Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Primary Question

MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:- Usanifu wa kina wa barabara ya Isandula (Magu) – Bukwimba Station – Ngudu hadi Hungumalwa ambayo ni kilometa 74 umeshakamilika:- Je, ni lini barabara hiyo itaingizwa kwenye bajeti ili ijengwe kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na maelezo mazuri sana ya Serikali, barabara hii imekuwa na maelezo ya muda mrefu kwa maana ya kwamba kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa Awamu ya Tano kwamba barabara hiyo itatengenezwa kwa kiwango cha lami. Kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba usanifu wa kina utakamilika Mei, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mwanza. Usanifu wa kina umeshakamilika na baada ya usanifu wa kina kukamilika nilienda kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, ofisini kwake, akaniahidi kwamba ataiingiza kwenye bajeti ya mwaka huu kwa maana ya 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kuuliza, kwa maelezo haya, Barabara ya Isandula – Hungumalwa itaingizwa kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha 2019/2020?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kama ahadi inatolewa na Mheshimiwa Rais na Serikali imekiri kwamba barabara hii ni muhimu na ni kiungo kikubwa kwa Sirari, Mwanza na Shinyanga: Je, Serikali sasa kwa umuhimu huo, iko tayari barabara hii ambayo ni muhimu kuiingiza kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza unipe ruhusa nimpongeze sana Mheshimiwa Richard Ndassa, Senator huyu, amekuwa akiifuatilia sana barabara hii na ni kweli barabara hii imeahidiwa muda mrefu na ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiifuatilia sana barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu huo, tumesimamia vizuri kuhakikisha kwamba usanifu unakamilika. Tulipokea rasimu ya kwanza ya usanifu wa barabara hii ambayo angalau ime-indicate kwamba barabara hii inaweza ikawa na gharama gani. Kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Ndassa avute subira na kwa sababu jambo hili tumelishika na tumedhamiria kujenga barabara hii na sisi tunaitazama barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili amezungumza juu ya bajeti, niseme tu kwamba asiwahishe shughuli, tunaitazama vizuri barabara hii, na Mungu akijaalia tunaweza tukaja na mapendekezo ya kuijenga barabara hii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Ndassa pamoja na wananchi wa Isandula, Bukwimba, Nyambiti, Ngudu, Nyamilama, Hungumalwa (Magu), Sumve na Ngudu kwa ujumla kwamba tunaona umuhimu wa kuijenga barabara hii. Tukipata fedha na bajeti ikiruhusu tutaijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.

Name

Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:- Usanifu wa kina wa barabara ya Isandula (Magu) – Bukwimba Station – Ngudu hadi Hungumalwa ambayo ni kilometa 74 umeshakamilika:- Je, ni lini barabara hiyo itaingizwa kwenye bajeti ili ijengwe kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mara kuna tatizo kubwa sana la barabara hasa barabara ya Wanyele – Kitario. Barabara hii imekatika, hakuna mawasiliano. Barabara ile inahitaji kujengewa daraja na barabara hiyo pia ilishaua watoto zaidi ya 20:-

Je, ni lini Serikali itaweka mkakati wa kipaumbele kuhakikisha inajenga daraja na tukichukulia kwamba kipindi cha masika kinakaribia? Ahsante.

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao utaratibu wa kutenga fedha kushughulikia maeneo korofi kama hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge anayataja. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge, labda tuwasiliane baadaye kwa sababu ni eneo limekuwa mahsusi na kwa wakati huu tuone kama lipo tatizo kwa kupitia utaratibu ambao tupo nao wa kushughulikia maeneo korofi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya barabara wakati wote, tuweze kushughulikia eneo hili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ili niipate sawasawa tuweze kushughulikia eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.