Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. PASCHAL Y. HAONGA aliuliza:- Kuna watumishi katika Halmashauri nyingi za Wilaya nchini walikuwa wanachama wa PSPF wamestaafu zaidi ya mwaka mmoja na hawajalipwa fedha zao za kiiunua mgongo (pension) na kwa sasa wanaishi maisha ya taabu na mateso makali:- (a) Je, ni lini sasa Serikali itawalipa wastaafu hawa? (b) Inasemekana kwamba Serikali imetumia vibaya fedha za PSPF ikiwa ni pamoja na kukopesha baadhi ya watu na taasisi: Je, Serikali haioni kwamba hii inaweza kuwa sababu mojawapo ya kucheleweshwa mafao kwa wastaafu? (c) Fedha za kiinua mgongo ni mali ya Mtumishi anayestaafu: Je, kwa nini Mifuko ya Pensheni isiwakopeshe wastaafu watarajiwa angalau 40% ya fedha hizo bila riba pale inapobaki miaka 10 kabla ya kustaafu?

Supplementary Question 1

MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa mtumishi anapokuwa anaajiriwa, mara ya kwanza na kwenye salary slip yake inaonesha muda atakaostaafu, hivyo inakuwa siyo suala ambalo ni la ghafla, lakini Serikali imekuwa ikichelewa sana kuwalipa watumishi hawa: Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka inapokuwa wamesababisha ucheleweshwaji wa mafao kwa watumishi wa Umma inataikiwa walipe kwa riba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Halmashauri ya Mbozi kuna watumishi 35 wamestaafu toka Septemba, 2018, hadi sasa hawajalipwa fedha zao na wanaidai Serikali na wanaishi maisha magumu sana: Je, ni lini sasa Serikali itaacha kuwatesa watumishi hawa wanaoishi maisha ya taabu sana kwa sababu ya ucheleweshaji wa fedha zao?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Haonga amezungumza kuhusu ucheleweshwaji wa ulipaji wa mafao. Kwa mujibu wa sheria ambayo tumeipitisha hapa ndani Bungeni hivi sasa, inautaka mfuko kulipa mafao ya mstaafu ndani ya siku 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zilikuwepo changamoto nyingi hapo awali, nyingi sio kwambwa zinasababishwa na mfuko husika lakini pia wale wastaafu katika namna moja ama nyingine katika uandaaji wa nyaraka na kufuatilia taarifa zao imekuwa pia ikileta changamoto. Baada ya kuunganisha mifuko hii na kwa kutumia sheria mpya, hivi sasa PSSF wameweka utaratibu na motto wao ni kwamba wanalipa mafao tangu jana.

Mheshimimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi sasa zoezi la ulipaji wa mafao kwa wastaafu linafanyika kwa kiwango kikubwa sana na kwa idadi ambayo nimesema tayari imeshalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu watumishi katika Jimbo lake la Mbozi, kwa sababu hii inakwenda case by case, nisilisemee kwa ujumla, lakini nichukue tu fursa hii kumwambia Mheshimiwa Haonga kwamba ofisi yetu iko wazi, kama kuna madai ya watumishi ambao mpaka hivi sasa bado hawajalipwa mafao yao, basi anaweza kuyasilisha ili sisi Ofisi ya Waziri Mkuu tuweze kufuatilia mkoa husika tujue changamoto ni nini na baada ya hapo tuweze kutatua changamoto yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kulipa mafao yao kwa wakati kabisa ili kuwafanya watumishi hawa waishi katika maisha ya amani.