Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oliver Daniel Semuguruka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:- Barabara ya Kyaka – Kasulu hadi Benako Ngara imeishia Bugene:- Je, ni lini barabara hiyo ya lami itajengwa hadi Benako?

Supplementary Question 1

MHE. OLIVER D. SEMGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, wananchi wamesubiria fidia kwa muda mrefu sana na kabla ya ujenzi wa lami, fidia huwa inatangulia. Sasa Serikali inawaambiaje wananchi wangu wanaoishi kwenye hii barabara kuanzia Nyakahanga, Nyaishozi, Nyakasindi hadi Benako Ngara?

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bugene kupitia Nkwenda – Kaisho - Mlongo ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa Karagwe, Kyerwa na Misenyi. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii muhimu kwa uchumi wa Wilaya hizi na Taifa kwa ujumla.

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) : Mheshimiwa Naibu Spika, ni utaratibu wa Serikali kulipa fidia kwanza kabla ya kuanza ujenzi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wa maeneo haya ambapo mradi utapita watalipwa fidia zao kabla ujenzi haujaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia mambo mbalimbali ya maendeleo katika eneo lake lakini pia niwapongeze wananchi kwa kupisha mradi; kwa maana hiyo kwamba kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa ajili ya maendeleo yetu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, amezungumza juu ya barabara hii ambayo inakwenda Mrushaka – Mlongo kilometa 125. Mimi nimetembelea eneo hili, ni eneo muhimu sana sasa kuunganishwa kwa sababu ni sera ya Serikali kuunganisha nchi yetu na nchi za jirani. Barabara hii Mheshimiwa Mbunge anaitaja inatuunganisha sisi Tanzania na Uganda. Kwa hiyo, tunayo mipango ya kuijenga kwa kiwango cha lami lakini namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, asiwahishe shughuli na ikiwezekana tunaweza kuteta ili ajue mpango wa Serikali juu ya kuijenga barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tunaendelea kuihudumia hii barabara na maeneo ambayo ni korofi. Kwa mfano, ile milima, maeneo ya Rwabunuka kuna mipangilio ya milima ambayo ni mikali sana. Tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza kushughulikia maeneo korofi wakati tunajiandaa kuiboresha hii barabara katika kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa maeneo haya wavute subira, tumejipanga vizuri na tunafahamu maeneo haya ni muhimu sana kwa uchumi. Tutashughulikia barabara hii muhimu.

Name

Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Primary Question

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:- Barabara ya Kyaka – Kasulu hadi Benako Ngara imeishia Bugene:- Je, ni lini barabara hiyo ya lami itajengwa hadi Benako?

Supplementary Question 2

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu linahusu barabara ya Kidatu – Ifakara; barabara yenye urefu wa kilometa 69.9. Mradi wake wenye thamani ya shilingi bilioni 109 ambao unafadhiliwa na DFID na European Union.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ilifunguliwa tarehe 5 Mei, 2018. Wakati inafunguliwa vifaa viliwekwa vingi na Mheshimiwa Rais lakini Mheshimiwa Rais alipoondoka na Mkandarasi akaondoa vifaa vyake. (Kicheko)

Je, Serikali inatuambia nini kuhusu barabara hii? Ina maana ndiyo tumepigwa changa la macho sisi pamoja na Mheshimiwa Rais?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) : Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mlinga kwa sababu mara zote amekuwa ukifuatilia sana ujenzi wa barabara hii. Niseme tu kwamba tunawaambia nini wananchi na Watanzania kwa ujumla kuhusu barabara hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tulivyoanza ujenzi wa barabara hii kulikuwa na changamoto kuhusu vifaa na material kwenye ujenzi wa barabara hii. Hii ilitokana na mabadiliko ya Sheria ya VAT, kwa hiyo, tulichelewa kidogo. Niwaambie wananchi na Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya changamoto hizi kutatuliwa, sasa Mkandarasi atakwenda kwa kasi kubwa na wananchi wategemee kupata barabara ya lami, bora na itakayowahudumia wananchi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.