Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Primary Question

MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:- (a) Je, Serikali imefikia wapi katika ujenzi wa bomba la maji la kwenda Tabora- Igunga kupitia Nzega? (b) Je, Serikali imefikia hatua gani katika kusambaza maji hayo katika Tarafa za Simbo na Choma kupitia Ziba kama Mheshimiwa Makamu wa Rais alivyoahidi?

Supplementary Question 1

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tumekuwa tunapata taarifa za Serikali juu ya kuanza kwa mradi huu kila mwaka na hata mwaka 2014 tulipata taarifa hiyo, je, Serikali inaweza kutuambia katika bajeti hii ya mwaka 2016/2017 imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya kuanza kwa mradi huo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ilikuwa ni ahadi ya Makamu wa Rais kutupatia maji ya Ziwa Victoria katika maeneo ya Choma na Tarafa ya Simbo na iliombwa kwa madhumuni ya kuwa, moja tunakwenda kupata Wilaya mpya, lakini pili katika maeneo hayo tuna hospitali ya rufaa ya Nkinga ambayo inahudumia karibu mikoa mitano, je, Serikali haijaona haja ya kupeleka maji katika maeneo hayo yaliyoombwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa ujenzi wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda maeneo ya Nzega, Tabora na Igunga ulianza mwaka 2012 na inatarajiwa sasa katika mwaka mpya wa fedha unaokuja 2016/2017 taratibu zile za manunuzi zitakuwa zimekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri mradi huu unafadhiliwa na tayari mfadhili amesha-commit dola milioni 268.35. Kwa hiyo, uhakika wa fedha tunao. Kama nilivyojibu katika hoja ya msingi kwamba sasa hivi tumeshamaliza kutambua Makandarasi na tumepeleka kwa mfadhili Benki ya India kwa jili ya kupata no objection ili tuweze kuendelea na hatua nyingine ili ifikapo mwezi Julai mwaka huu tuwe tumeanza kazi ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli taarifa ipo, kwamba Mheshimiwa Makamu wa Rais aliahidi kupeleka maji Manonga, lakini kama nilivyosema kwamba mchakato huu ulianza mwaka 2012 na tukaanza kufanya usanifu na kipindi hicho wakati tunatengeneza memorandum tulikubaliana kwamba kwa maana ya mradi huu utakwenda kilomita 12 kila upande wa bomba litakapopita lile bomba kuu. Kwa hiyo, ahadi imekuja wakati taratibu hii iko nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, huu siyo mwisho, ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais tunayo, kwa hiyo, asubiri tuanze ujenzi. Wakati wa ujenzi tutaangalia tutakachofanya ili kuhakikisha kwamba, tunatimiza ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais.