Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Primary Question

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:- Tatizo la ufisadi na wizi nchini limeachwa likaendelea kwa muda mrefu sana:- (a) Je, ni kwa nini TAKUKURU wasiachiwe kuendesha mashauri makubwa ya ufisadi na wizi Mahakamani moja kwa moja bila ya kuomba kibali cha DPP? (b) Je, DPP amezuia majalada mangapi ya uchunguzi kufikishwa Mahakamani na ni kwa nini? (c) Je, Serikali haioni kwamba DPP anaweza kutumika kulinda maslahi ya viongozi ambao kwa kiwango kikubwa wanajihusisha na vitendo vya wizi na ufisadi pamoja na matumizi mabaya ya madaraka?

Supplementary Question 1

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na maelezo mazuri ya Naibu Waziri, napenda niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, swali langu la (b) linauliza ni kesi ngapi DPP amezuia majalada hayo ya watuhumiwa, ndiyo msingi wa swali. Kwa maoni yangu swali hilo naomba lijibiwe sasa kwa sababu halikujibiwa katika maelezo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Halmashauri ya Mji wa Kasulu tuliibiwa fedha takribani shilingi bilioni 5.9 ingawa baadaye nasikia uhakiki ulibainisha kwamba takribani shilingi bilioni 2 zilikuwa zimeibiwa. Washtakiwa wale walisimamishwa kazi, wakahojiwa na TAKUKURU lakini cha ajabu ni kwamba watuhumiwa hawa hawajafikishwa Mahakamani eti kwa sababu DPP hajatoa kibali. Ni kitu gani hicho?

Name

Dr. Mary Machuche Mwanjelwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa kaka yangu Nsanzugwanko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana masuala ya watumishi wa Jimbo lake la Kasulu ambao wanategemewa kutoa huduma kwa wapiga kura wake ambao pia ni wapiga kura wake. Jambo la kwanza, kwenye majibu yangu ya msingi hapa nimesema DPP ni Ofisi inayojitegemea na ipo kwa mujibu wa Katiba. Kwa maana hiyo, siyo kwanza amezuia isipokuwa majalada haya yamechelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, Kasulu siyo kwamba kulikuwa na ubadhirifu wa shilingi bilioni
5.9 bali ni ubadhirifu wa shilingi bilioni 1.6 na kulikuwa na kesi 12. Katika kesi hizo 12 aliyekuwa DT wa Halmashauri hiyo ya Kasulu anahusika kwenye hiyo kesi moja lakini kesi sita zenyewe zilifutwa kwa sababu zilikosa ushahidi na kesi tano zinasuasua kwa sababu kuna mashahidi wengine wanaogopa kutoa vielelezo. Kwa hiyo, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu na kuwaasa Watanzania wote kwamba wawe na kiu ya kutoa ushirikiano na Taasisi yetu ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa sababu rushwa ni adui wa haki. Nakushukuru.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee kidogo maelezo kwa kuelezea mamlaka ya DPP kwa mujibu wa Katiba ambapo ni Ibara ya 59B(2) ambayo inampa Mkurugenzi wa Mashtaka uwezo wa kufungua, kuendesha na kusimamia mashtaka yote nchini. Kwa hiyo, ana mamlaka ya kufungua au kuendesha lakini kama haendeshi anasimamia mashtaka yote yanayohusu makosa ya jinai nchini. Hata Ibara ndogo ya (3) inaeleza vizuri kwamba mamlaka hayo anaweza kuyatekeleza yeye mwenyewe au mtu mwingine kwa maelekezo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la DPP ama anazuia au hazuii ma-file kwenda kwenye mashtaka, Mheshimiwa DPP hazuii bali anatoa kibali au hatoi kibali. Pia hafanyi hivihivi, anachopaswa kufanya DPP kwa sababu yeye siyo Mamlaka ya Uchunguzi bali ni mamlaka ya mashtaka, kwa hiyo ni lazima apime ushahidi ulioletwa kutoka kwenye Mamlaka ya Uchunguzi kama unajitosheleza kuweza kufungua mashtaka. Kama anaona kwamba ushahidi ulioletwa kutoka kwenye mamlaka ya uchunguzi haujitoshelezi kufungua mashtaka hatatoa kibali cha kufungua mashtaka, mpaka pale atakapojiridhisha kwamba ushahidi unajitosheleza. Ahsante.