Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Primary Question

MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:- Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea – Ruangwa - Nanganga utaanza kufanyika kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ya kutafutwa pesa kwa ajili ya barabara hii ni ahadi ya muda mrefu sana, lakini pia naomba niweke kumbukumbu vizuri kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, zoezi la kufanyia upembuzi yakinifu barabara hii lilikamilika mwaka 2015 wakati mimi naingia kuwa Mbunge na siyo 2008. Sasa naomba kujua, nini dhamira ya Serikali juu ya kutekeleza ahadi yake ya muda mrefu kuhakikisha fedha ndani ya mwaka huu wa bajeti inapatikana ili barabara hii iweze kufanyiwa kazi kwa kiwango cha lami? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ambalo naomba nipate majibu, barabara hii kwa mujibu wa nyaraka nilizonazo, mwanzo kabisa wakati inafanyiwa upembuzi yakinifu ilikuwa inasomeka Masasi – Nachingwea – Nanganga, lakini baadaye ikaja kuanza kufanyiwa kazi barabara ya kutoka Nanganga – Ruangwa – Nachingwea. Sasa hivi majibu yanayotoka, kuna kipande cha kilometa 45 cha kutoka Nachingwea kwenda Nanganga hakisemwi na hakionekani katika maelezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua msimamo wa Wizara juu ya kioande hili cha Nachingwea kwenda Nanganga ambacho ni kilometa 44.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa umakini na ufuatiliaji wa maendeleo ya Nachingwea lakini siyo Nachingwea peke yake, bali pia maeneo ambayo kimsingi yanaunganika na Wilaya hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kweli usanifu ulikamilika kipindi cha nyuma, lakini kwa jibu ambalo nimelitoa sasa hivi, kwa yale maandalizi ya kuanza ujenzi huwa kuna kitu ambacho tunaita mapitio. Tunafanya review ili tuweze kutangaza ujenzi wa barabara. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Masala kwamba records ambazo nimeziweka hapa kwa maana ya review ilikuwa ni maandalizi sasa ya kuanza ujenzi. Hivi tulikuwa tunafanya mawasiliano na wenzetu wa upande wa Wizara ya Fedha, fedha zikipatikana tunaanza kujenga barabara hii. Kwa hiyo, nimtoe hofu yeye pamoja na wananchi wa Nachingwea na majirani zake, ni kwamba harakati za kufanya ujenzi wa barabara hii tumezifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la (b); kutokana na review ambayo nimeisema hapa imefanyika ili tuanze ujenzi, haimaanishi kipande hiki cha Nachingwea - Nanganga kwamba tunakiacha. Hiki ni vipambele tu kutokana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Masala kipande cha Nachingwea - Nanganga na chenyewe kiko kwenye mpango na vile vile tuwasiliane baadaye, atakuja kuona kwenye mpango mkakati wetu baada ya review kwamba tumejipanga vipi kuanza kujenga kwa kiwango cha lami. Kwa maana hiyo ni kwamba tukipata fedha tunaanza ujenzi wa barabara hizi muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Masala ajue kwamba wakati huo tunajiandaa, tunaendelea kushughulikia maeneo ambayo ni korofi, tunaendelea kushughulikia maeneo ambayo ni maalum, tunaendelea kujenga madaraja. Labda kwa manufaa ya wananchi wa Nachingwea niseme kwamba tumeendelea kukamilisha daraja la Lukuledi ambapo barabara niliyoijibia itapita ili tuwaungenishe vizuri wananchi hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tunaendelea kujenga maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Lindi, madaraja ya kule Chumo, kuna daraja Mlowoka, Mtakuja na Nanjilinji. Hii ina maana kwamba maeneo ambayo tumeyatengea fedha za kutosha na maeneo ambayo wananchi walikuwa wanapata usumbufu kupita katika maeneo haya tumeyazingatia. Kwa hiyo, wananchi wa Ruangwa, Nachingwea na maeneo yote ya Lindi, ni kwamba tumejipanga ili tuwahudumie vizuri.

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:- Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea – Ruangwa - Nanganga utaanza kufanyika kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze sana Serikali kwa kuunganisha barabara nyingi za nchi yetu kutoka Wilayani na Makao Makuu ya Mikoa yetu. Sambamba na hilo napenda niulize swali langu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bungu - Nyamisati inaunganisha Wilaya ya Mafia na Kibiti. Sasa barabara hii iko chini ya kilometa 50 na kama mnavyojua historia, Mafia ni Kisiwa, wanatumia usafiri mmoja tu ambao ni ndege. Je, ni lini barabara hii itaunganishwa kwa kiwango cha lami ili kuwasaidia wananchi wa Mafia?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kikwete kwa namna anavyofuatilia maendeleo ya sehemu mbalimbali. Kwa hiyo mara nyingi nimemsikia akizungumza juu ya Lindi, leo anazungumza juu ya Pwani, kwa hiyo nampongeza sana. Hata maeneo mengine, nimemsikia pia akiwasemea walimu kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la Nyamisati ni eneo muhimu sana. Nifahamishe tu Bunge lako pamoja na wananchi kwa ujumla, ni kwamba tunatengeneza gati katika eneo hili la Nyamisati kwa lengo la kuhudumia kivuko ambacho pia tumeanza hatua za manunuzi, kivuko ambacho kitatuvusha kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni kule Mafia. Tunaendelea vizuri. Kwa hiyo, niwahakikishie tu wananchi hawa wa Nyamisati na wananchi wa Pwani na Watanzania kwa ujumla kwamba tutakuwa na kivuko ambacho kitatusaidia kupunguza usumbufu uliokuwepo kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotengeneza kivuko pamoja na gati hii lazima ule mnyororo wa usafiri tuuweke vizuri. Ndiyo maana nami nimetembelea eneo hili kilometa kama 48 hivi kutoka Bungu kwenda Nyamisati ili kuhakikisha kwanza barabara tunaiweka katika ubora unaohitajika, lakini pia mipango yetu ipo ili tuje kuweka lami barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii muhimu itatusaidia pia kusafirisha mizigo mingi kutoka Nyamisati kwenda hata sehemu hii ambayo tunajenga umeme (Stiegler’s Gorge) kwa sababu barabara hii kutoka Kibiti kwenda Stiegler’s Gorge tumeiboresha na tunaamini kwamba gati hii ikiboreshwa kutakuwa na vyombo ambavyo vitabeba mizigo mizito kuja Nyamisati ambavyo vinaweza vikahitajika kwenda kwenye maeneo ya mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatumaini kwamba barabara hii kuiboresha pamoja na kuiweka kiwango cha lami itatusaidia sana kubeba mizigo na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsnate sana.