Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Martin Alexander Mtonda Msuha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Primary Question

MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:- Hivi karibuni Serikali ilibadilisha mfumo wa ununuzi na uuzaji kahawa kwamba ni lazima kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi:- Je, ni Vyama vingapi vya Msingi vya Ushirika (AMCOs) vimeundwa Wilayani Mbinga kufuatia kubadilishwa kwa mfumo huo?

Supplementary Question 1

MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu ya Serikali lakini pia
nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa kupeleka mnada wa kahawa Wilayani Mbinga kuanzia msimu ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kumetokea changamoto kadhaa katika mfumo huu mpya ikiwemo kuchelewesha malipo kwa wakulima, wakulima kulipwa bei tofauti lakini pia kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya watendaji wa AMCOS. Je, Serikali imejipangaje kutatua kero hizi kwenye msimu ujao wa kahawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwepo mabadiliko ya bei msimu kwa msimu, je, Serikali inajipangaje ama ina mpango gani wa kuanzisha Mfuko wa Kuimarisha Bei ya Kahawa (Price Stabilization Fund) ili kuondokana na tatizo hili la mabadiliko ya mara kwa mara ya bei ya kahawa? Ahsante sana.

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martin Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita hasa ya kuchelewesha malipo kwa wakulima pamoja na wakulima kulipwa bei tofauti na bei ambayo ilitangazwa na Serikali ama iliyouzwa mnadani. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Msuha kwa ufuatiliaji wa wakulima wa kahawa nchi nzima kupitia wakulima hawa wa Mbinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujibu swali lake napenda kusema kwamba madai yake ni ya kweli, mimi mwenyewe nilifika katika Mkoa wa Ruvuma na tuliongea na wakulima walithibitisha hilo. Kilichotokea mwaka jana kama unavyokumbuka, ndiyo ulikuwa mwaka wa kwanza kutumia mfumo huu wakulima wenyewe kwenda kuuza kahawa yao Moshi kupitia vyama vyao vya ushirika. Kwa hiyo, kahawa ile walivyokoboa na kuipeleka mnadani ilichelewa sana kuuzika kutokana na anguko kubwa la bei katika soko la dunia na katika soko la mnada hapa nchini. Kwa sababu walienda kuuza wenyewe, ilikuwa hamna namna nyingine lazima wasubiri mpaka kahawa iuzwe ndipo walipwe. Hata hivyo, kadiri watakavyoendelea kuuza kwenye mnada ndivyo hivyo wakulima wataweza kulipwa pesa zao kwa kuzingatia na mauzo kwenye mnada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili amesema kwamba tumejipangaje. Mwaka huu tumejipanga kupeleka minada hiyo katika kanda zao lakini pili ni kuruhusu wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika kama wakipata soko la moja kwa moja kuuza nje ya nchi tutatoa vibali hivyo ili wauze moja kwa moja. Kwa taarifa tu ni kwamba mpaka sasa tumeshapata wanunuzi ambao wapo tayari kuingia mkataba na Serikali kwa ajili ya kuuza kahawa hiyo kupitia mnada wa moja kwa moja (direct export market) kwa ajili ya kahawa hiyo na tayari mahitaji ya wanunuzi wale ni makubwa kuliko uzalishaji uliopo nchini.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:- Hivi karibuni Serikali ilibadilisha mfumo wa ununuzi na uuzaji kahawa kwamba ni lazima kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi:- Je, ni Vyama vingapi vya Msingi vya Ushirika (AMCOs) vimeundwa Wilayani Mbinga kufuatia kubadilishwa kwa mfumo huo?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Zao la kahawa lina matatizo makubwa sana nchi nzima na matatizo yanayolikabili ni pamoja na pembejeo na bei yenyewe ya kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi hapa Dodoma tulikuwa na kikao cha wadau na Mheshimiwa Waziri uliongea vizuri sana, uzalishaji unapungua kila mara na maeneo mengine kwa mfano kwangu kule Rombo wanaamua kung’oa kahawa ile ya zamani wanapanda ndizi na kabichi. Je, ni mkakati gani ambao Serikali inao kuwasaidia wakulima ili kunyanyua kiwango cha uzalishaji wa kahawa yetu ambayo katika soko la dunia inasemekana ni kahawa tamu sana ukilinganisha na kahawa kutoka maeneo mengine?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selasini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, anataka kujua Serikali tuna mkakati gani wa kuongeza tija na uzalishaji wa zao la kahawa ili kuvutia bei nzuri kwa wakulima. Mkakati wa kwanza ni kwamba sasa hivi tupo kwenye mazungumzo ya makampuni ambayo yanatengeneza mbolea kama OCP kutoka Morocco ili kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea hapa nchini ili kurahisisha upatikanaji wa mbolea na pembejeo zingine kwa ajili ya kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kupitia Shirika letu la Maendeleo la Taifa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo, tunawawezesha wakulima kwa kuwapa mikopo na Serikali inadhamini zaidi ya asilimia 80 ya matrekta na nyenzo zingine za kilimo kwa ajili ya kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima. Lengo ni kuongeza tija na uzalishaji, kama alivyosema tuna miaka zaidi ya kumi hatujaweza kuongeza uzalishaji wa kahawa.

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:- Hivi karibuni Serikali ilibadilisha mfumo wa ununuzi na uuzaji kahawa kwamba ni lazima kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi:- Je, ni Vyama vingapi vya Msingi vya Ushirika (AMCOs) vimeundwa Wilayani Mbinga kufuatia kubadilishwa kwa mfumo huo?

Supplementary Question 3

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Pamoja na kupongeza ziara nzuri ya Mheshimiwa Rais Magufuli kwa baadhi ya Mikoa ya Kusini ambayo inalima korosho, Serikali itakubaliana na mimi kama ilivyotokea kwenye kahawa mabadiliko ya mfumo wa ununuzi wa korosho yameathiri mapato ya Halmashauri ambazo zilikuwa zinategemea ushuru wa korosho. Halmashauri nyingi kwa asilimia 70 mpaka 80 zilikuwa zinategemea mapato haya. Serikali ipo tayari kufanya tathmini ya madhara yatakayojitokeza baada ya maagizo ya Mheshimiwa Rais kwamba pesa hizi zisidaiwe na hivyo kuangalia namna ya kufidia ili hizi Halmashauri zisiathirike zaidi?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nape, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la msingi anasema kwamba, je, Serikali ipo tayari kufanya tathmini ya athari zilizopatikana kwa kushuka mapato ya Serikali ya Halmashauri? Kwanza nichukue nafasi hii kusema kwamba Serikali haijabadili mfumo wa ununuzi wa korosho hapa nchi. Kama mnavyofahamu tuliingia kwenye mfumo huo baada ya wakulima wenyewe kukataa kuuza katika mnada uliokuwa halali kwa wanunuzi wale kutokana na bei ambayo haikuwavutia zaidi ya minada mitatu minne. Kama Serikali tusingeweza kuangalia hali ile iendelee ndiyo maana tuli- intervene ili kuhakikisha wakulima hawa wanapata bei nzuri wanayostahili. Wakati ule tunaingia tulikuwa tunafahamu bei ni ndogo lakini tulienda kuwalipa wakulima bei ya Sh.3,300 ambayo ilikuwa huwezi kuipata mahali popote duniani zaidi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali lake la kama tupo tayari kufanya tathmini, napenda kusema kwamba tupo tayari na tumeshaanza kufanya tathmini hiyo lakini mapato yale ya Halmashauri ni ya Serikali na iliyolipa ni Serikali, kwa hiyo, Serikali haiwezi kumlipa Serikali mwenzie. Msimu ujao tutajipanga vizuri na mfumo utakuwa kama ulivyokuwa, mapato ya Halmashauri watayapata kupitia mfumo utakaokuwepo.

Name

Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Primary Question

MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:- Hivi karibuni Serikali ilibadilisha mfumo wa ununuzi na uuzaji kahawa kwamba ni lazima kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi:- Je, ni Vyama vingapi vya Msingi vya Ushirika (AMCOs) vimeundwa Wilayani Mbinga kufuatia kubadilishwa kwa mfumo huo?

Supplementary Question 4

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kutokana na swali la msingi, niipongeze Wizara ya Kilimo na Waziri Mkuu kwa kazi waliyoifanya Kagera. Wakulima wa kahawa Mkoa wa Kagera wa Muleba, Misenyi na Bukoba Vijijini kupitia KDCU na KCU mpaka leo kuna ambao hawajalipwa malipo yao ya kupeleka kahawa KDCU na KCU. La pili, bado kuna wakulima ndani wana kahawa…

MWENYEKITI: Swali ni moja tu Mheshimiwa.

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe tamko kwa wale wakulima ambao hawajalipwa haki yao, ni lini watalipwa haki yao?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Alhaj Abdallah Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna baadhi ya wakulima waliouza kupitia Vyama vya Ushirika vya KCU na KDCU hawajalipwa malipo yao mpaka sasa hata wale wa Tarime Vijijini katika Mkoa wa Musoma. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, walioenda kuuza kahawa ile ni wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika kwenye mnada wa Moshi, kwa hiyo watalipwa baada ya kahawa yao kuuzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea katika msimu wa mwaka jana kahawa ilianguka sana sokoni kwa hiyo wakulima wale waliona siyo busara kuuza kwa bei ya chini kuliko gharama za uzalishaji walizoingia. Pia, kahawa hii ambayo ikikobolewa inatoka madaraja zaidi ya matano, wakati mwingine inachelewa kwa sababu imeuzwa daraja moja, madaraja mengine hayajauzwa. Kwa hiyo, wanasubiri ili kuuza kahawa yote na kwenda kuwalipa wakulima na wanachama wao. Kwa hiyo, naomba waendelee kuwa na subira kwa sababu kahawa hiyo wameuza wenyewe kila wanapouza watalipwa.

Name

Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Primary Question

MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:- Hivi karibuni Serikali ilibadilisha mfumo wa ununuzi na uuzaji kahawa kwamba ni lazima kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi:- Je, ni Vyama vingapi vya Msingi vya Ushirika (AMCOs) vimeundwa Wilayani Mbinga kufuatia kubadilishwa kwa mfumo huo?

Supplementary Question 5

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na utaratibu wa hizi AMCOS zetu kuajiri ama kutokuwa na vigezo vya wale ambao wanaajiriwa kwamba hawawekewi elimu ni kiwango gani na kwa kiasi kikubwa wahasibu ndiyo wanakuwa ni watu pekee wenye elimu kiasi ambacho kinapeleka kufanya hujuma nyingi sana kwenye hizi AMCOS. Naomba kujua Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wale ambao wanafanyia kazi hizi AMCOS wanawekewa vigezo vya kielimu ili wakulima wasiweze kuibiwa kama ilivyo hivi sasa?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Serikali tulishaanza mpango huo tangu msimu uliopita kwa mfano Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru tulianza kuajiri Wahasibu wenye degree moja na kuendelea kwa ajili ya kuongoza vile vyama vya ushirika. Utaratibu ule tutaendeleza nchi nzima kupitia vyama vyote vya ushirika ili tupate Wahasibu wenye weledi ili kuweza kuwahudumia wakulima wetu.