Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:- Je, Serikali haioni ni wakati muafaka wakuleta Bungeni marekebisho ya Sheria ili kupunguza kiwango cha ushahidi kwenye kesi za ubakaji na hasa ubakaji wa Watoto?

Supplementary Question 1

MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba kuna changamoto kubwa sana ya ukatili kwa wanawake, ikiwemo na watoto kwenye masuala ya ubakaji. Nasi tunafahamu kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka kuwahakikishia usalama Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye makosa ya ubakaji, kama ilivyoainishwa kwenye Kifungu cha 5 cha Sheria ya Sexual Offences Special Provisions Act ya Mwaka 1998 ambayo imeenda kufanya marekebisho ya Kifungu cha 130 cha Sheria ya Adhabu (Penal Code), tunaona kwamba, kigezo au masharti ya kuthibitisha kosa la ubakaji ni mpaka yule aliyebakwa athibitishe kwamba kulikuwa kuna kuingiliwa (penetration). Mazingira hayo ni magumu sana katika utaratibu wa kawaida kuthibitisha kwamba mtu amekuingilia, yani ku- prove penetration siyo kitu kirahisi na hasa kwa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni swali la kwanza. Nataka kufahamu: Je, Serikali haioni katika mazingira haya kwamba kufanyike marekebisho ya sheria, ili standard of proof au ili kuthibitisha kosa la ubakaji ipunguzwe kiwango chake ili kusiwe kuna haja ya ku-prove penetration kwa sababu, watoto siyo rahisi kwao kuweza kuthibitisha jambo kama hilo, lakini mazingira yote kiujumla ya kosa hilo yaangaliwe ili kuweza kutoa haki. Hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuongeza adhabu kwa wale watakaothibitika kwamba wamefanya kosa la ubakaji ili adhabu yao iwe kali ili kuhakikisha kwamba makosa haya ya ubakaji yanakwisha na watu
waogope?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Serikali haioni kwenye kosa la ubakaji, mbakaji apewe adhabu ya kuhasiwa ili asije akarudia tena kufanya kosa kama hilo ambalo linaleta ukatili mkubwa sana kwa wanawake na watoto na linawaathiri kiasi kwamba, hata kama mtu amechukuliwa hatua, bado wale ambao wameathirika wanapata athari kwa muda mrefu zaidi? Nashukuru.

Name

Dr. Augustine Philip Mahiga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kusimamia haki za watoto na hasa wanawake katika kutoa ushahidi kwenye makosa ya aina hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza katika majibu yangu nimesema, la kwanza tumeondoa baadhi ya vigezo ambavyo vilikuwepo vya hasa watoto kuweza kutoa ushahidi wenyewe na kuachia Mahakama uamuzi wa busara na wa kitaalam kuweza kutoa ushuhuda huo kama kitendo hicho kimetokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimesema katika jibu langu kwamba sasa hivi kuna mfumo wa kutazama na kuboresha mfumo mzima wa kesi za jinai. Na katika hilo litakuwa hilo lingine linalohusiana na ubakaji; na kama itatoa mapendekezo, nina hakika pia mapendekezo hayo yatafuatana na adhabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie kweli kwamba, kwa makosa haya adhabu ambazo zipo mpaka sasa, ni kali na inafika mpaka miaka 30 na mmejadili katika Bunge hili. Kama itabidi kuongeza adhabu hizo baada ya marekebisho na mapitio ya sheria hizi, ninashauri kwamba Bunge hili likae na tushauriane na tuweze kuzungumzia suala hili. Linahitaji uamuzi wa kisheria kama tunataka kufanya adhabu kali zaidi kuliko zilizopo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshuhudia mwenyewe Magerezani kuwaona watu wenye makosa kama haya wamepewa adhabu ya miaka 30 na wengi wao pengine watafia Magerezani. Ahsante sana. (Makofi)

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba tu niongezee katika majibu mazuri sana aliyotoa Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria. Kuhusu swali la nyongeza la kwanza la Mheshimiwa Zainab kwamba bado vigezo inaonekana ni vikubwa sana katika kuthibitisha makosa; napenda tu kumwambia kwamba katika ile Sheria ya Sexual Offences Special Provisions Act ilipopitishwa, mojawapo ya masuala iliyoyaondoa kwenye Sheria ya Ushahidi ilikuwa ni ile requirement ya colaboration. Colaboration ilikuwa ni lazima uoneshe kwamba kuna ishara fulani zilizosalia baada ya lile tendo la ubakaji na hiyo ilikuwa inadhalilisha. Kwa hiyo, sheria hiyo iliondoa kitu hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku ni lazima haya yote yafuate misingi ya sheria za jinai, kwamba, lazima kuthibitisha pasipo kuacha shaka ili pia anayetuhumiwa asije akatuhumiwa isivyo sahihi au akapewa adhabu isivyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili suala la kuongeza adhabu, tayari sheria ile kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri, imeongeza adhabu imekuwa kali sana ni miaka 30. Sasa hili pendekezo la kuhasiwa lina tatizo moja, litatusababisha kuvunja Katiba, kwa sababu, Ibara ya 13(6) inaeleza kwamba ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha. Kwa hiyo, tukichukua pendekezo la kuhasiwa linatupeleka tena katika upande mwingine ambapo tutaweza kuvunja Katiba. Nafikiri adhabu zilizopo zinajitosheleza kwa sasa. Ahsante.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama sambamba na majibu mazuri ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Katiba na Sheria na swali zuri ambalo ameliuliza Mheshimiwa Zainab Katimba. Nilitaka tu kuweka mkazo. Sheria peke yake, hata tuwe na sheria kali kiasi gani hatutamaliza tatizo la ubakaji na ulawiti wa watoto na wanawake nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimesimama hapa kuendelea kutoa msisitizo kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutimiza wajibu wetu wa malezi na ulinzi wa watoto. Inasababisha mtoto anabakwa miezi mitatu bila mzazi kujua. Unajiuliza hivi huyu mtoto ana wazazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, narudisha mzigo kwa wazazi na walezi tutimize wajibu wetu, tuwafuatilie watoto wetu, tuwakague watoto wetu, tuwaulize watoto wetu, tujenge urafiki wa watoto wetu kutueleza changamoto na matatizo ambayo wanayapata. Tutaweka sheria kali, wazazi wata-negotiate na wabakaji mwisho wa siku hakuna hatua ambazo zitachukuliwa. Nakushukuru sana. (Makofi)