Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Primary Question

MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:- Manispaa ya Tabora ipo kwenye mradi mkubwa wa maji toka Ziwa Victoria na Bwawa kubwa la Igombe linalotumika kuhudumia Wakazi wa Tabora Manispaa litakuwa halina matumizi tena. Je, Serikali ina mpango gani wa kuliweka Bwawa la Igombe kwenye scheme za umwagiliaji ili wakazi wa Tabora waendeshe Kilimo cha umwagiliaji?

Supplementary Question 1

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo kwa majibu yake mazuri, lakini napenda niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata athari kubwa sana ya uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa miti ambayo inatumika zaidi kwa ajili ya mkaa na kuni. Hali hiyo
imepelekea Mkoa wa Tabora na maeneo ya jirani kupata mvua ya kusuasua ambayo ndio inatumika zaidi kwa kilimo. Sasa swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba pamoja na athari zote hizo zilizopatikana wananchi wataendelea na shughuli za kilimo kama kawaida?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pamoja na Serikali kuyaingiza maeneo ya Imalamihayo, Inala, Bonde la Kakulungu na Magoweko katika mpango wa umwagiliaji, lakini mpaka leo maeneo haya bado hayajaanza kufanya kazi. Sasa tunataka tupate majibu ya Serikali ni lini maeneo haya na skimu hizi zitaanza kufanya kazi kwani mpango huu unaonesha umeanza kazi tangu mwaka 2018?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekit, nashukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Juma Migilla kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anataka kujua mikakati ya Serikali kwa ajili ya kuendeleza kilimokwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hapo Tabora. Sisi kama Serikali cha kwanza tulichokifanya, mkakati mkubwa tuliokuwa nao ambao badala ya kutegemea fedha za kibajeti, lakini pia badala ya kusubiri fedha za washirika wa maendeleo kutoka nje ya nchi tumeielekeza Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo kuja kwenye halmashauri mbalimbali nchini kukaa nao na kubainisha yale maeneo yanayofaa kwa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kubainisha kujua mahitaji yenu wataenda kuingia mikopo kwa dhamana ya halmashauri na sisi Serikali tutawadhamini zaidi ya asilimia 80 ili kujenga miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo huu Mkoa wa Tabora ili wakulima waendelee kulima cha kisasa cha uhakika na chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anasema, ni lini kwamba miradi hi tuliyiotaja kwenye jibu letu la msingi kwamba itaanza kufanya kazi. Hii miradi itaanza kufanya kazi muda mfupi ujao baada ya upatikanaji wa fedha za kibajeti na kama nilivyosema kwenye jibu la awali chanzo kingine cha pesa ni kupitia mikopo kupitia Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo.