Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Primary Question

MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:- Wananchi wa Kata za Mpombo, Kandete, Isange na Luteba pamoja na Kata za Kabula, Lwanga na Lupata wanalima zao la chai kwa wingi lakini bei ya zao hilo ipo chini:- Je, ni lini Serikali itatafuta soko la uhakika la zao la Chai ambalo litasababisha kupanda kwa bei kuliko bei ya sasa ya Shilingi 315 kwa kilo?

Supplementary Question 1

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nipongeze Serikali kwa juhudi pekee ya kuinua bei ya zao la chai kutoka 241 kwa kilo ya majani mabichi chai mpaka kufikia 315, na nimpongeze kipekee Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Rais kwa kutembelea Jimbo hili la Busokelo na concern yetu ya zao la chai tuliwaambia na kuunda Tume kwa ajili ya kushughulikia tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, Bonde la Mwakaleli tuna Kiwanda cha Chai ambacho kimekuwa kikizalisha chai lakini kwa msimu, kuanzia mwezi wa Disemba mpaka Juni kila mwaka na hivyo miezi Sita mingine huwa hakifanyi kazi; Je, Serikali ina mpango gani mkakati wa kukifanya kiwanda hiki cha chai cha Bonde la Mwakaleli kiweze kufanya kazi mwaka mzima badala ya sasa tunaki- underutilize. (Makofi)

Swali la pili, hivi sasa katika Jimbo langu la Busokelo tunalima viazi mviringo na ni wakati wa msimu wa mavuno lakini bei yake ipo chini sana, kiasi kwamba hata wanunuzi wa viazi hivi wanawaibia zaidi wakulima wana-collude kwa kushirikiana na yale makampuni yanayotengeneza mifuko kwa kufanya kitu kinachoitwa lumbesa. Kwa mfano, mfuko mmoja ambao una debe tano wao wanafanya debe sita na nusu na wananchi hawa wanakuwa wamekopa wamenunua pembejeo, wamelima kwa shida, lakini bei zao ziko chini na kiasi hiki kinafanya mkulima akate tamaa kabisa kuendelea kulima zao hili la viazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inatoa tamko gani wewe ukiwa Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuja site ili uone namna mateso ya wananchi wangu wa Bonde la Mwakaleli, Busokelo pamoja na Wilaya nzima ya Rungwe hadi Uyole - Mbeya kwamba wanahitaji masoko ya uhakika katika zao hili la viazi. (Makofi)

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete Mbunge wa Busekelo kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mwakibete kwa pongezi kwa Serikali kuongezeka kwa bei ya chai kutoka shilingi 241mpaka shilingi 315 lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Mwakibete kwa kweli anawapambania wananchi wa Busekelo tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Fredy Mwakibete Mbunge wa Busekelo ni kuhusu Kiwanda cha Chai kuzalisha miezi Sita peke yake na yeye angetamani pamoja na wananchi wa Busekelo kuona kiwanda hiki kinazalisha kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoomba nitatenga muda niweze kwenda nae Jimboni Busekelo tutembelee Kiwanda hiko tuangalie changamoto zilizopo na kuona ni nini Serikali inahitaji kufanya na upande wa Mwekezaji wanahitaji kufanya nini ili kuhakikisha kiwanda hiki kinazalisha kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mwakibete angependa kuujua nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wa Busekelo tunawapatia soko la uhakika la viazi mviringo.

Mheshimiwa Spika, katika ziara ambayo nitaifanya tutahakikisha tunatoka na mkakati wa kuwapatia masoko ya uhakika wa viazi mviringo tunaujadili na pale inapowezekana tutawaunganisha wakulima hawa kwenye masoko ya viazi mviringo. Suala la lumbesa, halitasubiri ziara Mheshimiwa Mbunge baada ya maswali tutakaa pamoja tuangalie namna ya kushughulikia jambo hili, haliwezi kusubiri ziara, tutafuta namna ya kuliratibu vizuri ili wananchi wako wasiendelee kupunjwa kupitia mfumo wa lumbesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)