

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge nikuambie mimi nimeitumia TEMESA, nilikuwa Meneja wa TANROADS na nilikuwa Wizara ya Ujenzi, kwa hiyo TEMESA naielewa vizuri kwa undani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, amesema kwamba TEMESA imekuwa na usumbufu, gharama kubwa na ucheleweshaji, hayo anayoyazungumza ni kweli. Ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema kwamba TEMESA sasa hivi uongozi umebadilishwa na karakana zilizopo zinaboreshwa kwa kuwekewa vifaa vilivyo bora. TEMESA ilikuwa na shida ya namna ya kutumia sheria mliyoiunda ninyi Wabunge ya PPRA, sasa hivi wamewekwa wataalam ambao wataitumia ile sheria vizuri. Sheria ni nzuri sana lakini kulikuwa na wafanyakazi ambao sio waadilifu na Serikali hii ya Awamu ya Tano imechukua hatua ya kuhakikisha kwamba inawaondoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wazo lake la kusema chombo hiki kwa sasa kibadilishwe, ukianza kuunda kingine leo utaanza tena kuwafundisha mpaka wafike huko watakakofika. Sasa hivi hawa tayari wameshaiva, tunahakikisha wanaboreshwa ili TEMESA iwe na ufanisi mzuri kuliko garage nyingine yoyote ya kawaida. Naomba atupe muda na tushirikiane tuendelee kutekeleza suala hili.