Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Primary Question

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:- Je, Wizara ya Kilimo inashirikianaje na Wizara nyingine zinazohusika na uwekezaji wa mambo ya nje kutafuta soko la tumbaku nchini Misri badala ya kulazimika kutumia nchi za Uganda na Kenya peke yake?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa. Niipongeze Serikali kwa hatua inazozichukua kuimarisha soko la tumbaku nchini. Njia mojawapo ya kuimarisha soko la tumbaku kwa upande wa sisi Wanaruvuma ni kufufua Kiwanda cha Kuchakata Tumbaku kilichoko Songea ambacho kinamilikiwa na SONAMKU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SONAMKU kwa kushirikiana na mnunuzi wanakwamishwa na Serikali kwa kutoilipa VAT return ya jumla ya shilingi bilioni 12 Kampuni hiyo ya Premium Active Tanzania Limited na hivyo kampuni hiyo kushindwa kushirikiana na SONAMKU kuanzisha au kufufua kile kiwanda.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha hizi fedha zinalipwa ili sisi Wananamtumbo tuwe na uhakika na soko la tumbaku kwa kufufua hicho kiwanda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wananamtumbo tunajihusisha vilevile na kilimo cha Korosho na Mazao mchanganyiko ya mahindi mbaazi, ufuta, alizeti na soya. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha masoko ya mazao haya ili Wananamatumbo tuendelee kupata nafuu lakini na suala la mbolea au pembejeo kwa ujumla?

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Edwin Ngonyani kwa namna alivyoshirikiana na Serikali kupata soko la tumbaku kwa kampuni ya Premium Active Tanzania Limited. Nampongeza sana Mheshimiwa Ngonyani na kwa namna anavyohangaikia Wananamtumbo katika kuhakikisha wananufaika na sekta ya kilimo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ni kufufua viwanda vikiwemo viwanda ambavyo vinachakata mazao yanayotokana na kilimo likiwemo zao la tumbaku. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya Kilimo tutakaa na wenzetu upande wa Wizara ya Fedha kuangalia hili suala la VAT ambalo Mheshimiwa Ngonyani ameliuliza kama swali lake la nyongeza namba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali lake la pili ni kuhusu mkakati wa Serikali katika uhakikisha tunapata masoko ya uhakika ya mazao mchanganyiko pamoja na zao la tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya Serikali ya kuhakikisha tunapata masoko ya uhakika kwa wakulima wetu kwanza tumeanza na mikakati ya kupata institutional buyers na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, walishuhudia Serikali ikisaini mkataba na World Food Programme kwa upande wa zao la mahindi kwa wakulima wetu na tunaendelea kuongea na institutional buyers wengine ambao watasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara kwa kushirikiana na Balozi zetu nje ya nchi tunaendelea kuwasiliana nao na kuangalia mikakati ya kushirikiana ili tuweze kupata masoko zaidi katika mazao mchanganyiko na mazao ya kimkakati. Kwa mfano, mwezi Mei, kuna timu inaenda China hususan kwa ajili ya kutafuta soko la tumbaku pamoja na parachichi, karanga na mazao mengine.

Kwa hiyo napenda kumhakikishia Mheshimiwa Ngonyani pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inaendelea kujipanga na tayari tumefanikiwa katika maeneo ya kupata masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Waheshimiwa Wabunge kama Mheshimiwa Ngonyani alivyoshirikiana na Serikali kupata soko la tumbaku kuptia kampuni ya Premium Active Tanzania Limited, basi na wao waendelee kushirikiana na sisi Wizara ya Kilimo kuwasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika. Ahsante.