Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Meatu

Primary Question

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Ujenzi wa bwawa la Mwanjoro lililopo Wilaya ya Meatu ulianza mwaka 2009 lakini hadi sasa ujenzi wa bwawa hilo haujakamilika:- (a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa bwawa hilo ili liweze kutumika kwa ajili ya wananchi na mifugo katika Vijiji vya Jinamo, Mwanjoro, Itaba, Nkoma na Paji? (b) Je, ni lini Serikali italeta fedha za miradi ya aina hii kwenye Halmashauri ili Halmashauri ziweze kutafuta Mkandarasi kufanya usimamizi na ufuatiliaji wa karibu na hatimaye kuondoa usumbufu kwa wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kutia moyo wananchi wa Wilaya Meatu. Mradi huu ni wa muda mrefu wa mwaka 2009, yapata sasa miaka sita, wananchi walitoa eneo hilo na kuacha kufanya shughuli zao pasipo malipo, matokeo yake bwawa hilo limekuwa likijaa na kusababisha uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na mmomonyoko wa udongo. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie Wizara katika mpango mkakati wake wa mwaka 2016/2017, imepanga ni lini mradi huo utakamilika na uanze kutumika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, nimekuwa nikishuhudia miradi kama hii, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kuchimba mabwawa, lakini yamekuwa hayakidhi mahitaji kama ilivyokusudiwa, kwa mfano mradi wa maji Mjini Mwanuhuzi, naomba Serikali iniambie je, inaniahidi nini kukamilisha mradi huo na kuusambaza katika Vijiji vya Jinamo, Paji, Mwanjolo, Koma na Itaba?

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ameuliza ni lini bwawa la Mwanjolo litakamilika; katika bajeti yangu ambayo nitawasilisha hapa Bungeni muda siyo mrefu, tumeliwekea bwawa hili mpango wa kuweza kulikamilisha, kwa hiyo, tutaleta maelezo na kazi ambazo zitafanyika ili tulikamilishe bwawa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu mradi wa maji anaoelezea, lini tutakamilisha katika vijiji vingine; mambo yote haya tumeyaweka kwenye mpango, kwanza tunakamilisha miradi yote ambayo inaendelea iliyokuwa kwenye program ya maji awamu ya kwanza, halafu tunaingia awamu ya pili. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge nia ya Serikali ni kwamba, miradi yote ambayo ipo tutaikamilisha na tutakwenda kuikagua kuhakikisha kwamba inafanywa jinsi inavyotakiwa. Ahsante.