Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari wa kutibu magonjwa mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula?

Supplementary Question 1

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mimi nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali langu la kwanza; nataka tu kujua katika ile Hospitali ya Mkoa ya Ligula kuna Madaktari Bingwa wangapi na wanatibu magonjwa gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa hospitali ile ni ya mkoa, maana yake inahudumia mkoa mzima na ni ya rufaa na sisi hatuna hospitali ya kanda, Kanda ya Kusini, bado haijaanza kufanya kazi.

Katika jibu lake la msingi amesema Madaktari wa kufanya upasuaji wa kawaida na mifupa bado wapo masomoni wanasoma na ukizingatia kuna ajali nyingi zinazotokea, anawaambia nini vijana, wananchi wa Mtwara ambao wanapata matatizo, wanataka tiba ya upasuaji wa kawaida na mifupa; wasubiri mpaka mwaka 2021?

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza Malapo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mtwara, Ligula tuna Daktari Bingwa mmoja katika Magonjwa ya Akinamama, lakini tunatambua kwamba tunahitaji huduma za Madaktari Bingwa katika hospitali zetu za rufaa za mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tulitangaza nafasi hizi Madaktari hawa hawako mtaani na ndiyo maana sisi kama Serikali tumewekeza katika kuhakikisha kwamba tunatoa mafunzo kwa Madaktari Bingwa wengi iwezekanavyo na tumeendelea sasa hata kufanya mabadiliko ya mifumo ya kufundisha Madaktari ili tuweze kupata Madaktari Bingwa wengi kwa utaratibu wa fellowship ambao na sisi ndani ya Wizara tunakwenda nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwa lengo la kutibu changamoto ambazo tunazo Serikali imekuwa inafanya kambi mbalimbali za kutoa Madaktari Bingwa kutoka sehemu moja kwenda kwenye sehemu mbalimbali na hii tumekuwa tunafanya kwa kushirikiana na Bima ya Afya na kwenda katika kambi katika mikoa mbalimbali kuhakikisha kwamba zile huduma za dharura ambazo zinahitaji upasuaji nazo zinaweza zikafanyiwa kazi wakati tunasubiria kujenga uwezo wa kuwa na Madaktari Bingwa wengi zaidi.