Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Primary Question

MHE. IGNAS A. MALOCHA (K.n. y. MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI) aliuliza:- Tunaishukuru Serikali kwa kutujengea barabara ya lami kutoka Mpanda –Sumbawanga:- Je, ni lini Serikali itamaliza kipande cha kilomita 86 eneo la Hifadhi ya Katavi kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Eneo hilo la kilometa 86 ni eneo korofi na liko katikati ya mbuga ya wanyama, wakati mwingine kama gari zinasafiri inafika gari inakwama katikati ya mbuga, jambo ambalo ni hatari kwa raia ambao watakuwa wamepanda basi hilo. Je, Serikali ituambie imetilia umuhimu gani kuliko kusema kwamba itakapopata fedha kwa sababu jambo hili ni muhimu mno kuliko, naomba majibu ya Serikali katika suala hilo, ni lini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nashukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja la Mto Momba ambalo linaunganisha mikoa mitatu. Nataka kuuliza baada ya ujenzi wa daraja hilo ni lini sasa Serikali itatenga pesa kwa ajili ya upembuzi yakinifu, kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, barabara inayounganisha mikoa mitatu, Mkoa wa Songwe, Rukwa na Katavi?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malocha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii ambayo nimetoka kujibu swali lake kwa sababu utagundua kwamba asilimia 65 ya barabara hii baada ya usanifu tulifanya ujenzi na ujenzi ulizingatia maeneo korofi zaidi. Nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba sehemu hii iliyobaki bado ina maeneo changamoto wakati fulani. Sisi kama Serikali tumeendelea kutenga fedha ili kushungulikia maeneo haya korofi. Hata katika mwaka huu wa fedha unaoendelea tumekuwa na fedha za kutosha kuhakikisha maeneo korofi wakati wowote tunayapa umuhimu wa kuyafanyia matengenezo.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa eneo hili watakuwa mashuhuda wa kuona kwamba wakati wote tunahakikisha kwamba barabara hii inapitika wakati tunajiandaa kwa ajili ya kuitengeneza katika kiwango cha lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira kwa vile sehemu kubwa ya barabara tumeitengeneza hii sehemu ndogo iliyobaki tutakwenda kuitengeneza kwa kiwango cha lami. Tumeweka mapendekezo katika bajeti hii inayokuja kama Bunge lako litatupitishia na Serikali ikapata fedha tutakwenda na hatua ya mwisho kuikamilisha barabara hii.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu barabara hii inayopita katika Daraja la Mto Momba, Mheshimiwa Mbunge anafahamu na nimetembelea eneo hili, ujenzi wa daraja umekamilika kwa sehemu kubwa na sasa tunaweza kupita mto huu. Mheshimiwa Mbunge anafahamu barabara hii ni ndefu sana ukitoka Momba mpaka uje Majimoto na mimi nimeliipita. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeiweka kwenye mpango wetu mkakati kwa maana ya sasa kufanya usanifu baada ya kukamilisha sehemu ya Mto Momba ambayo ni korofi ili sasa tuweze kuitazama kwa ajili ya kuitengeneza katika kiwango cha lami. Kwa hiyo, tuvute subira Serikali ikipata fedha tutakamilisha barabara hii.