Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:- Moja kati ya changamoto zinazowakabili wakulima wa tumbaku katika Wilaya ya Urambo ni madeni yanayotokana na mikopo ya pembejeo ikiwemo mbolea: (a) Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuwasaidia wakulima kuepukana na changamoto hii? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kushusha bei ya pembejeo ili kumsaidia mkulima?

Supplementary Question 1

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza, naomba uniruhusu nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jitihada kubwa ambazo amechukua kusaidia zao la tumbaku kwa kuja kila wakati katika Mkoa wa Tabora. Pili, naomba nimshukruu pia Naibu Waziri kwa jibu zuri kwamba wataagiza mbolea kwa pamoja yaani bulk procurement ili kusaidia kupunguza bei lakini kufika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, upatikanaji au uagizaji wa mbolea kwa wakati unategemea sana makisio. Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuhakikisha kwamba makisio yanatolewa mapema ili mbolea iweze kuagizwa mapema na imfikie mkulima kabla ya mwezi Agosti?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mkulima anapata moyo wa kulima kutokana na bei anayotegemea kupata. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupata wanunuzi wengi zaidi ili soko lipatikane kwa wakati na kwa ushindani ili angalau mkulima apate bei inayoweza kumsaidia kumudu maisha na kazi kubwa anayoifanya ya kulima tumbaku? Ahsante.

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwapongeze wananchi wa Urambo kwa kuchagua Mbunge jembe. Mheshimiwa Mama Sitta anawahangaikia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwagiza Mrajisi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika afike Urambo haraka iwezekanavyo akae na Mkuu wa Wilaya ili waangalie namna bora ya kuratibu utaratibu wa kukusanya madeni kwa wakulima wa tumbaku hasahasa wale wakulima ambao wanadaiwa lakini wanaendelea na kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kuhusu kufanya makisio mapema. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mama Sitta pamoja na wananchi wake kwamba Serikali tumejipanga kuhakikisha makisio ya wanunuzi yanafanyika mapema ili wakulima waweze kujua ni kiasi gani cha mbolea wanatakiwa kuagiza na mbolea iwafikie kabla ya mwezi Agosti, kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu mkakati wa kuongeza wanunuzi. Naomba niwajulishe Waheshimiwa Wabunge na wakulima wetu kwamba kwa upande wa zao la tumbaku tayari Serikali tumekaa na wanunuzi waliopo na kuangalia changamoto zao ambazo tukizitatua zitawawezesha kununua tumbaku zaidi lakini tunaendelea kuongea na nchi ambazo zina mahitaji ya tumbaku ikiwemo China na Misri. Kwa hiyo, kwa mikakati hiyo Serikali itaweza kuwasaidia wakulima wa tumbaku kupata soko la uhakika na zaidi na kwa kufanya hivyo tutakuwa tumewasiaidia kuhakikisha tumbaku yao inatakiwa na inagombaniwa na wahitaji na kufanya hivyo kutasaidia kuchochea bei kupanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Name

Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:- Moja kati ya changamoto zinazowakabili wakulima wa tumbaku katika Wilaya ya Urambo ni madeni yanayotokana na mikopo ya pembejeo ikiwemo mbolea: (a) Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuwasaidia wakulima kuepukana na changamoto hii? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kushusha bei ya pembejeo ili kumsaidia mkulima?

Supplementary Question 2

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Changamoto za zao la tumbaku zinafanana kabisa na changamoto zinazokabili zao la kahawa. Suala hili la pembejeo hasa mbolea imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa sababu wakulima wa kahama wengi wanashindwa kulima kahawa vizuri, wanashindwa kuhudumia mashamba ya kahawa kwa sababu ya bei kubwa ya mbolea. Licha kwamba Serikali inatumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea wa Pamoja lakini bado haijawa suluhu kwa wakulima wa zao la kahawa. Je, ni lini sasa Serikali itajenga viwanda vya mbolea nchini ili angalau sasa mbolea iweze kushuka bei na wakulima wa kahawa waweze kunufaika na uzalishaji uweze kuongezeka?

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumkaribisha Mheshimiwa Haonga pamoja na Wabunge wengine, leo tuna kikao cha wadau wa kahawa kinafanyika hapa Dodoma, kimeanza saa mbili na nusu. Kwa hiyo, baada ya maswali na majibu tunawakaribisha Waheshimiwa Wabunge kushiriki kikao hiki na tuweze kupata maoni yenu ili kuboresha mfumo wa ununuzi wa kahawa hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la Mheshimiwa Haonga la lini Serikali itajenga viwanda vya mbolea, majibu ya Serikali ni kwamba inaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha tunajenga viwanda vya mbolea hapa nchini ikiwemo utumiaji wa gesi asilia ambayo tumeigundua ili kutengeneza mbolea na kusaidia wakulima wetu waweze kupata mbolea hapa hapa nchini na kwa bei nafuu.

Name

Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:- Moja kati ya changamoto zinazowakabili wakulima wa tumbaku katika Wilaya ya Urambo ni madeni yanayotokana na mikopo ya pembejeo ikiwemo mbolea: (a) Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuwasaidia wakulima kuepukana na changamoto hii? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kushusha bei ya pembejeo ili kumsaidia mkulima?

Supplementary Question 3

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu na mimi niulize swali moja la nyongeza kuhusu tumbaku kwa sababu tumbaku Tabora ndio siasa yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vyama vingi vya msingi vimekufa au vimesinzia au havifanyi kazi kutokana na mfumo wa zamani uliokuwepo na hasahasa utoroshaji wa tumbaku, kukwepa madeni kupitia vyama vya IF. Sasa mfumo mzuri umewekwa na kwamba madeni yamedhibitiwa. Je, Serikali kupitia Benki ya Kilimo haiwezi kuwadhamini wanachama hawa wa vyama sinzia ili vilime tumbaku kwa mkakati wa kulipa madeni?

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Maige, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kwa ufatiliaji wake wa karibu wakulima wake wa tumbaku. Swali la Mheshimiwa Maige ni kwamba TADB inawasaidiaje wakulima kupitia vyama vya msingi. Jibu ni kwamba Serikali inaendelea kufanya jitihada kwanza ya kufufua vyama vya msingi viweze kuzingatia utawala bora (good governance) kwani kwa kipindi cha nyuma vyama vya msingi baadhi ya viongozi walikuwa siyo waadilifu kwa hiyo fedha nyingi zilikuwa zinapotea kwa njia hiyo kwa sababu walishindwa kuzisimamia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mkakati wa Serikali wa kuboresha ushirika na kuhakikisha vyama vya msingi vinakuwa na viongozi waadilifu basi tumhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa na TADB na kuangalia ni namna gani tunaweza tukaratibu jambo hili ili wakulima kupitia vyama vya msingi waweze kupata mikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Name

Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:- Moja kati ya changamoto zinazowakabili wakulima wa tumbaku katika Wilaya ya Urambo ni madeni yanayotokana na mikopo ya pembejeo ikiwemo mbolea: (a) Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuwasaidia wakulima kuepukana na changamoto hii? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kushusha bei ya pembejeo ili kumsaidia mkulima?

Supplementary Question 4

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Bado narudi kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta kuhusu tumbaku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyojibu Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye kalenda ya Bodi ya Tumbaku ili pembejeo zifike nchini mwezi Agosti na Septemba, makisio hutolewa tarehe 31 Machi, ndiyo deadline. Sasa makisio yametolewa kwa makampuni matatu ambayo yanafanya biashara hapa nchini; kampuni moja haijatoa makisio, hiyo ina maana wakulima wa Tabora, Chunya, Ruvuma, Mpanda watakosa kulima tumbaku msimu ujao. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuitisha kikao cha dhararu kati ya Bodi ya Tumbaku na Wabunge wanaolima tumbaku ili kutatua tatizo hilo?

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwambalaswa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na mimi nakubaliana na yeye kwamba kukaa na wanunuzi kufanya makisio mapema iwezekanavyo ikiwezekana mapema mwezi Machi, ni jambo la msingi kwani litasaidia wakulima wetu kujua ni kiasi gani wanahitaji kuagiza kupitia bulk procurement system.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali ni kwamba tuko tayari kukaa na huyu mnunuzi mmoja ambaye bado hajatoa makisio? Jibu ni kwamba Mheshimiwa Mwambalaswa niko tayari na baada ya hapa nitatafuta namba zao na kuwapigia simu na kuona kwa nini mpaka sasa hawajatoa makisio kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.