Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Rungwe

Primary Question

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:- (a) Ranchi ya NARCO Mbarali ilianzishwa kwa ajili ya mifugo; Je, ni kwa nini eneo hilo sasa linatumika kwa kilimo? (b) Migogoro ya wakulima na wafugaji Mbarali imekuwa ni mingi; je, kwa nini Serikali isitoe eneo la Ranchi ya NARCO Mbarali ili litumike kwa ajili ya malisho ya mifugo?

Supplementary Question 1

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kutokana na jibu la msingi alilojibu Mheshimiwa Waziri ni kwamba ranchi ile imepewa wawekezaji wazawa, ni kweli; lakini wao wazawa wanawakodisha wananchi kulima na si kama vile mkataba unavyosema. Hiyo ni moja.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mkataba ni mkataba unaweza ukavunjwa kama unakiukwa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuvunja huo mkataba na kuwapatia wananchi wafugaji wa Mbarali waweze kufuga kwani hawana nafasi za kufuga kutokana na maeneo tengefu kuzuiwa na Serikali? Naomba Serikali iwapatie wananchi waweze kufuga mifugo yao. Ahsante.

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni juu ya wawekezaji wanavunja mkataba kwa kuwakodisha wananchi. Jambo hili tumelisikia na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumeweka mkakati kwanza kabisa tunathaminisha Ranchi zetu zote katika Taifa letu kwa kuangalia ile mikataba yote ambayo tuliwakodisha wawekezaji ambao hawakukidhi mahitaji yetu sawa na mikataba; tutavunja kwa kutangaza upya na kuwakaribisha wafugaji wote wenye uwezo wa kuweza kufuga kulingana na matakwa ya mkataba.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Mwakagenda anauliza kama tutawapa wananchi. Lengo letu sisi ni kuona kwamba ranchi hizi zinatumika kwa malengo mahususi; mosi ya kuhakikisha pia hata ranchi hizi zitusaidie katika kupunguza migogoro ya wafugaji na wakulima; lakini mbili, ranchi hizi ambazo zimetapakaa nzima, ziwe ni sababu kubwa ya kuongeza kipato katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, huu mkakati utakapokamilika na tutakapokuja nao; tunaomba Wabunge wote nchi nzima watupe ushirikiano ili tuweze kufanikisha ajenda hii ya kusukuma mbele tasnia ya ufugaji. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:- (a) Ranchi ya NARCO Mbarali ilianzishwa kwa ajili ya mifugo; Je, ni kwa nini eneo hilo sasa linatumika kwa kilimo? (b) Migogoro ya wakulima na wafugaji Mbarali imekuwa ni mingi; je, kwa nini Serikali isitoe eneo la Ranchi ya NARCO Mbarali ili litumike kwa ajili ya malisho ya mifugo?

Supplementary Question 2

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Tatizo la Ranchi ya Mbarali linafanana kabisa na tatizo la Ranchi ya Mkata iliyoko Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro ambapo Ranchi ile hivi sasa imegeuka kuwa pori na Serikali imeshindwa kuiendeleza. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kubinafsisha Ranchi ile, mashamba yatolewe kwa wakulima na wafugaji ili kupunguza migogoro ya muda mrefu?

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi na naomba nijibu swali la nyongeza ambalo ameuliza Mheshimiwa Devota Minja na kama ambavyo Naibu wangu amejibu vizuri sana maswali hapa Bungeni, tunataka Wabunge watuelewe. Kwanza Serikali haijashindwa kusimamia ranchi hizi, tunachokifanya kama Naibu Waziri alivyozungumza tunafanya tathmini sasa tupitie ranchi zetu zote tujue shughuli zinazofanyika.
Mheshimiwa Spika, tunajua upungufu uliopita kwamba zipo ekari sasa hivi, unakuta ekari moja imekodiwa mtu analipa Sh.500/= kwa mwaka. Kuna ekari zimekodiwa mtu analipa Sh.1,000/= kwa mwaka; kuna mahala ambapo uwekezaji hauendani na eneo lilivyo. Kwa hiyo tunafanya tathimini ili tuje na mpango mkubwa kwa sababu gani ranchi hizi shabaha ya kuanzishwa kwake haijaondoka toka tulivyoanzisha na ndio maana tunataka kupitia ranchi hizi tufanye mageuzi makubwa ya kuwa na viwanda vikubwa nchini kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wenye viwanda nchini wanapata mahali pa kutunzia mifugo yao kabla hawajachinja.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tunataka tuwa- transform wafugaji wetu, hatuwezi kuruhusu huu ufugaji wa mtu anafuga mifugo leo, anamchunga ng’ombe mpaka anakufa mwenyewe. Lazima tuwabadilishe wafugaji wetu tuwe na maeneo ambayo tutazalisha mitamba ya kutosha, tutazalisha ndama wa kutosha, tutazalisha mifugo ambayo inaweza ikagawiwa kwa wafugaji ili wafugaji wetu waweze kupata neema ya ufugaji huu.
Mheshimiwa Spika, kupitia ranchi hizi tunategemea kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi katika Taifa hili na kwa wafugaji Tanzania. Kwa hiyo, tuungeni mkono tutakapoleta mabadiliko yetu na Wabunge muache hili la kila mmoja kuhitaji ligawiwe kwa wananchi; tunataka ranchi hizi zitumike kwa faida ya Taifa na kwa mapana zaidi (Makofi).