Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Omary Ahmad Badwel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Primary Question

MHE. OMARY A. BADWEL aliuliza:- Kwa sasa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi yetu na kwa sababu hiyo idadi ya watu pamoja na mahitaji ya huduma mbalimbali ikiwemo chakula vitaongezeka. Wilaya ya Bahi ambayo ni miongoni mwa Wilaya za Dodoma ina fursa muhimu za uzalishaji mchele kutokana na jiografia yake lakini inakwamishwa na miundombinu chakavu na isiyokamilika katika skimu zake za umwagiliaji wa zao la mpunga:- Je, Serikali imejiandaa kuchukua hatua gani kutoa fedha za ukarabati na umaliziaji wa miradi hiyo ya umwagiliaji ili Wilaya ya Bahi ipate fursa ya uzalishaji mchele kwa wingi na kukidhi mahitaji ya chakula katika Mji wa Dodoma?

Supplementary Question 1

MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, lakini pia nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza habari ya tathmini na mimi nashukuru kwa kuniahidi kwamba kabla ya Desemba tathimini hizo zitakuwa zimefanyika ili waweze kujua fedha ngapi zinahitajika ili kumalizia na kukarabati miradi hiyo. Hata hivyo, kwa kuwa tayari tuna miradi ambayo fedha zake zinajulikana kwamba zikipatikana miradi hiyo inaweza kukamilika kwa mfano Mradi wa Umwagiliaji katika Kijiji cha Kongogo ambao umekuwa ni wa muda mrefu. Swali la kwanza, je, Serikali sasa iko tayari kupeleka fedha kabla ya hiyo tathmini kwa sababu tayari tathmini yake inajulikana ili mradi ule uweze kukamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amehusisha kwamba wako washirika mbalimbali ambao wanaweza kutusaidia katika suala zima la miradi yetu ya umwagiliaji na sisi Bahi tayari tunao wafadhili ambao wanatusaidia hususan Shirika la LIC ambalo nataka nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa namna ambavyo wamesaidiana na kushirikiana vizuri na wananchi wa Bahi katika miradi hii ya umwagiliaji. Tayari wameshatuandikia andiko na michoro mizuri kabisa ya utengenezaji wa bwawa katika Kijiji cha Chikopelo lakini bado hatujapata fedha. Je, Serikali sasa itakuwa tayari kupokea andiko hili kutoka wenzetu hawa Shirika la LIC ili kama alivyoahidi Mheshimiwa Waziri waweze kututafutia fedha katika mashirika haya mbalimbali ya wadau wetu? Ahsante.

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omary Ahmed Badwel, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kujua kama Serikali iko tayari kwa ajili ya kupeleka fedha kwa mradi huu wa skimu ya Kongogo ambayo ni ya muda mrefu. Kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Badwel kwa ufuatiliaji wa karibu sana na ushirikiano anaowapa watu wake wa Bahi. Sisi kama Serikali kwanza tuko tayari kwenda kupeleka fedha na ndiyo maana kwenye bajeti ya mwaka huu, mwaka 2019/2020 tumetenga zaidi ya shilingi milioni 217 kwa ajili ya kufanya tathmini ya miradi hiyo ukiwemo huu wa Kongogo.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anataka kujua pia kama Serikali tuko tayari kuchukua andiko walilofadhiliwa na wadau hao wa maendeleo. Serikali iko tayari na sisi binafsi tulishaanza lakini baada ya Bunge hili kwisha tunaomba atupe hilo andiko tulifanyie kazi. Kama tulivyosema hela tulishatenga tutafanya kila liwezekanavyo ili na hili andiko tulitekeleze haraka iwezekanavyo.