Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaunga mkono tamko la Kilimo ndiyo Uti wa Mgongo wa Taifa kwa vitendo?

Supplementary Question 1

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la MKUKUTA na Ilani ya Chama cha Mapinduzi sekta ya kilimo ilikuwa ikue kwa asilimia 8 ndani ya miaka 10 lakini uhalisia kuanzia mwaka 2011 na 2015 sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 3.4. Ndani ya miaka ya Awamu ya Tano katika miaka yake mitatu ya bajeti sekta ya kilimo imekua kwa wastani wa asilimia 1.9. Uhalisia unajionesha kwenye bajeti zake, bajeti ya mwaka 2016/ 2017…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016/2017 tulitenga shilingi bilioni 101 katika sekta ya kilimo lakini fedha iliyotoka ilikuwa ni shilingi bilioni 3 peke yake. Pia mwaka 2017/2018 tulitenga shilingi bilioni 150 ikatoka shilingi bilioni 24. Swali, hii ndiyo tafsiri ya Kilimo ni Uti wa Mgongo katika Taifa letu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wote tunajua kwamba Watanzania wengi wanaohitimu vyuo vikuu katika Taifa hili ni 800,000 lakini watu ambao wanaajiriwa kwenye sekta rasmi karibu watu 20,000 tu ambapo 780,000 wanakwenda kuajiriwa kwenye sekta ya kilimo. Hata hivyo, sekta ya kilimo kumekuwa na tatizo la uwekezaji, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wahitimu hawa wanapewa mikopo ili wajiajiri na wainue maisha yao pamoja na kuchangia pato la Taifa?

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwakajoka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mheshimiwa Mwakajoka anasema kwamba sekta ya kilimo imekua ikikua kwa asilimia ndogo kinyume na matarajio. Pamoja na mipango mizuri ya Serikali katika kukuza sekta ya kilimo nchini lakini kuna mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri productivity ya kilimo nchini. Hata hivyo, Serikali inayo mipango madhubuti kupitia Mpango wa Kilimo wa ASDP II kama nilivyotaja kwenye majibu yangu ya msingi, kuhakikisha tunatumia ardhi vizuri kwa kilimo, tunazingatia matumizi mazuri ya utumiaji wa maji ili kwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji yaani drip irrigation pamoja na mikakati mingine ambayo tumeiweka ndani ya Serikali kupitia Mpango huu wa Maendeleo ya Kilimo wa ASDP II.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Mwakajoka ni kwamba tuna vijana wengi ambao wanahitimu kwenye vyuo vikuu lakini kuna changamoto ya ajira; na wanaoenda kwenye kuajiriwa kwenye sekta ya kilimo ni wachache, asilimia ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali katika hili ni kuhakikisha tunaleta mageuzi ya kilimo na kufungamanisha kilimo na viwanda. Kama unavyojua Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge, Serikali inaendelea kufanya jitihada hizi kuangalia kilimo kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, asilimia 65 ya malighafi za viwandani zinategemea mazao yetu ya kilimo. Sasa mkakati wa Serikali ni kuongeza hizi asilimia ili tuweze kufungamanisha uchumi wa viwanda na kilimo.