Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:- Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji:- Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Supplementary Question 1

MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo ameyatoa hapa hivi sasa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza nataka kuuliza. Je, Serikali inasema nini katika kuboresha kilimo cha umwagiliaji maji kwa kupitia mito mikubwa, maziwa na mabwawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na kilimo cha umwagiliaji maji, je Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wakulima juu ya kilimo hicho. (Makofi)

Name

Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Answer

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumejibu kwenye swali letu la msingi ambapo Serikali imeweka mipango mikakati ya kuhakikisha kwamba kilimo cha umwagiliaji na hasa pale ambapo tunakuwa na matatizo ya ukame; matatizo ambayo yanasababisha mvua zisijulikane sana. Ndio maana mipango ambayo nimeisema katika majibu yangu ya msingi, inabidi izingatiwe.
Mheshimiwa Spika, vilevile wakulima wanashauriwa katika kilimo hiki cha kutumia maji vizuri, kikiwemo na kilimo hiki ambacho tunaita drip irrigation. Kilimo ambacho kinatumia matone ya maji na hivyo kuweza kuwa na maji mengi kwa ajili ya watumiaji wengine.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la pili ambalo ni la elimu kwa wakulima. Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la NEMC tumekuwa na mikakati mbalimbali ya kuwapa wakulima elimu. Vilevile kwenye Sikukuu ya Wakulima ya Nane Nane tumekuwa tukichapisha majarida mbalimbali; majarida mengine ambayo ninayo hapa ambayo baada ya hapa nitampatia Mheshimiwa Mbunge. Wadau mbalimbali na wakulima wamekuwa wakitembelea mabanda yetu na kupata vipeperushi pamoja na majarida mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia mikakati ambayo tumeizungumzia hapa, nitampatia Mheshimiwa Mbunge kuna hii ya National Climate Change Strategy ambayo tumeizungumzia ya mwaka 2012 halafu vilevile tunayo miongozo ambayo ni ya kisera kuhusiana na suala la sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, niseme pia kwa faida ya Watanzania wote, masuala ya mazingira ambayo yanaathiri kilimo yameanzia kwenye Biblia ukisoma Mwanzo 10:15 ambapo Mungu alianzisha utaratibu kwenye ile mito minne akamwambia mwanadamu nakuagiza ukalime na kuitunza.
Mheshimiwa Spika, hivyo, vyanzo vya maji ni asili yake kwenye Biblia. Hii ndio maana na sisi kwa kutunga Sheria hii namba 20 ya 2004, vilevile tumechukua kipengele hicho tukaweka kifungu cha sita (6) ambacho kinatoa wajibu wa kisheria kwa kila mtanzania kutunza na kuhifadhi mazingira.
Mheshimiwa Spika, Ahsante sana. (Makofi)