Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Najma Murtaza Giga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:- Masuala ya kunajisi na ubakaji kwa watoto pamoja na mapenzi ya jinsia moja yamekithiri nchini na kuongezeka siku hadi siku:- (a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya utafiti wa kina na kuona athari zinazoendelea kuikumba jamii katika suala zima la usagaji (lesbianism)? (b) Je, ni lini Serikali itaanza kuandaa sheria ya kuwaadhibu wanawake wanaoharibu vijana wa kiume chini ya umri wa miaka 18 na wale wenye kuwafunza na kuwaharibu watoto wetu wa kike katika masuala ya usagaji (lesbianism)?

Supplementary Question 1

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nashukuru Serikali kwa kukubali na kuelewa kwamba suala hili linatambulika na lipo.

Mheshimiwa Spika, kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, nataka ieleweke kwamba suala hili kama ilivyo ushoga yaani Lesbianism ni masuala ya usiri sana, kwa hiyo, kuyajua kwake siyo rahisi sana. Kwa hiyo, kwanza ningeomba Serikali isicheleweshe jambo hili la utafiti ili tuweze kujua kiwango cha athari hizo.

Mheshimiwa Spika, pia nataka ieleweke na itambulike kwamba kunyamaza kwetu kimya sasa hivi na kuogopa mambo haya miaka 50 ijayo ndani ya Bunge hili badala ya kujadili maandeleo na maadili mema ya Kitanzania watakuja kujadili namna gani ya kupitisha ndoa ya jinsia moja.

Mheshimiwa Spika, sasa narudi kwenye maswali yangu ya nyongeza. Swali la kwanza, nashukuru Serikali imeona umuhimu wa kutoa elimu pamoja na kwamba kuna sheria ambazo zinadhibiti suala hilo na baada ya utafiti wamesema pia watafanya marekebisho ya sheria. Swali langu lipo hapa, je, wakati tunaendelea kufanya utafiti huo, kwa nini sasa Serikali isishirikiane Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya kuona namna gani bora wanaweka mitaala katika shule zetu na kuonyesha madhara na athari ya mambo haya ambayo ni kinyume cha maadili ya Tanzania ili wanafunzi wetu ambao wanasoma waanze kujengeka na misingi ya maadali na kuachana na mambo haya popote watakapoyaona?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni kwamba tuna wanazuoni wengi sana katika Taifa hili wa dini mbalimbali, kwa nini Serikali sasa hakai nao na ikawataka watoe mahubiri ya kukataza masuala hayo ambayo Mwenyezi Mungu ameyakataza badala ya mambo mengine ambapo haya hawajayatilia mkazo? Maswali yangu ni hayo.

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Najma Giga ambaye ameongea kwa uchungu sana.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameuliza kwa nini Wizara ya Afya isikae pamoja na Wizara ya Elimu kuangalia mitaala ili masuala haya ya maadili yaweze kufundishwa katika shule mbalimbali. Tunapokea ushauri wake na sisi kama Serikali tutaenda kuufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza kwa nini tusiwatake wanazuoni nao wakatoa mahubiri kuhusiana na suala hili. Moja ya taasisi ambayo imekuwa inatujenga katika maadili mema ni pamoja na taasisi zetu za kidini. Kwa hiyo, naamini nao wanatusikiliza kupitia Bunge lako hili Tukufu na wao tuwaombe wachukue majukumu yao ya msingi kuhakikisha kwamba wanahubiri maadili mema ya kitaifa vilevile wanawajenga waumini wao katika maadili mema yanayozingatia misingi yetu ya maadili ya kitaifa. Kwa hiyo, sisi kama Serikali hatuwezi kusema taasisi za dini zifanye lakini taasisi za kidini nazo zina wajibu kuhakikisha kwamba zinajenga waumini wao na Watanzania katika msingi ya maadili mema.

Name

Ally Abdulla Ally Saleh

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Malindi

Primary Question

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:- Masuala ya kunajisi na ubakaji kwa watoto pamoja na mapenzi ya jinsia moja yamekithiri nchini na kuongezeka siku hadi siku:- (a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya utafiti wa kina na kuona athari zinazoendelea kuikumba jamii katika suala zima la usagaji (lesbianism)? (b) Je, ni lini Serikali itaanza kuandaa sheria ya kuwaadhibu wanawake wanaoharibu vijana wa kiume chini ya umri wa miaka 18 na wale wenye kuwafunza na kuwaharibu watoto wetu wa kike katika masuala ya usagaji (lesbianism)?

Supplementary Question 2

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Tatizo la ubakaji watoto linaoneka ni kubwa sana Mkoani Mara. Kamati ya Katiba na Sheria juzi ilikwenda Mara na tukapata taarifa za kutisha kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Malima. Kuna Mwalimu kwa mfano amewafanya wake zake watoto 10 wa darasa la kwanza.

MBUNGE FULANI: Darasa la kwanza?

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, nitarudia, amewafanya wake zake watoto 10 wa darasa la kwanza.

MBUNGE FULANI: Aaaah.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, kuna taarifa nyingi za kutisha juu za ubakaji kwa rika zote, kwa watu wazima na kwa watoto. Je, Serikali ama kupitia Wizara ya Afya au Bunge haioni haja sasa ya kuunda Tume au ya kutafuta utaratibu wa kwenda kulitazama tatizo hili ambalo ni kubwa inafika watu wanauliwa? Risasi zinatumika halafu watu wanakimbia upande wa pili wa Kenya inakuwa vigumu kulishughulikia. Mkuu wa Mkoa Adam Malima alikuwa na pain kubwa alipokuwa akituelezea juu ya suala hili. Naomba Serikali ifikirie jambo hili, ahsante.

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, pamoja na shinikizo kubwa kutoka nchi za Magharibi, shinikizo la ndoa za jinsia moja, shinikizo la kuuona ushoga kama haki za binadamu, bado nchi 38 kati ya nchi 54 za Afrika zinapinga masuala hayo na Tanzania ni mojawapo. Si hivyo tu, sisi tume-criminalize yaani vitendo hivyo ni makosa ya jinai na watu wanafungwa. Kwa hiyo, bado sisi ni moja ya nchi ambazo tumekaa vizuri katika kulinda jamii yetu.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa ni kwamba jamii inaficha haya matatizo. Kwa mfano, matatizo ya watoto kulawitiwa au kubakwa kwa sehemu kubwa yanafanywa na ndugu katika jamii. Tukianza upelelezi familia zinawalinda hawa watu hawatoi ushahidi, ni tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, katika sheria kama hakuna ushahidi huwezi ukamfunga mtu na kosa hili ni kubwa, adhabu ni kali sana.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe wito kwa Tanzania tatizo ni kubwa sasa, tunaomba ushirikiano kwa vyombo vya dola ili tuweze kuwapata hawa wahalifu wanaojaribu kuchafua generation ya kesho, kesho kutwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.