Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI) aliuliza:- Kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na kuongeza uwekezaji kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa vikwazo vinavyoathiri dhana hiyo vinaondolewa?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii ya Uwekezaji kwa majibu mazuri na ya kina. Pamoja na majibu haya nina maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza; kwa kuwa Watanzania wana hamu kubwa sana ya kuingia kwenye uchumi wa viwanda kama ambavyo kauli ya Mheshimiwa Rais ambayo siku zote amekuwa akiisema na kwa kuwa Wizara hii iko chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nini kauli ya Serikali ya kuleta mabadiliko ya haraka na ghafla yaani radical change yatakayowezesha kutekeleza mapendekezo ya Blueprint ambayo amezungumza hapa na mikakati mingine ya kuharakisha uwekezaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wako baadhi ya wawekezaji wa ndani na nje ambao wamekuwa wakizunguka ofisi baada ya ofisi nyingine wakitafuta vibali mbalimbali vya uwekezaji, kitu ambacho kimekuwa kikichafua sana nchi hii kwa sababu wanaposhindwa kupata vibali hivi kwa muda wanahama kwenda nchi zingine na hii inakuwa haileti dalili njema kwa nchi yetu. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kipindi hiki cha Bunge la Bajeti awaite wawekezaji wote ambao wana kero mbalimbali, akutane nao pamoja na Mawaziri wengine wote ili kuhakikisha kwamba matatizo yao yanatatuliwa mara moja? Ahsante.

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chegeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kuhusiana na tunatoa kauli gani ya kuleta mabadiliko ya haraka au kama alivyoeleza mwenyewe radical change, nipende kusema kwamba ni kweli ili tuhakikishe kwamba tunapata faida ya uwekezaji na biashara nchini, ni lazima mabadiliko ya kina yaweze kufanyika. Tayari kama nilivyoeleza kwenye majibu ya msingi Serikali imeanza kuchukua hatua kupitia maboresho mbalimbali na kama alivyoeleza mwenyewe mpango mzuri wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, tumeandaa pia mpango jumuishi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango kazi huu wa kuboresha mazingira ya biashara. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango huu utatekelezwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mpango kazi huo jumuishi tumeeleza kabisa ni masuala gani ambayo yanatakiwa kufayiwa kazi na Wizara ipi pamoja na taasisi zipi za kisekta na tutaendelea kuwafuatilia pia kwa mujibu wa road map ya utekelezaji wa mpango huo kwa namna tulivyojipangia. Pia tutaleta mpango huo kazi tutakapokuwa tayari ili na Waheshimiwa Wabunge waweze kuuona na kuweza kufuatilia na kuweza kujua ni hatua gani tumefikia katika utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili kama nitakuwa tayari kufanya kikao katika kipindi hiki cha Bunge kuwaita wawekezaji wote wenye kero mbalimbali. Kwanza nipende kusema ni ushauri mzuri, lakini la pili tayari tumeanza, nimejigawia vipaumbele, moja tumeanza na mikoa mbalimbali na tunaendelea kufanya hivyo kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa.

Pili, kwa kushirikiana na Mawaziri mbalimbali wa kisekta tutaendelea kufanya vikao mbalimbali vya kisekta kwa wawekezaji na wafanyabiashara ili kuhakikisha kwamba tunatatua kero zao mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Mbunge ni shuhuda tulipoenda Rungwe kupitia kampuni ile ya Rungwe Avocado pamoja na bwana Robert Clowes ambaye tulienda kuangalia na kutatua mgogoro ule kwenye sekta ile ya kilimo cha maparachichi.

Nimshukuru sana kwa ushirikiano ambao aliutoa kipindi hicho na naamini mgogoro ule sasa utafika sehemu nzuri na utaweza kumalizika. Pia nimhakikishie na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote na naomba pia ushirikiano wao wa dhati, endapo kuna mgogoro maalum kwa mwekezaji ambaye anamfahamu au katika Jimbo lake analoliongoza au mkoa wake, basi wasisite kunipa taarifa kwa sababu nimeteuliwa kwa kazi hiyo maalum na niko tayari kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, pamoja na mikoa, pamoja na sekta mbalimbali, ili kuweza kuhakikisha kwamba taswira yetu kama nchi katika uwekezaji tunaendelea kuikuza, wiki ijayo kuanzia tarehe 17 nitakuwa na kikao na wawekezaji wote wa kichina na tutaendelea kufanya hivyo na wawekezaji wa Uturuki, wa Marekani, Uingereza na nchi zingine kwa mujibu wa viwango vile vya nchi 10 zinazoongoza katika kuvutia mitaji nchini kwetu, lakini tutahakikisha pia na nchi zingine tutazingatia. Kwa hiyo nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, lakini nitaomba ushirikiano wa Waheshimiwa Wabunge wa dhati. Ahsante.